TAARIFA FUPI KWA WABUNGE KUHUSU HALI YA TAIFA KWA KIPINDI CHA JULAI HADI OCTOBA 2016.

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA FUPI KWA WABUNGE KUHUSU HALI YA TAIFA KWA  KIPINDI CHA JULAI HADI OCTOBA 2016.

  1. UTANGULIZI.

Tathimini hii imefanyika katika kipindi ambacho serikali ya awamu ya tano imeanza utekelezaji wa bajeti yake ya kwanza tangu ilipoingia madarakani .
Hii ndio hali halisi ya mwenendo wa serikali hii katika kipindi cha miezi sita ya kwanza tangu ilipoingia madarakani.
2.0 HALI YA UCHUMI WA TAIFA
Kwa mujibu wa Taarifa Kuhusu Hali ya Uchumi wa Tanzania  iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania Septemba,2016 imeonyesha kuwa hali ya uchumi wa taifa inaenda mwendo wa kusuasua karibia katika sekta zote  hapa nchini.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kukukua kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka 2015
Kuporomoka huku hakujawahi kufikiwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika robo ya kwanza tangu mwaka 2011 ukuaji wa pato la Taifa ulikuwa kama inavyoonekana kwenye mabano , 2011 (7.9), 2012 (7.1),2013(6.3),2014 (8.2) na 2015 (5.7)
Kwa mujibu wa ripoti hiyo shughuli zilizochangia ukuaji huu wa uchumi kwa kiasi kikubwa ni pamoja na kilimo (asilimia 11.7), biashara (asilimia 10.6), uchukuzi (asilimia 10.1), sekta ya fedha (asilimia 10.1) na mawasiliano (asilimia 10.0). Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu zaidi katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ni sekta ya fedha (asilimia 13.5), mawasiliano (asilimia 13.4), na utawala wa umma (asilimia 10.2)
Pamoja na taarifa hiyo kuonyesha kuwa uchumi unaimarika lakini wakati huohuo taarifa hiyo imeonyesha kuyumba kwa uchumi katika sekta zifuatazo;

  1. Mikopo itolewayo na mabenki ya biashara kwenye sekta binafsi, imeendelea kushuka  katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 na kuwa Shilingi bilioni 1,167.2, ikilinganishwa  na ongezeko la Shilingi bilioni 1,577.5 la mwaka 2015 katika kipindi kama hicho.Hii maana yake ni kuwasekta binafsi imenyanganywa au imekosa takribani shilingi Bilioni 410.3 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016.Hali hii imepelekea mzunguko wa sarafu na noti mikononi mwa watu kushuka kutoka asilimia 18.8 Disemba 2015 na kufikia asilimia 6.7 Mwezi Julai ,2016.
  2. Amana za wateja katika mabenki zilipungua kutoka shilingi trilioni 20.52 mwezi Desemba 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 20.24 mwezi June 2016.
  3. Katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016, nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje (current account deficit) ilipungua kwa asilimia 61.7 na kufikia nakisi ya dola za Kimarekani milioni 970.4, kutoka nakisi ya dola za Kimarekani milioni 2,532.5 mwaka 2015. Kupungua huko kulitokana zaidi na ongezeko la thamani ya bidhaa za viwandani, mapato yatokanayo na utalii na huduma za usafirishaji nje ya nchi, pamoja na kupungua kwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za mitaji, na bidhaa za matumizi ya kawaida katika kipindi hiki
  4. Hadi mwezi June 2016, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Kimarekani milioni 3,870.3 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4 tu ,hali ambayo hairidhishi hata kidogo kwa taifa ambalo halijatoka vitani nah ii imeendelea kusababisha kushuka kwa dhamani ya shilingi nchini
  5. Deni la Taifa limeendelea kuongezeka na kufikia dola za Kimarekani milioni 20,851 mwishoni mwa mwezi Juni 2016, kutoka dola za Kimarekani milioni 19,861 mwezi Desemba 2015. Deni la nje liliongezeka kwa asilimia 2.6 na kufikia dola za Kimarekani milioni 16,281 mwezi Juni 2016 (sawa na asilimia 77.8 ya deni la taifa), kutoka dola za Kimarekani milioni 15,864 mwezi Desemba 2015. Hii ilitokana na kuongezeka kwa mikopo mipya pamoja na malimbikizo ya malipo ya madeni.

