MSIMAMO WA BAVICHA JUU YA WANAFUNZI WA LIOSIMAMISHWA CHUO KIKUU CHA DODOMA


MSIMAMO WA BAVICHA JUU YA WANAFUNZI WA LIOSIMAMISHWA CHUO KIKUU CHA DODOMA
UTANGULIZI:
Ndugu Waandishi wa habari,
Mwaka 2014 Serikali kupitia Waziri wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  wa wakati huo, Dr. Shukuru Kawambwa ilitangaza kuanzishwa kwa Program Maalum ya Stashahada ya Elimu (Special Diploma in Education), na ilitakiwa ihudhuriwe na kusomwa na wanafunzi waliomaliza kidato cha nne ili waende wakawe walimu wa masomo ya Sayansi katika shule za Sekondari.

Na Wizara ya Elimu ilielekeza kwamba, Diploma hii itakuwa ya muda wa Miaka mitatu na itachukuliwa katika chuo kikuu cha Dodoma na wanafunzi watachaguliwa na kupelekwa katika chuo hicho kwa utaratibu utakaowekwa na Serikali

Serikali kupitia uongozi wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) walikubaliana na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma kufundisha vijana hawa wa Stashahda ya Ualimu, na kwamba wangelipwa shilingi milioni moja (1,000,000) kwa kila somo kwa Semester.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa muda wa wiki tatu au nne zilizopita, wahadhiri wa UDOM wamekuwa na mgomo wa kutokufundisha wanafunzi hawa wa Diploma maalum kwa sababu hawajalipwa fedha zao kwa mujibu wa makubaliano yao.

Ndugu waandishi wa Habari, Mgomo huu wa wahadhiri uliwasababisha wanafunzi hawa takribani 7108 na wao kuanza maandalizi ya kugoma kuingia darasai bila kufundishwa.
Uongozi wa Chuo ulipokea agizo la Waziri wa elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profes Joyce Ndalichako la kuwaondoa Chuoni hapo wanafunzi hawa, na bila kujiuliza, Uongozi wa Chuo uliwatangazia wanafunzi hawa kuwa waondoke Mara moja Chuoni hapo na kuwapa  saa 24 kuwa wameshaondoka tangu siku ya Jumapili tarehe 29.05.2016.

BAVICHA linapenda kuhoji mambo yafuatayo;

 • Hivi watoto hawa walijipeleka wenyewe huko UDOM?
 • Hivi watoto hawa walituma maombi ya kusomeshwa UDOM?
 • Hivi watoto hawa waliwaamuru wahadhiri wao kugoma?
 • Hivi kuna kosa gani kubwa la kuitisha magari ya polisi na maderaya ya maji ya kuwasha kwa watoto wenye kalamu na madaftari?
 • Hivi watoto hawa walikuwa na kosa gani kubwa la kupewa saa 24 wawe wameshapotea katika sura ya UDOM?
 • Hivi hapa nani wa kuwajibika kati ya wanafunzi, Chuo Kikuu cha Dodoma na Wizara ya Elimu?
 • Baraza la vijana la CHADEMA Taifa (BAVICHA), linalaani vikali maamuzi yaliyofanywa na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuwaamuru wanafunzi wa mafunzo maalumu ya diploma ya ualimu (special diploma in Education) waondoke mazingira ya chuo bila ya mpangilio na utaratibu unaofaa. Tunasema huu ni unyanyasaji na udhalilishaji kwa watoto hawa ambao hawakuomba wala hawakujipeleka UDOM.
 • Sote tunatambua asilimia kubwa ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Serikali (moja wapo UDOM), kwa asilimia kubwa inabeba watoto wanaotoka katika mazingira ya familia zenye maisha ya kawaida Hivyo kuwaamuru ,uondoka Chuoni na deadline ya muda huku wakiwa hawana makossa, ni kuwaonea kabisa.

