HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, MHESHIMIWA CECILIA DANIEL PARESSO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU BAJETI YA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO KWA MWAKA WA FEDHA WA 2020/2021

 

(Yanatolewa chini ya Kanuni za Bunge, Kanuni ya 99(9), toleo la mwaka 2016)

 

 

 

 1. UTANGULIZI

 

 1. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema wake na kwa kunipa afya njema ya kusimama mbele ya Bunge lako.
 2. Mheshimiwa Spika, pia nichukue fursa hii kumshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mhe.Freeman Aikael Mbowe kwa kuniamini na kuniteua tena kuwa Waziri Kivuli na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni chini ya Wizara hii. Vilevile nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Hawa Mwaifunga kwa kuaminiwa na kuwa Naibu Waziri Kivuli chini ya Wizara hii. Mheshimiwa Hawa ni mchapazi na asiyeyumbishwa kwa pamoja tutaendelea kuwasemea na kusimamia maslahi ya Watanzania wote. Aidha, nitoe pongezi kwa Waheshimiwa wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni walioteuliwa kuwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri vivuli na wasemaji wakuu katika Wizara mbalimbali na niwatakie kazi njema ya kuwatumikia Watanzania.
 3. Mheshimiwa Spika, nitoe pole kwa viongozi wa Vyama vya Upinzani na wanachama wote waliopatwa na madhila mbalimbali wakiwa wanatimiza wajibu wao wa kupigania haki na demokrasia ya kweli. Kila nikitazama mateso tunayopitia kama Upinzani naona tumaini kubwa la demokrasia ya kweli, uhuru wa kweli na Tanzania mpya yenye umoja, amani na mshikamano usiokuwa na shaka.
 4. Mheshimiwa Spika, pia nitoe pole kwa Watanzania wote kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona (Covid-19)ambao umeleta hofu kubwa hapa nchini na duniani kote na hivyo kusababisha kila mmoja kuangalia namna ya kubadili mfumo wake wa maisha aliozoea ili kuepuka maambukizi,nichukue fursa hii kuendelea kuwakumbusha watanzania wote kufuata ushauri wa watalaamu wa afya ili kupunguza maambukizi. Kambi Rasmi ya Upinzani iko pamoja na Watanzania wote katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu wa Covid-19 na itaendelea kuwasemea na kuishauri Serikali. Afya ya Watanzania ni kipaumbele cha kipekee na kamwe haiwezi kulinganishwa na chochote.
 5. Mheshimiwa Spika, mwisho ila sio kwa umuhimu nitoe shukrani za dhati kwa chama changu Chadema na viongozi wote kwa kunipa fursa ya kukitumikia kwa miaka mitano kama Mbunge. Pia, niwashukuru wananchi wote wa Kanda ya Kaskazini hususani Karatu kwa kufanya kazi na mimi nikiwa mmoja wa Wabunge wa Viti maalum Mkoa wa Arusha, na zaidi niishukuru familia yangu, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuwa pamoja nami katika kipindi chote cha utumishi wangu. Nasema asante nisana na Mwenyezi Mungu awabariki.
 6. MLIPUKO UGONJWA WA HOMA YA MAPAFU CORONA(COVID19)
 7. Mheshimiwa Spika, Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo tarehe 11 March iliitangazia Dunia kuwa ugonjwa wa CORONA(COVID 19)kuwa ni Janga la Dunia (Pandemic). Shirika hilo limetoa na linaendelea kutoa miongozi mbalimbali ya namna bora ya kukabiliana na janga hili. Mlipuko wa ugonjwa huu mpaka sasa umesababisha vifo vya watu 187,705 na waliopata maambukizi mpaka sasa ni watu 2,719,897 duniani kote na hii ni kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani iliyotolewa tarehe 25 April 2020. Kwa tawimu hizi ni dhahiri kuwa ugonjwa huu unakatisha maisha ya watu wengi na wengine wengi kupata maambukizi, hii inatokana na namna ugonjwa wenyewe unavyoambukizi. Taarifa mbalimbali za kitaalamu zinaeleza kuwa ugonjwa huu unaweza kudumu kwa mda mrefu zaidi kama hatua thabiti hazitachukuliwa za kuthibiti maambukizi mapya.
 1. Mheshimiwa Spika, Shirika la Afya Duniani (WHO) ilizitaka nchi zote zitoe taarifa kwa haraka na kwa usahihi mara tu ugonjwa unapoingia katika nchi husika ili kutoa tahadhari kwa umma na kuepusha maafa makubwa. WHO ilieleza kwa undani madhara ya kuficha takwimu na uchelewaji wa uchukuaji wa hatua za haraka dhidi ya Covid-19[i]. Tumeshuhudia nchi ambazo zilipuuzia utoaji wa taarifa kwa umma na kuchelewa kuchukua tahadhari zinajuta.

