Tusikubali Mhimili Wa Bunge Na Serikali Kuingilia Mahakama

Tangu demokrasia ya kale Katika nchi ambazo zinatumia misingi ya kisheria ni wazi kuwa kunakuwepo na vyombo vya aina tatu kwa ajili ya kugawana madaraka ili kuweza kuleta ufanisi na utendaji wa utoaji haki kwa wananchi wake yaani Bunge, Mahakama na Serikali.
Demokrasia inataka Serikali iwe na majukumu yake na yanakuwa wazi kabisa hasa ya kusimamia na kutekeleza majukumu ya kila siku na kuhakikisha kuwa huduma zote muhimu katika jamii zinapatikana na kuziwekea utaratibu na mfumo wa usimamizi wake, Bunge linakuwa chombo cha kutunga sheria na kusimamia utendaji kazi wa serikali kwa niaba ya wananchi na Mhimili wa Mahakama unakuwa ndio chombo pekee cha kutoa haki endapo yeyote atakuwa anaona kuwa anaonewa au kuomba kupata tamko la Mahakama kuhusu jambo lolote la utoaji haki  .
Niseme tu wazi kuwa nimestushwa sana na kitendo cha Mbunge wa Mtera CCM Mhe.Livingstone Lusinde kusimama ndani ya ukumbi wa Bunge siku ya jumanne tarehe 21 Juni,2016 na kuomba muongozo wa Spika kuhusu hukumu ya mahakama iliyotolewa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Huko Arusha juu ya kesi maarufu ya ‘makosa ya kimtandao’  ambapo kijana aliyejulikana kama Isaack Emilly Hababuki alitiwa hatiani kwa kosa la kuandika katika mtandao wake wa facebook kilichoonekana kuwa ni lugha ya maudhi/matusi dhidi ya Rais John Magufuli.
Mshitakiwa huyu alitiwa hatiani baada ya kukiri kosa kuwa ni kweli aliandika kwenye mtandao wake wa facebook, hivyo Hakimu akachukua sheria husika kama ilivyotungwa na Bunge na kuangalia kifungu cha adhabu ambacho mhusika alipaswa kuhukumiwa nacho na akakuta kuwa Bunge lilipotunga sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2015 liliweka adhabu ya ama kifungo ,faini au vyote kwa pamoja  kwa mtuhumiwa ambaye atatiwa hatiani kwa mujibu wa sheria hiyo ya makosa ya Kimtandao na nataka kuamini kuwa hicho ndicho kilikuwa msingi mkuu wa hukumu/uamuzi wa Hakimu katika kufikia hukumu yake aliyoitoa.
Ukiisoma sheria ya makosa ya kimtandao iliyotungwa na Bunge ya mwaka 2015   na kusainiwa na Rais Kikwete kuwa sheria tarehe 25 Aprili,2016 kifungu cha 18 kimeweka bayana adhabu ambayo mtuhumiwa atakapotiwa hatiani kwa kosa kama la Izack ni kifungo kisichopungua miezi 12 au faini isiyopungua shilingi milioni tano au vyote kwa pamoja yaani kifungo na faini. Hata kama kingetumika kifungu cha 16 cha sheria adhabu ni kama hiyo ambayo ilitolewa na hakimu katika shauri husika.
Katika hali ya kushangaza Naibu Spika wa Bunge Dr.Tulia Ackson aliruhusu mwongozo huo huku akijua wazi kabisa kuwa mwomba mwongozo alikuwa anataka kuingilia maamuzi ya mhimili mwingine na alikuwa akienda kinyume kabisa na katiba yetu na sheria zetu kwani kila mhimili una mamlaka yake ya kufanya maamuzi na kamwe hauwezi kuingiliwa na mhimili mwingine. Naibu Spika ambaye kitaaluma ni mwanasheria tena mwenye shahada ya uzamivu katika sheria na amekuwa mwalimu wa sheria chuo kikuu cha DSM akaona mwongozo huo ni sahihi na akauruhusu, Huku ni kuingilia mhimili wa Mahakama katika utendaji kazi wake .
Katika hali ya kushangaza zaidi ni kumwona waziri wa sheria tena mtu anayejinasibu kuwa mbobezi katika masuala ya sheria na msomi wa hali ya juu mwenye shahada ya uzamivu Dr.Harrison Mwakyembe naye akatoa maelezo kuwa analiomba Bunge muda ili serikali ikafanye mapitio ya shauri husika ndipo atatoa msimamo wa serikali Bungeni baada ya kupata taarifa kutoka Mahakamani.

