Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mhe. Tundu Lissu amesema kuwa ili kuharakisha utekelezaji wa agenda kuu za Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, zilizomo katika kauli mbiu ya Uhuru, Haki na Maendeleo ya Watu, atakuwa Rais wa Katiba Mpya, hali ambayo itamtofautisha na marais wengine wote watano ambao wameongoza Tanzania tangu uhuru hadi sasa.

Akiwataja kwa majina marais wastaafu hao, Mhe. Lissu amesema kuwa wote waliongoza nchi kwa kutumia mfumo wa utawala na siasa ambao msingi wake uliwekwa kwenye Katiba ya Mwaka 1962, unaotumika hadi sasa ambao umepora mamlaka ya wananchi kujiamulia mstakabali wa masuala yote yanayogusa nyanja mbalimbali katika maisha yao na kuyakabidhi kwa Rais ambaye ana nguvu kubwa za kuamua kila kitu kutokea makao makuu ya nchi, hali ambayo inawanyima haki wananchi, kuminya uhuru wao na kuchelewesha maendeleo yao.

Mhe. Lissu amesisitiza kuwa masuala yote ambayo anayazungumza kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kwa ajili ya Tanzania mpya ambayo itaweka mbele uhuru, haki na maendeleo ya watu, yanawezekana kutekelezeka kuanzia Oktoba 28, mwaka huu, wananchi watakapompigia kura nyingi kumchagua kuwa Rais wa sita wa Tanzania, ambapo ndani ya siku 100, kama inavyoelekezwa kwenye Ilani ya Chadema ya mwaka 2020, Serikali yake itaanzisha mchakato wa Katiba Mpya, ili kufanya mabadiliko makubwa, ikiwemo kurejesha mamlaka kwa wananchi.

“Agano langu kwenu ninyi Watanzania wa Kigoma na Watanzania wote kwa ujumla…naomba kusisitiza kuwa sitakuwa kama Rais Magufuli, Rais Kikwete, Rais Mkapa, Rais Mwinyi au Rais Nyerere. Agano langu na ninyi Watanzania wenzangu ni kwamba, nitakuwa Rais wa Katiba Mpya. Nyerere aliwahi kukiri alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza kuwa Katiba yetu ilikuwa imempatia mamlaka makubwa mno yanayoweza kumfanya awe dikteta. Wengine wote waliomfuata wametawala katika mfumo huo huo unaowafanya wawe madikteta. Sasa sitaki kuwa kama wao.

“Ninaposema kuwa sitaki kuwa kama Nyerere, au Mwinyi au Mkapa au Kikwete au Magufuli, ninamaanisha kuachana na mfumo huo wa kidikteta ambao ulimpatia Rais wa Tanzania mamlaka ya kuamua kila jambo katika nchi na kuyatoa mikononi mwa wananchi. Katika nchi yetu, Rais ni alfa na omega. Mfano rahisi ni uteuzi ambapo anaweza kuteua kila mtu au watu wote walioteuliwa wanafanya kazi kwa niaba ya rais. Hii si sawasawa. Mimi nitakuwa Rais wa Katiba Mpya ambayo itaweka msingi wa mabadiliko makubwa ya kurejesha mamlaka ya watu kujiamulia masuala yao, yanayohusu maendeleo yao hapo hapo walipo badala ya wote kugeuka kuwa ombaomba kwa rais. Yote haya yanawezekana mkinipigia kura za ushindi wa kimbunga na kunichagua niwe Rais wenu hapo Oktoba 28, mwaka huu.

“Ni hatari sana. Tumefikia mahali ambapo Katiba yetu inasema Rais halazimiki kufuata au kuzingatia ushauri kutoka kwa mtu yeyote. Hawajibiki kwa mtu yeyote. Mfumo huu umewanyima kabisa wananchi mamlaka ya kuamua kuhusu maendeleo yao. Nijuavyo ni Mungu tu ndiye hashauriki…Baba Askofu hapa ananiambia kuwa hata Mungu huwa anashauriwa na Roho Mtakatifu. Ndiyo maana sisi Chadema tunapendekeza kwenye Ilani yetu kwamba nchi yetu iwe na utawala wa majimbo,” amesema Mhe. Lissu.

Akizungumza katika mikutano ya kampeni iliyofanyika leo Jumamosi, Septemba 19, 2020, katika maeneo ya Tongwe, Mpanda Vijijini, mkoani Katavi, kisha Mwandiga na Kalinzi (Kigoma Kaskazini), Mnanila (Buhigwe) na kumalizia mkutano wa mwisho eneo la Mwanga Centre, Kigoma mjini, mkoani Kigoma, Mhe. Lissu amesisitiza agenda ya ya kuyapatia kipaumbele maeneo ya pembezoni mwa nchi, hususan yaliyoko mipakani, kwa kuyafanya maeneo maalum ya kiuchumi, ambapo wananchi watakuwa huru kufanya biashara kwa kuuza katika nchi ambazo Tanzania inapakana nazo, ili wajipatie kipato, kuongeza uzalishaji na kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimae taifa kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Lissu ametoa wito maalum kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma, kuendeleza msimamo wao usioyumba wa kuunga mkono mabadiliko tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, ambapo amewataka kuongoza kwa mfano hai katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kwa kuwachagua wagombea wa upinzani watakaokuwa na uwezo wa kuiondoa CCM madarakani, kuanzia udiwani, ubunge na urais, kwenye maeneo yote, mkoa mzima.

Akihitimisha mikutano ya leo, akiwa mjini Kigoma, Mhe. Lissu ametoa rai kwa watumishi wote wa umma, wakiwemo Askari Polisi, Wanajeshi, Walimu, Wauguzi na kadhalika na wengine wote watakaokwenda kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, kusimama upande wa haki, bila kupendelea upande wowote kwa sababu haki watakayoitenda, ndiyo itakayoliinua taifa letu.

Imetolewa leo Jumamosi, Septemba 19, 2020 na;

Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano

Share Button