HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA, MHESHIMIWA DAVID ERNEST SILINDE (MB), AKIWASILISHA MAPITIO YA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020 PAMOJA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZIKWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,Toleo la Januari, 2016

_____________________

  1. UTANGULIZI
  2. Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunijalia uhai, afya njema na   kunipa nguvu na uwezo wa kusimama mbele ya Bunge lako tukufu ili kutoa maoni ya Kambi  Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na makadirio ya mapato na matumizi  kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa naomba kutoa shukrani kwa KUB kwa imani yake kwangu na kuniteua kuwa Msimamizi na msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa wizara hii ya Viwanda na Biashara.
  4. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mujibu wa hati idhini iliyotolewa na Serikali tarehe 22 April, 2016 ilipewa dhamana ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera, maendeleo ya viwanda, biashara na Masoko. Aidha pamoja na majukumu mengine ndiyo wizara inayotakiwa kuhakikisha kuwa Tanzania ya viwanda inapatikana kama kauli mbiu ya awamu ya pili ya Mpango wa miaka mitano wa maendeleo ya Taifa.
  5. Mheshimiwa Spika, wizara hii pia isimamia mashirika matano ambayo ni shirika la Maendeleo la Taifa (National Development Corporation – NDC) Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (Small Industries Development Organization SIDO,) Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tanzania Industrial Research Development Organization TIRDO) shirika la Uhandisi na Usanifu wa Mitambo Tanzania TEMDO na Shirika la Viwango Tanzania TBS. Wizara inakituo cha kuendeleza Teknlojia, biashara na uwekezaji kinachojulikana kama kituo cha zana za kilimo na Teknlojia vijijini , wakala za vipimo na Usajili wa Biashara na Leseni, Mamlaka za kuzalisha bidhaa na kuuza nje yaani Export Processing zone Authority na Maendeleo ya Biashara Tanzania, yaani Tanzania Trade Development Authority- TANTRADE. Mabaraza ya ushindani, Fair Competition Tribunal na baraza la utetezi wa Haki za Mlaji. Hotuba yangu inajielekeza kuangazia ufanisi wa kiutendaji kwa wizara hii kwa kuzingatia majukumu kama yalivyoidhinishwa na hati idhini ya Serikali.  

 

  1. MAPITIO YA MWENENDO WA UTEKELEZAJI BAJETI YA MAENDELEO YA WIZARA

 

  1. Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2014/2015 Wizara ilitengewa shilingi 111,958,354,000.00 kati ya hizo shilingi 33,356,643,000 ni matumizi ya kawaida na shilingi 78,601,711,000 ni matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia April, 2015 Wizara ilikuwa imepokea shilingi 93,185,222,288 sawa na 82% ya fedha zilizotengwa ikiwa shilingi 27,905,758,188 ni za matumizi ya kawaida na shilingi 65,279,464,100 ni za matumizi ya maendeleo.
  2. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2015/2016,  Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji ilitengewa jumla ya shilingi 87,470,349,000 kati ya fedha hizo shilingi 52,082,968,000 zilitengwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 35,387,381,000 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
  3. Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia mwezi Machi, 2016, kati ya Shilingi 35,387,381,000 zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Shilingi 1,602,111,662 ndizo zilikuwa zimepokelewa na Wizara kutoka hazina, sawa na asilimia 5 tu ya fedha zote zilizotengwa. Fedha za ndani zilikuwa ni shilingi Zero na Fedha zote zilikuwa ni fedha za nje tu.

 

  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ilitengewa jumla ya shilingi 95,694,775,495 kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya Wizara. Kati ya fedha hizo shilingi 53,534,825,495 sawa na asilimia 56 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 42,159,950,000 sawa na asilimia 44 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/18 Wizara fungu 44 ilitengewa jumla ya shilingi 122,215,109,750; kati ya hizo shilingi 73,840,377,000 ni fedha za maendeleo. Lakini  hadi mwezi Machi 2018 wizara ilikuwa imepokea fedha za maendeleo jumla ya shilingi 7,000,000,000 tu sawa na asilimia 9.51.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 wizara fungu 44 iliomba kuhidhinishiwa jumla ya shilingi 117,287,008,000; kati ya fedha hizo fedha za miradi ya maendeleo ni shilingi 93,024,525,000. Maombi hayo yalikuwa  ni ongezeko la shilingi 19,184,148,000; kwa kulinganisha na fedha za maendeleo zilizotengwa mwaka wa fedha 2017/18, japokuwa fedha zilizotolewa kwa bajeti ya 2017/18 ilikuwa ni asilimia 9.51 tu.

