HOJA YA KUMWONDOA MADARAKANI NAIBU SPIKA WA BUNGE, MHE. DKT. TULIA ACKSON MWANSASU (Mb)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA HOJA YA KUMWONDOA MADARAKANI NAIBU SPIKA WA BUNGE, MHE.
 DKT. TULIA ACKSON MWANSASU (Mb)

Ndugu wanahabari, tumewaita hapa kuwaomba muwape taarifa Watanzania kuwa kwa niaba ya wabunge wenzangu nakwa mujibu wa kanuni ya 138 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016, naomba kuinukuu;

“Utaratibu wa kumwondoa Naibu Spika madarakani chini ya Ibara ya 85(4)(c) ya Katiba utakuwa kama ule wa kumwondoa Spika, isipokuwa tu taarifa ya kusudio la kumwondoa Naibu Spika madarakani inayoeleza sababu kamili za kuleta hoja hiyo,  itapelekwa kwa Spika ambaye ataiwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kuijadili.”

Jana tarehe 1 Juni 2016,nimewasilisha kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania “Taarifa Ya Kusudio La Kuleta Bungeni Hoja Ya Kumwondoa Madarakani Naibu Spika Wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb)”

Ndugu wanahabari, Kama Mtakumbuka tarehe 30 Mei 2016, Wabunge wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, tulitoka Bungeni kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb) kwa jinsi ambavyo analiendesha Bunge kwa ubabe dhidi ya Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambao kwa muda wote toka kuanza kwa Bunge la 11 wamekuwa wakitetea maslahi ya Watanzania, ikiwamo kuitaka Serikali kuwarudisha Chuoni Wanafunzi wa Diploma Maalumu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kuonesha Bunge live.

Ndugu wanahabari, Taarifa yetu ya Kusudio hilo imeorodhesha sababu kuu 6 kwanini Naibu Spika aondolewe madarakani kwa azimio la Bunge kwa kuvunja Sheria inayoendesha Bungena Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, kama ifuatavyo;

  1. Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb) ameweka Maslahi ya chama chake cha Siasa mbele kuliko Maslahi ya Bunge Kinyume na Kanuni ya 8(b) ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

  1. Tarehe 6 Mei, 2016 Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu(Mb)alitumia vibaya madaraka ya Kiti cha Spika kwa kutoa uamuzi wa mwongozo ambao ulikuwa unakiuka Ibara ya 12(2) ya  Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, isemayo kuwa “Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”Muongozo uliokuwa unapinga udhalilishaji wa wabunge wanawake.
  1. Tarehe 28 Aprili, 2016 Naibu Spika, alivunja Kanuni ya 64 (1) (f) na (g) zinazokataza mbunge kutumia lugha ya matusi kwa mbunge au mtu mwingine yeyote na kukataza matumizi ya lugha ya kuudhi au kudhalilisha watu wengine, ambapo Naibu Spika alinukuliwa akisema kuwa:  “….Mheshimiwa Bwege, usioneshe ubwege wako humu ndani…”

  1. Tarehe 30 Mei 2016 Naibu Spika, aliamua kwa makusudi kuvunjaibara ya 63 (2) ya        Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutumia vibaya kanuni ya 69(2) na 47 (4) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Januari 2016, kumzuia Mheshimiwa Joshua Nassari kwa upande mmoja na Bunge zima kwa upande wa pili kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali.
  1. Tarehe 26 Mei 2016, Naibu Spika akiongoza kikao cha Bunge, bila ridhaa ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alishiriki kufuta sehemu ya hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Elimu, Sanyansi na Teknolojia kinyume cha kanuni ya 99 (9) ya kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari, 2016, bila kushirikisha kamati yoyote ya Bunge.

  1. Kitendo cha Naibu Spika kukataa taarifa tofauti (dissenting opinion)iliyowasilishwa na wabunge wanne wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambao ni wajumbe wa kamati ya haki,maadili na madaraka ya Bunge [Mhe. Suzan A. Lyimo (Mb), Mhe.Rose Kamili Sukum (Mb), Mhe. Tunza Issa Malapo (Mb) na Mhe. Rashid Abdalah (Mb)]jambo ambalo ni ni kinyume cha kanuni ya 5(1) ambayo inamtaka Spika vilevile kuzingatia mila na desturi na maamuzi ya Maspika wa mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge la Tanzania.

Ndugu wanahabari, Kwa ujumla ni kuwa Naibu Spika amevunja Kanuni ya 8 (b) inayokataza upendeleo, kanuni ya 5(1) ambayo inamtaka Spika vilevile kuzingatia mila na desturi na maamuzi ya Maspika wa mabunge mengine, kanuni ya 8 fasili (a), Kanuni ya 64 (1) (f) na (g), kanuni ya 69(2) na 47 (4), kanuni ya 99 (9).

Ndugu wanahabari, aidha taarifa yetu ya Kusudio imeonesha bayana namna Naibu Spika alivyokiuka Katiba ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kwa kuvunja ibara ya Ibara ya 12(2), ibara ya 13 (4), ibara ya 63 (2) na ibara 11 (3).

Ndugu wanahabari,pia tumeonesha ni kwa namna gani Naibu Spika amevunja  Sheria ya Bajeti Na.11 ya mwaka 2015, kifungu cha 29 (1), (2), (3), (4) na (5) kushiriki kurudisha fedha za mfuko wa Bunge kwa Rais jambo ambalo pia ni kinyume na sheria ya Uendeshaji wa Bunge.

Ndugu wanahabari,taarifa yetu imeungwa mkono na wabunge 92 kuwakilisha wabunge wengine. Tunasubiria utaratibu wa Kanuni ya 138(1) uzingatiwe na Ofisi ya Spika ili kuwezesha hoja yetu kupelekwa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye tupitishe azimio la kumwondoa madarakani Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu(Mb).

Ninafanya yote haya kwa Maslahi ya Taifa letu na Ustawi wa Demokrasia Nchini mwetu.

…………………………………
James Kinyasi Millya (Mb)
JIMBO LA SIMANJIRO
2 Juni, 2016.

 

Share Button
Layout Settings