TAMKO LA KULAANI KAULI AU MAPENDEKEZO YA MZEE ALI HASSAN MWINYI YA KUTAKA KUVUNJWA KWA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
BARAZA LA WAZEE WA CHADEMA
TAMKO LA KULAANI KAULI AU MAPENDEKEZO YA MZEE ALI HASSAN MWINYI YA KUTAKA KUVUNJWA KWA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Ndugu waandishi wa habari.
Sisi, Baraza la Wazee wa CHADEMA tumewaiteni hapa kulaani kauli iliyotolewa na Mzee Ali Hassan Mwinyi (Rais Mstaafu) ambayo ilikuwa na lengo la kushawishi kuvunjwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, alipokuwa kwenye swala ya Eid El Fitr iliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam alinukuliwa  akisema “Kama si matakwa ya Katiba   ya nchi, uongozi wa Rais John Magufuli ulipaswa kuendelea kuwapo miaka yote…. laiti ingelikuwa Katiba iliyopo haikufupisha muda wa uongozi wa rais,  ningeshauri Rais Dk Magufuli awe  Rais wa Tanzania wa siku zote”.
Kauli hii imetusikitisha sana hasa kuona inatolewa na Mzee tena aliyewahi kuwa kiongozi Mkuu wa Nchi yetu kwa miaka 10, ambaye anapaswa kupima madhara ya kila neno analolitamka kwani “imani uja kwa kusikia
Ndugu waandishi wa Habari, na Watanzania mnaotusikiliza, tuwakumbushe kuwa wakina Nkurunzinza, Mugabe, Kabira na wengineo, walipata watu wachache walioanza kuwachochea na kuwapigia kampeni kuwa waendelee kuwaongoza na matokeo yake waliamua kufuata ushauri na wote tunafahamu matokeo ya ushauri huu na maamuzi haya kwa yale yanayoendelea katika nchi zao.
Kwakutambua madhara ya kauli kama hizi wazee wa CHADEMA tumeamua tusikae kimya.
Sisi kama wazee tulijipa muda wa siku kadhaa tukiamini kuwa mzee aliteleza ulimi na angeweza kuirekebisha kauli yake au Chama chake kingelitoa kauli ya kuweka marekebisho, lakini hakufanya hivyo na wala Chama chake hakikufanya hivyo na mbaya zaidi Raisi mwenyewe naye amenyamaza kimya kuhusiana na kauli hii. Kwahiyo tukajua wazi kuwa huu ni mkakati rasmi wa kuliandaa taifa kisaikolojia kuwa na “mfalme au Sultani” (yaani Raisi wa sikuzote kama kama alivyopendekeza kwenye kauli yake).
Hivyo sisi wazee wa CHADEMA Tunaulaani mkakati huu muovu unaoweza kulidumbukiza taifa letu katika machafuko kama ambavyo imetokea kwa nchi jirani zilizopuuzia uchochezi kama huu wa uvunjifu wa Katiba ya nchi.  
Mwl. Nyerere aliwahi kumkemea mzee Mwinyi kwa Swala hili.
Sisi wazee tunamkumbuka Mzee Mwinyi kuwa wakati anaelekea mwishoni mwa utawala wake yeye na wapambe wake walipenyeza pendekezo hili la hatari la kutaka kuibadili Katiba, ili Raisi Mwinyi aweze kuongoza bila kikomo, lakini Mwal. Nyerere akalizima jaribio hilo kwa kukulikemea vikali tena wazi wazi na alikwenda mbali zaidi na kulizungumzia ndani ya kitabu chake cha “Uongozi wetu na hatma ya Tanzania” alichokiandika mwaka 1994 ili vizazi vinavyokuja visfanye kosa kama hili.
Nitanukuu baadhi ya vifungu katika kitabu hicho: “Mapema mwezi Disemba 1992, Halimashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilikutana Dodoma kwa ajili ya kuzungumzia swala la utaratibu wa kuchagua Makamu wa Rais na mambo mengine mengine.  Mimi (Mwl. Nyerere) nilialikwa nitoe maoni yangu.
“Katika kikao cha faragha cha Viongozi wakuu wote wa Chama na Serikali, na wengine wa nyongeza. Rais (Mwinyi) alieleza kuwa mbali ya agenda zilizokuwa zimeandaliwa walikuwa (yaani Mwinyi na wenzake)  wamezungumza pia suala la muda wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa  Tanzania kuwepo madaarakani. Alieleza kuwa pamoja na kwamba ilikuwa imekubalika muda wa Rais kuwepo madarakani uanishwe lakini ni muda gani akae ulikuwa haujaamuliwaa…..”
“Nilishutuka sana kusikia jambo ili linaibuliwa tena ili lijadiliwe upya kwani uamuzi wa vipindi vya Raisi kuwa madarakani ulikwishafanyika”
“Lakini kabla ya hapo baadhi ya viongozi wa Chama walikuwa wameanza kampeni za kutaka Rais Mwinyi aongezewe vipindi vya muda wa kuwa Rais zaidi ya ule muda wa vipindi viwili uliokuwa umekubalika. Niliposikia hizo kampeni nilikwenda moja kwa moja kwa Rais na kumsihi azizime kampeni hizo; na viongozi wahusika nilitafuta nafasi nao nikawaomba wasilifufue jambo hili kwani lilikwisha fanyiwa maamuzi na kulifufua upya kungeleta athari kubwa”
“Sababu ya kuweka ukomo wa muda wa Raisi kuwa madarakani utamkwe na uwe ni sehemu ya Katiba ilikuwa ni kuondoa uamuzi huo mikononi mwa Rais Mwenyewe ,au kikundi chochote cha Chama au Dola……”
“Watawala wetu ni wanasiasa wa kawaida ambao wanapenda sana kutawala hata kama hawana uwezo wa kutawala ;na ambao wako tayari hata kuhonga ili wachaguliwe kuwa Watawala ,na wakishakuchaguliwa hawatoki bila kulazimishwa ………Kwa hiyo ni jambo la busara kabisa uamuzi wa muda wa kuwa Rais ufanywe mara moja , na ukishakufanywa uwe ni sehemu ya Katiba ya Nchi na Uheshimiwe!….” Mwisho wa kunukuu.
Sisi wazee wa CHADEMA tumeamua kunukuu maneno haya ya hayati baba wa Taifa Mwl.Nyerere ili ;
Kwanza, kumkumbusha Mzee Mwinyi kuhusu jambo hili kwani tunaona kuwa kiu yake ya tangu mwaka 1992 ya kutaka kuondoa ukomo wa muda wa kutawala kwa Rais bado anayo mpaka leo pamoja na kukemewa na Mwl. Nyerere.
Pili, tunawakumbusha Watanzania kuwa hatari aliyoiona Mwal Nyerere miaka hiyo bado iko pale pale kwani wote tumeshuhudia watawala wengi Afrika ambao wana mawazo ya Kidkteta wakiwa wanajiandaa kutawala milele na hatimaye kuziingiza nchi zao katika machafuko ya kisiasa kwa sababu tu ya uchu wa madaraka, hatutaki nchi yetu ielekee huko na kamwe sisi wazee hatutakuwa tayari kuona jambo hili likitokea katika Taifa letu.

