HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, MHE MCHUNGAJI PETER SIMON MSIGWA, AKIWASILISHA MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA HIYO KWA MWAKA WA FEDHA 2020/21

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 _______

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge lako tukufu lizingatie kwa kina maoni haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani linapojadili na kufanya maamuzi kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2020/21.

 

  1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, namtukuza Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na upendo, kwa kutuchagua tena kuiona siku ya leo. Kwa masikitiko makubwa nachukua fursa hii kumwomba Yeye-Mwenye-Enzi awalaze mahali pema peponi wabunge wenzetu, marehemu Balozi Augustine Mahiga aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria na pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Richard Ndassa aliyekuwa mbunge wa Sumve na Mama Getrude Lwakatare, ambao wote kwa pamoja wametutoka hivi karibuni. Aidha, Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa pumziko jema wabunge wengine wote waliotutangulia mbele za haki kutoka kwenye Bunge hili.Yehova akawe mfariji na mlezi mkuu wa familia zote za marehemu hawa. Amen!.
  2. Mheshimiwa Spika, kwa nafasi ya kipekee nampongeza Mhe. Joyce Mukya (Mbunge) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Namshukuru sana kwa mchango wake mkubwa wa mawazo uliofanikisha kukamilika kwa hotuba hii.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa miaka minne mfululizo mimi na viongozi wenzangu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), tumekuwa katika misukosuko mingi, majaribu na mateso makali ya kisiasa yaliyokusudia kudhohofisha chama chetu au kuzima kabisa wajibu wetu muhimu wa kuwatetea wananchi. Nachukua fursa hii kuwashukuru sana Watanzania kwa kusimama pamoja nasi. Kwa nguvu ya umma na uweza wa Mola, hatimaye tuliweza kuyashinda yote na kuthibitisha ule ukweli wa siku zote kwamba “Chadema ni Mpango wa Mungu”.

 

  1. Aidha, Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Iringa Mjini kwa kuendelea kuniamini na kuniunga mkono bila kusita. Siyo siri, ninajisikia fahari kubwa sana kuendelea kuwa mbunge wa Iringa, huku nikiwa nimeilinda vema ile historia na heshima kubwa ya Chifu Mkwawa na watu wa Iringa inayojulikana duniani kote. Naam! Iringa ya watu makini, Iringa ya watu jasiri, Iringa ya watu wenye msimamo usioyumba na Iringa ya watu wasionunulika kwa gharama yoyote ile!

 

 

  1. MWELEKEO WA MAONI YETU KUHUSU BAJETI YA WIZARA HII
  2. Mheshimiwa Spika, jukumu la msingi la Wizara ya Maliasili na Utalii ni kusimamia uhifadhi na matumizi endelevu ya raslimali za Maliasili na Malikale, na kukuza maendeleo ya Utalii kwa kushirikiana na wadau. Jukumu hili hutekelezwa kupitia sekta ndogo za Wanyamapori, Misitu, Ufugaji Nyuki, Utalii na Malikale.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hali halisi inayoendelea nchini na duniani kote, hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani itajikita zaidi katika kutoa tathmini na ushauri mahsusi kuhusu maendeleo ya sekta ya utalii ya kabla na baada ya kuibuka na kuenea kwa janga la ugonjwa wa covid-19 na kisha kushauri mwelekeo sahihi wa bajeti ya wizara hii. Pia tukubaliane kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii ni sekta ya utalii ndiyo ina beba Wizara nzima na pia inaibeba nchi katika kuingiza fedha za kigeni.

 

