HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI MHESHIMIWA ZUBEDA HASSAN SAKURU (MB) WIZARA YA MAJI KUHUSU UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2019/20 PAMOJA NA MPANGO WA MAENDELEO NA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2020/21

 (Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,

Toleo la Januari, 2016)

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na kuweza kusimama mbele ya ukumbi huu ili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu hoja iliyo mbele ya Bunge letu.

 

  1. Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe (Mb), ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi Hai, kwa imani yake kwangu kuwa Msemaji Mkuu wa Wizara ya Maji.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa kipekee kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwapa moyo watanzania wote hasa viongozi na wanachama wenzangu pamoja na wanaharakati wanaokabiliwa na kesi za aina mbalimbali nchini katika mapambano ya kudai haki na demokrasia katika nchi yetu. Mapambano yanaendelea.

 

  1. Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa utangulizi huo, naomba kutoa maoni ya Kambi Rasmi kuhusu Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha wa 2020/21.

 

  1. UMUHIMU WA MAJI

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa kwa ushirikiano wa shirika la afya duniami (WHO) na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), mabilioni ya watu duniani wanaendelea kutaabika kutokana na kukosa huduma bora za maji na masuala ya usafi. Takribani watu bilioni 2.2 duniani; hawana maji safi na salama ya kunywa, watu bilioni 4.2 hawana huduma salama za usafi na watu bilioni 3 wanakosa huduma za msingi na sehemu za kunawa mikono. VILEVILE, inakadiriwa kuwa kati ya watu 10 mmoja hana huduma za msingi na watu milioni 144 hunywa maji yasiyo safi na salama. Na takwimu zinadhihirisha kwamba watu 8 kati ya 10 katika maeneo ya vijijini wanakosa huduma hizo muhimu.
  2. Mheshimiwa Spika, hivyo ripoti hii imeweka wazi kuwa endapo nchi zitashindwa kuweka juhudi katika masuala ya usafi, maji salama na huduma za kujisafi basi tutaendelea kuishi na maradhi ambayo kitambo yangekua yamebaki kuwa kumbukumbu za kihistoria. hivyo, ni dhahiri kuwa ‘MAJI NI UHAI’.
  3. Mheshimiwa Spika, Maji ndio roho ya uchumi wa dunia, 19% ya matumizi ya maji ni kwa ajili ya viwanda, na 70% zaidi ni katika matumizi ya mnyororo wa uzalishaji kwenye sekta ya kilimo. Hivyo basi kuna jukumu la msingi kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals) kwenye sekta ya maji yanatekelezeka au yanatimizwa. Kwa mwaka 2018 hasara ya kifedha iliyotokana na maji Duniani ilikadiriwa kufikia dola za Kimarekani bilioni 36.[1]
  4. Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa maji safi na salama hupelekea kuwa na watu wenye afya bora ambacho ndio kichocheo cha ukuaji wa uchumi, vile vile afya bora inasaidia kuwepo kwa viwango bora vya elimu kwa wanafunzi. Takwimu zinaonesha kuwa upatikanaji wa maji safi na salama unaweza kuokoa kiasi cha takribani shilingi bilioni 521 kwa mwaka kwenye uchumi wa nchi. Au kuokoa tija yenye thamani ya 1% ya pato ghafi la Taifa ambayo ingepotea kutokana na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.

 

  1. Mheshimiwa Spika, takriban 60% ya watanzania wanapata maji, lakini swali kubwa la kujiuliza je, maji hayo ni safi na salama? Zaidi ya 50% ya watanzania wanatumia zaidi ya dakika 30 kufuata maji. Na ikumbukwe kuwa wahanga wakubwa wa ukosefu wa maji safi na salama ni kina mama na watoto kwani hutumia muda mwingi na kutembea umbali mrefu kufuata maji ambayo pengine pamoja na upatikanaji wake bado si salama. Tumeshuhudia katika majiji makubwa ikiwemo Dar Es Salaam, upangaji wa foleni, kutembezwa maji katika madumu yasiyo kidhi usafi ili kuweza kuhudumia familia zenye uhitaji wa maji. Hali ni mbaya kwa maeneo ya vijijini ambapo wananchi wameendelea kufuata maji kwa umbali mrefu, foleni zenye kuleta kero na fedhea ili kupata huduma muhimu ya maji ambayo bado tunatafsiri kuwa si safi na salama! Watanzania wengi wanalazimika kutumia takriban 5% ya matumizi yao kwenye maji kulinganisha na kiwango cha kimataifa cha 2%[2]. Hii maana yake ni kwamba maji bado ni tatizo kubwa katika maisha ya watanzania.

