HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA MAMBO YA NDANI, KUHUSU UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020 PAMOJA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA HIYO, KWA MWAKA WA FEDHA 2020/21

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,

 Toleo la Januari, 2016

_____________________

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na nguvu kuweza kusimama mbele ya hadhira hii ya Bunge ili kutoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2019/2020 pamoja na makadirio ya mapato na Matumizi ya Wizara hiyo Mwaka wa fedha 2020/2021.Vilevile namshukuru Mke wangu Neema na watoto wangu Allbless,Brilliant na Terrence kwa kuweza kuulewa wajibu wa siasa za sasa kwamba mara zote ninapokuwa polisi na mahakamani wameweza kutambua kuwa mimi sio mhalifu bali ni baba bora ninaye thubutu kujali haki za watu wengi.Imekuwa faraja kubwa kwao na maumivu yao yamegeuka kuwa thawabu na heshima kubwa.
  3. Mheshimiwa Spika, Sambamba na hilo ni washukuru viongozi wangu wa mikoa ya Kaskazini kwa kuniamini kuwa Mwenyekiti wenu wa Kanda hiyo, naahidi kuwa nitatumia wenyekiti wangu huo wa kanda kuhakikisha CHADEMA inafanya vizuri zaidi katika kanda hiyo.
  4. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa niwapongeze watanzania wote kwa ujumla bila ya kujali itikadi zao za vyama kwa moyo waliouonesha kuchanga fedha kiasi cha shilingi milioni mia tatu kumi na mbili ili kuwalipia viongozi waandamizi wa Chadema. Kwa Moyo na mshikamano huo unanikumbusha watanzania walivyojitolea pia katika kunusuru maisha ya aliyekuwa mnadhimu na Mwanasheria mkuu wa Chadema wakati alipopigwa risasi akiwa hapa hapa Bungeni. Nawashukuru sasa watanzania wapenda haki.
  5. Mheshimiwa Spika, aidha niwapongeze viongozi wote wa Chadema wakiongozwa na Mheshimiwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama chetu Taifa, kwa ustahimilivu wake wa kuhimili mishale yenye sumu kali iliyo na lengo la kukipasua chama chetu.
  1. Mheshimiwa Spika, niwashukuru waheshimiwa wabunge wenzangu kwa kazi zao ndani ya bunge walizokua wakifanya wakati mimi nikitumikia adhabu takribani mwaka mzima nikiwa nje ya bunge.
  2. Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa utangulizi huo, naomba kupitia hoja iliyo mbele ya Bunge letu;

 

  1. MUUNDO WA WIZARA YA MAMBO YA NDANI
  2. Mheshimiwa Spika, wizara ya Mambo ya ndani ndio wizara mama katika kuhakikisha inasimamia haki za msingi za Rai wetu na pia kulinda usalama wao na mali zao. Kufuatia muundo uliopitishwa mwaka 2013,Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inaundwa na Idara, na Vitengo vipatavyo kumi na tano(15), lakini kwa muktadha wa hotuba hii nitajikita katika idara nne(4) tu ambazo ni:-
  3. Idara ya Jeshi la Polisi (Jeshi la Polisi);
  4. Idara ya Huduma za Magereza (Jeshi la Magereza);
  • Idara ya Huduma za Uhamiaji (Idara ya Uhamiaji);
  1. Idara ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (Jeshi la Zimamoto na Uokoaji);
  2. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA);
  3. Mheshimiwa Spika, idara zote hizo zinafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu sana, japokuwa Idara ya Jeshi la Polisi naweza kuiita kuwa ndio Idara mama inayochukua sehemu kubwa ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Madhira yote ambayo wananchi wanakumbana nayo kwa zaidi ya asilimia 80 yanatokana na utendaji wa Jeshi la Polisi, iwe ni kwa kuelewa au kutokuelewa kuwa wanayoyafanya ni kinyume cha sheria au wanatekeleza “maelekezo kutoka juu”, kama ilivyozoeleka pale wanapotekeleza maagizo ambayo si ya kisheria bali ni kwa manufaa ya mtu fulani au chama tawala.
  4. Mheshimiwa Spika, “Uwajibikaji na usimamizi wa jeshi la polisi ni kiini cha utawala wa kidemokrasia, na ni muhimu katika kukuza utawala wa sheria na katika kusaidia kurejesha imani ya wananchi kwa jeshi la polisi; kuendeleza uzingatiaji wa haki za binadamu, uwazi na uadilifu katika jeshi la polisi; hali kadhalika, kutengeneza ushirikiano mzuri kati ya wananchi na polisi.” – Azimio Na. 103a la Tume ya Haki za Binadamu Afrika.
  5. Mheshimiwa Spika, Kama ilivyo kwa nchi zingine wanachama wa Jumuia ya Madola, Tanzania inatambua umuhimu wa kufanya mabadiliko ya mfumo wa sheria na usimamizi wa utendaji wa Jeshi la Polisi. Mathalan, mfumo uliopo wa sheria na sera ni ule uliorithiwa kutoka utawala wa kikoloni. Mfumo, ambao hauzingatii wala kukidhi viwango vya kimataifa vya demokrasia, hususan haki za binadamu. Nchi nyingi, hususan zinazofanya mabadiliko ya siasa za kidemokrasia, zimekuwa zikipitisha mfumo wa kidemokrasia wa usimamizi wa utendaji kazi wa polisi, wenye misingi ya haki na usawa, uwazi, ushiriki na uwajibikaji, na yenye kulinda haki za makundi ya watu au mtu binafsi[1]
  6. Mheshimiwa Spika, ieleweke kuwa uhiari wa umma kufuata agizo la polisi na kutoa ushirikiano, unatokana na uaminifu wake kwa jeshi la polisi kutokana na mfumo wa uwajibikaji wa polisi unaoaminika kwa umma.
  7. Mheshimiwa Spika, jeshi la polisi lina jukumu kubwa zaidi, kuliko vyombo vingine vya serikali, la kusimamia haki ili kuwezesha uhuru wa raia na hivyo uhitaji wa mifumo inayowawajibisha. Hivyo, inapaswa kuweka mamlaka ya jeshi la polisi katika mizania (check and balance) ili kuzuia matumizi mabaya ya mamlaka waliyo nayo, kwa kuanzisha mfumo utakao wawajibisha pale wanapokwenda kinyume.Kwahiyo kambi rasimi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuwepo na Independent Policing Oversight Authority (IPOA) kama ilivyo Nchini Kenya.

13.                  Mheshimiwa Spika, katika utendaji kazi wa Jeshi la polisi kuna sheria ambazo zinafuatwa ambazo ni; Penal Code 1945 Cap.16; Criminal Procedure Act 1985 ;Evidence Act 1967 – Admissibility of evidence in Courts; Prevention Of Terrorism Act 2002; Sheria ya makosa ya uhujumu uchumi sura ya 200 marejeo ya 2002

