RAIS JOHN MAGUFULI AJITOKEZE HADHARANI KUZUNGUMZIA AIBU HII

BARAZA LA VIJANA WA CHADEMA (BAVICHA)
RAIS JOHN MAGUFULI AJITOKEZE HADHARANI KUZUNGUMZIA AIBU HII
Ndugu wanahabari
Mtakumbuka kuwa Chama kupitia uongozi wa juu, Ijumaa iliyopita, Agosti 21, mwaka huu kilitoa tamko kwa umma kupitia mkutano na waandishi wa habari kuhusu “Gharama za Matendo ya Rais Magufuli zimeanza kufichuka; Bombardier imekamatwa Canada,” ambapo Chama kilieleza kwa kina na ushahidi usio na shaka namna ambavyo  taifa linaanza kulipa gharama za matendo ya ukiukwaji wa misingi ya demokrasia na utawala bora katika nchi yetu.
Kupitia taarifa hiyo, chama kilizungumzia kashfa kubwa ya kukamatwa na kuzuiliwa kwa ndege ya Serikali aina ya Bombardier Q400 kutokana na deni la shilingi bilioni 87 ambazo Tanzania inadaiwa kutokana na hukumu mbili za Mahakama ya Usuluhishi zilizotolewa dhidi ya nchi yetu mwaka 2009 na 2010, yakiwa ni matokeo ya maamuzi ya Rais John Magufuli wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi, kuvunja mkataba wa kandarasi ya ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill-Bagamoyo, kati ya Serikali na Kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd.
Kwa uhakika hii ni sehemu ndogo tu ya athari HASI za matendo ya Serikali ya CCM, chini ya Rais John Magufuli, hasa yanayohusu ukiukwaji wa Katiba ya Nchi, uvunjwaji wa sheria na kutozingatiwa kwa misingi ya utawala bora katika uendeshaji wa nchi yetu. Haihitaji kuwa mtabiri kujua kuwa huko tunakoenda, tukiendelea na utaratibu huu unaofanywa na Serikali hii, athari nyingi hasi zitaendelea kujitokeza na kufichuka.
Kutokana na uzito wa kashfa hiyo iliyoibuliwa na chama na kusemwa kwa ushahidi usiokuwa na shaka, tulitarajia kuwa Serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli, ilipaswa kuwa imejitokeza hadharani kujibu maswali ya msingi ambayo yalihojiwa katika tamko hilo.
Lakini katika hali ambayo bila shaka inaonesha kuwa serikali imepata kigugumizi kwa sababu hoja zilizozungumzwa ni ukweli mtupu, hadi leo hii tunapozungumza hapa zikiwa zimetimu siku nne tangu chama kilipoibua ufisadi huo, Serikali haijajitokeza hadharani kujibu hoja kwa hoja. Badala yake juzi Jumamosi, Agosti 19, kupitia Msemaji wa Serikali, Serikali ilitoa viroja badala ya hoja.
Kwa sababu masuala yaliyoibuliwa ni mazito yakiwa na athari hasi kwa nchi yetu na kututia AIBU KUBWA KAMA TAIFA, huku yakimgusa moja kwa moja Rais Magufuli na serikali yake, sisi vijana wa BAVICHA tumeona tutumie fursa hii kutoa wito kwa Rais Magufuli kujitokeza hadharani kujibu hoja kuhusu kashfa hiyo, vinginevyo imani ya wananchi kwakena Serikali ya CCM,  itazidi kuporomoka.  
Tunapenda kumkumbusha Rais Magufuli kuwa wananchi wanataka kusikia majibu yake kuhusu kuzuiliwa kwa ndege ya Bombardier Q400 iliyokuwa inatazamiwa kukabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania mwishoni mwa Julai 2017, kutoka kwa kampuni ya utengenezaji wa ndege hizo ya nchini Canada.
Tunamkumbusha Rais kuwa hadi leo siku ya nne, si yeye wala serikali yake, wamejitokeza hadharani kujibu hoja zilizotolewa na chama, hivyo tunaitaka Serikali ijibu maswali yafuatayo;
Kwanini Rais Magufuli wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi, alivunja mkataba wa Kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd? Kitendo ambacho kimesababisha nchi yetu kuingizwa hasara ya mabilioni ya shilingi?
Kwanini deni la Stirling Civil Engineering Ltd halikulipwa mara baada ya mahakama ya usuluhishi kutoa tuzo ya dola za Marekani milioni 25, kitendo ambacho kimesababisha deni hilo sasa kufikia dola milioni 38.711?
Kwanini serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kikanda inapambana kulificha suala la kukamatwa kwa ndege hiyo ili liwe siri? Nani anayelindwa katika kashfa hiyo na kwamba ikijulikana hadharani atakuwa shakani?
Wananchi wanataka kujua katika kashfa hiyo, nani atawajibika kijinai kwa kuisababishia taifa letu hasara ya shilingi bilioni 87 ili serikali hii ambayo imekuwa ikigamba kuwa inatumbua majipu basi itumbue jipu hili ambalo liko mshipa wa moyo?
Ni muhimu Rais Magufuli ajitokeze awaambie Watanzania kauli ya serikali inayolingana na uzito wa kashfa hii ambayo imesababisha ndege yetu kukamatwa nchini Canada na sasa mali zetu zilizoko katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Uingereza na Uganda pia ziko shakani katika hatari ya kukamatwa kutokana na tuzo hiyo.
Ni vyema ikumbukwe hapa hatuzungumzii mali binafsi za viongozi wa serikali hii, hizi ni mali za taifa hili, hivyo Watanzania hatuwezi kukubali kubebeshwa aibu kwa sababu ya makosa ya kukurupuka yanayofanywa na viongozi wasiojua maana ya dhamana kubwa wanazozishikilia kwa niaba ya wananchi.

 

Imetolewa Leo Na:

…………………………..
BAVICHA Taifa.
 tarehe 24/08/2017

Share Button
Layout Settings