 

  1. Mheshimiwa Spika, taarifa ya hali halisi ya sekta ya maji kama ilivyotolewa mwaka 2017 (National Environmental Status Report 2017) inaonesha kuwa kwa mwaka 2016, watu 6 kati ya 10 ambao ni sawa na 59.7 % wanapata maji kutoka kwenye vyanzo vya maji safi na salama. Lakini kwa maeneo ya mijini ni takriban watu 9 kati ya 10 wanapata maji ya kunywa kutoka vyanzo salama[3].

 

  1. Mheshimiwa Spika, kama nilivyoainisha awali taarifa hii kwa nchi zinazoendelea makundi ambayo ni wahanga wakuu wa tatizo la maji ni wanawake na watoto.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wanawake wamekuwa wahanga wakubwa katika tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama. Hii ni kutokana na shughuli nyingi za kifamilia zinazohitaji maji kama vile, matumizi ya maji katika uzalishaji na uandaaji wa vyakula, matumizi mahususi ya maji kwenye afya ya uzazi na kadhalika.
  2. Mheshimiwa Spika, jambo ambalo halina ubishani wa aina yoyote ni kuwa Wawanake ndio wanapoteza muda mrefu sana kwenda kutafuta maji hali inayodunisha vipato vyao pamoja na kuhatarisha ustawi wao.
  3. Mheshimiwa Spika, Wanawake pia ndio wamekuwa wahanga wakubwa kwa matukio ya udhalilishaji na ukatili kama vile ubakaji na kesi nyingine nyingi za kudhuru mwili wanazokumbana nazo wakiwa katika safari za kutafuta maji[4]. Pia kuna ushahidi wa kutosha kuwa ndoa nyingi  zimevunjika kutokana na changamoto za maji, hivyo inatosha kusema kampeni ya kumtua mwanamke ndoo kichwani imeshindwa.
  4. Mheshimiwa Spika, ukosefu wa kipaumbele na umakini katika kutatua changamoto za sekta ya maji nchini unaweka rehani ustawi wa sekta muhimu zinazotegemea maji kama chanzo hasa sekta ya uzalishaji, umwagiliaji na kilimo, viwanda na nishati ya umeme. Bila kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji hasa katika kipindi hiki tunapokabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ni dhahiri kuwa kama nchi , hatutaweza kufanikisha lengo lolote la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa sababu maji yanagusa kila lengo na mfumo mzima wa maisha ya binadamu.

 

  1. MAHITAJI NA MATUMIZI YA MAJI
  2. Mheshimiwa Spika, Hivi sasa matumizi ya maji hapa nchini kwa sekta mbalimbali za huduma na uzalishaji yanakadiriwa kufikia kilomita za ujazo 40. Takwimu zinaonesha kuwa kiasi cha maji kwa mtu kwa mwaka kimeendelea kupungua kutoka wastani wa mita za ujazo 7,862 mwaka 1962 wakati nchi ikiwa na idadi ya watu milioni 10.6 hadi kufikia wastani wa mita za ujazo 2,250 mwaka 2018 nchi ikiwa na idadi ya watu wapatao milioni 56[5]. Jambo hili linasababisha nchi yetu kuwa juu ya mstari wa uhaba wa maji dunia (water stress). Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji je ni mikakati endelevu ya utunzaji wa vyanzo vya maji imewekwa na Serikali nchini?

 

  1. Mheshimiwa Spika, sekta ya maji ina muongozo wake juu ya matumizi na namna gani ya kuendeleza sekta hiyo chini ya programu ya maendeleo ya maji ya mwaka 2006-2025(Water Sector Development Programme 2006-2025). Programu hii ni jumuiko la Sera ya taifa ya maji-NAWAPO ya mwaka 2002 pamoja na mkakati wa taifa wa kuendeleza sekta ya maji wa mwaka 2006 (National Water Sector Development Strategy –NWSDS, 2006). Programu ilikuja kama utekelezaji wa mkakati na sera ya maji ili kukidhi malengo ya MKUKUTA kwenye sekta ya maji.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa fedha zilizotumia kutekeleza awamu ya kwanza ya Programu ya maendeleo ya maji (WSDP Phase I (2007-2015) takwimu zinaonesha kuwa zilitumia bilioni 1.6 za kimarekani wakati Sekta ilihitaji takribani bilioni 3.33 za kimarekani kuondoa kabisa mapungufu katika kupanga utekelezaji wa awamu ya II ya WSSD ambayo ilitakiwa kutekelezwa hadi mwaka 2021. Kati ya kiasi hicho Serikali na wadau tayari walikuwa na kiasi cha bilioni 1.93 za kimarekani na hivyo kuwepo na upungufu wa bilioni 1.4 za kimarekani ambacho kingefidiwa kwa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta binafsi[6].

