TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SERIKALI YETU NA UVUNJWAJI WA KATIBA YA NCHI
Ndugu wana Habari, napenda kutoa shukrani na pongezi zangu za dhati kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuhabarisha umma.
Pia niwatakie ushindi watoto wetu wote wanaofanya mtihani wa darasa la saba, ulioanza leo Septemba 06, 2017. Mungu awajalie afya njema ili wapate ufaulu kwa asilimia 100.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 73 inasema kuwa, Nanukuu “wabunge wote wa aina zote watashika madaraka yao kwa mujibu wa Katiba hii, na watalipwa mshahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge”
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 135(2) inaeleza kwamba , nanukuu “Fedha ambazo hazitawekwa kwenye mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali ni zile zote ambazo zimetajwa na sheria kwamba zitumike kwa shughuli maalum au ziwekwe katika mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum”
Kwa mujibu wa ‘Sheria ya Uendeshaji wa Bunge ya mwaka 2008’, kifungu cha 31 kinaeleza kuwa fedha zote kwa ajili ya uendeshaji wa Bunge zinawekwa kwenye Mfuko maalum wa Bunge kama ulivyoanzishwa na sheria hiyo na msimamizi mkuu wa fedha hizo ni Katibu wa Bunge kwa mujibu wa kipengele cha (2) na (3).
Kati ya Juni 21, 2017 na Agosti 15, 2017 Katibu wa Bunge aliandika barua tatu tofauti akiomba fedha zaidi ya Shilingi Bilioni Tisa  (9,966,464,000.00) kwa Waziri wa Fedha na kwa Katibu Mkuu Hazina kwa ajili ya kugharamia bajeti ya ziada (Suplimentary budget) na fedha za matumizi mengineyo kwa ajili ya Bunge ikiwa ni nje ya Bajeti iliyokuwa imeidhinishwa na Bunge na kuwekwa katika mfuko maalum wa Bunge katika mwaka wa fedha 2016/17.
Tangu wakati huo mpaka tarehe 15 Agosti,2017 Serikali ilishatoa bajeti ya ziada kwa Bunge kiasi cha shilingi Bilioni 7 kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina bila kufuata Masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba inategemewa kuwa itaendelea kutoa (kama haijatoa) kiasi kinachozidi Shilingi Bilioni Mbili na Nusu (2,966,464,000.00) kwa ajili ya kulipia gharama za  posho ya Jimbo ya Mwezi Juni 2017 ambayo haijalipwa kwa ukamilifu. Fedha zilizotolewa kama bajeti ya ziada zilitumika kwenye kukidhi mahitaji ya kulipia posho mbalimbali za wabunge, ambazo ni posho ya Jimbo kwa wabunge ya mwezi Mei 2017; posho ya kujikimu kwa wabunge ya mwezi Juni 2017; posho ya vikao kwa wabunge ya mwezi Mei na Juni 2017; posho ya masaa mengi kwa watumishi ya mwezi Mei, na posho ya kikao kamati maalum.
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Bunge liliidhinisha fedha kwa ajili ya FUNGU 42 – MFUKO WA BUNGE kama ifuatavyo:-
(a)Matumizi ya kawaida – Shilingi 92,066,117,000 (bilioni 92.07). Kati ya hizo:
(i) Mishahara – Shilingi 23,798,609,000 (Bilioni 23.80)
(ii) Matumizi Mengineyo – Shilingi 68,267,508,000 (Bilioni 68.27)
(b)Miradi ya Maendeleo Fedha za Ndani – Shilingi 7,000,000,000 (Bilioni Saba).
Bunge ni taasisi ambayo kalenda yake inafahamika na idadi ya wajumbe wake inafahamika pamoja na idadi ya vikao na hivyo wanapopitisha bajeti wanakuwa wakijua ni kiasi gani kwa uhakika kinahitajika katika mwaka husika wa fedha.

Hoja yetu juu ya jambo hili ni nini?
Kwa mujibu wa Katiba ya Nchi yetu, pamoja na Sheria na Kanuni zinazoongoza Bunge na Serikali; kuwa Bunge pamoja na majukumu yake mengine lina jukumu la kuisimamia Serikali. Ili kuhakikisha utekelezaji wa takwa hili la kikatiba, Sheria ilitungwa ili Bunge liwe na fedha zake kwenye mfuko maalum likiwa kama mhimili unaojitegemea na unaopaswa kujiendesha bila kuwa tegemezi. Pia, hatutegemei Bunge kuminywa katika upatikanaji wa rasilimali fedha ili kujiendesha. Ikumbukwe pia Bunge ndiyo linalopitisha bajeti yake naya Serikali kwa mujibu wa Katiba. Bajeti ya Bunge huwekwa kwenye mfuko maalum.