  1. TATHMINI YA SEKTA YA UTALII CHINI YA AWAMU YA TANO.
  2. Mheshimiwa Spika, utalii ni sekta muhimu katika kuchochea ukuaji uchumi na maendeleo ya watu. Takwimu za serikali zinaonesha kuwa sekta ya utalii inachangia takribani 18% ya Pato la Taifa na ndiyo inayoongoza kwa kuiingizia nchi yetu fedha za kigeni kwa 25%. Aidha, sekta ya utalii imekadiriwa kutengeneza zaidi ya ajira 2,000,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
  3. Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa tano tangu serikali hii ya awamu ya tano iingie madarakani. Tunapojadili sekta ya utalii kwenye bajeti ya Wizara hii ni vema na haki Bunge lako tukufu likajiuliza maswali haya ya msingi:
  4. Hivi ni jambo gani kubwa, jipya, la kimageuzi au kimapinduzi ambalo Serikali ya Awamu ya Tano imelifanya ili kukuza sekta utalii ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita? Na ni jambo gani hilo ambalo halikuwahi kufanyika wakati wa serikali za awamu nne zilizopita?
  5. Hivi bajeti ya Wizara hii kwa mwaka 2020/21 ina kipi cha ziada kuhusu utalii ambacho hatukuwahi kuletewa hapa ndani ya miaka minne iliyopita ya utawala huu?
  6. Mheshimiwa Spika, maswali haya ni muhimu yakajibiwa kwa usahihi ili kuepuka kujifariji na mambo madogo-madogo yasiyotufikisha popote. Kama kweli tuna dhamira ya dhati ya kuiletea nchi yetu maendeleo makubwa, ya haraka, na endelevu, hatuna budi tufanye maamuzi makubwa sana ya kuinyanyua sekta hii kwa kasi.
  7. Mheshimiwa Spika, mtaalam mashuhuri wa mawasiliano ya kimkakati na mchambuzi wa maendeleo, Joscelyn Duffy, aliwahi kuandika hivi:

“Development is beyond solving-problems. When our work is solely about solving a problem, then doing so often it will not spur us beyond the status quo. It simply returns us to it. By solely solving a problem we are essentially not challenging ourselves to stretch beyond what we already know is possible. Beyond solution lies evolution and revolution…and there is where real development is”

  1. Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri nyepesi, mtaalam huyu anasema:

Maendeleo ni zaidi ya kutatua matatizo. Pale kazi yetu inapokuwa imejikita tu kwenye kushughulikia matatizo, basi kufanya hivyo hakuwezi kututoa kutoka katika hali tuliyopo sasa. Sana sana kunaturudisha pale pale tulipo. Kimsingi, kwa kuegemea tu kwenye utatuzi wa matatizo, tunakuwa hatujipi changamoto ya kufanya mambo mapya kuzidi kile ambacho tayari tunajua kinawezekana. Juuya “kupata suluhisho la kero na matatizo” kuna “mageuzi” na “mapinduzi” yanayopaswa kufanywa …na hapo ndipo maendeleo yalipo”