  1. Mheshimiwa Spika, ukweli ni kuwa sheria hizo zimetumiwa vibaya sana kati ya Jeshi la Polisi chini ya Ofisi ya DCI pamoja na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP). Watanzania wengi sana wamepata madhira sana kutokana na matumizi mabaya ya sheria tajwa hapo juu,wengi wako magerezani na wengine wamefariki dunia bila ya familia zao kujua chanzo cha vifo na wengine wamekuwa ni walemavu.
  2. Mheshimiwa Spika, uwili au utatu ukiingiza na Mahakama kutokana na baadhi ya mahakimu kutokujisimamia imekuwa ni balaa kubwa kwa watanzania, mimi nikiwa mhanga mkuu wa sheria hizo na ofisi mbili za (DPP na DCI –wateule wa Rais). Hii ni kuwa Jeshi la polisi linasemekana kuwa kazi yake ni “kuleta amani na utulivu”. Jambo hili sio kweli jeshi la polisi kazi yake ni kwa hali halisi ilivyo ni kutumia nguvu ili wananchi watulie na wenye dhamana ya kutawala wafanye wanavyotaka.
  3. Mheshimiwa Spika,uadilifu wa Jeshi la Polisi unatokana na uongozi unao heshimu misingi ya utawala bora, sheria na misingi ya demokrasia na haki. Jeshi la Polisi lolote Duniani ambalo halizingati misingi tajwa hapo juu linageuka kuwa kikundi cha majambazi kilichosajiliwa,kwa hiyo usafi wa jeshi la Polisi na uimara wa Jeshi la Polisi ni matendo yao katika haki,kweli na kuzingatia usawa wa Binadamu. Hivyo basi, uimara wake hauwezi kupimwa kwa uwezo wa silaha za kisasa walizonazo, vilevile Polisi mzuri ni yule anayetafuta haki katika matendo yake na sio cheo katika ubaya wake. Kamanda MKuu wa Jeshi la Polisi anapaswa kujivunia ueledi wake katika haki na nidhamu na sio maslahi kama mshahara mzuri,urafiki na mahusiano na viongozi wa juu kama Rais,kiinua mgongo pamoja na salute.
  4. Mheshimiwa Spika,kwa hiyo pamoja na sheria mbaya zilizopo za usimamizi wa Jeshi la Polisi kutoka kwenye mamlaka nyingine za juu sio kweli kwamba Polisi wanaojiamini wanaweza kushindwa kuwajibika katika mamlaka zao bila isipokuwa kukosa mahaba na haki na ukweli kumefanya Jeshi hilo kuwa la uonevu, sio tu kwa wanasiasa wa upinzani bali kwa watu wengi wanaopita katika mikono yao. Jeshi la Polisi kazi yake ni kutoa huduma na sio kudhurumu huduma. Kuna mifano mingi hotuba hii haitoshi kuelezea, hata tukiandika vitabu kumi vya kurasa elfu mbili havitoshi kuelezea hofu waliyonayo Wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi, kazi ya Polisi ni kazi ya heshima kuu(noble work), Polisi wanapaswa kuwa waadilifu kwa sababu wajibu wao umebeba kujitoa mhanga (sacrifices) ,kwa hiyo Polisi wanatakiwa kuyaonea aibu matendo mabaya na kuyachukia kwasababu ya thamani ya wajibu wao kama ambavyo watumishi wa Mungu waadilifu wanavyoogopa kuikaribia dhambi.
  5. Mheshimiwa Spika,tunajisikia vibaya kulisema Jeshi la Polisi lakini hatuna uchaguzi wa kukaa kimya kwani hata wachache ndani ya Jeshi hilo watatushangaa kama tutakaa kimya. Yako matukio mengi ya udhalilishaji, uonevu na ubaguzi, na ili kuthibitisha hilo rejea kauli za viongozi mbalimbali kutoka chama tawala hasa UVCCM dhidi ya uimara wa amani ya Nchi hii na ujenzi wa Demokrasia. Tunaposema kuwa sheria zetu zinatumika vibaya kutokana na uongozi na hivyo jeshi la polisi na ofisi ya Mwendesha Mashtaka kuwa ndio wameshikilia uhai wa watuhumiwa na sio mahakama basi ni shida. Mfano mwingine ni mahabusu Arusha kuna Mashekhe zaidi ya 50 sasa ni takriban miaka saba kwa tuhuma za ugaidi. Inakuwaje mtu anakaa mahabusu kipindi chote hiki bila uwapo wa ushahidi na ofisi tajwa wapo na wanaendelea kulipwa mishahara ya walipa kodi? Mfano mwingine ni watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi wamejaa magerezani, kesi zao wengine hazijawahi kuwatajwa zaidi ya mara mbili lakini wamekaa miaka zaidi ya mitatu.
  6. Mheshimiwa Spika, ni muda mwafaka sasa Sheria za ushahidi zifanyiwe marejeo ili kuwepo na kipindi maalum kwa waendesha kesi kuwa wamekamilisha ushahidi ili wahusika wakamatwe na kesi zao ziendelee na sio kukamata mtuhumiwa wakati ushaidi haupo na mhusika anaozea mahabusu eti ndio ushahidi unatengenezwa. Hii ni kinyume na haki za msingi za binadamu. Aidha mtu asikamatwe na kufikishwa Polisi mpaka hapo upelelezi umekamilika na vilevile makosa mengi yana dhaminika polisi lakini polisi wamekuwa wagumu kutoa dhamana ya kipolisi kwa sababu ya ukatili na roho mbaya.Vilevile tunapendekeza sehemu ya mafunzo ya jeshi la polisi na waendesha mashtaka wa serikali iwe ni pamoja na kwenda kukaa mahabusu kwa muda wa kutosha ili wajue wanako wapeleka wenzao sio hotelini na wajue umuhimu wa Uhuru wa mtu kama ilivyo andikwa na Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
  7. Mheshimiwa Spika, sio kama tunasema mambo haya bila kuwa ni wahanga wa mambo haya, sasa hivi imefikiwa kipindi watuhumiwa kulazimishwa kukiri kosa bila ya kesi kufikishwa mahakamani na hakimu kusikiliza ushahidi wa pande zote, kwa maana mengine watu wananunua uhuru wao. Jambo la kujiuliza ni nani ataweza kukaa magereza kwa miaka miwili au mwaka mzima na akatae kukubaliana na DPP kulipa fedha ili awe huru? Kwa wengi ambao hamjawahi “experience” adha ya jela mtaona ni jambo la utani, lakini ukweli ni kuwa uhuru wa mtu hauna bei na mhusika yuko tayari kwa bei yoyote kupata uhuru wake. Sasa kwa kuelewa hivyo, Ofisi ya DPP kwa kushirikiana na Ofisi ya DCI-Jeshi la Polisi wanafanya mambo ambayo naweza kuyaita ya “kihuni” ili kupata kile walichokusudia toka kwa wahusika. Hii ni mbaya sana kwa nchi ambayo inahitaji mshikamano wa hali ya juu katika kuhakikisha nchi yetu inakuwa moja na kuijenga kwa jasho na damu la kila mtanzania.
  8. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia tena kuwa “nguzo kuu ya amani na utulivu” katika nchi ni uongozi (Leadership) wa juu wa nchi na sheria ziwe mbaya zitaonekana ni nzuri na sheria zikiwa ni nzuri zinaweza kuonekana ni mbaya kulingana na jinsi zitakavyotumika na kusimamiwa.
  9. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria za Msingi za Utumiaji wa silaha za moto na Maofisa wa kutekeleza Sheria ya Umoja wa Mataifa (UN Basic Principles) zinataka ukaguzi na ripoti yakinifu unaohusu silaha za moto zilizotumika na polisi ama utumiaji wa nguvu na kusababisha madhila wakati wa kutimiza wajibu wao. Kanuni za Umoja wa Taifa zinafanya kazi kwa namna ambayo kwanza, serikali na polisi wanapaswa kujiridhisha kuwa viongozi wa ngazi mbali mbali katika jeshi wanawajibishwa kulingana na uelewa wao ama walipaswa kuwa na taarifa, ama walikuwa na taarifa na hatua yoyote haikuchukuliwa juu ya vitendo vya kutumia nguvu au silaha kinyume na sheria utakaofanywa na maafisa wa polisi wa ngazi ya chini. Hata hivyo imekuwa kasumba ya kawaida siku hizi kwa jeshi la polisi kuua majambazi,wezi na watuhumiwa wengine bila kuwafikisha mahakani, hii kasumba mbaya na kwamba inaondoa utawala wa sheria katika nchi. Kazi ya polisi ni kukamata, kupeleleza na kupeleka mahakamani,na nafasi ya magereza inasimama kama chuo cha mafunzo. Ieleweke kwamba wahalifu wanaweza kubadilika kuwa watumishi wa Mungu,kwa hiyo nafasi ya pili kwa maisha ya Mwanadamu ni muhimu sana. Polisi wasihukumu kwa risasi (extra judicial killings).
  10. Mheshimiwa Spika, tuna amini kwamba kuna mazingira ambayo polisi wanapaswa kutumia nguvu kubwa lakini kwa hali ilivyo sasa watu wema wanaweza kuuwawa na asiwepo mtu wa kuthibitisha kuwa hawa ni majambazi au ni watu wema,rejea kesi ya Abdalah Zombe na Mrakibu wa polisi SP  Christopher Bageni ambaye alihukumiwa na mahakama kuu ya Tanzania kunyongwa mpaka kufa. Kwa mazingira kama haya Abdalah Zombe katika taarifa yake ya awali aliwataja wafanya biashara wa madini kutoka Mahenge kama Majambazi jambo ambalo lilibainika kuwa sio kweli. Wafanyabiashara hao ni Savings Chigumbi, Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi wa Manzese Juma Ndugu waliuwaa Januari 14, 2006 kwa kupigwa risasi Mbezi Louis, Dar.
  11. Mheshimiwa Spika, adhabu inapaswa kutolewa kwa afisa wa polisi atakayekataa kutoa ushirikiano wa kutumia vibaya nguvu ama silaha au kutoa taarifa kuhusu vitendo vya aina hiyo vinavyofanywa na maafisa wenzake. Mwisho, haitakuwa halali kwa polisi kujitetea kuwa alitekeleza amri iliyotolewa na kiongozi wa ngazi ya juu ya polisi iliyosababisha kifo ama majeraha, hususan kama alikuwa anaelewa matokeo yake na uhuru wa kukataa agizo hili.
  12. Mheshimiwa Spika, msingi mkuu wa hoja hapo juu ni kuonesha ni jinsi gani jeshi letu la polisi lisivyofuata sheria za misingi ya utumiaji wa Silaha za moto. Tukumbuke kwamba Viongozi wakuu na waadamizi wa Chadema walikuwa mahakamani kwa takriban miaka miwili, lakini chanzo kikuu cha kesi hiyo kilikuwa ni kifo cha Binti Akwilina Akwilin aliyepigwa risasi na askari polisi. Kwa mstuko mkubwa muuaji alikamatwa lakini katika mazingira ya kutatanisha ambayo sasa Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka WAZIRI awaeleze watanzania ni kwanini muuaji huyo hakushtakiwa na badala yake bado yuko huru?
  13. Mheshimiwa Spika, kutokana na mfumo wa kiutendaji au kiuwajibikaji kwa jeshi letu la polisi inawezekana kabisa jeshi hili likaendelea kupewa lawama na kutoaminika mbele ya wananchi kutokana na ukweli kwamba, “internal discipline” kwa askari waandamizi wanawajibika kwa katibu mkuu wa wizara na Rais, ambaye ni raia au amewekwa pale kulinda maslahi ya kisiasa. Askari wa chini wanawajibika kwa IGP na Kamishna General wa Magereza.
  14. Mheshimiwa Spika, siasa kwa kiasi kikubwa ndizo zinaendesha Jeshi la Polisi, na jambo hili ni hatari sana, Rais ndiye mwenye uwezo wa moja kwa moja kutoa amri kwa jeshi la polisi (direct command), pia uwezo wa kuajili na kumwondosha IGP na askari waandamizi wa Jeshi la Polisi. Hivyo uhakika wa nafasi zao za utumishi ni hisani za Rais- Rejea “Emergence power Act 1986”, Waziri mwenye dhamana na Jeshi hilo amepewa uwezo wa kutoa amri kwa jeshi hilo na kupuuza maoni ya kamati yake ya ushauri (Advisory Committee). Hawa wote ni wanasiasa na wanatoa maelekezo kwa jeshi kuhakikisha chama kinachotawala kinaendelea kutawala[2].
  15. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo wa mnyororo wa uwajibikaji kwa Jeshi la Polisi, hakuna nia njema katika kuhakikisha Demokrasia ya kweli inapikana katika mfumo huu wa siasa za vyama vingi hapa nchini. Mfumo uliopo sasa wa jeshi hilo ni ule ulioasisiwa ili kukidhi matakwa ya chama kimoja.
  16. Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo sasa ya uwajibikaji wa Jeshi la polisi kimuundo ni dhahiri kwamba; “polisi ni wakala wa chama tawala na serikali yake wanaovaa sare kwa minajili ya kuwadhibiti wapinzani/ wananchi wenye mlengo tofauti na watawala”. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema ili kuondoa mtazamo huo kwa wananchi ni muhimu sana upatikanaji wa DCI pamoja na IGP ukawekwa kikatiba zaidi kuliko kuwa hisani ya Rais kama ilivyo Nchini Kenya.
  17. Mheshimiwa Spika, ni muda mwafaka sasa kuwa na vyombo madhubuti vya kuhakikisha uwajibikaji wa jeshi la polisi, lakini Kambi Rasmi ya Upinzani inaungana na wadau kushauri hatua zifuatazo zihusuzo taratibu za uwajibikaji wa polisi kwa kushindwa kwa serikali kuchunguza vifo ama mauaji yaliyofanywa na vyombo vyake, na kushindwa kuchukulia hatua wahusika ni kukiuka haki ya binadamu ya kuishi. Aidha, ni lazima uchunguzi ufanyike ndani ya muda uliopangwa, uwe wazi, wa kina, na bila upendeleo;
  18. Kuanzisha mifumo na taratibu za sheria madhubuti za uchunguzi na uwajibikaji wa polisi.
  19. Uwajibikaji unahitaji uchunguzi na kuhoji jinsi mashtaka ya kesi za jinai yanavyoendeshwa. Huu unahusisha, hatua za kinidhamu, fidia, kusimamia ukweli na kutojirudia kwa utendaji makosa.
  • Fidia inapaswa kuwa sawa na uzito wa kosa na madhara yaliyosababishwa kwa mtu. Pia waathirika wanapaswa kulindwa na kuheshimiwa.
  1. Uwazi ni sehemu muhimu ya uwajibikaji. Ili kuwepo na utekelezaji wa haki ya kuishi, ni muhimu kuwa na uwazi wa sera, sheria, mapungufu na zoezi zima la uchunguzi.
  2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kupata majibu ya maswali yafuatayo ili jamii yetu iweze kuwa na imani na IGP hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu itaingia katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani,
  3. RPC wa Dar es Salaam alisikika katika vyombo vya habari kuwa jeshi hilo lilikuwa likiwashikiria askari watuhumiwa wa mauaji ya Binti Akwilina Akwilini, lakini kwa mshangao wa wengi hadi sasa hajawahi kutoa taarifa yoyote kuhusiana na watuhumiwa wa huuaji wa binti huyo, sasa Kambi Rasmi inataka Waziri Mwenye dhamana atoe kauli kuhusu muuaji huyo yuko wapi?
  4. RPC wa Mkoa wa Dar es salaam, alisikia anawatangazia wananchi kwamba, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee Mangula amepewa sumu na ndio chanzo cha kulazwa Muhimbili, sasa Watanzania wanataka kujua mazingira ya uharifu huo, kwani tayari upelelezi wa awali ulikwishafanywa na jeshi hilo na ndio sababu ya kutolewa taarifa kwa umma. Waarifu hao au washukiwa wa tukio hilo ni akina nani?
  5. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huu ni dhahiri mambo tunayo ambiwa mara zote kuwa, askari walikuwa wanatekeleza wajibu wao yatakuwa hayana mashiko.

