HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MADINI, MHESHIMIWA JOHN HECHE (MB), AKIWASILISHA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA, KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,

Toleo la Januari, 2016

_____________________

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Madini, Naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
  3. Mheshimiwa Spika, kabla sijawasilisha maoni hayo napenda kutumia fursa hii kuwapa pole wananchi wote walioathirika kwa namna moja au nyingine na janga la Corona lililoikumba nchi yetu. Aidha kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni napenda neno la faraja kwa watanzania wote kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu na kwamba waendelee kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambuki ya Virusi vya Corona kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya na waendelea kumtumaini Mungu ili aliepushe taifa na janga hili.
  4. Mheshimiwa Spika, Napenda pia kutumia fursa hii kumshukuru Kiongozi wa kambi Rasmi ya Upinzani kwa kutambua uwezo wangu na kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara hii. Aidha namshukuru waziri kivuli mwenye dhamana hii, Mheshimiwa John Heche (Mb) kwa kunipa heshima ya kusoma hotuba hii kwa niaba yake
  5. Mheshimiwa Spika, Napenda pia kuwapongeza waheshimiwa Wasemaji wa kambi Rasmi ya Upinzani katika wizara mbalimbali pamoja na wasaidizi wao kwa kuaminiwa na kuteuliwa katika nafasi walizo nazo. Ninawatakia kila la kheri katika majukumu haya ya kuwatumikia watanzania na Taifa hili kwa ujumla.
  6. Mheshimiwa Spika, sitawatendea haki wananchi wa Jimbo la Mikumi kama nisipowashukuru kwa heshima kubwa waliyonipa ya kunichagua kuwa mbunge wao, jambo ambalo limenipa heshima ya kitaifa ya kuwa Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Nishati na Madini, kwao wote nasema asante sana.
  7. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Hati Idhini Na.144 ya tarehe 22 April, 2016 iliyofanyiwa marekebisho tarehe 15 Octoba, 2017 majukumu ya wizara ya Madini ni:
  8. kubuni, kuandaa na kusimamia Sera,
  9. Kuanda Mikakati na Mipango ya kuendeleza sekta ya Madini,
  • kusimamaia migodi na kuhamasisha shughuli za uchimbaji pamoja na utafutaji wa madini kwa kutumia tafiti za kijiofizikia na kijiolojia,
  1. kuratibu na kusimamia uongezaji thamani madini kwenye biashara ya Madini,
  2. kukuza ushiriki wa wazawa kwenye shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini nchini,
  3. kusimamia na kuratibu shughuli na maendeleo ya wachimbaji wadogo,
  • Kusimamia taasisi na mamlaka zilizoko chini ya wizara pamoja na kuratibu na kusimamia maendeleo na utekelezaji majukumu kwa watumishi wa Wizara. Aidha Wizara pia inasimamia taasisi sita ambazo ni Tume ya Madini Tanzania, Chuo cha Madini, kituo cha Jemolojia Tanzania, na Taasisi ya uhamasishaji Uwazi katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (Tanzania Extractive Industries Transparency Initiative- TEITI)
  1. Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni moja ya Wizara muhimu miongoni mwa wizara zinazosimamia rasilimali za Taifa, ambazo kama zingetumika ipasavyo taswira ya Taifa hili ingekuwa inafanana na utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo mwenyezi Mungu amelijalia Taifa hili. Lakini katika hali ambayo inashangaza, ni jambo la kawaida kuona maisha ya wananchi wetu yakiwa duni, huduma za Afya zisizoridhisha, miundombinu mibovu, huko vijijini upatikanaji wa maji ni shida, yote haya unaweza kujiuliza yanawezekanaje katika Taifa ambalo limejaliwa neema ya raslimali ikiwemo Madini.
  2. Mheshimiwa Spika, Jawabu kwa matatizo hayo ni moja tu, nalo ni sera za CCM zisizowanufaisha watanzania. Kwa kutambua hilo sisi CHADEMA kama Chama kinachojiandaa kuchukua Serikali, tumeandaa Sera mbadala, toleo la Julai, 2018 kuhusu usimamizi madhubuti na endelevu wa sekta ya Madini; kwamba Serikali chini ya CHADEMA itahakikisha inafanya mambo yafuatayo:
  3. CHADEMA itahakikisha Sekta ya Madini inasimamiwa kwa maslahi mapana ya Taifa na Wananchi.
  4.  CHADEMA itahakikisha inarekebisha Sheria zote zinazosimamia Madini.
  • CHADEMA itahakikisha tunaanzisha Mfuko wa Taifa wa Maendeleo kwa ajili ya kutunza kiwango cha faida inayotokana na Maadini, Mafuta na Gesi ili zitumike kwa maendeleo ya vizazi vijavyo hata baada ya rasilimari hizi kuisha. Jambo kama hili linafanyika Norway kwenye mfuko wa Gesi na Botwana kwenye madini ya Vito.
  1. Itahakikisha kwamba uwepo wa madini unatumika kama dhamana kwa ajili ya serikali kupata fedha za kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo ambayo ni endelevu.
  2. CHADEMA itahakikisha inatoa mikopo kwa wachimbaji wadogo na wa kati, kwa ajili ya kufanya tafiti, kuendeleza na kuchimba madini.
  3. CHADEMA itahakikisha kunakuwepo na mkakati wa kurudisha Mazingira katika hali yake ya kawaida baada ya shughuli za Uchimbaji.

 

  1. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Wizara katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 iliidhinishiwa jumla ya shilingi 49,466,898,200.00 Kati ya fedha hizo jumla ya shilingi 7,039,810,200.00 fedha za ndani sawa na 14% zilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya maendeleo. Kiasi cha shilingi 42,427,088,000.00 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Aidha kati ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida shilingi 25,953,263,000.00 (OC) zilikuwa kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 16,473,825,000.00 zilitengwa kwa ajili ya Mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara.
  2. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ukusanywaji wa maduhuli ya Serikali, Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ilipangiwa kukusanya shilingi 470,897,011,000.00 kutokana na vyanzo mbalimbali katika jitihada za kuhakikisha sekta ya Madini inaongeza mchango wake katika Pato la Taifa.

 

  1. Fedha za Maendeleo zilizopokelewa
  2. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 Wizara iliomba na kuidhinishiwa jumla ya shilingi 7,039,810,200.00 kwa ajili ya miradi ya Maendeleo; hadi kufikia February, 2020 Wizara haikupokea fedha yoyote kwa ajili ya miradi ya maendeleo kati ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge hili. Kwa maneno mengine Wizara ilipokea fedha (0%). Wizara hii ni miongoni mwa Wizara muhimu kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali, haiingii akilini kwamba inatengewa shilingi Bil 7 lakini haijapewa fedha yoyote.
  3. Mheshimiwa Spika, Yapo maelezo kutoka kwa serikali kwamba, Katika kipindi cha mwezi Julai, 2019 hadi Februari, 2020 licha ya kutopokea fedha za maendeleo, Wizara iliendelea na utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kutumia fedha za Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP). Na kwamba fedha hizo kiasi cha Shilingi 2,839,151,286.14 ziliwekwa katika akaunti ya amana wakati wa kufunga mradi mwezi Desemba, 2018 kwa ajili ya kukamilisha miradi iliyokuwa inaendelea.
  4. Mheshimiwa Spika, Shughuli hizo zimetajwa kuwa ni ni pamoja na ukamilishaji wa ujenzi wa Vituo vya Mfano vya Katente na Itumbi, vituo vya umahiri vya Songea na Chunya.  Lakini pia, ujenzi wa kituo cha pamoja cha Mirerani kwamba shughuli za uwekaji wa mfumo wa ulinzi na kamera za usalama pamoja na miundombinu ya umeme kuzunguka ukuta wa Mirerani zilifanyika kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha Shilingi 3,358,024,278.25.
  5. Mheshimiwa Spika, Ukweli ambao haubishaniwi hapa ni kwamba Serikali imeshindwa kutoa fedha yoyote kwa ajili ya miradi ya maendeleo kati ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge lako tukufu. Kwetu sisi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunaona sasa uwezo wa kwa wizara umefikia kikomo, na ili tuweze kutekeleza majukumu yetu yaliyoainishwa katika Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali kupitia Wizara ya Madini walieleze bunge lako tukufu ni kwa nini hadi Mwezi Februari, 2020 Wizara ilikuwa haijapata fedha kama zilivyoidhinishwa na Bunge hili.
  6. Mheshimiwa Spika, hata hivyo kiasi cha fedha kilichotumika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa gharama za shilingi Shilingi 2,839,151,286.14 na kiasi kingine cha shilingi 3,358,024,278.25. kilitolewa bila kuidhinishwa na Bunge hili. Kwa utaratibu huu, kama Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ikisema Serikali inalizarau bunge tutakuwa tumekosea?
  7. Mheshimiwa Spika, takwimu ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, zinaonesha kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu sasa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeshindwa kupeleka fedha kwenye miradi ya maendeleo ya Wizara hii. Mwaka wa fedha 2017/2018 serikali ilitoa fedha za kugharamia Miradi ya maendeleo kwa Wizara ya Madini kwa 3.83%, Mwaka wa fedha 2018/2019 hali ikawa mbaya zaidi, Serikali sasa ilitoa fedha za kugharamia Miradi ya Maendeleo kwa asilimia 0.5%. ya bajeti yote ya Miradi ya maendeleo iliyopangwa na kupitishwa na Bunge na kwa mwaka wa fedha 2019/2020, serikali haijatoa fedha yoyote (0%).  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka majibu kutoka serikalini sababu hasa za kushindwa kupeleka fedha za maendeleo kwenye wizara hii kwa miaka mitatu mfululizo?
  8. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utangulizi wa randama ya Wizara ya Madini, fungu 100 inaeleza kwamba; Katika kuandaa Mpango na Bajeti wa Mwaka 2020/21 na miaka mingine iliyopita Wizara imekuwa ikizingatia miongozo mbalimbali ya Kitaifa. Na kwa kuwa moja ya Miongozo iliyotajwa kuzingatiwa ni pamoja Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi  ya Mwaka 2015 – 2020;  Hivyo basi ni dhahiri kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kusema kwamba, Sera zisizo na tija na ambazo zimeshindwa kutekelezeka ni pamoja na Ilani yenyewe na hivyo Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo imetekeleza Miradi ya Maendeleo chini ya 4% ya bajeti yote iliyotengwa kwa ajili ya miradi husika.
  9. Mheshimiwa Spika, Mpango wa pili wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, unaelekeza Bajeti ya Taifa kutenga 40% ya bajeti yote kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni kwanini dhana hii isitekelezwe kwenye sekta mbalimbali za Wizara. Haiwezekani kwa bajeti ya taifa kufikia lengo hilo wakati wizara haitengi 40% ya bajeti yake kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Utaratibu wa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya matumizi mengineyo, ni utaratibu ambao haulisaidii taifa hili na unapaswa kubadilishwa.
  10. Mheshimiwa Spika, CHADEMA baada ya kugundua kwamba Serikali inapeleka na wakati mwingine haipeleki kabisa fedha za Miradi ya Maendeleo kama ilivyoidhinishiwa na Bunge lako tukufu, na kwamba kutokupelekwa kwa fedha hizo ni matokeo ya sera mbaya za Serikali ya CCM ambazo zinasababisha Serikali hii kukosa fedha za kupeleka kwenye miradi ya Maendeleo. Ndiyo sababu CHADEMA katika sera Mbadala kama tulivyoainisha katika aya ya 8, tunatarajia kuanzisha Mfuko maalumu wa fedha zinazotokana na uwekezaji wa madini ili zitumike katika miradi mikubwa yenye manufaa kwa nchi na kutoa huduma za kijamii kwa wananchi, Sera hii itaondoa tatizo la Serikali kushindwa kupeleka Fedha za Miradi ya Maendeleo kama ilivyo sasa.

 

  1. Maombi ya fedha kwa ajili ya mwaka 2020/2021.
  2. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 62,781,586,000 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake. Kati ya fedha Shilingi 8, 500, 000,000.00 sawa na asilimia 13.54 ya Bajeti yote ni fedha kwa ajili ya kugharamia Miradi ya Maendeleo; na Shilingi 54,281,587,000 sawa na asilimia 86.46 ya Bajeti yote ni  kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida.  Kati ya fedha za Matumizi ya kawaida, Shilingi 21,045,927,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi na Shilingi 33,235,659,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) kwa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.
  3. Mheshimiwa Spika, kutokana na maombi hayo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kupata ufafanuzi wa mambo yafuatayo:
  4. Kuhusu miradi ya maendeleo: Ikiwa Wizara ilishindwa kupata fedha hata shilingi moja kwa ajili ya Miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2019/2020, wizara imewezaje kuongeza bajeti ya fedha za Miradi ya maendeleo kutoka Shilingi 7,039,810,200.00 kwa mwaka 2019/2020 hadi Shilingi 8,500,000,000.00 kwa mwaka 2020/2021 sawa na ongezeko la 20.74%?  Ikiwa wizara imeomba kiasi hiki tunasisitiza kwamba kiasi hiki cha fedha kitoke kwa sababu uzoefu unaonesha kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo serikali imeshindwa kutoa fedha za maendeleo.
  5. Kuhusu fedha za Matumizi ya kawaida kwa ujumla wake: Bajeti ya Matumizi ya kawaida iliyoombwa kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ilikuwa ni shilingi 42,427,088,000.00 na mwaka huu 2020/2021 fedha inayoombwa kwa ajili ya fedha za matumizi ya kawaida ni Shilingi 54,281,587,000.00. Kiasi hiki kinachoombwa kimeongezeka kwa Shilingi 11,854,499,000.00, hivi Mheshimiwa Spika, kuna matumizi gani yameongezeka kwa wizara kwa bilioni 11.9?
  • Kuhusu fedha za Mishahara ya watumishi: Bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya Mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi zilizoko chini yake ilikuwa shilingi 16,473,825,000.00 na Bajeti inayoombwa kwa mwaka huu wa fedha, 2020/2021 ni Shilingi Shilingi 21,045,927,000  kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara. Maombi haya yanaongezeko la shilingi 4,572,102,000.00.  Katika mazingira ambayo Serikali haijatoa ajira kwa watanzania, watumishi mbalimbali hawajapandishwa mishahara na madaraja, tulitarajia gharama za mishahara itapungua lakini kinyume chake bajeti inapanda kwa takribani bilion 4.6;  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka maelezo ya kiasi hiki cha Bilioni 4.6 zimetengwa kwa ajili ya kulipa mishahara watumishi gani walioongezeka?
  1. Kuhusu fedha kwa ajili ya matumizi Mengineyo (OC); Mwaka wa fedha 2019/2020 fedha zilizoombwa kwa ajili ya matumizi mengineyo ilikuwa ni Shilingi 25,953,263,000.00 na kwa mwaka 2020/2021 Wizara inaomba jumla ya  Shilingi 33,235,659,000.00 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) kwa Wizara na Taasisi zilizo chini yake. Maombi haya yameongezeka kwa Shilingi 7,282,396,000.00 ambazo hazina maelezo ya nini kimeongeza matumizi kwa takribani bilioni 7.3 Kambi Rasmi inataka maelezo ya kina kuhusu ongezeko hili kubwa la fedha.

 

  1. MABADILIKO KATIKA SHERIA ZA RASILIMALI MADINI NA HOFU YA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA MADINI.
  2. MheshimiwaSpika, pamoja na juhudi kubwa ya Serikali kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya Madini, mabadiliko hayo yamezua hofu kubwa kwa wawekezaji na wabia wa sekta hii. Hofu inatokana na maamuzi mengi kufanywa nje ya mfumo wa kisheria. Aidha ili Kwa nchi kunufaika kwa muda mrefu, inatakiwa sera na sheria zinazolenga mafanikio ya muda mrefu ujao bila madadiliko ya mara kwa mara. Mabadiliko ya mara kwa mara yanayotokana na malengo ya muda mfupi yanakwamisha uwekezaji wenye tija.
  3. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inashauri Serikali kuandaa mjadala wa kitaifa utakaotufikisha kuwa na dira ya sekta ya madini(County Mining Vision),ili kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji na kuwaondolea mkanganyiko watendaji wanaosimamia sekta hii.Hii pia itaendana na Dira ya Kuendeleza Madini Afrika (Africa Mining Vision) iliyopitishwa na Viongozi wa Africa 2009.