Itambulike kuwa  wanafunzi hawa waliokuwa wanasoma kozi maalum si kwamba hawakidhi vigezo bali ni urasimu unaotendeka dhidi yao kupitia utawala wa chuo.
BAVICHA tunaitaka serikali ya Dr Magufuli itambue kuwa madai ya waalimu wa Chuo Kikuu cha DODOMA ni ya msingi. Hivyo waalimu walipwe madai yao ili wanafunzi warejee chuoni na waendelee kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu badala ya Prof Ndalichako kujitoa ufahamu na kuuleza umma wa watanzania kuwa madai ya wahadhiri wa UDOM sio ya msingi, na kama madai yao sio ya msingi kwa nini wasifukuzwe wao, na badala yake wamefukuzwa watoto wasio na hatia?
Kwa kuwa madai ya waalimu  ni ya msingi na ni madai ya muda mrefu lakini uongozi wa chuo wamekuwa wakipuuza na kudharau. Tunaitaka Serikali ithibitishe usimamizi wa sera yao ya kipaumbele cha elimu waliyoahidi kwa wananchi kwa kuhakikisha wanafunzi wanarudi chuoni na kuendelea na masomo.

 • BAVICHA tunaitaka ofisi ya Mkaguzi wa hesabu za Serikali achunguze matumizi ya pesa ndani ya Chuo Kikuu cha Dodoma, kwa kuwa inaonekana kuna ubadhilifu unaojitokeza na kupelekea kuwa na migomo ya mara kwa mara kwa wahadhiri na kupelekea wanafunzi kuathirika kimasomo.
 • BAVICHA tumeshangazwa na kusikitishwa na kauli iliyotolewa na Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoona tatizo la UDOM kama ni la dharura, na linapaswa kujadiliwa Bungeni ili kutoa fursa kwa watoto hawa kuweza kunusuriwa na hatari mbalimbali, hasa ikizingatiwa kuwa Dr. Tulia Ackson ni mama, hivyo alichokifanya ni kitendo kisichokubalika, na ni kukosa huruma ya MZAZI, na hivyo kuweka walakini wa uhalali wake wa kuwa kiongozi wa mhimili wa Bunge na kwa kauli hii tunamtaka Dr. Tulia kujitafakari kama anastahili kuendelea kuwa Naibu spika wa Bunge letu.
 • Maamuzi haya ya kuwafukuza watoto hawa kwa njia za kikatili namna hii, ni ushahidi tosha kwamba badala ya wao kuonekana kuwa hazina ya taifa, na wao wamegeuzwa kuwa “JIPU” na kwa hiyo wametumbuliwa kama ilivyo dira ya serikali ya Magufuli ya utumbuaji wa majipu bila kuwa na uhakika kama yameisha kuwa tayari kutumbuliwa au lah!
 • BAVICHA linaweka wazi kwa watanzania kuwa, Serikali yoyote itokanayo na CCM, ni serikali dhaifu, isiyojipanga na isiyokuwa na dira wala malengo ya kutekelezeka kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake, hivyo ni vyema sasa, kuanza kujiandaa kuiondoa madarakani, kwani hakuna kipya ambacho anakuja nacho mtumbua majipu.

Hii inadhihirisha kukinzana kwa kauli iliyohaidiwa na Mh. Rais alipokuwa anagombea urais mwaka 2015 kwa kusema“elimu ndio kipaumbele chake cha kwanza”. Na serikali haikujipanga na agenda ya elimu na haipo makini katika kusimamia haki na mahitaji ya elimu katika Idara zake kiujumla.
HITIMISHO:
BAVICHA tunasikitishwa na kitendo hiki kilichotokea UDOM. Tunatambua Serikali ya awamu ya kwanza ilithamini elimu na kuwajali wasomi na ndio mana leo wapo wazee ambao wamekuwa sehemu ya mafanikio na matunda ya Serikali ya awamu ya kwanza na ndio mana wamefika walipofika. Tunasikitisha serikali ya awamu ya nne na tano imeshindwa kusimamia taaluma ya elimu imesaliti misingi iliyoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa katika suala zima la elimu.
BAVICHA linaitaka serikali kupitia kwa waziri wa Elimu kuulea umma wa watanzania, kama suala ni vigezo vya kudahiliwa kwa wanafunzi hawa, nani wa kulaumiwa? Na ikumbukwe kuwa mpaka sasa wanafunzi hawa walikuwa wanapewa mkopo kutoka bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), sasa je, nani atawajibika kulipa hasara kubwa iliyokwisha lipata Taifa kwa kuwalipa mabilioni ya shilingi watato hawa na kisha kuwafukuza?
BAVICHA tunaikumbusha Serikali ili Taifa lolote liweze kuendelea inapaswa wasomi na waalimu wake wa ndani ya nchi waheshimike na wathaminike.
Imetolewa na  Julius Gabriel Mwita ,
Katibu Mkuu wa BAVICHA Taifa.
                                                                                                                  

                                                       
                                                                                   

Share Button
Layout Settings