HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHESHIMIWA PASCAL YOHANA HAONGA (MB) WIZARA YA KILIMO, KUHUSU UTEKELEZAJI MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2020/21

(Inatolewa chini ya Kanuni 99(9) ya Kanuni za Bunge Toleo la mwaka 2016)

  1. UTANGULIZI

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu na afya kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili kutoa Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Kilimo, kwa mwaka 2019/20 na Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2020/21.

 

  1. Mheshimiwa Spika, nawashukuru wananchi wa Jimbo la Mbozi kwa kuendelea kuniamini na kuniunga mkono mimi na chama changu wakati wote ninapoendelea kuwatumikia licha ya changamoto mbalimbali za kisiasa ninazopitia. Kikubwa waelewe kwamba ili dhahabu ing’ae lazima ipitie kwenye moto. Pia waamini kwamba siyo kila changamoto ninayoipitia lengo lake ni kunidhoofisha bali nyingine zinanijenga na kuniimarisha zaidi.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa heshimwa kubwa sana nitoe shukrani kwa KUB Mheshimiwa Freeman Mbowe(Mb) na Mwenyekiti wa Chama Taifa, kwa imani yake kubwa kwangu pamoja na Naibu wangu Mheshimiwa Annatropia Theonest kwa kutuamini kuwa wasemaji wakuu wa Wizara hii ya Kilimo. Kwa pamoja tunasema asante sana, na imani inazaa imani hatutakuangusha katika hili.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa napenda nitoe pole kwa watanzania ambao kwa namna moja au nyingine wamekumbwa na majanga ya mlipuko wa gonjwa hatari la Corona. Mwenyezi Mungu azidi kuwapa roho ya ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu sana kwa nchi yetu na dunia kwa ujumla.

 

  1. HALI YA CHAKULA KWA MSIMU UJAO WA KILIMO
  2. Mheshimimwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa hali ya upatikanaji wa chakula kwa misimu miwili ya 2017/18 ilikuwa ni yenye kutia matumiani sana kwani uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2017/18 ulifikia tani 16,981,974 na mahitaji ya chakula kwa msimu 2018/19 yalikuwa ni tani 13,569,285 na hivyo kuwa na ziada ya tani 3,322,689.
  3. Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanywa na Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI ilibaini kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa katika msimu wa 2018/2019 ulikuwa tani 16,293,637. Kati ya tani hizo mazao ya nafaka ni tani 8,896,830 na yasiyo nafaka tani 7,396,807. Uzalishaji huo ulipungua kwa tani 688,337 sawa na asilimia 4.05 ikilinganishwa na uzalishaji wa msimu wa 2017/2018. Uzalishaji wa nafaka umepungua kwa tani 641,027 sawa na asilimia 7.2 ambapo uzalishaji wa mahindi umepungua kwa tani 621,145 na mchele tani 156,030 sawa na asilimia 11 na 7.6 mtawalia.
  1. Mheshimiwa Spika, kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya nafaka kwa kipindi tajwa hapo juu na kwa kuangalia hali halisi ya mvua ilivyokuwa kuanzia mvua za vuli hadi masika ni dhahiri kuwa uzalishaji kwa msimu huu unaweza kuwa chini zaidi kulinganisha na msimu uliopita.
  2. Mheshimiwa Spika,kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaihasa Serikali kupitia wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula- NFRA na pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kununua nafaka kwa bei ambayo itawainua wakulima  katika kuendeleza kilimo ili iweze kuwa na akiba ya kutosheleza mahitaji ya nchi pale bidhaa hizo zitakapoadimika kwenye soko.
  1. UMUHIMU WA SEKTA YA KILIMO-(MAZAO)
  1. Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba chakula chote kinacholisha watanzania kwa asilimia mia moja kwa mwaka mzima kama hali ya hewa inakuwa nzuri inatokana na kazi ya wakulima wadogo wadogo na wa kati. Hivyo basi umuhimu wa sekta ya kilimo kwa watanzania na Tanzania ni mkubwa sana. Mbali ya umuhimu kwa chakula, pia mauzo ya nje kwa asilimia kubwa inategemea mazao ya kilimo, hakuna njia yoyote au kauli yoyote inayoweza kutumika inayoweza kuifanya sekta ya kilimo (mazao) kuwa ndogo au kutokuwa na umuhimu kwa taifa letu. 
  2. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kilimo ndiyo sekta kiongozi au ndio muhimili mkuu katika uchumi wa nchi yetu. Sekta hii inachangia takriban asilimia 25.3 ya Pato la Taifa (GDP), asilimia 30 ya mauzo ya nje; na asilimia 65 malighafi ya viwanda vyetu vya ndani. Aidha, takwimu zinaonesha kuwa  sekta ya kilimo kilitoa ajira kwa takriban wastani wa 85%, 75% na 65.5% kwa mwaka 2001, 2006 na 2016 mtawalia[1], wakati huo viwanda na sekta za utoaji wa huduma kwa kipindi hicho hicho ajira zilikuwa ni  3%, 5%, 6%; na  15%, 20%, 27% kwa mtawalia.  Pia kwa asilimia hizo za waajiriwa katika sekta ya kilimo, kati yao asilimia 53 ya nguvu kazi yote ni wanawake. Aidha takwimu zinaonesha zaidi kuwa asilimia 80 ya watu masikini wanategemea kuedesha maisha yao kupitia kilimo.
  3. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa kilimo katika maisha ya watanzania, Chadema inaamini kwamba mustakabali wa kilimo cha kisasa, endelevu na cha kibiashara upo katika soko la mazao ya bidhaa za kilimo, ambapo wakulima na wanunuzi wataendesha shughuli zao za kibiashara katika mazingira yanayotabirika, na kwamba wakulima wanaweza kupata bei nzuri kwa mazao yao.
  4. Mheshimiwa Spika, Soko hilo tunaamini litasaidia kukuza matumizi ya teknolojia itakayosaidia kuboresha shughuli za kilimo ili kukidhi viwango vya ubora vya kimataifa na hivyo kuhakikisha walaji wanapata bidhaa bora.
  5. Mheshimiwa Spika, Katika kutimiza hilo tutaanzisha mfumo wa kisheria wa kusimamia biashara, kuweka utaratibu wa mikataba kati ya wazalishaji na wanunuzi wa mazao ya bidhaa za kilimo.
  6. Mheshimiwa Spika, takwimu hizi zinaonesha kuwa kama  Serikali itaamua kwa dhati kuwekeza katika sekta ya kilimo ni dhahiri mabadiliko makubwa ya uchumi wa Tanzania sambamba na watanzania tutaondokana na umasikini wa kipato uliokithiri kwa miaka nenda rudi.
  7. Mheshimiwa Spika, kuna mchumi mmoja humu ndani ya Bunge alitoa hoja yake kuwa toka azimio la Malabo kusainiwa Tanzania ni nchi ambayo imeishapitilia katika utekelezaji wake kwa kutenga zaidi ya asilimia 10 kwenda kwenye sekta ya kilimo. Lakini hoja yetu ya msingi ni kutaka kufahamu kama kweli imeishavuka utekelezaji wa azimio hilo inakuwaje ukuaji wa uchumi bado haujafikia viwango vilivyowekwa?
  8. Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi wetu umejikita katika wastani wa asilimia 6 kwa mwaka, ambapo ukuaji wa pato la nchi ni asilimia 7 toka mwaka 2013. Wachumi wabobezi wanasema kuwa ukuaji wa uchumi ungekuwa ni zaidi ya hapo kama Sekta ya kilimo ingekuwa kwa wastani wa asilimia 6 kama kiwango  cha uwekezaji wa asilimia 10 cha azimio la Malabo/CAADP kingezingatiwa, na hivyo  uchumi ungekuwa kwa asilimia 8 – 10 kwa mwaka na nchi ingefikia lengo lake la kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa mwaka 2025.
  9. Mheshimiwa Spika, uwekezaji kwenye kilimo unajikita kwenye asilimia 4.7 ya jumla ya bajeti kuu ya taifa kwa mwaka 2017/18 kwa kulinganisha na asilimia 7.8 kwa mwaka 2010/11 kiwango cha chini pia kwa kulinganisha na makubaliano ya asilimia 10 ya wakuu wa nchi za SADC kule Malabo. Pia Tanzania ilitoa asilimia 0.29%  mwaka  2014  na   0.19%  mwaka  2016 kama sehemu ya Mchango wa Kilimo kwenye GDP katika kuwekeza kwenye (R&D) utafiti na maendeleo ya kilimo kulinganisha na makubaliano ya asilimia 1 kwa kila nchi za NEPAD na UN kwa nchi zinazoendelea.
  1. Mheshimiwa Spika, pamoja na azimio hilo, Tanzania bado imeshindwa kutekeleza. Takwimu zinaonyesha kwamba; kwa miaka miwili 2015 na 2016 ukuaji wa kilimo nchini Tanzania ulikuwa ni 2.3% na 1.7% mtawalia.

 

  1. SEKTA YA MAZAO
  1. Mheshimiwa Spika, Tanzania imebahatika kuwa katika ukanda ambao takriban mazao mengi ambayo yanatumika kwa chakula na biashara yanastawi. Kwa muktadha wa hotuba hii tutapenda kuangalia zaidi mazao machache kati ya yale yanajulikana kama ya biashara.Tumechagua mazao hayo kutokana na umuhimu wa mazao hayo katika maisha ya kila siku ya watanzania na pia katika kuliingizia mapato taifa letu;
  1. Pamba
  1. Mheshimiwa Spika, zao la Pamba ni zao ambalo linalimwa na wakulima wadogo wadogo,  hadi Februari 2020, bodi ilikuwa imesajili wakulima 556,306 sawa na asilimia 111 ya lengo katika wilaya 49 za mikoa 17 ya Tanzania bara, japokuwa asilimia 80 ya Pamba yote inalimwa katika mikoa minne ya Simiyu, Shinyanga, Singida na Mwanza. Katika mwaka 2019/20 mahitaji ya mbegu za pamba yalikuwa tani 20,000. Hadi kufikia Februari, 2020 kiasi cha mbegu kilichosambazwa kwa wakulima ni tani 17,942 sawa na asilimia 89.71.
  2. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Bodi ya Pamba ilipanga kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka tani 222,000 hadi tani 700,000 na tija kutoka 300 hadi 600 kwa ekari. Aidha, uzalishaji wa pamba umeongezeka kutoka tani 222,039 za msimu wa 2017/2018 hadi tani 352,000 katika msimu wa 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 57. Uzalishaji huo ni sawa asilimia 77.5 ya lengo la kuzalisha tani 450,000 katika msimu wa 2018/2019. Lengo kwa mujibu wa takwimu hizo ni tani 700,000 na tija ya kutoka kilo 300 hadi 600 kwa ekari. Je tunakwenda sawa hapa?
  3. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa Pamba unaathiriwa kwa kiwango kikubwa na changamoto zifuatazo:- kucheleweshwa kwa pembejeo; ubora hafifu wa pembejeo (mbegu na madawa); kutokutabirika kwa bei kwenye soko la dunia na bei elekezi kupangwa bila wakulima kushirikishwa; huduma za ugani kuwa duni na hivyo wakulima kutokufuata mahitaji sahihi ya kilimo cha Pamba; matumizi hafifu ya teknolojia katika kilimo cha Pamba (Use of Agricultural mechanization); Kutokuwepo kwa vyama vya ushirika vilivyo imara; Mauzo ya Pamba ghafi kwenda nje inanyima fursa ya ajira kwa watanzania wengi na  hivyo kuongeza kipato chao.
  4. Mheshimiwa Spika, changamoto hizo kwenye zao la Pamba zimekuwepo kwa kipindi kirefu na Serikali imeshindwa kuzitafutia ufumbuzi. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa mustakabali wa kilimo biashara upo katika soko la mazao na bidhaa za kilimo, ambapo wakulima na wananunuzi wataendesha shughuli zao za kibiashara katika mazingira yanayotabirika, na kwamba wakulima wanaweza kupata bei nzuri kwa mazao yao na kwa wakati.
  5. Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitika sana na kutoa pole kwa wakulima wa pamba ambao wamekuwa na utamaduni wa kukopwa fedha zao na wanunuzi wa pamba, na hivyo kupelekea udunifu wa zao lenyewe. Kama wakulima wanalima na wanauza lakini hawapewi fedha za mauzo ya pamba yao ni kuua kabisa zao hilo kwa makusudi.  Mfumo wa ushindani na uliowazi katika ununuzi wa pamba ambapo mkulima atakuwa na chaguo kulingana na bei, hii ndiyo njia pekee ya kuinua kilimo kuwa cha kibiashara na kisasa na hivyo kumnufaisha mkulima kuondokana na umasikini.
  1. Kahawa
  1. Mheshimiwa Spika, Kahawa ni zao linalolimwa hapa nchini katika mikoa ya Songwe, Njombe-(Ludewa), Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Ruvuma- (Mbinga), Kagera, Tanga, Iringa, Morogoro, Kigoma, Manyara, Mwanza, Rukwa na Mara. Inakadiriwa kuwa Jumla ya eneo la hekta 265,000 ndilo linatumika kwa ajili ya kilimo cha Kahawa aina ya ARABICA NA ROBUSTA ambazo ndizo zinalimwa sana hapa Tanzania.
  2. Mheshimiwa Spika, Kahawa inalimwa na takriban familia 450,000 kwa mikoa ambayo imeainishwa hapo awali na familia hizo zinachangia takriban asilimia 90 ya uzalishaji wote wa Kahawa hapa nchini. Asilimia 10 iliyobaki katika uzalishaji inachangiwa na mashamba makubwa yanayomilikiwa na watu au Kampuni binafsi. Kwa ujumla asilimia 6 ya idadi ya watu wote Tanzania (ambayo kwa sasa ni takriban watu milioni 56) wanategemea uchumi wa Kilimo cha Kahawa kuendesha maisha yao.
  1. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa Kahawa Afrika baada ya Ethiopia, Ivory Coast na Uganda ambapo kila mwaka huzalisha wastani wa tani 46,000 hadi 60,000 huku mkoa wa Kagera ukizalisha takribani tani 12,131.
  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania uzalishaji  kwa mwaka 2014/15 jumla zilizalishwa tani 42,768; mwaka  2015/16  tani 60,188; mwaka 2016/17 tani 47,591.5; mwaka 2017/18 tani 41,679.4
  1. Mheshimiwa Spika, Kwa takwimu hizo za uzalishaji wa Kahawa hapa nchini ni dhahiri kuwa kuna tatizo sehemu katika sekta ndogo ya Kahawa, na hivyo ni jukumu letu kama wawakilishi wa wananchi kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
  2. Mheshimiwa Spika, mbali ya changamoto za madawa kwenye zao la kahawa lakini tatizo kubwa zaidi linalowakumba wakulima ni kutokuwepo kwa soko la uhakika la kuweza kununua kahawa kwa bei ambayo italifanya zao hilo kuendelea kulimwa kitaalam zaidi.
  3. Mheshimiwa Spika, ukweli ni kuwa changamoto za soko zilikuwepo hata miaka iliyopita, lakini kwa sasa tatizo limekuwa kubwa zaidi kwa sababu limeibuka suala kuhodhi soko la Kahawa kwa ushirika na vyama vyake vya msingi na hivyo kutokuwepo kwa ushindani katika soko, Wakulima wanakosa fursa ya kuchagua mnunuzi kulingana  bei anayotoa ili kukidhi gharama za uzalishaji.  Kambi Rasmi bado inasisitiza katika uwepo wa mfumo huru wa soko ambapo Mkulima na Mnunuzi watakutana na kupanga bei kulingana na gharama za uzalishaji na kila upande unufaike na biashara hiyo.
  4. Korosho
  5. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa takwimu za Randama ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2018/19  zinaonesha kwamba, mwenendo wa uzalishaji wa zao la korosho kwa miaka mitatu kuanzia msimu wa mwaka 2015/16 hadi msimu wa 2018/19 umekuwa unapanda ambapo mwaka 2015/16 uzalishaji ulikuwa  tani 155,416; 2016/17 tani  265,238 na 2017/18  uzalishaji ulifikia tani 311,899. Aidha, matarajio kwa mwaka 2018/19 yalikuwa ni kuzalisha tani 350,000.
  6. Mheshimiwa Spika, takwimu hizo zinaonesha kwamba, wakulima takribani 318,407 wanaendesha maisha yao na familia zao kutegemea moja kwa moja zao la Korosho kwa kulima kati ya eka moja hadi mbili na kufanya eneo linalolimwa zao hilo kufikia ekari 400,000. Na kwa sasa eneo hilo litakuwa limeongezeka kutokana na mwamko wa wananchi kulima zao hilo.
  7. Mheshimiwa Spika, takwimu za bodi ya korosho zinaonesha kuwa uzalishaji wa korosho ghafi kwa msimu wa 2019/2020 ni tani 213,994 zenye thamani ya Shilingi bilioni 557.402. Lakini ukifanya ulinganisho wa matarajio ya uzalishaji kwa mwaka 2018/19 ni kuwa uzalishaji umepungua kwa tani136,006. Aidha, wakati mahitaji ya wanunuzi wa korosho ghafi yalikuwa tani 681,419.446 na kiasi kilichouzwa ni tani 192,095.845 zenye thamani ya Shilingi 507,934,371,246.00. Korosho iliuzwa kwa kupitia minada ambapo, bei kwenye minada ilikuwa ni kati ya Shilingi 2,073 na Shilingi 2,890 kwa daraja la kwanza na la pili mtawaliwa.
  8. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilipanga kununua tani 275,198 za korosho za msimu wa mwaka 2018/2019. Hadi Februari 2020, tani 222,561.179 za korosho ghafi zimenunuliwa kutoka kwa wakulima sawa na asilimia 81 ya lengo. Hadi Februari 2020, tani 210,445.524 za korosho ghafi za msimu wa 2018/2019 zimeuzwa ambapo tani 148,077.892 ziliuzwa kwa utaratibu wa Malipwani (FOB) na tani 62,367.632 ziliuzwa kwa utaratibu wa malighalani (ex-warehouse) thamani ya korosho zilizouzwa ni Dola za Marekani 233,864,795.62 sawa na shilingi 526,195,790,145/[2]– na Shilingi 3,246,739,000.
  9. Mheshimiwa Spika, kama fedha kiasi hicho zimepatikana kutokana na mauzo ya korosho kwa msimu husika, inakuwaje wakulima bado hawajalipwa fedha zao za korosho kiasi cha shilingi 20,421,479,180.00?
  10. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema, mkulima sio mtu wa kukopwa fedha zake na Serikali, kwani kufanya hivyo ni kupunguza uzalishaji kwa msimu unaofuata kwani jambo hilo linamkatisha tama katika kuongeza uzalishaji. Hili ni kosa ambalo Serikali inalifanya kwa makusudi ili kukidhi haja yake ya kuwafukarisha wakulima wa nchi hii.
  11. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kufahamu, ikiwa hiyo ndiyo bei iliyokuwa ya mnadani, je bei ambayo mkulima alipata ni shilingi ngapi na wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika wamelipwa fedha zao au bado wanaendelea kudai, wakati msimu mpya unatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa?
  12. Mheshimiwa Spika, Korosho kama ilivyo kwa mazao mengine hapa nchi, tatizo kubwa ni soko kuhodhiwa na vyama vya ushirika, wakati huo huo vyama hivyo kushindwa kutoa bei ambazo zinawatoa wakulima kwenye umasikini na pengine kuendelea kununua mazao yao kwa mkopo. Jambo la msingi ni kuwa na wanunuzi wengi ambao watashindana kwa njia zilizo wazi na hivyo mkulima kunufaika katika ushindani huo.
  13. Mheshimiwa Spika, Uchumi wa Viwanda kwa nchi hii utafikiwa tu, pale bei za mazao ya kilimo zitakapokuwa nzuri na hivyo kumfanya mkulima kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia bora na kisasa. Kambi Rasmi Tunaamini kwamba mustakabali wa kilimo cha kisasa, endelevu na cha kibiashara upo katika soko la mazao ya bidhaa za kilimo, ambapo wakulima na wanunuzi wataendesha shughuli zao za kibiashara katika mazingira yanayotabirika, na kwamba wakulima wanaweza kupata bei nzuri kwa mazao yao. Rejea Sera ya Chadema uk.55 sura ya 9.3 Biashara ya Mazao na Bidhaa za Kilimo.

 

 

  1. MIWA
  1. Mheshimiwa Spika, Kilimo cha miwa ni kilimo chenye tija kwa mkulima, kilimo hiki kinaweza kufanywa na mtu yeyote yule aidha awe ameajiriwa au laaa! Jambo la msingi ni kuhakikisha anajitoa kikamilifu katika kuhakikisha anawekeza akili yake katika kulima kilimo hiki.
  2. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2019/2020, viwanda vya sukari nchini vililenga kuzalisha tani 378,000 za Sukari ambapo hadi Februari 2020, tani 234,727.65 za sukari zimezalishwa.
  3. Mheshimiwa Spika, Wazalishaji wakubwa wa sukari nchini ni: Kilombero Sugar Co. Ltd.; TPC Ltd.; Kagera Sugar Ltd. na Mtibwa Sugar Estates Ltd.  Na katika maeneo hayo yote kuna wazalishaji wa nje. Kwa Kampuni ya Sukari ya Kilombero -wakulima wa nje 8,500 wanazalisha 43% ya miwa inayokamuliwa na viwanda vya K1 na K2.
  4. Mheshimiwa Spika, Makadirio ya mahitaji ya Sukari kwa matumizi ya nyumbani na viwandani yataongezeka kutoka tani 580,000 mwaka 2016/17 hadi tani 695,000 – 755,000 mwaka 2020/21.

 Sukari kwa matumizi ya nyumbani; Mahitaji yataongezeka kutoka tani 445,000 mwaka 2016/17 na kufikia tani 535,000 – 580,000 ifikapo mwaka 2020/21. Sukari kwa matumizi ya viwandani: Mahitaji yataongezeka kutoka tani 135,000 hadi tani 160,000 – 175,000 ifikapo mwaka 2020/21[3].

