MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU SHERIA MPYA YA VYAMA VYA SIASA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
(CHADEMA)
MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU SHERIA MPYA YA VYAMA VYA SIASA

1.0 UTANGULIZI
Kwa kuwa, Ibara ya 20 ya Mkataba unaonzisha Umoja wa Mataifa unatoa haki ya kujumuika na inazuia mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na taasisi yoyote ikiwemo Vyama vya siasa;
Kwa kuwa, Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948 ibara ya 2 linatoa haki kwa watu wote bila ubaguzi ikiwemo Ubaguzi wa kisiasa;
Kwa kuwa, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ibara ya 1 inatoa haki kwa mtu yeyote kuwa na maamuzi huru ikiwemo uhuru wa kushiriki shughuli za kisiasa;
Kwa kuwa, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu ibara ya 11 inatoa haki kwa kila mtu ya kujumuika na watu wengine;
Na kwa kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ibara ya 3 ambayo inaeleza pamoja na mambo mengine kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na yenye kufuata mfumo wa Vyama vingi vya Siasa;
Hivyo basi, sisi CHAMA CHA DEMOKRASI NA MAENDELEO (CHADEMA),kama wadau wa siasa na kwa kuzingatia wito uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa tunatoa maoni yetu ambayo yanatakiwa kuzingatiwa katika utungwaji wa Sheria mpya ya Vyama vya Siasa kama ifuatavyo;

 MAONI NA MAPENDEKEZO MAHUSUSI KUHUSU SHERIA MPYA YA VYAMA VYA SIASA
Maoni yetu yamezingatia maeneo ya kipaumbele ambayo tunaamini kuwa yanahitaji kuingizwa katika sheria mpya itakayotungwa kwa lengo la kuboresha mfumo wa Demokrasia ya Vyama vingi nchini . Aidha, maoni haya yamezingatia uzoefu kutoka katika mbalimbali kama vile Ghana, Ujerumani, Kenya na Uingereza.

2. OFISI MSAJILI WA VYAMA WA VYAMA VYA SIASA
2.1 Kutakuwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itakayokuwa huru na itakayojitegemea na ambayo itapata fedha za kugharamia bajeti yake kutoka ‘Mfuko Maalum’ wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ulioanzishwa kwa mujibu wa Sheria hii.
2.2  Kutakuwa na Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye atakuwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
2.2.1 Majukumu ya Msajili wa Vyama vya Siasa yatakawa kama ifuatavyo;

  1. Kupokea na Kusajili maombi ya kuanzishwa kwa Vyama vipya vya Siasa
  2. Kutayarisha na kuchapisha taarifa za fedha za kila mwaka za ukaguzi wa fedha kwa kila Chama cha Siasa
  3. Kusimamia utekelezwaji wa sheria ya Vyama vya Siasa

Bila kujali majukumu yake kama yalivyoainishwa katika sheria hii Msajili wa Vyama vya Siasa hatakuwa na mamlaka ya kufuta Chama chochote cha Siasa chenye usajili wa kudumu isipokuwa  kwa maombi mahususi yatakayowasilishwa Mahakama Kuu.
2.3  Nafasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itatangazwa na Tume ya Utumishi wa Umma kwenye vyombo vya habari vya umma na vya binafsi.

      1.  Watu wote wenye sifa kwa mujibu wa Sheria hii wataruhusiwa kuomba kazi hiyo kupitia Tume ya Utumishi wa Umma na baada ya mchujo Tume ya Utumishi wa Umma itapendekeza majina sita kwenye Bunge. Baada ya Bunge kupokea mapendekezo ya majina hayo, Bunge litapendekeza kwa Rais majina yasiyozidi matatu kwa ajili ya Rais kuteua jina moja miongoni mwa majina hayo.
      2.  Ikiwa Rais hatakubaliana na mapendekezo ya majina yaliyowasilishwa kwake na Bunge atalazimika kulitaarifu Bunge kwa maandishi sababu za kukataa mapendekezo hayo na mchakato wa kumpata Msajili wa Vyama vya Siasa  utaanza upya .
    1. Sifa za Msajili wa Vyama vya Siasa zitakuwa kama ifuatavyo ;
  1. Awe raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano Tanzania
  2. Awe na angalau shahada ya Sheria iliyotolewa na Chuo kinachotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu.
  3. Awe ameshashika madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani kwa muda usioungua miaka mitano.
  4.  Asiwe mwanachama wa Chama cha Siasa
  5. Asiwe amewahi kutiwa hatiani kwa kosa la utovu wa uaminifu, kukwepa kodi au kuvunja Sheria ya Maadili ya viongozi wa umma.
  6.  Awe ni mtu anayeheshimika na kuaminika katika jamii
    1. Kutakuwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa atakayeteuliwa na Rais na utaratibu wa kumpata ni kama utaratibu wa kumpata Msajili wa Vyama vya siasa.

