MSIMAMO WA VYAMA VYA CUF, NCCR -MAGEUZI,CHAUMMA NA CHADEMA- KUHUSU KUSHIRIKI UCHAGUZI MDOGO WA MARUDIO WA TAR 13-01-2018 .

UTANGULIZI
Serikali ya awamu ya tano imeonyesha wazi kuwa haiko tayari kufuata Katiba na Sheria za nchi katika utendaji wake wa kazi na imejipambanua wazi kuwa haiheshimu Demokrasia na Haki za Binadamu zimeendelea kuvunjwa na hakuna hatua zozote zinazoonekana kuchukuliwa ili kuithibiti hali hii.
Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Nchi na sheria zimeendelea kuvunjwa na viongozi wa nchi, pia tumeanza kushuhudia matukio ya watu kutekwa , kupotezwa na wengine wanaokotwa wakiwa wamekufa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi na hatuoni uchunguzi ukifanywa wala hatua madhubuti zikichukuliwa na watawala ili kuithibiti hali hiyo.
Baadhi ya vitendo ambavyo vimeonyesha wazi kuwa kuna ukiukwaji wa Katiba na Sheria za Nchi ni pamoja na vifuatavyo;

  1. Kupiga Marufuku Mikutano ya Vyama vya Siasa:

Serikali ilipiga marufuku kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa mpaka mwaka 2020. Huu ni uvunjaji wa Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Aidha, katazo hili linakiuka Sheria namba 5 ya Vyama vya siasa ya mwaka 1992 ambayo imetoa haki kwa vyama vya siasa kufanya kazi ya siasa.

  1. Mauaji, Unyanyasaji na Uonevu unaofanywa dhidi ya Viongozi wa Vyama vya Upinzani:

Uonevu na unyanyasaji dhidi  viongozi wa kisiasa wa vyama vya upinzani unaendelea kufanywa kwa kuwakamata, kuwaweka rumande na kuwafungulia mashtaka viongozi hao ukiwa ni mkakati wa kuwafunga midomo wapinzani wanapotekeleza jukumu lao la msingi la kuikosoa Serikali.Aidha wapo ambao wameshambuliwa kwa lengo la kuwauwa (Tundu Lissu), wengine wamepotezwa na mpaka sasa hawajulikani walipo (Ben Saanane) na wengine wameuwawa na wengine wanaendelea kushambuliwa maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

  1. Chaguzi kugeuzwa uwanja wa vita, badala ya kushindanisha hoja za vyama

Tumeshuhudia chaguzi za marudio hasa kwenye kata 43 zikiendeshwa bila kufuatwa kwa sheria , taratibu, kanuni na maadili ya uchaguzi na badala yake viongozi wa vyama vyetu wameendelea kukamatwa na kufunguliwa mashitaka kwenye mahakama mbalimbali na wengine wapo mahabusu za Polisi mpaka sasa .Aidha , viongozi wetu kwenye kata hizo walishambuliwa kwa mapanga na wengine mbele ya Polisi na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya wahalifu haobadala yake walikuwa wanalindwa na Polisi ili kutimiza uhalifu wao.

  1. Mauaji na watu kupotezwa

Kumekuwa na utamaduni mpya ambapo sasa wananchi wanauwawa na miili yao inaokotwa ikiwa inaelea ama baharini au maeneo mbalimbali ya nchi wakiwa wamewekwa kwenye Sandarusi na hatuoni hatua zozote za kuchunguza mauaji haya. Aidha kumekuwa na utamaduni mpya wa watu kutekwa na kupotezwa, na hakuna juhudi zinazofanywa na vyombo vya dola kuthibiti hali hii.

  1. Vyombo vya habari kuminywa

Tumeshuhudia vyombo vya habari nchini vikiendelea kuminywa na vingine kufungiwa kwa sababu tu vimekuwa na ujasiri wa kuisema serikali , hali hii imeenda mbali zaidi sasa tunashuhudia waandishi wa habari wakitekwa na kupotezwa na hakuna hatua za kufuatilia kwa kina jambo hili na hatuoni dalili za kukomeshwa kwa matukio haya ambayo ni mapya kwenye nchi yetu.

