Makamu Mwenyekiti Bara wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mheshimiwa John Heche na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Mheshimiwa Said Mzee Said wamepokea mamia ya watu waliohama vyama vyao na kujiunga na chama hicho.
Mapokezi hayo yamefanyika kwenye mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Maalim Seif Garden uliopo Kilwa Kivinje Jumatano, Juni 03, 2026.
Aliyekuwa diwani wa kata ya Lihimalyao kwa tiketi ya CUF kabla hajahamia ACT Wazalendo, Mahadhi Nangona wakati akihutubia maelfu ya watu waliohudhuria mkutano huo alisems amegundua vyama vyote vya upinzani kasoro Chadema, havina dhamira ya kuiondoa CCM madarakani.
Naye aliyekuwa diwani wa Kata ya Tingi na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF, wilaya ya Kilwa, Dayani Mkenda au maarufu kwa jina la Upanga wa Saidna Ally alisema chama chake cha awali kilikuwa ni tawi la CCM na kilikuwa kinapangiwa siasa gani wafanye.
“Niliwaambia wenzangu wa CUF kuwa tusiende kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 mpaka ipatikane Tume Huru ya Uchaguzi, waliniambia CCM wamewaambia watatupatia wabunge 10.
“Kauli hiyo ilinishangaza na bahati nzuri kwenye uchaguzi ule hatukupata hata kiti kimoja cha ubunge. Nilipowauliza wenzangu wakasema hakukuwa na uchaguzi. Niliwashangaa” alisema Dayani Mkenda.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo kata ya Kivinje, Zidadu Nango alisema yeye na wenzake walikaa na marehemu Bwege (aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo la Kilwa Kusini) walifanya tathmini na kwa pamoja waligundua kuwa chama pekee chenye nia yakweli ya kupambana na CCM ni Chadema na ndio maana wameamua kujiunga.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Mheshimiwa John Mnyika alisema Kilwa ni kitovu cha mapambano ya kudai haki ikiwemo kuwa vinara wa vita vya majimaji hivyo wamefanya sahihi kujiunga na Chadema ili kupambania haki na demokrasia kwenye taifa.
Makamu mwenyekiti Chadema upande wa Zanzibar, Mheshimiwa Said Mzee Saidi wakati akihutubia mkutano huo alisema wananchi wa Kilwa wamefanya maamuzi sahihi kwenye muda sahihi kujiunga na Chadema.
Naye Makamu Mwenyekiti Bara, Mheshimiwa John Heche aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa njia pekee ya mwanzo ya kuboresha maisha ya Watanzania ni kuiondoa CCM madarakani.
Mheshimiwa Heche aliwaambia Wanakilwa kuwa CCM imeshindwa kutumia raslimali za Watanzania kuboresha maisha ya watu wa Kilwa.
Chadema waliutumia mkutano huo wa hadhara kumkumbuka aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kilwa kusini, marehebu Bwege ambaye alifariki siku chache kabla hajapokelewa rasmi na kuwa mwanachama wa Chadema
© Copyright 2025. Developed By: CHADEMA
Leave A Reply