HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA, MHESHIMIWA ESTHER NICHOLAS MATIKO (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA  WIZARA HIYO, KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii itakuwa ni hotuba yangu ya mwisho kama Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Bunge hili la 11linalomaliza muda wa uhai wake; napenda kuchukua fursa hii kipekee na kwa dhati ya moyo wangu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwanza; kwa kunijalia uhai na afya njema; na pili kwa kuniwezesha kuvishinda vikwazo na changamoto nyingi za kisiasa  zilizonikabili toka nilipoapishwa kushika madaraka haya ya ubunge mpaka dakika hii ninapohitimisha kipindi cha miaka mitano ya utumishi wangu kama Mbunge ndani na nje ya Bunge hili.
  3. Mheshimiwa Spika, si nia yangu kutaja changamoto na vikwazo nilivyopitia, ila itoshe kusema kwamba mapito hayo yamenijenga na kuniimarisha zaidi katika uga wa siasa za ndani na kimataifa pia.
  4. Mheshimiwa Spika, ninapohitimisha kipindi changu cha miaka mitano ya Ubunge; napenda kutumia pia fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa chama changu Chadema, chini ya uongozi mahiri na shupavu wa Mwenyekiti wa Chama Taifa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (Mb)  kwa kuniamini na kunipa ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini lakini pia kwa kunipa heshima ya kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa. Napenda kutoa mrejesho kwa chama kwamba imani na heshima walivyonipa nimevitendea haki; na majukumu niliyokabidhiwa nimeyatekeleza kikamilifu na kwa uaminifu mkubwa. Ninaondoka katika wadhfa wangu wa ubunge nikiwa nimeacha alama ya utumishi uliotukuka; na ninapenda kukihakikishia chama kuwa niko tayari kupokea na kutekeleza kwa unyenyekevu mkubwa majukumu mengine nitakayopewa na chama kwa mustakabali mwema na maslahi mapana ya chama chetu.
  5. Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia utangulizi wangu kwa kuwashukuru sana wananchi wote wa Jimbo la Tarime Mjini ambao ni wapiga kura wangu kwa upendo na ushirikiano mkubwa walionipa toka naapishwa kuwa Mbunge wao mpaka leo ninampomaliza kipindi changu cha ubunge. Sitasahau sala na majitoleo yao kwangu hasa kwa nyakati zilizokuwa ngumu kwangu kama vile nilipowekwa gerezani – sala ambazo zimenifanya kuwa mtu huru tena! Kwao wote nasema asante sana. Napenda kuwahakikishia kuwa bado niko imara; na wasisite kuniunga mkono tena ikiwa chama changu kitanipa ridhaa tena ya kupeperusha bendera ya kuwawakilisha katika Uchaguzi  Mkuu wa Oktoba, 2020.

 

