HOTUBA YA BARAZA LA WAZEE KUPITIA VYOMBO VYA HABARI SIKU YA WAZEE DUNIANI 1/10/2017

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA )
BARAZA LA WAZEE WA CHADEMA
HOTUBA YA BARAZA LA WAZEE KUPITIA VYOMBO VYA HABARI SIKU YA WAZEE DUNIANI 1/10/2017

Ndugu wanahabari
Tunashkuru kwa fursa hii nyingine ya kukutana na kuzungumza na Watanzania kupitia vyombo vyenu vya habari.
Kama mjuavyo leo ni Siku ya Waze Kimataifa ambayo uadhimishwa kila Tarehe moja mwezi wa Oktoba kila mwaka.Hii nikutokana na azimio la Mkutano wa wanachama wa Umoja wa Mataifa lililofanyika mjini Madrid Hispania mwaka 2002 na kujulikana kwa jina la Madrid International Plan of Action on Ageing (MIPAA). Lengo la mkutano huo lilikuwa kuandaa mpango kabambe wa kushughulikia maswala ya uzee na kuzeeka. Ni baada ya kutambua kuwa idadi ya wazee ilikuwa imeongezeka duniani kwa kasi na kuonekana kwa umuhimu wa kuwa na mpango thabiti kwani mahitaji ya wazee yalionekana kutopata kipaumbele ipasavyo.
Hivyo mkutano ule ulitoa mapendekezo yahusuyo hali za wazee katika Nyanja zaafya, uwakilishi,ushirikishwaji,elimu,uchumi,n.k. Ikakubaliana kila nchi ikaandae mipango yake kuhusu uzee na kuzeeka kulingana na mapendekezo ya mkutano ule.
Kama sehemu ya maadhimisho ya siku hii, Baraza la Wazee wa CHADEMA, limeomba kukutana nanyi ili kufikisha ujumbe kwa jamii ya Watanzania wenzetu katika masuala kadha wakadha yanayohusu wazee kwakuzingatia Kauli mbiu ya taifa ya wazee mwaka huu inayosema “Kuelekea uchumi wa viwanda: Tuthamini mchango, uzoefu na ushiriki wa wazee kwa maendeleo ya taifa.”

 

 

 • Hali ya Wazee nchini

Ndugu wanahabari,
Kwa ujumla hali ya wazee nchini si nzuri katika nyanja zote zilizokusudiwa kuboreshwa na azimio lililopitishwa na Umoja wa Mataifa huko Madrid, yakiwemo maswala ya afya, uwakilishi,ushirikishwaji,uchumi n.k. Kama kauli mbiu ya wazee ya taifa inavyosema mwaka huu ili tufanikiwe kujenga uchumi wa viwanda lazima taifa lithamini mchango, uzoefu, ushiriki wa wazee. Kinyume chake ndoto hii ya kujenga uchumi wa viwanda haiwezi kufikiwa.

 • Afya – Matibabu bure kwa wazee

Sera ya wazee ya mwaka 2003 inatamka wazi kwamba wazee wote wenye umri wa miaka 60+, (Miaka sitini na kuendelea), wapatiwe huduma za afya bila malipo katika hospital zote  za serikali, vituo vya afya na zahanati.
Pamoja na maagizo hayo ya sera na matamko mbalimbali ya serikali kupitia viongozi wake, hali ya huduma kwa wazee bado ni mbaya sana. Sehemu ya changamoto wananzokutana nazo wazee ni pamoja na:

