Bawacha

Baraza la Wanawake wa Chadema - BAWACHA

Kwa kuwa, CHADEMA ni Chama kinachozingatia haki, uhuru
na demokrasia katika jamii;
Kwa kuwa, tunaamini kwamba wanawake ndiyo chimbuko la maendeleo katika Taifa lolote lile duniani kutokana na nguvu, ubunifu na wingi wao, hivyo basi kifungu cha 7.8 na 7.8.3 cha Katiba ya Chadema ya mwaka 2006 kimetoa mamlaka ya uanzishwaji wa Mabaraza ya Chama likiwemo Baraza Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA);

Hivyo basi, sisi wajumbe wanawake tuliohudhuria Mkutano Mkuu wa Chama na kwa kuzingatia umuhimu wa uanzishwaji wa Baraza letu, tumekubaliana kukaa kama Mkutano Maalumu wa kuandaa rasimu ya Mwongozo wa uendeshaji wa shughuli za wanawake wa CHADEMA na kupendekeza kwa Baraza Kuu la Chama ili upitishwe na kuwa mwongozo rasmi, wa kuongoza
wanawake kuanzia ngazi ya msingi mpaka Taifa.

FASILI YA UFAFANUZI

Maneno yafuatayo yanatumika ndani ya mwongozo huu yatakuwa na maana au fasili ya   fafanuzi kama inavyoelekezwa hapa chini:-

“Baraza” ina maana ya Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA).

“Mwanachama wa Baraza” ina maana ya mwanachama hai wa CHADEMA ambaye amejiunga na Baraza la Wanawake kwa kutimiza masharti ya Katiba ya Chama na Mwongozo huu. “Viongozi wa Serikali” ina maana ya viongozi wa Serikali wanaotokana na Chama.

SURA YA KWANZA

1.0 JINA

1.1 Jina la Baraza litakuwa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA)

1.2 MAKAO MAKUU YA BARAZA

1.2.1 Makao Makuu ya Baraza yatakuwa Dar es Salaam na patakuwa na ofisi ya Baraza Zanzibar.

SURA YA PILI

2.0 MAADILI NA ITIFAKI

2.1 Maadili na Itifaki ni kama ilivyoainishwa ndani ya Katiba
na Kanuni za Chama

2.2 KAULI MBIU YA BARAZA:

2.2.1 Kauli mbiu ya Baraza itakuwa “Wanawake” – “Chimbuko la Maendeleo”.

2.2.2 Kauli mbiu hii itakwenda sambamba na kauli mbiu ya Chama kwa kuanza na ile ya Chama:

“CHADEMA” – “VEMA”

“CHADEMA” – “MABADILlKO YA KWELI, UHURU WA KWELI”

“WANAWAKE”- “CHIMBUKO LA MAENDELEO”

SURA YA TATU

3.0 LENGO KUU LA BARAZA

Kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki katika masuala yote ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

3.1 KAZI ZA BARAZA

(a) Kutambua, kusimamia, kuendeleza na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika masuala mbalimbali yanayohusu mustakabali wa Chama.

(b) Kusimamia, kuendeleza na kulinda maslahi ya Chama.

(c) Kubuni na kutekeleza mikakati ya kueneza sera za Chama kupitia wanawake ndani ya jamii.

(d) Kubuni na kupanga mafunzo ya wanawake kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.

(e) Kuhamasisha wanawake kushiriki kugombea uongozi katika uchaguzi wa Chama na chaguzi za serikali.

(f) Kuhamasisha na kuunda timu za wanawake kwa ajili ya kampeni za wagombea wa Chama katika chaguzi za serikali.

(g) Kuanzisha na kuendeleza ukuaji wa vikundi vya michezo na sanaa kwa wanawake wa Chama kama chombo cha mvuto kwa wanawake wengi kujiunga.

(h) Kushirikiana na wanawake wa vyama vingine vya siasa na visivyo vya siasa ndani na nje ya nchi kwa maelekezo ya Chama.

SURA YA NNE

4.0 Uanachama

4.1 Uanachama wa Baraza la Wanawake unazingatia kuwa:

4.1.1 Lazima awe mwanachama wa CHADEMA.

4.1.2 Atimize masharti ya Mwongozo huu..

4.2 Haki na Wajibu

4.2.1 Haki, wajibu kama ilivyoainishwa ndani ya Katiba
ya Chama.

4.3 Kukoma kwa Uanachama

4.3.1 Kukoma uanachama ni kama ilivyoainishwa ndani
ya Katiba ya Chama Ibara 5.4

4.3.2 Asipotimiza masharti ya Mwongozo huu.

Makala, Taarifa, Habari, Matukio ya Bawacha

Share Button
Layout Settings