  1. MAPAMBANO DHIDI YA JANGA LA KIMATAIFA LA

COVID -19

  1. Mheshimiwa Spika, nibahati mbaya sana kwamba ninatoa hotuba hii kipindi ambacho dunia imesimamishwa na adui mkubwa mwenye kuogofya na asiyeonekana – Covid-19. Karibu kila Nchi sasa hivi imesimamisha mambo mengi ya msingina kuelekeza nguvu zake kwenye kupambana na virusi hivi, ili kulinda na kuokoa maisha ya raia wake. Mimi mwenyewe ninatoa hotuba hii nikiwa niko kwenye zuio binafsi la kutochangamana (self isolation) kama sehemu ya hatua iliyoamuliwa na chama ya  kujilinda lakini pia kudhibiti kuenea kwa virusi hivi vya Corona.
  2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inatambua kuwa, mamilioni ya watu duniani wameambukizwa virusi hivi vya Coronana malaki wamepoteza maisha. Tunachukua wasaa huu kuwapa pole wale wote waliathirika, kuwaombea wale wote waliopteza maisha na kuwatakia kheri wale wote wanaopatiwa matibabu ili wapone na kurejea tena katika shughuli zao za kawadia.
  3. Mheshimiwa Spika, Wakati nchi nyingine duniani zikichuka hatua ngumu na madhubuti za kisayansi ambazo zinabadilisha utaratibu wa maisha uliozoeleka ili kupambana na COVID19, Kambi Rasmi  ya Upinzani Bungeni inasikitishwa na ama kutokuwepo kwa hatua stahiki ama hatua finyu na legevu zisizofaa zilizochukuliwa na Serikali yetu katika kupambana  na COVID – 19. Kwa matendo na kauli za Serikali inaonekana shabaha kuu ni kulinda uchumi ambao ni legevu hata bila kuwepo kwa COVID19 na sio uhai au masha ya Watanzania.
  4. Mheshimiwa Spika, tunaikumbusha Serikali kuwa, janga la COVID19 ni suala la kiduania. Ukiacha athari za kiafaya, kuporomoka na kudorora kwa uchumi ni athari ambazo dunia haiwezi kukwepa na hata baada ya vita hii kufanikiwa, kila nchi kwa namna yake itaonja  machungu ya athari za Corona. Ndio maana Jumuiya ya kimataifa ikiongozwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) inahimiza nchi  kusimamisha kila kitu na kupambana na COVID19 kwa sasa ili sote tutoke pamoja kwenye vita hii salama na kuangazia mambo mengine.
  5. Mheshimiwa Spika, kutokana na kukosekana kwa uongozi makini na madhubuti kuongoza mikakati sahihi na makini dhidi ya COVID19 hapa nchini, ni dhahiri kuwa wakati dunia ikitoka kwenye vita hivi Tanzania itakua kisiwa na “A no-go-zone” kwa sababu ndiko COVID19 itakua imetamalaki. Kwa maana hiyo, hakuna biashara ya utalii itakayofanyika, hakuna uwekezaji kutoka nje utafanyika Tanzania kwa sababu tu ya hofu ya maambukizi itakayo kuwepo wakati huo na hivyo sio tu kuusulubu uchumi wa nchi hii bali kuuzika kabisa.
  6. Mheshimiwa Spika, serikali iligoma kufunga mipaka ya nchi mapema kwa nia tu ya kuulinda uchumi wa nchii hii ilhali mataifa mengine hata yale tunayopakana nayo yaliamua kufunga mipaka yao ili kuzuia virusi kuinguia nchini mwao. Hata vivyo, nchi hizo ziliendelea kuchukua hatua ngumu na chungu zaidi kwa kuzuia wananchi wao kutotoka nje kabisa (total lockdown) ili kudhibiti virusi hivi kuendelea kusambaa. Lakini hapa kwetu licha ya kutambua kuwa kuna ongezeko la usambaaji wa virusi hivyo, tumeendelea na biashara kama kawaida na kutotoa uzito juu ya janga hili kama inavyotakiwa. Sasa hivi, mathalani, kwa ukanda wa Afrika Mashariki na hata kwenye Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) tunajulikna kama wasafirishaji na wasambazaji wa COVID19.
  7. Mheshimiwa Spika, kama dalili  ya hatua za kutengwa zinazokuja mbeleni, tayari nchi majirani zimeshaanza kuchukua hatua dhidi ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kuzuia raia wetu kuingia nchini mwao hata kama ni kwa shughuli za kibiashara. Tunaikumbusha serikali, wakati nchi hizi, hasa majirani zetu zitafungua mipaka yao, bila kujali taratibu za kikanda na kidugu, zitaifungia Tanzania mipaka yao kutokana na unyanyapaa kwamba Watanzania ni wagonjwa wa COVID – 19.Ni muhimu serikali ikaaamka sasa na kuchukua hatua sahihi, madhubuti na zinazoonekana huku ikizngatia uwazi na ushirkishwaji wa raia wote nchini. Dunia iko vitani; ikiwa sisi watanzania tutamficha adui, basi tutakuwa ni wasaliti na dunia itatutenga. “If we do not lock down Tanzania (fully or partially) and knock out COVID-19, then COVID-19 will knock us down and the world will lock us out”

 

