MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI YA MWAKA 2020 (THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS)

(Chini ya Kanuni ya 86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Januari, 2016)

________________

 1. UTANGULIZI
 2. Mheshimiwa Spika, naomba kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na nguvu kuweza kuendelea kutekeleza majukumu yangu ya kibunge nikiwa na utimamu wa mwili na akili. Naomba pia kuwatakia heri waumini wa dini ya kiislamu mfungo mwema wanaoendelea nao, funga zao zipokelewe na Mwenyezi Mungu na zikafanyike sadaka ya kulinusuru Taifa hili na janga la Corona linalotukabili.
 3. Mheshimiwa Spika, Napenda pia kutoa Shukrani zangu za dhati Kwa Kiongozi wa kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (MB) kwa kuniteua kuwa msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara hii. Uteuzi huu, ni ishara ya imani aliyonayo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwangu mimi binafsi, Ni heshima kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, familia yangu, wanachama wenzangu na viongozi wenzangu ambao kwa nyakati mbalimbali mawazo yao yamenifanya kuwa hivi nilivyo leo hii, nawashukru sana. 
 4. Mheshimiwa Spika, Napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Sabrina H. Sungura (Mb) anayewakilisha Mkoa wa Kigoma kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Naibu waziri kivuli na Msaidizi wangu katika wizara hii, sote kwa pamoja tunaahidi utendaji uliotukuka.
 5. Mheshimiwa Spika, Mabadiliko haya yanafuatia kadhia aliyopata aliyekuwa msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara hii, kwa kuvamiwa na kushambuliwa, na kulazimika kupelekwa ughaibuni kupata tiba na hatimaye kupoteza Ubunge wake akiwa huko. Mabadiliko haya, kwa mara ya kwanza, katika historia ya Taifa hili, yamepelekea kuundwa kwa Baraza Kivuli la Mawaziri lenye uwakilishi wa wananawake kwa zaidi ya 50%. Napenda kutumia fursa hii kumpongeza Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa kutambua na kuthamini uwezo wa wanawake katika utendaji.
 6. Mheshimiwa Spika, Napenda pia kutumia fursa hii kuwapongeza waheshimiwa Wabunge wenzangu ambao wameteuliwa kuwa wasemaji wa Kambi yetu katika wizara mbalimbali, binafsi ninaamini kwamba wataonesha uwezo mkubwa katika wizara husika na watawatumikia watanzania kwa uaminifu Mkubwa. Nawatakia kila la kheri katika majukumu mapya. Ushauri wangu kwao, wahakikishe wanajipambanua kwa kuwa waumini wa kuheshimu matakwa ya Katiba na sheria za taifa hili, waamini kwamba Tanzania ni kubwa kuliko mtu yoyote hata awe na madaraka makubwa kiasi gani.
 7. Mheshimiwa Spika, Mwisho lakini si kwa umuhimu, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru familia yangu kwa kunivumilia pale ninapokuwa mbali nao katika kutekeleza wajibu na majukumu yangu ya kisiasa, Nawashukuru kwa kuendelea kuniunga mkono na kuniombea wakati wote, uimara wenu umekuwa ni nguzo muhimu sana kwangu katika kipindi chote cha utumishi wangu hapa Bungeni. Mumekuwa nguvu yangu asanteni sana!
 8. Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo,  sasa naomba  nijielekeze kwenye Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 8 wa mwaka 2020 (THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) 2020)
 9. Mheshimiwa Spika, Muswada huu unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria Kumi na Nne ambazo ni:
  1. Sheria ya Mawakili, Sura ya 341,
  2. Sheria ya Mfuko wa Pembejeo, Sura ya 401.
 • Sheria ya Umeme, Sura ya 131,
 1. Sheria ya Mbolea, Sura ya 378,
 2. Sheria ya Misitu, Sura ya 323,
 3. Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali ya Vyakula vya Mifugo, Sura ya 180,
 • Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1,
 • Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300,
 1. Sheria ya Ulinzi wa Taifa, Sura ya 192,
 2. Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura ya 282,
 3. Sheria ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Sura ya 284,
 • Sheria ya Mbegu, Sura ya 308,
 • Sheria ya Tasnia ya Sukari, Sura ya 251 na
 • Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 283.
 1. Mheshimiwa Spika, katika mabadiliko hayo ya sheria hoja kubwa inayosemwa kusukuma mabadiliko haya ni maboresho yanayolenga kuwezesha sheria husika ziendane na mabadiliko ya wakati na kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake. Ikiwa jambo hili ni kweli, basi kulikuwa na haja ya kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sheria hizi ili waweze kutoa maoni yao kuhusu maboresho haya. Uharaka na mabadiliko ya ratiba kuhusu mswaada huu unaminya muda na maandalizi kwa wadau mbalimbali kutoa maoni yenye lengo la kulisaidia Taifa hili.

