BARAZA LA WAZEE WA CHADEMA: TAARIFA ILIYOSOMWA MBELE YA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 13/03/2018

BARAZA LA WAZEE WA CHADEMA
TAARIFA ILIYOSOMWA MBELE YA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 13/03/2018
 
Ndugu wanahabari
 
Baada ya tafakuri ya kina kuhusu mwenendo wa hali ya kisiasa nchini na na kuona hatari kubwa inayoikabili nchi yetu, Baraza la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tumeona tubebe jukumu la kutuma ujumbe wenye ushauri kwa Rais John Pombe Magufuli ili achukue hatua za haraka kuinusuru nchi isiyumbe na kutumbukia katika janga la kisiasa.
 
Tulipokutana na ninyi kwenye mkutano kama huu wakati wa kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani, Oktoba 1, mwaka jana, tulitumia fursa hiyo kutoa ushauri wetu kwa Rais John Magufuli, juu ya mwenendo wa masuala mbalimbali nchini ambayo yalikuwa yamesababisha sintofahamu kubwa kwa Watanzania, ndani na nje ya nchi.
 
Hali hiyo mtambuka ilikuwa inahusisha mwenendo wa nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii, ikiwa ni mjumuiko wa kauli na matendo ambayo sisi kama Wazee tuliona kuwa yakiachwa kuendelea bila kutafutiwa ufumbuzi, yatakuwa na athari kubwa kwa taifa letu na kuiweka jamii nzima katika hatari kubwa inayoweza hata kusababisha vurugu au machafuko ya kisiasa kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia katika nchi zingine.
 
Tulisema kuwa tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya CCM ya awamu ya tano, kumekuwa na mwenendo ulio kinyume na misingi imara ya amani, utulivu na maendeleo.
 
Tuliitaja baadhi ya misingi hiyo kuwa ni; HAKI na MATUMAINI ya watu kwa viongozi wao, uwepo wa demokrasia na utawala bora unaozingatia Katiba, Sheria na taratibu zingine zinazosimamia dhamana ya kuongoza nchi kwa niaba ya wananchi wote.
 
Tulitoa mifano michache ambayo ilikuwa inashadidia hoja zetu, ambayo ilikuwa ni;
 
1. Kukamatwa, kubambikiwa kesi, kuteswa, kutekwa, kushambuliwa na hata kuuwawa kwa viongozi wa kisiasa na wananchi wengine wanaoonekana kukosoa utendaji kazi wa Rais Magufuli na Serikali.
 
Tulifanya rejea ya matukio kama ya kushambuliwa kwa kukusudia kumuua Mbunge na Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Mhe. Tundu Lissu, kuuwawa kwa aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa CUF Jimbo la Mtopepo, Ali Juma Suleiman.
 
2. Miili ya watu waliouwawa kuokotwa katika fukwe za Bahari ya Hindi hapa kwetu huku Serikali ikitoa maelezo tatanishi na taarifa zisizotoa majawabu ya maswali wanayohoji Watanzania juu ya jambo hilo geni kabisa hapa nchini.
 
3. Kuminywa kwa haki za kikatiba na kisiasa, kinyume kabisa na sheria za nchi yetu, mf; kuzuiwa kwa shughuli za kisiasa ambazo zipo kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi.
 
4. Kuminywa kwa uhuru wa maoni na kupata taarifa, mathalani; kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara, maandamano, Bunge live, kufutwa na kufungiwa kwa magazeti yanayoandika habari za kumkosoa Rais na Serikali yake.
 
5. Mhimili wa dola kuingilia mihimili mingine ya Serikali yaani bunge na mahakama.
 
6. Kauli na matendo tata, yenye kuvunja sheria za nchi kutoka kwa Mhe. Rais na wakuu wa mikoa na wilaya.
 
*Hali inazidi kuwa mbaya, hakuna aliye salama*
 
Ndugu wanahabari, ndani ya miezi sita tangu tulipozungumza hayo, hali imezidi na inazidi kuwa mbaya zaidi karibu kila siku kunapokucha. 
 
Kama ni matukio ya kutekwa, kuteswa, kuuwawa au vitisho vya kutekwa na kuuwawa, hasa kwa watu wanaoonekana kutoa mawazo mbadala na kuikosoa Serikali ya Rais Magufuli na viongozi wake, yameongezeka zaidi. 
 
Mtakumbuka matukio ya hivi karibuni kabisa ya kutekwa, kuteswa kwa Daniely John na mwenzake Godfrey Malya kisha kuuwawa kwa Daniely ambaye alikuwa Katibu wa CHADEMA Kata ya Hananasif, kutekwa na kuteswa kwa mgombea wa CHADEMA wa Udiwani Kata ya Buhangaza, Muleba, Ndugu Nelson Makoti, na kutekwa kwa Abdul Nondo, Kiongozi wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, kupotea kwa Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, kuuwawa kinyama kwa Diwani wa CHADEMA Godfrey Luena wa Kata ya Namwawala Kilombero. Mifano ni mingi mno.
 
