MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA  WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI, KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA KUSIMAMIA NA KUENDELEZA UVUVI WA BAHARI KUU WA MWAKA 2020 (THE DEEP SEA FISHERIES MANAGEMENT AND DEVELOPMENT ACT, 2020)

(Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la mwaka 2016)

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa Kanuni ya 86(6) naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 2020.
  3. Mheshimiwa Spika, kabla sijatoa maoni hayo, naomba kuchukua fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kunijalia afya njema na nguvu ya kusimama mbele ya Bunge hili kuwasilisha maoni ya Upinzani kuhusu Muswada nilioutaja hivi punde.
  4. Mheshimiwa Spika, napenda pia kuchukua fursa hii pia kuupongeza sana ungozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (M) ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa kusimamia kwa vitendo nidhamu na uwajibikaji ndani ya chama; lakini zaidi kwa kuonyesha njia ya nini  Serikali natakiwa lifanye hasa kwa kipindi hiki kigumu ambacho taifa linakabiliwa na janga la Corona. Pamoja na mawimbi ambayo chama kinapitia kwa sasa, uongozi umeweza kukiweka chama pamoja na hakika kiko imara leo kuliko jana!
  5. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kuwa, Janga la Corona bado lipo; hivyo kila mwananchi aendelee kuchukua tahadhari kadiri inavyoelekezwa na wataalam wa afya; lakini pia tunatoa pole kwa wale ambao kwa namna moja ama nyingine wameathirika na janga hili; ama kwa kuuguliwa au kufiwa na wapendwa wao kutokana na janga hili. Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa faraja na uponyaji walio wagonjwa na wale waliotangulia mbele ya haki basi awape pumziko la milelel – Amina.
  6. Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia utangulizi wangu kwa kutoa nasaha hasa kwa wabunge wenzangu wa upinzani kwamba “When the going gets tough, only the tough get going”  Baada ya utangulizi huo, naomba sasa nijielekeze kwenye Muswada ulio mbele yetu.

 

  1. MAONI NA MAPENEKEZO YA KAMBI RASMI YA UPIZNANI BUNGENI KUHUSU MUSWADA
  2. Mheshimiwa Spika, Muswada huu unapendekeza kutungwa kwa Sheria ya Kusimamia na Kuendeleza Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 2020 pamoja na kuweka masharti bora ya usimamizi, udhibiti na uhifadhi wa rasilimali za uvuvi katika Ukanda Maalum wa Uchumi wa Bahari (EEZ). Kutungwa kwa Sheria hii kutaimarisha utekelezaji wa matakwa ya Sheria na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa katika kudhibiti na kuhifadhi rasilimali za uvuvi. Aidha, Muswada huu unakusudia kuifuta Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Sura ya 388.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla maudhui ya muswada yako vizuri. Hii ni kutokana na Muswada huu kuzingatia mambo muhimu ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiyapendekeza kwa kipindi chote toka mwaka 2005 hadi sasa. Kitendo cha kuzingatia ushauri huo, kinaifanya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iamini kwamba sasa eneo hili la uvuvi wa bahari kuu;  kama litasimamiwa vizuri; linaweza kuifikia ndoto ya mageuzi makubwa ya kiuchumi katika eneo hilo kwa kuwa na mchango mkubwa wa fedha za kigeni na chanzo cha ajira kwa watanzania wengi.
  4. Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema ya muswada huu na licha ya muswada huu kuzingatia mambo mengi muhimu ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiishauri Serikali; yapo baadhi ya maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuifanya sheria inayopendekezwa kuwa bora zaidi. Maeneo hayo ni kama ifuatavyo:-
  5. Tafsiri ya Maana ya Maneno yaliyotumika kwenye Muswada
  6. Mheshimiwa Spika, kifungu cha (3) cha muswada kinachohusiana na tafsiri ya maneno yanayotumika katika muswada, kuna baadhi ya maneno yameshindwa kupatiwa tafsiri na badala yake inatolewa kwenye majukumu ya Mkurugenzi, mfano ni maneno “fishery inspector na fishery observer” hawa ni watu wawili tofauti; lakini majukumu yao hayajaainishwa bayana ili kuwatofautisha jambo ambalo linaweza kuleta mkanganyiko wakati wa utekelezaji wa sheria inayopendekezwa.  Kambi Rasmi ya Upinzani inaona ni muhimu sana katika kifungu hiki cha tafsiri kutoa maana inayoeleweka kwa wale wataokuwa wanatumia sheria hii ili kuondoa mkanganyiko usio kuwa na ulazima.
  7. Eneo la Makao Makuu ya Mamlaka
  8. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5(3) cha muswada kinachohusu makao makuu ya mamlaka kuwa yatakuwa ni Zanzibar, au mamlaka inaweza kufungua ofisi yake katika eneo lolote la Tanzania Bara, au nje ya Tanzania Zanzibar– (3) The headquarters of the Authority shall be in Tanzania Zanzibar, ———- or outside Tanzania Zanzibar)
  9. Mheshimiwa Spika, ili kuwa na uelewa uliokusudiwa ni vyema haya maneno “outside Tanzania Zanzibar” yakafutwa kwa kuwa yakiendelea kuwepo maana yake mamlaka inaweza kuwa na ofisi Mombasa, Comoro, Ushelisheli nk. kwani ni nje ya Tanzania Zanzibar pia.
  • Kazi za Mamlaka inayoanzishwa na Muswada
  1. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 6(3)(iii) cha muswada kinahusu kazi za mamlaka hii inayoundawa. Kifungu hicho kinachosema kwamba; “concluding agreements for fisheries access by non-citizens and non-nationals, including foreign fishing vessels”. Hapa ndipo kumekuwa na tatizo kubwa sana kwa kuwaachia watu ambao tumewapa mamlaka kwa kuwaamini lakini ukweli wanatuangusha sana. Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba mamlaka iongozwe na Sheria za Mamlaka ya Nchi ya Usimamizi wa Mali na Rasilimali asili (The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act) na Sheria ya Mapitio na Maelewano Mapya ya Masuala yenye Utata kuhusu Mali na Rasilimali Asili  (the Natural Wealth and Resources (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act 2017 (“Contract Review Act”)”; ili kuziba mianya ya rushwa na utashi binafsi katika kuingia mikataba yenye maslahi ya kiuchumi kwa Taifa.

