1. UTANGULIZI

SISI WAJUMBE WA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) AMBAO MAJINA YETU YAMEAMBATANISHWA HAPA CHINI, tuliokutana hapa Mtwara kati ya tarehe 4 hadi 6 Machi, 2024, kwa niaba ya Wanachama, wafuasi wanaotuunga mkono na kwa niaba ya Watanzania wote wanaopenda mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu tunasema yafuatayo;

 1. TUMECHOKA kuvumilia dharau na ukaidi wa CCM wa kukataa madai ya haki na ya muda mrefu ya Watanzania ya Katiba Mpya, mfumo mpya na wa kidemokrasia wa uchaguzi na mfumo bora wa kiuchumi utakaohakikisha kila Mtanzania anapata nafuu katika hali ya maisha yake, huduma bora za kijamii hususan afya, elimu, maji na umeme.

Mwaka 1991 Tume ya Rais ya mfumo wa Chama kimoja au Vyama vingi vya Siasa (Tume ya Nyalali) iliyoundwa na Marehemu Rais Ali Hassan Mwinyi ilipendekeza kutungwa kwa Katiba Mpya na ya kidemokrasia kwa ajili ya Tanzania Mpya ya mfumo wa Vyama vya Siasa.

Tume ya Nyalali ilipendekeza pia kuundwa kwa mfumo mpya wa kidemokrasia wa uchaguzi utakaokuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Sheria mpya na bora za uchaguzi zitakazohakikisha uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika.

Aidha, Tume ya Nyalali ilipendekeza kufutwa kwa Sheria zote za ukandamizaji na kutungwa kwa Sheria mpya zitakazohakikisha kuwa kila Mtanzania anapata haki sawa.

 1. Serikali sio tu imekataa mapendekezo haya ya Tume ya Nyalali, lakini pia imekataa mapendekezo mengi yaliyotolewa na Tume nyingine zote zilizofuata ambazo iliziunda yenyewe.

Serikali ya marehemu Benjamin William Mkapa ilikataa mapendekezo ya Katiba Mpya na Muundo mpya wa Muungano yaliyotolewa na Tume ya Jaji Robert Kissanga mwaka 1998.

Serikali ya Rais Mkapa ilikataa pia mapendekezo ya Kamati ya Jaji Mark Bomani iliyopendekeza mabadiliko makubwa ya kikatiba na kisheria ya mwaka 2003.

Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete ilikataa mapendekezo ya Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba iliyotengeneza hadi Rasimu ya Katiba Mpya ya mwaka 2014.

Serikali ya Marehemu Rais John Pombe Magufuli sio tu ilikataa mabadiliko yoyote ya Kikatiba, bali pia ilitumbukiza Taifa letu katika  utawala wa kidikteta uliosababisha mauaji, utesaji na ukandamizaji mkubwa wa haki za Watanzania.

Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekataa sio tu madai ya Katiba mpya, bali pia imekataa mapendekezo yote ya CHADEMA nay a Wadau wengine ya mabadiliko ya kikatiba na kisheria yaliyolenga kuipatia nchi yetu mfumo mpya wa kidemokrasia wa uchaguzi wenye Tume Huru ya Uchaguzi na Sheria mpya za uchaguzi ili kuhakikisha wizi wa uchaguzi unakomeshwa na Watanzania wanapata viongozi waliochaguliwa kihalali katika uchaguzi huru wa haki na unaokubalika.

 1. Kwa kukataa Katiba Mpya na Mfumo mpya na wa kidemokrasia wa uchaguzi, CCM imeendelea kuiba kura na kuvuruga chaguzi zote tangu tuingie katika mfumo wa Vyama vingi vya Siasa1995, 2000, 2005, 2010, 2015 na hasa 2020. Sasa CCM ya Rais Samia inajiandaa kuiba kura na kuvuruga uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
 2. Katika kipindi chote ambacho Serikali imekataa mabadiliko ya msingi ya kisiasa, kikatiba na kisheria , hali ya maisha ya Watanzania imeendelea kuwa mbaya zaidi.

 

Ufisadi, ubadhirifu na wizi wa fedha na mali za umma ya Watanzania umeongozeka mwaka hadi mwaka.

 

Viongozi wa CCM na Serikali yake wameendelea kujitajirisha na kuishi kwa anasa wao, familia zao na marafiki zao, huku wananchi wa kawaida wa Tanzania wakiishi katika lindi la umaskini mkubwa.

Vipato halisi vya Watanzania :- wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyakazi wa kuajiriwa na wa kujiajiri, wamachinga, bodaboda vimeendelea kushuka mwaka hadi mwaka huku umaskini wao ukiongezeka.

 

Mamilioni ya Watanzania hasa vijana wameendelea kuishi bila ajira na hivyo kuwa mzigo mkubwa kwa familia zao na kwa jamii kwa ujumla;

 

Bei za bidhaa na gharama za maisha na huduma zote muhimu:- chakula, maji, umeme, afya, usafiri na malazi zimepanda sana na kuongeza ugumu wa maisha ya Watanzania.

