MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU AZIMIO LA BUNGE LA KURIDHIA MKATABA WA KIMATAIFA WA VIWANGO VYA MAFUNZO NA UTOAJI VYETI KWA WAFANYAKAZI WA VYOMBO VYA UVUVI WA MWAKA 1995 (INTERNATIONAL CONVENTION ON STANDARDS OF TRAINING, CERTIFICATION AND WATCHKEEPING FOR FISHING VESSEL PERSONNEL, 1995)

___________________

 

 1. UTANGULIZI
 2. Mheshimiwa Spika,Kwa mujibu wa Kanuni ya 53(6) (c), naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Viwango vya Mafunzo na Utoaji Vyeti kwa Wafanyakazi wa Vyombo vya vya Uvuvi wa Mwaka 1995.
 3. Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni hayo, naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, aliye chimbuko la uhai wa viumbe vyote; kwa kunijalia uhai na afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge hili, kuwasilisha maoni ya Upinzani kuhusu Azimio lilipo mbele yetu.
 4. Mheshimiwa Spika,Kwa kuwa bado tupo katikati ya janga la Corona, napenda kutumia fursa hii pia kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuwakumbusha wananchi wote kwamba; janga hili bado lipo, hivyo waendelee kuchukua tahadhari zote za kujikinga, kama inavyoelekezwa na wataalam wa afya. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kuwafariji, kuwatia moyo na kuwaombea wale wote waliopata athari za moja kwa moja za COVID -19, kwa kuugua wao wenyewe, kuuguliwa na au kufiwa na wapendwa wao; ili Mwenyezi Mungu awaponye na pia kuwapa pumziko la milele wale wote walioaga dunia kwa janga hili popote duniani.
 5. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba sasa nijielekeze kwenye hoja iliyoletwa na Serikali ya Kuliomba Bunge liazimie kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Viwango vya Mafunzo na Utoaji wa Vyeti kwa Wafanyakazi wa Vyombo vya Uvuvi wa Mwaka 1995.
 1. MAONI YA JUMLA KUHUSU AZIMIO
 2. Mheshimiwa Spika, Azimio hili linatufunza jambo moja kubwa sana; Kwamba; Tanzania sio kisiwa. Na kwa kuwa Tanzania sio kisiwa; ni lazima iendane mfumo wa dunia (The World Order) na mifumo mingine changamano ya kimataifa (Global Intergrated Systems) ili iweze kuendelea kuwepo katika dunia ya utandawazi na ushindani.
 3. Mheshimiwa Spika, mara kadhaa Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikieleza katika hotuba zake kuwa, mahusiano ya kimataifa kupitia mikataba na itifaki mbalimbali ni jambo lenye afya kwa usitawi wa mataifa husika kama ilivyo muhimu kwa viumbe hai kutegemeana kupitia Ikolojia (Symbiosis) ili viweze kuendelea kuishi.
 4. Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba sisi ni Taifa huru lenye mamlaka kamili (Sovereign State); lakini uhuru huo hauna maana kwamba tunajua kila kitu au tunaweza kila kitu. Yapo mambo ambayo ni lazima kushirikiana na mataifa mengine ili tuweze kuwa bora zaidi.
 5. Mheshimiwa Spika, kimsingi Mkata huu ambao Bunge linaombwa kuuridhia; una maudhui mazuri kwa kuwa utawafanya wananchi wetu ambao ni wafanyakazi wa vyombo vya uvuvi,  kuwa na viwango vya kimataifa na hivyo kuwa na ushindani katika soko la ajira la kimataifa. Aidha kifungu cha tisa (9) cha Mkataba huu kinatoa fursa kwa nchi wanachama kuomba kupatiwa msaada wa kitaalam (technical assistance) kutoka Shirika  la Bahari Duniani (International Maritime Organization – IMO) kuhusu masuala kadhaa ya msingi kama vile:-
 6. Mafunzo ya wafanya kazi katika ngazi ya uongozi na utaalam
 7. Kuanzisha vyuo vya mafunzo ya wafanyakazi wa vyombo vya uvuvi
 • Kutoa vifaa na nyenzo nyingine za ufundishaji katika vyuo vya mafunzo.
 1. Uandaaji wa Programu za Mafunzo za kutosha ikiwa ni pamoja na Mafunzo kwa Vitendo juu ya Vyombo vya Uvuvi Baharini
 2. Kusaidia mbinu na mikakati mingine kwa ajili ya kukuza weledina ufanisi wa wafanyakazi wa vyombo vya uvuvi; hasa kwa misingi ya kitaifa na kikanda kwa ajili ya kufikia malengo ya Mkataba; na kwa kutilia maanani ya mahitaji maalum ya nchi zinazoendelea.
 1. Mheshimwia Spika, pamoja na fursa hizo; yapo mambo kadhaa ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kuyazingatia:- Mambo hayo ni kama ifuatavyo:-
 2. Kuleta Bungeni Muswada waSheria ya Kusimamia Utekelezaji wa Mkataba.
 3. Mheshimiwa Spika, Tanzania imeridhia mikataba na itifaki nyingi za kimataifa. Hata hivyo, Serikali imekuwa haitekelezi mikataba hiyo kutokana na kukosekana kwa sheria za ndani ili kutoa mwongozo wa utekelezaji wa mikataba husika. Jambo hilo halina afya kwa mahusiano yetu kimataifa na pia halina afya kwa ustawi wetu wa ndani. Nasema hivi kwa sababu; kukwepa uwajibikaji wa ndani kwa kushindwa kufuata masharti ya mikataba ya kimataifa ni kuwadhulumu wananchi ambao wanalindwa na mikataba hiyo. Kwa hiyo, ili tuweze kuwa sehemu yenye tija katika   Jumuiya ya Kimataifa katika jambo hili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri na kupendekeza kwamba; Serikali ilete haraka iwezekanavyo Muswada wa Sheria ya Kusimamia utekelezaji wa makataba huu kama Ibara ya 63(3)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 
 4. Ukamataji na Udhibiti wa Vyombo vya Uvuvi vilivyokiuka Masharti ya Mkataba
 5. Mheshimiwa Spika, kifungu cha nane (8) cha Mkataba huu kinatoa masharti kwamba Chombo cha Uvuvi cha nchi mwanachama wa mkataba huu kitakapokuwa kwenye Bandari ya nchi mwanachama mwingine; basi kitakuwa chini ya ukaguzi na udhibiti wa maafisa wa mamlaka za nchi hiyo ili kuthibitisha kama wafanyakazi wa chombo hicho wamekidhi viwango vya mafuzo vilivyoanishwa na Mkataba huu.
 6. Mheshimwa Spika, kifungu hiki kinaendelea kueleza kwamba, ikiwa wafanyakazi watagundulika hawajakidhi vigezo vya mkataba huu na ikaonekana kuendelea kwao kufanya kazi kunaweza kusababisha madhar kwa watum mali na mazingira basi watachukua hatua ya kukishikilia chombo hicho na kuhakikisha kwamba hakiendi kokote mpaka masharti na vigezo vilivyowekwa na Mkataba huu vitakapotekelezwa. Unduly detained
 7. Mheshimiwa Spika, kifungu hiki kimetoa masharti kwamba ikiwa chombo kitakamatwa kutokana na kutokidhi masharti ya mkataba huu, basi ukamataji huo lazima ufanyike kwa namna ambayo hautaathiri chombo na au kusababisha ucheleweshaji usio wa lazima. Ikiwa ukamataji utafanyika kiholela na kukishikilia chombo bila sababu za msingi basi mkamataji atatakiwa kulipa fidia ya hasara kwa upotevu au uharibifu wowote unaotokana na ukamataji huo. 
 8. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imefanya rejea ya kifungu hicho ili kutoa angalizo kwa maafisa au mamlaka zitakazokuwa na jukumu la kukamata kuwa makini wasije wakaiingiza nchi kwenye hasara ya kulipa fidia kutokana na ukamataji wa kizembe! Kumekuwa na desturi ya kamamata kamata ya kiholela kwa ajili tu ya kujipatia umaarufu kwenye vyombo vya habari lakini mwishowe tunashindwa kesi nyingi na kulazimika kulipa mamilioni ya shilingi kama fidia jambo ambalo linaisababishia nchi hasara kubwa.
 9. Mheshimiwa Spika, Tuna mfano hai wa Meli ya Uvuvi iliyokamatwa na Samaki aina ya jodari maarufu kama Meli ya Magufuli; Meli iliozea baharini na samaki wakataifishwa lakini matokeo yake tulishindwa kwenye ile kesi na kulazimika kulipa fidia. Kifungu hiki kiwe fundisho na ndio maana tunasisitiza itungwe sheria ya kusimamia utekelezaji wa mkataba huu ili kusiwe na ukamataji holela. Na sheria itamke bayana ikiwa afisa au mamlaka iliyopewa jukumu la kukamata, itakamata kizembe,na kuisababishia Serikali hasara ya kulipa fidia basi mkamataji huyo au mamlaka hiyo iwajibishwe kutokana na uzembe huo.