 • Ukosefu wa dawa, wazee wanapofika katika sehemu mbalimbali za huduma za afya huishia kupewa tu dawa za maumivu. Kwa kuwa wanatakiwa wahudumiwe bure, huambiwa dawa hakuna na waende wakanunue. Pia kulazimishwa kulipia huduma za vipimo mbalimbali.
 • Ukosefu wa wataalamu wa magonjwa ya wazee, mpaka sasa hakuna hospitali, kituo cha afya au zahanati zilizo na daktari aliyebobea katika magonjwa ya wazee. Hali hii imenyima fursa wazee wengi kukosa haki yao ya kupata matibabu kwa kukosa watu wa kuwahudumia. Pia ukitilia maanani madaktari wengi ni vijana kwa mila na desturi zetu na aina ya magonjwa ya wazee inakuwa ni changamoto zaidi kwa kufikiri kila Daktari anaweza kumuhudumia Mzee.
 • Ukosefu wa madirisha ya kuhudumia wazee. Wazee wengi wamejikuta kupanga foleni na kuhudumiwa na watu wengine kwa kuwa vituo vingi vya afya havina madirisha ya kuhudumia wazee. Hata maeneo ambayo wameweka madirisha hayo hakuna wahudumu. Mfano halmashauri yenye kata 26, utakuta kuna madirisha mawili tu ya kuhudumia wazee.
 • Upatikanaji wa vitambulisho vya wazee kwa ajili ya kupatiwa matibabu bado ni changamoto kubwa sana. Halmashauri nyingi zimeshindwa kutenga fedha kwa ajili ya kutengeneza vitambulisho vya matibabu kwa wazee. Suala la vitambulisho vya matibabu kwa wazee huonekana kama jambo la ziada na lisilokuwa na umuhimu.
 • Umbali wa vituo vya afya, kwa mujibu wa malengo ya MKUKUTA imejata uwepo wa huduma za afya kwa umbali usiozidi km 5 ili kutoa fursa ya upatikanaji wa huduma za afya kwa urahisi hususani kwa wazee. Sehemu kubwa hili halijafanyika, bado huduma zipo mbali na kufanya wazee kushindwa kupata huduma za afya.
 • Uwakilishi katika Vyombo Mbalimbali vya Kimaamuzi

Sera ya Wazee inataka wazee wawakilishwe katika ngazi zote za maamuzi kuanzia ngazi ya mtaa/kijiji, kata, Halmashauri,mkoa hadi Taifa. Lengo ni kuwa na msemaji anayetokana na wazee wenyewe atakayewasilisha kero, changamoto na matatizo mbalimbali yanayowakabili wazee kwa jumla wao. Pamoja na sera kutamka wazi wazee kuwa na uwakilishi katika vyombo vya uwamuzi bado utekelezaji wake umebaki kuwa ndoto tu kwa wazee. Pamoja na Rais kupewa nafasi ya kikatiba kuteua wabunge kumi kuingia katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano, bado wameshindwa kutumia nafasi hiyo kuteua nafasi ya mwakilishi wa wazee. Ila wapo wawakilishi wa vijana, wanawake na walemavu. Hali hii inawafanya wazee washindwe kuwa na mtu wa kuwasemea katika vyombo hivi muhimu vya kufanya maamuzi ya nchi.

 • Kiuchumi
 • Ucheleweshwaji wa mafao kwa wastaafu

Kumekuwepo na kilio cha muda mrefu sasa cha wastaafu kucheleweshewa mafao yao baada ya kustaafu. Kinyume kabisa na taratibu za nchi wapo wazee wastaafu ambao wanaangaikia kupata mafao yao zaidi ya miezi sita hadi mwaka na mbaya zaidi wengine wanafariki kabla ya kulipwa mafao yao. Jambo la kusikitisha ni sababu za kucheleweshewa malipo yao, kwa mujibu wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) sababu za kushindwa kulipa kwa wakati ni serikali kuchelewa kulipa madeni iliyokopa kwenye mifuko ya jamii husika.

 • Pensheni ya jamii kwa Wazee

Wazee wengi wamekuwa wakililia serikali kuwalipa pensheni baada ya kulitumikia taifa kwa muda mrefu katika nyanja mbali mbali ikiwemo kilimo, uvuvi,ufugaji n.k. Pamoja na tafiti mbalimbali kufanyika na kuonyesha uwezekano wa serikali kulipa pensheni kwa wazee, bado serikali imekuwa na kigugumizi na kukosa utashi wa kisiasa wa kuwalipa wazee pensheni kama ilivyoelezwa katika Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003.

