Somo Nililojifunza Kutokana na Uchaguzi Mkuu wa Kenya wa Mwaka 2017

Ndugu Mhariri, naomba kupata nafasi ili kuweza kuyaweka maoni yangu binafsi juu ya mambo ambayo niliweza kujifunza kutokana na uchaguzi Mkuu wa Kenya uliomalizika hivi karibuni .

Kenya ni nchi ambayo inakadiriwa kuwa na watu takribani milioni 48 na kati yao inakadiriwa kuwa asilimia 70 ni vijana . Imekuwa ikijidhihirisha kila mara panapokuwa na uchaguzi Kenya kuwa kura hupigwa kwa kutumia kigezo kikubwa ambacho ni Ukabila wa wagombea ama wa watu ambao wanawaunga mkono wanatokea katika kabila gani, yaani ni sawa na kusema kuwa wanasiasa wa Kenya wamejimilikisha Makabila yao na wao ndio wanakuwa na sauti kwa niaba ya makabila yao .

Pamoja na uwepo wa jambo hilo katika siasa za Kenya , uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umekuja na masomo mahususi na ambayo sisi kama taifa yafaa tukajifunza wakati tunajiandaa kuelekea uchagzu Mkuu wa mwaka 2020.Mambo niliyojifunza ni kama ifuatavyo;

  1. Katiba Mpya –taasisi imara

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2007 kukumbwa na vurugu na kusababisha mauaji , Wakenya walijifunza kuwa katiba yao ilikuwa na mapungufu ambayo yalipelekea kuwepo kwa vurugu zile na hivyo kwa kauli moja waliamua kuanzisha mchakato wa kuwa na Katiba mpya ambayo itaendana na hali halisi ya sasa na itaweza kuziba mianya na uwezekano wa kutokea kwa vurugu katika chaguzi zitakazofuata huko mbeleni.

Katiba ya Kenya iliweka uwepo wa taasisi imara na ambazo haikuwa rahisi kwa viongozi wa kisiasa kuweza kuziingilia , kwa mfano uwepo wa tume huru ya uchaguzi na ambayo imeonekana kuwa ilikuwa haipendelei upande wowote ule uwe upande wa watawala ana wapinzani uliwapa imani wakenya kuwa kura zao zitakuwa salama na ndio maana wamejitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura .

Aidha Katiba mpya ya Kenya imeweka utaratibu wa matokeo ya rais kupingwa mahakamani na upande wowote ambao utaona kuwa haukutendewa haki kutokana na matokeo hayo. Hii inawafanya wakenya wawe na fursa na kuwasilisha malalamiko yao na kutokana na uwepo wa kifungu hiki kwenye katiba ya yao utaratibu wa lini na wapi rais ataapishwa umewekwa kwa mujibu wa katiba na kuondoa sintofahamu ya mwaka 2007 ambako wakati tume yao ya uchaguzi inatangaza matokeo ya mwisho Mgombea mmoja (Mwai Kibaki) alikuwa anaapishwa tena Ikulu na hili lilitokea kwa sababu yeye alikuwa Ikulu kwa wakati huo ndio maana katiba ya sasa ya Kenya inasema wazi rais ataapishwa lini na wapi na wako wazi kabisa kuwa asiapishiwe katika viunga vya Ikulu.

Kuundwa kwa kamati ya mpito ya kukabidhiana madaraka (transitional team) Ndio maana pamoja na ukweli kuwa Uhuru ndio rais lakini amelazimishwa na Katiba kuunda kamati ya mpito (transition team) kwa ajili ya kupokea na kukabidhi madaraka kwa utawala mpya , kazi ya timu hii ya mpito ni pamoja na kupokea taarifa kutoka kwenye utawala unaoondoka juu ya hali halisi ya Kenya kama vile madeni, rasilimali za serikali zilizopo, hali ya ulinzi na usalama ikiwemo siri za vyombo vyao vya ulinzi na usalama pamoja na masuala mengine yote muhimu juu ya taifa la Kenya .

Jeshi la polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama Kenya walijiendesha kama taasisi huru na zinazojitegemea na hawakuwahi kuonekana kuwa wanaendeshwa kwa mashinikizo kutoka upande mmoja wa wanasiasa, jambo hili limeifanya Kenya kuendelea kuwa mbele katika kuonyesha kuwa Demokrasia yao imekuwa na iko viwango vya juu ukilinganisha na nchi nyingi za bara la Afrika .

Katiba mpya ya Kenya imeweka utaratibu wa kumpata mkuu wa polisi kutoka ule wa zamani wa kuteuliwa na rais na kuweka utaratibu kuwa anatakiwa kuomba ajira na iko tume mahususi na lazima aidhinishwe na Bunge la nchi hiyo , utaratibu wa kumuondoa madarakani pia umewekwa hivyo hawezi kuondolewa kwa sababu amekataa kupokea mashinikizo ya wanasiasa , hili linamfanya atomize wajibu wake kwa weledi mkubwa bila kuwa na hofu ya kuondolewa na Yule aliyemteua !

  1. Wapiga kura wapya

Kwa mujibu wa taarifa za Tume ya Uchaguzi na mipaka ya Kenya (IBEC)ni kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu (2017) wapiga kura wapya waliojiandikisha walikuwa milioni 5 ukilinganisha na uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, hii maana yake ni kuwa hawa ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 22 ambao walienda kupiga kura kwa mara ya kwanza katika maisha yao.

Kwa vigezo vyovyote vile hawa wapiga kura wapya walikuwa na chachu ya kipekee katika uchaguzi huo na walikuwa na mvuto wa kipekee kwa kila upande kujihakikishia kuwa wanaweza kuzivutia kura hizi mpya na ambazo ni kwa mara ya kwanza wanakutana na sanduku la kura.