 

 1. MAPITIO YA VIFUNGU KATIKA MUSWADA NA MAONI YA KAMBI RASMI
 2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani itapitia marekebisho ya vifungu katika sheria zile tu ambazo imeona kuna umuhimu wa kufanyiwa marekebisho.
 3. Sheria ya Mfuko wa pembejeo, Sura ya 401.
 4. Mheshimiwa Spika, Mabadiliko yanayopendekezwa katika Sheria hii ni pamoja na marekebisho katika kifungu cha 2, ambacho inapendekezwa kuongezwa tafsiri ya msamiati “agricultural machinery” ndani ya Sheria hiyo kwa lengo la kutoa tafsiri pana ya msamiati huo kujumuisha nyenzo zote muhimu zilizokusudiwa na Sheria. Aidha kwa mujibu wa mswaada, Kifungu cha 7 kinarekebishwa ili kuainisha wajumbe wa Bodi ya Wadhamini watakaoteuliwa na Waziri.
 5. Mheshimiwa Spika, Inapendekezwa kuwa, kifungu kipya cha 9A kiongezwe ili kuweka utaratibu wa kuomba mikopo katika Mfuko wa Pembejeo. Aidha, kifungu kipya cha 12A kinapendekezwa kuongezwa ili kuweka utaratibu wa rufaa kwa mtu asiyeridhika na maamuzi ya Bodi. Lengo ni kuweka mfumo madhubuti wa kushughulikia malalamiko ya wakulima dhidi ya Mfuko wa Pembejeo.
 6. Mheshimiwa Spika, ukiangalia mapendekezo ya marekebisho ya Sheria huu, utagundua kwamba si vifungu vyote vinavyofanyiwa mapendekezo na au vifungu vilivyokuwepo katika sheria mama ambavyo vinaondoa kero ya wakulima kwenye pembejeo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba mabadiliko kwenye sheria hii, iongeze kifungu cha kuitaka serikali kuhakikisha inatenga asilimia 40 ya bajeti ya wizara ya kilimo kwa ajili ya pembejeo za kilimo. Aidha ni muda sasa kupitia marekebisho ya sheria hii kuongeza kifungu kinachotoa adhabu kali kwa watumishi wa Serikali wanaotumia madaraka yao vibaya na kuiba pembejeo ambazo zinalenga kuwasaidia wakulima na badala yake zinaishia kuwanufaisha watendaji wa serikali huku wakulima wakikosa pembejeo. 
 7. Sheria ya Umeme, Sura ya 131
 8. Mheshimiwa Spika, Sehemu ya Nne ya Muswada uliwasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu unapendekeza marekebisho katika Sheria ya Umeme. Kifungu cha 3 tafsiri ya misamiati “licensee” na “supply” vinarekebishwa kwa lengo la kuboresha tafsiri ya misamiati hiyo na pia kuongeza tafsiri ya misamiati mingine ambayo kwa sasa haijatafsiriwa katika Sheria. Kifungu kipya cha 4A kinapendekezwa kuongezwa ili kuweka nafasi ya Kamishna wa Masuala ya Umeme na kuainisha mamlaka na majukumu yake. Lengo la marekebisho haya ni kutambua kisheria nafasi na majukumu ya Kamishna wa Masuala ya Umeme kama ilivyo kwa makamishna wengine wa mafuta na madini na ambao nafasi na majukumu yao yapo kisheria.
 9. Mheshimiwa Spika, Swali ambalo kila mtanzania anapaswa kujiuliza ni ikiwa changamoto ya Taifa hili kwenye sekta ya umeme ni kukosekana kwa kamishina wa umeme au ni changamoto za uzalishaji na usambazwaji wa umeme hapa nchini. Ni muhimu kutafakari jamabo hili kwa kina kwa vile inaonekana kama tukishapata kamishina kama mapendekezo ya sheria yalivyo changamoto za umeme hapa nchini zitakuwa zimefikia kikomo, jambo ambalo siyo la kweli.
 10. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 18 cha mswaada kinarekebisha Kifungu cha 28(8) cha Sheria ya Umeme kwa lengo la kuwezesha mteja kurudishiwa gharama na mtoa huduma ambazo mteja amegharamia wakati wa kuunganishiwa umeme. Kifungu hicho kinasema
 11. “The principal Act is amended in section 24, by-

(a) deleting subsection (8) and substituting for it the following:

“(8) Notwithstanding any payments made for supply of electrical energy, electric supply lines shall be property of the licensee and may be used to supply other persons:

Provided that, such use does not prejudicially affect the supply of electrical energy to the person who first required such electric supply lines to be laid down or erected.