Deni la ndani liliongezeka kufikia shilingi bilioni 10,038.4 mwishoni mwa mwezi Juni 2016 kutoka shilingi bilioni 8,597.0 mwezi Desemba 2015. Ongezeko hilo lilitokana na Serikali kukopa kupitia dhamana na hati fungani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, ikichangiwa pia na kupungua kwa misaada na mikopo kutoka nje.

  1. Serikali ilikuwa inakopa ili kulipia madeni ya nyuma pamoja na riba na hii inaonekana kwenye jedwali ambalo limeambatanishwa , juu ya makusanyo ya serikali kwa miezi sita pamoja na matumizi yake .

Maeneo mengine ambayo yameathirika kutokana na maamuzi ya serikali ya awamu ya tano na kusababisha kuyumba kwa uchumi wa taifa ni pamoja na yafuatayo;

  1. Katika kipindi hiki serikali imesitisha ajira kwa kigezo kuwa inafanya uhakiki wa watumishi wake ,jambo hili limepelekea kuyumba kwa uchumi kwa baadhi ya familia ambazo zina watu wenye sifa ya kuajiriwa katika sekta ya umma kama vile waalimu,manesi na madaktari. Kusimamishwa huku kwa ajira kumewafanya nguvu kazi iliyokuwa na uwezowa kuzalisha kuishi kama ombaomba na hivyo kuporomosha.
  2. Serikali hii imewaumiza sana wafanyabiashara wakubwa na wa kati kwa kukamata mali zao kama Rais alivyofanya kwa kukamata mali za mfanyibiashara kwa kitanzania Salim Baharesa ,sukari yake ilishikiliwa na serikali bila kutoa sababu zozote zile na Rais aliamua kuachia sukari hiyo bila kutoa sababu zozote za maana kwa umma . Hali iko hivyo kwa wafanyabiashara wengi ambao akaunti zao Benki zimeshikiliwa na Serikali bila kuelezwa sababu, jambo linalopelekea kuporomoka kwa uchumi kwa kasi katika taifa letu.
  3. Sekta ya kilimo imeathirika sana hasa kutokana na uamuzi wa Benki kuu kuzuia baadhi ya Benki kukopesha wakulima kama ilivyofanya kwa Maendeleo Benki kwa hoja kuwa kama wakiendelea kukopesha miradi ya kilimo hakuna uhakika wa mikopo hiyo kurejeshwa.
  4. Sekta ya Hoteli na utalii iko ICU na hasa kutokana na uamuzi wa serikali kuanzisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT ) kwenye huduma zote za utalii jambo ambalo limepelekea kushuka kwa idadi ya watalii wanaotembelea nchi yetu na hivyo kufanya hoteli zilizokuwa zinafanya biashara ya utalii pamoja na makampuni yaliyolkuwa yakijihusisha na biashara ya utalii kwa ujumla.
  5. Serikali za mitaa zimeathirika sana kutokana na uamuzi wa serikali kuamua kukusanya kodi ya Majengo kupitia TRA badala ya Halimashauri ambazo awali zilikuwa zikifanya jukumu hilo, na hasa ikizingatiwa kuwa uamuzi huu ulifanyika baada ya bajeti za Halimashauri kupitishwa na TAMISEMI na kuwa miongoni mwa vyanzo vya mapato ya Halimashauri husika.

  1. HALI YA AFYA NCHINI

Tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani sekta ya afya imekuwa ikizorota kwa kasi kubwa kutokana na serikali kutokuiona sekta hii kama kipaumbele chake muhimu.
Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia ukosefu mkubwa wa madawa, chanjo na vifaa tiba katika Hospitali zetu mbalimbali hapa nchini.
Hali hii imepelekea wananchi kupoteza maisha kutokana na kukosekana kwa dawa na kundi la watoto limeathirika sana kutokana na kukosekana kwa chanjo kwenye hospitali zetu.
Kamati Kuu ijadili hali hii na kutoa ushaurikwa serikali hii ya awamu ya tano nini wafanye ili kuweza kulinusuru taifa na hali hii.

Wakati hospitali hazina dawa serikali mwezi septemba ilitumia kiasi cha shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kupunguza deni hospitali ya Apolo India ambako tunadaiwa kiasi cha shilingi Bilioni 31.320.