 

  1. UWAJIBIKAJI WA JESHI LA POLISI
  2. Mheshimiwa Spika, nidhahiri kuwa Jeshi la Polisi mbali ya kuwa limejengwa katika mfumo mbaya wa uwajibikaji ambao unalilazimisha kuwajibika kwa viongozi wa kisiasa hasa wale walio katika chama tawala, lakini bado lina matatizo kadhaa ya kiutendaji.
  3. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa hadi mwaka 2012 Tanzania ilikuwa na vituo vya polisi vikiwemo vile vidogo vidogo (police outposts) 194, vituo hivi ni vichache kulingana na idadi ya watu na ukubwa wan chi yetu. Sambamba na hilo ni kwamba, wastani wa kuhudumia raia kwa askari mmoja kwa nchi yetu ni kwa uwiano wa 1:1400, wakati kwa viwango vya kimataifa ni 1:450. Viwango hivi vinatuonesha ni kwa jinsi gani ugumu wanaoupata askari wetu katika kuhudumia wananchi.
  4. Mheshimiwa Spika, sio hilo tu suala la vitendea kazi nalo limekuwa ni shida kubwa japokuwa sasa hivi vitendea kazi vinavyopewa kipaumbele zaidi ni vile vya kuhakikisha wanaoandamana kufikisha kilio chao sehemu fulani wanasambazwa kwa kipigo au maji ya washawasha badala ya kuwa na njia nzuri zaidi za kuhakikisha wahusika wanatimiza azma yao bila kujeruhiwa. Kwa ujumla askari wetu bado wanafanyakazi katika mazingira magumu, kulinganisha na majukumu yao.
  5. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mishahara na maslahi mengine kwa askari polisi nao pia kwa kuwa wanapata ajira yao kwa sheria ya utumishi wa umma hivyo na wao, mfumo ule ule wa kanuni zinazo walinda watumishi wa umma inabidi pia na wao utumike. Lakini kutokana na mazingira hatarishi wanayofanyia kazi kuna stahili za nyongeza ambazo pia wanatakiwa kupata.
  6. Mheshimiwa Spika, ukiangalia bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2019/20 Jeshi la Polisi lilitengewa jumla ya shilingi 2,792,924,679.00 lakini hadi kufikia mwezi februari 2020 zilikuwa zimetolewa jumla ya shilingi 3,500,000,000. Fedha hizo ni kwa ajili ya kununulia helikopta ya polisi. Hii maana yake ni kwamba bajeti ya maendeleo iliyokuwa imepangwa ya bilioni 2.8 ni dhahiri haikutumika, na mipango yote ya maendeleo kwa ajili ya maendeleo binafsi ya askari (nyumba) au jeshi haikutolewa. Kwa muktadha huo ni kuzidi kuzorotesha utendaji wa jeshi la polisi.

 

  1. KAMISHENI YA OPERESHENI NA MAFUNZO
  2. Mheshimiwa Spika, kamisheni hii ndiyo yenye jukumu pamoja na kazi zingine ambazo zinaweza kujitokeza kwa kadri uhitajio unavyotokea la;
    1. Kuratibu na kusimamia mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi
    2. Kuratibu na kusimamia operesheni mbalimbali kwa kufanya Doria na Misako mbalimbali nchi kavu, ukanda wa bahari, ukanda wa maziwa makuu na angani kwa lengo na kuzuia uhalifu na wahalifu.
  • Kuratibu na kusimamia ulinzi wa rasilimali muhimu za nchi na wawekezaji kama vile Barabara, madaraja, viwanda, migodi, Mabenki na miundombinu ya umeme na mawasiliano.
  1. Kukusanya maduhuri ya serikali kupitia tozo za makosa ya usalama Barabarani
  1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani itaongelea zaidi dhana ya mafunzo katika kukusanya maduhuri yotakanayo na tozo za makosa ya halali au yasiyo na uhalali yatokeayo barabarani. Ukusanyaji wa fedha ni utaalam na sio tu kwa kuwa ni askari basi kazi hiyo atafanya. Ni muhimu watanzania wakafahamu ni mafunzo gani askari wanaokusanya maduhuri hayo wanapatiwa ili kufanya kazi hiyo. Kwa kuwa tunaamini Kamisheni ya mafunzo ina jukumu la kuwapa mafunzo askari hao, kinyume chake ni yale yanayotokea la uchonganishi wa Jeshi la Polisi na raia kwani wahusika wanatumia mamlaka yao vibaya katika kadhia nzima ya ukusanyaji wa maduhuri.
  2. Mheshimiwa Spika, yapo malalamiko pia kwamba, mafunzo yanayotolewa kwa Askari kwa ajili ya kuboresha utendaji wa jeshi la Polisi zinagharamiwa na askari wenyewe kwa kukatwa posho zao, badala ya kugharamiwa na mwajili. Na pale wanapokwenda kusoma kwenye vyuo mbali na vile vya Kijeshi inawabidi watumie utaratibu wa kukopa. Pia zipo taarifa dhidi ya Jeshi la Polisi kutumia fedha nyingi za walipa kodi kwa ajili ya kugharamia mafunzo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni kwanini hasa Askari wanaokwenda kozi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi, wanakatwa fedha zao za posho ili kugharamia mafunzo hayo? Tukumbuke pia askari hawa pia wanafamilia zao na wana majukumu mengine ya kijamii kama walivyo watumishi wengine.
  3. Mheshimiwa Spika, ni mara nyingi Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikiitaka Serikali kuhakikisha kuwa askari polisi hasa wale wanaojiunga na jeshi hilo wanapatiwa makazi yenye staha kulingana na hadhi ya jeshi hili la polisi. Makazi duni kwa askari ni kuwafanya askari kuwa dhariri mbele ya macho ya jamii. Tunarudia tena Serikali ihakikishe askari wanaishi katika mazingira bora ili kutenda kazi zao wakiwa na mori zaidi.
  4. TOZO ZA BARABARANI (Traffic Notifications)

 

  1. Mheshimiwa Spika,mapato yatokanayo na adhabu kwa madereva wanaokutwa na hatia ya kuvunja sheria za usalama barabarani Serikali(Polisi) imetoa kadirio la makosa milioni 3.1. kwa mwaka 2020/21 ambayo yataingiza mapato ya shilingi 118,922,470,000.
  2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inadhani chanzo hiki cha mapato sio cha haki au sahihi, kwani ukisha weka kwenye makadirio, maana yake unawalazima askari polisi badala ya kuelimisha watumiaji wa barabara wao watakuwa wanafanya kazi ya kuwawekea makosa ambayo sio ya haki. Hili jambo linazidisha uhasama usio wa lazima kati ya Jeshi la Polisi na raia. Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuacha kuweka chanzo hiki kwenye makadrio kwenye bajeti yake.
  3. Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hii ya madhira kwa jamii yanayofanywa na jeshi la polisi ni makubwa kiasi kwamba, nguvu zilizopitiliza zinatumiwa na jeshi hilo kwenye matukio ya kijamii (masuala ya kisiasa, watu kufikisha hisia zao kwa maandamano-wanafunzi, wafanyakazi n.k.)

 

  1. Mheshimiwa Spika, CHADEMA inashauri Jeshi la Polisi kuwa ni chombo cha kutoa huduma kwa jamii badala ya kuwa chombo cha kutumia mabavu, “police service instead of being police force”. Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa jeshi letu la polisi kufanyiwa maboresho ili kuwa la kutoa huduma zaidi, kuwa na weledi zaidi katika kukabiliana utoaji wa huduma badala ya kutumia nguvu na mabavu yaliyopitiliza.

 