 

  1. Mheshimiwa spika, kwa mwaka wa fedha 2018/2019, Fungu 44 & Fungu 60 ilitengewa jumla ya shilingi100,024,525,000 kwa matumizi ya maendeleo sawa na 70% ya bajeti yote ya wizara hii kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Kati ya fedha hizo, Shilingi 90,500,000,000.00 zilikuwa na shilingi 2,524,525,000.00 zilikuwa ni fedha za nje. Hadi kufikia mwezi machi, 2019 kati ya Shilingi 90,500,000,000.00 zilizokuwa zimetengwa Wizara ilikuwa imepokea Shilingi 6,477,221,314.00 sawa na 6.5 % ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo, kutoka ndani kwa Fungu 44, wakati fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo kutoka Fungu 60, zilikuwa ni Shilingi 7,000,000,000.00 na hadi kufikia mwezi Machi, 2019 hazina ilikuwa imetoa shilingi 0.00 sawa na 0% ya fedha za maendeleo kwa fungu 60.

 

  1. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/20 wizara iliidhinishiwa jumla ya shilingi 51,500,000,000.00 zikiwa ni fedha za maendeleo, lakini hadi februari 2020 hakuna hata shilingi iliyokuwa imetolewa. Ukiangalia Randama ya mwaka 2020/21 uk 23 kielelezo na.2 kina mgawanyo mzuri sana wa fedha za maendeleo kwa mfumo wa asilimia kwa kila taasisi, lakini kwa bahati mbaya sana nguvu na muda viliyotumika kuandaa kazi hiyo ni zero. Kwani hakuna hata shilingi iliyotolewa na Hazina.
  2. Mheshimiwa Spika, imetulazimu kutoa muendeleo wa utolewaji wa fedha za miradi ya maendeleo kwa wizara ili kuonesha ni kwa jinsi gani Serikali ya CCM isivyoweza kutembea kwenye kauli zake. Hiyo Tanzania ya Viwanda inatoka wapi kama fedha za maendeleo kwa Wizara ya Viwanda hazitolewi?
  3. Mheshimiwa Spika, Kwa nyakati tofauti serikali ya awamu ya tano imejinasibu kwamba imedhamilia kujenga uchumi wa viwanda ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Hata hivyo inaelekea kwamba kauli za serikali ni maneno tu, kwa vile hayaendani na uhalisia, uchumi wa viwanda hauwezi kujengwa kwa maneno matupu bila vitendo.
  4. Mheshimiwa Spika, Matokeo ya Serikali inayojinasibu kujenga Tanzania ya uchumi wa Viwanda kushindwa kutoa fedha za maendeleo kwa miradi mbalimbali iliyo chini ya wizara ya Viwanda na Biashara, kumesababisha miradi mingi iliyokuwa imepangwa kutekelezwa kwa minne kushindwa kutekelezeka na hivyo kuathiri maisha ya watanzania ambao pamoja na mambo mengine walitarajiwa kupata ajira kutoka katika miradi hiyo.
  5. Mheshimiwa Spika, Hii ndiyo maana halisi ya madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba Bajeti za Serikali ya awamu ya tano zimekuwa ni Bajeti hewa zenye lengo la kuwalaghai watanzania. Miradi iliyotarajiwa kutekelezwa kwa bajeti hiyo hewa, ambayo kwa vyovyote vile itakuwa imeathirika na vitendo cha Serikali kutotekeleza Bajeti yake, ni pamoja na Mradi wa Makaa ya mawe Mchuchuma na Liganga, Special Economic Zone za Bagamoyo, Benjamini Mkapa, EPZ Development, Kurasini SEZ,EPZ katika mikoa ya Kigoma Tanga, Manyara,  Mara, Ruvuma, kiwanda cha matairi Arusha, Leather Value Addition-Dodoma Cluster na Lake Natron/Engaruka ni miongoni mwa miradi ambayo watanzania waliaminishwa kwamba ni vipaumbele vilivyozingatiwa katika matumizi ya fedha za Maendeleo.

 

  1. Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitika sana kuona kuwa wale ambao wanapewa kusimamia wizara hii baada ya kukosa au kunyimwa bajeti ya kusimamia miradi ya maendeleo, waliamua kuwa vituko kwa kuwa watu wa propaganda na wachekeshaji ili kuficha hali halisi ilivyo mbaya kwenye wizara hii. Ukweli mara zote una tabia ya kujiweka wazi hata kama utafichwa kwa kutumia nguvu kiasi gani.

 

 

  1. KUFUNGAMANISHA KILIMO NA MAENDELEO YA VIWANDA (AGRO ECONOMY)

 

  1. Mheshimiwa Spika, Katika bajeti ya serikali 2018/2019 iliainisha sekta ya kilimo kama kipaumbele cha serikali lakini haijaonyesha ni kwa namna gani hasa inalenga kufanya Mapinduzi ya Kilimo (Agrarian Revolution) ili kuweza kusisimua na sekta ya viwanda
  2. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya Mpango ya Waziri inaonesha kuwa  mchango katika sekta za kiuchumi katika Pato la Taifa  kilimo kilichangia asilimia 30.1 mwaka 2017 huku Sekta hiyo  inachangia  hutoaji wa ajira kwa asilimia 66, lakini ukuaji wake  ni  wa wastani wa asilimia 3.7. Katika kujiuliza sekta hiyo ambayo inatoa ajira asilimia 66 inachangia mapato ya kodi kiasi gani?
  3. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuangalia unyeti wa sekta hii katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati na uchumi wa viwanda ni lazima sekta ya kilimo iwe ndiyo ingine ya kutupeleka huko. Hivyo basi, pamoja na mambo mengine Kambi Rasmi ya Upinzani italenga kuondoa kodi zote kwenye uwekezaji katika sekta ya kilimo (kilimo,uvuvi na mifugo).
  4. Mheshimiwa Spika, viwanda mia mbili(200) kila mkoa alivyosema Mheshimiwa waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI nusu au robo yake vingeweza kupatikana kama tu wizara ya Viwanda na Biashara ingeweka mpango mzuri wa kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa kwa kuhamasisha kilimo kinakuwa cha kisasa zaidi katika uzalishaji wake na hivyo viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo vingefunguliwa maeneo mengi ya nchi yetu.
  5. Mheshimiwa Spika, ni ukweli pia, Tanzania ya viwanda ni lazima itokane na viwanda vinavyojihusisha na uchakataji wa mazao ya kilimo au vinavyojihusisha na utengenezaji wa vifaa vinavyotumika katika kilimo.
  6. Mheshimiwa Spika, hii ni pamoja na kuondoa kodi kwenye uingizaji wa mashine mbalimbali zinazoingia katika mnyororo wa uongezaji thamani wa bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda vinavyotengeneza na kukarabati mashine na zana nyingine za kilimo kama vile matrekta, pampu za umwagiliaji, mashine za uvunaji, viwanda vya kutengeneza madawa, mbolea, mbegu,na vifungashio, zana za uvuvi kama vile mitumbwi, nyavu, na zana nyingine za uvuaji. Katika mifugo itahakikisha kodi za mifugo zinaondolewa, na kodi za viwanda vinavyotengeneza madawa na chanjo mbalimbali za mifugo, pamoja na kupunguza kodi katika viwanda vya kuongeza thamani za mazao.
  7. Mheshimiwa Spika, Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini – (CAMARTEC) kinashindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi na hivyo kutengeneza na kuuza zana zake kwa bei himilivu, hivyo ni muhimu sana Wizara kutenga bajeti ya kutosha ambayo itawawezesha kutosheleza asilimia kubwa ya gharama za uzalishaji jambo litakalowawezesha kuuza bidhaa zao kwa gharama nafuu na kuwanufaisha watu wa hali zote katika mnyororo wa thamani wa bidhaa za kilimo.
  8. Mheshimiwa Spika, Dhana ya kuanzisha kituo cha CAMARTEC iliwalenga watanzania wa hali ya chini kwa kuzalisha zana za kilimo na teknolojia vijijini, lakini zana zinazotengenezwa na kituo kwa sasa zimekuwa na gharama ya juu hivyo walengwa wameshindwa kuzimudu na hivyo kupoteza maana halisi ya uanzishwaji wake.