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika Randama ya Wizara inaonesha kuwa Wizara imepanga kufanikisha malengo ya muda wa kati kwa kuhakikisha kuwa makundi yote ya jamii yanapata huduma inayoridhisha ya maji safi na usafi wa mazingira kwa kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kufikia asilimia 85 kwa wakazi wa vijijini na kufikia asilimia 95 kwa maeneo ya mijini ifikapo 2020;Lakini katika taarifa ya Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Maji, inaonesha kuwa ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa maji safi na salama kwa vijijini utafikia 95%;  makao makuu ya mikoa na Jiji la Dar es Salaam itafikia 100%.Uwiano kwa nyumba za vijijini ambazo zitakuwa na huduma bora za usafi wa maji kwa 85%; makao makuu ya mikoa na wilaya 70% na Dar es Salaam, 60%.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Twaweza[7] ulibaini changamoto kuu tatu katika upatikanaji wa maji vijijini ambazo ni umbali wa vyanzo vya maji, uhaba wa vyanzo vya maji na maji machafu. Tunapofikia ukomo wa miaka mitano ya awamu ya tano ambayo ni mwaka 2020, je ni kweli Serikali imeweza kufikia asilimia 85 kwa vijijini na asilimia 95 kwa mijini kama ilivyoahidi pia katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015 au bado tunaendelea na hekaya za abunuwasi?

 

  1. Mheshimiwa Spika, tumefanya nukuu ya takwimu za matumizi ya fedha za awamu ya kwanza ya WSDP kwa lengo kuonesha wingi wa fedha ambao tayari umetumika, lakini ukweli na hali halisi ni kuwa tija yake ni ndogo na haijatatua changamoto katika kuhakikisha kila mtanzania anapata maji safi na salama. Hili linatokana na usiri unaogubika kuanzia mradi wenyewe, gharama zake na utoaji wa zabuni kwa mkandarasi. Je, wananchi walishirikishwaje katika kuhakikisha nao wanakuwa sehemu ya miradi hiyo ya maji? Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoweka mazingira ya usiri, ubabaishaji katika kutekeleza miradi ambayo inalenga kuwapa wananchi maji safi na salama.

 

  1. MFUMO WA MAJI TAKA
  2. Mheshimiwa Spika, ni bahati mbaya sana kuwa Serikali imeshindwa kuwekeza vya kutosha katika kukabiliana na tatizo la majitaka nchini hali inayopelekea mifumo ya maji taka kuingiliana kwa kiasi kikubwa na mifumo ya maji safi na hivyo kuhatarisha afya na mazingira kwa ujumla hasa kwa miji mikubwa.
  3. Mheshimiwa Spika, ni ajabu kuona mpaka sasa, Serikali imeweka lengo la kuwa na mifumo ya maji taka katika miji na makao makuu ya mikoa kufikia asilimia 30 tu ifikapo mwaka 2025. Hii inatoa taswira kuwa, serikali haina mpango wa kuhakikisha usalama wa watumiaji wa maji kwa asilimia 70 kufikia mwaka 2025. Hivyo bado kuna hatari kubwa kwa maeneo yanayoendelea kuwa na mvua kubwa kukumbwa na mafuriko kwa kuwa miundombinu ya sehemu hizo itaendelea kuelemewa na maji taka yanayotokana na kutapishwa kwa vyoo na kufanya tatizo hilo kuzaa matatizo mengine ikiwemo matatizo ya kiafya.

 

  1. Mheshimiwa Spika, aidha, tafiti zilizofanywa na TAWASANET (“no one left behind”) zinaonesha kuwa 35% ya vyanzo vya maji katika maeneo mengi ya Dar na 52% kwa maeneo ya Mkoa wa Morogoro yalionesha uwepo wa mchanganyiko wa “vinyesi” katika mifumo ya maji yanayotumiwa na wananchi. Hii ina maana kuwa, kuna hatari kubwa ya magonjwa ya milipuko hasa kwenye vipindi vya masika.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Dar es Salaam 57% ya kinyesi (vyoo vya shimo) kinaingia  kwenye mfumo wa mazingira bila kuwekewa dawa ya aina yoyote  na ujazo wa 2164m3 ya maji taka yasiyo tiwa dawa unaingia kwenye mfumo wa maji ya Dar Es Salaam  kila siku.  Kwa takwimu hizo za kutisha zinachangia kuongezeka kwa gharama za kukabiliana na magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.  Toka Augusti mwaka 2015 nchi imeshuhudia wagonjwa 33,421 na vifo 542 kutokana na kipindupindu.