  1. TASWIRA YA TANZANIA KIMATAIFA
  2. Mheshimiwa Spika, taswira na heshima ya taifa lolote duniani hujengwa na matendo ya ndani na nje ya taifa hilo. Matendo hayo huonekana kupitia serikali za mataifa hayo kwenye maeneo tofauti mathalani, kuheshimu na kulinda haki za binadamu, kudumisha demokrasia na utawala wa sheria, na utungaji shirikishi wa sera madhubuti za kiuchumi zinazotabirika.
  3. Mheshimiwa Spika,kwa miaka mitano ya utawala huu, taswira na heshima ya Tanzania kimataifa imechafuka hasa kutokana na matendo ya hovyo yasio ya kibinadamu kushamiri nchini, huku serikali ikiwa kimya. Watanzania wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa baada ya kuona wenzao wakitekwa, wakiteswa, wakipotezwa, wakiuwawa, na kwa mara ya kwanza kutokea jaribio la mauaji ya kisiasa lililoshindwa huku serikali ikiwa na kigugumizi cha kuchukua hatua juu ya mambo hayo.
  4. Mheshimiwa Spika, Mashirika mbalimbali ya Kimataifa yenye hadhi na kuaminika duniani kama State Department, Freedom House, Human Rights Watch yameandika na kuhabarisha dunia juu ya matendo haya huku mashirika mengine yakienda mbali kuhusisha vyombo vya ulinzi na usalama katika matukio haya.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Kwa matukio haya na kwa ukimya wa serikali ni kwamba Tanzania imekua ikivunja Ibara ya 6(d) ya Mktaba wa Jumuiya ya Afrika Mashikiri, Ibara ya 4(c) ya Mkataba wa Juiya ya Nchi za Kusini  mwa Afrika (SADC) , Ibara ya 4 (m) na (o) ya mkataba wa uanzishwaji wa Umoja wa Afrika pamoja na ibara za 4,5,19 na 20 za Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Jumuiya ya kimataifa haiwezi kukaa kimya pale inapoona wananchi wa mwanachama mmojawapo wanatendewa mambo ya hovyo yasio ya kibinadamu huku serikali yao ikiwa kimya. Hivyo basi, ni katika awamu hii, kwa mara ya kwanza Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) kwa nyakati tofauti wameikemea Tanzania kutokana na uvunjivu mkubwa wa haki za binadamu.
  2. Mheshimiwa Spika, kutanda kwa taarifa za mambo haya duniani na kiguguizi cha serikali kuchukua hatua sahihi zinazoonekana sio tu kumeifanya Tanzania kuonekana sio sehemu salama kwa raia wa ndani bali pia raia wa nje wenye nia ya kuwekeza na kufanya biashara nchini. Kitendo cha Ripoti ya uwekezaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa ya mwaka 2018 kuonyesha kushuka kwa kiwango cha uwekezaji wa nje kwenye  nchi yetu ni ushaihidi tosha wa jambo hili. Aidha, kukosekana kwa uwekezaji wa ndani na nje kunadhibitishwa na kuporomoka kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania kutoka 7% 2015 hadi 6% mwaka 2020; kama inavyoonyeshwa na Ripoti ya Benki ya Dunia mwaka 2020. Kwa hali na mwenendo huu, ni wazi kuwa diplomasia ya uchumi ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeshindwa vibaya mno. Hivyo, tunawasihi Watanzania kutokurudia makosa mwezi Oktoba na kuhakikisha kuwa wanaipa Chadema ridhaa ya kuunda Serikali itakayojenga taswira bora na heshima ya nchi kwenye jumuiya ya kimatifa kupitia Diplomasia ya Uchumi na Usalama.

 

  1. WATANZANIA WAISHIO NJE YA NCHI (DIASPORA)
  2. Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekua ikipiga kelele za kuikumbusha Serikali kuhusu umuhimu wa kuweka mazingira na uratibu mzuri kwa raia wetu wanaoishi nje ya nchi. Lakini kwa bahata mbaya sana, Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni ama imekuwa kiziwi au imeamua kwa makusudi kutojali raia wetu hawa wenye mchango mkubwa sana kwa taifa hili.
  3. Mheshimiwa Spika, Chadema inatambua kwa kina umuhimu wa Diaspora katika maendeleo ya taifa letu kiuchumi. Mpaka sasa Diaspora, kwa takwimu za mwaka 2018, wanachangia 0.8% ya GDP ya Taifa letu. Na kama Diaspora wangekua wanathaminiwa, basi kwa mazingira na uratibu mzuri wangeweza kuchangia zaidi ya hapo kama ilivyo kwa majirani zetu Kenya wanaochangia 3% ya GDP
  4. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwa mapana umuhimu wa Diaspora katika kukuza na kuimarisha fursa za kibiashara kati ya taifa letu na mataifa mengine duniani. Aidha, inatambua fika umuhimu wa Diaspora katika kulipatia taifa rasilimaliwatu katika maeneo mbali mbali yenye tija sambamba na kuongeza ubunifu, ukuaji wa teknolojia ndani ya taifa letu, kuongeza mitaji na ujuzi. Ndio maana, bila kusita, Chadema ambayo ndiyo inaunda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliwaahidi watanzania kupitia Sera yake ya Mambo ya Nje kuwa suala la uraia pacha halitakua la mjadala ikiwa itapata ridhaa ya kuunda Serikali.Hili litaenda sambamba na uandaaji wa kanzi data kwa haraka sana bila kuchelewa; ili kuwa na idadi kamili ya watanzania waishio nje pamoja na shughuli wanazofanya.