Idadi ya miili ya watu wanaookotwa fukweni wakiwa wameuwawa inazidi kuongezeka. Hatuoni hatua zozote za kusaidia kujulikana chanzo na wahusika wa unyama huo na kuudhibiti. Tunajiuliza, walioko madarakani wanaona kuwa hii ni mizoga tu?
 
Haki za msingi kabisa za kikatiba na kisiasa, ikiwemo watu kukusanyika na kutoa maoni yao bado zinakandamizwa na kusiginwa wazi wazi mchana kweupe kama vile ni jambo la kawaida tu. Ukandamizaji huo unashereheshwa na kauli na matendo ya viongozi wa serikali ambao kimsingi walipaswa kuwa mstari wa mbele kabisa kuzilinda kwa sababu ndiyo msingi wa kiapo chao cha dhamana ya kutuongoza.
 
Sambamba na hayo, uhuru wa mihimili ya Bunge na Mahakama kuwatumikia wananchi bila kuingiliwa, unazidi kuwa shakani. Hivyo sintofahamu iliyokuwepo miezi sita iliyopita, imeongezeka na hali inaonesha kuwa tunakoelekea siyo kuzuri. 
 
Hivyo ni wajibu wetu kama Baraza la Wazee kutoa ushauri wa kulinusuru Taifa letu, yamkini ushauri wetu utapokelewa.
 
*Ushauri wetu kwa Rais*
 
Ndugu wanahabari
 
Pamoja na hali hii kutishia mstakabali wa taifa hili, bado hatuoni jitihada za wenye dhamana kufumbua macho na kufungua masikio yao na kutafuta suluhu ya pamoja kama taifa.
 
Tunazidi kusikia tambo za wasaidizi wa Mhe. Rais Magufuli (wakiwemo wakuu wa mikoa na mawaziri) na yeye mwenyewe za kubeza, kupuuza na hata kutoa kauli za vitisho badala ya kusikiliza maoni, ushauri na hisia za watu na kushughulikia sababu za ‘kelele’ wanazozisikia, badala ya kutoa vitisho dhidi ya ‘wapiga kelele’ na kujiandaa kuwashughulikia.
 
Watambue tu ndimi zao zinaweza kutumika kama ushahidi kwenye Mahakama ya ICC, The Hague, iwapo zitasababisha uhalifu dhidi ya ubinadamu, kama ambavyo imewahi kutokea kwa wasaidizi wengine wa viongozi wakuu wa nchi ambao ndimi zao zilisababisha matendo ya kihalifu na wakajikuta kizimbani.
 
Taifa letu linapita katika kipindi kigumu na majaribu makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Nchi inazidi kuvimba na watu wanahitaji kupumua. Ni muhimu wenye dhamana walione hili. Ni lazima kama taifa, tuchukue hatua mapema kabla hatujachelewa. Hasa ya kusikilizana katika tofauti za kimawazo na mitazamo, almuradi kila mtu akitambua kuwa sote tunataka kujenga nchi moja. 
 
Katika hatua ya sasa, Baraza la Wazee wa CHADEMA tunashauri ifuatavyo;
 
1. Rais Magufuli ambaye ni Mzee mwenzetu, aongozwe na busara za kiuongozi na hekima za uzee, akubali na kuitikia wito wetu wa (yeye) kukutana na Wazee katika kikao cha pamoja ambao watakuwa na ujasiri wa kumshauri na kumwambia ukweli ili tuiepushe Tanzania isielekee kwenye hatari kubwa inayotukabili.
 
2. Awe tayari kusikiliza na kupokea ushauri na ukosoaji wao kama ambavyo amekuwa akifurahia kupokea hongera.
 
3. Wazee hao ni pamoja na; Viongozi wa dini mbalimbali wastaafu, Viongozi wa Serikali wastaafu na Wazee kutoka vyama vya siasa.
 
4. Wazee wastaafu ndani ya nchi yetu wasimame imara na kujitokeza hadharani kukemea mwenendo mbaya wan chi yetu ikiwemo ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ukiukwaji wa Katiba na Sheria za Nchi pamoja na kauli na matendo mabaya yanayoivimbisha nchi kwa sasa. Kwani nchi ikipasuka, ukimya wao itakuwa ni hukumu kwao.
 
5. Kwa ajili ya kutibu majeraha na kuondoa makovu yanayosababishwa na mwenendo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini, suluhu ya kudumu ambayo italiweka taifa pamoja na kupata mwafaka wa kitaifa, inahitajika, nayo
ni KATIBA MPYA.
 
KATIBU MKUU BARAZA LA WAZEE TAIFA
 
RODERICK LUTEMBEKA
Share Button
Layout Settings