MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI-MHESHIMIWA PASCHAL YOHANA HAONGA (MB), WIZARA YA KILIMO KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA AFYA YA MIMEA WA MWAKA 2020 (THE PLANT HEALTH ACT, 2020)

(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la mwaka 2016)

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu na kuweza kusimama mbele ya Bunge hili, ili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu mapendekezo ya Serikali kuhusiana na muswada wa afya ya mimea wa mwaka 2020.
  3. Mheshimiwa Spika, pia kwa unyenyekevu mkubwa ni washukuru waheshimiwa wabunge wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani ambao kwa umoja wetu tulijadili na kukubaliana kuhusu kujitenga na Bunge hili hadi pale suala zima la usalama wa wabunge litakapopewa kipaumbele kinachotakiwa. Ninashukuru Bunge na Serikali wamezingatia jambo hilo.
  4. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii ni nafasi yangu ya Mwisho katika Bunge hili la kumi na moja(11) kusimama hapa mbele na kutoa maoni, hivyo kwa heshima kubwa naomba niwashukuru wananchi na wanachama na wapenzi wote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo popote walipo hapa nchini na hasa wale wa jimbo langu la uchaguzi la Mbozi kwa kutuvumilia na kuwa pamoja nasi kama chama na tunaomba wazidi kuwa na imani na sisi na tuendelee kushirikiana katika uchaguzi ujao na kuhakikisha nchi hii inakuwa katika himaya salama kwao na kwa maisha ya watoto wao na mali zao.
  5. Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa nitoe shukrani zangu za dhati kwa KUB Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kuniamini na kunikabidhi kusimamia wizara ambayo inalisha watanzania takribani milioni 56 na kutoa ajira kwa takriban watanzania asilimia 67. Na pia kuchangia katika pato la taifa kwa asilimia 27.
  6. Mheshimiwa Spika, afya ya mimea inaendana na utafiti, lakini hali halisi ni kuwa kumekuwa na Uhaba mkubwa  wa fedha katika Vituo vya Utafiti ni tatizo la muda mrefu, fedha zao nyingi za utafiti hupatikana toka kwa wafadhili tu.  Hoja ya msingi ya kujiuliza ni kwa kiasi gani tamko la serikali  la asilimia moja (1%) ya pato la taifa kupitia COSTEC zinawafikia/zinagawiwa kwa watafiti wa Wizara ya kilimo.
  7. Mheshimiwa Spika, taarifa ya Wizara inasema kuwa Serikali imeendelea kushirikiana na Taasisi za ndani na nje ya nchi, Vyuo Vikuu na Mashirika mbalimbali ambapo imesaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) 23 zenye bajeti ya thamani ya shilingi 11,987,842,280 kwa ajili ya masuala ya utafiti wa kilimo nchini; kati ya fedha hizo ni kiasi gani kinaelekezwa kwenye afya ya mimea?
  8. Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa utangulizi huo, sasa naomba kurejea kwenye hoja iliyo mbele yetu.

 

