Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kuwaarifu viongozi, wanachama, na umma wa Watanzania juu ya hali ya hatari inayojitokeza kwa kasi dhidi ya vyama vya siasa vinavyopigania mabadiliko ya kweli nchini. Hali hii inaashiria juhudi za kurejea kwa enzi za utawala wa kiimla unaotumia Vyombo vya Dola na Mahakama kama zana za kukandamiza sauti mbadala, badala ya kulinda haki za wananchi na utawala wa sheria.
Kwanza, tunaendelea kushuhudia njama zilizo wazi zinazoratibiwa kupitia ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na watu waliopoteza uhalali wa kisiasa. Kupitia kesi isiyo na msingi, ni dhahiri kuwa kuna njama za makusudi za kuingilia, kuchafua, na kuvuruga uongozi halali wa Chadema kwa lengo la kuua Operesheni yetu ya No Reforms, No Election (bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi), harakati za kidemokrasia zinazodai mazingira huru na haki ya uchaguzi.
Pili, tumekuwa mashuhuda wa kilele cha siasa za vurugu na hujuma dhidi ya mikutano yetu ya hadhara. Kwa maelekezo ya wazi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Polisi wamekuwa wakilazimisha kubadili viwanja vya mikutano, wakurugenzi wa halmashauri wakitunyima tusitumie viwanja tunavyoomba hata baada ya kupokea malipo kutoka kwetu kwa madai yasiyo halali, na kuendesha shughuli ambazo hazikuwa kwenye mipango yao. Zaidi ya hayo, makundi ya vijana wasio na ajira yamekuwa yakitumika kuleta vurugu, kuwatisha wananchi, na kujaribu kuzima ujumbe wa matumaini na mabadiliko tunayoueneza nchi nzima.
Tatu, leo tarehe 10 Juni 2025, katika hatua ya wazi ya kuingilia uhuru wa kisiasa wa Vyama, Mahakama chini ya Jaji Hamidu Mwanga imetoa amri ya kusitisha kwa muda wa siku 14 shughuli za kisiasa za Chadema, kutokana na kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar kwa miaka 15, Bw. Saidi Issa Mohammed, pamoja na
wenzake wawili, wajumbe wa bodi ya udhamini ya chama. Jaji alitoa uamuzi huu bila Chama kuwa na mawakili wake baada ya wakili wetu, Jebra Kambole, kujitoa kutokana na kuhisi kutotendewa haki. Jebra Kambole aliomba kusitishwa kwa kesi hadi Chama kitakapopata wakili mwingine, lakini Jaji alikataa na kuendelea kusikiliza kesi kwa upande mmoja tu na kutoa uamuzi wake. Kwa mtazamo wetu, uamuzi huu umechochewa zaidi na shinikizo la kisiasa badala ya msingi wa kisheria au haki, huku ukizingatia hali ya kisiasa ilivyo nchini mwetu.
Chadema inachukulia hatua hizi kama ishara hatari ya kuporomoka kwa demokrasia nchini. Viongozi wa chama watafanya mkutano wa dharura kutathmini hali hii na kuamua msimamo rasmi wa chama kuhusu hatua za kuchukua.
Tunatoa wito kwa viongozi, wanachama, wafuasi wetu, na Watanzania wote wanaoamini katika misingi ya uhuru, haki, na demokrasia, kuwa tayari kupokea maelekezo kutoka kwa viongozi wakuu wa chama.Hatutarudi nyuma katika kudai Tanzania yenye mfumo wa haki, uhuru, na utawala wa sheria.
© Copyright 2025. Developed By: CHADEMA
Leave A Reply