(9) A person who made payment in terms of subsection (8) shall be entitled to repayment by the licensee through reimbursement of cost of the electricity purchased or consumed at the rate and in the manner specified in the regulations.”;

 1. Mheshimiwa Spika, hoja yetu ya msingi katika kifungu hiki ni namna gani mteja ataweza kurejeshewa gharama ambazo ametumia katika kuunganishiwa huduma ya umeme. Ni kwa nini sheria isimpatie jukumu hilo mtoa huduma la kuwaunganishia wateja huduma bila kuwataka wapata huduma kulipa gharama husika kwa kisingizio cha kurejeshewa gharama hizo. Chnagamoto ya kifungu hiki iko katika kanuni ambazo sasa zitatungwa ili kuleta utekelezwaji wako, Kmabi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawasiwasi kwamba huenda yaliyowahi kutokea kwenye utungwaji wa kanuni, likiwemo sakata la kikokotoo likajirudia na hivyo kutoleta tija kwa mpata huduma ya umeme.
 2. Mheshimiwa Spika, ikiwa kwa mfano hadi sasa, yako madai ya marejesho ya VAT returns ambazo kwa taarifa za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni zinaonesha Serikari bado inadaiwa na wafanya biashara na hadi sasa hawajalipwa, uhalali wa kusema wananchi watakaounganishiwa umeme watarejeshewa gharama zao unatoka wapi? Ni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba, gharama za kuunganishiwa huduma ya umeme zitolewe na kugharamikiwa na mtoa huduma ya umeme, wajibu wa mwananchi na mpata huduma iwe ni kulipia huduma hiyo lakini gharama za miundombinu ya nishati ya umeme liwe na mtoa huduma.
 3. Mheshimiwa Spika, Kifungu kipya cha 48A kinaongezwa kwa lengo la kubainisha adhabu ya jumla kwa makosa ambayo adhabu yake haikuainishwa mahsusi katika Sheria. Hata hivyo kiwango cha adhabu kinaonekana kuwa ni kikubwa na hakiaksi uhalisia na madhumuni ya dhana nzima ya adhabu.
 4. Mheshimiwa Spika, kifungu cha 27 cha Mswaada kinarekebisha sheria mama kwa kuongeza kifungu kipya cha 48A ambacho kinahusu adhabu kwa mamkosa yasiyokuwa na adhabu, kifungu hicho kinasomeka kama ifuatavyo:
 5. The principal Act is amended by adding immediately after section 48 the following:

“General penalty

48A. A person convicted of an offence under this Act for which no specific penalty is expressly provided, shall upon conviction, be liable to a fine of not less than three million shillings but not exceeding ten million shillings, and in the case of a continuing offence, to a fine not exceeding one million shillings for every day during which the offence continues after conviction.”

 1. Mheshimiwa Spika, kwa mustakabari mwema wa uendeshaji wa sekta ya umeme ni muhimu sana sheria hii ikaweka adhabu ambazo zinatekelezeka. Mapendekezo haya ambayo yanalenga kutoza adhabu ya shilingi milioni moja kwa kila siku ni mapendekezo ambayo yanakwenda kinyume na dhana nzima ya adhabu kwa binadamu, hata hivyo ni jambo la kushangaza kwa sababu inaonekana tunatunga sheria ambayo hata sisi wenyewe humu ndani, hakuna uhakika kama tunaweza kulipa adhabu hii ambayo inapendekezwa na sheria hii.
 2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kipindi cha miaka Mitano sasa, imekuwa inalishauri Serikali mambo mengi yanayohusu sekta ya Umeme hapa nchini, ambayo tulitarajia sasa kuyaona hata yakijitokeza katika mabadiliko ya sheria ya umeme. Mabadiliko haya (reform) ingeboresha huduma hii na hivyo kuwa chachu ya maendeeo kwa wananchi; baadhi ya matarajio yetu yalikuwa ni sheria kufanyiwa maboresho katika Nyanja zifuatazo:
 3. Kwamba, Sheria ingefanya maboresho katika Shirika la Umeme Nchini TANESCO na kuligawa kama ambavyo tumekuwa tukipendekeza. Hoja hii inatokana na ukweli kwamba huwezi kufanya marekebisho ya sheria ya umeme bila kuathiri shirika lenye dhamana ya umeme hapa nchini na ufanisi wake.
 4. Sheria kuanisha bei za umeme zinazopitishwa na EWURA kuzingatia gharama halisi zinazotumiwa na TANESCO kuzalisha umeme au kununua toka kwa makampuni binafsi ya uzalishaji umeme kuliko hali ilivyo kwa sasa kwa kuwa shirika linaonekana kuendeshwa kwa kuficha ukweli kuliko uhalisia ambao hauwekwi wazi.
 • Kwa kuwa miongoni mwa majukumu ya shirika hili ni pamoja na kufua na kuimarisha mitambo ya umeme ya shirika, kununua kutoka kwa wazalishaji binafsi na nchi za jirani, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuhakikisha manunuzi ya umeme toka kwenye makampuni binafsi ya uzalishaji umeme yanafanyika kwa uwazi na ushindani kama inavyotakiwa na sheria ya manunuzi ili kuiweesha TANESCO kununua umeme kwa bei nafuu.
 1. Ili kuhakikisha shirika linatimiza jukumu lake la kuwekeza kwenye miradi mipya ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji na kufanya tafiti za vyanzo mbalimbali vya nishati ya umeme kama vile nguvu za maji (hydropower), gesi asilia, makaa ya mawe (coal), jua na upepo; Serikali iliwezeshe shirika la umeme nchini (TANESCO) ili iweze kuwekeza kwenye uzalishaji umeme wa bei nafuu hivyo kusaidia kuepukana na utaratibu wa kununua toka vyanzo vya gharama kubwa.