  9. Mheshimiwa Spika, Shughuli za kilimo zinahusisha mnyororo wa thamani mrefu mpaka bidhaa kumfikia mlaji sokoni, kwa lengo la kuwasidia wakulima wetu na kulinda ubora wa mazao yao. CAMARTEC kuwezeshwa vyema inaweza kuwa ndio chimbuko sahihi la uchumi wa viwanda katika kuzalisha zana/mashine ambazo zitamsaidia mkulima kuanzia hatua ya kuandaa shamba, kulima, kuvuna, kuongeza thamani na mwisho kufika kwa mlaji.
  10. Mheshimiwa Spika, Randama uk wa 29 aya ya d inasema kuhusu viwanda vinavyojihusisha na na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na chuma hapa nchini kuwa ni viwanda 25. Lakini kwa bahati mbaya ni kuwa viwanda hivyo vyote vinapata malighafi zake kutoka nje, lakini pia chuma chakavu kinachopatikana humu humu nchini.
  11. Mheshimiwa Spika, jambo hili la kutumia chuma chakavu ni fikirishi sana, kwani bidhaa hizo zinazozalisihwa kwa chuma chakavu ni kweli zinaweza kuuzwa nje ya Tanzania? Wateja wanalalamika kuhusu na ubora hafifu wa bidhaa zetu kumbe tatizo ni malighafi zinazotumika. Pia jambo hili ni sababu ambayo inasababisha bidhaa zetu zisiweze kuwa shindani katika masoko ya kimataifa.
  12. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inafahamu kuwa mradi wa Chuma wa Liganga na Mchuchuma ndio ambao ungekuwa unatoa malighafi kwa viwanda vya ndani vya chuma, hivyo fedha za kigeni zinazotumika kuagiza malighafi za viwanda zingekuwa zinabakia hapa hapa nchini na kwa minajili hiyo tusingekuwa tunazalisha bidhaa ambazo ubora wake unatiliwa mashaka katika soko la nje kutokana na matumizi ya chuma chakavu.
  13. Mheshimiwa Spika, ni muda mwafaka sasa, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha mradi wa chuma wa Liganga na Mchuchuma unaanza kuzalisha ili miradi yote ambayo inatumia chuma iweze kutekelezwa kwa kutumia chuma tunachozalisha wenyewe badala ya kuagiza nje chuma kwa ajili ya matumizi yetu ya ndani.
  14. BIASHARA YA SUKARI
  15. Mheshimiwa Spika, kumekuwapo na matatizo makubwa kwa Serikali kurejesha fedha za ongezeko la thamani ya bidhaa (VAT 18) na rejesho ya 15% ya Sukari ya viwandani (15% return of industrial sugar). Fedha hizo hazirudishi kwa Wafanyabiashara kama inavyotakiwa jambo ambalo ni kinyume na Sheria.
  16. Mheshimiwa Spika, Kutokurudi kwa fedha za VAT na 15 % Sukari ya Viwandani ni changamoto ya muda mrefu takribani miaka 5 sasa jambo ambalo linapelekea kupungua kwa mitaji ya wenye viwanda na pia kuongeza gharama za uzalishaji ambapo mwisho wa siku inapelekea viwanda husika kupunguza wafanyakazi ili kufidia gharama za uzalishaji.
  17. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza kwa mtindo huo, Kuna haja ya kutafuta sababu ya kiini cha bidhaa za nchini kushindwa kushindana na bidhaa za nje? Au kiini cha wafanyabiashara kuishiwa mitaji na wafanyakazi kupunguzwa katika ajira rasmi?
  18. Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba viwanda vyetu vingi vya ndani havizalishi sukari ya viwandani lakini viwanda hivyo ndivyo vinaagiza sukari hiyo toka nje na kuviuzia viwanda vyetu vya ndani. Katika mzunguko huo ni dhahiri kuwa mitaji yao inazungushwa sana na inapotokea Serikali inashindwa kurejesha fedha za VAT na zile 15%. Maana yake ni kuwa viwanda vinakosa uwezo wa kufanya uwekezaji wake.
  19. Mheshimiwa Spika, ukipitia randama zote mbili kwa fungu 43 ya wizara ya kilimo na hii fungu 44 viwanda na biashara kwa suala la sukari inaonesha kuwa tatizo moja wapo la upungufu wa uzalishaji ni kutokana na uchakavu wa mitambo na hivyo kushindwa kupokea mzigo mkubwa wa miwa au na matatizo mengine yahusuyo mitambo.
  20. Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi rasmi ya Upinzani inazidi kusisitiza kuwa ni muda mwafaka kuhakikisha wanaoidai Serikali kurudishiwa fedha hizo ili kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya sukari kuwa na uwezo wa kupokea mzigo wa kutosha kutoka kwenye mashamba ya sukari yanayohamsishwa kufunguliwa.