2.5.1 Kama Msajili wa Vyama vya Siasa atatoka upande mmoja wa Muungano, Naibu Msajili atatoka upande mwingine wa Muungano.

    1. Kutakuwa na Watendaji katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa watakaoajiriwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma kulingana na mahitaji.

3. VYAMA VYA SIASA
3.1 Kutakuwa na Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu na usajili wa muda.
3.2 Utaratibu wa kutoa usajili wa muda wa vyama vya siasa utaainishwa kwenye Kanuni zitakazotungwa na Msajili wa Vyama vya Siasa baada ya kushariana na Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu na kuidhinishwa na Kamati ya Bunge inayohusika na Sheria Ndogo.
3.3 Vyama vyenye usajili wa kudumu kabla ya Sheria hii vitachukuliwa kuwa vimesajiliwa rasmi mara baada ya Sheria hii kuanza kutumika.

3.4 Haki na Wajibu wa Vyama vya Siasa vyenye usajili wa Kudumu itakuwa kama ifuatavyo;

  1. Vyama vya siasa vitakuwa huru kufanya mikutano ya hadhara na maandamano kutafuta wanachama au kueneza sera zao wakati wowote kwa mujibu wa Sheria hii.
  2. Chama cha Siasa kinachotarajia kufanya mkutano au maandamano kitalazimika kutoa taarifa ya maandishi kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya saa 48 kabla ya muda wa kufanya mkutano au maandamano hayo kwa lengo la kupatiwa ulinzi.
  3. Vyama vya Siasa vitaendeshwa kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na Taratibu walizojiweka.
  4. Katiba za Vyama vya Siasa zitasajiliwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
  5. Vyama vya siasa vitalazimika kumjulisha Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu Marekebisho ya Katiba za Vyama vyao kwa mujibu wa Kanuni.
  6. Vyama vya Siasa vitakuwa na haki na jukumu la kutoa elimu ya uraia, kushindanisha sera zake na zile za Chama kingine.
  7. Vyama vya siasa vitakuwa na uhuru wa kutoa maoni na mtazamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na Kimataifa.
  8. Chama cha Siasa chenye usajili wa muda kitakuwa na haki ya kwenda Mahakama Kuu kama kitakataliwa kwa sababu yoyote ile kupewa usajili wa kudumu.
  9. Vyama vya Siasa vitakuwa na haki ya kuweka Wagombea katika chaguzi zote zinazoratibiwa na Tume ya Uchaguzi au Mamlaka nyingine yoyote.
  10. Itakuwa ni marufuku kwa Chama cha Siasa kutumia vyombo vya dola kukandamiza na kutoa vitisho kwa Chama kingine cha Siasa au kwa wanachama wake.
  11. Chama cha siasa, kiongozi, mwanachama au mtu yeyote atatakiwa kuepuka kuteremsha bendera au kuharibu kwa namna yoyote ile kitu chochote ambacho ni ishara au Nembo ya Chama kingine cha Siasa. Chama cha siasa, kiongozi, mwanachama au mtu yeyote atakayekiuka masharti haya atakuwa ametenda kosa la kuharibu mali kwa mujibu wa sheria ya Kanuni ya Adhabu.
  12. Chama cha Siasa kitatakiwa kuepuka kutumia mamlaka, rasilimali za serikali, vyombo vya dola au wadhifa wa kiserikali kwa namna yoyote ile ili kukinufaisha au kwa lengo la kukandamiza Chama kingine au wanachama wake.
  13. Vyama vyote vya siasa vitakuwa na haki sawa ya kutumia vyombo vya habari vya umma.Na itakuwa marufuku kwa vyombo vya habari vya umma kupendelea Chama chochote cha siasa

Bila kujali masharti ya kifungu hiki na Sheria nyingine yoyote, Kamanda wa Polisi wa Wilaya hatakuwa na mamlaka ya kuzuia Mikutano au Maandamano ya Vyama vya Siasa wakati wowote ule isipokuwa akilazimika kufanya hivyo kwa sababu zozote zile atalazimika kwanza kushauriana na Chama husika na pia atakijulisha Chama husika kwa maandishi.
3.5 Itakuwa ni jukumu la Serikali kutoa ruzuku kwa Vyama vyote vya Siasa vyenye usajili wa kudumu ili viweze kujiendesha.
3.6 Chama cha Siasa kitakuwa na uhuru na haki ya kushirikiana na au kuungana na Chama au Vyama vingine vya siasa bila kupoteza usajili wake wa awali.
3.7 Chama cha Siasa kitakuwa na wajibu ya kusaidia ulinzi kwa kushirikiana na maafisa wa Polisi wakati Chama hicho kitakapokuwa kinafanya mikutano, maandamano au shughuli zingine za kisiasa.
3.8 Masuala yote ya uendeshaji wa Vyama vya Siasa yatashughulikiwa na Vyama husika kwa kufuata Katiba, Kanuni na Taratibu walizojiwekea.

