HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA HALIMA JAMES MDEE (MB), KUHUSU BAJETI YA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016

_______________

 

  1. UTANGULIZI:
  2. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, Mheshimiwa Halima James Mdee, naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021.
  3. Mheshimiwa Spika, kabla sijawasilisha maoni hayo, napenda kutumia fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwasilisha taarifa hii. Aidha, ninapenda kutumia fursa hii, kumshukuru Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb) kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango.
  4. Mheshimiwa Spika, nikiwa kama Mtunza Hazina wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) Taifa, ninapenda kutumia nafasi hii kwa niaba ya Bawacha kukishukuru sana Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa kuona na kuthamini uwezo wa wanawake katika masuala nyeti kama haya ya usimamizi wa Fedha na Uchumi wa Taifa kwa ujumla. Kwa niaba ya Bosi wangu – Waiziri Kivuli wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Halima James Mdee (Mb) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema Taifa; napenda kukihakikishia chama chetu kuwa tutendelea kuitendea haki dhamana tuliyopewa kwa uaminifu mkubwa; na daima tutahakikisha kuwa maslahi ya chama yanalindwa kwa wivu mkubwa!
  5. Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia utangulizi wangu kwa kuwashukuru sana wananchi wote wa Mkoa wa Mara na hususan wa Jimbo la Serengeti ambao kwa muda wote wamekuwa wakinipa ushirikiano wa kila hali katika kutekeleza majukumu yangu ya kibunge. Napenda kuwahakikishia kuwa nafasi waliyonipa ya kuwatumikia imeniimarisha zaidi; naimenipa hamasa ya kuendelea kuwatumikia. Hivyo ninawaomba wasisite kuniunga mkono ikiwa chama kitanipa ridhaa ya kuwawakilisha Bungeni.
  6. MAJUKUMU NA WAJIBU WA WIZARA YA FEDHA
  7. Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa Instrument ya Mgawanyo wa kazi kwa kila Wizara; Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo msimamizi mkuu wa Uchumi wa nchi, na majukumu yake  mahsusi ni pamoja na  kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na ya nje;  kusimamia matumizi ya Serikali, kusimamia utendaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma, kusimamia manunuzi ya Serikali na Taasisi na Mashirika ya Umma, kusimamia Deni la Taifa na dhamana za Serikali, kutafuta suluhisho na kusimamia mfumo wa kodi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kupambana na Fedha haramu. Aidha, jukumu linguine ni kusimamia na kutekeleza Mpango wa Kupunguza Umasikini nchini kupitia  Programu ya  MKUKUTA II.
  8. Mheshimiwa Spika, Kutokana na majukumu hayo muhimu nan yeti kwa mustakabali wa uchumi wa Taifa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitazama Wizara ya Fedha Mipango pamoja na mafungu yote yaliyo chini yake kama ndio moyo wa Serikali; na kwa sababu hiyo, Wizara hii haina bundi kutazamwa kwa jicho kali na kutilia shaka kila jambo linalofanywa na Wizara hii kwa lengo la kuhakikisha kwamba kila kitu kinafanywa wa usahihi na ufanisi mkubwa ili moyo huu usisimame; kwa kuwa ukisimama maana yake ni kifo cha uchumi; na uchumi ukifa ni kifo cha Taifa.
  1. Mheshimiwa Spika, ni katika msingi huo, ambapo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itatimiza wajibu wake wa kikatiba na kikanuni kuisimamia ipasavyo Wizara ili fedha za umma, ziweze kutumiwa kimaadili kwa manufaa ya umma wenyewe; lakini zaidi sana mipango ya uchumi iweze kutekelezwa kwa ufanisi ili kuleta ustawi na maendeleo kwa wote.
  2. USIMAMIZI WA SERA ZA FEDHA
  3. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa majukumu ya Wizara ya fedha ni pamoja na kusimamia sera ya fedha kikamilifu. Hata hivyo, wizara hii imeonyesha udhaifu mkubwa sana katika kuutekeleza wajibu huo.
  4. Mheshimiwa Spika, suala la vitambulisho vya wajasiriamali lilitakiwa, kwa mujibu wa sheria, kuratibiwa na kutekelezwa kwa asilimia 100 na Wizara ya Fedha. Kinyume na uhalisia huo, Taifa limebaki kwenye mshango mkubwa kuona suala hilo likishughulikiwa na vyombo vingine ambavyo havina mamlaka ya kisheria kuhusu masuala ya fedha.
  5. Mheshimiwa Spika, jambo hili limeleta mkanganyiko mkubwa na mgongano wa majukumu miongoni mwa Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.  Mpaka sasa Wizara ya Fedha haijatoa tamko au mwongozo wowote, wa namna ya kuendesha zoezi hilo. Matokeo yake kila Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa anajitengenezea mwongozo wake. Na kutokana na mkanganyiko huo, zoezi hilo ni kama vile limepoteza mwelekeo. Hatusikii tena  habari ya vitambulisho vya wajasiriamali likizungumzwa. Ni jambo lilizuka tu na kuwa kuwa halikuwa katika utaratibu wa kisera basi linaelekea kufa kiholela kama lilivyoanza kiholela.
  6. Mheshimiwa Spika, pamoja na vitambulisho vya wajasiriamali kutofuata utaratibu, zoezi hilo limekwenda pia kunyang’anya vyanzo vya mapato vya halmashauri na kuziacha zikiwa muflisi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo, ni kwa nini Ofisi ya Rais TAMISEMI inaingilia majukumu ya Wizara ya Fedha? Aidha, tunaitaka Serikali ilieleza Bunge hili ni mapato kiasi gani yamepatikana kutoka na utaratibu wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo na utaratibu huo ni endelevu kwa kiwango gani?
  7. DENI LA TAIFA NA HATMA YA UCHUMI WA NCHI
  8. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa majukumu msingi ya Wizara ya fedha  ni pamoja  kusimamia deni la Taifa. Wizara imeonyesha udhaifu mkubwa katika kusimamia  Deni la Taifa, kwa kuwa Deni hili  limeendelea kuwa  kubwa kila mwaka jambo ambalo limekuwa na athari kubwa katika bajeti ya Serikali na hivyo kuathiri uchumi wetu na maisha ya wananchi kwa jumla.
  9. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2018/19; ni kwamba hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2019, deni la Serikali lilikuwa limefikia Shilingi trilioni 53.1. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 14.9 zilikuwa ni deni la ndani na shilingi trilioni 38.2 zilikuwa ni deni la nje.
  10. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti hiyo, deni la Serikali limeongezeka kwa shilingi trilioni 2.2sawa na asilimia 4.3ikilinganishwa na deni la Shilingi trilioni 50.9lililoripotiwa tarehe 30 Juni, 2018.
  11. Mheshimiwa Spika, sababu zilizotolewa na CAG kuhusu ongezeko hili la deni la Serikali, ni mikopo kwa ajili ya kulipa mitaji na riba ya dhamana za Serikali za muda mfupi pamoja na mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
  12. Mheshimiwa Spika, jedwali Na. 1 hapo chini  linaonyesha mwenendo wa ukuaji wa deni kwa miaka minne iliyopita:-