  1. HALI YA ELIMU NCHINI

 

3.1  Elimu Bure
Serikali ya awamu ya tano iliamua kudandia hoja ya elimu bure bila kuwa na maadalizi ya kutosha na ya kuweza kutekeleza ajenda hiyo na sasa imesababisha madhara makubwa sana kwenye sekta nzima ya elimu nchini.
Hali katika shule za umma imekuwa mbaya sana kutokana na serikali kushindwa kupeleka fedha za uendeshaji kwenye shule hizo na hivyo kufanya suala zima la elimu ya msingi na Sekondari kuwa katika hali mbaya na huenda baada ya muda mfupi ujao shule hizi zinaweza kuanguka kutokana na kukosekana kwa fedha za uendeshaji.
Serikali badala ya kuweka utaratibu mzuri wa kuweza kuendesha shule hizi wameishia kutoa waraka kwa viongozi mbalimbali na kuwataka watekeleze, waraka huo umeambatanishwa .

Kwa mfano mwezi Septemba 2016 serikali ilitenga fedha  kwa ajili ya kugharimia elimu bure kiasi cha shilingi 18,777,000,000 ambapo kiasi cha shilingi 15,714,000,000 kinatakiwa kupelekwa Halimashauri na shilingi 3,063,000,000 zinatakiwa kupelekwa NECTA kwa ajili ya fidia ya mitihani.
Kwa vyovyote vile fedha hizi ni kidogo  sana kwa ajili ya kuendesha shule za msingi na sekondari zote zilizopo nchini .
Kwa mujibu wa tovuti kuu ya takwimu huria ya serikali (www.pendadata.go.tz) takwimu za mwezi machi 2016 zinaonyesha kuwa serikali ina jumla ya shule za msingi 16,084 zenye jumla ya wanafunzi 8,340,128 kwa nchi nzima .
Kwa takwimu hizi za idadi ya wanafunzi maana yake ni kuwa serikali inatenga kiasi cha shilingi 1,884 kwa mwezi kwa kila mwanafunzi wa shule ya Msingi .Ikumbukwe kuwa fedha hizo zinajumuisha pia wanafunzi ambao wanasoma kwenye Sekondari za serikali, hivyo kiasi ni kidogo zaidi ya hizo

3.2  Mikopo Elimu ya Juu
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari na vyanzo vingine, Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) imeweza kudahili takriban wanafunzi wapya 58,000 kwa ajili ya elimu ya juu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa mwaka huu wa masomo.
Kwa mujibu wa Gazeti la The Guardian la Oktoba 18, mwaka huu, Serikali ya CCM, chini ya Rais Magufuli imesema itawakopesha wanafunzi wapatao 24,000 idadi ambayo haifiki hata nusu ya wanafunzi wote waliodahiliwa na TCU.
Hii maana yake ni sawa na kusema kuwa Serikali ya awamu ya tano imeamua kuwanyima mikopo wanafunzi ambao wanaenda kujiunga na Vyuo Vikuu Nchini katika mwaka huu wa masomo na hata kuwapunguzia mikopo wale ambao walikuwa wanaendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini.
Wapo wanafunzi ambao wana sifa za kujiunga na vyuo vikuu ambao watakosa fursa hiyo kwa sababu serikali imeamua kuwanyima fursa hiyo.

Aidha ikumbukwe kuwa serikali inadaiwa na vyuo mbalimbali nchini kiasi cha shilingi bilioni 60.798 ambazo ni fedha za ada za wanafunzi walizokopeshwa lakini serikali haikupeleka mkopo huo kwenye vyuo husika kwa mwaka wa masomo 2015/16.Jambo hili linahitaji kufuatiliwa kwa kina kwani likiachwa kama lilivyo litasababisha vyuo kushindwa kujiendesha kwani na kugharimia gharama nyingine za uendeshaji.

Hii ni serikali ambayo iko tayari kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya kupambana na UKUTA lakini haioni haja ya kuwekeza kwenye elimu ya vijana wake
Serikali mwezi Septemba ilipitisha kutumia shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuzima mwenge,shilingi 2,199,740,340 kwa ajili ya kuwalipa viongozi ambao “walitumbuliwa” kikiwemo kiasi cha shilingi 196,842,000 kama posho ya usumbufu. Serikali ilitumia kiasi cha shilingi 251 milioni kwa ajili ya kugharimia mkutano wa dharura wa siku moja wa wakuu wa nchi za EAC.