  1. MAZONGE ZONGE YA JESHI LA POLISI
  2. Mheshimiwa Spika, kwa kumbukumbu za Hansard ni kuwa Mheshimiwa Susan Lyimo alifungiwa na Kamati ya maadili kwa kusema kuwa Jeshi la Polisi lilinunua magari ya washawasha yapatayo mia saba. Sasa katika taarifa iliyosomwa na Mwenyekiti wa Pac ni kuwa bado upelelezi unaendelea juu ya ununuzi wa magari 777 yenye thamani ya USD milioni 29.6 uliofanywa na Jeshi hilo bila ya uwepo wa Mikataba.
  3. Mheshimiwa Spika, jeshi hilo lilitumia jumla ya shilingi milioni 888.5 malipo ya posho za resheni kuwalipa watu wasiokuwa askari polisi au watu wasiostahili. Lakini hadi sasa upelelezi unaendelea!!!!! Hatujawahi kusikia kesi ya wahusika ipo katika mahakama ya hakimu mkazi yupi hapa Tanzania.
  4. Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kuna malipo yalifanyika kwa huduma hewa yenye thamani ya shilingi milioni 798.78. Upelelezi bado unaendelea hadi leo, lakini mwisho wa siku watuhumiwa wataachiwa huru, kwani wahusika wakuu ni wao kwa wao( Watuhumiwa, wapelelezi na wasimamamizi wa kesi)
  5. Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa ubia kati ya Jeshi la Polisi na Mwekezaji eneo la Osterbay, mradi uliogharimu jumla ya dola za marekani milioni 700 na hadi kufikia mwezi Oktoba 2018 ulikuwa umekamilika kwa asilimia mia moja[3], lakini Rais akausitisha kutokana na harufu ya rushwa. Lakini hadi sasa uchunguzi/ upelelezi bado unaendelea.
  6. Mheshimiwa Spika, kuna kashfa nyingine ya Mbunge Mwenzetu, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu mikataba ya vifaa vya Jeshi la Zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Tsh trilioni 1.04 kutoka kampuni ya nje ya nchi bila kufuata sheria. Jambo ambalo Mheshimiwa Rais alitengua uwaziri wake pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi hilo, Kamishna Generali Thobias Andengenye. Lakini hadi sasa tunasikia upelelezi bado unaendelea na wahusika wapo huru. Ushahidi wote Rais alikuwa nao na ndio sababu ya kufikia maamuzi aliyoyafanya. Je, tunakwama wapi katika kuchukua hatua za kuwapeleka mahakamani wahusika?
  7. Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumekuwa tunasema, kuwa ni lazima kuwepo na uhuru wa chombo kingine kuliangalia jeshi la polisi jinsi kinavyofanya kazi zake. Sasa kwa mifano hiyo ya ubadhirifu wa mabilioni ya fedha, DCI na DPP ndio wenye jukumu la kusema kuna kesi au hakuna. Kama ikitokea na wao ni sehemu ya ubadhirifu huo ni nani atahusika katika kutafuta ukweli? Hapa ndipo kile kinachoitwa “Organized Crime” kilipo katika mazingira kama haya.
  8. ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA
  9. Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limekuwa na utamaduni wa kuzuia Mikutano ya hadhara ambayo ipo kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa na kanuni zake. Utamaduni huu mmbovu umeshamiri Zaidi Katika serikali hii ya awamu ya tano,  kisingizio mara zote imekuwa ni taarifa za Kiintelijensia na mara zote taarifa hizo huwepo kama anayetaka kufanya Mikutano ni mpinzani.
  10. Mheshimiwa Spika, zuio la Mikutano limefikia pabaya zaidi kwa sisi wabunge na Madiwani wa upinzani kuzuiliwa kufanya mikutano kuzungumza na.wapiga kura wetu ili kuweza kutambua na hatimaye kutatua changamot zao kwa kushirikisha wananchi wenyewe.
  11. Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa uchaguzi na tunategemea Kuwa na kampeni, tunatoa wito kwa jeshi la polisi liwajibike kwa mujibu wa sheria na kusimamia kampeni kwa haki na Bila upendeleo wowote Kwani haki huinua taifa!  Hatutegemei kuendelea kusikia visingizio vya taarifa za Kiintelijensia bali tunataka Kuona uchaguzi ukiliunganisha taifa badala ya kuligawa taifa letu.
  12. Mheshimiwa Spika, watanzania Wanaelekea kufikia ukomo wa uvumilivu wao na wamechoka kuonewa mara kwa mara. Nimeyasema haya ili kila mmoja atimize wajibu wake kwa Taifa. Twendeni tukashindane kwa hoja, tusitegemee kubebwa na mbeleko ya Majeshi Kwani wananchi wakiamua hakuna popote Duniani ambako waliwahi kushindwa!
  13. TUME HURU YA UCHAGUZI
  14. Mheshimiwa Spika, tunapodai tume huru ya uchaguzi sio kama tunataka CHADEMA au ACT-Wazalendo washinde uchaguzi, la hasha, bali ni kuwa na uhakika wa usalama wa nchi.
  15. Mheshimiwa Spika, usalama wan chi nyingi hasa katika ulimwengu wa nchi zinazoendelea umelegalega kutokana na uchaguzi katika mataifa yao. Mchakato wa uchaguzi ukiwa unatiliwa mashaka baina ya pande husika na uchaguzi huo, ni chanzo kikubwa cha kuondoa amani ya nchi.
  16. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inavitaka vyombo vyote vinavyohusika na mchakato wa uchaguzi kuhakikisha kunakuwepo na tume huru ya uchaguzi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi wa kumi 2020.
  17. Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingi sana zinazohusiana na namna gani uwepo wa Tume huru ya uchaguzi inavyoweza kuimarisha hali ya usalama na amani katika nchi. Lakini kutokana na ufinyu wa muda inatosha kusema kuwa ili jeshi la polisi na vyombo vingine ambavyo vina jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao kuwa katika mazingira ambayo hayataleta madhara na yataepusha uhatarishi wa amani na usalama kwa raia na mali zao, ni vyema Tume huru ya uchaguzi kikawa kipaumbele kwa sasa.
  18. IDARA YA MAGEREZA
  19. Mheshimiwa Spika, Hali ya Magereza na Vituo vya Mahabusu imeendelea kuwa mbaya na hivyo kutishia maisha. Msongamano, usafi duni wa vyoo, na huduma duni za afya vilikuwa vimeshamiri. Kufikia mwaka 2015, magereza, ambayo yalijengwa kuwa na uwezo wa kushikilia jumla ya wafungwa 29,552, yalishikilia 31,382, ikiwa ni asilimia 6 zaidi ya uwezo wake.
  20. Mheshimiwa Spika, Wafungwa wanaosuburi kusomewa mashtakana, wafungwa waliohukumiwa wote wanawekwa pamoja. Watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane pamoja na watu wazima katika magereza kadhaa wanakaa pamoja kutokana na uhaba wa sehemu zenye nafasi za kuweka watu kizuizini. Mwaka 2013 idara huru ya serikali, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), ilitembelea magereza na sehemu kadhaa zilizoteuliwa za kuweka watu kizuizini na walikuta watoto 452 waliokuwa wameshikiliwa katika magereza ya watu wazima. Kati yao, 101 walikuwa wafungwa waliokutwa na hatia na 351 walikuwa wakisubiri kusomewa kesi zao.
  21. Mheshimiwa Spika, katika magereza mengi ya watu wazima, watoto walikuwa wamewekwa katika vyumbatofauti lakini walichanganywa na watu wazimawakati wamchana na walipokuwa wakipelekwa mahakamani. Katika magereza mengine watoto na watu wazima walichanganywa pamoja wakati wote. Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa raia kwa Serikali kurekebisha kwa haraka hali hii iliyopo ili kuondoa udhalilishaji ambao unapelekea nchi yetu kuwa kwenye taarifa za Haki za Binadamu juu ya uvunjifu wa haki za watoto walio magerezani.
  22. Mheshimiwa Spika, inasemwa kuwa Magereza ni kituo cha kurekebisha tabia, lakini ukweli ni kuwa ni chombo cha kuwafanya watu kuwa sugu zaidi na hivyo kuwa na tabia zingine ambazo hawakuwa nazo wakati wanahukumiwa.

 

  1. Mheshimiwa Spika, ukweli huu unapata nguvu zaidi pale wafungwa wanapopewa msamaha wa Rais na chini ya juma moja la wahusika kukaa uraiani wanafanya matukio makubwa zaidi ya yale waliyohukumiwa nayo na hivyo kurudishwa tena magereza.

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika hili la kuhakikisha magereza zetu zinachukua taswira iliyo kusudiwa ni vyema askari wetu wanaosimamia wafungwa kwanza kupata mafunzo na pia kupatiwa mishahara na marupurupu mengine yanayowawezesha wao na familia zao kuishi kwa staha. Kwani hali ilivyo askari hao wanachukia sana wafungwa na kuwaona kama sio binadamu na hivyo kuwafanyia vitendo vyote vya kuwadhalilisha utu wao kama binadamu, na matendo hayo ni utaratibu wa kawaida kufanyiwa wafungwa pale wanapoingia magereza. Ukweli ni kuwa mahabusu na wafungwa wanapigwa mno na madhira mengine mengi tu, haya mateso sio kama yanawarekebisha bali yanawafanya kuwa wanyama zaidi na pale wanapotoka au kumaliza muda wao wanafanya mabaya zaidi kuliko hapo awali.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Jimbo la Viktoria nchi ya Australia wana program katika magereza zao ya kuwaandaa wafungwa wanaomaliza muda wao, namna ambavyo watarudi katika jamii na kukubalika na wao kuwa na amani na wakiwa na shughuli za kufanya kutokana mtaji wanaopewa kutokana na uwekezaji ambao wanakuwa wanafanya kwa kipindi chote cha uzalishaji wanapokuwa wanatumikia kifungo.

 

  1. Mheshimiwa Spika, program hii ni kutokana na ukweli kwamba wengine wakimaliza vifungo wanakuta hawana sehemu za kuishi na hivyo hawana sehemu ya kuanzia katika kuonesha matumizi ya taaluma zao walizotokanazo jela. Hivyo ni muhimu sana magereza zetu kuangalia ni kwa namna gani eneo hili linakuwa ni kituo cha watu kujifunza na kuwa na taaluma za kusaidia kuendesha maisha yao na kuongeza ajira kwa jamii inayo wazunguka.[4]

 

 

  1. SHIRIKA LA MAGEREZA
  2. Mheshimiwa Spika, Shirika la Magereza lilianzishwa mwaka 1983 kwa Sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1974 (the Corporation Sole Act No. 23/1974) chini ya kifungu cha 3(1) na kanuni zake za mwaka 1983. Shirika lilikuwa na mwelekeo wa kuendesha shughuli zake kibiashara, kuzalisha mali kwa ubora katika mazingira ya ushindani ili kupata faida.