 • Haki na Kutambuliwa na Kuenziwa

Wazee tuna haki ya kutambuliwa /kuenziwa na jamii. Serikali iliagiza katika MKUKUTA 1 wa 2005 kuwa ifikapo 2010 kila halimashauri iwe imetambua wazee wake wote kwa kuwapa vitambulisho kwa lengo la kurahisisha huduma za matibabu. Hili swala limekuwa gumu kutekelezeka katika Halmashauri nyingi kwasababu za utashi wa kisiasa. Tuchukue nafasi hii kumpongeza Meya wa Kinondoni Mh. Boniphace Jocob anayetoka CHADEMA kwa kuonyesha utashi wa kisiasa na kusimamia vema zoezi la kutoa vitambulisho vya matibabu bure kwa wazee walioko kwenye Halmashauri ya Kinondoni.

 • Ushauri wetu kama wazee wa CHADEMA juu sintofahamu inayoendelea nchini

Ndugu wanahabari
Kila mpenda amani na uzalendo atakubaliana nasi msingi imara wa amani na utulivuna maendeleondani ya nchi yeyote ni uwepo wa haki, watu kuwa na matumaini na viongozi wao, uwepo wa demokrasia na utawala bora unaozingatia Katiba, Sheria na taratibu zingine hasa za kuongoza nchi na kusimamia serikali kwa niaba ya wananchi wote.
Kwa bahati mbaya sana ndani ya nchi, hususan tangu kuingia madarakani kwa Serikali hii ya CCM ya awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli, tumeshuhudia mwenendo ulio kinyume kabisa na misingi hiyo.
Kumekuwa kauli na matendo ambayo ama yenyewe ni ukiukwaji mkubwa wa Katiba na sheria za nchi au yote kwa pamoja yamepelekea uvunjifu mkubwa wa sheria za nchi kiasi cha kuiweka nchi nzima katika sintofahamu kubwa. Tutoe mifano michache tu:

 • Kukamatwa, kubambikiwa kesi, kutekwa, kuteswa, kushambuliwa na hata kuuwawa kwa viongozi wa kisiasa na wananchi wengine wanaomkosoa Rais Magufuli na serikali yake. Rejea ni tukio la kushambuliwa kwa kusudio la kuua Mbunge na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu na hivi karibuni tukio la kuuwawa kwa Kaimu Mwenyekiti wa CUF Jimbo la Mtopepo, Ali Juma Suleiman.
 • Kuokotwa mara kwa mara miili ya watu waliouwawa na serikali kutoa maelezo tatanishi.
 • Kuminywa kwa haki za kikatiba na kisiasa kinyume cha sheria eg. Kuzuiwa kwa shughuli halali za siasa.
 • Kuminywa kwa uhuru wa maoni na kupata taarifa e.g kuzuiwa kwa bunge live, kufutwa na kufungiwa kwa magazeti yanayomkosoa Rais.
 • Mhimili wa dola kuingilia mihimili mingine ya serikali yaani bunge na mahakama
 • Kauli na matendo tata kutoka kwa viongozi wa serikali. Rejea kauli za Mh. Raisi na matendo ya wakuu wa mikoa na wilaya.

Masuala haya pamoja na mengine mengi ambayo hatujayataja yamezidi kuipasua nchi na kuibua sintofahamu ambayo mtu yeyote anaweza kuona wazi kunatishia mstakabali mwema wa nchi yetu. Mambo haya yameongeza kilio katika macho ya wananchi ambao wanaamini katika haki, demokrasia na utawala bora kama nguzo muhimu za maendeleo tunayoyawaza na kuyahitaji. Ukifuatilia mijadala katika vyombo vya habari na mitandaoni  unaona kuwa taifa liko katika wakati mgumu sana.