  1. Mheshimiwa Spika, ukiangalia takwimu za uzalishaji wa sukari kwa viwanda vyetu vya ndani na mahitaji ya nchi ni dhahiri kuwa bado tunaupungufu mkubwa ambao unatakiwa kufidiwa kwa kuagiza sukari toka nje. Kwa kutumia takwimu za kitafiti zilizotolewa na Katibu Mtendaji wa Chama cha wazalishaji Sukari Tanzania ni kuwa tuna upungufu wa tani 300,272.35
  2. Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa sababu kadhaa za upungufu wa Sukari ambazo zinatokana na uzalishaji wa miwa na zile zinazotokana na uchakavu wa mitambo ya kusindika miwa katika mchakato mzima wa kuzalisha sukari. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kufahamu suala la wazalishaji wa nje ambao huzalisha miwa na kuviuzia viwanda, wamekuwa wakipunguza uzalishaji kutokana na bei ya kukatisha tamaa ambazo viwanda vinatoa wakati wa kununua miwa yao.
  1. Mahindi
  1. Mheshimiwa Spika, zao la mahindi ni zao linalolimwa katika mikoa yote ya Tanzania bara na hivyo kulifanya kuwa zao maarufu sana katika nchi yetu kuliko zao lingine. Sambamba na hilo ni kwamba mahindi ndio chakula kikuu kwa watanzania takriban asilimia 90. Mahindi yanazalishwa kwenye ukanda ulio kwenye urefu wa mita 2,400 kutoka uswa wa bahari, kulingana na aina ya mbegu kwenye ukanda husika. Kwa ujumla ni kuwa tija katika uzalishaji wa mahindi ni ya chini sana kwani wazalishaji wengi wanazalisha kwa mazoea tu.
  2. Mheshimiwa Spika, Ukanda mzuri wa kilimo cha mahindi  unaoangukia kwenye urefu wa mita 500-1500 kutoka usawa wa bahari  kama ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na Ukanda wa Ziwa Viktoria unachangia kwa uzalishaji kwa 26% na 25% . Kanda hizi zinafuatiwa na ukanda wa mashariki 13% na ukanda wa Kaskazini 12%, Ukanda wa Magharibi 10%, Kusini 8% na mwisho ni ukanda wa kati 6%. Wakulima wadogo ndio wazalishaji wakubwa wa mahindi kwa takriban 85% ya uzalishaji wote Katika nchi hii, wakifuatiwa na wakulima wakubwa na wa kati kwa 10% na 5% mtawalia[4]
  3. Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu zao hilo kutoka kuwa zao la chakula na kuwa zao la kibiashara unazidi kuwa mkubwa mno kwa kadri siku zinavyokwenda mbele na kuifanya Serikali kuweka mazingira wezeshi zaidi kwa wakulima ili uzalishaji wake uwe wa kisasa zaidi na usiotegemea kwa kiwango kikubwa mabadiliko ya majira na pia wafanyabiashara ya zao hilo wafahamu umuhimu wa zao hilo kwa watanzania na hivyo bei zao kwa wakulima ziendane na hali halisi ya uzalishaji.
  4. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2018/2019, uzalishaji wa mahindi ulikuwa tani 5,652,005 sawa na asilimia 71 ikilinganishwa na lengo la tani 8,000,000. Lengo halikufikiwa kutokana na upungufu wa mvua za vuli na baadhi ya mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka.
  5. Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2019/20 kuna uwezekano mkubwa uzalishaji ukapungua kutokana na ukweli kuwa mvua za vuli zilikuwa ni nyingi na msimu huo ukaja kuungana na msimu wa masika, jambo ambalo lilisababisha wakulima wengi wanaotumia trekta kushindwa kulima maeneo makubwa.  Mfano, wakulima ambao wanakawaida ya kulima ekari 20 hadi 100 sasa wamelima chini ya ekari 20.
  6. Mheshimiwa Spika, japokuwa Serikali katika mwaka 2019/2020, imesimamia upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima ambapo jumla ya tani 32,638.51 za mbegu bora za mahindi zinapatikana, lakini kama mashamba hayakulimwa ni dhahiri upatikanaji wa pembejeo hawezi kusaidia katika uzalishaji.
  1. MADENI YA WAKALA WA PEMBEJEO
  1. Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali bado inadaiwa na mawakala waliokuwa wanasambaza pembejeo katika maeneo mbalimbali hapa nchi. Lakini kutokana na Serikali kukosa sababu ya kutokufanya malipo hayo, ililazimika kutafuta kisingizio cha uhakiki wa ukweli wa madai hayo.
  2. Mheshimiwa Spika, sasa hivi imeishazidi miaka minne toka mawakala walete madai na serikali ifanye uhakiki wa madeni hayo, lakini hadi sasa Serikali imekaa kimya bila ya kusema chochote khusiana na madeni hayo. Kuna mdau mmoja anaidai Serikali kiasi cha shilingi 258,705,000/- kwa mujibu wa barua yake na nyaraka za madai alizoziwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana ni kuwa Serikali inashindwa kufahamu kuwa inapoingia mkataba na mtu kufanyakazi kwa niaba yake, na kazi inapofanyika na Serikali ikashindwa kulipa au ikachukua muda mrefu kufanya malipo ina mtia umasikini mhusika, kwani yeye anafanyakazi hiyo na msululu wa watu wengine. Hivyo mnyololo wote huo unakuwa umetiwa umasikini na Serikali.
  4. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kiasi gani hasa hadi sasa wakala wa Kusambaza Pembejeo za Kilimo wanadai na ni lini watalipwa fedha zao?
  1. KILIMO KUWA CHA KISASA NA ENDELEVU
  1. Mheshimiwa Spika, mkulima kwa “level” yake ya uzalishaji na miundombinu anayotumia katika kilimo anauwezo wa kukifanya kilimo chake kuwa cha kisasa na endelevu na hivyo tija kuwa kubwa.
  2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa wakulima wa Tanzania kwa nafasi zao wanaouwezo wa kuitumia teknolojia mpya, rahisi na ya kisasa katika kilimo chao cha kila siku. Lakini katika kufikia hapo jambo la muhimu sana ni kupatiwa soko bora za mazao yao, kwa kupatiwa soko bora ni dhahiri wataweza kuzalisha kutokana na teknolojia itakayohitajika ili kukidhi mahitaji ya soko.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka sera na sheria zinazotoa uwepo wa ushindani ulio sawa na huru katika soko la mazao ya kilimo. Jambo hilo litaondoa ukiritimba wa kuhodhi soko kwa baadhi ya mazao na  hivyo mkulima  atakuwa na wigo mpana wa kuchagua mazao yake auze wapi kulingana na gharama zake za uzalishaji.
  1. WAKALA WA TAIFA WA HIFADHI YA CHAKULA
  1. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2019/2020, Wizara kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula umenunua tani 3,841.863 za mahindi sawa na asilimia 3.5 ya lengo.  Wakala ulianza mwaka ukiwa na akiba ya tani 67,335.617 za nafaka katika maghala yake.
  2. Mheshimiwa Spika, takwimu za wakala kununua mahindi  asilimia 3.5 tu ya lengo lake ni jambo ambalo linafikirisha mno na kuona kuwa tatizo ni fedha za kufanya manunuzi au ni mahindi katika msimu husika hayakuwepo au, tatizo lilikuwa ni nini hasa?
  3. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa Wakala anatakiwa kuwa na fedha za kutosha ili kununua mahindi kwa wakulima kwa bei ambayo itawawezesha wakulima kuendelea na kilimo cha mahindi au bei shindani na wanunuzi wengine. Samba na hilo ni kwamba kulingana na hali halisi ya ugonjwa wa Korona ni muhimu sana kama nchi kuwa na akiba ya kutosha ya chakula.
  4. Mheshimiwa Spika, usalama wan chi ni uwezo wake wa kulisha wananchi wake, kama usalama wa uhakika wa chakula ukiwa mashakani ni dhahiri kuwa nchi haiku salama. Kwa muktadha huo, kama Wakala wa hifadhi ya Chakula-NFRA hauna uwezo wa kununua chakula kingi na cha kutosha kutoka kwa wakulima na kuhifadhi chakula hicho, maana yake ni kuwa nchi haipo salama.