  1. MAPITIO YA MUSWADA
  2. Mheshimiwa Spika, Muswada huu unapendekeza kutungwa kwa Sheria ya Afya ya Mimea ya mwaka 2020. Lengo la Sheria pendekezwa ni kuunganisha Sheria ya Hifadhi ya Mimea, Sura 133 na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kitropikia (TPRI), Sura 161 ili kuweka mfumo wa pamoja wa kisheria ambao utasimamia hifadhi ya mimea na viuatilifu. Vilevile Muswada huu unapendekeza kuanzisha Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu kama chombo kikuu cha usimamizi wa hifadhi ya mimea, udhibiti wa viuatilifu, kuweka masharti ya kusimamia uhifadhi wa afya ya mimea, kuzuia, kuingiza na kuenea kwa visumbufu, udhibiti wa usafi wa mimea, udhibiti wa viuatilifu, udhibiti na usimamizi wa majaribio ya ufanisi wa viuatilifu, kuwezesha biashara ya mimea na mazao ya mimea pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo kufanyika kwa ufanisi na kwa ushindani
  3. Mheshimiwa Spika, muswada huu wa sheria unaua Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kitropikia (TPRI), ili kuunda chombo kipya kitakachokuwa na mamlaka ya kusimamia majukumu yaliyokuwa yanafanywa na TPRI na majukumu mapya ya afya ya mimea.
  4. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa afya ya mimiea kama muswada unavyosema ni jambo kubwa ambalo sio tu la viuatilifu bali pia linahusisha na mbegu zinazotumika katika uzalishaji mashambani. Tunaposema kuhusu mbegu maana yake ni kuhusu uzalishaji wa mbegu unasimamiwaje au mbegu zinazoingizwa toka nje ya nchi ubora wake kwa mazingira yetu ya kijamii na kiuchumi yamezingatiwa kwa kiwango gani?
  5. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira duniani UNEP linasema mimea ni chanzo kikubwa cha hewa tuvutayo na asilimia kubwa ya chakula tunachokula, lakini changamoto imekuwa ni kupuuza kuhakikisha mimea hiyo iko katika afya bora na kuweza kuzalisha zaidi.
  6. Mheshimiwa Spika, aidha, shirika la FAO linasema inaweza  kuwa na athari mbaya sana, likikadiria kwamba hadi asilimia 40 ya mimea ya chakula hupotea kila mwaka kutokana na magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea.  “Afya ya mimea zaidi na zaidi iko katika tishio. Mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu vimemomonyoa mfumo wa maisha, kupunguza bayoanuai na kuweka mazingira mapya ambayo wadudu wanashamiri.”
  7. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa suala hili la afya ya mimea kwa jumla wake ni suala la kibiashara, suala la usalama wa nchi, pale madawa yasipokuwa katika mikono salama ya watumiaji. Aidha ni suala mtambuka linapohusisha mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu.
  8. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema hayo kwa kuangalia ukweli uliopo sasa wa uzalishaji wa mbegu ambapo mbegu zetu nyingi za asili zimepotea hasa mbegu kwa ajili ya uzalishaji wa matunda na mboga mboga na zinazoletwa na makampuni makubwa toka nje ni zile zinazotumika kwa mpando mmoja tu.
  9. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa matumizi ya viuatilifu (pesticides) husababisha baadhi ya mimea kupotea kabisa katika uso wa dunia na mimea mingine kubadilika mfumo wake wa vinasaba hivyo kukosa uhalali wa kuzalisha kama ulivyokuwa unazalisha mazao. Pia matumizi haya ya viuatilifu inafanya kilimo chetu kutoka kuwa kilimo hai (organic agriculture) ambacho sasa kinatiliwa sana mkazo katika ulimwengu wa sasa na kuingia kwa nguvu katika “kilimo cha madawa”. Kwa kuwa kupanga ni kuchagua basi kama taifa tutaingia huko kwenye Inorganic Agriculture japokuwa bado tunasuasua kutokana na wakulima wetu kutokuwa tayari kiuelewa.
  10. Mheshimiwa Spika,katika muktadha huo wa mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu kutaka kubadilisha Genetic make up ya mimea yetu na kutoa kitu ambacho kwa uhalisia wake wakulima wetu wanalazimika kupoteza hazina yao ya asili ya mimea na mbegu na hivyo kadri muda unavyopita wanazidi kuwa tegemezi kwa wazalishaji wa hizo mbegu au mimea. Hii ndiyo sababu kubwa ya kusema kuwa hiki kitu afya ya mimea kinaweza kuwa na pande mbili ambazo ni kwa uzuri na ubaya.
  11. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inajaribu kutoa tahadhari kwa upande ambao Serikali haitaki kuuonesha ili tunapotunga sheria hii tuwe na uelewa mpana na wa pamoja katika kulinda afya ya mimea yetu.