  1. Mheshimiwa Spika, kinyume kabisa na nasaha za msomi huyu, nasikitika kulitaarifu bunge lako tukufu kwamba hakuna jambo jipya lililofanywa na wizara ndani ya miaka minne iliyopita kwenye sekta hii ya utalii. Mengi ya yale yanayoitwa “mafanikio na maendeleo makubwa ya sekta ya utalii” ni mambo madogo-madogo tu yasiyolingana hata na malengo ya msingi kukuza sekta yenyewe wala muda uliotumika. Kambi Rasmi ya Upinzani inathibitisha ukweli huu kama ifuatavyo:
  2. Mheshimiwa Spika, ni vema ikakumbukwa kuwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Miaka Mitano (2016/17-2020/21), serikali hii ilijiwekea lengo la kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka 1,200,000 wa mwaka 2016/17 hadi kufikia watalii 2,000,000 ifikapo mwaka 2020.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya Waziri Mkuu ya mwezi April mwaka huu, hadi kufikia mwaka 2019 idadi ya watalii wanaoingia nchini ilifikia 1,505,702 kutoka watalii 1,200,000 wa mwaka 2016. Aidha, mapato ya utalii yalifikia dola za Marekani bilioni 2.6 kutoka dola bilioni 2.1 za mwaka 2016.
  4. Mheshimiwa Spika, hili ni ongezeko la watalii 305,702 tu ndani ya kipindi cha miaka minne; na ambalo ni sawa na kupata wastani wa watalii 76,425 tu kwa mwaka! Pia hii ni sawa na kuongeza mapato ya dola milioni 500 tu kwa miaka minne, sawa na wastani wa kuingiza dola milioni 125 tu kwa mwaka!
  5. Mheshimiwa Spika, kwa vigezo vyovyote vile hizi si takwimu za kujivunia hata kidogo. Mafanikio haya madogo-madogo hayalingani hata kidogo na wingi wa vivutio vya utalii vilivyopo nchini na wala hayakaribiani na kasi ya washindani wetu katika sekta hii ya utalii.
  6. Mheshimiwa Spika, hatupaswi tu kufurahia kwenda mbele, tunapaswa kujiuliza …hivi tunakwenda mbele kwa mwendo wa Konokono au kwa kasi ya Nyoka? Maana wakati serikali yetu ikishindwa kutimiza lengo dogo la kufikia watalii 2,000,000 kwa zaidi ya miaka minne, washindani wetu, nchi jirani ya Kenya, ndani ya mwaka mmoja tu,waliweza kufikisha watalii 2,025,206 mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la watalii 550,535 kutoka watalii 1,474,671 iliokuwa nao mwaka 2017.
  7. Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2014 (miaka 6 iliyopita), kupitia ripoti ya hali ya uchumi wa Tanzania iliyoangazia zaidi sekta ya utalii, Timu ya Wataalam wa Benki ya Dunia (Word Bank Group) iliainisha mapendekezo mbalimbali inayoamini yatasaidia sana kuongeza mapato na idadi ya watalii hadi kufikia watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2025. Ripoti hiyo iliyoitwa – “The Elephant in the Room: Unlocking the Potential of Tourism Industry for Tanzanians”, ilitoa mapendekezo ya kukuza utalii yaliyogawanyika kwenye mihimili mikuu mitatu:
  8. Mheshimiwa Spika, katika Mhimili wa Kwanza. Wataalam hao wakiongozwa na mchumi na mwandishi mkuu wa ripoti hiyo, Jacques Morisset, walipendekeza kufanyike “Diversification of geographic locations and tourism segments”, yaani tuongeze maeneo tofauti-tofauti ya utalii pamoja na kuongeza wigo wa mazao ya utalii”.
  9. Mheshimiwa Spika, kimsingi, katika eneo hili watalaam waliona ipo haja ya kukuza maeneo mengine ya kitalii mbali na Arusha, Kilimanjaro na Zanzibar pamoja na kuongeza mazao ya utalii hususan utalii wa fukwe, utamaduni na utalii wa kibiashara ili kuvutia watalii kwa kuwapa fursa nyingi zaidi za kutalii (tourism options)
  10. Mheshimiwa Spika, katika Mhimili wa Pili, ripoti ilipendekeza “Integration of tourism activities at existing attractions”, yaani kujumuisha zaidi shughuli mpya za utalii katika hifadhi zilizopo. Katika hili, ripoti imefafanua kwamba utalii Tanzania bado haujatengeneza thamani kubwa wala ajira nyingi kwa wenyeji.
  11. Mheshimiwa Spika, kwa mfano, hoteli na maeneo mbalimbali ya kupumzikia watalii bado yanaagiza vitu, vifaa na vyakula vingi kutoka nje ya nchi, wakati yote haya yangepaswa kuwa fursa ya kuongeza thamani na ajira kwa wenyeji.
  12. Mheshimiwa Spika, katika Mhimili wa Tatu, ripoti hiyo ilipendekeza “Improvement in the quality of governance”, yaani kuboresha utawala wa sekta yenyewe ya utalii. Hapa ripoti imefafanua kwamba tasnia ya utalii Tanzania inakabiliwa na utitiri mwingi wa kodi na ushuru, hali inayokatisha tamaa wawekezaji wengi hususan wawekeza wadogo wasiwekeze kwenye eneo hili na wakati huo huo ikichochea rushwa.
  13. Mheshimiwa Spika, jambo hili tulifafanua pia katika hotuba yetu ya mwaka jana. Kimsingi, Kambi Rasmi ya Upinzani tulieleza na kuainisha sheria na kanuni 13 zinazokinzana na kusababisha ukiritimba uliopitiliza katika sekta hii ya utalii. Ajabu, bado halijafanyiwa kazi kikamilifu.
  14. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ina uhakika kuwa sekta ya utalii ingeweza kukua kwa kasi kubwa zaidi ya ilivyo sasa kama serikali ingezingatia na kutekeleza vema mapendekezo yote hayo ya wataalam wa Benki ya Dunia na ushauri ambao tumekuwa tukiutoa mara kwa mara. Mambo yote haya yalihitaji uwekezaji mkubwa na wa kimkakati wa kifedha na ulio endelevu.
  15. Mheshimiwa Spika, kinyume chake, fedha zinazotolewa na serikali zimekuwa ndogo sana kulinganisha na malengo. Kwa miaka minne iliyopita, yaani kutoka mwaka wa fedha 2016/17 hadi 2019/20, jumla ya fedha zilizoombwa na kuidhinishwa na Bunge kwaajili ya miradi ya maendeleo ya wizara hii ni shilingi bilioni 99.4 tu.
  16. Mheshimiwa Spika, pamoja na kutengwa kwa fedha chache, bado serikali iliendelea kutoa pesa pungufu zaidi kuliko kiasi kilichoidhinishwa. Mathalan, katika mwaka wa fedha 2017/18, wizara iliidhinishiwa bilioni 51.8 kwaajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi 2018 ni bilioni 27.9 tu ndizo zilizotolewa kwaajili hiyo, sawa na asilimia 53 tu ya fedha zote.
  17. Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo, katika mwaka wa fedha 2018/19, wizara iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 29.9 kwaajili ya miradi ya maendeleo, lakini hadi kufikia Machi 2019 wizara ilikuwa imepokea bilioni 10.1, sawa na asilimia 33 tu ya fedha zote. Halafu serikali inasema tumepiga hatua kubwa sana!

 

  1. Mheshimiwa Spika, hapa hakuna umakini wala utashi wa kiasiasa! Fedha hizi ni ndogo sana kwa serikali yoyote ile makini yenye nia ya dhati ya kukuza uchumi kupitia utalii. Huku ndiko kufanya mambo madogo-madogo yasiyoifikisha nchi popote.
  2. Mheshimiwa Spika, mfano wa maamuzi yasiyo na tija ambayo yamekuwa yakifanywa na serikali kwenye sekta hii ya utalii, ni uamuzi wa kuyapandisha hadhi mapori sita ya akiba – Burigi, Kimisi, Biharamulo, Ibanda na Rumanyika – kuwa hifadhi za taifa!
  3. Mheshimiwa Spika, ni vema ikazingatiwa kuwa wakati Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) lilipokuwa linahudumia mbuga 16, ni mbuga tano tu ndizo zilikuwa zinafanya vizuri. Mbuga 11 zikiwemo za ukanda wa kusini “Southern circuit” zilihitaji kufanyiwa uwekezaji wa kuboresha miundombinu,utoaji huduma (hospitality and customare care) na kufanyiwa matangazo ya kutosha (promotion). Hata hivyo, TANAPA haikuwa na uwezo wa kutosha kufanya hivyo wakati wote.
  4. Mheshimiwa Spika, hatua ya kuongeza mbuga mpya 5 inafanya kuwe na jumla ya mbuga 21 ambazo zinaongeza mzigo mkubwa wa uendeshaji kwa TANAPA. Kwa nfano, katika mwaka wa fedha 2019/20, TANAPA ilihitaji takribani shilingi bilioni 3.9 ili kuhudumia mbuga hizo mpya 5 zilizoongezwa. Matumizi ya pesa hizi yangekuwa na tija ya haraka zaidi kama yangeelekezwa katika baadhi ya mbuga ambazo tayari zilikuwepo na zilihitaji tu kuongezewa nguvu. Lakini sasa kwa uamuzi uliofanyika tunazidi kwenda pole pole sana.
  5. Mheshimiwa Spika, wakati wataalam wa Benki ya Dunia walionesha jinsi inavyowezekana kufikisha watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2025, ni vema ikaeleweka kwamba kwa mwendo wa serikali hii wa kuongeza wastani wa watalii 76,425 kwa mwaka, itaichukua Tanzania miaka 104 kuweza kufikia lengo hilo. Ni dhahiri kuwa lengo hilo haliwezi kufikiwa ndani ya muda uliokusudiwa (2025) kama bunge lako halitailazimisha wizara hii kufanya mabadiliko makubwa ya mikakati, shughuli na bajeti zake.

 

  1. JANGA LA VIRUSI VYA COVID-19 KATIKA SEKTA YA UTALII
  2. Mheshimiwa Spika, nchi yetu ipo katika vita dhidi ya janga kubwa la covid- 19 sawa na ilivyo kwa mataifa mengi duniani. Hata hivyo, namna nchi yetu inavyopambana na janga hili tayari imeibua mashaka makubwa katika jumuiya ya kimataifa kwa kuonekana hatufuati kikamilifu njia zilizoshauriwa kisayansi za kujikinga na janga hili.
  3. Mheshimiwa Spika, Sir Winston Leonard Spencer-Churchil, aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Uingereza na aliyeiongoza Uingereza katika vita vya pili vya dunia, aliwahi kusema hivi, namnukuu:

“In every age there comes a time when a leader must come forward to meet the needs of the hour. Therefore, there is no potential leader who does not have an opportunity to make a positive difference in society. Tragically, there are times when a leader does not rise to the hour”

  1. Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi, Kiongozi huyu mashuhuri duniani aliyewahi pia kuwa afisa wa jeshi na mwandishi, alimaanisha hivi:

“Katika kila zama hufikia kipindi ambapo kiongozi hulazimika kujitokeza kukabiliana na mahitaji ya wakati. Kwa hiyo, hakuna kiongozi yeyote mzuri ambaye hana fursa ya kufanikisha jambo muhimu katika jamii. Kwa bahati mbaya, kuna nyakati ambazo kiongozi hushindwa kuibuka kukabiliana na mahitaji ya wakati”

  1. Mheshimiwa Spika, serikali imekosa uongozi wenye maono na mikakati sahihi ya kupambana na covid-19. Matumizi ya nyungu na mikusanyiko mingi iliyoruhusiwa kuendelea nchini havitujengei picha nzuri duniani. Ni lazima Mkuu sio tu ajitokeze hadharani lakini pia atuongoze kukabiliana na mahitaji haya ya wakati tulionao kama anavyosema Winston Churchill.
  2. Mheshimiwa Spika, kama Mkuu wa nchi asipojitokeza waziwazi na kuliunganisha Taifa kwa usahihi dhidi ya covid-19, basi upo uwezekano Taifa likazidi kupoteana na kuhatarisha zaidi uhai wa watu na uchumi hususan dhidi ya sekta hii ya utalii.
  3. Mheshimiwa Spika, kimsingi, tayari janga hili limeshaathiri sekta ya utalii ikiwemo eneo la ukusanyaji wa maduhuli. Wakati wizara ilitarajia kupata ongezeko kubwa la watalii na kukusanya kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 71.5 katika mwaka wa fedha 2019/2020, hadi kufikia mwezi Februari 2020 ni shilingi bilioni 40.2 pekee ndizo zilizokusanywa, huku taasisi zilizo chini ya Wizara zikikusanya bilioni 12 tu.
  4. Mheshimiwa Spika, kama makusanyo ya maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019/2020 yameshindwa kufikia asilimia 60 ya makadirio yote, ni dhahiri kuwa katika kipindi hichi cha mlipuko mkubwa wa Corona (Covid-19) ambapo soko la utalii limeporomoka kabisa, hali ya wizara hii itakuwa ni mbaya zaidi!
  5. Mheshimiwa Spika, tangu kuanza kwa janga la korona mwezi Desemba 2019, mashirika ya ndege kutoka nchi mbalimbali duniani kama British Airways, Qatar, Lufthansa, Emirates, KLM, Air France, Swiss Air na nyingine nyingi yamefunga safari zao za kwenda nchi mbalimbali duniani, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huu.
  6. Mheshimiwa Spika, kuathirika kwa shughuli za usafiri wa ndege duniani na kufungwa kwa mipaka kumeathiri biashara ya utalii duniani kote. Kumeathiri ajira, kilimo, ufugaji, uvuvi na biashara nyingine nyingi. Kabla ya kuanza kwa janga la Korona, sekta ya utalii ilikuwa inachangia 10.4% ya GDP na 16% ya ajira duniani. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO 2018). Mpaka sasa shirika hilo limetabiri kutokea kwa anguko kubwa la uchumi hasa kwa nchi ambazo uchumi wake unategema utalii.
  7. Mheshimiwa Spika, kufuatia kuongezeka kwa kasi ya Covid -19 mnamo mwezi Machi 2020, sekta ndogo ya hoteli za kitalii na huduma zinazotokana na utalii (hospitality industry) imeporoka sana.
  8. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayo taarifa kuwa hadi kufikia tarehe 21 mwezi Machi, takribani asilimia 95 ya hoteli zote za kitalii Zanzibar zilikuwa zimefungwa. Pia, hoteli kubwa zaidi ya 15 zilizopo ndani ya hifadhi za Serengeti, Ngorongoro, Manyara na Tarangire zimefungwa. Hoteli za kitalii katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa na Songwe nazo zimeathirika zaidi kwa kuwa ndio mikoa inayopokea watalii wengi.
  9. Mheshimiwa Spika, kufuatia kufungwa kwa hoteli za kitalii wananchi wengi wanaotegema sekta hii wamepoteza ajira na wengine wamelazimika kupewa likizo bila mishahara wakisubiri hali hii kutengamaa.Vijana wengi wanaofanya kazi ya kupanda mlima Kilimanjaro na Meru kama wapagazi, sasa wako mitaani hawana kazi.
  10. Mheshimiwa Spika, aidha, wapishi na wahudumu wa mahoteli, kada ya usafi, wanaowatembeza watalii (tour guides), madereva, wakalimani pamoja na wafanyabiashara wanaotegemea soko la utalii kama wauza vinyago, wachoraji na mafundi wengine wa sanaa wengi wamepoteza ajira. Makundi haya yote yana watu wengi wanaowategemea (dependants) ndani ya familia na hata katika jamii kwa ajili ya kuwasaidia kupata mahitaji.