 

 1. HITIMISHO
 2. Mheshimiwa Spika, mkataba huu utukumbushe kuwa sisi kama taifa ni Sehemu ya Jumuiya ya Kimataifa; na kwa sababu hiyo, ni lazima tushiriki na  tufuate mifumo ya Kimataifa ili tuweze kuendelea kuwepo katika dunia ya utandawazi.   Ili tuweze kuwa kweli sehemu ya Jumuiya ya Kimataifa ni lazima kuwe na dhamira ya dhati na  utashi wa kisiasa (political will) katika kutekeleza kikamilifu mikataba na itifaki mbalimbali za kimataifa. Hivyo, kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mikataba na itifaki hizo ni kilelezo cha dhamira njema na utashi wa kisiasa cha utekelezaji wa mikataba na itifaki hizo. Aidha, utungaji wa sheria hiyo, utasaidia kutoa mwongozo wa utendaji, na hivyo kuliepusha taifa na hasara itakanayo na ulipaji fidia kwa makosa ya uzembe kama vile ya ukamataji holela wa vyombo vya uvuvi kutokana na kufanya kazi kwa mazoea.
 3. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

Susan Limbweni Kiwanga (Mb)

KNY. MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI

 BUNGENI, KATIKA WIZARA YA UJENZI,

UCHUKUZI NA MAWASILIANO

21 Mei, 2020

 

 

Share Button