Jedwali Na. 1. Mwenendo wa Ukuaji wa Deni la Serikali kwa miaka minne iliyopita

  2015/16 2016/17 2017/18 2018/2019
  Shilingi bilioni  
Jumla ya Deni 41,039 46,081 50,927 53,105
Deni la Nje 29,846 32,746 36,194 38,241
Deni la Ndani 11,193 13,335 14,732.45 14,863

Chanzo: CAG 2017/18 ; 2018/19

 

  1. Mheshimiwa Spika, ukiangalia mwenendo huo wa ukuaji wa deni utaona kwamba Serikali hii ya awamu ya tano inayojigamba kwamba haikopi nje, na kwamba inatumia fedha zake za ndani kuendesha miradi yake ya maendeleo,  ilikuta deni la taifa likiwa  shilingi trilioni 41.039 ilipoingia madarakani; ikaongeza deni hilo  kwa shilingi trilioni 5 hadi kufikia shilingi trilioni 46.081 kwa mwaka wake wa kwanza tu madarakani. Aidha, katika mwaka wake wa pili madarakani, Serikali hii imeliongeza deni kwa shilingi kwa takribani shilingi trilioni 5 nyingine hadi kufikia shilingi trilioni 50.927.
  2. Mheshimiwa Spika, kana kwamba kuwa na madeni mengi ni sifa; Serikali hii, licha ya kuonywa na kupewa maangalizo mengi juu ya athari za kukopa kwingi kuliko uwezo wa kulipa; bado imeendelea kuongeza deni kwa takriban shilingi bilioni 2 zaidi na sasa limefikia shilingi trilioni 53 .105.
  3. Mheshimiwa Spika,deni la shilingi trilioni 53.105 ni sawa na asilimia 38.9 ya Pato la Taifa ambalo kwa sasa ni Dola za Kimarekani bilioni 59[1] ambazo ni sawa na shilingi trilioni 136.504 kwa kiwango cha ubadilishaji fedha cha dola moja kwa shilingi 2,313.63[2]cha tarehe 14 Mei, 2020.Kiwango hiki cha deni ni kikubwa mno na kina mwelekeo wa kuiweka nchi rehani kwa kuwa kinakaribia kufikia nusu ya pato letu.
  4. Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameshaeleza kuwa sababu kubwa ya deni la taifa kuongezeka kwa kasi ni kuongezeka kwa mikopo ya ndani na nje – ambapo mikopo peke yake inachangia ukuaji wa deni kwa asilimia 77; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarejea tena ushauri wake ambao imekuwa ikiutoa miaka yote kuwa; mikopo yote ya Serikali iwe inaidhinishwa na Bunge kabla ya kukopa.
  5. URATIBU WA MAKUSANYO YA MAPATO
  6. Mheshimiwa Spika, kutokana na mwenenendo wa Serikali hii ya awamu ya tano kufanya makisio ya makusanyo makubwa ya mapato na kushindwa kukusanya mapato hayo kila mwaka wa fedha; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inathubutu kusema pasi na shaka yoyote kuwa, Wizara ya fedha imeshindwa kuratibu makusanyo ya mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania.
  7. Mheshimiwa Spika, ukifanya tathmini ya miaka mitatu iliyopita utaona kwamba kuna tatizo kubwa kwenye ukusanyaji wa mapato. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 29.54[3] lakini iliweza kukusanya mapato kutoka vyanzo vyote yaliyofikia shilingi trilioni 20.7[4] sawa na asilimia 70.1 ya lengo. Hii ina maana kwamba, asilimia takriban 30 iliyobaki (sawa na shilingi trilioni 8.83) ilikuwa ni nakisi ya bajeti husika na kwa maana hiyo kiasi hicho ilibidi kikopwe ili kukidhi matumizi ya bajeti husika. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali ilipanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 31.71[5] lakini iliweza kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 21.89[6] sawa na asilimia 69 ya lengo. Hii ina maana kwamba, asilimia 31 iliyobaki (sawa na shilingi trilioni 9.82)ilikuwa ni nakisi ya bajeti na hivyo kiasi hichoilibidi kikopwe ili kukidhi matumizi ya bajeti husika.Katika mwaka wa Fedha 2018/19 Serikali ilipanga kukusanya shilingi trilioni 47 hata hivyo iliweza kukusanya shilingi trilioni  28.8 sawa na asilimia 79.1 ya lengo. Hivyo kiasi cha shillingi trilioni  6.65 hakikukusanywa ikiwa ni  sawa na asilimia 20.1 ya lengo.  Hata hivyo makusanyo ya  mwaka wa fedha 2018/19 ni pungufu ya makusanyo ya mwaka uliotangulia 2017/18 kwa kiasi cha shilingi trilioni  1.87.
  8. Mheshimiwa Spika, ili kudhihirisha kuwa ufanyaji wa makisio makubwa kuliko uwezo wa makusanyo ndiyo desturi ya Serikali hii; ukiangalia upande wa makusanyo ya mapato ya kodi utaona kuwa mwenendo ni ule ule. Mathalani kwa mwaka fedha 2018/19, Mamlaka ya Mapato ilikadiria kukusanya mapato ya kodi jumla ya shilingi trilioni 18.297 lakini iliweza kukusanya shilingi trilioni 15.744 tu ikiwa ni pungufu ya shilingi trilioni 2.552 ambazo ni sawa na asilimia 14 ya malengo.
  9. Mheshimiwa Spika,kwa mwaka uliotangulia 2017/18; hali ilikuwa hivyohivyo. Kwa mwaka huo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya jumla ya shilingi trilioni 15.386 ikiwa ni pungufu ya shilingi trilioni 1.929 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 17.315. Upungufu huo ni sawa na asmilimia 11 ya lengo[7].
  1. Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG ya mwaka 2017/18inaonyesha kwamba; idara zote tatu za mapato zilishindwa kufikia malengo kwa mwaka wa fedha 2017/18. Taarifa hiyo inaonesha kwamba Idara ya walipa kodi wakubwa ilikusanya asilimia 41 ya makusanyo yote ambayo ndiyo sehemu kubwa kuliko idara zote; ikifuatiwa na Idara ya Forodha yenye asilimia 40 na idara ya kodi za ndani yenye asilimia 19 ambayo ndiyo ya mwisho kwa mwaka wa fedha 2017/2018, makusanyo haya hayahusishi vocha ya misamaha ya kodi kutoka Hazina.
  2. Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, taarifa ya CAG ya mwaka 2018/19 imeendelea kuonyesha udhaifu huo wa idara kushindwa kufikia malengo yake ya makusanyo. Taarifa hiyo inaonyesha kwamba, kwa mwaka wa fedha 2018/19 Idara ya Forodha na Ushuru wa bidhaa iliongoza kwa kukusanya asilimia 40.2 ya mapato yote; ikifuatiwa na Idara ya Walipakodi wakubwa iliyokusanya asilimia 39.8 na Idara ya Kodi za Ndani iliyokusanya asilimia 20. Makusanyo haya hayahusishi vocha za misamaha ya kodi kutoka Hazina.
  3. Mheshimiwa Spika, Kutokana na mchanganuo huo, ni dhahiri kuwa mchango wa makusanyo kutoka Idara ya Mapato ya Ndani umekuwa nyuma ikilinganishwa na idara nyingine. Aidha, taarifa hiyo inaonesha kuwa  mwelekeo wa makusanyo ya mapato kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa wastani, ulikuwa chini ya makadirio yaliyoidhinishwa, isipokuwa kwa mwaka wa fedha 2015/16 wakati wa Serikali ya awamu ya nne  ndipo makusanyo halisi yalikuwa juu ya makadirio kwa asilimia 0.13.
  4. Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa Taarifa hiyo ya CAG, ni dhahiri kwamba Serikali ya awamu ya tano imeshindwa kufikia malengo ya makusanyo ya mapato kadiri ya mpango iliyojiwekea.Na hakuna fedheha na aibu mbaya kama kujiwekea lengo na kushindwa kulifikia. Kitendo hicho kikitokea, kinadhihirisha uwezo mdogo wa kufikiri, kupanga na kutekeleza. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni mantiki ya Serikali hii kutafuta umaarufu mwepesi (cheap popularity) kwa wananchi kwa kuwaaminisha kuwa ina uwezo mkubwa wa kukusanya mapato wakati tofauti kati ya  tambo hizo na  uhalisia wenyewe ni sawa na tofauti ya umbali kati ya Mbingu na Ardhi.
  5. Mheshimiwa Spika, uwezo mdogo wa TRA kukusanya kodi unafahamika pia kimataifa. Ripoti ya CAG inasema kwamba; Mchanganuo linganifu wa ufanisi wa kodi kwa nchi za Afrika Mashariki unaonesha kwamba, Tanzania ilishika nafasi ya mwisho katika ukusanyaji mapato kwa mwaka wa fedha 2017/18. Kambi Rasmi ya Upinzani inaionya Serikali kuacha kujitapa kuwa ina uwezo mkubwa wa kukusanya mapato wakati tafiti zimeonyesha kuwa ina uwezo mdogo na badala yake ijielekeze kutekeleza mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tuliyoyatoa siku nyingi.
  6. Mheshimiwa Spika, mapendekezo hayo ni pamoja na kuongeza wigo wa vyanzo vya kodi, kudhibiti mianya ya upotevu wa kodi na kuwapa motisha walipa kodi, ili kuongeza ulipaji kodi kwa hiari.
  7. MFUKO MKUU WA HAZINA YA SERIKALI
  8. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ibara ya 135 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, makusanyo yote ya Serikali yanatakiwa kuwekwa katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali. Hata hivyo, licha ya maelekezo hayo ya kikatiba; imebainika kuwa utaratibu huo haufuatwi. Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka wa fedha 2018/19 kati ya shilingi bilioni 659 ambazo ni makusanyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, ni shilingi bilioni 105 tu ndizo zilithibitika kupokelewa na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.
  9. Mheshimiwa Spika, Sambamba na hilo, kati yashilingi trilioni  4  ambazo ni makusanyo yote  ya mikopo ya nje  ni shilingi trilioni  2.17 tu ambazo ziliripotiwa na Mfuko Mkuu wa Hazina. Hii ina maana kwamba, kiasi ambacho hakikuripotiwa hakijulikani kilikwenda wapi na kwa kazi gani jambo ambalo linatoa taswira kwamba kuna uwezekano mkubwa wa uwepo wa ubadhirifu na ufisadi unaofanyika kwa kutopeleka makusanyo yote  katika Mfuko Mkuu wa Hazina kama Katiba ya Nchi inavyoelekeza. Na hii inadhihirishwa na uhalisia kwamba,Jumla ya fedha zilizoripotiwa katika Mfuko mkuu wa Hazina ni shilingi trilioni  24.2 lakini jumla ya fedha zilizotumika ni shilingi trilioni 26.6, na hivyo kuwa na nyongeza ya matumizi ya shilingi trilioni  2.3 ambayo  hayakupita katika  Mfuko Mkuu wa Hazina.
  10. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa maelezo mbele ya Bunge hili ni kwanini haipeleki makusanyo yote kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina na ni kwanini inafanya matumizi ya fedha ambazo hazijapita katika Mfuko Mkuu wa Hazina.