  11. Mheshimiwa Spika, makampuni ya utalii yameingia hasara kubwa kutokana na wageni kusitishwa kwa safari kwasababu ya hofu ya maambukizi na mazuio yaliyowekwa na nchi zao ili kujilinda na janga hili. Imelazimu pia baadhi ya makampuni kurudisha sehemu ya fedha za watalii (refund) kutokana na kusitishwa kwa safari (cancelation of flights). Mpaka sasa makampuni mengi yameshindwa kupokea bookings mpya wakati huu wa kuelekea msimu wa watalii wengi (high season).
  12. Mheshimiwa Spika, ni vema ikazingatiwa kuwa madhara ya Covid-19 kwenye sekta hii, pia yanasababisha sekta ya kilimo hususani kilimo cha mbogamboga na matunda (fruits and vegetable farming) nayo kuathirika sana. Hoteli nyingi hutegemea vyakula kutoka kwenye masoko yetu ya ndani. Mtalii mmoja anaweza kutumia kuanzia dola 16 mpaka 28 kwenye chakula kwa siku, sawa na shilingi za Kitanzania 37,000/ mpaka 64,000/ kwa siku.
  13. Mheshimiwa Spika, sekta ya mifugo na uvuvi pia imeathirika kutokana na kuanguka kwa soko la nyama, mayai, maziwa na samaki ambazo ni bidhaa muhimu katika masoko ya hoteli za kitalii. Madhara ya Corona pia yataendelea kwenye sekta hii kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa bookings mpya za wageni.
  14. Mheshimiwa Spika, kwa kawaida bookings hufanywa miezi mitatu na zaidi kabla ya mtalii kuingia nchini. Endapo hali hii ikiendelea tutapoteza fedha nyingi zaidi. Mgeni anapoingia nchini kwa siku hutumia kuanzia kiasi cha dola ($) 400 mpaka $450 kwa siku. Kwa hiyo endapo mgeni atakaa kwa wastani wa muda wa siku kumi atatumia wastani wa $4,000. Kati ya fedha hizo $4,000 asilimia 45 huingia serikalini kama direct tax.
  15. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018, watalii walioingia nchini ilikuwa 1,505,702 na endapo kwa mwaka huu mpya wa fedha Tanzania itapoteza nusu ya Watalii maana yake itapoteza fedha nyingi ambazo huingizwa serikalini kwa siku kama direct tax. Pia, serikali tayari inapoteza fedha nyingi ambazo hukatwa kama PAYE kutokana na maelfu ya Watanzania kupoteza ajira.
  16. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kuna dosari kuu mbili zinazoiweka nchi yetu katika hali mbaya zaidi ya kufikwa na anguko kubwa na refu la sekta ya utalii na uchumi: Mosi, ni hatua za serikali dhidi ya corona kukosa uwazi wa kutosha na kutiliwa shaka na baadhi ya watu na nchi; na pili ni serikali kutochukua hatua zozote kuhami utalii na uchumi kwa ujumla dhidi madhara ya covid-19.
  17. Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa uwazi wa kutosha, umma kutilia shaka taarifa za maambukizi na vifo vitokanavyo na ugonjwa huu, kukawia kwa serikali kufunga mipaka na kushindwa kudhibiti mikusanyiko mikubwa kama ya ibada, ni miongoni mwa mambo yanayoifanya nchi yetu ionekane haina umakini wa kutosha katika kukabiliana vizuri na kisayansi dhidi ya janga hili la covid-19.
  18. Mheshimiwa Spika, kwa dosari hii ya kutiliwa shaka, ni dhahiri kuwa hata wakati ambapo janga hili litakuwa limeisha au limepungua sana, bado nchi yetu itakawia sana kuaminika kama kweli ni sehemu salama kwa watu wa mataifa mengine kuja. Sekta yetu ya utalii inaweza kukabiliwa na anguko la muda mrefu zaidi hata baada ya corona, kwani watalii watakuwa wanavutika kwenda kwenye nchi ambazo kweli zinaaminika zina uwazi, zilichukua hatua sahihi na zipo salama kweli.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa ufafanuzi huo, Kambi Rasmi ya Upinzani tunaishauri serikali kuongeza uwazi katika mapambano dhidi ya covid-19 na kuchukua hatua zote zinazokubalika na zinazoendana na uhalisia wa nchi yetu.
  2. Mheshimiwa Spika, katika dosari ya pili, inasikitisha kuona serikali ikisukuma maisha ya kibiashara na kiuchumi vile vile kana kwamba hakuna tatizo lililotokea. Serikali bado imeendelea kuyadai kodi makampuni bila kujali hasara kubwa inayowakumba wafanyabiasha wa utalii ambayo ni nje ya matakwa na uwezo wao. Kuibuka kwa ugonjwa wa Covid-19 hakukutarajiwa na kampuni yoyote.
  3. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tunaishauri serikali kuchukua hatua zifuatazo ili kuinusuru sekta ya utalii nchini dhidi ya anguko kubwa na refu zaidi la kiuchumi:
    1. Serikali iandae mkakati wa kuokoa na kuhami sekta ya utalii (Recovery and Protection Plan)
    2. Itenge fedha ya kuendelea kuboresha miundombinu ya utalii,
  • kutangaza na kulinda soko, iv. kuboresha viwanja vya ndege hasa katika kupitia mpango wa kupambana na majanga ya dharura (preparedness).
