Mgombea Chadema Salum Mwalimu akamatwa na Polisi Magomeni

Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Chadema jimbo la Kinondoni, Salum Mwalimu amekamatwa muda huu na polisi katika kituo cha kupigia kura cha Idrisa kata ya Magomeni.

Muda mfupi uliopita baadhi ya wananchi wa kata hiyo wamedai kuwa katika kituo hicho kuna mtu ametoroka na sanduku lenye kura, baadaye kukamatwa na polisi akiwa amelibeba sanduku hilo.

Baadhi ya waandishi wa habari wa timu ya MCL Digital iliyopiga kambi katika kata zote 10 za jimbo hilo, imeshuhudia Mwalimu akikamatwa nje ya kituo hicho na kupakizwa katika gari la polisi aina ya defender huku taarifa za awali zikidai kuwa alikwenda eneo hilo na kundi kubwa la watu.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Mwalimu amesema kuwa hana taarifa zozote.

Baada ya kufikishwa kituo cha polisi Magomeni, Mwalimu aliingizwa ndani na kukaa takribani robo saa na kuachiwa na muda huu anaelekea ofisi za kanda za Chadema kuzungumza na waandishi wa habari.

Share Button
Layout Settings