MAJUKUMU YA WAKURUGENZI WA HALIMASHAURI-JE WALIOTEULIWA WANA WELEDI NA UWEZO WA KUYAMUDU

MAJUKUMU YA WAKURUGENZI WA HALIMASHAURI-JE WALIOTEULIWA WANA WELEDI NA UWEZO WA KUYAMUDU ?

Kutokana na uteuzi uliofanywa na Rais wa kuteua Wakurugenzi wa Halimashauri za Miji, Wilaya, Manispaa na Majiji kwa mujibu wa Katiba yetu, na kwa kuwa kwenye jamii kumekuwa na sintofahamu kubwa kuhusiana na weledi na uwezo wa wateule hawa na hasa kwenye mitandao ya kijamii jambo ambalo lilimpelekea hata Rais mwenyewe kulisemea jambo hilo wakati wateule hao walipokuwa wanakula kiapo cha uadilifu kwa utumishi wa umma .

Mjadala mkubwa zaidi ulitokana na aina ya watu ambao wameteuliwa kwani katika uteuzi huu wateule wengi ni makada wa CCM na ambao walishindwa katika kura za maoni za ndani ya chama chao katika uchaguzi wa mwaka 2015 na hata Rais katika hotuba yake alisema wazi kuwa hawezi kuteua watu ambao sio makada wa CCM kwani hawatatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM!

Nimeona ni vyema nikatumia kalamu yangu kuweza kuweka Majukumu ya wateule hawa kwa mujibu wa katiba na sheria na wakati jamii ikiendelea na mjadala juu ya weledi na uwezo wa wateuliwa hawa wakawapima kulingana na majukumu ambayo wamepewa kwa mujibu wa katiba ,sheria na kanuni mbalimbali za kuendesha Halimashauri

Nimeona kuwa ni vyema kuandika kwani hata Rais alipokuwa anazungumza nao alisema kuwa juu ya suala la uzoefu ,halina sababu za msingi kuwepo kwani wataupata uzoefu huo wakiwa kazini ,hapa ni kuwa alikiri kuwa wapo wateule ambao hawana uzoefu , ni hakika kuwa kwa mujibu wa majukumu yao huenda wengi wao wakapwaya na hata kushindwa kutimiza wajibu wao kwani majukumu wanayotakiwa kuyasimamia ni makubwa sana kwa mujibu wa katiba na sheria .

Majukumu kwa Mujibu wa Katiba.

Kwa mujibu wa Katiba ibara ya 146 (1) inasomeka kuwa “Madhumuni ya kuwapo serikali ya Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.Na vyombo vya serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa ujumla”

Hii maana yake ni kuwa wanatakiwa kuhakikisha kuwa hawafanyi ubaguzi wa kisiasa ama wa aina yoyote ile wakati wa kuwashirikisha wananchi katika kujiletea maendeleo yao, na wanaenda kufanya kazi kwenye maeneo ambayo yana viongozi wa kuchaguliwa na wananchi kama Wabunge na Madiwani kutoka vyama tofauti , na ijulikane wazi kuwa kama eneo Fulani wananchi wamemchagua Diwani kutoka CHADEMA maana yake ni kuwa walikubaliana na ilani ya Uchaguzi ya Chama husika kuwa ni bora zaidi kuliko ya vyama vingine ambavyo vilikuwa vinagombea nafasi husika.Hivyo ni wajibu wa Wakurugenzi husika kuheshimu maamuzi ya wananchi wakati wakitekeleza majukumu yao.

Aidha kwa mujibu wa ibara ya 146 (2) imeweka bayana majukumu ya kila chombo cha serikali za mitaa kwa mujibu wa sheria ilichokianzisha kuwa ni majukumu ya aina tatu ambayo ni pamoja na kutekeleza kazi za serikali za mitaa katika eneo lake,kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi na kuimarisha Demokrasia katika eneo lake na kuitumia demokrasia kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Hivyo ni wazi kuwa Wakurugenzi wanatakiwa kwa mujibu wa katiba kuhakikisha kuwa wanakuza demokrasia na kuitumia Demokrasia hiyo katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wa eneo husika .Hali ni hiyo hiyo kwa wakuu wa Mikoa na Wilaya wanatakiwa kutekeleza Katiba kwa vitendo , ndio maana huwa nashangaa sana ninapowasikia Baadhi ya wakuu wa Mikoa na Wilaya wanapokuwa wakitoa kauli za kibabe na maagizo , huwa ninajiuliza hawajui juu ya ibara hii ya katiba au wanaamua kufanya makusudi kwa malengo ambayo wanayataka wao.