 

HALI YA MAAMBUKIZI HAPA NCHINI

 1. Mheshimiwa Spika, Tarehe 16 March 2020 mgonjwa wa kwanza alitangazwa hapa nchini kuwa na maambukizi ya Corona na mgonjwa huyu alitoka nje ya nchi, hata hivyo hadi kufikia sasa idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona inazidi kuongezeka kwa kuwa maambukizi ya sasa ni ya ndani ya nchi. Katika hatua za awali kabisa, Kambi Rasmi ya Upinzani tulishauri mambo ya haraka ya kufanyiwa kazi na Serikali ili kuthibiti maambukizi kutokuenea kwa kasi ;
  1. Tulishauri mipaka yote ya nchi ifungwe ili kutoruhusu wageni kuingia nchini kwakuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kama wote wanaoingia nchini walikuwa na maambukizi ama hawana,
  2. Tuliitaka Serikali kuweka wazi mipango yake ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kiasi gani cha bajeti kimepangwa kukabiliana na ugonjwa huu,
  3. Tuliishauri serikali kuhakikisha wataalamu wetu wa afya wanapatiwa vifaa vyote muhimu vya kujikinga ili wasipate maambukizi kwa kuwa wao wapo mstari wa mbele katika mapambano haya.
  4. Tuliishauri Serikali iwe na mkakati wa dharura na wa muda mrefu wa kukabiliana na athari za kiuchumi na za kibiashara zitakazotokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona.
  5. Tulishauri Serikali kufunga jiji la Dar es Salaam kutokuwa na mwingiliano na mikoa mengine angalau kwa siku kati ya 14-21 ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi katika mikoa mengine kwakuwa jiji hilo limeonyesha kuwa na maambukizi mengi zaidi.
  6. Tuliitaka Serikali kupiga marufuku mikusanyiko yote isiyokuwa ya lazima katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba za ibada, kwenye baa,kumbi za disco n.k

Kambi Rasmi ya Upinzani imetoa ushauri mwingi kwa Serikali kupitia taarifa yake kwa Vyombo vya Habari nchini iliyotolewa tarehe 20/03/2020, 13/04/2020 na tarehe 19/04/2020. (Tazama Viambatanisho)

 

 1. Mheshimiwa Spika, Ni kwa masikitiko makubwa sana mambo mengi ambayo yameshauriwa na Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na wadau mbalimbali Serikali imeshindwa kuyafanyia kazi kwa haraka na kwa wakati kiasi cha kupelekea maambukizi na vifo kuwa vingi. Aidha, wananchi wengi kuwa na taharuki huku wakikosa matumaini ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huu.
 2. Mheshimiwa Spika, Tumeshuhudia nchi mbalimbali barani Afrika wakipambana na janga hili kwa kutumia nguvu na rasilimali za kutosha kulinda uhai wa wananchi wao bila kujali athari za kiuchumi ambazo zitaikumba nchi husika. Naomba kunukuu kauli ya Rais wa Ghana alipotoa wito kwa viongozi wa Afrika   dhidi ya janga hili alisema, “We know how to bring the economy back to life, what we do not know is how to bring  people back to life”mwisho wa kunukuu kwa tafsiri isiyo rasmi “Tunajua namna ya kuufufua uchumi na kurejesha katika hali yake ya kawaida,tusichokijua ni namna ya kurejesha ustawi wa watu kwenye maisha”. Kwa kauli hii ni dhahiri kuwa kuna nchi ambazo hazijali anguko la kiuchumi katika nyakati hizi bali uhai wa watu wao kwanza.
 3. Mheshimiwa Spika, Serikali yoyote makini katika nyakati hizi za majanga kama haya kipaumbele cha kwanza ni uhai na afya ya wananchi wake na si vinginevyo. Bila afya hakuna uchumi. Ni vema Serikali na Viongozi wake wakatambua kuwa uchumi ukianguka unaweza kufufuliwa na si uhai wa watu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaendelea kusisitiza na kuitaka Serikali kuwekeza nguvu zake zote katika mapambano dhidi ya janga la Corona ili kuokoa uhai wa wananchi wake ili kuzuia maambukizi
 4. Mheshimiwa Spika, Tunaitaka Serikali kuendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa umma wa watanzania bila kificho kwani janga hili la mlipuko wa Corona sio ilani wala sera ya chama chochote cha siasa kwa hiyo uwepo wake sio udhaifu wa ilani bali ni janga la dunia ambalo mikakati ya kulikabili ifanyike kwa uwazi na kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
 5. Mheshimiwa Spika, Aidha, utoaji wa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa maambukizi ya Corona unatiliwa shaka sana, watanzania wengi tunaendelea kujiuliza usahihi wa taarifa hizo na kama kuna uwazi wa kutosha juu ya idadi halisi ya watu walioambukizwa na idadi ya vifo. