BAVICHA: RAIS MAGUFULI – NCHI YETU INAVIMBA!

BARAZA LA VIJANA WA CHADEMA (BAVICHA)
TAARIFA KWA UMMA
RAIS MAGUFULI – NCHI YETU INAVIMBA!

Ndugu waandishi wa Habari,
Kwanza tunawashukuru kwa kuitikia wito wetu siku hii ya leo.
BAVICHA tumewaomba kukutana nanyi hapa, ili kueleza kile ambacho kinaendelea katika nchi hii ambacho kwa tafsiri ya haraka tunaweza kusema kwamba, Rais Magufuli hataki kuambiwa wala kusikia ukweli kutoka kwa watu asiowapenda.
BAVICHA tunamtaka Rais ajue ukweli kwamba nchi inavimba au inazidi kuvimba kutokana na mambo kadha wa kadha yanayoendelea katika nchi yetu hasa mwelekeo wa demokrasia na uhuru wa kutoa maoni na kupata habari.
Ndugu waandishi wa habari,
Mosi, Wananchi wanajengewa chuki ndani ya mioyo yao kutokana na kauli za Rais na maelekezo yake ambayo kwa nyakati tofauti yamesababisha mkanganyiko miongoni mwa wananchi  na ambayo kwa kiasi kikubwa yanawakandamiza wapinzani, nitatoa mifano michache;

  • Kwanza kitendo cha Rais kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ilhali yeye Rais anatumia Jukwaa la URAIS kukifanyia mikutano chama chake cha CCM, jambo hili linawakera wananchi, hawalikubali na wanaona Rais anatumia madaraka vibaya na hii inazidisha chuki na hasira miongoni mwa watanzania wapenda Demokrasia, swali kubwa wanalojiuliza wananchi ni kuwa; "Je, CCM kimekufa kiasi ambacho hakiwezi kufanya mikutano chenyewe hadi kitegemee mbeleko ya jukwaa la URAIS?"
  • Rais Magufuli anatumia nafasi yake ya URAIS, kufanya kazi za siasa za kukieneza chama chake cha CCM, huku akiwa ametumia mamlaka ya URAIS kupiga marufuku shughuli za kisiasa, kinyume kabisa na Katiba na Sheria za Nchi. Tunatoa wito kwa Rais, atambue kuwa suala hili ni kubwa na linawakera sana wananchi na ‘kujaza vifua vyao’.
  • Jambo lingine ambalo linawakera na kuwachukiza wananchi ni kauli mbalimbali ambazo Rais Magufuli anazitoa ambazo kwa namna moja au nyingine zinaminya uhuru wa watu kutoa maoni yao, au hata kumshauri. Mathalani, kitendo cha kuwaambiwa wanasiasa "WACHUNGE MIDOMO YAO" ni kauli ya kibabe, inayoonyesha kuwa Rais hataki kusikia ushauri wowote toka kwa wanasiasa wenzake..!!

Itakumbukwa kwamba kauli hii aliitoa kwa Mhe. Edward Lowassa, kujibu ushauri wa Mhe. Lowassa wa kutaka Masheikh wanaoshikiliwa Mahabusu ama wapelekwe mahakamani na kushitakiwa ili wahukumiwe kwa mujibu wa sheria au waachiliwe na polisi, lakini cha kushangaza Mhe. Rais anakuja kutoa kauli ya kumuonya Mhe. Lowassa, badala ya kuwaonya na kuwachukulia hatua Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka kwa kushindwa kuwapeleka mahakamani watu hawa. Mbaya zaidi Mhe. Rais anakwenda mbali kwa kutolea mfano Gereza la Guantanamo ambalo linasifika kwa utesaji na unyanyasaji mkubwa dhidi ya watuhumiwa, Je Rais anatwambia kuwa leo katika nchi hii kuna Guantanamo?
Je Rais wetu anajua kuwa ahadi ya kulifunga Gereza la Guantamano ilikuwa mojawapo ya agenda kubwa zilizompatia kura nyingi Rais Barrack Obama na kupata uungwaji mkono miongoni mwa jamii ya Waislam nchini mwake?

