Baraza la Uongozi la Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IDU) limeitaka Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kurudisha mara moja mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya pamoja na kufanya mabadiliko ya sheria na mifumo yote ya kitaasisi inayohusika na uchaguzi ili pamoja na mambo mengine kuhakikisha uwepo wa uchaguzi huru, wa haki, shirikishi na unaokubalika kabla ya mwaka 2025.

Msimamo huo wa IDU umetolewa kupitia azimio lake maalumu lililoangazia hali ya siasa na Demokrasia Tanzania.

Kupitia azimio hilo, IDU imesema kwamba ni muhimu Serikali ikaanzisha kwa haraka mchakato wa kuandika katiba mpya ya nchi ili kuleta mabadiliko makubwa yatakayohakikisha na kuwezesha upatikanaji wa Tanzania salama, shirikishi na yenye maendeleo.

Baraza hilo lililoongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa 22 wa Canada Mheshimiwa Stephen Harper pamoja na Waziri Mkuu mstaafu wa Norway Mheshimiwa Erna Solberg limeeleza pia kupitia tamko lake juu ya Tanzania kwamba limeyapokea maamuzi ya kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa Vyama vya Siasa Tanzania kwa tahadhari huku likitaka kufutwa kwa sheria zote kandamizi zilizotungwa na Serikali ya awamu ya Tano.

Aidha IDU imeeleza masikitiko yake kufuatia kitendo cha Bunge la Tanzania kupitisha sheria mpya ya usalama wa Taifa ambayo linaiona kama hatua ya kuhalalisha matendo maovu ya maafisa wa taasisi hiyo yanayoweza kuirudisha Tanzania kwenye matendo ya kupotezwa kwa raia, ukamataji wa hovyo, utesaji, mauaji na unyanyasaji wa viongozi, wanachama na wafuasi wa Vyama vya Upinzani kama ilivyokuwa kwenye utawala uliopita.

Katika tamko hilo lililoazimiwa Jijini London nchini Uingereza ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya miaka 40 ya kuanzishwa kwa IDU na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali mashuhuri wakiwemo Mawaziri Wakuu wastaafu Boris Johnson (Uingereza), John Howard na Morison Scott (Australia) pamoja na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani Michael Pompeo, IDU imeitaka Serikali ya Rais Samia Hassan kufuta kwa haraka sheria zote zinazominya uhuru wa kujieleza na kukutana nchini ikiwa ni sehemu ya kutaka kuona Tanzania inawekwa kwenye mstari sahihi wa ustawishaji wa demokrasia na kuimarisha utawala wa sheria.

Ili kuzuia wizi wa uchaguzi nchini kama ilivyokuwa mwaka 2019 kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2020 IDU kupitia tamko hilo limeitaka Serikali ya Rais Samia kuhakikisha kuwa Tanzania haiendi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kabla ya kufanya mabadiliko makubwa ya kikatiba na kisheria juu uendeshaji wa chaguzi nchini.

Imetolewa leo 12 Julai, 2023 Jijini Dar es salaama na;

John Mrema
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya nje