Historia fupi ya bei ya sukari

  1. Mheshimiwa Spika, hakuna ambaye hafanyi matumizi ya Sukari nyumbani kwake Sukari inatumiwa kila nyumba ya Mtanzania Kwa maana hiyo Sukari ni muhimu Sana kwenye maisha ya kila siku hapa nimekusogezea japo Kwa uchache historia ya bei ya sukari tangu mwaka 1998 – 2020.
  2. Mheshimiwa Spika, mwaka 1998 Sukari ilikuwa inauzwa shilingi  500/- kwa kilo  na nusu kilo kwa shilingi 250. Mwaka  2000 Sukari ilikuwa inauzwa  shilingi  800/- kwa kilo.  Miaka ya 2005-hadi 2008 ilikuwa inauzwa shilingi 850/-,900/- na 950/- hapa wananchi pia walilalamika Ila Kwa kiwango kidogo Kwa kuwa Uchumi wa wananchi  ulikuwa sio mbaya kuweza kumudu.
  3. Mheshimiwa Spika, Sukari kwa miaka ya 2010-2011-2012 Hadi na 2014 sukari ilikuwa inauzwa shilingi 1000/-,1,100/- hadi shilingi 1,200/- hadi inapanda kutokea hapo bei kubwa ya Sukari,kipindi hiki watu walilalamika Sukari kuuzwa bei hizo. Mwaka 2015 sukali ilikwenda hadi ikauzwa shilingi 1,500/-  1,600/- bei hizo zilienda  hadi mwaka 2016 na 2017 sukari ikapanda bei na kuwa  shilingi 1,700/-  hadi 1,800/- kwa kilo. Kwa mwaka  2018-2019 Sukari ikawa inauzwa 2,500 tena ikawa imehadimika sana hadi msako maalum kwenye maghala ya wafanyabiashara yakawa yanapekuliwa ili kutafuta sukari iliyofichwa.
  4. Mheshimiwa Spika, Mara zote hizo upandaji wa bidhaa ya Sukari huwa unakuwa upo kwenye misimu ya sikuu na kipindi cha mfungo wa mwezi wa ramadhani mwaka huu 2020 Sukari imevunja rekodi Kwa kuuzwa kati ya shilingi  3000/-,3500/-,4000/-,4,500/- na 5,000/- Kwa kilo moja katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
  5. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza, kama uzalishaji wa ndani upon a pia kuna ziada inaagizwa kutoka nje ni kwanini sukari inaadimika kiasi hicho na kusababisha bei kupanda kila mwaka? Je kwanini maeneo ambayo yana viwanda bei ya sukari bado iko juu kuliko maeneo ambayo hayana viwanda vya kuzalisha sukari?
  6. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ina wasiwasi hii biashara ya sukari inahujumiwa na Serikali yenyewe kama ambavyo tumeonesha hapo awali kuhusu fedha za VAT na ile 15% ya sukari ya viwandani.

 

  1. SHIRIKA LA MAENDELEO LA TAIFA-NDC
  2. Mheshimiwa Spika, Shirika la Maendeleo la Taifa – NDC ndio shirika mama ambalo kihistoria ndio lilianzisa Mashirika, makampuni na viwanda vyote vya Serikali nchini. NDC inamilikiwa na Serikali kwa asilimia miamoja na linatekeleza majukumu yake yaliyowekwa kisheria kwa kuzingatia Sheria ya Makampuni ya Mwaka 1992 pamoja na uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa Mwaka 1996 Paper Na. 6/96.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia Sheria tajwa Shirika linatekeleza majukumu ya kusimamia na kuendeleza viwanda vya kimkakati ambavyo vilianzishwa na Serikali vikikusudiwa bidhaa zake kuwa malighafi ya viwanda vingine. NDC kuwa ndio msimamizi kwa niaba ya  Serikali pale ambapo mwekezaji anataka kuwekeza kwa ubia na Serikali; na kuanisha na kuendeleza maeneo yenye fursa za kiuchumi ambapo sekta binafsi haioneshi nia ya kutaka kuyaendeleza.
  4. Mheshimiwa Spika, NDC inajukumu kubwa la kuhakikisha inatambua fursa mbalimbali za kiuwekezaji na kuingia ubia na wawekezaji kwa niaba ya Serikali katika kutekelezaji miradi mbalimbali. Lakini tatizo kubwa limekuwa NDC kushindwa kuweka mchango wake wa ubia katika kuendeleza miradi ya ubia na hivyo miradi mingi ya ubia kushindwa kuanza kulingana na mikataba.

 

  1. MAMLAKA YA MAENDELEO YA BIASHARA TANZANIA (TANTRADE)

 

  1. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) ni taasisi ya Serikali iliyoundwa chini ya Sheria Na. 4 ya Mwaka 2009 kwa dhumuni la kuwezesha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa kuendeleza na kutangaza biashara ndani na nje ya nchi. TanTrade inatekeleza dhima yake kwa kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, kushauri maendeleo ya biashara nchini na kusimamia Sekta ya Maonyesho nchini.
  2. Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa sana tulilonalo hapa nchini kuhusiana na uzalishaji wetu ni kukosa masoko ya ndani na nje, na hata pale yanapopatikana basi wazalishaji wanashindwa kunufaika nayo kutokana na bei zinazotolewa kwa bidhaa zetu.
  3. Mheshimiwa Spia, hoja ya msingi ni kutokana na mtazamo ambao wazalishaji wetu wamekuwa nao wa kuzalisha kwa soko la ndani, hivyo basi kutokana na mtazamo huo, bidhaa zinazozalishwa zinashindwa kuwa na ubora unaohitajika katika kushindana katika soko la nje.
  4. Mheshimiwa Spika, kutokana na jambo hilo, TANTRADE imekuwa inajitahidi kuandaa maonesho ambayo kwa kiasi kikubwa ni kutofauta masoko ya bidhaa za nje hapa nchini. Mtazamo huu wa uzalishaji kwa soko la ndani ndio ambao kwa miaka mingi iliyopita ilikuwa ni sera ya Serikali ya CCM ya kuzalisha vitu ili kuzuia bidhaa za nje zijiingizwe nchini (Import substitution policy).
  5. Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana ni kwamba bado hadi sasa Serikali ya awamu ya tano ina mtazamo huo huo katika ujenzi wa viwanda, lakini inasahau kuwa vipuri kwa viwanda ambavyo vinazalisha kwa soko la ndani vinanunuliwa nje kwa fedha za kigeni.
  6. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema TANTRADE iwe ni kiunganishi kati ya wafanyabiashara na balozi zetu za nje katika kuangalia fursa mbalimbali na ikiwezekana ihusishwe katika kusimamia makubaliano mbalimbali ya kibiashara ambayo wafanyabiashara wadogo na wakati wanaweza kupata fursa nje kupitia balozi zetu.

 

  1. KURASINI LOGISTIC CENTRE, SEZ NA EPZA
  2. Mheshimiwa Spika, Tanzania-China Logistics Centre – Kurasini, hadi kufikia mwezi Septemba, 2014 Wizara kupitia EPZA ilikuwa imelipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 53 kwa watu 538. Aidha kiasi cha fedha kinachodaiwa kumalizia kulipa fidia na malalamiko mbalimbali ya mapunjo yaliyotokana na makosa ya kiuthamini ni shilingi bilioni 3.75.
  3. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa, fedha iliyotolewa na Wizara hadi kufikia Machi 2016 ni shilingi 3,048,904,930 tu ambazo zilikuwa zimetolewa na serikali kwa ajili ya ulipaji wa fidia kwa pale Kurasini  Tanzania –China Logistic Center na kufanya jumla ya uwekezaji wa shilingi  bilioni 56.
  4. Mheshimiwa Spika, ukirejea taarifa ya kamati ya viwanda na Biashara kwa mwaka huo ni kwamba fidia katika maeneo yote yaliyofanyiwa tathmini yaliyopo chini ya EPZ na SEZ kufikia Mwaka wa Fedha 2015/2016; gharama ilifikia Shilingi Bilioni 60.
  5. Mheshimiwa Spika, naomba kunukuu sehemu ya taarifa ya Kamati ya Kadumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira kuhusiana na mradi huu wa kituo cha biashara cha Kurasini;