 

  1. Mheshimiwa Spika,Shirika wakati linaanzishwa lilikuwa na malengo makuu yafuatayo:
  2. Kuwa chombo cha urekebishaji wafungwa kwa kuwafundisha stadi za kazi na kuwaongezea ujuzi kwa wale ambao tayari wana ujuzi.
  3. Kuendesha shughuli zake kiuchumi na kibiashara kwa kujitegemea (Revolving fund).
  • Kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama za uendeshaji wa Magereza.
  1. Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa shirika hili ni sehemu ya Jeshi la Magereza na muundo wa Utawala wa Shirika hili ni ufuatao:

 

 

  1. Mheshimiwa Spika,mfumo huu unaweza kuwa ni wa kikiritimba sana, hasa katika kufikia maamuzi, na hasa katika mazingira halisi ya kibiashara,ili biashara iweze kushamiri maamuzi ya haraka ni muhimu sana. Hivyo kwa mfumo ulivyo unatoa nafasi kwa ubadhirifu kufanyika na hadi maamuzi ya kurekebisha yafanyike nidhahiri athari zinakuwa zimefanyika na kurekebisha kwake uhitaji gharama kubwa mno.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Shirika lina vitengo vikuu vya mashirika matatu na mashirika hayo matatu yana jumla ya miradi 23. Vifuatavyo ni vitengo vya shirika hilo ambalo mtendaji wake mkuu kwa mujibu wa muundo wa Jeshi la Magereza ni Kamishna Generali wa Magereza  (CGP).
  2. Ujenzi na Ukarabati
  3. Kilimo, Mifugo na Mazingira.
  • Viwanda vidogovidogo.
  1. Mheshimiwa Spika, Mashirika hayo tajwa hapo awali yana jumla ya Miradi 23, kati ya hiyo miradi 15 ni ya kilimo pamoja na mifugo na miradi 8 ni ya viwanda vidogo vidogo, pia zipo shughuli za mradi wa Kikosi cha Ujenzi zinazosimamiwa na Shirika.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Takwimu zinaonesha kwamba Shirika hilo lililo chini ya Magereza lina miradi ya kilimo na mifugo yenye jumla ya ekari 110,541 (Hekta 44,216.4) ambazo zinafaa kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo kama ifuatavyo:
No. Kituo Mkoa Ukubwa/ekari
1. Shamba la ng’ombe wa maziwa Kingolwira Morogoro 13,750
2. Shamba la mahindi gereza Songwe Mbeya 4,225
3. Shamba la mifugo Wami Gereza Mbigiri Morogoro 17,730
4. Shamba la kilimo na Mifugo Gereza la Kitengule Kagera 15,000
5. Shamba la Kilimo na Mifugo Gereza la Mollo Sumbawanga 8,100
6. Shamba la Mitamba Gereza Mugumu Mara 6,000
7. Shamba la Kilimo Gereza Ludewa Iringa 3,750
8. Shamba la kilimo na Mifugo gereza Isupilo Iringa 8,893
9. Shamba la kilimo  Gereza la Kiberege Morogoro 6,250
10. Shamba la Kilimo Gereza la Idete Morogoro 7,940
11. Shamba la Kilimo na Mifugo Gereza Kitai Ruvuma 7,806
12. Shamba la Kilimo Gereza Mkwaya Ruvuma 3,442
13. Shamba la Kilimo Gereza Bagamoyo Pwani 6,250
14. Shamba la Kilimo Gereza la Mang’ola Arusha 320
15. Shamba la Kilimo Gereza  Arusha. 1,085
    JUMLA 110,541

 

  1. Mheshimiwa Spika, Kwa miradi 15 ya kilimo na mifugo na kama kweli shirika linaendeshwa kibiashara ni ukweli usio na shaka kuwa miradi hiyo inatosha kulisha taasisi nzima ya magereza na ziada kubwa ya kuuzwa ndani na nje ya nchi. Kwa maana nyingine ni kwamba shirika lina kitu kinachoitwa “comparative Advantage” kulinganisha na mashirika mengine ya kilimo. Kwani nguvu kazi yake ni bure!!!!!!!!!!
  2. Mheshimiwa Spika, magereza inatakiwa kuwa ni kituo kikubwa sana cha kutoa taaluma kwa wafungwa kulinganisha na ilivyosasa, magereza ni idara ya “kukomoa na kukomesha watu” haiwezekani kwa teknolojia zilizopo sasa, wafungwa wawe ni watu wa kupewa kazi ngumu ya kulima (ikiwezekana walime kwa meno) na kupasua kuni. Jambo hilo linawafanya wafungwa hata wakitoka wanatoka bila ya kuwa na taaluma yoyote na zaidi wanapata ujuzi wa kuwa sugu zaidi katika mipango ya uhalifu.
  3. Mheshimiwa Spika, gereza la Segerea hapo mjini lina miliki akari takriban mia mbili, sasa hivi ndio eneo hilo linasafishwa kupanda mikorosho. Tukumbuke kuwa eneo hilo kama lingetumiwa kwa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa hata mia moja tu, na kulima malisho yenye ubora, kwa ng’ombe mmoja wa maziwa anatoa lita 25 hadi 35 kwa siku. Soko la maziwa ni kubwa sana. Pia magereza ya Segerea kingekuwa ni kituo kikuu cha kuuza mitamba na ushauri kwa wafugaji wadogo wa mikoa ya Dar na Pwani. Sasa tuulize miaka yote fursa hii bado haionekani chini ya utawala wa CCM, katika mazingira kama hayo hayo ya Gereza la Segerea. Kule Bagamoyo Gereza lina miliki ardhi ya ekari 6,250 lakini takriban robo tatu ya eneo hilo kuna mtu binafsi anafuga na hakuna chochote kinachoingizwa na Magereza.
  4. Mheshimiwa Spika, magereza ya wenzetu, watu wakishamaliza muda wao tayari wanakuwa na taaluma za kuweza kuwasaidia katika maisha yao, mfano mzuri ni kijana mmoja pale TARIME anaitwa COBRA jina maarufu, alikuwa amefungwa kule HongKong, lakini baada ya kumaliza kifungo na kurudi, sasa hivi Tarime nzima yeye ndiye mtengenezaji mkuu wa Green houses, Money Maker pumps, plough zinazotumia motor za kuendeshea pikipiki na kufunga umeme unaozalishwa kwa maji na ubunifu mwingi tu katika uzalishaji.
  5. Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na tuhuma nyingi za ubadhirifu wa mifugo hasa kwenye gereza la Kitengule ambapo Mkuu wa Gereza anamiliki ng’ombe na Gereza nalo lina miliki ng’ombe. Hapo ni dhahiri maslahi binafsi hayawezi kukosekana na utagundua ni kwanini miaka yote uzalishaji kwenye gereza hauwezi kupanda, lakini ngo’ombe binafsi za mkuu wa gereza zinaongezeka mwaka hadi mwaka.

 

  1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kiasi gani cha uzalishaji kinapatikana kila mwaka kutoka kwa kila shamba kulingana na mpangilio uliooneshwa hapo juu?

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kikosi cha Ujenzi nacho kimekuwa kikifanyakazi kadhaa kwa “advantage” kubwa kuwa kinapata kazi bila ya uwepo wa ushindani. Kwa msingi huo Kambi Rasmi ya Upinzani inatarajia kuwa ubora wa kazi zake kwa teknolojia inayotumika ungekuwa wa hali ya juu sana kiasi kwamba kinaweza kuwa shindani hata kwa kazi ambazo sio za Serikali. Lakini jambo hilo halionekani katika tasnia ya ujenzi.