 

  1. Mheshimiwa Spika, inabashiriwa kuwa janga kubwa la mafuriko hasa kwa mijini linaweza kuchangia takribani anguko la 2% ya GDP kutokana na mabadiliko ya tabianchi tufikapo 2030. Hivyo, kutokuwa na mifumo mizuri ya maji taka kuna athari kubwa katika maisha ya jamii ya kila siku kwa kuwa maji taka yamekua kero kubwa kwa biashara kama yadi, mama ntilie, masoko, matumizi ya barabara na hata kuleta athari kubwa kwenye mazingira ya shule ambapo wanafunzi uathiriwa na uchafuzi wa mazingira unaotokana na mifumo duni ya maji taka[8].

 

  1. Mheshimiwa Spika, takwimu za randama zinaonesha kuwa tangu tupate uhuru hadi desemba mwaka 2018  kaya ambazo zilikuwa zimeunganishwa katika mifumo wa maji taka nchini ni 48,566 tu, na kufikia desemba 2019 zikaongezeka kaya 1842 na hivyo kufanya jumla kuwa kaya 50,408.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kaya hizo zipo katika miji 10 tu, ambayo ndiyo yenye mitandao ya maji taka. Maana yake ni kwamba itatuchukua tena miaka hamsini kuweza kuweka mtandao wa maji taka nchi nzima.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kupitia wizara ya Maji , kuweka mkakati mathubuti utakaokabiliana na mahitaji ya kuwa na mifumo imara ya majitaka kwa kiwango kikubwa hasa katika maeneo korofi nchini ili kukabiliana na changamoto za kimazingira na kiafya zinatojitokeza kwa kushindwa kuwa na mifumo hiyo hasa katika kipindi hichi cha mabadiliko ya tabia nchi.

 