 

  1. MGAWO WA FEDHA ZA MAENDELEO KATIKA KILA WIZARA
  2. Mheshimiwa Spika, Kwa muda mrefu sasa Serikali kupitia Wizara ya Fedha imekuwa ama ikichelewa kupeleka fedha kwenye wizara na idara mbalimbali za Serikali au kutoa fedha pungufu na katika mazingira mengine kutokutoa fedha kabisa kama ambayo zimeidhinishwa na Bunge. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka Serikali kuandaa makisio yake ya mwaka, yanayoshabihiana na makusanyo ya mapato!!Kwa kufanya hivyo, inatarajiwa kwamba shughuli zilizopangwa zitatekelezwa kama zilivyopangwa.
  3. Mheshimiwa Spika, Hali hii inaondoa umuhimu wa Bunge kukaa kwa gharma kubwa kupitisha bajeti ya Serikali ambayo haitekelezwi ipasavyo. Tofauti na awamu za utawala wa CCM zilizotangulia, Serikali hii ya awamu ya tano ambayo imekuwa ikijigamba kwamba imefanikiwa kukusanya mapato kwa kiwango cha hali ya juu kuzidi makisio iliyoyaweka kila mwezi, lakini ukweli ni kuwa, imekuwa na hali mbaya zaidi katika utekelezaji wa bajeti na hasa bajeti ya maendeleo kuliko awamu zilizopita.
  4. Mheshimiwa Spika,nitatoa mifano michache ya sekta zinazoguza maisha ya watu moja kwa moja kuona namna ambavyo Serikali hii haitekelezi bajeti za maendeleo zinazoidhinishwa na Bunge. Ukichukua sekta ya Kilimo mathalani, ambayo inakadiriwa kuajiri takriban asilimia 80 ya watanzania, bajeti ya maendeleo imetekelezwa kwa wastan wa asilimia 17.55 kwa miaka yote minne ya utawala wa Serikali hii. Hii ni kwa mujibu wa Randama za Wizara ya Kilimo ambapo, mwaka 2016/17 bajeti ya maendeleo kwenye Kilimo ilitekelezwa kwa asilimia 2.22; mwaka 2017/18 asilimia 11, mwaka 2018/19 asilimia 42, na mwaka 2019/2020 asilimia 15.
  5. Mheshimiwa Spika, ikiwa Serikali imetekeleza bajeti ya maendeleo kwenye kilimo kwa wastani wa asilimia 17.55; hii ina maana kwamba, asilimia 82.45 ya bajeti ya maendeleo kwenye Sekta ya Kilimo haikutekelezwa! Kwa maneno mengine, asilimia 82.45 ya miradi ya maendeleo ya Kilimo haikutekelezwa! Hapa utajua ni kiasi gani cha ajira kwa wananchi wanaotegemea kilimo zilipotea. Aidha, unaweza pia kufanya hesabu ni kiasi gani cha hasara kilichopatikana kutokana na kutotekeleza miradi hiyo kwa kuzingatia mnyororo wa thamani ya mazao ya Kilimo (Value chain in Agro Economy)
  6. Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Sekta ya Afya – ambayo ndiyo sekta inayoshikilia sekta nyingine kwa maana kutoa hakikisho la nguvu kazi yenye afya (healthy labourforce); hali ni mbaya zaidi. Kwa mfano, Bajeti nzima ya Afya ilipungua kutoka shiingi trilioni 1.07 mwaka 2017/18 mpaka kufikia shilingi billion 866.233 mwaka 2018/19 ikiwa ni anguko la shilingi bilioni 211.468 sawa na asilimia 19.622.
  7. Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali kuporomoka kwa bajeti ya afya; bado utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwenye sekta ya afya umekuwa kizungumkuti! Kwa mujibu wa Taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Sekta ya Afya ni kwamba kwa mwaka wa fedha 2019/2020 fedha za miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya zilizowa zimetolewa hadi kufikia Machi, 2019 zilikuwa ni asilimia 16 tu! Hii ni sawa na kusema kwamba bajeti ya maendeleo katika sekta ya afya haikutekelezwa kwa asilimia 84 kwa mwaka husika.
