Juzi siku ya Jumamosi tarehe 22 Julai, 2023 majira ya jioni katika viwanja vya Bulyaga Wilaya ya Temeke, Jijini Dar Es salaam ambako kulikuwa na maandalizi ya mkutano wa hadhara uliofanyka jana Jumapili tarehe 23 Julai, 2023 ambao umeandaliwa na Chadema na kuwashirikisha wadau wengine mbalimbali nchini (Sauti ya Wananchi).

Walijitokeza vijana waliojitambulisha kuwa ni kutoka CCM na walivamia watu waliokuwa wanaendelea kufanya maandalizi na kuwajeruhi kwa kutumia zana mbalimbali, walipokuwa wanajaribu kuharibu vifaa mbalimbali vya matangazo kwa hoja kuwa nao walikuwa na haki ya kuandaa Mkutano wao eneo hilo hilo na walipotakiwa kuonyesha barua ya Polisi hawakuwa nayo kwani Polisi walitoa barua ya kuutambua mkutano wa Chadema.

Waandishi wa habari kutoka kampuni ya Mwananchi walifika eneo la tukio ikiwa ni moja ya majukumu yao, walivamiwa na kundi hilo la vijana na kuanza kupigwa na kujeruhiwa vibaya ikiwa ni pamoja na gari ya Kampuni waliyokuwa nayo kuharibiwa vibaya, simu zao kuporwa na wahalifu hao.

Tukio hilo limetokea dakika chache baada ya kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM kutoa kauli ya kuagiza vijana wa jumuiya hiyo ‘kuwapiga’ aliowaita maadui! akiwa kwenye mkutano wa hadhara Jijini Arusha, mbele ya Katibu Mkuu wa Chama chake Taifa.

TUNALAANI kwa nguvu zote tukio hili la kihalifu na ambalo linahatarisha amani na utulivu wa nchi yetu, tukio hili limefanywa na watu WAOGA na ambao hawana uwezo wala majibu kuhusu Mkataba wa Bandari zote za Tanganyika na DP world ya Dubai. Wanatumia nguvu kuzima hoja badala ya kutumia hoja zenye nguvu.

Tunavitaka vyombo vya dola vichukue hatua mara moja kuwachukulia hatua kali za kisheria waovu hawa ili kuhakikisha kuwa nchi inaendelea kuwa ya amani, utulivu na usalama.

Kuumiza waandishi wa habari wakiwa kwenye majukumu yao kisheria ni jambo ambalo halivumiliki kwa sababu yoyote ile .

Tunaendelea kufuatilia tukio hili kuona Serikali na vyombo vyake vya dola watachukua hatua gani madhubuti kuhusu tukio hili.

Imetolewa leo Jumatatu Julai 24, 2023 na;

John Mrema
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya nje.

Share Button