  1. UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2019/20

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/20, Wizara iliomba na kuidhinishiwa jumla ya shilingi Bilioni 610.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya kiasi hicho shilingi Bilioni 349.4 zilikuwa ni fedha za ndani na shilingi 261.0 Bilioni zilikuwa ni fedha za nje. Hadi Februari 2020, Wizara ilikua imepokea jumla ya shilingi Bilioni 312.7 sawa na silimia 51.2 ya fedha zote za miradi ya maendeleo ambapo fedha za ndani zilizokuwa zimetolewa ni shilingi Bilioni 151.3 sawa na 43% tu na fedha za nje shilingi 161.5 sawa na 57%. Hii inaonesha kuwa, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutegemea fedha za wahisani na kushindwa kuhudimia sekta ya maji ambayo ndio sekta ya muhimu kwa fedha zake za ndani na hivyo kuendeleza utegemezi wa Bajeti kwa wahisani.
  2. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa muda mrefu imeendelea kuwa na miradi ambayo imeshindwa kuisimamia kiikamilifu ili iweze kukamilika na kuwa na tija kwa muda wa miaka minane mfululizo ikiwemo mradi wa bwawa la kidunda na wa visima vya Mpera na Kimbiji. Madhara yake ni kwamba gharama zinazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na ukweli kwamba thamani ya shilingi yetu dhidi ya Dola ya Kimarekani inazidi kuporomoka. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kukamilisha miradi hii ambayo imeendela kuwa kiporo kabla ya kuanzisha miradi mingine ili kuongeza ufanisi, tija na kutimiza ahadi zake kwa wananchi.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa mradi wa bwawa la Kidunda ambao ungesambaza maji kwa mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Pwani ni mradi ambao ungeweza kupunguza madhara ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa maeneo mengi ya Mkoa wa Morogoro ambao tumeona ni jinsi gani wananchi wa kata nyingi za vijijini wanavyopata taabu sana na upatikanaji wa maji safi na salama.
  4. Mheshimiwa Spika, kuna mradi ambao pia ulikuwa katika mpango wa kwanza wa maendeleo wa miaka mitano wa kuboresha upatikanaji wa maji katika miji ya Same na Mwanga ambao ulikuwa umetengewa jumla ya shilingi 29,281,000,000.00. Lakini hadi mwezi februari zilikuwa zimetolewa jumla ya shilingi 2,135,860,946.18 sawa na 7.3% ya fedha zilizoombwa na kuidhinishwa na Bunge.
  5. Mheshimiwa Spika, pia kuna mradi mkubwa wa kutoa maji ziwa Viktoria kwenda Shinyanga/Kahama hadi Tabora wa shilingi 23,500,000,000.00 hakuna hata shilingi iliyotolewa na tukumbuke kuwa wakandarasi wako site. Jambo hili linazidisha gharama za mradi. Aidha kuna mradi wa ziwa Viktoria Shinyanga hadi Kahama wa shilingi 23,810,000,000.00 hadi februari zimetolewa shilingi 3,332,861,207.50 tu sawa na 13.99%.
  6. Mheshimiwa Spika, mradi wa maji wa Masasi/ Nachingwea ulioidhinishiwa kiasi cha shilingi 1,500,000,000.00 lakini hadi kufikia mwezi februari 2020, hakuna hata shilingi iliyotolewa kwa ajili ya mradi huo. Ni dhahiri kuwa Serikali imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa kushindwa kuwa na vipaumbele vya msingi hususani katika kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.
  7. Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo la kutokutolea fedha za miradi ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama, Randama inaonesha kuwa zilitolewa jumla ya shilingi 5,909,000,000.00 kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi wa wizara na mamlaka za maji mijini ili kutekeleza program ya WSDP.
  8. MFUMO WA TAIFA WA USAMBAZI MAJI (NATIONAL WATER SUPPLY GRID)
  9. Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa mfumo wa Taifa wa Usambazi Maji umelenga kuhusisha utoaji wa maji katika vyanzo vya uhakika vya maji ikiwemo maziwa makuu matatu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa na kuyafikisha katika mikoa yenye uhaba wa maji ikiwemo mikoa ya Singida na Dodoma.
  10. Mheshimiwa Spika, ni mara nyingi tumekuwa tukiihasa Serikali juu ya utiririshaji wa maji yenye heavy metals kama vile cyanide na mercury kwenye vyanzo vya mito inayomwaga maji yake hasa kwenye ziwa Viktoria, lakini hatujawahi kupatiwa jibu kuhusiana na jambo hilo. Tukumbuke kuwa shughuli za wachimbaji wadogo wadogo wa madini hasa dhahabu zinafanyika sana kwenye mito na pale mvua za masika zinapoanza, mabaki yote ya mercury na cyanide yanaelekea kwenye ziwa Victoria. Kwa maneno mengine mfumo huo wa usambazaji wa maji wa taifa usiposimamiwa kikamilifu ikiwemo kuyatibu maji hayo ipasavyo basi itakua ndio chanzo kikuu cha ugonjwa wa kansa kwa watanzania.

 

  1. USIMAMIZI NA UENDELEZAJI WA RASILIMALI ZA MAJI
  2. Mheshimiwa Spika, Kati ya kiasi cha maji cha mita za ujazo bilioni 126 zinazokadiriwa kupatikana hapa nchini kwa mwaka, asilimia 43.4[9] ya maji hayo yapo katika vyanzo vya majishirikishi. Vyanzo hivyo vipo katika Mabonde saba kati ya tisa yaliyopo nchini ambavyo ni maziwa ya Victoria, Tanganyika, Nyasa, Natron, Chala na Jipe pamoja na mito ya Kagera, Mara, Malagarasi, Momba, Mwiruzi, Umba, Ruvuma na Songwe. Usimamizi wa rasilimali za majishirikishi unafanyika kupitia Taasisi za Kikanda na Kimataifa zilizoundwa kwa ushirikiano wa nchi wanachama. Tanzania ni mwanachama katika Taasisi zifuatazo: Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika, Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi (Zambezi Watercourse Commission – ZAMCOM); Taasisi ya Mpito ya Bonde la Mto Nile (Nile Basin Initiative – NBI); Kamisheni ya Bonde la Mto Songwe; Mamlaka ya Usimamizi wa Bonde la Ziwa Tanganyika (Lake Tanganyika Authority – LTA); na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria.
  3. Mheshimiwa Spika, kutokana na ushirikiano huo wa maji, gharama za usimamizi na uendelezaji wa kamisheni hizo nazo zinakuwa ni shirikishi, jambo hilo linatoa unafuu mkubwa kwa Tanzania. Na ukweli ni kuwa majirani zetu wao wanathamini sana sekta hii ya maji hivyo wanafanya juhudi kubwa kuhakikisha kunakuwepo na uendelevu wa kamisheni hizo za usimamizi wa mabonde hayo.

