info@chadema.or.tz Daima Street, Mikocheni, Dar Es Salaam

Chadema yatoa msimamo kushiriki mazungumzo. Yasisitiza Lissu aachiwe.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kuuarifu umma kuwa hakipo tayari kushiriki mazungumzo yoyote na watu wanaotaka mazungumzo wakati Mwenyekiti wa Chama akiwa gerezani.

Msimamo huo kwa niaba ya Chama umetolewa na Makamu Mwenyekiti upande wa Zanzibar, Mheshimiwa Saidi Mzee Saidi wakati akihutubia mkutano wa kudai Katiba Mpya na kumuachia huru Mwenyekiti Tundu Lissu uliofanyika Katoro mkoa wa Geita, jana Jumamosi Mei 16, 2026.

Mheshimiwa Makamu amesema hauwezi kutaka mazungumzo na mtu ambaye amekatwa kichwa akimaanisha Mwenyekiti Lissu ndiye kiongozi mkuu anayeongoza vikao, hivyo kitendo cha kutokuwepo uraiani ni kukizuia Chama kushiriki mazungumzo yoyote ya uwazi na ukweli yenye lengo la kuwaunganisha Watanzania.

Naye Makamu Mwenyekiti upande wa bara, Mheshimiwa John Heche ameendelea kusisitiza kuwa mamlaka zisipomuachia huru Mwenyekiti Lissu basi Chama kitaitisha maandamano nchi nzima ya kutaka Mheshimiwa Lissu aachiwe.

Mheshimiwa Heche amesema maandamano ni haki ya chama cha siasa na wananchi kwa ujumla hivyo Chama kitatumia haki hiyo kutaka Mheshimiwa Lissu aachiwe.

Awali kwenye mkutano huo wa hadhara, Katibu Mkuu wa Chama, Mheshimiwa John Mnyika amewataka wanachama wa Chadema kutokubali kutolewa kwenye mjadala wa kudai Katiba Mpaya na Mheshimiwa Lissu aachiwe kwa vitisho kutoka kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

Mheshimiwa Mnyika amesema kitendo cha ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kutishia kukifungia ama kukifuta Chama kina lengo la kuwatoa kwenye mstari viongozi, wanachama na wananchi kwenye vuguvugu jipya la kudai katiba mpya na kumuachia huru Mheshimiwa Lissu.

Chama leo Jumapili Mei 17 kitafanya mkutano wa hadhara Geita mjini na kesho mchana kitafanya mkutano wa hadhara Kahama mkoani Shinyanga

Leave A Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *