CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO

(CHADEMA)

 

MSIMAMO WA KAMATI KUU YA CHAMA KUHUSU MISWADA 3 YA SHERIA ILIYOWASILISHWA BUNGENI TAREHE 10 NOVEMBA, 2023

 

 1. UTANGULIZI

Kamati Kuu ya Chama iliketi kwenye kikao chake Cha dharura tarehe 8/01/2024 na ilikuwa na ajenda mbili mahususi; kujadili miswada 3 ya Sheria za Uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa iliyowasilishwa Bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza tarehe 10 Novemba, 2023 na Kujadili Hali ya ugumu/kupanda kwa gharama za maisha nchini.

 

Katika uchambuzi wake Kamati Kuu ya Chama ilijiridhisha pasipokuwa na shaka kwamba, miswada yote mitatu kama ilivyowasilishwa Bungeni haina na wala haionyeshi dhamira au nia njema ya kuwezesha kuwepo kwa uchaguzi ulio huru na haki; na kwa kiasi kikubwa miswada hiyo hailengi kukuza Demokrasia katika Taifa letu bali kuididimiza.

 

 1. TATHIMINI YA KAMATI KUU

 

Kamati Kuu katika tathimini yake imechambua na kujiridhisha kwamba Serikali haitaki kuwepo kwa maboresho ya msingi katika mfumo wa uendeshaji wa chaguzi nchini na ukuaji wa demokrasia (katika kufanya na kuendesha siasa za usawa baina ya vyama) na hii ni kutokana na sababu zifuatazo;

 

 1. Rais aliunda Kikosi kazi ambacho kilitumia mabilioni ya Fedha za watanzania na kiliandika ripoti yake na kuweka mapendekezo mahususi juu ya haja na nia ya kuwa na Tume Huru ya uchaguzi ili kuliwezesha Taifa kuwa na uchaguzi huru na haki; Lakini katika hali ya kushangaza miswada iliyowasilishwa Bungeni haikuzingatia mapendekezo ya Kikosi Kazi cha Rais mwenyewe.

 

 1. Tangu mfumo wa Vyama vingi vya siasa uanze nchini mwaka 1992, kwenye chaguzi zote waangalizi wa kimataifa na ndani wa chaguzi zote wamekuwa wakiandika taarifa za mwenendo wa uchaguzi na kuonyesha mapungufu mengi kwenye usimamizi wa chaguzi zetu ikiwa ni kutokana na kukosekana kwa Tume Huru ya Uchaguzi na hivyo kila wakati wamekuwa wakishauri haja na umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, ila mapendekezo yao yametupwa yote na miswada hii iliyowasilishwa Bungeni na Serikali.

 

 1. Wadau mbalimbali wakiwemo vyama vya siasa, asasi za kiraia, Viongozi wa Dini na Makundi mbalimbali ya kijamii wametoa maoni yao kuhusu umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya uchaguzi, ila kwenye miswada hii maoni ya wadau hao hayakutiliwa maanani na Serikali na yamepuuzwa yote.

 

4.Yamefanyika Makongamano mbalimbali ambayo yamekuwa yakiratibiwa na Baraza la Vyama vya Siasa, TCD na wadau wengine na maoni ya kuboresha mfumo wa uendeshaji wa chaguzi zetu yalitolewa kwa kina, ila kwenye miswada iliyowasilishwa Bungeni maoni ya wadau hao hayakuzingatiwa kabisa pamoja na Serikali kuahidi kuwa itazingatia maazimio ya wadau katika kuboresha mifumo ya chaguzi zetu.

 

 1. Chadema tumekuwa na vikao vya maridhiano na Serikali na CCM na tuliwasilisha mapendekezo ya namna ya kukwamua mkwamo uliopo nchini hasa kwenye maeneo ya Katiba Mpya na kuboresha mifumo ya chaguzi zetu ikiwa ni pamoja na mapendekezo  mahususi ya jinsi ya kuipata Tume Huru ya uchaguzi nchini, ila miswada hii imepuuza kabisa mapendekezo yetu na hawakuona umuhimu wa kuyazingatia.

 

 1. Mashauri mbalimbali yamefunguliwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki, ikiwemo iliyofunguliwa na Freeman Mbowe na wenzake dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( kesi namba 3&4,2019) ambayo walalamikaji walilalamikia mabadiliko ya Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2019 na hususani vifungu vya 3,4,5,9,15 na 29 kuwa vinakiuka mkataba wa Afrika ya Mashariki ibara za 6(d),7(2) na 8(1)(c).

 

Mahakama ya Afrika Mashariki katika hukumu yake ya tarehe 25/3/2022 ambapo kesi hiyo ilisikilizwa na Majaji 5 ilikubaliana na waleta maombi kwamba vifungu husika vya sheria ya vyama vya siasa vinakiuka mkataba wa Afrika Mashariki na kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurekebisha  au kufuta vifungu husika ili wasiendelee kuvunja mkataba ambao Serikali yenyewe ilisaini lakini katika miswada hii, serikali haijakubali kutekeleza maamuzi haya ya Mahakama kinyume kabisa na dhana ya utawala Bara.

 

6.(b) Kesi iliyofunguliwa katika Mahakama ya Afrika ya Haki ambayo ilifunguliwa na Bob Chacha Wangwe na LHRC dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo walalamikaji walikuwa wanalalamikia vifungu vya Sheria ya uchaguzi ya mwaka 1985 vifungu vya 6(1),7(2) na 7(3) vinavyowapa mamlaka Wakurugenzi wa Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

 

Katika uamuzi wake Mahakama ya Haki ya Afrika ilitoa uamuzi kuwa  Wakurugenzi wa Halimashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi  ni kukiuka mkataba wa Afrika ibara ya 13(1) na hivyo kuitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuondoa vifungu hivyo vya Sheria . Aidha Mahakama ilitoa amri Kwa Tanzania kuwasilisha kwenye Mahakama hiyo taarifa ya utekelezaji wa uamuzi huo na ilipewa muda wa miezi 12 kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa uamuzi huo ambao uliyolewa tarehe 13/06/2022.

 

 

Pamoja na uwepo wa amri ya Mahakama ya Haki ya Afrika, miswada iliyowasilishwa Bungeni imepuuza kabisa amri hii ya Mahakama na inaendelea kupendekeza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri waendelee kuwa Wasimamizi wa uchaguzi.

 

 1. Taarifa ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2020 iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa mapendekezo yake jinsi ya kuiwezesha Tume kuwa huru na iweze kusimamia uchaguzi wa Haki, ambapo miongoni mwa mapendekezo ya Tume ni;

(i)Itungwe Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo itaiwezesha Tume kutekeleza Majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

(ii)Kuwe na watendaji wa Tume Hadi ngazi ya Halimashauri

 

Pamoja na udhaifu na mapungufu ya Tume ila kwenye haya mapendekezo yake wameuona udhaifu wao na kutoa mapendekezo ambayo yataiwezesha kufanya majukumu yake kwa uhuru na kutenda Haki! Miswada iliyowasilishwa Bungeni haikuzingatia kabisa mapendekezo haya ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo imeendesha chaguzi mbalimbali nchini na kuona udhaifu ulipo.

 

Kutokana na uchambuzi wa kina na tathimini ya kikao cha Kamati Kuu imeazimia mambo yafuatayo;

 

Miswada iliyowasilishwa Bungeni tarehe 10 Novemba, 2023 iondolewe Bungeni na badala yake yafanyike mambo yafuatayo;

 

 1. Serikali iwasilishe muswada Bungeni wa kukwamua mchakato wa Katiba Mpya pamoja na mwelekeo (Road Map) wa kila hatua mpaka ipatikane Katiba Mpya itakayopatikana kwa kuzingatia muafaka wa Kitaifa.

 

 1. Serikali iwasilishe Bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya mpito (minimum Reforms) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) ya mwaka 1977 ili uchaguzi uwe huru na haki baada ya kuondoa mapungufu ya kikatiba yaliyopo sasa kwa sababu Sheria zinatungwa kwa mujibu wa Katiba ambayo kwa sasa ina mapungufu mengi ambayo yanaathiri Sheria zinazoenda kutungwa.

 

 1. Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa; Serikali iwasilishe Bungeni muswada ambapo pamoja na mambo mengine ya uchaguzi huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ipewe mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na sio kusimamiwa na TAMISEMI kwa Kanuni ambazo zinatungwa na Waziri.

 

 1. ⁠Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya siasa (Sheria ya Vyama vya Siasa kama ilivyorekebishwa mwaka 2019 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi) uondolewe kwa sababu haitatui changamoto zilizopo. Aidha muswada haujazingatia Amri za Mahakama ya Afrika Mashariki ambapo baadhi ya vifungu iliamriwa kwamba vinakiuka Mkataba wa Afrika ya Mashariki.

 

 1. ⁠Miswada iliyowasilishwa Bungeni tarehe 10 Novemba, 2023 iondolewe na kuandikwa upya kwa mujibu wa marekebisho ya mpito ya Katiba ya JMT ya mwaka 1977 yatakayofanyika kama ilivyopendekezwa hapo awali.

 

 1. Katibu Mkuu wa Chama aongoze jopo la chama litakalowasilisha maoni na msimamo wa Chama mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na utawala. Katibu Mkuu wa Chama alifanya hivyo ila alikataliwa kusoma mbele ya Kamati maoni yetu ya ujumla kuhusu miswada hiyo na kutakiwa kusoma uchambuzi wa vifungu kwa vifungu jambo ambalo linaonyesha kuwa tayari Kamati imeshafanya uamuzi na ndio maana haitaki kusikiliza maoni ambayo yako nje ya vifungu husika vya miswada.

 

 1. MAAZIMIO YA KAMATI KUU

Kwa kuwa mapendekezo yote hayo yameonekana kukataliwa hivyo basi Chama kinatangaza maandamano ya amani ya kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali wa uchaguzi nchini ambayo yataanza Dar Es salaam tarehe 24/01/2024 mpaka hapo Serikali itakapoondoa miswada hiyo Bungeni .

Kuhusu kupanda kwa gharama nchini, Kamati Kuu inaitaka serikali kuchukua hatua madhubuti ili kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi wake ikiwa ni pamoja na;

 • Kupunguza kodi na tozo kwenye bidhaa na huduma muhimu za wananchi
 • Iondoe Matumizi ya anasa Serikalini
 • Ithibiti Rushwa na Ufisadi uliokithiri Serikalini
 • Ipeleke Mpango na mkakati wa kuwakwamua wananchi na Hali ngumu ya maisha  Bungeni ikiwa ni pamoja na kushusha bei ya bidhaa muhimu au kuweka ruzuku kwenye baadhi ya bidhaa.

 

Imetolewa Leo Tarehe 13 Januari, 2024 Na;

 Freeman Aikaeli Mbowe,

Mwenyekiti wa Chama- Taifa.

 

 

Share Button