  1. Mfano katika kuhami sekta yake ya utalii, nchi ya Indonesia imetoa fedha za stimulus package katika maeneo yafuatayo:
  1. Imetenga USD 6 milioni kwa ajili ya mashirika ya ndege na Mawakala wa safari za ndege (travelling agencies)
  2. Imetenga USD 7.1milioni kwa ajili ya kutangaza na kutafuta masoko ya utalii,
  3. Imetenga USD 5milioni kwa ajili ya mitandao ya kijamii yenye wafuasi wengi zaidi kutangaza utalii
  4. Imetenga USD 27 milioni kama fidia ya punguzo la bei kwa watalii watakaotembelea vivutio vinavyotangazwa na serikali
  5. Imelielekeza shirika la Mafuta la Serikali PT Pertamina kutoa punguzo la bei ya mafuta ya ndege kiasi cha dola 18 milioni ili kufidia punguzo la bei ya 30% ya bei ya tiketi za ndege katika viwanja 10 vilivyopo maeneo ya utalii yaliyotangazwa.
  6. Mheshimiwa Spika, pia Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri serikali iweke mpango mkakati wa kulinda wanyama dhidi ya magonjwa yanayoambukizwa kwa hewa ambayo huwapata wanyama kama sokwe. Nchi kama Rwanda na Congo wamefunga baadhi ya maeneo yenye sokwe wengi. Japokuwa bado watalaamu wa afya hawajadhibitisha kama ugonjwa wa Covid-19 unaweza kuambukizwa kwa wanyama hawa kama ilivyo kwa mafua na kikohozi, lakini yatupasa kuchukua tahadhari.
  7. Mheshimiwa Spika, kufuatia janga hili, upo uwezekano kabisa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) kuja na vigezo vipya katika kukidhi matakwa ya kupokea wageni. Hivyo, serikali ijiandae katika kuangalia upya bei zetu, kuandaa mazingira mazuri ya kiushindani, kupitia sera za utalii na kuondoa mapungufu yaliyopo.
  8. Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo, mashirika ya ndege duniani (Airlines) yanaweza kuja na masharti mengi ili kuhakikisha usalama wa abiria na biashara zao. Kwa kuwa biashara ya utalii na usafiri wa anga zinategemeana sana, hivyo ni vyema Bodi ya Utalii nchini (TTB) na Mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania (TCAA) wakakutana na wadau wa utalii ili kufanya uchambuzi wa kina wa hali ya kibiashara ilivyo kwa sasa na kuja na mipango ya muda mfupi na mrefu wa kurejesha biashara pamoja na kuangalia namna bora ya kukabiliana na soko la dunia.
  9. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tunashauri zaidi serikali ifanye tathmini ya haraka na kuondoa kabisa baadhi ya kodi au kuzipunguza kwa makampuni ya utalii na hoteli ili kuziepusha na anguzo zaidi la biashara na hivyo kuokoa ajira zinazodi kupotea.
  10. Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Serikali ya Kenya imepunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14 kuanzia mwezi Aprili, 2020. Hatua hii imekwenda sambamba na Mamlaka ya Mapato ya Nchi hiyo (KRA) kutakiwa kuharakisha kulipa kiasi kilichohakikiwa cha shilingi za Kenya Bilioni 10 za madai ya marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT refund claims) kwa wafanyabiashara ili kuhakikisha kwamba kuna mzunguko wa fedha wa kutosha katika biashara.
  11. UFISADI WIZARA YA MALIASILI NA UTALI
  12. Mheshimiwa Spika, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2018/19, imezungumzia ufisadi wa shilingi bilioni 2.5 iliyotumika kufanya tamasha la Urithi Festival ambapo shilingi milioni 500 zilitumika vibaya kununua basi moja tu. Aidha, Gazeti la Jamhuri la tarehe 21 Januari kupitia website yake ya www.jamhurimedia.co.tz, iliandika kwa undani tabia na mwenendo usiofaa wa Waziri wa wizara hii.
  13. Mheshimiwa Spika, baadhi ya tuhuma za waziri zilizoandikwa ni pamoja na uchotaji wa pesa katika mashirika yaliyo chini ya wizara na kutumia ndege za wizara mara kwa mara kubeba rafiki zake binafsi na wasanii. Kwamba amewahi kutumia ndege mojawapo ya Hifadhi za taifa (TANAPA) kumtoa mwandishi mmoja wa habari kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha na kwamba hata Mwandishi huyo alipochelewa kwa zaidi ya masaa 7, bado kwa agizo la Waziri ilimlazimu Rubani kumsubiri mpaka alipofika.
  14. Mheshimiwa Spika, kwa tuhuma zote hizo zinazochafua wizara na kukiuka maadili ya utumishi wa umma, Kambi Rasmi ya Upinzani inamshauri Mheshimiwa waziri Kigwangalla, kwa utashi wake mwenyewe ni vema akajiondoa kwenye wadhifa huo.
  15. Mheshimiwa Spika, iwapo Mhe Kigwangalla atashindwa kujiwajibisha wenyewe, basi Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri mamlaka yake ya uteuzi kumwajibisha ili kunusuru heshima na hadhi ya serikali dhidi ya ufisadi.