 “Kamati inaishauri Serikali kuwa makini wakati wa kulipa fidia za maeneo waliyoyatwaa kwa ajili ya Uwekezaji, vilevile kuangalia kiasi cha fidia kinacholipwa katika eneo husika kiendane na ukubwa au manufaa ya Mradi utakaowekwa. Mfano kwa sasa Kurasini Logistic Centre ilifidiwa Bilioni 191 ikiwa inatizamiwa kuwekwa Business Park, lakini mradi unaoenda kutekelezwa pale ni kuweka maghala ya chai ambapo mradi huu hautaweza rudisha fedha zilizotumika kutoa fidia”

  1. Mheshimiwa Spika, kwa ushauri huo wa kamati ni kwamba Serikali ya CCM haina kile kinachoitwa “continuity” kama utekelezaji wa miradi, jambo hili linaturudisha nyuma sana kama nchi, miaka yote miradi mikubwa haitaweza kutekelezeka kwani kila Serikali itakayoingia itakuja na mipango yake. Hii ni aibu kubwa sana katika utawala wan chi ambayo inaongozwa na chama kile kile.
  2. Mheshimiwa Spika, kwa takwimu za sasa fidia inayotakiwa kulipwa kutokana na kuchelewa kulipwa imeongezeka hadi kufikia shilingi Bilioni 190.9, fidia hii ni kwa maeneo ambayo tayari yalikwisha fanyiwa uthamini ambayo ni  Bagamoyo SEZ  hekta 5473, Ruvuma (2033), Tanga(1363), Mara (1360), Kigoma(691), Manyara (530.87), Manyoni-Singida (755). Maeneo ambayo bado hayajafanyiwa tathmini ni hekta 21634.
  3. Mheshimiwa Spika, Tukumbuke kwamba eneo hilo lote waliokuwa wamiliki hadi sasa wamezuiwa kuliendeleza  wananchi  bado wanaendelea kuteseka na Serikali haifahamu ni lini fidia itatolewa kwa wamiliki wa maeneo hayo iliyoyatwaa. Huu ni unyanyasaji mwingine wa Serikali dhidi ya Raia wake.
  4. KORONA NA SEKTA YA BIASHARA NCHINI
  5. Mheshimiwa Spika, sekta ya biashara hapa nchi inahusu sanasana na kununua na kuuza bidhaa mbalimbali ikiwezo huduma kwa watumiaji wa mwisho. Mbali na majadiliano ya biashara ya huduma kwa sekta sita za kipaumbele katika nchi wanachama wa SADC, sambamba na kutekeleza itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwenye masuala ya Bidhaa na Huduma.
  6. Mheshimiwa Spika, sekta ya biashara na bhuduma ni ya pili kwa kuwavutia wawekekezaji kwenye Jumuiya ya Afrika ya Mashariki baada ya sekta ya madini, ambapo Tanzania inaongoza kwa kupata uwekezaji unaotokana na ufugaji wa Biashara ya Huduma.Sekta zinazofanya vizuri kwenye Jumuiya kwa upande wa Tanzania ni Utalii, uchukuzi na mawasiliano.
  7. Mheshimiwa Spika, madhara ya ugonjwa wa korona kwenye biashara kwa kweli ni makubwa sana kwani sekta ya utalii ambayo ni sekta kiongozi katika biashara ya kutoa huduma imeanguka kwa takriban asilimia mia moja. Biashara zingine za kununua na kuuza bidhaa (trades) nazo zinasuasaua kwa kiwango kikubwa bidhaa hizo zinanunuliwa kutoka nje ya Tanzania. Mataifa mengi bidhaa hizo zinapotoka (China, India, Dubai, Ulaya na pia Kenya, Afrika ya Kusini, n.k) walikuwa wamefunga mipaka ya nchi zao hivyo hakuna kutoka wala kuingia na hivyo kupelekea anguko la sekta ya biashara kwa nchi yetu.
  8. Mheshimiwa Spika, mbali ya bidhaa zinazotoka nje ya nchi kuwa tatizo katika upatikanaji wake pia hata uuzwaji wake kwa wateja nalo limekuwa shida kubwa kutokana na ukweli kwamba, maambukizi ya ugonjwa wa Korona yanazidi kuwa makubwa na kinga yake kubwa ni kuachiana nafasi ya kutosha baina ya mtu na mtu. Jambo hilo katika mazingira ya biashara sio rafiki kabisa.
  9. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla sekta ya biashara iwe ya kuuza au kununua nje (export or import) zimeathirika sana sambamba na biashara za ndani za aina zote zimeathirika na hivyo kuwa ni pigo kwa mamlaka ambazo zinategemea kukosa ushuru/ kodi kutokana na biashara hizo.