  1. Matukio ya aibu katika uchaguzi kata 43

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza uchaguzi mdogo wa marudio katika majimbo ya Longido,Singida Kaskazini , Songea Mjini na Kata sita ambao utafanyika tarehe 13 Januari,2017.
Itakumbukwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi wa marudio katika kata 43 mnamo tarehe 26 Novemba ,2017. Uchaguzi huu ulifanyika bila ya kufuata misingi ya sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi,baadhi ya matukio hayo ni kama ifuatavyo;

  1. Mawakala walitolewa nje ya vituo vya kupigia kura; hili lilifanywa kwa ushirikiano baina ya polisi na wasimamizi .
  2. Vituo kuvamiwa wakati wa kuhesabu kura; vituo vya uchaguzi vilivamiwa na watu wa CCM na kuharibu zoezi la kuhesabu kura.
  3. Fomu za malalamiko; mawakala wetu walikataliwa kujaza na wale wachache waliojaza hawakupewa kabisa nakala za fomu husika
  4.  Kukatwa mapanga; Viongozi na wanachama wetu kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya
  5. Viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wilaya; kuingia kwenye vituo vya kupigia kura wakati hawaruhusiwi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi
  6. Wasimamizi wa uchaguzi; walifanya hujuma za wazi kama vile kuwanyima barua za viapo mawakala wetu,kuwazuia wagombea wetu kufanya kampeni na kuwaengua wengine bila kufuata taratibu.
  7. Matokeo halisi kutokutangazwa; wasimamizi wa uchaguzi waliamua kutangaza matokeo ya uongo na kuipa CCM ushindi pamoja na fomu zote kuwepo na kuonyesha kuwa vyama vya upinzani vimeshinda .

MAANA YA MATUKIO HAYA .

  1. Hakuna tena uchaguzi utakaofuata sheria ,kanuni na taratibu zilizopo
  2. Tume ya Taifa ya uchaguzi imekosa uhalali wa kuendelea kusimamia chaguzi
  3. Jeshi la polisi wameonyesha wazi kuwa wapo upande wa CCM na hata tuliporipoti matukio mbalimbali hawakuchkua hatua
  4. CCM kwa kushirikiana na serikali yake hawako tayari kutangazwa kuwa wameshindwa kwenye uchaguzi.
  5. Wasimamizi wa uchaguzi wameonyesha dhahiri kuwa wao ni CCM .

HITIMISHO.
Itakumbukwa kwamba, kwa nyakati tofauti kabla ya uchaguzi wa marudio wa Novemba 26, tayari kumekuwepo na kauli tata za maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dokta John Pombe Magufuli kwa wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa ya kwamba hatowaelewa ikitokea wakimtangaza mgombea wa chama cha upinzani kuwa mshindi. Kauli hii imejithibitisha katika uchaguzi huu wamarudio.
Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini alitumika kuweka pingamizi kwa Mgombea wa Kata ya Saranga (CHADEMA) na kusababisha kuenguliwa kwake kabla ya Mgombea huyo kushinda Rufaa yake Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Kutokana na matukio hayo tumeamua kuwa hatutashiriki kwenye uchaguzi mdogo wa Majimbo yaliyotangazwa pamoja na Kata husika, badala yake tutaelekeza nguvu zetu katika kudai Katiba mpya yenye Tume huru ya Uchaguzi .
Aidha , tumeamua kwenda kufungua kesi ya Kikatiba Mahakamani kuwashitaki wasimamizi wote wa uchaguzi ambao ni Makada wa CCM, ambao wameteuliwa kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 74 (14) na (15)(e).
Na mwisho tutaunganisha nguvu zetu na makundi ,asasi, wadau na wananchi  wote kwa ujumla katika kudai uchaguzi huru na haki katika Nchi yetu
……………………..
MHE.JULIUS MTATIRO
M.KITI KAMATI YA UONGOZI –CUF
…………………….
MHE. FREEMAN MBOWE
M.KITI –CHADEMA
……………….
MHE. HASHIM RUNGWE
M.KITI –CHAUMMA
…………………..
MHE. DANDA JUJU
KATIBU MKUU –NCCR –MAGEUZI
…………………
MHE. TOZI MATWANGA
KATIBU MKUU –NLD

Share Button
Layout Settings