 

  1. TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI (Fungu 05)
  1. Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilianzishwa kwa Sheria Na. 04 ya Taifa ya Umwagiliaji ya mwaka 2013 kama Taasisi ya Serikali inayojitemea chini ya Wizara inayohusika na Umwagiliaji. Tume  imepewa  mamlaka  ya  kuratibu, kuendeleza  na  kusimamia  Maendeleo  ya  Sekta  ya Umwagiliaji nchini. Pamoja na mabo mengine ina jukumu la kuishauri Serikali katika utekelezaji na kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Umwagiliaji, Mkakati wa Maendeleo ya Umwagiliaji, Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji na Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji;
  2. Mheshimiwa Spika, toka mwaka 2006,azma ya serikali ilikuwa ni kwamba ifikapo mwaka 2020 eneo ambalo litakuwa linatumika kwa kilimo cha umwagiliaji litakuwa ni hekta 1,000,000. Kwa sasa hivi takwimu zinaonesha kuwa eneo linalotumiwa kwa umwagiliaji ni 5% (475,052ha) tu kati ya eneo lote la hekta milioni 29.4 zilizo na uwezo wa kutumiwa katika kilimo cha umwagiliaji.
  3. Mheshimiwa Spika, azma hiyo iliyowekwa mwaka 2006, imepotezewa na sasa ukisoma Randama ya Umwagiliaji inaonesha kuwa; “Lengo la Serikali ni kujenga miundombinu yenye jumla ya hekta 1,000,000 katika skimu za wakulima wadogo, wa kati na wakubwa ifikapo mwaka 2025”. Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza tutaendelea kuhamisha magoli hadi lini? Mipango na malengo tunaweka sisi wenyewe yakishindwa kutekelezeka tunahamishia mbele. Hii ni kujichelewesha sisi wenyewe katika safari ya kujikwamua katika umasikini wa kipato kwa nchi na wananchi wetu.
  4. Mheshimiwa Spika,  Sababu kubwa ya uchache huu wa eneo linalotumiwa kwa kilimo cha umwagiliaji  ni kuwa kilimo kinapewa kipaumbele cha nyuma katika mipango ya nchi, japokuwa Tanzania ili saini na kuridhia Mkataba wa Maputo wa mwaka 2003.  Sababu nyingine inaweza kuwa ni utashi wa kisiasa zaidi kwani bahati mbaya wale wenye mamlaka kilimo na wakulima wao wanaona ni sekta na watu wasiohitajika zaidi katika kukuza uchumi wan chi. Mhe. Spika, “Investing in irrigation could help Tanzania feed its growing population, and boost economic growth by increasing agricultural exports.”
  5. Mheshimiwa Spika, Tume ya taifa ya umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2018/19 ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 25.82 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 6 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 19.82 ni fedha za nje.
  6. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Februari 2019 shilingi bilioni 5.27 zilikuwa zimetolewa sawa na asilimia 20.4 ya fedha zote za maendeleo zilizokuwa zimeidhinishwa. Licha ya utekelezaji mdogo wa bajeti katika eneo hili la umwagiliaji, bado Serikali imeendelea kuwa tegemezi kwa wahisani wa maendeleo kutoka nje.
  7. Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2019/2020, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 37,485,090,830 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi 4,983,628,217 ni fedha za matumizi ya kawaida na Shilingi 32,501,462,613 ni fedha za maendeleo.
  8. Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Februari 2020, Shilingi 4,760,000,000.00 sawa na asilimia 14.6 ya fedha za maendeleo zilizokuwa zimeidhinishwa zilitolewa na hazina.
  9. Mheshimiwa Spika, kwa miaka miwili mfululizo unaweza kuona jinsi utolewaji wa fedha za maendeleo ulivyo na shida. Hii ni ushahidi tosha kuwa kilimo bado sio kipaumbele kwa Serikali ya CCM.  Suluhisho la jambo hilo ni kukiweka pembeni chama hiki ambacho sasa kinachukuliwa kilimo kuwa ni hisani isiyohitaji teknolojia na uwekezaji.
  10. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2020/2021, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetengewa Shilingi 17,726,845,000 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi 12,801,180,000 sawa na asilimia 72.2 ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Ukiangalia fedha za maendeleo zimepungua kwa shilingi 19,700,282,613.00 sawa na puguzo la asilimia 60.61
  11. Mheshimiwa Spika, kutokana na fedha kidogo zilizotolewa kwa Tume, miradi mingi ya umwagiliaji imeshindwa kutekelezwa na mingine kuchukua muda mrefu kukamilika hivyo kuondoa maana halisi ya kupunguza utegemezi wa mvua katika kilimo. Hivyo basi; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuboresha zaidi mazingira ya utendaji kwa Tume ili eneo hili la umwagiliaji liweze kuokoa zaidi ya dola za kimarekani milioni 800 (dola milioni 225, kwenye ngano, dola milioni 132 kwenye sukari, dola milioni 75 kwenye mchele, bado kwenye mafuta ya kupikia n.k) ambazo ni takriban Shilingi trilioni 1.84 zinazotumika kuagiza chakula kutoka nje ya nchi kila mwaka.
  12. Mheshimiwa Spika, mbali ya uwepo wa changamoto cha kifedha kwa Tume, pia kuna changamoto zifuatazo ambazo kwa kiwango kikubwa zinachangia kutokuwepo kwa uwajibikaji ndani ya Tume yenyewe, na changamoto hizo ni zifuatazo;
  1. Tume haijawahi kuwa na Mkurugenzi Mkuu kama sheria na.4 ya mwaka 2013 inavyotaka, na pia wakurugenzi wanakaimu kwa muda mrefu, hivyo kukosa uhalali wa kufanya maamuzi stahiki.
  2. Tume haijawahi kuwa na Bodi kama sheria inavyotaka.
  • Majukumu ya Tume kwenye ngazi za Halmashauri kuna mwingiliano wa kiutendaji na hii inatokana na sheria kutotoa mwongozo bayana.
  1. Idara ya Umwagiliaji itaundwa na Waziri wa Tamisemi kwa kushirikiana na Waziri wa Kilimo kwa ushauri wa Tume.Wakati huo huo Halmashauri zina kitengo cha Umwagiliaji hivyo. Afisa Umwagiliaji wa wilaya anawajibika kwa Tume huku yupo kwenye idara ya halmashauri.)