 

  1. Mkanganyiko juu ya Matumizi ya Sheria iliyofutwa
  2. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 102(2) (b) kinasomeka kwamba; “all licences, permits, authorizations and other instruments or documents granted or issued under the repealed Act, shall, so long as they on the date of commencement of this Act continue in full force and effect until they expire, cease to have effect or are replaced;”

 

  1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ina wasiwasi na maudhui ya kifungu hicho kwa kuwa inaweza tokea tasnia moja ikawa inatumia sheria mbili tofauti kama ambavyo inatokea kwenye tasnia ya madini kwa baadhi ya makampuni kutumia sheria ya zamani na mengine kutumia sheria mpya kutokana na mikataba na leseni na vibali vilivyokuwa vimetolewa kabla ya matumizi ya sheria mpya. Jambo la kuangangalia ni kwamba uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu ni chombo cha mtu anayefanya biashara hiyo tu kuwa kina viwango vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria tu na sio jambo lingine. Hivyo ni tofauti sana na uwekezaji kwenye rasilimali zingine kama mafuta, gesi na madini mengine.
  2. Uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu
  3. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 15 kinachohusu uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, na kifungu kidogo cha (3) kinasema kuwa; ili kudumisha Muungano,  Mkurugenzi Mkuu na Naibu Mkurugenzi Mkuu mmoja wapo lazima awe ametoka upande wa pili wa Muungano. Kifungu kinasomeka kama ifuatavyo namba kunukuu “(3) For the purpose of ensuring equal representation of both sides of the Union, the Director General and Deputy Director General shall, at any given time, be appointed one from Mainland Tanzania and the other from Tanzania Zanzibar, and subsequent appointments for each position shall alternate between the two sides of the Union”.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kifungu hiki kinachoweka ulazima wa watu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa mazingira ya sasa ya Dunia kuhusu ajira ni dhahiri kifungu hiki hakina tija katika ulimwengu wa biashara. Tukumbuke kwamba Mamlaka inayoanzishwa ni chombo cha kibiashara na hivyo tuangalie mtu wa kuendesha chombo hiki awe ni mtu makini bila ya kuangalia uraia wake, au upande wa Muungano anakotoka. Kinachohitajika ni kuhakikisha anaendesha Mamlaka hii kwa weledi na ufanisi  ili ikidhi matakwa ya uwepo wake.

 