 

  1. MAKUBALIANO YA TANZANIA NA KAMPUNI ZA UCHIMBAJI MADINI.
  2. Mheshimwa Spika, Pamoja na Serikali kuingia makubaliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation na hatimaye kuundwa kwa kampuni iitwayo Twiga Mineral Corporation; ikumbukwe historia ya jambo hili ilitokana na Serikali kuzuia usafirishwaji wa mchanga wa makinikia nje ya nchi na hivyo kupelekea kuundwa kwa kamati mbili ambazo ni kamati ya Mruma na Osolo.
  3. Mheshimiwa spika, Kamati hizi zilibainisha ukwepaji wa kodi na utoroshwaji wa madini yenye thamani ya bilioni 190 dola za Kimarekani ambazo ni sawa na trioni 426. Madai ya kamati hizi yalithibitishwa pia na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA). Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako Tukufu ni lini kiasi hicho cha fedha kitalipwa kwa Serikali ili fedha hizo zipelekwe kwenye miradi ya maendeleo; na Je, wahusika wote waliohusika wamechukuliwa hatua gani.
  4. Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali kupitia aliyekuwa Waziri Katiba na Sheria Prof Kabudi, ilikuwa ni kwamba kabla ya kuanza majadiliano hayo, Kampuni ya BARRICK italipa fedha za utangulizi alizoziita kishika uchumba, dola za kimarekani milioni mia tatu (300) sawa na shilingi za kitanzania bilioni 600. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuliambia Bunge lako tukufu; ni kwanini Serikali ilianza mazungumzo hayo kabla ya kulipwa kiasi hicho cha fedha. Pili Serikali iliambie Bunge lako tukufu ni lini kiasi hicho cha fedha kitalipwa.
  5. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 9(1) cha sheria ya The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act kimezuia makinikia kusafirishwa nje ya nchi na kuyataka Makampuni yanayo chimba madini kujenga mtambo wa kuchenjua makinikia. Taarifa za sasa zinaonesha kwamba Serikali imeruhusu Makinikia yaliyokuwa yanashikiliwa bandari ya Dar Es Salaam kusafirishwa nje ya nchi kinyume na matakwa ya kifungu cha 9(1). Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ilieleze Bunge hili;
  6. Kwanini Serikali imeruhusu makinikia hayo kusafirishwa nje ya nchi kinyume na matakwa ya kifungu cha 9(1).
  7. Kwanini miaka miwili na zaidi baada ya jambo hili kutokea smelter haijajengwa na wala hakuna taarifa wala dalili za kujengwa kwa mtambo huo kama makubaliano yalivyokuwa.
  • Nini mpango wa serikali kuhusu Wafanyakazi wa Tanzania zaidi ya 2000 waliopoteza ajira kutokana na mgodi wa Bulyankuru uliokuwa unazalisha makinikia kufungwa.
  1. Mheshimiwa Spika, wakati wa majadiliano baina ya Serikali na BARRICK, moja ya makubaliano ilikuwa Tanzania kufaidika kwenye faida za kiuchumi kwa uwiano wa 50 kwa 50. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa ufafanuzi kuwa hizo faida za kiuchumi ni zipi; Pili ni utaratibu gani unaotumika ili kufikia huo mgao wa 50 kwa 50. Tatu, Serikali iwaambie watanzania hadi sasa tumeshapata asilimia ngapi ya hizo faida za kiuchumi.
  2. Mheshimiwa Spika, kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kuliambia Bunge lako tukufu ni lini itaanzisha majadiliano na makampuni yote yanayo fanya shughuli za uchimbaji wa madini ili kuendana na matakwa ya sheria mpya ambazo ni “The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act ya mwaka 2017 (“Sovereignty Act”) na “the Natural Wealth and Resources (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act 2017 (“Contract Review Act”).
  3. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2017, Bunge lako tukufu lilitunga na kupitisha sheria mbili ziitwazo The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act 2017 (“Sovereignty Act”) na “the Natural Wealth and Resources (Review and Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act 2017 (“Contract Review Act”). Mojawapo wa malengo ya sheria zile ni kuhakikisha kuwa Tanzania tunannufaika ipasavyo na rasilimali zetu, na kuzuia migogoro ya kibiashara kati yetu na wawekezaji kutopelekwa nje ya nchi.
  4. Mheshimiwa Spika, tukitoa maoni yetu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tulishauri jambo hili kuangaliwa kwa upana wake bila mafanikio. Pamoja na kutochukuliwa kwa maoni yetu kama kambi, Mchakato wa upitishwaji wa sheria zile uliliaminisha Taifa kuwa kuanzia muda huo tutaweza kufanya maamuzi kuhusu madini yetu bila uoga wowote.
  5. Mheshimiwa Spika, Taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo zinaonesha kwamba, utekelezwaji wa nia ya kutatua migogoro baina ya wawekezaji wa nje na Tanzania kwa kutumia mahakama zetu za ndani chini ya kifungu cha 11 cha sheria ya “the Natural wealth and Resources Permanent Sovereignty) Act” katika mazungumzo kati ya Serikali yetu na Barrick Gold Corporation, unaonekana kukwama.
  6. Mheshimiwa Spika, Taarifa za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutoka vyanzo vyake, zinadai kwamba Mawasiliano kwa nyakati mbali mbali kati ya Barrick Gold na wadau wake yanaonyesha kuwa Tanzania imekubali kuwa migogoro itakayozuka kuhusu uendeshaji wa Twiga Mineral ipelekwe kwenye utaratibu wa utatuzi wa migogoro nje ya nchi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua sababu hasa za Tanzania kukubali kutumia mahakama za nje ya nchi kutatua mgogoro utakaozuka wakati awali, ilikataa mapendekezo yaliyohusiana na kifungu cha 11 cha sheria ya Natural wealth and Resources (Permanent Sovereignty) Act.
  7. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni inasisitiza kwamba ni bora Serikali ianze sasa kukubali ushauri unaotolewa na wadau mbalimbali yakiwemo maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni linapokuja swala linalohusu maslahi mapana ya Taifa hili. Hoja inatokana na ukweli kwamba Tanzania siyo kisiwa na hivyo haiwezi kuwa na utaratibu wa peke yake. Tusione aibu kufanya marekebisho ya Sheria zetu kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