 

 

 

  1. IDARA YA UHAMIAJI

 

  1. Mheshimiwa Spika, uhamiaji ni moja ya idara zilizo chini ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi ikiwa na Majukumu ya ambayo yameelezwa katika Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54 Rejeo la mwaka 2016. Jukumu la msingi la Idara ya Uhamiaji ni kulinda usalama wa nchi kwa kudhibiti uingiaji, ukaaji na utokaji nje ya nchi kwa raia na wageni.
  2. Mheshimiwa Spika, ukinyumbulisha jukumu hilo la msingi utaona ni jinsi gani idara hii ilivyokuwa na umuhimu mkubwa wa kutunza mahusiano na nchi mbalimbali duniani. Jinsi ambavyo Idara hii itakavyo watendea wageni wanaoingia au watakaokuwa wanatoka ndivyo nchi yetu itakavyo inapata sifa nzuri au mbaya nje ya mipaka yetu.
  3. Mheshimiwa Spika, mbali na kuwa idara ya kutengeneza mahusiano na wenzetu duniani, vile vile ni chombo cha ukusanyaji wa mapato kutokana na malipo ya huduma za kiuhamiaji. Pia idara hii inatumika kutengeneza kanzi data ya wale wanaoitwa walowezi katika nchi hii.
  4. Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na malalamiko mengi sana juu ya Idara hii ya uhamiaji kutumika kwa maslahi ya kisiasa hasa kutokana na jukumu ambalo wamepewa la kutengeneza kanzi data ya wale wanaoitwa walowezi katika nchi hii. Hili neon walowezi limekuwa likitumika vibaya kuwanyanyasa wale wote ambao washindani wanadhani ni watu ambao wanajitambua na wanaushawishi mkubwa katika jamii. Mifano iliyo hai ni mwingi lakini kuna watu ambao walishawahi kusemwa kuwa ni walowezi na hivyo ikawalazimu kutetea uraia wao kwa nyaraka na wengine hadi sasa hati zao za kusafiria bado zimeshikiriwa na Idara (Jeneral Ulimwengu,Hussein Bashe, Abdul Nondo, Baba Askofu Severini Niwemugizi,Aidan Eyakuze)
  5. Mheshimiwa Spika, ukiachilia hayo ya Idara hii ya Uhamiaji kutumiwa kisiasa bado kuna utata mwingi sana jinsi idara hii inavyotimiza majukumu yake hasa katika zoezi zima la utoaji vibali vya muda wa nyongeza wa kazi kwa wageni ambao wanafanyakazi kazi hapa nchini. Jambo hili limelalamikiwa sana na wananchi hasa kwa wageni wanaofanyakazi ambazo watanzania wengi wana taaluma husika.

 

  1. URAIA PACHA
  2. Mheshimiwa Spika, CHADEMA tunaamini katika uraia pacha, na hili ni kutokana na ukweli kwamba watanzania ambao wanaishi nje ya Tanzania katika kutafuta riziki kwa familia zao zilizo nje na ndani wapato milioni mbili wanatakiwa kuwa sehemu ya maendeleo ya nchi yetu. Hivyo watanzania hao kuwa na haki zote za msingi ambazo wenzao wanaoishi Tanzania wanazipata.
  3. Mheshimiwa Spika, Wengi wa watanzania hawa walizaliwa Tanzania, wamesomea Tanzania, wana familia Tanzania na mioyo yao ni Tanzania.Watanzania hawa wanasononeka kupoteza uraia wa KUZALIWA kwa sababu tu wamebahatika kupata uraia wa nchi nyingine ili kuweza kurahisisha jinsi ya kupata elimu, huduma za afya na kufanya kazi kwenye mataifa hayo wanayo ishi.
  4. Mheshimiwa Spika, kwa kuendelea kukaza shingo kwa Serikali ni kuipotezea Tanzania fursa ya nguvu kazi kwani Watanzania hawa kuna nguvu kazi madaktari, wanasheria, mainginia, wenye vipaji vya michezo, wenye miradi na wajuzi wa fani mbali mbali ambao ni hazina kubwa kwa taifa letu. Hawa waTanzania wanashindwa kuwekeza nyumbani kwa kuwa wanakosa haki ya kuitwa waTanzania huku UHALISIA wamezaliwa Tanzania. Ni muda mwafaka sasa Watanzania hawa kutoa ushirikiano wao wa hali na mali kwa Chama ambacho kinaamini katika URAIA PACHA kuhakikisha kinashinda uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2020,ili Tanzania itambue rasmi uwepo wa Watanzania wenye uraia wa mataifa mengine.
  5. Mheshimiwa Spika,kwa mujibu wa taarifa zilizotolea na taasisi ya Trade Mark East Africa inaonesha kuwa nchi za Afrika ya Mashariki kati ya mwaka 2013 hadi 2018 zilipokea jumla ya dola za kimarekani bilioni 17.39, toka kwa raia wao wanaoishi katika mataifa mbalimbali duniani. Kati ya fedha hizo Kenya ndiyo ilipokea kiasi kikubwa cha dola bilioni 10.74; ikifuatiwa na Uganda dola bilioni 6.24; Sudani ya Kusini dola bilioni 2.85; Tanzania dola bilioni 2.39; Rwanda dola bilioni 1.13 na mwisho ilikuwa ni Burundi dola milioni 257[5].
  6. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ina wasiwasi Tanzania haina takwimu zozote kuhusiana na fedha zinazoingia kutoka kwa watanzania waishio nje, kwani haina mfumo madhubuti wa utambuzi wa fedha hizo. Takwimu hizo za dola bilioni 2.39 ni fedha nyingi kiasi kutoka watanzania waishio mataifa ya Marekani, Kenya, Uganda, Afrika ya Kusini, Australia, Malawi na Burundi tu. Hatujaweka wale waishio Bara la Ulaya na nchi zingine za falme za Kiarabu. Hii ni fursa ya kutekeleza mipango yetu ya ndani kama kutakuwepo na utambuzi kisheria (Uraia pacha) na uratibu mzuri, sio tu fedha bali pia nguvu kazi yao pindi wanaporudi nyumbani au kutumia mitandao yao wataalam wengine duniani katika sekta mbalimbali za maendeleo.
  7. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ina uhakika kabisa Serikali ya CCM inafahamu faidi nyingi zaidi za uwepo na umuhimu wa uraia pacha, lakini kutokana na kutokujiamini (inferiorty complex) na kufikiria zaidi nafasi zao za kimadaraka kuwa watanzania waishio nje wanauelewa mpana zaidi kuwazidi wale waliokaria viti vya madaraka, hivyo watachukua nafasi na hilo ndio tatizo kubwa la Serikali ya CCM.

 

  1. HATI ZA KUSAFIRIA ZA KIELEKTRONIKI (E-PASSPORT)
  2. Mheshimiwa Spika, nchi yetu iko kwenye mageuzi makubwa ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inaimarisha mfumo wetu wa usalama, na pia kuhakikisha mfumo wa kudhibiti mapato yatokanayo na uuzwaji wa hati za kusafiria.
  3. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa kuingia kwenye mfumo huu wa kielektroniki wa matumizi ya hati za kusafiria ni kuhakikisha kuwa inakabiriana na uharifu ambao unaweza kujitokeza na wahusika kutokomea nchi za wenzetu bila kujulikana. Hati za kielektroniki zinaendana na mitambo ambayo inatakiwa kufungwa kwenye vituo vyote vya mipakani ambavyo ni njia halali za kutoka na kuingia nchini.
  4. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza watanzania kama vituo vyote mbali ya viwanja vya ndege vina mitambo yaku-scan passport na kupata taarifa za muhusika kutoka kwenye mifumo mingine kama vile polisi, tra, wizara ya elimu n.k? Kama mifumo hiyo haijafungwa au haipo katika maeneo hayo ya mipakani ambapo wasafiri wanatoka na kuingia nchini kila kukicha, nini umuhimu hasa wa hati hizo za kielektroniki?

 