 

  1. Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana kuwepo kwa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji hapa nchini, lakini rasilimali za maji ambazo zimezoeleka kwa wengi ni zile ambazo ziko juu ya ardhi. Takwimu zinaonesha kuwa na wastani wa mita za ujazo bilioni 105[10], na mita za ujazo bilioni 21 chini ya ardhi.
  2. Mheshimiwa Spika, mojawapo ya sababu zinazoongeza ukiritimba mkubwa katika matumizi ya rasilimali maji iliyo chini ya ardhi, Serikali inasema kwamba;

Udhibiti wa Uchimbaji Holela wa Visima Udhibiti wa uchimbaji holela wa visima umeendelea kwa kuratibu na kusajili kampuni za utafiti na uchimbaji wa visima pamoja na kutoa leseni na vibali vya uchimbaji kwa makampuni yanayokidhi vigezo. Aidha elimu imeendelea kutolewa kwa wananchi wanapotaka kuchimbiwa visima waombe vibali vya kuchimba visima kutoka katika Bodi za Maji za Mabonde. Vibali hivyo vinawawezesha kulindwa kisheria na kupata taarifa sahihi za uwepo wa maji na ubora wake katika maeneo yao kabla hawajachimba. Hadi mwezi Februari 2020, leseni mpya 52 za utafiti na uchimbaji wa visima na vibali 225 vya kuchimba visima vya maji katika maeneo mbalimbali nchini vimetolewa. 

 

  1. Mheshimiwa Spika, maana yake ni kuwa hata wale ambao wanahitaji kuwekeza kwenye kilimo hawataweza kuchimba visima kwa ajili ya kuendeleza kilimo kulingana na aina ya mazao anayolima. Hii ni changamoto kubwa kwa kuwa kwani jambo hili limekuwa la jumla mno na pia linaweza kuleta migogoro mkubwa pale mkulima anapotoa fedha kwa ajili ya kuchimbiwa kisima na matokeo yake inakuwa kama ile miradi ya visima kumi kila wilaya, ambavyo hadi leo havitoi maji na hiyo hasara ilikwenda kwa walipa kodi.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka mfumo madhubuti na imara wa uratibu kwenye matumizi ya rasilimali ya maji yaliyo ardhini chini ya idara ya umwagiliaji na sio kuhusisha makampuni binafsi ya wafanyabiashara.

 

 

  1. UNAFUU WA ANKARA ZA MAJI KUKABILIANA NA JANGA LA KIDUNIA LA KORONA
  2. Mheshimiwa Spika, wakati huu ambao dunia nzima inapambana na janga kubwa la Virusi vya Korona, yaani COVID-19, kumekua na ongezeko kubwa la matumizi ya maji nchini hasa ukizingatia kuwa kumekua na kampeni mbalimbali za kuwataka wananchi kutumia maji yanayotiririka kama njia mojawapo ya kukabiliana na ugonjwa huu.
  3. Mheshimiwa Spika, Mamlaka mbalimbali duniani na Afrika, zimechukua hatua zaidi kwa kuwaondolea wananchi kadhia za ukosefu wa maji safi na salama kwa kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji wa maji safi na salama muda wote. baadhi ya nchi zilizochukua hatua hizo ni pamoja na Ghana, Kenya, Chad . Hivyo basi, Kambi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuziagiza mamlaka za maji nchi kutokata maji kwa wadaiwa wa maji kwa kipindi hiki pamoja na kuchukua jukumu la kulipia Ankara za maji kwa wananchi wote kwa kipindi cha miezi sita toka kampeni za kujikinga kwa kunawa zilipoanza yaani Mwezi Machi 2020.
  4. Mheshimiwa Spika, hatua hii si tu itaweza kuwaokoa wananchi, bali itasaidia kuwapa wananchi ahueni ya kiuchumi. Kuna maana nyepesi ya Serikali iliyotolewa na aliyewahi kuwa Rais wa Marekani, Abraham Lincolin government of the people, by the people, for the people’ yaani “Serikali ya watu, kutokana na watu kwa ajili ya watu”. Serikali haiwezi kuwa Serikali ya watu iwapo itashindwa kutoa ahueni kwa watu wake ili kuwaokoa na janga hili la korona kwa kutoa msamaha wa Ankara katika kipindi hichi kigumu.