Ninafikiri kuna haja ya semina elekezi kwa wateule hawa na somo kuu liwe ni kuhusu umuhimu wa kuimarisha Demokrasia kwenye maeneo yao kwani bila demokrasia ni vigumu kuweza kupatikana kwa maendeleo ya kweli, na hasa ikizingatiwa kuwa hili ni jukumu la kikatiba ambalo wanatakiwa kulitekeleza kwa ukamilifu wake .

Kazi na Majukumu ya Mkurugenzi wa Halimashauri

Majukumu na kazi zote za Halmashauri hufanywa na watendaji wa Halmashauri. Hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri akiwa ndiye Mtendaji Mkuu na Afisa Masuuli wa Halmashauri anawajibika kuhakikisha kuwa majukumu na kazi zote za halmashauri zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia maelekezo na mipango ya Halmashauri husika

Kwa msingi huu na kwa kuzingatia maelekezo ya Katiba na Sheria mbalimbali zinazo simamia utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri, majukumu na kazi za Mkurugenzi zimegawanyika katika makundi yafuatayo;-

  1. Majukumu na kazi za kisheria
  2. Majukumu na kazi za kiutawala
  • Majukumu na kazi za ukatibu
  1. Majukumu na kazi za kifedha

Majukumu ya Mkurugenzi kisheria

Sheria imempa Mkurugenzi wa Halmashauri madaraka ya kuwa msimamizi wa usalama na amani katika eneo la Mamlaka ya Halmashauri hii ni kwa mujibu wa  kifungu cha 51(1) na (4) cha Sheria ya Mahakama za mahakimu Na. 2 ya 1984.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, Mkurugenzi ni Mlinzi wa Amani na kama Mlinzi wa Amani katika eneo lake anao uwezo wa Kuendelea kumweka ndani mtu ambaye tayari amewekwa ndani na Hakimu wa Wilaya, Kuendeleza dhamana ya mtu yeyote ambaye amepewa dhamana na Hakimu wa Wilaya na Kumweka ndani ya gereza, korokoni au mahali pengine penye usalama kwa wakati wowote mtu aliyekamatwa bila hati ya kukamatia kwa muda usiozidi siku saba ili mradi jumla isizidi siku 28 n.k.

Hata hivyo, kutokana na kuwepo Mahakimu wengi zaidi sasa kuliko wale waliokuwepo wakati sheria ilipotungwa mwaka 1963 na kufutwa na kutungwa upya katika mwaka 1984 na pia, kutokana na kuwepo vituo vya Polisi na Askari Polisi wengi zaidi kuliko ilivyokuwa wakati sheria inatungwa haitegemewi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ataapishwa na kusimikwa na Hakimu wa Wilaya kuwa mlinzi wa amani Wilayani katika karne hii ya sasa japo sheria inatambua jukumu hilo .

Kwa mujibu wa Kifungu cha 177(1) cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na Kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura 288 Mkurugenzi, kama Mlinzi wa Amani, amepewa kisheria uwezo wa kukamata mtu yeyote anayevunja Sheria Ndogo ya Halmashauri bila hati ya kukamata.

Ni kutokana na mamlaka hii ya kukamata ndio maana kwenye Halimashauri mbalimbali utakuta kuna jeshi la Mgambo ambalo lipo chini ya mamlaka ya Mkurugenzi na ambalo linamtii yeye moja kwa moja na kuwajibika kwake ili aweze kutumia mamlaka yake ya kukamata bila kutakiwa kuwa na hati ya mahakama ya kukamata. Ni kutokana na sheria kama hii ndio maana Mkurugenzi hatakiwi kabisa kuwa kada wa chama chochote ili atakapokuwa akitumia mamlaka yake hii kwa mujibu wa sheria asionekane kuwa anatenda kwa sababu za kiitikadi , ndio maana wanatakiwa kutokuwa na upendeleo wakati wa kufanya maamuzi (principle of neutrality).

Mkurugenzi anatakiwa chini ya Sheria ya Uthamini wa Mali zilizoko Mjini (Urban Authorities Rating Act) ya mwaka 1983 iwapo mwenye mali akikataa kulipa kodi anayodaiwa katika muda wa siku kumi na nne, kutoa waranti kwa “Court Broker” akimtaka akamate mali binafsi za huyo mhusika zenye thamani ya kodi anayodaiwa.

Kifungu hiki cha sheria natambua kuwa katika mwaka huu wa fedha (2016) kimepunguzwa sana nguvu baada ya serikali kuu kuamua kukusanya kodi ,ushuru na tozo mbalimbali kwenye Halimashauri kwa kutumia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) , japo nasubiri kuona kanuni za utekelezaji wa sheria mpya ya fedha ya mwaka 2016 na kuona utekelezaji wake utakavyokuwa.

Mkurugenzi huweka saini nyaraka mbalimbali za Halmashauri, k.m. mikataba chini ya  Kifungu cha 200 Sura 287 na kifungu 117 cha Sura 288, hii maana yake ni kuwa  Mkurugenzi wa Halimashauri amepewa wajibu mkubwa sana ndani ya Halimashauri wa kusaini mikataba kwa niaba ya wananchi wa Halimashauri husika iwe ni kwa ajili ya uwekezaji ama miradi mbalimbali kama ya ujenzi wa Barabara , shule , miradi ya maji ,afya na kandarasi nyingine mbalimbali. Aidha Mkurugenzi huingia mikataba kwa niaba ya Halmashauri mikataba ya ajira za watumishi kwenye Halimashauri husika.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya anaagizwa na Sheria kwamba, akipata habari kuwa mtu yeyote katika eneo la Halmashauri ametenda kosa linalomfanya astahili kukamatwa bila hati ya kukamatia au hati ya kumkamata imetolewa, ana wajibu wa kumkamata mtu huyo bila kuchelewa na kumfikisha kwa Hakimu wa Mahakama yenye Mamlaka juu yake.

Kadhalika Mkurugenzi wa Halimashauri akipata habari kuwa kuna mali ya aina yoyote, ambayo imeibiwa nje au katika eneo la Halmashauri, na imehifadhiwa katika eneo lake la Halmashauri, anaagizwa kuhakikisha mali hiyo inakamatwa na kuhifadhiwa sehemu salama akisubiri amri ya hakimu mwenye Mamlaka katika suala hilo na atapaswa mara moja kutoa taarifa kwa Hakimu juu ya ukamataji na uhifadhi wa mali hiyo.

Mwisho ni kuwa Mkurugenzi wa Halimashauri amepewa uwezo kisheria wa kumwita mtu yeyote aishie katika eneo la Halmashauri ambaye kazi za Halmashauri zinamhusu afike kwake kwa madhumuni ya shughuli yoyote ya Halmashauri na iwapo mtu huyo atakataa kuja Mkurugenzi anaweza kuagiza akamatwe na kuletwa kwake.

Ni vyema ikaeleweka kuwa mamlaka hii ya kisheria isipotumiwa vizuri na Mkurugenzi wa Halimashauri inaweza kabisa kusababisha uonevu kwa baadhi ya watu na hata kusababisha uvunjifu wa amani katika halimashauri husika. Ikitokea Mkurugenzi akaamua kutumia mamlaka haya kukomoa watu kwa sababu za kisiasa ama sababu zozote zile ambazo wananchi wa eneo husika wanaona kuwa hazina msingi ni jambo la hatari kwa usalama wa eneo husika.

Ni kutokana na mamlaka haya makubwa ambayo Mkurugenzi amepewa kwa mujibu wa sheria zetu ndio yamenipelekea kufanya uchambuzi huu kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kujua kuwa uteuzi wa Wakurugenzi wa Halimashauri ni jambo kubwa na ambalo abadani isitokee wakateuliwa kwa sababu za kuwa ni makada wa vyama vya siasa na ambao wakiamua kutumia mamlaka yao vibaya wanaweza kusababisha uvunjifu wa amani na usalama kwenye maeneo yetu na kusababisha kurudisha nyuma maendeleo yetu kama Taifa.

Majukumu na kazi za Kiutawala

Mkurugenzi wa Halimashauri ana wajibu wa Kupokea na kusikiliza matatizo ,changamoto na au malalamiko ya wananchi kwenye Halimashauri husika na anawajibu wa kuzitafutia majibu ya kina changamoto hizo ama kwa kufanya moja kwa moja au kwa kuwaagiza wasaidizi wake  kuhakikisha kuwa matatizo ya wananchi yanapata ufumbuzi kwa uharaka .

