Sauti kutoka nje ya Bunge

Ndugu Mhariri ,

Ninaomba nafasi kwenye gazeti lako ili nami ambaye sauti yangu inatoka nje ya Bunge iweze kusikika na hasa baada ya ‘sauti kutoka Bungeni’ kusikika kupitia kwa mtu aliyejitambulisha kuwa anaitwa Owen Mwandubya ambaye ni mkuu wa kitengo cha habari ,elimu na mawasiliano ,ofisi ya Bunge . Makala yake ilichapishwa tarehe 15 Juni, 2016 ,toleo Na. 5801 katika ukurasa wa 16.

Katika makala yake yenye kichwa cha habari ‘Kanuni zikiheshimiwa hakuna atakayesusia Bunge’ mwandishi amejaribu kujenga hoja zake kwa kuonyesha kuwa kinachoendelea Bungeni kwa wabunge wote wa Kambi ya upinzani kugomea kushiriki vikao ambavyo vinaongozwa na Naibu Spika Dr.Tulia Ackson ni kitendo cha kulisusia Bunge, jambo hili sio la kweli bali ni upotoshaji wa makusudi ambao unafanywa kwa malengo mahususi ya kisiasa . Ieleweke kuwa wanachofanya wabunge wa upinzani ni kususia vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika wa Bunge na sio kususia Bunge.

Mwandishi amejaribu kuonyesha kuwa Naibu Spika alipokuwa anatoa Mwongozo juu ya hoja ya Mhe.Nassari alitumia ‘kanuni kwa umahiri mkubwa’na amejaribu kumtetea na kuwataka wale ambao hawakuridhishwa na umahiri huo wa kanuni basi wakate rufaa kwa mujibu wa kanuni ya 5 ya Kanuni za Kudumu za Bunge , kana kwamba hiyo ndio njia pekee ya kikanuni iliyopo ya kuweza kushughulikia jambo hilo.

Mwandishi wa makala hii ni Afisa wa Bunge tena mwenye wajibu wa kutoa taarifa sahihi kwa umma juu ya kinachoendelea Bungeni, badala yake mwandishi ameonekana kuegemea upande mmoja wa kutetea uamuzi wa  Naibu Spika na kudiriki kuonyesha kuwa kitendo kinachofanywa na wabunge wa Upinzani cha kususia vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika Dr.Tulia ni kwenda kinyume na kanuni ya 146 ya kanuni za kudumu za Bunge, jambo ambalo halina ukweli kwani wabunge wanashiriki vikao vyote ambavyo naibu spika sio Mwenyekiti na ukweli huu anaujua .

Mwandishi wa makala hiyo Ndugu Owen ametoa hitimisho la kushangaza umma kwa kuandika ifuatavyo; ‘Ni dhahiri kuwa Naibu Spika ametumia vyema kanuni za kudumu za Bunge na kwa msingi huu ni kwamba hakupindisha kwa namna yoyote kuhusu kufikia uamuzi huo’

Mtumishi huyu wa Bunge ameonyesha wazi kuwa yeye ameshafikia uamuzi na kuhitimisha jambo hili bila kujali kuwa jambo hili liko mikononi mwa Spika wa Bunge na ambaye tayari ameshaliwasilisha jambo hilo kwenye Kamati ya haki, kinga na madaraka ya Bunge ili matakwa ya katiba ibara ya 85(4)(c) ya utaratibu wa kumwondoa Naibu Spika madarakani uweze kufuatwa .

Kwa hitimisho hili la mtumishi wa Bunge mwenye kusimamia kitengo cha kutoa habari za Bunge, nitakuwa sifanyi kosa kama nikisema kuwa ameamua kutoa hukumu ambayo itatolewa na kamati ya haki,kinga na madaraka ya Bunge kwani huyu ni mtoa taarifa rasmi za Bunge na ameshafanya hivyo au atakuwa anaiandaa kamati ya Haki ,kinga na madaraka ya Bunge Kisaikolojia kuwa Naibu Spika alitumia kanuni kwa umahiri mkubwa wakati akitoa uamuzi wake Bungeni. Nani amemtuma kuwahisha shughuli za Bunge ?