Tatu, tunataka kuwakumbusha wazee wenzetu ambao bado wako CCM na huwa kila mara wanajinasibu kuwa wanafuata misingi na miongozo ya Mwl.Nyerere wakumbuke maneno hayo na wajitokeze hadharani wazi wazi kukemea kauli za Mzee Mwinyi na wamtake aheshimu misingi ya Katiba yetu kama alivyofanya Mwl.Nyerere kama kweli bado wanamuenzi Mwalimu.
Nne, Tunawataka wazee wa CCM waungane nasi (Wazee wa CHADEMA) kumtaka Rais Magufuli ajitokeze hadharani waziwazi na kukemea kampeni hizi ambazo zinaratibiwa na Mzee Mwinyi na aweke wazi kuwa yuko upande gani.
Tano,Tunawataka watanzania wote wenye mapenzi mema na wazalendo wa kweli kwa nchi yetu kuupinga kwa nguvu zote utaratibu wa kutaka kuturudisha nyuma , ni lazima katiba iliyopo iheshimiwe na hasa katika kipindi hiki cha kutaka katiba mpya na asiwepo yeyote miongoni mwetu anayetaka kuharibu misingi tuliyokwisha kujiwekea kama Taifa kwa kipindi kirefu.
HITIMISHO
Sisi wazee wa CHADEMA tunaona jitihada za wazi wazi kabisa za kuvunjwa kwa Katiba yetu hali Maraisi wastaafu na Makamu wa Raisi wakiendelea kukaa kimya na wale wanaopata fulsa ya kusema ndio hawa aina mzee Mwenyi ambao wanachochea uvunjifu wa Katiba.
Tumeshuhudia watanzania wakibaguliwa kwa misingi ya itikadi za kisiasa huku vyama vya siasa vikinyimwa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Tunapenda kuwakumbusha watanzania kuwa kitendo cha kuvunja Katiba ya nchi yetu ni kosa la uhaini.
Hima wazee tusimame imara katika kipindi hiki na tumuenzi Hayati Baba wa Taifa kwa vitendo kwa kumkemea yeyote yule ambaye anashawishi au anataka kuvunjwa kwa misingi ya Katiba yetu na Heshima kubwa ambayo kama taifa tumeishajiwekea mpaka sasa tangu uhuru.     

Imetolewa leo tarehe 29 Juni, 2017
Roderick Lutembeka
Katibu mkuu Baraza la Wazee CHADEMA Taifa

Share Button
Layout Settings