Mkurugenzi ana wajibu wa Kuwa Afisa Uhusiano na Msemaji Mkuu wa maamuzi ya  Halmashauri, yaani Mkurugenzi ndiye msemaji Mkuu wa maamuzi na maazimio ya Halmashauri na iwapo atapotosha maazimio hayo ni yeye atakayechukuliwa hatua, kwa hiyo ni muhimu yeye mwenyewe kutoa taarifa katika vyombo vya habari au kwenye mikutano ya kiutendaji pamoja na maelekezo kwa watendaji wa Halimashauri husika.

Mkurugenzi ana wajibu wa kuitisha na kuendesha mikutano ya menejimenti ambapo mambo mbalimbali ya Halmashauri yatajadiliwa na kutolewa uamuzi. Mikutano ya menejimenti pia itakuwa na majukumu ya Kutayarisha rasimu za ajenda za mikutano ya Kamati  zitakazokutana kila mwezi ,taarifa na mapendekezo yatakayowasilishwa kwenye mkutano wa Halmashauri au Kamati ya Fedha, n.k.

Mkurugenzi ndiye Msimamizi Mkuu wa shughuli zote za Halmashauri hivyo anatakiwa kusimamia na kuratibu Idara zote za Halmashauri na kuratibu utekelezaji wa majukumu na kazi za Halmashauri. Katika kufanikisha haya anatakiwa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Idara zote za Halmashauri. Kusimamia na kudhibiti masuala yote ya Watumishi wa Halmashauri ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu kwa wakati na kwa mujibu wa sheria, Kubuni sera na mipango ya Maendeleo ya Halmashauri na Kusimamia na kutekeleza sera, mipango na maamuzi ya Halmashauri na kuhakikisha kazi za Halmashauri, hasa zile za msingi na za lazima, zinatekelezwa kwa mujibu wa Sera na Sheria .

Mkurugenzi ana wajibu wa Kushauriana na kujadiliana na Mwenyekiti/Meya wa Halimashauri mara kwa mara juu ya masuala mbalimbali ya Halmashauri hasa yale yanayoweza kuleta athari za kisiasa na mara nyingine kushauriana na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali katika eneo la Halimashauri husika ili kuhakikisha kuwa mfumo wa Serikali za Mitaa kwenye ngazi za jamii unafanya kazi na kuchukua hatua haraka.

Mkurugenzi wa Halimashauri ana wajibu wa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha kuwa anamshirikisha Mwenyekiti wa Halimashauri pamoja na Madiwani ili kujenga utulivu ndani ya Halmashauri kwani bila kuwashirikisha kikamilifu viongozi wa kisiasa ambao wamechaguliwa na wananchi na ndio wawakilishi wao katika Halimashauri husika.

Mkurugenzi wa Halimashauri kwa mujibu wa Sheria ni Katibu wa Mikutano ya Halmashauri na ana majukumu ya Kutayarisha ajenda ya mikutano ya Baraza/Kamati akimshirikisha Mwenyekiti/Meya wa Halmashauri au Mwenyekiti wa Kamati, Kutoa taarifa ya mikutano ya Halmashauri na ya Kamati kulingana na Kanuni za Kudumu za Halmashauri,anawajibika Kutoa au kutuma mihutasari na nyaraka mbalimbali kwa Madiwani na kwa Mkuu wa Mkoa na Wilaya kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Halimashauri

Mkurugenzi wa Halimashauri ana wajibu wa Kuandika mihtasari ya mambo yaliyojadiliwa kwenye mikutano mbalimbali ya Halimashauri nah ii ni kwa mujibu wa sheria  (Sheria Na. 7 na 8 za  1982 Vifungu 68 na 35),anatakiwa Kuhakikisha kuwa  muhtasari wa kila mkutano unasomwa na kuthibitishwa kwenye mkutano unaofuata na ana wajibu wa Kutunza rejesta ya matamko ya maslahi yatolewayo na Madiwani na Maafisa wa Halmashauri kwenye mikutano ya Halmashauri na Kamati zake chini ya Kanuni ya 16(1) ya Kanuni za Maadili ya Madiwani za mwaka 2000.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 33(4) cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 kinamtaja Mkurugenzi wa Halmashauri kuwa Afisa Masuuli (Accounting Officer). Kisheria kazi ya Afisa Mhasibu ni kuhakikisha yeye binafsi kuwa fedha za umma zilizo katika fungu lake zinakusanywa kikamilifu, zinatunzwa kwa usalama na matumizi ya fedha yanafanywa kwa njia halali na kwa mujibu wa bajeti ya Halmashauri .