Watanzania wametwishwa mzigo mkubwa wa kodi, tozo, ushuru, ada, kikokotoo ambao umepunguza vipato vyao na kuwadidimiza zaidi katika umaskini na maisha magumu.

 1. Mlango mmoja ukifungwa, Mlango mwingine unafunguliwa. Kwa vile Serikali imekataa mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka kwa njia za mazungumzo na maridhiano; sasa Watanzania watayapata mabadiliko hayo kwa njia ya nguvu ya umma na njia nyingine za mashinikizo ya umma kama vile maandamano, migomo na njia nyingine za aina hiyo. Ili kutekeleza azma hii, sisi CHADEMA kwa sasa tutachukua hatua zifuatazo:-

 

Baada ya maandamano makubwa na yaliyofanikiwa ya Majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha; sasa tunaingia katika hatua ya pili itakayohusisha wiki ya maandamano katika Makao Makuu ya Mikoa yote Nchi nzima yatakayoanza tarehe 22 hadi 30 Mwezi Aprili, 2024.

 

Sambamba na hilo kwa kuwa tulitoa mwito kwa Serikali kuleta mpango mkakati wa kupunguza gharama za maisha na wameshindwa. Kamati Kuu inaelekeza Kamati ya Wataalam wa Chama kuandaa mpango mbadala wa kunusuru wananchi na ugumu wa Maisha, kupunguza bei za bidhaa na huduma muhimu na mzigo mkubwa wa maisha magumu unaokabili wananchi wetu.

Aidha, Kamati Kuu inaagiza Wanachama wetu waliopo Diaspora kuanza maandalizi ya maandamano katika maeneo yao

Tutazidisha na kuendeleza mapambano haya hadi hapo CCM itakapotekeleza madai halali ya muda mrefu ya Watanzania ya Katiba Mpya, Mfumo mpya wa kidemokrasia wa uchaguzi na hadi hapo Watanzania watakapopata nafuu ya hali yao ya maisha kwa kupunguziwa gharama za maisha, bei za bidhaa na huduma zote muhimu katika maisha yao.

Maeneo ya mfumo wa uchaguzi tunayodai yabadilishwe ni haya yafuatayo;

 • Kuundwa kwa Tume Huru ya uchaguzi na kubadilishwa kwa mfumo mzima wa kuendesha na kusimamia chaguzi zote nchini.
 • Kubadilishwa kwa mfumo mzima wa kutenga Majimbo ya uchaguzi ili kuhakikisha kwamba Majimbo ya uchaguzi yanazingatia idadi sawa ya Watu wanaowakilishwa.
 • Kubadilishwa kwa mfumo mzima wa uandikishaji wa wapiga kura ili kuhakikisha kwamba kila mwenye sifa ya kupiga kura anaandikishwa kama mpiga kura na kuondoa masharti ya kibaguzi ya kuandikisha Wapiga Kura.
 • Kubadilishwa kwa mfumo mzima wa uteuzi wa Wagombea ili kukomesha vitendo vya kuengua Wagombea wa Upinzani.
 • Kubadilishwa kwa mfumo wa uendeshaji wa kampeni za uchaguzi ili kukomesha vitendo vya kunyanyasa Wagombea wa Vyama vya Upinzani na kuwezesha matumizi sawia ya Vyombo vya Habari.
 • Kubadilisha mfumo mzima wa gharama za uchaguzi na namna ya kuusimamia.
 • Kubadilisha mfumo mzima unaohusu maadili ya uchaguzi na namna ya kuyasimamia ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa Wagombea wa Upinzani kwa kisingizio cha maadili ya uchaguzi.
 • Kubadilisha utaratibu wa upatikanaji na uapishaji wa mawakala wa Vyama au Wagombea na utaratibu wa kupiga na kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi.
 • Kuweka mfumo mpya na bora zaidi wa kutatua migogoro yote ya uchaguzi katika hatua zote za mchakato wa Uchaguzi.
 • Kubadilisha utaratibu wa uteuzi wa Madiwani na Wabunge wa Viti Maalum.
 • Kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaowezesha Wagombea Binafsi kushiriki katika uchaguzi kama Wagombea katika ngazi zote za uchaguzi.

CHADEMA itaendelea kuunganisha nguvu za Watanzania wote kwa kushirikisha Vyama, makundi mbalimbali ya kijamii katika hatua hii muhimu ya mapambano ya kidemokrasia katika nchi yetu.

 

Tunaendelea kuitaka Serikali ya CCM kusikiliza na kuheshimu matakwa ya Watanzania wote ili hatimaye tujenge Taifa lenye Haki, Uhuru, Demokrasia ya kweli, Maendeleo ya wote na utengemano wa Taifa.

 

Share Button