 

  1. HITIMISHO
  2. Mheshimiwa Spika, “Nearly anyone can offer a solution. Some can offer innovative solutions but world-class leaders offer evolution and revolution”,

“Karibu kila mtu anaweza kutoa suluhisho.Baadhi wanaweza kutoa masuluhisho yenye ubunifu fulani lakini viongozi bora duniani hufanya mageuzi na mapinduzi”

  1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haiungi mkono bajeti ya wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2020/21 kwasababu haijalenga hata kidogo kufanya mageuzi wala mapinduzi ya msingi, bali imelenga kufanya mambo yale yale madogo-madogo yasiyoweza kuifikisha nchi yetu popote. Mbaya zaidi, bajeti hii haijazingatia kwa kina athari za janga la covid-19 wala kuweka mikakati madhubuti ya kuihami sekta ya utalii dhidi ya anguko linaloendelea.
  2. Aidha, Mheshimiwa Spika, kupitisha bajeti hii katikati ya tuhuma kubwa za ufisadi zinazoikabili wizara hii, itakuwa ni sawa na sisi wabunge kushindwa kutimiza kikamilifu wajibu wetu wa msingi wa kuisimamia na kuiwajibisha serikali.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani haiungi mkono bajeti hii na tunalisihi Bunge lako tukufu lisiipitishe mpaka serikali itakapozingatia masula yote ya msingi tuliyoainisha; na mpaka hapo kiongozi mkuu wa wizara, Mhe Kigwangalla atakapojiwabisha au kuwajibishwa na Bunge hili au mamlaka yake ya uteuzi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha

……………………..

Peter Simon Msigwa (Mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

Mei, 2020

Share Button