Kwa ujumla ni kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri, akiwa kama Mtendaji Mkuu wa Halmashauri, ana madaraka na uwezo mkubwa kisheria, kiutawala na kifedha. Hata hivyo, madaraka haya hayana maana kuwa Mkurugenzi atafanya anavyotaka yeye bali atafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na desturi za Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Pamoja na mamlaka haya ya wakurugenzi haitegemewi kuwa wataenda kufanya majukumu yao bila kushirikisha Baraza la Madiwani ambalo kisheria ndio lenye wajibu wa kupanga na kuamua juu ya Halimashauri zao na wao wanaowajibu wa kumsimamia Mkurugenzi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku na kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa majukumu ya mipango na bajeti ya Halimashauri.

 

HITIMISHO .

Ni mategemeo yangu kuwa wakurugenzi hawa wapya ambao wengi wao ni makada ambao walishindwa kwenye kura za maoni za CCM kwenye majimbo mbalimbali ya uchaguzi nchini watatakiwa kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi na sio kwa mujibu wa katiba ya chama chao .

Wakurugenzi hawa nashauri kuwa wapatiwe mafunzo au semina elekezi maana wapo watu ambao wameteuliwa hawajawahi hata kushika ofisi ya umma na wengine wao ukiwauliza utaratibu wa kiserikali wa kufanya maamuzi wanakuwa hawaujui na hata ukiwauliza wengine nini maana ya Dokezo au dokezo sabili watashindwa kukuelezea kwani hawajawahi kufanya majukumu ya kiserikali achilia mbali kusimamia ofisi na Bajeti kubwa kama ambavyo sasa wanaenda kufanya majukumu hayo.

Ni vyema pia ikaeleweka kuwa Mkurugenzi anapaswa kutii maagizo ya halmashauri hata kama hakubaliani nayo iwapo maagizo hayo si kinyume na Sheria. Pale ambapo maagizo yanavunja sheria, kanuni na taratibu, Mkurugenzi anatakiwa kutoa taarifa kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na sio kutumia ubabe au kukataa kwa sababu tu yeye ni mteuliwa wa Rais, wanapaswa kukumbuka kuwa katiba inawataka wakaimarishe demokrasia kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

Ni vyema ikaeleweka pia kuwa jukumu la kusimamia chaguzi za kisiasa sio la kisheria kwa wakurugenzi ila hawa ni watu ambao tume ya taifa ya uchaguzi inawapa mamlaka hiyo na kusimamia kwa niaba ya tume . Ila kutokana na uteuzi huu wa wakurugenzi ambao haukuzingatia kanuni za utumishi wa umma bali umezingatia makada ,Tume ya Uchaguzi lazima sasa ijitazame na kuwa na waajiriwa wake kwenye ngazi za Halimashauri ili waweze kusimamia uchaguzi na waonekane kuwa hawa ni watu ambao sio makada .

Tume ianzishe mchakato na wadau wa kisiasa ili kuanza kujipanga mapema katika kuwezesha uwepo wa uchaguzi huru na haki ambao hautakuwa ukiendeshwa kwa misingi ya kisiasa, na hili ni vyema liwe sasa kwani sioni Katiba mpya ikipatikana kabla ya 2020 na hasa ikizingatiwa kuwa mikutano ya kisiasa imeshapigwa marufuku na hizi ni dalili kuwa hapatakuwa na kura ya maoni kuhusu katiba kwani itahusisha kampeni za mikutano ya kisiasa ! Nawaza tu kwa sauti katika hili

Nahitimisha kwa kuwataka watanzania wenzangu wote tuwapime Wakurugenzi hawa kwa mujibu wa majukumu yao waliyopewa kwa mujibu wa katiba na sheria na tuone kama watayaweza au laa kwani Rais alishatuambia kuwa kama ni uzoefu basi watakutana nao kazini .

John Mrema

Share Button
Layout Settings