 

  1. TANZANIA NA JUMUIYA ZA KIKANDA
  2. Jumuiya ya Afrika Mashariki
  3. Mheshimiwa Spika, Taifa letu ni mwanachama kinara wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jumuiya ya Afrika Mashariki kwetu sisi kama taifa ni ya kipekee kwa sababu inatuleta pamoja kushirikiana na mataifa yote tunayopakana nayo na pia kuzungumza lugha moja.
  4. Mheshimiwa Spika, Licha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoa fursa muhimu za kukuza uchumi, kuimarisha ulinzi na usalama kwetu na kudumisha undugu, bado Tanzania chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi haitoi umuhimu kwa jumuiya hii na bado imejawa na mashaka katika kutekeleza na kusimamia mipango ya jumuiya yenye kulenga kuleta utangamano wa kina baina yetu.
  5. Mheshimiwa Spika,Jumuiya ya Afrika Mashariki iko kwenye hatua muhimu ya utangamano ya soko la pamoja. Katika hatua hii, wananchi wa nchi wanachama wanapaswa kuwa huru kwenye maeneo manne ya mitaji, uhamiaji bila vikwazo, usafirishaji wa bidhaa na huduma pamoja na wafanyakazi. Zaidi, raia wa nchi wanachama wanapaswa kuwa na haki za kuishi na kuanzisha makazi kwenye nchi wanachama.
  6. Mheshiwa Spika, Kwa kutambua hili, nchi za Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi zimeondoa tozo kwenye maombi ya vibali vya kazi kwa raia kutoka nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki isipokua kwa Tanzania; na pia kuruhusu raia kuingia na kutoka kwenye nchi moja hadi nyingine bila viza na kwa kutumia kitambulisho chochote kati ya hati ya kusafiria, na kitambulisho cha taifa lakini Tanzania ikihitaji raia wa mataifa mengine kutumia paspoti ili kuingia nchini. Kwa hali hii ni wazi kuwa Tanzania chini ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi ni kikwazo kwa utangamano wa kina kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
  7. Mheshimiwa Spika, Kasumba ya Tanzania kunyima vibali vya kazi nchini raia wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki sio tu ni kielelezo kingine cha ukwamishaji wa utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki bali pia hofu na woga usio na maana yoyote katika ushindani ndani ya
  8. Mheshimiwa Spika, jambo jingine la kushangaza ni kwamba, wakati Tanzania tumeondoa hitaji la visa kuingia nchini kwa raia wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, bado inaonekana visa ni hitaji muhimu kwa raia wa Burundi kuingia nchini. Kama sivyo, ni kwa nini Burundi haimo kwenye orodha ya nchi zisizohitaji visa kuingia nchini?

 

  1. TANZANIA NA TAASISI ZA KIMATAIFA
  2. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni mwanachama wa taasisi mbali mbali za kimataifa. Kwa kipindi kirefu taifa letu limekua likitekeleza wajibu wake unaotokana na kuridhia malengo na taratibu za taaisis hizi. Hata hivyo, kwa kipindi cha miaka mitano ya utawala huu, Tanzania imejikuta katika migogoro na taasisi kadhaa za kimataifa kutokana na Tanzania yenyewe kutokuheshimu na kutekeleza wajibu wake kama mahitaji ya taasisi hizi zinavyohitaji. Jambo hili kwa kiwango kikubwa limefanya taifa letu kuonekana kituko mbele ya jumuiya ya kimataifa na hivyo kuiporomosha hadhi ya taifa letu.
  3. Mheshimiwa Spika, Kitendo cha Shirika la Afya Duniani (WHO) kulalamika kuwa Tanzania imekua ikificha taarifa za majanga ya kiafya kama ilivyokua kwa Ebola mwaka jana ni ushahidi tosha kuwa uwamu ya tano hakutilia maanani mshikamano na mashirikano ambayo taifa letu limekua likiyapata kutoka kwa mashirika na taasisi za kimataifa.

 

 

  1. WASIMAMIZI NA WAANGALIZI WA KIMATAIFA WA UCHAGUZI MKUU WA 2020
  2. Mheshimiwa Spika, ni utaratibu wa kimataifa kuwa na waangalizi wa kimataifa wa chaguzi katika nchi nyingine kwa lengo la kuhakikisha kuwa chaguzi zinakuwa huru na za haki. Pamoja na uhalisia huo, na licha ya nchi yetu kufanya hivyo mara nyingi, kulikuwa na dalili za wazi za Serikali hii ya CCM kupitia Tume Taifa ya Uchaguzi, za kutowaalika waangalizi hao kuja kutazama mwenendo wa Uchaguzi Mkuu wa 2020.
  3. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitoa angalizo ndani ya Bunge hili mwaka jana kuwa kulikuwa na taarifa kwamba nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa UNDP ambao wamekuwa washirika wakubwa wa Tume ya Uchaguzi; walikuwa  hawajapelekewa mialiko rasmi kama ilivyo utaratibu ili waweze kujipanga kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kushiriki kama waangalizi wa kimataifa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
  4. Mheshimiwa Spika,kitendo cha kuwacheleweshea wasimamizi na waangalizi hao mwaliko wa kuja kusimamia Uchaguzi Mkuu kilisababisha mashaka ikiwa kama uchaguzi Mkuu wa 2020 utaendeshwa kwa uhuru na haki. Hata hivyo, licha ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhoji juu ya suala hilo hakukuwa na majibu ya kuridhisha juu ya uwepo wa waangalizi wa Kimataifa kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inasisitiza na inaitaka Serikali kutoa taarifa ya hali halisi (status) ya waangalizi wa kimataifa ambao tayari wamepewa mwaliko wa kuja kusimamia na kutazama Uchaguzi Mkuu wa 2020. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Jumuiya ya Kimataifa kutonyamaza au kukaa pembeni kusubiri mwaliko kwani kufanya hivyo ni kuruhusu mbinu chafu na mizengwe kwenye uchaguzi huo – jambo ambalo litasababisha uchaguzi huo usiwe huru na wa haki.

 

  1. HITIMISHO
  2. Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya awamu ya tano inaondoka madarakani baada ya kumaliza mhula wake wa miaka mitano ikiwa imeacha mahusiano ya nchi yetu na Jumuiya ya Kimataifa katika hali mbaya kuliko awamu zote za Serikali zilizotangulia. Ni katika awamu hii ambapo nchi yetu imesutwa na Jumuiya ya Kimataifa kutokana na kukithiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini, ukandamizaji wa hali ya juu wa demokrasia, uminyaji wa kutisha wa uhuru wa habari, na utawala usiozingatia misingi ya sheria (impunity) – mambo ambayo yalipelekea nchi yetu kunyimwa misaada ya kibajeti na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa washirika wetu wa Maendeleo.
  3. Mheshimiwa Spika, ukiachilia mbali tatizo la nchi yetu kwa kipindi hiki cha awamu ya tano kugoma kushiriki katika mikutano ya kimkakati ya kimataifa na hivyo kujiweka kando na hali halisi ya dunia inavyokwenda; bao Serikali hii ya CCM imegoma kuungana na juhudi za Kimataifa katika kupambana na janga la Corona ambalo linaendelea kuuwa wananchi wetu mamia kwa maelfu huku Serikali ikificha taarifa za athari za janga hilo.
  4. Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali hii kutoshughulikia janga la Corona kwa uzito stahiki, tayari tumeanza kutengwa na majirani zetu kwa kufunga mipaka yao na hali itakuwa mbaya zaidi ziku za usoni tutakapopigwa marufuku kwenda nchi za nje kwa kunyimwa visa kutokana na nchi hizo kutunyanyapaa kuwa tuna Corona!
  5. Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kuiasa Serikali hii kuwa; hakuna nchi inayoweza kufaulu katika michakato yake ya maendeleo ikiwa itajitenga na mfumo unaoiendesha dunia (The World Order) ambapo nchi zote zilizopo duniani lazima ziufuate – vinginevyo zitaishia kuanguka! Kutoka kwenye huo mfumo mkuu ipo mifumo mingine changamano ya kidunia (Global Intergrated Systems) ambayo hutegemeana kwa kiwango cha juu ili dunia iweze kwenda! Utangamano huo wa mifumo unafanana sana na namna viumbe hai vinavyotegemeana katika Mfumo wa Ikolojia ili viweze kuishi (Symbiosis). Kwa sababu hiyo, Serikali hii kujitenga na Jumuiya ya Kimataifa na kuona kwamba inaweza kufanya mambo yote peke yake; ni kujidanganya na ni kuliongoza Taifa kwenye anguko kuu la kiuchumi, kisiasa na kijamii katika uga wa siasa za Kimataifa.
  6. Mheshimiwa Spika, kutokana naudhaifu mkubwa ulioonyeshwa na Serikali hii katika mahusiano ya Kimatafa; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia Chadema inawaahidi wananchi; ikiwa itapewa ridhaa ya kuunda Serikali hapo Oktoba, 2020; kufufua tena na kuimarisha mahusiano yetu na Jumuiya ya Kimataifa; tukiongozwa na Sera ya Uchumi wa Soko Jamii ambapo Sekta Binafsi itapewa kipaumbele katikakuboresha mahusiano hayo.
  7. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha.

Esther Nicholas Matiko (Mb)

WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NJE, USHIRIKIANO

WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA

13 Mei, 2020.

Share Button