Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Hayati Mzee Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichotokea jana Februari 29, 2024 jijini Dar es salaam.

Chadema itamkumbuka Hayati Mzee Mwinyi kwa namna alivyosimamia mageuzi ya sera za kiuchumi za Tanzania na kuruhusu mifumo ya uhuru wa soko, sera ambayo imekuwa ndio msimamo wa Chadema katika kukuza uchumi na kuchochea maendeleo.

Chadema inaungana na wa-Tanzania kuomboleza msiba huu wa kitaifa. Aidha, Chama kinatoa pole kwa Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dokta Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wajane wa Marehemu, familia, ndugu, jamaa na marafiki

Kama alivyowahi kusema wakati wa uhai wake kuwa maisha ni hadithi nae ameikamilisha hadithi ya maisha yake. Atakumbukwa kwa hekima, busara, uwajibikaji na kujituma kwake wakati wote akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata kabla aliposhikilia wadhifa wa Rais wa Zanzibar na nyadhifa nyengine mbalimbali katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikiwemo nafasi ya Uwaziri na Ubalozi wa Tanzania nchini Misri.

Chadema inaungana na wa-Tanzania wote katika kuomboleza msiba huu na kuenzi mchango wa Hayati alhaj Mwinyi katika utumishi wa Umma.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa Mheshimiwa Freeman Mbowe ataongoza ujumbe wa Chadema katika maziko yaliyopangwa kufanyika Jumamosi Mjini Unguja.

Innalillahi Wainna Ilayhi Rajiuun.

Salum Mwalim
Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar

Share Button