 • Wazee na Katiba Mpya

Ndugu wanahabari
Ni ukweli ulio wazi kuwa changamoto zinazowakabili Wazee na dhana ya uzee hapa nchini, ufumbuzi wake unapaswa kuwa wa Kikatiba, kisheria na kisera. Ili wazee wa leo na wale wa kesho waache kuukimbia au kuugopa uzee kwa kudhani kuwa ni mateso au kifo, tofauti na nchi za zilizoendelea ambako watu hutamani uzee kwa sababu ya mafao ya uzeeni na utaratibu mzima wa kuwajali ikiwa ni pamoja na makazi, matibabu.
Ndiyo maana tumeona ni vyema pia kupitia siku hii ya leo, Wazee wa CHADEMA kwa pamoja tuunge mkono msimamo wa Chama chetu na kilio cha Watanzania wengi kuhusu umuhimu wa nchi yetu kuwa na Katiba Mpya na bora.
Kwa hakika umuhimu wa nchi yetu kuwa na Katiba Mpya unazidi kuoneka kila siku. Na hapa ieleweke vyema kuwa hatupazi sauti zetu katika mapambano ya kudai Katiba kwa ajili ya kutatua matatizo ya Wazee pekee, la hasha. Watanzania sasa wanaitaka Katiba Mpya kwa ajili ya kutibu majeraha ya taifa hili.
Kama tulivyoelezea hapo juu, taifa letu linapita katika kipindi kigumu na majaribu makubwa ya hali ya kisiasa, kiuchumi ambayo pia yataathiri hali ya kijamii pia.
Hakuna njia nyingine ya mkato ya kulisaidia taifa letu kwa sasa bali kuwa na Katiba Mpya itakayowapatia wananchi mamlaka ya kuamua namna ya kujitawala huku viongozi wakijua kuwa wana dhamana tu ya kuongoza kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania.
Kama wananchi wa kawaida hata mitaani wanazungumza na kuona umuhimu wa Katiba Mpya iliyo bora, viongozi wetu wasipoliona hili watakuwa wanazidi kujipotezea uhalali wa kuwa WAONGOZA NJIA ma hivyo kutostahili kuwepo madarakani wakati ujao.
Ushauri wetu:

 • Tunamshauri Rais Magufuli kukutana na Wazee katika kikao cha pamoja ambao hawataogopa kumwambia ukweli ili tuliepushe taifa na madhara makubwa yanayoweza kulipata taifa letu. Wazee ambao tunashauri Rais Magufuli akutane nao katika kikao cha pamoja ni pamoja na wazee kutoka vyama vya siasa, viongozi wastaafu wa dini mbalimbali nchini, wastaafu serikalini, wastaafu serikalini, na awe tayari kusikiliza na apokee ushauri na ukosoaji wao kama ambavyo anasikiliza na kupokea hongera.
 • Ni wakati sasa serikali kupeleka muswada wa sheria ya wazee nchini ili kutekeleza sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 na kama serikali haitafanya hivyo, basi wawakilishi wa wananchi, (Wabunge) watumie kanuni ya Bunge kuwasilisha muswada binafsi kuhusu sheria ya wazee nchini.
 •  Serikali ianzishe mfuko wa kutoa mikopo kwa wazee kwa ajili ya miradi ya uzalishaji kama inavyofanya kwa vijana na wanawake kupitia halmashauri na manispaa.
 • Wazee nao wapatiwe mwakilishi katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ili aweze kuwasilisha matatizo yao kama ilivyo kwa wabunge wananwake na walemavu walivyo na wawakilishi katika Bunge.
 • Viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali na wawakilishi, (Madiwani na Wabunge) wawe na utaratibu wa kukutana mara kwa mara na wazee na kusikiliza kero na matatizo yanayowakabili wazee na kuyatatua kwa wakati.
 • Serikali ihakikishe katika vituo vya Afya, zahanati na hospitali panakuwa na wataalamu wa magonjwa ya wazee.
 • Serikali iwe na utashi wa kuanza kulipa pensheni kwa wazee wote nchini bila kujali kama waliajiriwa serikalini au la kama wanavyofanya Zanzibar na kama tafiti mbalimbali zilivyopendekeza.
 • Jamii na serikali iwatumie wazee katika kurudisha maadili ya jamii hususani kwa vijana ambao kwa sasa wamepoteza maadili.