  • Lakini la Mwisho, ni kitendo cha Rais Magufuli kufika bandarini, akakuta vichwa kumi na tano vya treni, akaambiwa havina mwenyewe, (Ilhali vina nembo ya TRL) na yeye hakuchukua hatua yoyote, huku akiwaaminisha wananchi kwamba anapambana na Ufisadi..!! Kuna ufisadi mkubwa zaidi ya huu?? Hivyo vichwa 15 vya treni vimeshuka kutoka mbinguni?
  • Suala hili ni mojawapo ya mifano inayoonesha kuwa Rais wetu ana ‘double standards’ katika kushughulikia na kuchukua hatua katika vita anayosema anapambana dhidi ya ufisadi.

Ndugu waandishi wa Habari,

  • Pili, wananchi hawakubaliani na vitendo vya wateuliwa wa Rais ambao ni Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya ambao wanafanya Uvunjaji mkubwa wa Sheria, Tararatibu na Kanuni za Nchi ama kwa maelekezo yake au kwa mbwembwe au kutaka kumridhisha  na pengine kulewa madaraka, na hapa nitaeleza mifano michache ambayo pia inadhihirisha uvunjifu wa misingi ya utumishi wa umma na maadili ya uongozi wa umma na utawala bora.
  • Mkuu wa wilaya ya Hai kwa nyakati tofauti, amevunja kanuni za maadili kwa kushambulia na kuharibu miundombinu ya shamba la Mwenyekiti wa Chama chetu Mhe. Freeman Mbowe, kinyume cha sheria ya Mazingira na muongozo wa Baraza la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) na mpaka leo hakuna hatua zozote zimechukuliwa.
  • Pili, Mkuu wa Wilaya ya Meru, kwa nyakati tofauti amewatukana na kuwadhalilisha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akawadhalilisha waandishi wa Habari na kuwambia hataki wafike kwenye Wilaya yake na bado hakuna hatua ambazo zimechukuliwa.
  • Tatu, ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ambaye alitoa amri ya kumkamata na kumuweka Mahabusu Meya wa Ubungo na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Mhe. Boniface Jacob, Kinyume cha Sheria ya Tawala za Mikoa, lakini pia DC huyu alikwenda mbali zaidi na kutaka hata Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Fredrick Sumaye naye akamatwe, hii inaonyesha kiwango cha kulewa madaraka ambacho wasadidizi wake wamelewa.
  • Nne, ni maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda kumzuia Mbunge wa Bunda Mjini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Mhe. Esther Bulaya kufanya ziara za Kibunge hadi apate kibali cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mkuu huyu wa Wilaya anasahau kauli ya bosi wake Mhe. Magufuli aliyosema wakati wakizuia mikutano ya hadhara kwamba wenye ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara ni wale waliochaguliwa tu, hili nalo Mhe. Rais hajaliona? nalo tukimwambia atakasirika?
  • Mwisho ni hatua ya Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Kutoa amri ya kumkamata na kumuweka Mahabusu Mbunge wa Kawe, Mwenyekiti wa BAWACHA na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Mhe. Halima Mdee kwa kutoa ushauri kwa Rais Magufuli huku DC huyo akiuita ushauri wa Mhe. Mdee kuwa ni Uchochezi, tunaomba Rais Magufuli awaelekeze wasaidizi wake kujua Katiba ya Nchi na kuzielewa kanuni zinazowaongoza kwani kitendo cha DC huyu wa Kinondoni ni Mbwembwe, za kumpotezea wakati Mhe. Mdee, na pia kuidhalilisha Serikali.