Kutoakana na hali hii pamekuwa na maswali mengi kutoka kwa wadau mbalimbali wa demokrasia na mijadala kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na ndio hasa mjadala huu umenisukuma kuandika makala hii kwa ajili ya kushirikisha na watanzania wenzangu tuweze kutafakari kwa pamoja katika kujibu maswali mbalimbali ambayo yameibuka katikati ya mjadala huu.

Hivi ni kwanini ni katika hukumu hii tu ndio serikali na Bunge wanataka kuingilia uhuru wa mahakama? Mbona kuna hukumu nyingi zimetolewa na mahakama na hazijawahi kuhojiwa na Mbunge na hata pale wabunge baadhi walipojaribu kuhoji walijibiwa kuwa huko ni kuingilia uhuru wa mahakama , na hapa nakumbuka hukumu maarufu ya fedha za DECI ambako Mbunge wa Ubungo wakati huo Mheshimiwa John John Mnyika alizuiliwa kuhoji juu ya jambo hilo na hata hivi majuzi sakata la Escrow lilipokuwa limeshika kasi wabunge walizuiliwa kulihoji kutokana na kanuni za Bunge kuzuia jambo kama hilo kujadiliwa. Ukweli ni kwamba wakati wa Bunge la kumi jambo lolote kuwa Mahakamani ilikuwa ni kichaka cha kuzima mijadala ndani ya Bunge lengo likiwa kuzuia kuingilia mhimili mwingine wa dola

Tukio hili limenikumbusha maandishi ya Mwanafalsafa wa kale ambaye naweza kumuita ni baba wa Mihimili ya dola Baron Montesquieu aliyewahi kuandika kuhusu mgawanyo wa madaraka “Pale ambapo madaraka ya Bunge na ya Serikali kuu yanakuwa yamehodhiwa na mtu mmoja, au katika chombo hicho hicho cha hukumu, hakutakuwa na uhuru, kwa sababu hofu itazuka, utawala huo huo au bunge litatunga sheria kandamizi na kuzitekeleza kwa mfumo kandamizi. Pia hakutakuwa na uhuru endapo madaraka ya Mahakama, Bunge na Serikali hayatatenganishwa. Pale ambapo madaraka ya Serikali kuu yanapokuwa yamefungamanishwa na Bunge, uhai wa Bunge na Uhuru wake unakuwa katika hatari kubwa ya kudhibitiwa kiholela: kwa kuwa jaji hawezi kuwa mtunga sheria. Pale ambapo Serikali kuu imefunganamishwa na Mahakama, basi jaji anaweza kuwa na tabia ya mabavu na ukandamizaji. Inakuwa mbaya zaidi, pale ambapo mtu huyo huyo au chombo hicho hicho, iwe ni wateule wa Serikali au watu wengine wanapotumia hayo madaraka ya kutunga sheria, kutekeleza maazimio ya umma na kutoa hukumu za jinai au tofauti za watu”