  8. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2019/20 wizara ya Afya ilitengewa jumla ya shilingi 544,137,902,597. Hadi kufikia mwezi Machi, 2020 kiasi cha fedha kilichokuwa kimetolewa ni shilingi 83,066,202,217.19 tu sawa na asilimia 3% na kati ya fedha hizo fedha za ndani ni asilimia 9.2 na za nje ni asilimia 21.
  9. Mheshimiwa Spika, Tumwombe Mungu apitishe Corona mbali, kwa kuwa kwa utekelezaji wa bajeti ya afya namna hiyo, ni dhahiri kuwa tutakufa wote! Kimsingi Serikali haiko makini kabisha na maisha ya watu, inahangaika na vitu bila kujali kwamba bila ustawi wa watu, vitu hivyo havina tija yoyote! Na uthibitisho kuwa Serikali hii inashughulika na vitu zaidi kuliko ustawi wa watu ni namna inavyotekeleza bajeti za miradi ya vitu kwa ukamilifu.
  10. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Wizara ya Maji,kwa mwaka wa fedha 2018/19 Wizara ya Maji ilitengewa shilingi bilioni 673.214 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo; lakini hadi kufikia mwezi februari, 2019, ni shilingi bilioni 100.068 sawa na asilimia 14.5 tu ndizo zilizokuwa zimetolewa na hazina.Hii ina maana kwamba asilimia takriba asilimia 85 ya bajeti ya miradi ya maji hakikutekelezwa. Na pia takwimu zinaonesha kuwa fedha za maendeleo zinazotolewa katika wizara hii zimekuwa na mserereko wa kupungua kila mwaka. Huu ni ushahidi tosha kwamba, maji sio kipaumbele kwa Serikali yah ii ya CCM.
  11. Mheshimiwa Spika,kwa mwaka wa fedha 2019/2020, hali imekuwa hivyohivyo. Fedha za maendeleo zilizoidhinishwa kwa mwaka huo ni shilingi bilioni 610.5. Fedha iliyokuwa imetolewa hadi mwezi februari 2020 ni shilingi bilioni 312.684 sawa na asilimia 51 ya fedha iliyoidhinishwa na Bunge. Hii ina maana kuwa takriban asilimia 50 ya miradi ya maendeleo katika sekta ya maji haikutekelezwa.
  12. Mheshimiwa Spika,si nia yangu kutaja kila wizara ila wizara nyingi hazijapewa mgawo wake wa fedha za maendeleo kama zilivyoidhinishiwa na Bunge. Kwa kifupi, ukitafuta wastani utakuta kwamba bajeti ya maendeleo imetekelezwa chini ya asilimia 50 jambo ambalo ni kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwa vyovyote vile utekelezaji huu duni unatokana na mipango duni inayoandaliwa na wizara ya fedha kuanzia kwenye kupanga makisio ya bajeti, ukusanyaji wa mapato na ugawanyaji wa fedha kwa kuzingatia vipaumbele vya taifa katika bajeti ya mwaka wa fedha husika.
  13. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha haiwezi kukwepa lawama kwa uzembe na udhaifu huo. Kwa mantiki hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri wa Fedha alieleza Bunge hili kuna nini kinamkwamisha katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi? Je, ni ukosefu wa rasilimaliwatu wenye ujuzi wa masuala ya mipango; Je ni Serikali imekosa fedha kabisa ; au ni changamoto gani inaifanya wizara ya fedha ishindwe kupeleka fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo?

 

  1. HITIMISHO
  2. Mheshimiwa Spika, mdororo wa uchumi wetu kama taifa, hali ya maisha kwa wananchi kuendelea kuwa ngumu; kuongezeka kwa umaskini na madhila mengine yanayotokana na kupungua kwa ukwasi, yanatokana pasi na shaka yoyote, na udhaifu mkubwa wa Wizara ya Fedha wa kupanga mipango inayotekelezeka sambamba na kutunga na kusimamia sera na sheria za fedha.
  3. Mheshimiwa Spika, Wizara ya fedha ndio inayoandaa mpango wa maendeleo wa taifa na ndiyo inakusanya na kugawa fedha kwa ajili ya kuutekeleza mpango huo. Kushindwa kukusanya fedha za kutekeleza mpango iliyouandaa yenyewe ni dalili ya kukosa weledi na ujuzi  katika masuala ya mipango; na badala yake kuongozwa na matamanio yasiyo halisi ya kisiasa jambo linalopelekea kufanya makisio makubwa ya makusanyo kuliko uwezo halisi kukusanya mapato hayo. Hali ya namna hiyo nihatari kwa kuwa inapoteza imani ya wananchi kwa Serikali.
  4. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri wa Fedha na Mipango aache kumdanganya Rais kuwa makusanyo ya mapato ni makubwa kwa kuwa Taarifa ya CAG imeonyesha ukweli wote jinsi ambavyo TRA imeshindwa kukusanya mapato kufikia malengo iliyojiwekea. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa agalizo kali kuhusu deni la taifa; deni kwa sasa linakaribia nusu ya Pato la Taifa. Kwa hiyo, Serikali iwe makini; isije ikakopa kupita kiasi na kukiacha kizazi kijacho kikiwa hakina rasilimali yoyote isipokuwa mzigo wa madeni.
  5. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.

Catherine Nyakao Ruge (Mb)

K.N.Y. WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, KATIKA WIZARA YA

 FEDHA NA MIPANGO

15 Mei, 2020

[1] Pato la Taifa kwa mwaka 2019 kama lilivyorekodiwa  kwenye tovuti  https://tradingeconomics.com/tanzania/gdp iliyosomwa tarehe 14 Mei, 2020.

[2] Hicho ni kiwango cha ubadilishaji fedha (exchange rate) cha dola moja ya marekani kwa shilingi ya Tanzania kwa tarehe 14 Mei, 2020 kama kilivyorekodiwa kwenye tovuti: https://www.xe.com/currencyconverter/convert/?Amount=1&From=USD&To=TZS

[3] Rejea Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Seriakali  kwa Mwaka wa Fedha 2016/17

[4]Ibid.

[5] Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango akiwashilisha Bungeni Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha  2017/18

[6]Ibid.

[7] Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18

Share Button