  12. Mheshimiwa Spika UNEP na FAO wanasisitiza kwamba kulinda mimea dhidi ya wadudu na magonjwa ni zaidi ya kukabiliana na dharura kubwa ya afya ya mimea na kutaka kila mtu, kila nchi na wadau wote kuchukua hatua kuhakikisha afya ya mimea inalindwa. Hili ni kweli kabisa lakini suala la mbegu zetu za asili ambazo zinabadilishwa vinasaba ili ziendane na matakwa yao ya kibiashara, kiusalama au ya kisiasa muswada huu haukuangalia katika muktadha huo.
  13. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa afya ya mimea ni zaidi ya magonjwa na wadudu pamoja na madawa yanayotumika ili kuhakikisha uzalishaji wake. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa afya ya mimea inaanzia kwenye utengenezaji wa mbegu na vipando ili kuwa na uhakika wa usalama wa mimea husika.
  14. Mheshimiwa Spika, kitendo cha Muswada kutokuzingatia uhalisia wa kuwa Tanzania tunajitosheleza kwa mbegu kwa asilimia chini ya 45 tu na asilimia iliyobakia inategemea kutoka nje ya nchi. Usalama wa mbegu hizo kwa muktadha wa Tanzania ukoje? Kwani mimea (mbegu na vipando) inaweza kuwa na afya lakini usalama wake katika muktadha wa wakulima wetu na mimea yao ya asili uko vipi?
  15. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inafahamu kuwa kuna sheria mahususi inayohusina na uzalishaji wa Mbegu na pia Bunge limekwisha ridhia mikataba ya Kimataifa inayohusina na wagunduzi wa mbegu mpya, Lakini sheria hizo na mikataba hiyo haiangalii ubadilishwaji wa vinasaba kwa mimea hiyo inayozalishwa na hivyo afya nzima ya mimea na usalama wake kwa muktadha wa mazingira yetu haviangaliwi.
  16. Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye tafsiri ya maneno, “phytosanitary action” means an official operation, such as inspection, testing, surveillance or treatment, undertaken to implement phytosanitary measures; Kwa maana hii ni kuwa hapa hakuna kuhusika na usalama wa mbegu kwa upana wake na mamlaka zinazohusika na mbegu hazihusiki na usalama wake.
  17. Mheshimiwa Spika, ukiangalia tafsiri ya neno “plant” means any living plants or the parts thereof, including seeds and germplasm; na ukiangalia kifungu cha 21 cha muswada, kinachohusu uagizaji wa mimea kutoka nje; “A person who imports plants, plant products, pesticides or regulated articles shall apply for an import permit in a manner prescribed in the regulations.”
  1. Mheshimiwa Spika, hapa hakuna sehemu inayoonesha kuwa mamlaka inatakiwa kuhakikisha afya ya mimea hiyo inayoingizwa kutoka nje kwa kuangalia genetic makeup yake kama imebadilishwa au vipi. Kifungu cha 23 kinahusu kuzingatiwa kwa kanuni za usafi wa mimea husika,kwa ujumla Kambi Rasmi ya Upinzani inaona litakuwa ni jambo la busara kama Mamlaka hii mpya ya  “Tanzania Pesticides and Plant Health Authority” au kwa kifupi TPPHA pamoja na majukumu yake kama yanavyoainishwa katika muswada pia wangefanya kazi ya kuhakiki mbegu na vipando ambavyo usalama wake sio mzuri kwa mimea ya asili, kwani zinakuwa zimebadilishwa mfumo mzima wa vinasaba vyake na hivyo kuwa rahisi kuharibu kabisa uotaji wa mimea ya asili katika eneo husika.
  2. Mheshimiwa Spika, tunasema haya yote kwa ukweli kuwa sasa hivi kuna mbegu zote ambazo zimeandikwa F-1 hizi maana yake ukishazipanda huwezi pata mbegu kwa ajili ya kupanda tena, inakulazimu ukanunue mbegu upya ili upande. Je ni mazao mangapi ambayo yanahitaji mbegu zikishapandwa katika msimu mmoja inakulazimu kununua mbegu upya na uwezi kuchagua mbegu na kuhifadhi kutokana na mavuno?
  3. Mheshimiwa Spika, tunaamini kabisa Tanzania ina wataalam wengi sana katika sekta hii ya utafiti hasa wa madawa, wadudu lakini katika eneo la ugunduzi wa mbegu na vipando, taaluma inayotumika sana ni ile ya “cross breeding” nasio ya kufanya “genetic modification- kama inavyojulikana kama GMO”. Hivyo basi ni rai yetu kuwa pamoja na uzuri wa muswada huu lakini afya ya mimea ni zaidi ya madawa na wadudu ni muhimu pia tukaangalia usalama wa mimea kwa wananchi wetu ambao takriba asilimia 85 inategemea kilimo.
  4. Mheshimiwa Spika, hoja yetu hapo msingi wake ni kutokana na majukumu ya mamlaka (functions and powers of the Authority) kifungu cha “5(1)(b) surveillance of growing plants, including both areas under cultivation and wild flora and of plants and plant products in storage or in transportation, particularly with the object of reporting the occurrence, outbreak and spread of pests, and of controlling such pests”.