Wito kwa Wazee katika Siku ya Wazee Duniani
Tunapenda kutoa wito kwa Wazee wote bila kujali tofauti zozote zile;

 • Wasimame imara na kujitokeza hadharani kukemea mwenendo mbaya wa nchi yetu ikiwemo ukiukwaji wa haki za binadamu, ukiukwaji wa sheria na Katiba ya Nchi, kauli na matendo mabaya yanayozua sintofahamu kubwa kwa Watanzania.
 • Kutoa ushauri bila kuchoka kwa watu wote hasa kwa vijana wetu na viongozi wenye mamlaka.
 • Kushiriki kikamilifu katika kuendelea kuwatengenezea nchi Wazee wa kesho (vijana au watu wazima wa leo), hasa kudai Katiba Mpya.
 • Tuidai serikali ieleze kwanini malipo ya pensheni hayalipwi kwa wakati baada ya kustaafu kwa wafanyakazi waliokuwa kwenye sekta rasmi ya ajira? Kwanini serikali imeshidwa kuweka mfumo mzuri utakaowahakikishia Wazee makazi (vituo) vyenye hadhi? Kwanini Wazee nchini hatuna jukwaa linalotuunganisha sote kutoa michango ya mawazo yanayogusa maisha yetu na jamii nzima kwa ujumla?

Hitimisho
Kwa mujibu wa mila na desturi zetu katika jamii, Wazee wamekuwa na jukumu kubwa la kiuongozi, ulezi, ushauri na upatanishi, kwa kuzingatia hayo pamoja na kauli mbiu ya Siku ya Wazee Duniani, tunasisitiza wito wetu wa kumtaka Rais Magufuli akutane na Wazee watakaomsaidia mawazo, ushauri kwa ajili ya tiba ya muda mfupi kuliokoa taifa kabla manung’uniko yanayoendelea nchini, hayazidi na pengine kuwa kitu kingine kibaya kinachoweza kutishia hatma yetu sote kama taifa.


MFANO WA KUIGWA UBUNGO

Leo siku ya Jumatatu ya tarehe 04 september 2017, *Mstahiki Meya Manispaa ya Ubungo,* Mheshimiwa *Boniface Jacob.*
Amemkaribisha *waziri wa Afya,Maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto,* *Mh.Ummy Mwalimu,* katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo,kata ya sinza viwanja vya TIP.
Ambapo mheshimiwa Waziri, *amezindua rasmi utoaji wa Kadi za Matibabu ya bure kwa wazee wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo*.
*Awamu ya kwanza wazee 7,299wamenufaika katika kupata Vitambulisho hivyo,* vitakavyo wasaidia wazee kupata huduma ya kumuona daktari,kupimwa na Matibabu ya dawa za aina zote watakazo hitaji.
Mtahiki meya amewashukuru watendaji wa Halmashauri, Wabunge na Madiwani wa manispaa ya Ubungo waliofanikisha kutenga *bajeti ya billioni 1.8*ambayo itafidia huduma ya Matibabu ya bure kwa wazee wote wa Halmashauri ya manispaa ya Ubungo.
Aidha Mheshimiwa waziri, Ummy Mwalimu, amempongeza Mstahiki Meya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa kuwa Mfano wa kuigwa na kuingia kwenye orodha ya kipekee ya *”MARAFIKI WA WAZEE”* kwa kuwajali na kujitoa kwa ajili yao.
Mheshimiwa waziri ameahidi kusaidia *bima watoto 100,* kama njia ya kuunga mkono juhudi za Halmashauri katika sekta ya Afya pamoja na *kujenga Wodi ya mama na mtoto,chumba cha kujifungulia na vifaa vyake* ndani ya mwaka huu 2017 kama njia ya kufurahishwa na kazi nzuri ya Halmashauri ya Ubungo.

MWISHO.
Wazee wa Ubungo wamekubaliwa Ombi lao kwa Waziri kuwa vitambulisho hivyo watakavyopewa na Halmashauri ya Ubungo viweze kitumika katika hospitali za rufaa ikiwemo, Muhimbili na Jakaya kikwete ya Moyo kama njia ya muendelezo wa Huduma bure kwa wazee.

Share Button
Layout Settings