Uwepo wa kundi hili uliwafanya wanasiasa kubadili mbinu na hata kulazimika kubadili ajenda zao za uchaguzi kulingana na matakwa ya kundi hili kwani walilazimishwa kuvutia kura hizi ambazo hawakuwa na uhakika kama watapiga kura zao kwa utamaduni wa kikabila ama laa maana walikuwa hawawezi kuitabiri tabia yao kwa uhakika .

Uwepo wa kundi hili jipya ukiongeza na idadi ya vijana wengine wenye miaka 23-35 uliwafanya wanasiasa wa Kenya kubadilisha kabisa mbinu za kuwasiliana na kura hizi ambazo zilikadiriwa kufikia asilimia 70 ya kura zote , hivyo walilazimika kutumia mawasiliano ya kidigitali kama vile facebook , tweeter na WhatsApp ili kuweza kulifikia kundi hili .

Mfano Rais Uhuru Kenyatta katika kuelekea mwisho wa kampeni zake na kwa kutambua nguvu za kundi hili aliamua kuwa na siku maalum ya kufanya ‘charting’kupitia ukurasa wake wa facebook na alikuwa akijibu maswali ya papo kwa papo aliyokuwa akiulizwa na Wakenya bila kujali kuwa yanatoka kwenye kundi la wanaomuunga mkono ama laa, fikiria kijana ambaye anaenda kupiga kura kwa mara ya kwanza halafu maswali yake yanajibiwa na Rais unafikiri kura yake na ya marafiki zake ambao anaushawishi nao wataipeleka wapi kura yao .

Kwa wagombea walioshindwa kulifikia kundi hili kwa uhakika waliweza kupoteza kura na hatimaye kupoteza nafasi zao na ndio maana baada ya uchaguzi huu Kenya leo inaenda kuwa na Bunge ambalo zaidi ya asilimia 90 ya wabunge wake ni wapya na hali iko hivyo hivyo kwa Maseneta na Magavana .

Vijana wa Kenya wameonyesha kuwa wanaweza kuweka mabadiliko wanayoyataka na kuyasimamia mpaka dakika ya mwisho, na kwa hili ni somo kubwa kwa vijana wa Tanzania na Afrika kwa ujumla .

  • Ajenda

Siasa za ajenda mahususi zilitawala kampeni za uchaguzi Mkuu wa Kenya , kwa upande wa Upinzani (NASA) Mgombea wao wa urais Raila Odinga alijikita zaidi katika kukosoa utawala uliopo na madhaifu yake , wakati Uhuru Kenyatta na JUBILEE wao walijikita katika kusema wamefanya nini na wakiongezewa muda wataenda kufanya nini cha ziada .

Hili ni somo kubwa kwa wanasiasa wa Tanzania kuwa waliopo madarakani wanatakiwa kujua kuwa ifikapo 2020 wananchi watataka kuona kilichofanyika na sio vinginevyo na wale walioko upinzani kama mimi tunatakiwa kusema tunataka kufanya nini kwa ajili ya Tanzania na tuonyeshe hivyo.

  1. Demokrasia iliyokomaa

Hii inatokana na ukweli kuwa wakati wote wa kampeni za Kenya hatukusikia matukio ya wanasiasa kukamatwa na kuwekwa ndani kwa sababu tu wanakuwa na hoja kinzani na zile za watawala .

Wakati wa kukusanya matokeo tumeshuhudia jinsi ambavyo vyombo vya habari vilikuwa huru katika mchakato mzima wa kukusanya na kutangaza matokeo ya kura za rais . Tulishuhudia vyombo vya habari kama vile citizen TV wakiwa na vituo vyao vya kukusanya na kuchakata matokeo ya kura za rais (Tallying centres ) , hili ni somo kubwa kwetu watanzania kuwa tujifunze uwazi huu kwa ajili ya chaguzi zijazo .

Kenya wameruhusu uwepo wa wagombea huru (Independent Candidates) kwenye kila ngazi ya uchaguzi na hili limewafanya watu ambao ama hawana vyama au vyama vyao havikuwapitisha kugombea kuwa na fursa ya kugombea na wameweza kushinda kwenye baadhi ya maeneo , watu hawa watakapokuwa Bungeni watakuwa hawawasilishi maslahi ya vyama vyao bali watakuwa ndio wasemaji kwa niaba ya wakenya ambao hawana vyama au hawashiriki shughuli za vyama vya siasa.

Hata baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa tumeona kuwa aliyeshinda ameruhusu wale ambao wanampinga wafanye maandamano yao kwa amani bila kufanya uharibifu, hiki ni kiwango cha juu kabisa cha demokrasia kwani inaonyesha jinsi ambavyo viongozi wanaheshimu katiba na sheria zao ambazo zinatoa haki kwa wananchi ya kuandamana . Somo hili lazima viongozi wetu wajifunze kote barani afrika kuwa haki za msingi za wananchi wao haziwezi kuminywa kwa misingi ya kiitikadi .

  1. Muungano wa vyama (Coalition)

Katika uchaguzi huu tumejifunza kuhusu umuhimu wa vyama kufanya muungano kwa ajili ya kutafuta kura , ila Muungano huo ni lazima uundwe kwa umakini na kwa vigezo ambavyo vyama vitakuwa vimekubaliana .

Hapa kwetu Muungano wa vyama hautambuliki kwa mujibu wa sheria zetu , hivyo ni muhimu kwa msajili wa vyama kujifunza somo hili na kupeleka mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa na kuweka kipengele hiki cha kuruhusu vyama kuungana.

Nitaendelea wiki ijayo.

John Mrema

Mkurugenzi wa Itifaki,Mawasiliano na Mambo ya Nje

CHADEMA

0758 144 555.

Share Button
Layout Settings