  10. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara hii ndio wizara mlezi wa biashara, hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inatarajia kuwa Wizara hii ndiyo itayarishe mpango mkakati (back up or recovery strategy) wa jinsi ya kuokoa biashara zitakazokuwa zimezama au zimefilisika ili ziweze kurejea tena katika kuendelea na biashara zao pale ugonjwa utakapokuwa umedhibitiwa
  11. MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA 2020/21
  12. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/21 wizara inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 81,366,902,000.00 kati ya fedha hizo fungu 44  ni shilingi 57,414,395,000.00 na fungu 60 ni shilingi 23,952,507,000.00. Kiasi kinachoombwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ni shilingi 29,687,886,000.00, ambazo kati ya fedha shilingi 29,187,886,000.00 ni fedha za ndani na shilingi 500,000,000.00 ni fedha za nje.
  13. Mheshimiwa Spika, tukumbuke pia kwa bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2019/20 fedha iliyoidhinishwa na Bunge ya shilingi 51,000,000,000. Hadi mwezi februari, 2020 hakuna hata shilingi iliyokuwa imetolewa. Sasa hizo zinazoomba kwa mwaka wa fedha 2020/21  na kwa kuangalia hali halisi ya uchumi ilivyo kwa kweli ni sawa na kuwahadaa wananchi kuwa Serikali iko makini katika kuhakikisha Tanzania ya Viwanda inafikiwa.
  14. HITIMISHO
  15. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wizara ya viwanda na biashara pamoja na taasisi zake imebakia jina tu na majukumu mengi iliyokabidhiwa kwa mujibu wa hati idhini yake. Lakini kwa hali halisi kiutendaji sio hivyo.
  16. Mheshimiwa Spika, Wizara imebakia kufanya jukumu la kutunga miongozo na ushirikiano wa kikanda tu, lakini utekelezwaji wa miongozo hiyo kwa wahusika inakuwa vigumu kwani hawawezi kuingia kwenye ushindani wa kibiashara kutokana na kutokuwa na nyenzo au uwezeshwaji.
  17. Mheshimiwa Spika, nchi zote zilizo makini zimekuwa zikihakikisha kuwa wafanyabiashara pale wanapoanzisha biashara ambazo zinaonesha kuwa na mwanga mzuri hapo baadae, wanapatiwa ruzuku(subsidies) kwenye baadhi ya maeneo ambayo yanakuwa ni kikwazo kwao, nao huo ndio uwezeshaji wa kuikuza tasnia ya biashara.
  18. Mheshimiwa Spika, taasisi zote zinaotakiwa kutoa teknolojia rahisi katika uzalishaji bidhaa ili kuwa shindani katika soko, ziko hoi kwa kutopatiwa fedha za maendeleo, sasa tutashindanaje na bidhaa za nje ambazo zinazalishwa kwa teknolojia ya kisasa na tahisi zaidi?
  19. Mheshimiwa Spika, sekta ya biashara ndiyo nyenzo rahisi na ya haraka zaidi katika kukusanya kabla ya kuanza kuingia katika viwanda. Hivyo kitendo cha kusitisha mradi wa ujenzi wa kituo cha kibiashara cha Kurasini japokuwa uwekezaji na mbia alikuwa amepatikana ni jambo ambalo limeionesha Serikali ya awamu ya tano kuwa haina mwelekeo wa kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati hapo ifikiapo 2025.
  20. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema, wizara hii pamoja na taasisi zake haitaweza kuwa kiongozi katika kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda, kama hakuna mnyororo wa wazi wa ushirikiano baina yake na sekta ya kilimo na wadau wake ambao ni wakulima walione hilo kwa uwazi.
  21. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

……………………………

DAVID ERNEST SILINDE (MB)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI-WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA

APRIL,2020

 

 

 

 

Share Button