 

  1. MAPITIO YA BAJETI KWA MIRADI MAENDELEO YA MAJI KUANZIA 2015/16 HADI 2018/19
  2. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 Wizara ya Maji na Umwagiliaji Fungu 49 na Fungu 05 iliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 565.9. Fungu 49, liliidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 512.5 kati ya fedha hizo shilingi bilioni 27 ni fedha za matumizi ya kawaida (fedha hizi zinajumuisha mishahara shilingi bilioni 18 na matumizi mengineyo shilingi bilioni 9 . Na kiasi cha shilingi bilioni 485.3 zilitengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.
  3. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Aprili 2016, fungu 49 lilikuwa limepokea fedha za maendeleo shilingi bilioni 137 tu kati ya shilingi bilioni 485.3 zilizotengwa ambazo ni sawa na asilimia 28 ya bajeti yote ya maendeleo.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 Fungu 49 likiidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 938.3. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 913.8 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
  2. Mheshimiwa Spika, lakini hadi mwaka huo wa 2016 /17 unamalizika wizara fungu 49 ilipokea fedha za maendeleo jumla ya shilingi bilioni 231. tu sawa na asilimia 25.7 ya bajeti yote ya maendeleo.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/18 fungu 49 liliidhinishiwa na Bunge fedha za maendeleoz jumla ya shilingi bilioni 624. Lakini hadi mwezi Machi 2018 fedha za maendeleo zilizokuwa zimepokelewa ni shilingi bilioni 135.2 sawa na asilimia 22 ya fedha zote za bajeti ya maendeleo kwa Wizara ya Maji-fungu 49.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 bunge lilinaombwa kuidhinisha fedha za miradi ya maendeleo yenye jumla ya shilingi bilioni 673.2 kati ya fedha hizo shilingi bilioni 443.2 sawa na asilimia 66 zilikuwa ni fedha za ndani na shilingi bilioni 230 sawa na asilimia 34 zilikuwa ni fedha za nje.
  2. Mheshimiwa Spika, hadi Mwezi February 2019 jumla ya shilingi bilioni 100.1 sawa na 15% ndizo zilizokuwa zimetolewa. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 95. 3 sawa na asilimia 22 ya fedha za ndani. Fedha za nje zilizotolewa ni shilingi bilioni 4.7 tu sawa na asilimia 2.06 ya fedha za nje. Takwimu hizi zinaonesha kuwa fedha za maendeleo zinazotolewa zinakuwa zikipungua kila mwaka hii ni dhahiri kuwa Maji sio kipaumbele kwa Serikali ya CCM.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/20 wizara iliomba fedha za maendeleo jumla ya shilingi bilioni 610.5 au 610,469,888,530.00 kati ya fedha hizo shilingi bilioni 349.45 au 349,449,000,000.00 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 261.021 au 261,020,888,530 ni fedha za nje. Bajeti ya maendeleo ilikuwa ni pungufu kulinganisha na ile ya mwaka 2018/19 kwa shilingi bilioni 62.7 au 62,744,145,147.00 sawa na asilimia 9.32
  4. Mheshimiwa Spika, hadi mwezi februari 2020 fedha za maendeleo za ndani zilizokuwa zimetolewa ni shilingi 151,284,580,290.00 sawa na 43.29% tu, ya fedha za ndani zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge na fedha za nje zilizokuwa zimetolewa hadi februari 2020 ni shilingi 161,485,277,389.00 sawa na 61.9% ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge. Hii maana yake ni kuwa Serikali imeshindwa hata kufikisha asilimia 50 ya fedha zake za ndani katika kutekeleza miradi ya maendeleo huku fedha za wahisani zikivuka asilimia 50 katika miradi ya maendeleo. Hii inaonesha kuwa kuna utegemezi mkubwa wa fedha za wahisani katika miradi ya maendeleo na Serikali imeshindwa kuipa sekta ya maji kipaumbele kinachostahili.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/21, fedha zinazoombwa kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni Shilingi 697,085,149,000 kupitia Fungu 49 (Wizara ya Maji). Kati ya fedha hizo, jumla ya Shilingi 349,449,000,000 sawa na asilimia 50.1 ni fedha za ndani na Shilingi 347,636,149,000 sawa na asilimia 49.9 ni fedha za nje.
  2. Mheshimiwa Spika, ukifanya ulinganisho wa fedha zinazoombwa mwaka 2020/21 kiasi cha shilingi 697,085,149,000.00 na zile zilizoidhinishwa mwaka 2019/20 shilingi 610,569,888,530.00 kunatofauti ya jumla ya shilingi 86,515,260,470.00. Utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2019/20 haukufikia asilimia 55, sasa inawezaje kuongeza bajeti kwa kiasi hicho na wakati huu duniani kumekuwa na anguko kubwa la uchumi kutokana na janga la Korona na na hivyo kuathiri makusanyo yetu ya kodi kuliko miaka yote?

