KAULI YA BAVICHA KULAANI UDHALILISHAJI ULIOFANYWA NA SPIKA DHIDI YA MBUNGE WA KIBAMBA NA NAIBU KATIBU MKUU WA CHAMA MHE. JOHN JOHN MNYIKA

BARAZA LA VIJANA WA CHADEMA (BAVICHA)
KAULI YA BAVICHA KULAANI UDHALILISHAJI ULIOFANYWA NA SPIKA DHIDI YA MBUNGE WA KIBAMBA NA NAIBU KATIBU MKUU WA CHAMA MHE. JOHN JOHN MNYIKA
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwanza tunawashukuru kwa kuitikia wito wa BAVICHA na kufika kutuunganisha na watanzania kuhusu masuala kadhaa ya kitaifa yanayoendelea nchini kwa sasa.
Ndugu Waandishi wa Habari,
BAVICHA linaungana na Viongozi, wanachama na watanzania wote katika msiba mzito uliotupata wa kuondokewa na Muasisi wa Chama chetu Mhe. Philemon Ndesamburo, BAVICHA tunasikitika zaidi kwani, mzee huyu alikuwa mlezi wa BAVICHA kitaifa, alikuwa nguzo kubwa ya Chama chetu, lakini kikubwa,  siku ya leo alikuwa aende Mkoani Tabora kuwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya vijana wa Chadema wa Vyuo Vikuu (CHASO).
Ndugu Waandishi wa Habari,
Jana Ijumaa, tarehe 02 mwezi June 2017 katika kikao cha Bunge la kumi na moja, sote tulishuhudia udhalilishaji mkubwa uliofanywa na Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama ambaye ni mbunge wa Kibamba Mhe. John John Mnyika baada ya Mhe. Mnyika kuomba utaratibu na kumtaka Spika kumuagiza Mbunge wa Mtera Mhe. Livingstone Lusinde kufuta kauli yake dhidi ya Upinzani kwamba UPINZANI NI WEZI, lakini pia wakati Mhe. Mnyika akiomba utaratibu huo, kuna mbunge mmoja wa CCM aliwasha maiki (bila ruhusa) na kutamka "Mnyika ni Mwizi, Mnyika ni Mwizi", jambo lililosababisha Mhe. Mnyika kulazimika kumtaka Spika amwagize Mbunge huyo kuthibitisha kauli hiyo au kuifuta.

 

Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika hali ya kushangaza, Spika alidai kwamba hajasikia kauli hizo zote mbili na kutaka Bunge liendelee, jambo hili lilimlazimu Mhe. Mnyika kuendelea kuomba utaratibu na hapo ndipo Spika wa Bunge alipomtaka atoke nje, na wakati akitoka nje, Spika aliita Askari wa Bunge na kuwaagiza kumtoa nje Mhe. Mnyika, na katika kutekeleza agizo hilo, askari huyo anaoneka akimsukasuka na kisha kumsukuma nje Mhe. Mnyika.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Sisi Vijana wa CHADEMA kwanza tumesikitishwa na tabia hii ya aibu na isiyo ya kiuongozi aliyoinyesha Spika wa Bunge ya kujifanya hakusikia kauli za Lusinde na ile ya mbunge wa CCM dhidi ya Upinzani na Mhe. Mnyika. Tunamtaka Spika afuatilie HANSARD za Bunge na asikilize kipande hicho wakati Lusinde anachangia na aujulishe uuma wa Watanzania kama kweli hakusikia au ni upuuzi wa vionzgozi wa CCM kuendeleza upendeleo kwa wabunge wa CCM na uonevu dhidi ya wabunge wa Upinzani.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Pili, BAVICHA linaalani vikali kauli ya Mbunge wa Mtera Bw. Lusinde, kwamba Upinzani ni Wezi, na tunapenda kuwakumbusha watanzania kuwa wizi wote unaofanyika ndani ya nchi hii, unafanywa ama na wanachama/viongozi wa CCM chini ya serikali ya CCM, mfano katika sakata la Mchanga wa madini ulioundiwa tume mbili, tunaona kwamba kilichozuiwa bandarini ni MCHANGA wakati dhahabu na madini mengine yanaendelea kusafirishwa nje, na kwa mujibu wa ripoti ya tume, huu ni wizi na unaendelea kufanyika chini ya Serikali ya CCM.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Tatu, BAVICHA linalaani vikali kitendo cha askari wa bunge kumsukuma Mhe. Mbunge John Mnyika ilihali Mhe. Mnyika hakukaidi amri ya Spika katika jambo hili, cha ajabu askari wa Bunge walitumia nguvu iliyopita kiasi. BAVICHA linalaani kitendo cha Spika kuwaagiza Askari kumtoa nje kwa nguvu Mhe. Mnyika hata pale ambapo Mhe. Mnyika alikuwa anajiandaa kutoka ndani ya Ukumbi wa Bunge kistaarabu kwa hadhi yake kama Mbunge.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Ni vyema viongozi wa Serikali wanaotokana na CCM wakatambua kuwa nchi hii haiongozwi kwa matakwa yao bali kwa misingi ya Katiba na Sheria zilizopo katika taratibu zetu za kila siku katika utawala wa nchi, hivyo waache kutekeleza majukumu na wajibu wao kwa misingi ya upendeleo na uonevu kama ilivyo sasa.
UTEKAJI, UBAMBIKAJI KESI NA UVUNJAJI WA HAKI BINADAMU
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa kipindi kirefu kumekuwa na tabia na desturi ya vikundi vya watu waovu "wasiojulikana" kuvunja sheria kwa kutishia, kuteka na hata kuua raia, hususani vijana ambao hawana hatia.
Wote tunajua, hadi sasa ni mwezi wa nane ndugu yetu na rafiki yetu Benard Sanane hajulikani alipo, na Jeshi la Polisi liko kimya bila kutoa taarifa yoyote ya wapi aliko Ben Sanane na kwa nini awe huko. Mnakumbuka majibu ya Waziri Mkuu alipoulizwa kuhusu alipo Ben, alitafuna maneno, hali iliyoonyesha anajua nini kinaendelea kuhusu Ben. BAVICHA tunamtaka IGP mpya Simon Sirro kutoa kauli ya Jeshi la polisi kuhusu wapi aliko Ben hasa kwa kuwa aliahidi kuwa vitendo vya kihalifu vitakoma, na tunamtaka aanze na hili la Ben.
BAVICHA pia tunamtaka IGP Sirro kubadili mfumo wa Utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwani kwa sasa jeshi la Polisi limekuwa kama Instrument ya uonevu dhidi ya raia, kuminya uhuru wa maoni na kukamata na kubambikia kesi raia wasiokuwa na hatia.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Hivi tunavyozungumza, yupo kijana mmoja ambaye ni Katibu Mkuu wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, (Tanzania Students’ Network Project – TSNP) Bw. Alphonce Lusako alikuwa na kongamano la kuzindua Kitabu chake cha HAKI ZA WANAFUNZI VYUONI, lakini cha ajabu jeshi la Polisi limekwenda mahali alipopaswa kuzindulia kitabu hicho (Blue Pearl Hotel) na kuzuia shughuli hiyo, na pia kukamata baadhi ya washiriki wa kongamano hili kwa madai kwamba kutatokea uchochezi.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Swali la kujiuliza hapa, hivi polisi ni watabiri? au ni wapiga ramli? na utabiri na ramli zao zipo kwenye masuala yanayohusu haki za raia  wanaharakati tu? Kwa nini ramli na Utabiri Huu usijielekeze kwenye kukamata vikundi vinavyoteka na kunyanyasa vijana? kwa nini zisielekezwe kule Kibiti na Mkuranga ambapo raia wanaishi kwa hofu ya kuuawa na watu wasiojulikana?
BAVICHA tunamtaka IGP Sirro kukomesha mara moja jambo hili kwani linaondoa ushirikishwaji wa wananchi katika kulisaidia Jeshi kwa masuala ya kiusalama, na pia kuwajengea hofu wananchi na kuliogopa jeshi hili, na hivyo hata kujenga uhasama baina ya raia na askari polisi, jambo ambalo ni la hatari kwa mustakabali wa Nchi yetu.
Ndugu Waandishi wa Habari,
BAVICHA linaunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa Chama na Kiongozi wa Upinzani Bungeni Mhe. Freeman Mbowe kuhusu suala la Umakinikia wa Mchanga, kwamba suala sio kukamata na kuzuia mchanga kusafirishwa nje ya nchi, bali suala ni mikataba mibovu ambayo imesainiwa chini ya Serikali ya CCM na kwa hiyo tunamtaka Rais Magufuli badala ya kufanya siasa nyepesi ya kuwalaghai watanzania kuwa wameibiwa madini ya thamani kubwa, anapaswa kuiweka mikataba hiyo hadharani na ipitiwe ikiwezekana ifanyiwe marekebisho ya dhati ili kutuwezesha kama taifa kunufaika na rasilimali zetu.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Ikumbukwe kwamba suala la rasilimali za watanzania kutumika vibaya haliko kwenye madini tu, bali hata kwenye vitalu vya uwindaji wa wanyampori, vitalu vya uchimbaji wa gesi, misitu, ardhi nk kumekuwa na mikataba mibovu ambayo haiakisi hali halisi ya uhitaji wetu wa kuimarisha uchumi wa nchi yetu kwa kutumia rasilimali hizo.
BAVICHA tunamtaka Rais, kama kweli yupo makini, basi jambo la msingi la kufanya ni kuiweka hadharani mikataba yote ya madini, gesi, uwindaji wa wanyamapori nk ili tujue nini kinachojiri katika matumizi endelevu ya rasilimali za taifa letu.
Mwisho, tunawatakia waislamu wote Ramadhan Kareem, na kuzitaka mamlaka zinazohusika kuhakikisha zinasimamia bei za vyakula ili kutowaathiri wakati huu wanapotimiza nguzo muhimu katika imani ya dini ya Kiislamu.
Imetolewa na,
Patrobas Katambi
Mwenyekiti wa BAVICHA TAIFA
Leo Jumamosi tarehe 03.06.2017
Dar es Salaam.

Share Button
Layout Settings