Tukio hili limenikumbusha maandishi haya kwa sababu sasa Bunge na Serikali vinataka kujifungamanisha na kutaka kutoa maelekezo kwa Mahakama ni aina gani ya hukumu wanatakiwa kutoa hata kama hukumu hiyo itakuwa kinyume cha sheria zilizotungwa na Bunge lenyewe, au wanataka kuitisha mahakama kuwa kama hakimu au Jaji akitoa hukumu ambayo wanaiona sio sawa basi itawasilishwa hoja Bungeni na kujadiliwa badala ya kufuatwa kwa misingi na taratibu za  kisheria zilizopo kwa mujibu wa katiba yetu katika kushughulikia jambo kama hilo.
Kwenye shauri hili (Kijana Emily) serikali ndio ilifungua kesi na imeshinda kesi , sasa sijui waziri anataka kupata taarifa gani kutoka mahakamani ili atoe tamko la serikali tena Bungeni,nijuavyo ni kuwa kama hawajaridhika na hukumu hii kuna taratibu za kisheria zinazotakiwa kufuatwa na upande wa serikali na sio kuwasilisha hoja au msimamo wa serikali Bungeni , huku ni kwenda kinyume cha Katiba na sheria zetu, tunataka kufungamanisha Bunge na serikali dhidi ya mahakama , hii maoni yangu sio jambo la afya kwa taifa letu na linafaa kupingwa kwa nguvu zote.
Chombo kilichopewa jukumu la kutoa haki kwa mujibu wa katiba yetu sura ya tano ni Mahakama , ibara ya 107A ya Katiba yetu inaweka bayana chombo chenye mamlaka ya kutoa haki na kama kuna upande haujaridhishwa na uamuzi wa mahakama kuna utaratibu wa kufuatwa ili kushughulikia jambo hilo.
Ibara ya 107A (1) ya katiba yetu inasema ‘mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa idara ya Mahakama na idara ya mahakama ya Zanzibar ,na kwa hiyo hakuna chombo cha serikali wala cha Bunge au Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kitakachokuwa na kauli ya mwisho katika utoaji haki’ Ibara hii ina maana kuwa waziri wa sheria na Naibu Spika wameshaisahau ? Mbunge aliyeomba muongozo naweza kumsamehe katika hili kwani yeye sio mwanasheria na hivyo inawezekana kabisa kwa kutokujua sheria (japo kutokujua sheria haiwezi kuwa kinga kwake) ndiko kulimpelekea kuomba muongozo huo ila kwa hawa wanasheria wawili yafaa tutafakari zaidi kabla ya kufikiria kuwa walitenda kwa kutokujua maana wanajua ! ni waalimu wa sheria hawa!
Mbona hukumu nyingi na maarufu hazijawahi kuhojiwa na au kuwasilishwa Bungeni? Nani hakumbuki Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge aliwahi kutiwa hatiani kwa makosa matatu tarehe 29 disemba, 2010 ambayo yalikuwa kuendesha kwa uzembe na kusababisha vifo vya wanawake wawili, Uharibifu wa mali na kuendesha gari ambayo haikuwa na hati ya Bima. Alipigwa faini ya shilingi laki saba au kifungo cha miaka mitatu gerezani, mtuhumiwa alilipa faini na mpaka leo sio Bunge wala serikali waliowahi kuhoji kuhusu hukumu hii, zipo pia kesi nyingine nyingi ambazo hatujawahi kusikia Bunge likitaka maelezo juu ya hukumu na wala serikali haikuwahi kuwasilisha  maelezo ya aina hiyo na badala yake mara zote walikuwa wakitumia utaratibu wa kukata rufaa pale ambapo walipoona kuwa hawakuridhika na hukumu iliyotolewa .
Ni muhimu sana katika wakati kama huu tukajaribu sote kuwarejesha viongozi wetu kwenye misingi ya kikatiba na kisheria pale ambapo tunaona kuwa sasa wanaelekea kuwa kwenye hangover za kutokutaka kufuata na kutii sheria zetu wenyewe litakuwa jambo la hatari sana ambalo linalikumba taifa kwa sasa na huko mbeleni tuendako ambako wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa,kijamii na kisheria wanashindwa mpaka sasa ‘kubashiri’ uelekeo wetu katika Nyanja ya kisheria na kisiasa kama Taifa.
Nataka nitoe wito kwa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika ,viongozi wa kisiasa, waandishi wa habari, viongozi wa dini, na wanaharakati wa haki za binadamu kuwa sasa yafaa wakawa mstari wa mbele katika kufuatilia kwa makini kila kauli na matendo ya viongozi wetu na kwa zile kauli au matendo ambayo yanalenga kukandamiza haki, demokrasia na uhuru basi zisiungwe mkono bali kwa pamoja wapaze sauti zao , maana wahenga walisema ukiona mwenzako ananyolewa , wewe tia maji!
Naomba nieleweke kuwa si kuwa wananchi au Bunge linazuiwa kujadili hukumu ya Mahakama ambayo imekwisha kutolewa, la hasha! Kinachopingwa na ambacho ni kinyume cha Katiba na Sheria zetu ni pale ambapo Serikali na Bunge wanataka kujadili hukumu ambayo imeshatolewa na kulitaka Bunge kuazimia na kutoa maelekezo kwa serikali kuhusu hukumu iliyotolewa na Mahakama. Kuomba Muongozo wa Spika kuhusu hukumu ya Mahakama maana yake ni kutaka kiti cha Spika kitoe maelekezo kuhusu hukumu hiyo. Hilo litakapofanyika ni wazi kuwa misingi ya kikatiba na kisheria itakuwa imekiukwa.
Kwa leo namalizia kwa kutoa wito kwa Bunge na serikali kuwa wawe makini katika kutimiza majukumu yao kwani watakapotaka kuchukua mamlaka ya Mahakama ,watu ambao kimsingi hawana pa kusemea au kujitetea ni kuwaonea na tutafanya kosa kubwa sana kwani tutaua misingi ya kikatiba na kisheria ambayo ilijengwa kwa miongo mingi na ndicho kimetufanya kuwa kama taifa, vinginevyo tukiua misingi hii hatutakuwa tena Taifa.

John Mrema –
Mkurugenzi wa masuala ya Bunge –CHADEMA
+255 758 144 555

Share Button
Layout Settings