CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinapenda kutuma salaam za pongezi na hongera nyingi kwa Chama Rafiki cha Malawi Congress Party (MCP) pamoja na mgombea wake wa nafasi ya urais, Lazarus Chakwera, kwa kushinda kura za marudio ya uchaguzi wa rais, baada ya uchaguzi wa awali kubatilishwa na Mahakama Kuu ya Malawi, kufuatia kasoro zilizoufanya usiwe huru na haki.

Aidha, Chadema inatoa salaam za pongezi nyingi na dhati kwa wapiga kura wa Malawi. Wao ndiyo wadau wakubwa wa uchaguzi na ushindi huo, ambao kwa hakika umepatikana kwa nguvu ya umma. Wananchi wa Malawi walipigania haki ya kuwa na uchaguzi ulio huru na haki, kwa njia mbalimbali, ikiwemo kufanya maandamano makubwa na kupaza sauti zao kila mahali bila kuchoka kupinga ukandamizwaji wa demokrasia, hususan haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa, kupitia sanduku la kura.

Halikadhalika, Chadema inatoa pongezi kwa taasisi za nchi hiyo, zikiwemo Mahakama, Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Ulinzi na Jeshi la Polisi, zilizosimama imara kuhakikisha haki ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka kwa mujibu wa sheria, si tu inatendeka, bali inaonekana ikitendeka.

Katika kuhakikisha haki na uhuru wa wananchi unalindwa na kuheshimiwa, tulishuhudia wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wakisimamia matakwa ya wananchi na nchi, badala ya kulinda maslahi ya chama kilichoko madarakani na yao binafsi. Hata kama iliwalazimu ama kujiuzulu au kufukuzwa kazi, kwa sababu waliamini ukuu na mamlaka ya nchi yanatoka kwa umma.

Mambo yote yaliyotokea hasa katika kusimamia utendekaji wa haki, maslahi na matakwa ya wananchi huku vyombo vya dola vikiheshimu na kujiepusha kupendelea upande wowote, iwe funzo kwa vyombo na mihimili katika nchi zingine za Bara la Afrika, hususan kwa nchi zitakazofanya uchaguzi mkuu mwaka huu, ikiwemo nchi yetu ya Tanzania.

Chama cha MCP na Chadema ni vyama marafiki katika familia ya Muungano wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (International Democratic Union-IDU) pia kupitia Muungano wa Vyama vya Kidemokrasia Afrika (Democratic Union of Africa-DUA).

Kutokana kuwa na imani sawa kwenye misingi ya demokrasia, ikiwemo uhuru wa watu, haki za binadamu na utawala bora unaozingatia sheria, kuwa ndiyo nguzo imara za maendeleo na ustawi wa watu, Chadema na MCP vimekuwa na ushirikiano wa kikazi wa muda mrefu, kupitia njia mbalimbali, ikiwemo vikao.

Chadema inawatakia kila la heri MCP pamoja na Rais Mteule Lazarus Chakwera wanapoanza safari ya kutafsiri kwa vitendo imani hiyo ya demokrasia katika kuunda serikali, kushika dola na kuongoza nchi kwa niaba ya wananchi wa Malawi.

Chadema inawahakikishia ushirikiano kwa wakati wote wa uongozi wao ili kudumisha uhusiano mwema si tu wa nchi na nchi, bali pia baina ya wananchi wa nchi hizi mbili ambao wengine ni ndugu wa damu au kabila moja.

Imetolewa leo, Jumapili, Juni 28, 2020 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
Chadema

Share Button