 

  1. UCHIMBAJI WA MADINI YA TANZANITE
  2. Mheshimiwa Spika, Biashara ya madini ya Tanzanite ina dolola na Madini ya Tanzanite yanaendelea kushuka bei na wachimbaji wengi wana kata tamaa. Zipo taarifa kwamba kabla ya janga la Corona virus pandemic madini ya Tanzanite yalisha shuka bei kwa zaidi ya asilimia 50, lakini Sasa madini hayo yameshuka kwa zaidi ya asilimia 70, kitendo hiki kimepelekea hofu iliyotanda kwenye madini ya Tanzanite kuwa kubwa sana.
  3. Mheshimiwa Spika, Uchimbaji wa madini ya Tanzanite unawezekana tu pale ambapo madini haya yatakuwa na thamani kubwa kwani gharama za uchimbaji ni ghali sana kulinganisha na madini mengine ya vito.
  4. Mheshimiwa Spika, Sababu mojawapo ya kushuka kwa thamani ya Madini ya Tanzanite ni kuwa na mashaka ya uwekezaji (uncertainity) na kuondoka kwa wanunuzi wakubwa wa madini hayo (Master dealer) kuweka vituo vyao vya biashara nchini Kenya na wengine wameacha kabisa biashara hii. Ni bahati mbaya kuwa Serikali haitambui kuwa kutotabirika kwa mazingira ya biashara kunaua biashara kuliko hata wingi wa kodi pamoja na ukosefu wa amani kwa wafanya bashara, mwenendo wa Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Maafisa madini kuwanyanyasa na kuwatisha wafanya biashara imeondoa kabisa morali ya biashara hii.
  5. Mheshimiwa Spika, kutokana na mwenendo huo, Kambi rasmi ya upinzani inaitaka Serikali kuwatambua wafanyabiashara wote nchini, wakiwemo wafanya biashara ya madini kama wadau wakubwa wa biashara nchini. Aidha ujengwe utamaduni wa migogoro ya kodi iendeshwe na sheria za kodi tofauti na hali ya sasa ambako TAKUKURU na Ofisi ya DPP kuichukulia migogoro ya kikodi kama makosa ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi, jambo ambalo limefanya wafanyabiashara kuogopa kuja kuwekeza Tanzania kwa sababu jambo dogo la kutatuliwa na baraza la kodi la usuruhishi wa migogoro linaweza kumsababishia mfanya biashara kuwekwa ndani na kukosa dhamana kwa makosa ya uhujumu uchumi.
  6. Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wakiwemo wa madini wanmeamua kuacha kufanya biashara hii na kulazimika kuanzisha biashara ambazo hazina madhira kama yanayowakumba wafanya biashara za madini hapa nchini.
  7. Mheshimiwa Spika, Uchimbaji wa Tanzanite Mererani imegubikwa pamoja na hoja zilizoainishwa hapo juu, umegubikwa na sintofahamu baada ya Wizara ya Madini kusitisha majadiliano kati ya Serikali na Kampuni ya TanzaniteOne na badala yake Leseni ya Kitalu C iliyokuwa inamilikiwa na Sky Associate kwa ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mnamo Machi 2020.
  8. Mheshimiwa Spika, taarifa za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kwamba, yapo madai kutoka Wizara ya Madini kuwa ufutaji wa leseni hiyo ulikuja kufuatia maelekezo ya Kamati Maalum ya bunge iliyoundwa kuchunguza biashara ya Madini ya Tanzanite kubaini kuwa leseni hiyo ilitolewa kinyume cha Sheria. Ikiwa madai haya yanaukweli, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tulitarajia na bado tunategemea kupitia Bunge hili, Wizara italiambia Bunge hili tukufu ni akina nani walihusika na maamuzi hayo na hatua gani zilizochukuliwa dhidi yao.
  9. Mheshimiwa Spika, Hata hivo kumekuwa na kauli kinzani toka Tume ya Madini kuwa, Tume ya Madini ndiyo iliyoifuta Leseni ya Tanzanite mnamo tarehe 23 Desemba, 2019 baada ya kampuni ya TML kuandika barua serikalini Desemba 10 kuomba kuachia eneo hilo na mbia mwenza STAMICO aliridhia ombi hilo Desemba 19, 2019. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni hasara kiasi gani nchi imepata kwa kusitisha uzalishaji wa magodi wa TanzaniteOne na Serikali imechukua hatua gani kuwasaidia wafanyakazi 420 stahiki zao baada ya mgodi kufungwa. Serikali ina mpango gani wa kuanza uzalishaji kwenye mgodi huo baada ya kufungwa kwa taakribani miaka mine iliypita.
  10.  
  11. MAPITIO YA TAASISI ZILIZOCHINI YA WIZARA YA MADINI
    1. Tume ya Madini.
  12. Mheshimiwa Spika, Tume ya Madini imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya madini 2010, kama ilivyofanayiwa marekebisho na Sheria No. 7 ya Mwaka, 2017. Mamlaka ya kuanzisha Tume na majukumu yake yameainishwa katika kifungu cha 21 na kifungu cha 22, ambapo, miongoni mwa majukumu ya Tume hiyo ni kusimamia, kuratibu, kupanga, kudhibiti na kutekeleza masuala na shughuli zote zinazohusu madini na pia kuishauri Serikali kuhusiana na shughuli zote zinazohusu Sekta ya Madini nchini.
  13. Mheshimiwa Spika, Tume ya madini ni chombo chenye mamlaka kamili ya kushitaki au kushitakiwa pale inapobidi. Changamoto kubwa ambayo inaikabili tume ni kutokueleweka kwa sheria ya madini kwa wadau na wafanya biashara, ambao husababisha ugumu kwa Tume kukusanya baadhi ya tozo mbalimbali zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria ya Madini.
  14. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashauri Wizara kuhakikisha tume ya Madini kuwa na mkakati kabambe wa kutoa elimu kwa Umma mara kwa mara. Aidha itumie njia mbalimbali kama vile televisheni, redio za kitaifa na kijamii pamoja na mitandao ya kijamii ili Umma watanzania uelimike kuhusu Sheria ya Madini na kazi na mamlaka ya Tume ya Madini.