  1. Mheshimiwa Spika, tunakumbusha tena katika taasisi kama hizi kuingiza siasa katika utendaji ni jambo ambalo litapelekea kushindwa kufikiwa kwa lengo kuu la uanzishwaji wake kabla hata kuanza kazi zake kwa mujibu wa sheria, hivyo basi tutafute watu makini ikiwezekana toka kwa wenzetu ambao wamefanya kazi hizi kwa muda mrefu sana na wanavyo viwanda vingi vya samaki (fish processing ports),tusitunge sheria ya kutufunga katika kupata watendaji wazuri wenye ujuzi na exposure kubwa katika kile tunachotaka kukifanya. Kwa kuweka kumbukumbu sawa ni kwamba Mtendaji Mkuu wa Kwanza wa TANROADS hakuwa Mtanzania, vivyo hivyo kwa MSD, hivyo basi jambo hilo halitakuwa na ukakasi kwani kinachohitajika ni kuhakikisha mamlaka inafanya kazi kwa faida zaidi na mafanikio makubwa.
  2. Kinga ya Kutowajibishwa kwa Maafisa wa Mamlaka
  3. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 18 cha muswada kinatoa kinga kwa maafisa wa mamlaka ya kutowajibishwa kwa upotevu au uharibifu watakaoufanya watakapokuwa wakitekeleza majukumu yao kwa nia njema. Kifungu kinasomeka kama ifuatavyo naomba kunukuu; “A person authorized to perform the functions of the Authority shall not be personally liable for any loss or damage suffered to any person by reason of anything done or not done in good faith”.
  4. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani mara nyingi imekuwa ikikataa utunzi wa sheria zenye kifungu kama hiki kwa kuwa  katika tafsiri ya maneno hakuna maana ya neno “good faith” na hiyo nia njema haijulikani  inaanzia wapi na kuishia wapi! Tukumbuke biashara hii inahusu  bidhaa zinazowahi kuharibika-“Perishable products”, hivyo jambo lolote litakalofanywa na watendaji dhidi ya mfanyabiashara mwenye leseni na vibali halali kuhusu biashara yake, na kumsababishia hasara ni lazima mhusika awajibike katika hasara hiyo kwa mujibu wa sheria.

 

  1. Mheshimiwa Spika, dhana ya kifungu hiki inaendana na kifungu cha 67(7) ambacho kinasema Mkurugenzi Mkuuau  wakaguzi au afisa yoyote wa mamlaka hatawajibika kwa uharibufu au kuoza  au kupotea ubora wa bidhaa zilizo kamatwa.  Haki hapo iko wapi kwa mfanyabiashara?

 

  1. Mheshimiwa Spika, sasa ni kipindi cha matumizi ya teknolojia hivyo tusitunge sheria kwa kuangalia kukinga makosa ambayo tayari yamefanywa huko nyuma na Serikali kuingia hasara kubwa kutokana na makosa hayo. Tutunge sheria kulingana na wakati uliopo na ujao ili tuokoe tasnia hii, na pia tusiweke kinga kuwa makosa au hujuma zitakazofanyika. Vifungu vya namna hiyo visiporekebishwa vinaweza kupunguza uwekezaji mkubwa katika eneo hilo kwa kuwa hakuna mfanya biashara atakayekubali kupata hasara kwa uzembe wa watendaji ambao wanalindwa na sheria.

 

  • Utungaji wa Kanuni
  1. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 24(7) cha muswada kinasema Waziri ndiye atakaetunga kanuni kuhusiana na taratibu za utawala kama vile kuweka faini na adhabu na vile vile vibali. Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri utaratibu huo hasa faini na adhabu viwe ndani ya sheria nasio kwenye kanuni kwani historia inaonesha kuwa wahusika wanakuwa na matumizi mabaya ya madaraka hayo, hivyo ni muhimu sana  mambo hayo yakawa ndani ya sheria mama.

 

  • Usiri wa Taarifa
  1. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 53(1), (2) na (3) vinahusu usiri wa taarifa. Kambi Rasmi ya Upinzani inajiuliza katika biashara inayohusu rasilimali za taifa, na hususani uvuvi wa samaki na mazao ya baharini kwa maana ya ni kiasi gani kimevuliwa; kuna meli ngapi za uvuvi na wamiliki wake pamoja na  mapato ya nchi kutokana na biashara hiyo; usiri unawekwa kwa ajili ya kupata faida gani?  Kwa mtazamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni usiri ni ukiritimba; na ukiritimba ndio chanzo kikuu cha rushwa kubwa kubwa hasa katika rasilimali zetu. Kwa muktadha huo tunataka vifungu hivi vya usiri wa taarifa vifutwe.

 

  1. Uuuzaji wa Bidhaa zilizokamatwa
  2. Mheshimiwa Spika,kifungu cha 67(1) kuhusiana na uuzaji wa bidhaa zilizokamatwa na zinazoharibika kuwa Mkurugenzi mkuu atafanya mashauriano na Mkurugenzi wa Mashtaka kuwa ziuzwe au kutoa  idhini ya kuuza. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa Mamlaka sahihi kwa jambo hilo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Tukumbuke kuwa tasnia hii ya Uvuvi katika bahari kuu inahusu makampuni ya nje na ikitokea chochote katika mchakato wa kibiashara mhusika mkuu atakuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sio Mkurugenzi wa Mashtaka.

