BUNGE LA WANANCHI, KAMATI YA AFYA NA MAENDELEO YA JAMII

WITO WA DHARURA KUHUSU KITITA KIPYA CHA NHIF NA HATUA ZA AWALI ZINAZOPASWA KUCHUKULIWA NA SERIKALI ILI KUNUSURU WANANCHI

1. Bunge la Wananchi limepokea kwa tahadhari kubwa taarifa za mgogoro uliojitokeza baina ya Wizara ya Afya na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) – kwa upande mmoja – waliotangaza mpango wa kuanza kutumika kwa Kitita Kipya cha NHIF cha Bei za Huduma za Afya – na Chama cha Watoa Huduma Binafsi za Afya (APHFTA) – kwa upande mwingine – ambao wametangaza kutokuwa tayari kutoa huduma za afya kupitia Kitita hicho.

2. Bunge la Wananchi linamtaka Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Mhe Ummy Mwalimu, wachukue hatua za dharura, ya kuingilia kati mgogoro huu, kwa kusitisha kwa muda kusudio la kutumia Kitita Kipya cha NHIF kilichopendekezwa na Kamati Teule ya Waziri Afya, ili pamoja na mambo mengine:

a) Vyama vya Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini viweze kupewa haki ya kushirikishwa, kusikilizwa na kutoa hoja na mapendekezo yao dhidi ya athari za bei za huduma za afya zilizopangwa kwenye Kitita Kipya cha NHIF.

b) Waziri Mkuu aongoze mazungumzo ya pamoja baina ya Wizara ya Afya iliyopendekeza Kitita hicho kupitia Kamati Teule yake na Chama cha Watoa Huduma Binafsi za Afya nchini (APHFTA) ili kupata suluhu ya pamoja na kuepusha vifo na madhara makubwa ya kiafya yanayoweza kuwafika Watanzania wengi wanaohudumiwa na vituo binafsi vya afya, ikiwa pande hizo mbili zitaendelea kusigana na kutunishiana misuli. Tathmini iliyofanywa na Benki ya Dunia (WB) imethibitisha kuwa sekta binafsi ya afya nchini Tanzania ina mchango mkubwa unaokadiriwa kufikia theluthi moja ya huduma zote za afya zinazotolewa nchini. Kwa namna yoyote ile wadau wa sekta binafsi ya afya hawapaswi kupuuzwa.

3. Pamoja na wito huu wa dharura, Bunge la Wananchi, kupitia Kamati hii ya Afya na Maendeleo ya Jamii, linaendelea kufanya mapitio na uchambuzi wa kina kuhusu Kitita Kipya cha NHIF na ndani ya siku chache tutatoa tamko lenye uchambuzi na ushauri wa ziada kwa serikali ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza iwapo serikali haitoshughulikia suala hili kwa uzito unaostahili.

4. Nia ya Bunge la Wananchi ni kuona nchi yetu inakuwa na Mfumo Shirikishi wa Uendeshaji wa Bima ya Afya, wenye kuhakikisha upatikanaji endelevu na toshelevu wa huduma za afya, zenye ubora wa hali ya juu na unafuu unaokidhi hali ya vipato vya Watanzania walio wengi, lakini bila kuangamiza ustawi wa vituo vya afya na taasisi zinazomiliki au kuendesha vituo hivyo.

5. Bunge la Wananchi linaamini kwamba uboreshaji wa Kitita cha NHIF unapaswa kwenda sambamba na udhibiti wa vitendo vya kifisadi na ufujaji wa fedha za michango ya wanachama ambao umekithiri kwa muda mrefu. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2021/22 imeainisha ufujaji mkubwa wa fedha za NHIF, ukiwemo ule wa wafanyakazi wa NHIF kujikopesha zaidi ya Shilingi Bilioni 41 na kushindwa kuzirejesha kwa wakati. Bunge la Wananchi, kwa mara nyingine tena, linaitaka serikali kukomesha ufisadi na ufujaji huu mkubwa unaoendelea ndani ya NHIF ili mfuko huu uweze kurejesha ukwasi wake na kumudu kulipia gharama za afya za wanachama wake.

6. Mwisho, Bunge la Wananchi linaendelea kuikumbusha serikali kwamba bado mfumo wa bima ya afya uliopo nchini bado peke yake hauwezi kumuhakikishia Mtanzania huduma bora na za karibu za afya kwani bado nchi yetu ina uhaba mkubwa wa miundombinu ya afya. Serikali inapaswa kutimiza wajibu wake wa kujenga na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya ili watanzania wengi zaidi waweze kufikiwa kwa ukaribu na huduma za afya badala ya kulazimika kutembea au kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

Imetolewa leo tarehe 1 Machi 2024, na:

Mhe Ashura Masoud

Mwenyekiti Kamati ya Afya na Maendeleo ya Jamii.
Bunge la Wananchi