 

  • Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi asilia Tanzania (TEITI).
  1. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2015 Tanzania ilipitisha sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2015 (The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act 2015. Pamoja na uharaka uliotumika kupitisha sheria ile, kanuni zake zilitungwa mwezi wa pili 2019, takribani miaka minne baada ya kupitishwa kwa sheria mama. Hii inafuatia kuteuliwa kwa Ndugu Ludovick Utouh kuwa Mwenyekeiti wa Kamati ya TEITI, na kumrithi Mwenyekiti aliyemtangulia Mhe Jaji mstaafu Mark Bomani mnamo Juni 2018.
  2. Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inatambua kwamba sheria haiwezi kutekelezwa bila kanuni zake. Kucheleweshwa kwa kanuni za sheria hii kwa kipindi chote hicho, ni dalili ya udhaifu katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali na mambo mazito ya kitaifa. Ni vyema sasa Sheria inapotungwa ikawekewa muda maalumu (time frame) kwa waziri husika na kutengeza kanuni za sheria husika.
  3. Mheshimiwa Spika, Licha ya sheria ya Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2015 (The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act 2015 na kutambulika kwa nafasi ya kamati tekelezi (TEITI Commitee) ambayo inapaswa kutekeleza malengo ya taasisi husika, Ila ukweli ni kwamba; Kamati hii chini ya Ndugu Ludovick Utouh haina rasilimali na miundombinu inayoweza kuwahakikishia Watanzania usimamizi bora wa rasilimali zake. Kwa sasa taasisi hii haina Mtendaji Mkuu kwa miaka miwili sasa wala ofisi maalum pamoja na vifaa. Aidha, pamoja na bajeti yake kupitishwa na Bunge lako, Kamati hii imeendelea kufanya kazi kwa hali ngumu kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha. Changamoto zote hizo zinapelekea taasisi hii kuwa kama mtoto yatima.
  4. Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo ni kwamba usaili wa nafasi ya mtendaji Mkuu ulifanyaka tangu Mai 2019, lakini hadi sasa kilichokuwa kinahitajika ni uthibitisho kutoka kwa Waziri. Aidha Kucheleweshwa kwa uthibitisho huo na kutokana na ushindani wa soko la ajira, taarifa zinaonesha kuwa aliyepaswa kuthibitishwa kuwa Mtendaji Mkuu ameshapata ajira sehemu nyingine. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako tukufu ni kwanini hadi sasa Waziri ameshindwa kuthibitsha mtendaji mkuu kwa kipindi cha miaka miwili sasa.
  5. Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba, serikali ilijitoa kwenye makubaliano ya kimataifa ya kuendesha Serikali kwa uwazi (Open Government Partnership) katika mpango wa uwazi lakini inapaswa kutekeleza baadhi ya majukumu ambayo tayari kabla ya kusitishwa kwa mpango huo yalikuwepo. Kwa mantiki hiyo, Serikali kupitia Wizara ya madini iharakishe mchakato wa upatikanaji wa taarifa na Uwazi wa Mikataba ya Madini, na rasilimali zingine kwa kuzingatia kwamba, msingi mkuu wa kuanzishwa TEITI ni kwa ajili ya kukuza na kuboresha Uwazi na uwajibikaji katika uvunaji wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia.
  6. SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA – STAMICO
  7. Mheshimiwa Spika, Shirika la Madini la Taifa STAMICO ni moja kati ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini. Hili ni shirikia linalomilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja, ambalo lilianzishwa rasmi mwaka 1972 chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma (1969). Mwaka 2015 Shirika lilifanyiwa marekebisho makubwa ya kimuundo (restructuring) chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma (mabadiliko ya uanzishwaji wa mashirika ya Umma) 2015.