 

  1. UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA FUNGU 43 MWAKA 2018/19; 2019/20 NA MPANGO WA MWAKA 2020/21
  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2018/19 wizara illidhinishiwa jumla ya shilingi 98,119,516,000.00 kama fedha za miradi ya maendeleo kwa fungu 43, kati ya fedha hizo shilingi 82,000,000,000.00 zilikuwa ni fedha za ndani na shilingi 16,119,516,000.00 zilikuwa ni fedha za nje. Hadi kufikia mwezi Machi, 2019, shilingi 41,222,448,778.00, sawa na asilimia 42 ya fedha zote za bajeti ya maendeleo kwa fungu 43 zilizokuwa zimeidhinishwa ndizo zilikuwa zimetolewa. Kati ya fedha hizo fedha za ndani zilikuwa shilingi 39,964,621,000.00 na fedha za nje ni shilingi 1,257,827,778.00. Fedha za ndani zilizotolewa zikiwa sawa na asilimia 48.74 ya bajeti ya fedha za ndani na asilimia 7.8 ya fedha za nje.
  2. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/20 Wizara fungu 43 inaomba jumla ya shilingi 208,115,500,575.00  Kati ya fedha hizo shilingi 143,577,033,140 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na shilingi 64,538,467,435.00 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 17,992,293,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya wizara.
  3. Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo zinaoombwa  mwaka 2019/20 ni ongezeko la shilingi 45,457,517,140.00 sawa na asilimia 31.66 kwa kulinganisha na zile zilizoombwa mwaka wa fedha 2018/19
  4. Mheshimiwa Spika, hadi Februari, 2020 Shilingi 21,414,787,233.00 sawa na asilimia 14.92 ya shilingi 143,577,033,140.00, zilizoidhinishwa ndizo zilizo kuwa zimetolewa na kutumika.
  5. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Wizara inaomba kutengewa jumla ya Shilingi 202,504,117,000.00 kwa ajili ya matumizi ya Kawaida na Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi 137,273,144,000.00 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo na zinahusisha Shilingi 82,180,000,000.00 zilizotokana na makusanyo ya ndani ya nchi na Shilingi 55,093,144,000.00 ni fedha za nje zilizotokana na mikopo na misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo.

 

  1. HITIMISHO
  1. Mheshimiwa Spika,

………………………………

Pascal Yohana Haonga (Mb)

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya kilimo

.05.2020

[1] Bajeti ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi-2017/18

[2] Bot exchange rate  1usd  to Tsh 2250/-

[3]  Wasilisho la Katibu Mtendaji -Chama cha Wazalishaji Sukari Tanzania (TSPA), 06 Desemba 2017

[4] 2018 Tanzania Corn, Wheat and Rice Report

Share Button