 

  1. MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA 2020/21
  2. Mheshimiwa Spika, mpango wa maendelo kwa mwaka wa fedha 2020/21 kwa asilimia kubwa ni muendelezo wa miradi ya ambayo ilikuwepo na miaka yote tokea awamu ya nne ya Serikali ilikwishaanza lakini imekuwa haipatiwi fedha.
  3. Mheshimiwa Spika, miradi ambayo kwa bajeti inayomalizika hakuna fedha iliyotengwa lakini mwaka huu zimetengwa fedha zile zile au zimeongezwa ni kama ifuatavyo; Mradi wa maji wa Masasi Nachingwea, ulikuwa umetengewa jumla ya shilingi 1,500,000,000.00 sasa kwa mwaka 2020/21 umetengewa jumla ya shilingi 2,000,000,000.00; Mradi wa maji toka ziwa Viktoria kwenda Kahama na Shinyanga ulikuwa na shilingi 23,810,000,000. Zikatolewa shilingi 3,332,681,207.50 tu, sasa umetengewa shilingi 26,491,000,000.00; Ujenzi wa bwawa la Kidunda mwaka jana ziidhinishwa jumla ya shilingi 3,000,000,000.00 lakini haikutolewa hata senti moja, mwaka huu wa fedha zimetengwa tena shilingi 3,000,000,000.00; Uchimbaji wa visima vya Mpera na Kimbiji zilikuwa nimeiidhinishwa jumla ya shilingi 3,000,000,000.00 lakini hakuna hata senti moja iliyotolewa, mwaka 2020/21 zimeombwa tena shilingi 3,000,000,000.00.; Kuboresha upatikanaji wa maji katika miji ya Mwanga na Same zilikuwa zimeethinishwa shilingi 29,281,000,000. Zikatolewa shilingi 2,135,860,946.10 tu. Mwaka huu wa fedha zinaombwa shilingi 29,200,000,000.00. Sasa hii ni mifano tu, na tukumbuke mazingira ya upatikanaji wa fedha za kodi kwa mwaka huu yatakuwa ni magumu sana kutokana na hali halisi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona ulivyo athiri biashara nyingi hapa nchini.
  4. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa Serikali imeendelea kuweka mipango ambayo haiwezi kutekelezwa kwa kuwa haina fedha za kutosha kuweza kuitekeleza. Huu unakua ni muendelezo wa hila za Serikali kwa wananchi.

 

  1. HITIMISHO
  2. Mheshimiwa Spika,nimalizie kwa kuitaka Serikali kujitafakari kwa kina ni kwa kiwango gani imeweza kutatua changamoto za maji nchini hasa kwa kuhakikisha kuwa watanzania wanapata maji safi na salama . Lakini kwa kuwataka waheshimiwa wabunge, hasa ambao walitumia tatizo la uhaba wa maji katika majimbo yao kama kete ya kuombea kura kwa wananchi, je, ndani ya miaka mitano ya awamu ya tano; wameweza kutatua kero ya maji katika majimbo yao? Je, mwanamke ametuliwa ndoo ya maji kama kaulimbiu illivyokuwa inataka? tunaporudi kuomba kura kwa mara nyingine….. mjiulize, tulipowaahidi kuwatatulia changamoto ya maji, tulitekeleza ama ndio yatakua yale yale ya mfalme Juha na watu wake?
  3. Mheshimiwa Spika, napenda kuwatakia waislam wote mfungo mwema wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Ramadhan Kareem.
  4. Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

 

Zubeda Hassan Sakuru (MB)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI-WIZARA YA MAJI

27.04.2020

[1] RIPOTI YA MAJI DUNIANI   “Global Water Report 2018”

[2] Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET) March 2019, Water Sector Equity Report 2019,

[3] Sectors Ministers’ meeting 2019, San Jose’ –Costa Roca 4-5 April, Tanzania Country Report.

[4] Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Sera ya Wanawake- Machi 2020

[5] RANDAMA YA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA YA MAJI KWA MWAKA 2020/21-  Machi  2020

[6] Sector Ministers’ Meeting  2019,  San Jose’ –Costa Rica 4-5 April

[7] Safi na salama? maji, usafi na Afya Mazingira (2017)

[8] Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET) March 2019, Water Sector Equity Report 2019

[9] Randama ya wizara ya maji 2020/21 uk.22

[10] Randama ya Wizara 2020/21 uk.9

Share Button