        Sheria ya Mbolea, Sura ya 378

 1. Mheshimiwa Spika, Mapendekezo yanayopendekezwa katika mswaada huu ni pamoja na Kifungu cha 4, kinachorekebishwa ili kupanua wigo wa majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania na kuainisha mfumo bora wa uingizaji mbolea nchini na usafirishaji mbolea nje ya nchi. Lengo la marekebisho haya ni kuboresha usimamizi na udhibiti wa mbolea inayoingizwa nchini au kusafirishwa nje ya nchi.
 2. Mheshimiwa spika, pamoja na maboresho yanayolenga udhibiti wa mbolea inayoingizwa na kusafirishwa nje ya nchi, ni rai yetu kwamba, sheria ya Mbolea ingeboreshwa zaidi ili kuwawezesha wazalishaji na waingizaji wa Mbolea hapa nchini kupata msamaha wa kodi ili mbolea ipatikane kwa urahisi.
 3. Mheshimiwa Spika, kwa mfano Kifungu cha 40 kinarekebishwa ili kuongeza katika orodha ya makosa vitendo vya kuuza mbolea kwa bei ya juu kuliko bei elekezi na kuuza mbolea katika mifuko ya wazi au kinyume na matakwa ya Sheria hiyo. Pamoja na dhamira hiyo ya kuhakikisha kila mtu anazingatia bei elekezi na mbolea kuuzwa kwa kuzingatia sheria na hivyo kumlinda mteja. Kifungu hicho pia kinarekebishwa ili kuhuisha adhabu kwa makosa mbalimbali chini ya Sheria. Ni ushauri wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba, Serikali ihakikishe inafanya maboresho ya sheria katika mapana yake ili kuhaikikisha wakulima wanapata ruzuku ya mbolea na kuchochea uzalishaji kwa kuwa Tanzania hii inawakulima wengi kuliko kundi linguine lolote.
 4. Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 40A kinacholekebishwa ili kuweka masharti ya kuwasilisha taarifa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka pale ambapo Mamlaka itafililisha makosa chini ya Sheria hiyo, hata hivyo kifungu hiki hakisemi lengo la taarifa hiyo na ikiwa sasa chini ya sheria hiyo Mkurugenzi wa Mashitaka anageuka na kuwa mamlaka ya kupokea taarifa na au anapaswa kupata taarifa kwa maana ya kuchukua hatua.
 5. C. HITIMISHO
 6. Mheshimiwa Spika, kwa kuhitimisha ni kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa rai kwa waheshimiwa wabunge na Bunge hili tuangalie kwa tafakuri pana marekebisho ya sheria zinazoletwa na Serikali ili kupata ridhaa ya kuwa sheria.
 7. Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba mambo mengi ambayo yanakuwa na hila mara nyingi yamekuwa yanaletwa kupitia miswada hii ya marekebisho ya sheria mbalimbali, kwani kwa njia hizi ni uhakika kwamba kamati za kisekta kwa baadhi ya sheria zinazokuwa zinafanyiwa marekebisho hazipatiwi nafasi kujadili kwa kina marekebisho husika, jambo hilo linafifisha tafakuri ya kina kuhusu marekebisho yanayokuwa yanaletwa na wizara au sekta husika.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo naomba kuwasilisha!

 

…………………………………………

Salome Wycliffe Makamba (mb)

MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI

KATIKA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

18 Mei, 2020

Share Button