Hapo inaonesha kuwa kazi ya uthibiti inahusisha maeneo mengi ya mimea na bidhaa za mimea.

 

  1. Mheshimiwa Spika,katika tafsiri ya maneno, neno “infestation” means presence in commodity of a living pest of the plant products concerned- katika hili mbegu au vipando vilivyobadilishwa vinasaba vinaweza kuwa navyo ni hatari kwa mimea yetu ambayo haijafanyiwa marekebisho ya vinasaba na hivyo kuharibu kabisa afya ya mimea ya asili na hivyo kuleta taharuki kubwa katika jamii. Jambo hili linatakiwa nalo lishughulikiwe na Mamlaka hii ya “TPPHA”
  2. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa viwango vya kimataifa kuhusu afya ya mimea kama vilivvyo kubaliwa na “Commission on Phytosanitary Measures (CPM)”, ambayo ni bodi  ya kimataifa inayolinda  na kusimamia mkataba wa kimataifa wa kulinda mimea “International Plant Protection Convention (IPPC)” uliosainiwa na nchi 184 duniani.  Vigezo au viwango hivyo vilivyowekwa na kukubalika na mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania mwaka 1993, ni kwamba; kulinda na kuwa na kilimo endelevu na hivyo kuondokana na uhaba wa chakula duniani; kulinda mazingira , misitu na bioanuai kwa ujumla na mwisho ni kuendeleza uchumi na biashara kwa ujumla wake.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo wa viwango vya kimataifa kuhusuiana na afya ya mimea ni dhahiri kwa nchi yetu bado hatujafikia uko, kilimo cha kisasa na endelevu kama ambavyo dhima ya Sera yetu ya kilimo inavyosema, maana yake ni matumizi bora ya mbolea na viuatilifu ambavyo havina madhara yoyote kwa ardhi na mimea mingine na pia katika uhifadhi wa mazingira.
  4. Mheshimiwa Spika, katika hoja hiyo ni kuwa matumizi ya viautilifu bila ya kuwa na uelewa sahihi wa madhara yake kwa eneo, wadudu ambao hawakuwa katika mpango wa kuangamizwa au mimea mingine ambayo haikutakiwa kuangamizwa ni shida kubwa na hivyo kuondoa dhana nzima ya afya ya mimea kwa kutumia kemikali.
  5. Mheshimiwa Spika, viuatilifu vingi vina madhara makubwa kwa afya ya watumiaji, na hivyo ni chanzo kikuu cha magonjwa yasiyoambukizwa kama vile cancer kutokana na uvutaji wa hewa yenye sumu ya viuatilifu, na pia pengine kupoteza kabisa uwezo wa kuona. Jambo hili ni muhimu sana likatiliwa mkazo kwa kuangalia hali halisi ya watanzania ambao wanajihusisha katika kilimo kama ndio shughuli yao ya kila siku. Kwa muktadha huo Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kuwa kunatakiwa kuwepo na pesticides risk analysis kama ambavyo kuna pests risk analysis inavyofanyika ili kuepusha madhara ambayo watumiaji wanaweza kuyapata na pia nchi kwa ujumla wake.
  6. Mheshimiwa Spika, hoja yetu hapo juu msingi wake ni kifungu cha 16(b) cha muswada kinachosomeka kwamba; “the pesticide contains one or more active ingredients present in any pesticide already registered.” Kambi Rasmi ya Upinzani inafahamu kuwa viuatilifu vingi vina hicho kitu kinachoitwa kitaalam kuwa ni “active ingredient” na hiyo kitu ndiyo inapambana na “fungi, bacteria, herbs(magugu) au pests”
  7. Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kifungu cha 20 cha muswada kinachohusu matumizi ya viuatilifu, kifungu kidogo cha (2) kinasomeka kwamba; “(2)  A person shall not use, store, discharge, release, place or cause to be placed any pesticides in a manner likely to cause adverse effect to the environment. Sasa kwa muktadha wa kifungu hiki ni nani ataruhusiwa kutumia viuatilifu sasa, kwani wananchi wetu wanatumia kwa kadri walivyonunua ili kukidhi mahitaji yake, sasa hayo mahitaji yake yanaweza yasiwe yale yanayo shauriwa kitaalam na mwisho wake ikawa ni uharibifu wa mazingira. Kambi Rasmi ya Upinzani bado inasisitiza elimu ya kutosha kwa watumiaji na wataalam wa kutosha kwani madhara yanaweza kuwa makubwa mno kuliko makusudio ya matumizi.  Au kifungu hiki ni mtego wa panya kwa watumiaji wa viuatilifu, kwani mazingira ya uhifadhi wake yanaweza kutumiwa na mamlaka kutengeneza makosa na hivyo sheria kuchukua mkondo wake.
  8. Mheshimiwa Spika, muswada huu wa sheria ya afya ya mimea kwa upana wake unahusisha pia afya ya wanadamu kwani wao ndio wahusika wakuu katika kuhakikisha afya ya mimea inakuwepo. Hivyo basi, ni muhimu sana taasisi zingine zinazojihusisha na afya za binadamu zikahusika pia kwani suala hili ni mtambuka.
  9. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache kuhusiana na muswada huu, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.

……………………………….

PASCAL YOHANA HAONGA (MB)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI-WIZARA YA KILIMO

19.05.2020

Share Button