  8. Mheshimiwa Spika, STAMICO inamiliki makampuni kadhaa ya madini yakiwemo STAMIGOLD, Buhemba Gold, Makaa ya Mawe Kiwira kwa lengo la kuyaendesha kifaida. Miongoni mwa changamoto zinazoikabili STAMICO ni uhaba wa rasilimali fedha zinazohitajika kuendesha shirika hilo.
  9. Mheshimiwa Spika, Jambo la kusikitisha ni kwamba STAMICO imeshindwa kununua mtambo wa kusaga kokoto zilizotakiwa kwa ajili ya mradi wa Standard Gauge Railway kwa gharama ya Dola za kimarekani 200,000 na hivyo kupoteza mteja muhimu na mapato ambayo shirika lingepata.  
  10. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepata na taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa nyakati mbalimbali, STAMIGOLD kampuni tanzu ya STAMICO, imekuwa inajiendesha kwa hasara takribani miaka 3 iliyopita kutokana na madeni, uwekezaji mdogo na kampuni kutofanya shughuli za uzalishaji.
  11. Mheshimiwa Spika, Kifungu namba 9 cha marekebisho ya Sheria ya Madini 2010, kupitia Sheria ya marekebisho Anuai sheria No. 7, 2017, Sheria inaelekeza umiliki wa Serikali usiopungua asilimia 16 katika makampuni ya madini, hata hivyo kutokana na mapungufu ya kisheria na kikanuni, sheria na kanuni zake hazitoi mwongozo kuhusu mamlaka ipi ya Serikali itahusika na jukumu la kusimamia umiliki huo. Kutokana na upungufu huu, chadema inakusudia kupitia sheria zinazosimamia madini kwa mujibu wa sera zake ili ziwe na manufaa kwa wawekezaji na uchumi wa nchi yetu.
  12. Mheshimiwa Spika, Kutokana na kwamba Serikali haifanyi vizuri kuhusu STAMICO, pamoja na changamoto zinazozikabili Shirika la Madini la Taifa, na ikizingatiwa mwamba shirika linajiendesha kwa hasara, Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza mambo yafutayo;
  13. kwanza tunapendekeza Serikali ifanye uwekezaji mkubwa kwa STAMICO ikiwa ni pamoja na kuipa ruzuku  na pia kuchukua dhamana ya madeni yanayoikabili ili iweze kuwa na uwezo wa kujiimarisha kifedha ili kumudu gharama za uzalishaji.
  14. STAMICO ifanyiwe mabadiliko makubwa ya kimuundo na kimfumo ili iwe kampuni hodhi (Holding company) inayoweza kumiliki hisa au sehemu ya umiliki katika makampuni mengine ya migodi na pia iweze kukuza mtaji kwa kuingia makubaliano ya kimkakati.
  15. Mheshimiwa Spika, tulipendekeza katika hotuba zetu za miaka iliyopita na sasa tunarejea tena kupendekeza kwamba, STAMICO ifanyiwe mabadiliko na ipewe jukumu la kusimamia na kuratibu umiliki wa asilimia 16 za Serikali katika makampuni ya madini kwa niaba ya Serikali. Aidha STAMICO ijitanue na kufanya utafiti na uwekezaji katika aina tofauti za madini kama vile “graphite”, coal”. Kwa ushauri huo tunapenda kupata majibu ya hatua zilizochukuliwa na Serikali hadi sasa.

 

  1. UKAGUZI WA FEDHA NA TAARIFA KWENYE SEKTA YA UZIDUAJI
  2. Mheshimiwa Spika, Kwa nyakati tofauti, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, amekuwa hapewi taarifa za kifedha na za kimikataba kutoka mashirika na makampuni ya sekta ya madini, na sekta nyingine kama mafuta na gesi asilia.
  3. Mheshimiwa Spika, Changamoto hii imesababisha ofisi yake kushindwa kufanya ukaguzi kwa mujibu wa Sheria. Aidha Ili kuweza kuchochea ongezeko la uwazi na uwajibikaji kwenye sekta ya madini pamoja na sekta nyingine zinazogusa rasiliamali za Taiafa hili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inashauri kwamba sheria zinazohusu rasilimali za nchi hii kama Sekta ya madini, mafuta na gesi asilia zipitiwe upya ili kumpa mamlaka ya moja kwa moja Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali kupata taarifa zitakazosaidia ukaguzi wake kwa maslahi mapana ya nchi.