  1. Bunge limevunja Katiba ibara ya 137 (3) (a) na (b) kwa kuomba fedha za ziada nje ya bajeti yake iliyoidhinishwa na Bunge bila kwanza kupitisha maombi hayo Bungeni kama ambavyo  Katiba inataka.
  2. Waziri wa fedha amevunja Katiba ibara ya 136 na 137 (3) kwa kutoa fedha za ziada nje ya Bajeti iliyopitishwa na Bunge kwani katiba inamtaka kuwasilisha Bungeni maombi ya Bajeti ya ziada au maelezo ya matumizi ya nyongeza Bungeni na baada ya Bunge kuyakubali maombi hayo atawajibika kuwasilisha kwenye Bunge Muswada wa sheria ya Matumizi ya fedha za serikali kwa ajili ya kuidhinisha matumizi ya fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.
  3. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mujibu wa Katiba ibara ya 143 (2) (a) na (b) anatakiwa kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa na kwamba zinatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 136 ya katiba na iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yametekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe. Hatutaki kuamini kuwa CAG amehusika katika kuidhinisha Malipo haya maana hata kwenye mawasiliano yaliyopo hajawahi kupewa hata nakala.
    1. Serikali inatoa wapi fedha hizi kwani tayari bajeti ya mwaka 2016/17 ilishakwisha na sasa tupo kwenye mwaka wa fedha 2017/18 na hakuna fungu la Bajeti lililotengwa kwa ajili ya kugharamia bajeti ya ziada ambalo lilipitishwa na Bunge. Au ndio kusema serikali inaendeleza utamaduni wake wa kutokuheshimu bajeti iliyopitishwa na Bunge kama ambavyo tumeyashuhudia matumizi ya serikali yasiyozingatia bajeti kama vile ununuzi wa Ndege, ujenzi wa uwanja wa ndege Chato na mengineyo mengi.
    2. Je, ni sahihi kusema kuwa sasa Bunge limeshindwa kuisimamia Serikali na kwamba sasa limekuwa kama sehemu yake na ndio maana linapelekewa mambo kwa ajili ya kuidhinisha tu na sio kuweka maoni yake? kama ambavyo kwenye Bunge hili la Septemba 2017 wanapelekewa kupitisha ‘Azimio la kuridhia mkataba wa ujenzi wa Bomba la Mafuta baina ya Tanzania na Uganda, huku uzinduzi wa ujenzi wa Bomba hilo ukiwa umeshafanyika tangu tarehe 5 Agosti 2017 na Mkandarasi yuko eneo la kazi (kwa kuwa serikali inauhakika kuwa Bunge haliwezi kukataa kuidhinisha Mapendekezo yake au hata kutaka kuuona na kubadilisha baadhi ya vipengele vyake kamba ambavyo itapendezewa!

Hii inaonyesha udhaifu mkubwa kabisa katika uongozi wa Bunge, na ni ishara tosha kwamba Bunge limekuwa sehemu ya Serikali. Kwa kuwa, Bunge limejipambanua kuwa ni sehemu ya Serikali kwa uongozi wake kutekeleza kauli ya Rais kwa Spika wa Bunge ya kwamba “Pambana na Wabunge Bungeni na mimi nitapambana nao nje ya Bunge” huku ikionekana dhahiri kwamba aliwalenga wabunge wa kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani. Huu ni udhaifu mkubwa sana katika uongozi wa Bunge, kwani vitisho bila kufuata sheria ni dalili tosha kabisa ya udhaifu.
HITIMISHO
Mambo yote haya yanawezekana kufanyika kwenye Nchi ambayo Katiba yake haifuatwi kikamilifu na hakuna taasisi zinazoweza kusimamia utekelezwaji wa Katiba ya Nchi kwa ukamilifu wake.
CHADEMA Tunaamini kuwa Haya yanaweza kumalizika kama TUTAKUWA NA KATIBA MPYA ILIYOTOKANA NA MAONI YA WANANCHI NA AMBAYO ITAIMARISHA TAASISI ZETU.
Tunaitaka Serikali na Bunge kutoa majibu ya kina kuhusu ukiukwaji na uvunjwaji huu wa Katiba yetu na wale wote waliohusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa Sheria na taratibu zilizopo.
Aidha, tunawataka Wabunge kutimiza wajibu wao wa Kikatiba wa kuisimamia Serikali na kuhakikisha kuwa wanasimamia utekelezwaji wa Katiba ya Nchi na kamwe wasiruhusu kuona Inavunjwa na mamlaka yoyote katika Nchi.
Imetolewa leo tarehe 6 Mei 2017

……..………………………….
Dr. Vincent B. Mashinji
Katibu Mkuu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

Share Button