Ndugu zangu Watanzania na wanaCHADEMA,

Nawasalimu kwa upendo mkubwa kutoka Kodivari, Pwani ya Pembe au Cote d’Ivoire kama wanavyoita wenyewe. Nimekuwa huku tangu Disemba 28 iliyopita kwa ajili ya kuiunga mkono timu yetu ya Taifa ambayo, kama mnavyofahamu, iko hapa kwa ajili ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), yaliyoanza wiki moja iliyopita. Sisi sio taifa linalojulikana kwa kufanya vizuri katika mambo mengi ya kimataifa, hasa katika mashindano ya michezo. Kwa vile timu yetu ya Taifa imejitahidi kufuzu katika mashindano ya mwaka huu, kama ilivyofanya kwenye mashindano ya mwaka 2019, niliona ni vyema kuwaunga mkono kwa kuja kuwashangalia na kuwatia moyo uwanjani. Wote tunafahamu wameanza vibaya lakini tusiwakatie tamaa. Bado wanaweza kushinda mechi mbili zilizobaki na kuingia katika ngazi zinazofuata katika mashindano haya.

Ndugu zangu na wanachama wenzangu,

Sasa naomba nizungumzie masuala ya kisiasa ya nchi yetu. Wiki iliyopita, Mwenyekiti wetu wa chama, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, alitoa msimamo wa chama chetu kuhusu miswada mitatu ya sheria zinazohusu masuala ya uchaguzi na vyama vya siasa; na kuhusu mustakbali wa mageuzi ya kidemokrasia katika nchi yetu kwa ujumla. Msimamo huo ulifikiwa kufuatia kikao cha Kamati Kuu ya chama iliyokutana kidigitali mnamo tarehe 8 Januari kutafakari miswada hiyo na hali ya kisiasa nchini kuelekea Uchaguzi wa Vijiji na Mitaa wa baadae mwaka huu, na Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao.

Kama ambavyo chama chetu kimesema mara kwa mara tangu miswada hiyo ilipochapishwa rasmi mwezi Oktoba iliyopita, kwa miswada hii, ni wazi CCM na Serikali ya Rais Samia Suluh Hassan haitaki kufanya mabadiliko yoyote ya maana katika mfumo wetu wa kikatiba na katika mfumo wetu wa uchaguzi. Na kama tulivyosema tangu mapema mwaka jana, hata baada ya mazungumzo ya takriban mwaka mmoja na licha ya ahadi zake ndani na nje ya Tanzania, Rais Samia na CCM yake wamekataa maridhiano ya kisiasa ambayo yangeiwezesha nchi yetu kuondoka kwenye kivuli cha utawala wa kiimla wa chama kimoja na madhara yake yote kwa nchi yetu.

Huu ni mwaka wa Uchaguzi wa Serikali za Vijiji na Mitaa. Kwa sababu ya Katiba na sheria za hovyo za uchaguzi tulizo nazo sasa, kwenye uchaguzi huo miaka mitano iliyopita, wasimamizi wa uchaguzi waliowekwa na CCM waliwaengua wagombea karibu wote wa vyama vya upinzani. Matokeo yake ni kwamba wagombea wote wa CCM walitangazwa washindi wa uchaguzi huo bila kupigiwa kura na mtu yeyote.

Kwa mara ya kwanza katika historia yetu ya Uhuru, kwa miaka mitano inayoishia mwaka huu, tumetawaliwa katika vijiji na mitaa yetu na watu ambao hawajachaguliwa na mtu yeyote. Kwa kukataa maridhiano ya kisiasa na mabadiliko ya maana ya mfumo wa uchaguzi, Rais Samia na CCM wanataka twende kwenye Uchaguzi wa Vijiji na Mitaa wa mwaka huu kwa utaratibu ule ule wa kuengua wagombea wa upinzani na kutawaliwa na watu wasiokuwa na ridhaa ya Watanzania. Kwenye hili hatukubali na hatutakubali.

Ndugu zangu na wanachama wenzangu,

Mwaka ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu. Kwa sababu ya Katiba na sheria za hovyo za uchaguzi tulizo nazo sasa, kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, wasimamizi wa uchaguzi huo waliowekwa na CCM waliwaengua wagombea ubunge wa upinzani katika majimbo 28 ya uchaguzi, takriban asilimia 11 ya majimbo yote ya uchaguzi nchini. Aidha, wasimamizi hao waliwaengua wagombea udiwani katika kata 872, asilimia 22 ya kata zote nchini. Matokeo yake ni kwamba, kwa mara ya kwanza katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, tuna Bunge lenye wabunge wengi ambao hawajachaguliwa na mtu yeyote; na tuna halmashauri za serikali za mitaa yenye madiwani wengi ambao hawajachaguliwa na mtu yeyote.

Kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, wasimamizi wa uchaguzi waliowekwa na CCM waliiba kura na kutangaza matokeo feki ya kura walizopata wagombea urais, ubunge na udiwani. Kura za wabunge, ziwe halali au za wizi, zinaamua idadi ya wabunge wa viti maalum wanaoteuliwa kutoka kila chama; na kiwango cha fedha za ruzuku zinazotolewa kwa vyama vinavyoshiriki kwenye Uchaguzi Mkuu. Idadi ya madiwani, wawe wamepatikana kihalali au kiharamia, inaamua pia idadi ya madiwani wa viti maalum wanaoteuliwa kutoka kila chama kinachoshiriki kwenye Uchaguzi Mkuu. Wizi wa kura, kwa hiyo, unaamua sio tu nani, wa chama gani, ndio waende bungeni na kwenye baraza la madiwani, bali pia nani, wa chama gani, ndio watakaounda serikali na kututawala.

Kwa sababu ya wizi huo wa kura, tuna Rais ambaye hawezi kuthibitisha alishindaje uchaguzi kwa kuwa hawezi kuonyesha kura alizopata kutoka katika jimbo lolote la uchaguzi nchini. Anachoweza kufanya, kwa Katiba hii ya hovyo, ni kusema tu kwamba alitangazwa mshindi na Tume ya Uchaguzi. Aidha, tuna wabunge wa majimbo, wa viti maalum na

madiwani ambao wamepatikana kwa kura feki; na CCM inapata fedha za ruzuku ambazo hazijatokana na kura halali. Kwa miswada hii ya sheria, Rais Samia na CCM inataka twende kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao ili wagombea wetu wakaenguliwe tena, na ili wagombea wa CCM wakapitishwe bila kupingwa tena. Vile vile, Rais Samia na CCM inataka kura za rais, wabunge na madiwani zikaibiwe tena ili CCM iendelee kupata rais, wabunge na madiwani isiowastahili; na ili CCM iendelee kupata fedha za ruzuku isizozistahili. Na kwenye hili pia, hatukubali na hatutakubali.

Ndugu wananchi na wanachama,

Katiba, sheria na taratibu za hovyo za uchaguzi zina madhara ya moja kwa moja kwa wananchi. Uchaguzi Mkuu wa hovyo unazaa Rais asiyekuwa na uchungu wowote na wananchi wala na rasilimali za taifa. Matokeo yake tumeyaona kwa Rais Samia huyu huyu. Bandari zetu zote zimekabidhiwa kwa Waarabu wa Dubai. Hifadhi zetu za misitu na wanyama pori zimekabidhiwa kwa Waarabu hao hao na Wazungu ili wajenge mahoteli ya kitalii au wafanyie biashara ya carbon, wenye kutajirika watajirike na wenye kufukarika – wananchi wetu – waendelee kufukarika. Na wakati udalali huu wa rasilimali za taifa unaendelea, wananchi wetu wanauawa, au kujeruhiwa au kufukuzwa kwenye maeneo yao Ngorongoro, Loliondo, Mbarali, ukanda wote wa magharibi wa Serengeti na karibu katika kila hifadhi ya taifa ya wanyama pori au ya misitu ya nchi hii.

Uchaguzi wa hovyo unazaa Bunge la hovyo na halmashauri za serikali za mitaa na za vijiji za hovyo. Na matokeo yake tumeyaona vile vile. Bunge linalopitisha miswada ya sheria zinazokandamiza wananchi; na

lisilo na uwezo wa kuiwajibisha serikali na watendaji wake kwa matumizi mabaya ya madaraka, ufisadi na utapanyaji wa rasilimali za nchi yetu. Uchaguzi wa hovyo huzaa halmashauri za hovyo zisizokuwa na uwezo wa kusimamia miradi ya maendeleo na huduma za jamii katika maeneo yao kwa manufaa ya wananchi.

Kwa kifupi, serikali ya ukandamizaji wa wananchi na ukiukaji wa haki zao; utitiri wa tozo, kodi, ushuru, ada, michango na kila aina ya unyang’anyi wa mapato ya wananchi. Kwa maneno mengine, uchaguzi wa hovyo huzaa umaskini, uonevu na kila aina ya adha kwa wananchi. Kwa kukataa maridhiano ya kisiasa na kwa miswada hii, Rais Samia na CCM wanataka haya yaendelee. Hatukubali na hatutakubali.

Ndugu wananchi na wanachama,

Tumesubiri CCM na serikali zake wabadilishe msimamo wao kwa miaka mingi. Tumewabembeleza kwa muda mrefu wakubali nchi yetu iondokane na Katiba ya sasa ambayo, kwa misingi na maudhui yake, ni Katiba ya chama kimoja na ya utawala wa kiimla. CCM na serikali zake imeshauriwa na wataalamu iliyowateua yenyewe, wengi wao wakiwa wanaCCM, kwamba nchi yetu inastahili kuwa na Katiba Mpya ya kidemokrasia itakayokuwa na mfumo huru wa uchaguzi.

Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali ilipendekeza hivyo mwaka 1991 wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi. Tume ya Jaji Robert Kissanga ikarudia mapendekezo hayo mwaka 1998 wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa; ambaye pia alipokea mapendekezo hayo hayo kutoka kwa Kamati ya Jaji Mark Bomani mwaka 2003. Tume ya Waziri Mkuu mstaafu Joseph Sinde Warioba ilitengeneza mpaka na

rasimu ya Katiba Mpya mwaka 2013, baada ya kazi kubwa ya kihistoria iliyochukua miaka miwili na gharama kubwa wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Bunge Maalum la Katiba liliketi kwa karibu miezi sita, na kwa gharama kubwa, na kutengeneza Katiba Inayopendekezwa mwaka 2014.

Nje ya jitihada hizi za kiserikali, serikali za CCM zimeshauriwa na watazamaji wa chaguzi zetu zote tangu mwaka 1995, wa kitaifa na wa kimataifa, kwamba ili chaguzi zetu ziwe huru, za haki na zinazokubalika kwa mujibu wa misingi ya chaguzi za kidemokrasia ya kimataifa, ni lazima kuwe na mabadiliko ya kikatiba na kisheria katika mfumo wetu wa uchaguzi. Baada ya Uchafuzi Mkuu wa mwaka 2020, watazamaji wa uchaguzi waliotumwa na Umoja wa Afrika walipendekeza katika taarifa yao rasmi kwamba serikali ya Tanzania ikamilishe mchakato wa Katiba Mpya uliokwamishwa na serikali ya CCM mwaka 2014, ili uchafuzi wa 2020 usirudiwe mwaka 2025.

Jitihada zote hizi zimeshindikana kwa miaka yote hii kwa sababu moja tu. CCM na serikali zake haitaki mabadiliko ya aina yoyote ya kisiasa na ya kikatiba yatakayoiletea nchi yetu Katiba Mpya, mfumo mpya wa uchaguzi na utaratibu mpya wa kujitawala. Na CCM na serikali zake haitakubali mabadiliko yoyote bila kulazimishwa kwa nguvu ya umma ya wananchi wote wenye nia njema na nchi yao. Mpigania haki za Waafrika aliyeishi karne ya kumi na tisa aliwahi kusema: ‘Mamlaka kandamizi huwa haitoi chochote bila madai. Haijawahi kuwa hivyo, na haitakaa iwe hivyo.’

Kwa sababu hiyo, wote tunaotaka mabadiliko chanya katika maisha yetu; tunaotaka mfumo bora wa utawala unaojali mahitaji na maslahi ya

wananchi walio wengi, badala ya kikundi kidogo cha watawala na familia zao na marafiki zao; wote tunaotaka mfumo bora wa uchaguzi utakaotupatia viongozi halali wa kuchaguliwa wanaojali shida za wananchi, wenye uchungu na rasilimali za taifa letu na wanaowajibika kwetu, hatuna budi kuungana ili kumdai Rais Samia na CCM yake wabadili msimamo wao kuhusu Katiba Mpya na mfumo mpya na huru wa uchaguzi.

Chama chetu kimeshatangaza kwamba baada ya Rais Samia na CCM kukataa maridhiano ya kisiasa na mabadiliko ya kikatiba na ya kisheria, wakati umefika sasa wa kuyadai mabadiliko hayo kwa njia za kidemokrasia na za amani zinazokubalika duniani kote: yaani maandamano ya amani na njia nyingine za kidemokrasia za kushinikiza mabadiliko ya kisiasa. Chama chetu kimeshatangaza tarehe 24 ijayo kuwa ndio siku ya kuanza harakati hizi mpya za kuleta mabadiliko ya kweli katika nchi yetu.

Pamoja na umuhimu wa kuiunga mkono timu yetu ya taifa katika kipindi ambacho inatuwakilisha katika mashindano haya makubwa barani Afrika, mustakbali wa baadae wa nchi yetu ni muhimu zaidi. Mashindano ya AFCON yataendelea kuwepo; nchi yetu inaweza kuingizwa kwenye maafa makubwa ya kisiasa endapo utawala huu wa CCM utaachwa kuendelea madarakani kwa misingi ya sasa ya kikatiba, kisheria na kiutawala.

Hivyo basi, napenda kuwafahamisha kwamba mimi nitakuwepo Dar es Salaam na nitashiriki maandamano ya amani ya siku ya tarehe 24 ya wiki ijayo. Lakini hili haliwezi kuwa jukumu langu peke yangu, au la Mwenyekiti Mbowe peke yake au la wanaCHADEMA peke yao. Kwa

sababu Katiba Mpya na bora na mfumo bora wa uchaguzi vinatuhusu sisi wote, naomba kila mmoja wetu ajitafakari na atafakari nafasi yake katika mapambano haya na katika ustawi wa taifa letu. Kwa sababu hiyo, ninatoa rai kwa wananchi wengine wote wa Tanzania wenye nia njema na nchi yetu nao wawepo Dar es Salaam siku hiyo ya kihistoria ili nao washiriki katika maandamano hayo.

Asanteni kwa muda wenu na kwa kunisikiliza.

Tundu A.M. Lissu MAKAMU MWENYEKITI

Share Button