 

  1. MADAI YA FIDIA KWA WANANCHI WALIOATHIRIWA NA MAJI YA SUMU KUTOKA KATIKA MGODI WA DHAHABU WA ACACIA NORTH MARA.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara ambao kwa sasa ni BARRICK, uliopo nyamongo wilayani Tarime ulitoza faini ya bil 5.6 kwa kushindwa kuthibiti bwawa la maji yenye sumu na hivyo kuhatarisha afya za wakazi wanaozunguka mgodi huo.
  2. Mheshimiwa Spika, Kitendo cha Serikali kutoza faini Kampuni hiyo kunathibitisha malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Tarime wanaozunguka mgodi huo. Malalamiko ya wananchi hawa yamewahi kuchunguzwa na kamati mbalimbali za Bunge hili kwa nyakati tofauti tofauti bila mafanikio.  kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake Mhe, James Lembeli iliwahi kufanya ziara Nyamongo.  Madhumuni ya ziara hiyo ilikuwa ni kukagua utekelezaji wa maelekezo ya kamati hiyo iliyoyatoa mwaka 2010. Pamoja na serikali kuwatoza faini ya shilingi bil 5.6 tulitegemea Serikali ingeweza kuwa;lipa fidia wananchi ambao ndiyo waathirika wakubwa wa kemikali hizo, lakini hadi leo hawajalipwa fidia yoyote.  
  3. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ieleze ni lini itawalipa wananchi hawa ambao ni waathirika wakubwa wa kemikali ikizingatia kwamba Serikali tayari ilishapata shilingi bilioni 5.6 kutokana na Mgodi kutiririsha maji yenye sumu yaliyoleta athari kwa wananchi na mazingira.

 

  1. MUUNDO WA WIZARA YA MADINI
  2. Mheshimiwa Spika, Kuna umuhimu wa kupitia upya muundo wa Wizara ya Madini na kufanya marekebisho katika idara au taasisi ambazo zinaonekana kuwa na majukumu yanayofanana. Mathalani, kuanzishwa kwa Tume ya Madini kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya Madini 2010, inapokonya mamlaka na kazi ambazo idara ya madini chini ya kamishna wa madini alikuwa nazo. Kwa mantiki hiyo, Kuendelea kuwa na idara na taasisi ambazo zinafanya kazi zinazofanana siyo tu kwamba zinatoa taarifa ya utendaji unaofanana ila pia ni kuingia gharama zisizo na tija kitu ambacho Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaona ni matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.

 

  1. HITIMISHO
  2. Mheshimiwa Spika, Napenda kumalizia hotuba yangu kwa kusisitiza mambo yafuatayo;
  3. Kwa kuwa huu ni mwaka wa mwisho wa kipindi cha Miaka Mitano kwa Serikali hii ya awamu ya Tano, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwaambie watanzania hatima ya majadiliano na Kampuni ya ACACIA na fedha ambazo ilipaswa kulipwa kama zimeshalipwa kwa sababu ni jambo ambalo umma wa watanzania ulishirikishwa tangu mwanzo. Na ikiwa bado hazijalipwa ni kwanini fedha hizo hazijalipwa. Ikiwa Makampuni haya yalikwepa kodi kama ambavyo watanzania tuliambiwa ni kwanini hadi sasa bado hayalipa fedha hizo. Na ikiwa Serikali iliudanganya umma, ni lini sasa Serikali itatoa taarifa sahihi kuhusu fedha hizo.
  4. Pili, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuliambia Bunge lako tukufu sababu za kutopeleka fedha yoyote kwenye miradi ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2019/2020 pamoja na kwamba Bunge hili lilipitisha na kuidhinisha jumla ya shilingi 7,039,810,200.00 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
  • Serikali iliambie Bunge hili tukufu sababu ya Wizara hii kuwa na ongezeko la 11,854,499,000.00  kwa ajili ya matumizi ya kawaida.  Ni jambo linalostajabisha kwa sababu, Randama zinaonesha kwamba;
  1. Kuna ongezeko la shilingi 4,572,102,000.00 kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi) shilingi 4,572,102,000.00 zimeongezeka katika bajeti ya mwaka  huu kutoka shilingi 16,473,825,000.00 ambazo Wizara ilipitishiwa kwa ajili ya kulipa Mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi zilizoko chini yake. Ongezeko hilo linaifanya wizara kuomba Shilingi 21,045,927,000.00. kwa ajili ya kulipia mishahara tu; sasa Katika mazingira ambayo Serikali haijatoa ajira kwa watanzania, watumishi mbalimbali hawajapandishwa mishahara na madaraja, tulitarajia gharama za mishahara itapungua lakini kinyume chake bajeti inapanda kwa takribani shilingi bilion 4.6;  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka maelezo ya kiasi hiki cha Bilioni 4.6 zimetengwa kwa ajili ya kulipa mishahara watumishi gani walioongezeka?
  2. Ongezeko la Shilingi 7,282,396,000.00 kwa ajili ya matumizi Mengineyo (OC); Ikiwa Mwaka wa fedha 2019/2020 fedha zilizoombwa kwa ajili ya matumizi mengineyo ilikuwa ni Shilingi 25,953,263,000.00 na kwa mwaka huu wa  2020/2021 Wizara inaomba jumla ya  Shilingi 33,235,659,000.00 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) kwa Wizara na Taasisi zilizo chini yake. Maana yake ni kwamba, maombi haya yameongezeka kwa Shilingi 7,282,396,000.00. Kambi Rasmi hapa inataka kufahamu kilichotokea hadi wizara kuwa na matumizi mengineyo ya nyongeza kwa gharama ya takribani bilioni 7.3.  
  3. Wananchi walioathirika na maji ya sumu kutoka Mgodi wa NorthMara watalipwa kiasi gani cha fedha kama sehemu ya fidia ya Madhara waliyopata kwa kipindi kirefu.
  4. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.

 

                                  …………………….

                                  Joseph Leanard Haule (Mb)

    K.NY MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI

                  KATIKA WIZARA YA MADINI.

                                 20 April, 2020

 

 

 

 

Share Button