  1. MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA URAIA-NIDA
  2. Mheshimiwa Spika, Kuna watanzania wengi Zaidi ya Milioni 5 ambao simu zao zimezimwa (Kwa mujibu wa TCRA) Kwa sababu hawana vitambulisho vya Nida au namba za Nida. Watanzania Hawa wamekoseshwa mawasiliano na wengine vipato vyao Kwani simu ni benki na pia kama unafanya biashara taarifa ndio msingi wa biashara wenyewe.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa hesabu ndogo tu, tuchukulie kwa idadi hiyo ya simu kwa siku kutokana na mihamala inayofanyika kodi kwa serikali ni shilingi 250 kwa kila moja, sasa kwa mwezi mmoja maana nayake ni milioni tano maea 250 mara siku 30  sawa na shilingi bilioni 37.5 ambazo serikali inapoteza kwa mwezi kutokana na kufungia laini za simu milioni 5.
  4. Mheshimiwa Spika, kutokana na simu hizo kuzimwa kumeifanya serikali ikakosa mapato yake yatokanayo na kodi na ushuru mbalimbali wanazokatwa watumiaji wa simu hizo zilizozimwa. Watanzania waliozimiwa simu zao wengine ni kwa sababu ya NIDA kushindwa kuwapa namba na kuwasajili.
  5. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imemsikia Waziri wa mambo ya ndani akiwaomba radhi watanzania waliozimiwa simu zao kutokana na uzembe wa Nida. Tunamtaka waziri asiishie kuomba radhi Bali simu zote ambazo zimefungiwa zifunguliwe Mpaka hapo NIDA itakapokuwa na uwezo wa kusajili na kutoa namba na vitambulisho  kwa watanzania wote wenye sifa.
  6. Aidha, Mheshimiwa Spika, watanzania wote waliosajiliwa na Nida waweze kupatiwa Vitambulisho vyao vya Taifa kwani wanapoenda Maeneo mbalimbali ya huduma kama vile kudhamini ndugu zao vituo vya polisi au mahakamani hutakiwa kuwa na Vitambulisho vya Taifa wakati Nida imeshindwa kuwapatia Vitambulisho hivyo; Vilevile unapotaka kusajili biashara au kupata leseni unatakiwa kuwa na kitambulisho cha Taifa.
  7. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tunamshauri Waziri wa mambo ya ndani kuongeza wigo wa Vitambulisho ambavyo vinaweza kutumika vikiwemo; Hati ya kusafiria, leseni ya udereva, Vitambulisho vya mpiga kura kama sheria ya “Epoca” na marejeo yake inavyohitaji kwani itapunguza usumbufu kwa wananchi wetu ambao tatizo liko mikononi mwa serikali na wanaadhibiwa wao kwa kuonewa ili kuficha uzembe wa NIDA.
  8. HITIMISHO
  9. Mheshimiwa Spika, kukosekama kwa utawala bora ni kigezo kikubwa kwa taifa kuvurugika na kukosa mwelekeo, na hivyo mamlaka ambazo zinasimamia utawala bora zinafanya kazi zake bila kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na hivyo kuongeza chuki kubwa miongoni mwa jamii.
  10. Mheshimiwa Spika, ukimya uliopo sasa sio mafanikio ya vyombo dola kudhibiti usalama, kwani taifa lenye watu wengi wenye chuki ni taifa linaloweza kulipuka wakati wowote. Msingi wa amani ya nchi unajengwa na furaha ya watu katika maisha ya kila siku na sio hofu inayojengwa katika jamii kama njia ya kutawala. Kwa sasa watu wengi wanaumia na kuumizwa na kukaa kwao kimya  ni ushindi kwa Serikali na vyombo vyake vya dola, lakini kumbe tabia hizo zinajengwa mpasuko mkubwa mno katika jamii na kuna siku chuki dhidi ya uonevu zitaungana bila ushawishi toka kwa makundi mbalimbali.
  11. Mheshimiwa Spika, ni muhimu serikali ikafahamu kuwa Taifa huru na la amani halijengwi kwa silaha za kisasa isipokuwa ni katika utawala unaozingatia haki, ukweli na usawa. Waliopo serikalini kimsingi huwa ni vigumu sana kuelewa ukweli huu na wanaelewa pale wanapotoka katika madaraka. Kwa mwenendo wa Serikali hii ni bora sasa bajeti ya wizara ya mambo ya ndani kuhusu uboreshaji wa magereza, yaani kanuni na mazingira mkaipa kipaumbele sasa kwa maana wengi wenu Serikalini mnaweza mkajikuta mnaishi magereza kwa muda mrefu sana hatakama utawala utabakia wa Chama cha Mapinduzi.
  12. Mheshimiwa Spika, Frederick Sumaye alikuwa Waziri Mkuu wa kipindi cha miaka kumi, wakati nikiwa magereza nilisikia kuwa ameporwa mashamba yake Morogoro na Dar es salaam, nilimwandikia barua ya kumpa pole kutoka gerezani. Alipokuwa gerezani kunisalimia alikuwa analalamikia ubaya wa sheria za ardhi, sheria ambazo yeye kama Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka kumi hakuwahi kuona tatizo la sheria hizo. Vile vile baada baada ya uchaguzi mkuu wa 2015, Mheshimiwa Lowasa ambaye alikuwa mgombea wa CHADEMA alilalamikia kuhusu muundo wa Tume ya uchaguzi na taratibu zinazotumika katika kutangaza washindi na mchakato mzima wa uchaguzi hadi kupigwa kwa kura.
  13. Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Lowasa alikuwa kiongozi mwandamizi wa CCM hadi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kabla  hajajiunga na  Kuna mambo mengi yanapaswa kuwafundisha, kwamba unaweza kuwa salama kesho kama utakuwa mwema leo, kwani “KARMA IS A BITCH, WHAT GOES AROUND COMES AROUND”, kwa hiyo hakuna sheria mbaya mnayotunga leo wala utaratibu mbaya mnaothibitisha leo ambao nyie na watoto wenu hamtavuna matunda yake.
  14. Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kwamba kuwa jeshi la polisi linakutana na changamoto kubwa katika ulinzi wa raia na mali zao, lakini ukweli ni kwamba changamoto ya ulinzi na usalama wa nchi iko zaidi katika dhana ya utawala bora na utawala wa sheria kuliko jeshi la polisi kukabiliana na wezi wa Tv na simu mitaani.
  15. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, uimara na amani ya nchi unaanza na misingi yote ya utawala bora, haki, usawa na demokrasia imara.
  16. Mheshimiwa Spika, wakati ulimwengu unapita katika changamoto ya virusi vya Corona ni lazima vyombo vya ulinzi na usalama viandaliwe, kwani pamoja na matatizo ya kiafya lakini kuna matatizo ya kiuchumi na kijamii yanayosababisha umasikini mkubwa na umsikini ni njaa na mutu mwenye njaa ni mtu mwenye hasira.
  17. Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali katika janga hili la corona unapaswa kutenga bajeti ya ziada kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na kuvipatia vifaa vya kujikinga vya kutosha. Mfano jana, katika ofisi yetu ya Dodoma ya Chama, polisi waliokuja kuzuia kikao cha Mwenyekiti wa Chama Taifa na waandishi wa habari, kati ya askari polisi takriban 15 waliokuwa kwenye gari lile ni askari mmoja tu aliyekuwa amevaa barakoa. Na barakoa hiyo illionekana kama imevaliwa kwa siku zisizopungua sana.
  18. Mheshimiwa Spika, ni hatari wakati wa mapambano ya corona Virus, askari kuanza kupata maambukizi kabla ya watu wengine kwani wanahitajika sana katika kipindi hiki cha changamoto ya hali ngumu ya maisha na ugonjwa wa corona, Afya zao ni muhimu sana.
  19. Mheshimiwa Spika,tatizo la corona ni mtambuka, tunaomba Serikali isone aibu ku-copy na ku-paste kila njia bora inayofanywa na mataifa mengine katika kukabiliana na ugonjwa huu, kwa maisha ya kila siku ya watanzania, Serikali isipoamua sasa kuchukua hatua ngumu na shirikishi kukabiliana na tatizo hili bila shaka watu wetu wengii sana watapoteza maisha. Tumeshauri mara kadhaa Bungeni kwa michango yetu kuna baadhi ya maeneo yamefanyiwa kazi ikiwa na bunge lako mwenyewe lakini tatizo bado ni kubwa sana kulinganisha na hatua ambazo tayari zimechukuliwa.
  20. Mheshimiwa Spika, katika hilo hasa la usalama wa wananchi kuhusu ugonjwa wa CORONA, kambi Rasmi ya Upinzani inashauri yafuatayo:
  21. Baa zote zinazouza vilevi ziwe ni maduka ya vilevi, kwa maana kuwa wateja waende kununua na kuondoka mahali hapo.
  22. Majumba ya starehe na klabu za usiku pamoja na kumbi za disco vyote vifungwe kwa kipindi cha mwezi mzima.
  • Jeshi la kujenga nchi, (JKT) litumike kuongezea nguvu kwa askari polisi wa usalama barabarani kuhakikisha kuwa usafiri wa boda boda kofia za kujikinga hazivaliwi na abiria ili kuondoa uwezekano wa kuambukizana virusi vya Corona.
  1. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

…………………………….

Godbless Jonathan Lema(Mb)

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Mambo ya Ndani.

23.04.2020

[1] http://hakinausalama.org/ – UWAJIBIKAJI NDANI YA JESHI LA POLISI, MEI 2017

[2] Francis K. Kiwanga, Legal and Human Rights Center- Police Accountability in Tanzania

[3] Kamati ya Kudumu ya Bunge ya hesabu za Serikali-PAC, taarifa ya shughuli za kamati kwa  mwaka 2018, ilitolewa febeuari, 2019

[4] https://www.corrections.vic.gov.au/release/transitional-programs

[5] https://www.trademarkea.com/news/east-africas-diaspora-remittances-hit-17b/

Share Button