Hapa ieleweke kuwa kwa mwandishi ambaye ni mtumishi wa umma ana wajibu wa kuujulisha umma ukweli wa kinachoendelea Bungeni na hasa kabla ya kuwahukumu wabunge ambao kimsingi ni mabosi wake, alipaswa walau kuwaeleza umma kuwa wabunge wa upinzani wameendelea kushiriki kwenye vikao vya kamati za kudumu za Bunge ambako ni wajumbe na hivyo sio kweli kuwa hawawakilishi wananchi na wanaenda kinyume na kanuni ya 146 kama alivyojaribu kuupotosha umma. Wabunge ambao wanatokana na Vyama vya upinzani wameendelea kushiriki vikao vya kamati za bunge na shughuli nyingine za bunge ambazo haziongozwi na Naibu Spika Dr.Tulia Ackson huo ndio ukweli ambao mwandishi hataki kuuweka wazi kwa umma .

Aidha , mwandishi huku akijua wazi kuwa zipo kanuni nyingine mbalimbali ambazo zinaweza kutumika katika jambo kama hilo na zinakubalika na tayari wabunge wa Upinzani kupitia kwa Mbunge James Millya (Mbunge –Simanjiro) tayari walishawasilisha kusudio la hoja ya kukosa imani na Naibu Spika kwa mujibu wa kanuni ya 138 la kutaka bunge lifanye azimio la kukosa imani naye; tayari Spika wa Bunge ameshakubaliana na Hoja ya Millya na ameshawasilisha hoja hiyo kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Haki,Kinga na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya hatua za mashitaka kuanza kusikilizwa kwa mujibu wa kanuni ya 138 ya kanuni za kudumu za Bunge .

Kanuni anayotaka mwandishi huyu (Afisa wa Umma) itumike yaani ile ya 5 ambayo kimsingi ni kukata rufaa kwa kamati ya kudumu ya kanuni za Bunge , atakumbuka kuwa katika uhai wa Bunge la 10 chini ya Spika Anna Makinda na Naibu Spika Job Ndugai (Spika wa sasa) wabunge wa upinzani waliitumia sana na hasa wabunge wa CHADEMA kama John Mnyika na Tundu Lissu , ila kwa kipindi chote cha miaka 5 ya uhai wa Bunge hilo kamati hiyo haikuwahi kuitishwa ili kujadili na kutoa uamuzi juu ya mashauri/ malalamiko zaidi ya 12 yaliyokuwa yamewasilishwa kwenye kamati hiyo yaliyokuwa yanamhusu Spika na Naibu Spika. Leo anataka kuushawishi umma kuwa wabunge waendelee kutumia kanuni hiyo hiyo katika kushughulikia hili la sasa la naibu Spika Tulia.

Ni vyema pia ikawekwa wazi hapa kuwa mwandishi wa makala hiyo kama mtumishi wa umma ana wajibu wa kutokuegemea upande wowote ule ili (Principle of neutrality) haki ionekane inatendeka na kuwa watumishi wa Bunge sio makada wa vyama bali ni watumishi wa umma ambao wanatakiwa kuwa tayari kufanya kazi na wabunge wote bila kuwabagua kwa misingi ya vyama vyao vya siasa na pia hawapaswi kufanya siasa bali ni kufuata na kusimamia misingi ya sheria za utumishi wa umma. Hali hii ikiachwa iendelee kumea miongoni mwa watumishi wa umma italigawa taifa na hasa utumishi wa umma katika misingi ya kiitikadi .

Dhana ya uwepo wa Vyama vya Upinzani ndani ya Bunge.