  1. MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI

Serikali imeamua kuwasilisha Bungeni muswada wa sheria ya huduma za habari ambao pamoja na mambo mengine umeweka mambo ya hatari kama yakiachwa na kupitishwa kama yalivyo utakuwa ndio kilele cha Udikteta ambao tunaupinga , hii ni kutokana na mambo yaliyomo kwenye mswada huo, na baadhi ni kama yafuatayo;

  1. Uthibiti na usimamizi wa mitandao ya kijamii –hii ni mitandao kama Jamii Forums ,Bloggers nk kuwa chini ya udhibiti wa serikali na hili lipo kwenye kifungu cha tatu –Tafsiri , ambacho kimeweka mitandao ya kijamii kama sehemu ya vyombo vya habari …….Chombo cha habari za Kielektroniki…….imetafsriwa kama “aina ya mawasilisho ya maudhui kwa umma kwa njia ya …………..kwa njia nyingine yeyote ya kielektroniki na vifaa ikijumuisha mitandao ya kijamii na njia nyingine zinazoendana na hizo”
  2. Mitandao ya kijamii imewekewa tafsiri kuwa ni …….’mawasiliano miongoni mwa watu kwa njia ya mtandao ambayo yameanzishwa na watu hao kwa ajili ya kubadilisha habari na taarifa katika mitandao na majukwaa mengine ya teknolojia ya kisasa’. Sheria hii inaenda kusimamia hata mawasiliano kwa njia ya Whatssap , Instagramu au facebook na kila mmoja atatakiwa kuandika kwa mujibu wa sheria hii.
  3. Kwa mujibu wa kifungu cha 7 (b) vyombo binafsi vya habari vitakuwa vinaelekezwa na serikali ni aina gani ya habari wanatakiwa kuitangaza kwa umma , kinasema “kutangaza au kuchapisha habari au masuala ambayo ni muhimu kwa taifa kwa kadri Serikali itakavyoelekeza” Jambo hili ni la hatari sana kama likipitishwa lilivyo, si ajabu katika kanuni waziri akaelekeza kuwa TV binafsi zijiunge na TBC wakati wa taarifa za habari na taifa likalishwa propaganda za aina moja .
  4. Sheria haijaweka tafsiri ya maana ya masuala muhimu kwa taifa jambo ambalo litamfanya waziri aweze kuelekeza kwa utashi wake binafsi bila kufuata sheria .
  5. Sheria imepiga marufuku kuchapisha ama kutangaza taarifa za Baraza la Mawaziri , hata kama mtu akipata nyaraka inayoonyesha uamuzi wa hovyo uliofanywa na Baraza la Mawaziri ukizichapisha unakuwa umetenda kosa kwa mujibu wa kifungu cha 7(2)(c ) .Kifungu hiki kinaingilia uhuru wa kupashana habari ,uhuru na haki ya wahariri .
  6. Serikali imeamua kuwa na aina ya waandishi wa habari ambao inawataka wao kama serikali nah ii ni kutokana na kuanzishwa kwa bodi ya Idhibati kwa wanahabari Nchini , na ni bodi ambayo itakuwa inaundwa na serikali yenyewe . Kifungu cha 11 cha sheria hii kimeunda bodi hiyo ya UTHIBITI na sio Ithibati kama wanavyotaka umma uelewe. Waziri mwenye dhamana na masuala ya habari ndiye mwenye mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bodi hii .
  7. Bodi hii ya waziri imepewa mamlaka makubwa sana ikiwamo kuwasimamisha au kuwaondoa wanahabari waliothibitishwa katika orodha , kifungu cha 13 (a)
  8. Adhabu imewekwa kubwa sana kuwa mtu akifanya makosa kwa mujibu wa sheria hii atapigwa faini ya kati ya shilingi milioni tano mpaka milioni 20 au kifungo cha miaka 3 na kisichozidi miaka mitano jela au vyote kwa pamoja. Jambo hili ni la hatari kwani sasa Bodi inajipa mamlaka ya kuhukumu na kutoza faini bila Mahakama .
  1. Unapiga marufuku vyombo vya habari kuwa ni lazima 51% imilikiwe na watanzania –chombo kama Mwananchi na Citizen wanaomilikiwa 100% na Nation media group ya Kenya watatakiwa kuuza hisa zao

Hayo ni baadhi ya mambo ambayo yapo kwenye mswada huo ambao umeshapelekwa Bungeni .

Share Button
Layout Settings