Ndugu waandishi wa Habari,

  • Tatu, tunataka Mhe. Rais ajue kuwa wananchi hawakubaliani na kinachoendelea bungeni dhidi ya wabunge wa upinzani maana kuna mambo yanafanyika ambayo hayakubaliki. Nitatoa mifano,
  • Mtakumbuka kauli ya Rais kwa Spika wa Bunge kuwa yeye awashughulikie Bungeni na Mhe. Rais atawashughulikia nje ya Bunge, kwa hiyo inatulazimisha kuamini kuwa, kilichofanyika dhidi ya Mhe. Mdee, Mhe. Bulaya na Mhe. Mnyika ni ushahidi wa wazi wa  utekelezaji wa Maagizo ya Mhe. Rais kwa Spika wa Bunge .
  • Mtakumbuka pia kwamba, juzi mbunge wa Viti Maalum wa CCM Juliana Shonza aliwatukana na kuwadhalilisha wabunge wa UKAWA, lakini cha ajabu, Spika wa Bunge alitoa tamko la kuwakamata wabunge ambao wengine hawakuwepo Dodoma (Cecil Mwambe), hii ni ishara ya chuki za wazi dhidi ya wapinzani na ni jambo ambalo watanzania hawakubaliani nalo kabisa.
  • Mbunge wa Ukonga, na Mwenyekiti wa Dar es Salaam Kuu, Mhe. Mwita Waitara ameitwa kuhojiwa na Polisi Mkoani Dodoma kwa kuandaa futari wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, Leo tunahitajika kupata kibali cha Serikali kuandaa ibada?

HITIMISHO:
BAVICHA tunasema yafuatayo, kwanza tunaunga mkono kauli iliyotolewa na Baraza la Wazee wa CHADEMA kulaani kauli ya Rais Mstaafu wa Awamu ya pili Ali Hassani Mwinyi ambayo ilikuwa inachochea uvunjaji wa Katiba ya Nchi na kumuongezea muda wa kuongoza kinyume cha Katiba ya Nchi.
Pili, tunaunga mkono kauli ya Mwenyekiti wa BAWACHA na Mjumbe wa Kamati Kuu kuhusu wasichana wanaopata Ujauzito kupata haki yao ya Elimu na kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kufuata sheria na kanuni za Utumishi wa Umma.
Tatu, BAVICHA tunamshauri Rais Magufuli kuwa Nchi inavimba, na inaendelea kuvimba, na hatua za kuzuia kuvimba huku zisipochukuliwa, ni wazi hatutakuwa salama kabisa katika taifa hili.
Tunamshauri Rais Magufuli kwamba, anapofurahia kupongezwa, akubali pia kukosolewa, akubali kushauriwa na akubali kupokea maoni, fikra na mawazo mbadala kwani hayo ndiyo hujenga nchi moja na mshikamano na Umoja wa kitaifa.
Tunamtaka Rais Magufuli ajitokeze hadharani kukemea na kuwachukulia hatua wateule wake wanaotumia madaraka yao vibaya kama nilivyoonesha hapo juu, ili Watanzania wajue kuwa haya yanayofanyika si maelekezo yake ili kupunguza manung’uniko ya wananchi ambayo yanaifanya nchi kuendelea kuvimba kwa sababu wanyonge wananyongwa na hawana pa kusemea wala kupumulia.
Tunamtaka pia atambue kuwa haya yanayofanywa na wateule wake kuvunja Katiba, Sheria, Kanuni na taratibu za nchi au washauri wake kumshauri kumridhisha, ni matokeo ya kukosa maelekezo, ikiwa ni pamoja na semina elekezi na mafunzo ya kiuongozi ambayo yamepigwa marufuku kwenye serikali hii ya CCM awamu ya tano.   
Tunatoa wito kwa Watanzaniam hususan vijana, kuanza maandalizi na kuunga mkono kwa vitendo kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, aliyoitoa ndani ya bunge kuwa ni wakati wa Watanzania kurejesha Vita ya Majimaji kwa silaha ya kadi ya kupigia kura ili kuiondoa CCM madarakani.
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki CHADEMA
Imetolewa Leo, 05, July 2017
…………………..
Julius Mwita
Katibu Mkuu – BAVICHA.

Share Button
Layout Settings