4.0 MASUALA YA FEDHA
4.1 Kutakuwa na Mfuko Maalumu wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
4.2 Bunge litatenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya uendeshaji wa mfuko maalum wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
4.3 Ruzuku kwa ajili ya Vyama vya Siasa itatolewa kupitia Mfuko Maalum wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
4.3 Bila kuathiri masharti ya kifungu hiki cha Sheria hii, Serikali italazimika kutenga asilimia mbili ya Bajeti ya Matumizi ya Kawaida kwa ajili ya Ruzuku kwa Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu.
4.4 Matumizi ya fedha za Mfuko maalum wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa zitatumika kwa kuzingatia masharti ya sheria ya Fedha za Umma .
4.5 Mapato na Matumizi ya Mfuko Maalum wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa utakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mujibu wa Sheria.

    1. Mapato ya Vyama vya siasa yatatokana na vyanzo vifuatavyo;
  1. Ada ya uanachama
  2. Michango ya hiari ya wanachama
  3. Ruzuku ya serikali
  4. Faida itokanayo na uwekezaji kwenye miradi mbalimbali ambayo Chama kimewekeza.
  5. Michango na misaada kutoka kwa wahisani wa ndani na nje ya nchi
  6. Michango, misaada, mikopo, wakfu au urithi wa aina yoyote.

 

5.0 MAMBO YA JUMLA
5.1 Kutakuwa na Baraza la Vyama vyote vya Siasa vyenye usajili wa kudumu litakaloundwa kwa mujibu wa Sheria hii.
5.2 Majukumu ya Baraza la Vyama vya Siasa yatakuwa kama ifuatavyo;

  1. Kumshauri Msajili wa Vyama vya Siasa
  2. Kushauriana juu ya mambo mbalimbali yanayohusiana na uwepo na uendeshaji wa Vyama vya Siasa.
  3. Kujadili kwa nia ya kusuluhisha migogoro kati ya Chama kimoja na Chama kingine cha siasa au kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Chama au Vyama.
  4. Kutunga na kupitisha maadili ya vyama vya siasa
  5. Kumshauri Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu Kanuni zitakazotungwa kwa mujibu wa Sheria hii kabla ya Kanuni hizo kuwasilishwa kwenye Kamati ya Bunge.

Mgogoro wowote baina ya Vyama vya Siasa au Vyama vya Siasa na Msajili wa Vyama vya Siasa ukishindwa kupatiwa suluhisho, upande wowote usioridhika utakuwa na haki ya kuwasilisha maombi Mahakama Kuu.
5.3 Kutakuwa na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa.
5.4 Msajili wa Vyama vya Siasa atakuwa ndiye Katibu wa Baraza la Vyama vya Siasa.
5.6 Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa watakuwa kwenye Madaraka hayo kwa kipindi cha miezi sita isipokuwa  Mwenyekiti hatakuwa na sifa za kukabidhiwa madaraka tena mpaka mzunguko wa Vyama vyote utakapokamilika.
5.7 Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa hawatatoka kwenye Chama kimoja cha siasa au upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano.
5.8 Kutakuwa makundi mawili ya Vyama vya siasa kama ifauavyo;

  1. Vyama vyenye uwakilishi Bungeni
  2.  Vyama visivyo na Uwakilishi Bungeni

5.9 Ikiwa Mwenyekiti anatoka kwenye Chama cha Siasa chenye Uwakilishi Bungeni, Makamu Mwenyekiti atatoka kwenye Chama kisicho na uwakilishi Bungeni.
5.10 Kutakuwa na ada ya kusajili Chama cha Siasa kwa kiasi ambacho kitaainishwa na Kanuni kwa mujibu wa Sheria hii.
5.11 Kila Chama cha Siasa  kitakuwa na Bodi ya Wadhamini ambayo itasajiliwa kwa mujibu wa Sheria.
5.12 Bodi ya Wadhamini ya kila Chama itakuwa ndiyo yenye mamlaka ya kumiliki mali za Chama husika, itakuwa na mamlaka ya kushtaki au kushtakiwa  na itakuwa na uwezo wa  kukopa pamoja na kuingia katika makubaliano au mikataba kwa mujibu wa Sheria.

Share Button
Layout Settings