 

  1. Kuachiwa kwa Chombo au Bidhaa baada ya kuwekewa Dhamana
  2. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 68 cha muswada kinahusu uachiwaji wa chombo na bidhaa baada ya kuwekwa kwa dhamana na mahitaji mengine. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kifungu hiki kinaweka mazingira makali, magumu na ya kukomoana sana na mbaya zaidi hakikusema pale chombo kilichokamatwa kabla ya kuachiwa kitakuwa kimesimama tu bila kufanya kazi yoyote na uangalizi wake utakuwaje? Wenzetu wa Botswana waliopokuwa wanakamata meli katika eneo lao la bahari kuu, meli hizo zinaendelea kufanyakazi na wahusika hao hao huku kesi inaendelea na nchi inaendelea kunufaika na sio kuiacha meli ikaoza na kuharibika.

 

  1. Kutaifisha Chombo na Bidhaa zilizopo kwenye Chombo baada ya Kukamatwa
  2. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 71 cha muswada kinachohusu kutaifishwa kwa chombo na bidhaa zilizomo kwenye chombo wakati kinakamatwa, lakini muswada unasema mali zote zilizotaifishwa zitakuwa ni mali za Serikali, vivyo hivyo na kwa kifungu cha 72. Kambi Rasmi ya Upinzani inakumbusha ukamataji wa meli ya wavietnam maarufu kama meli ya Samaki wa Magufuli, meli hiyo ilishindwa kufanya kazi na badala yake ikahujumiwa na mwisho Serikali ikatakiwa kulipa gharama za meli na bidhaa zilizokuwemo baada ya kesi kumalizika. Hivyo basi badala ya kusema itakuwa ni mali ya Serikali muswada uende mbele zaidi kueleza ni eneo gani meli au mali hizo zitakapowekwa ili kuondoa mivutano na ukiritimba usiokuwa na maana unaokuwa na lengo la hujuma au maslahi binafsi.

 

 

  • Uwezo wa Mamlaka Kukopa Fedha
  1. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 86 cha muswada inatoa uwezo kwa Mamlaka kukopa fedha kutoka kwenye taasisi za fedha pale inapopata idhini kutoka kwenye Kamati Tendaji. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa Mamlaka inatoa mpango wa matumizi ya fedha za kukopa, lakini kifungu hakioneshi njia au mpango gani wa kurejesha mkopo huo. Taasisi nyingi zinashindwa kuaminika kutokana na kutokuwa na mpango imara wa kurejesha mikopo na mwisho wa siku hiyo “burden” ya mkopo inarudi Serikali kuu. Tukumbuke kuwa kuna sheria inazitaka mamlaka na wakala wa Serikali kutoa asilimia 10 ya pato ghafi kwenda Hazina na hivyo kinachobakia wakipiga mahesabu inaweza kushindwa kurejesha mkopo.
  2. HITIMISHO
  3. Mheshimiwa Spika, ,Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiishauri Serikali kuwekeza kwenye uvuvi wa Bahari Kuu kwa kuanzisha badari ya uvuvi , sambamba na kuwa na vifaa vya kuweza kutambua meli zinazovua kwenye eneo letu la bahari kuu bila Kambi Rasmi ya Upinzani imefarijika kuona kwamba  Muswada huu umetambua umuhimu wa kuwa na vifaa vya kutambua shughuli za meli za uvuvi katika bahari kuu, jambo ambalo ni jema sana katika kuhakikisha rasilimali za Taia zinatumika kwa manufaa ya watanzania wote na si vinginevyo;
  4. Mheshimiwa Spika, pamoja na maudhui hayo mazuri ya Muswada; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kutoa ngalizo kwa Serikali juu ya utekelezaji wa Sheria hii inayopendekezwa kuwa kuwa bado kuna baadhi ya vifungu ambavyo ni kikwazo kwa utekelezaji wa sheria inayopendekezwa. Kwa mfano vifungu vinavyowakinga watendaji kutochukuliwa hatua za kisheria kwa makosa waliyoyafanya wakitekeleza wajibu wao ni moja ya kiwakwazo cha utekelezaji bora wa sheria inayopendekezwa.
  5. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muswada wa sheria hii hautabadilisha mikataba na taratibu zote ambazo ziliingiwa kwa kutumia sheria inayofutwa; na kwa kuwa kuendelea kutumia sheria na taratibu za mikataba ya sheria inayofutwa maana yake ni kuendelea na tatizo lile lile na inaweza kuchukua zaidi ya miaka mitano ijayo kabla matunda ya sheria mpya kupatikana; hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuangalia kwa makini maeneo ambayo yanaweza kuleta ugumu katika utekelezaji wa sheria hii na kuyafanyia marekebisho kabla ya kupitishwa kwa muswada huu kuwa shieria ili sheria hii iweze kutekelezeka na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
  6. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

 

Dr. Sware I. Semesi (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI-WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI

20 Mei, 2020.

Share Button