Ikumbukwe kuwa uwepo wa vyama vya upinzani ndani ya Bunge letu ni zao la katiba na sheria zetu na hivyo wabunge wa Upinzani ni sehemu muhimu sana ya Bunge letu kwani wamechaguliwa na wanawakilisha wananchi zaidi ya milioni 6 ambao waliwapigia kura kwenye majimbo mbalimbali nchini mwetu .

Dhana ya Upinzani na majukumu yake  ilianza tangu miaka  ya 1720 katika mfumo wa Kibunge wa Kiingereza uliojulikana kama “West- Minster”. Katika mfumo huo, Upinzani uliitwa“Her Majesty’s Loyal Opposition”. Dhana nzima ya kuwa na Upinzani katika Bunge ni kuhakikisha kuwa vyama ambavyo havikubahatika kuunda Serikali vinatoa changamoto kwa Sera na Mawazo mbadala  kwa  Chama kinachoongoza Serikali kwa uhuru na uwazi , bila kuonewa ama kuminywa kwa njia yoyote ile.

Neno Upinzani kwa maana pana linahusisha Upinzani kama linavyojieleza, pili linahusu upinzani kama dhana inayohusu majadiliano na shughuli zote zinazopingana na sera za wengi na serikali yao na kutoa mtazamo mbadala. Lakini kwa dhana nyingine sio kwamba Upinzani ni lazima upinge sera za wengi na Serikali yao, ila chama cha upinzani kinaweza kuamua kuunga mkono sera za chama chenye wengi kwa makubaliano maalum. Ufafanuzi huu wa neno Upinzani ulitolewa katika taarifa ya “The Role of the Opposition in Democratic Parliament” iliyowasilioshwa katika Bunge la Ulaya (Venice Commission 84th Plenary Session Venice 15-16 October, 2010).

Taarifa hiyo inaendelea kueleza kwamba, Kazi ya Upinzani katika jamii ya Kidemokrasia  ni dhana pana sana ambayo maandiko na tafiti nyingi zinaonesha kuwa imejikita kwenye kiini cha Demkokrasia ambacho kwa miaka kadhaa imekuwa ni mjadala mpana kwa wanataaluma wa siasa na mambo ya katiba na mapendekezo kadhaa yamekuwa yakitolewa.

Kwa mujibu wa maafikiano (Resolution) namba 1601 ya mwaka 2008 ya Venice Commission kwa tafsiri isiyo rasmi yanasema kwamba uwepo wa Upinzani wa Kisiasa ndani na nje ya Bunge ni kipengele muhimu katika mfumo wa kidemokrasia unaofanya kazi zake vizuri

Aidha, moja ya haki za Upinzani Bungeni ni haki ya kuzuia au kuchelewesha maamuzi ya walio wengi yasifanyike. Kwa hali ya kawaida kwenye Bunge la Kidemokrasia haki hii haiwezi kufanyika kwa kushikana mashati au kupigana bali haki hii itatekelezeka kwa kuwa na hoja za msingi. Na kwa njia hii ndio njia pekee inayoweza kuzuia ubabe wa wengi katika kupitisha maamuzi kandamizi dhidi ya wachache.

 

Nihitimishe kwa kusema kuwa Upinzani ndani ya Bunge unahitajika sana na hasa katika wakati huu kuliko wakati mwingine wowote ule , ni haki ya wabunge wa upinzani kushinikiza kusikilizwa, Bunge linapaswa kuweka mazingira sawazishi na wezeshi kwa wabunge hawa kupata fursa sawa ya kutimiza majukumu yao. Yafaa ikafahamika kuwa walioko upinzani leo ndio watakuwa watawala kesho –Utumishi wa umma ni wa kudumu

Nawashauri watumishi wa Bunge wajiepushe na ukada na upotoshaji wa makusudi kwa masuala mbalimbali kwa vile tu yamefanywa au kusemwa na wabunge wa Upinzani .Haki itendeke kwa wabunge wote bila kujali itikadi za vyama vyao.

Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.

John Mrema –

Mkurugenzi wa masuala ya Bunge –CHADEMA

+255 758 144 555

Share Button
Layout Settings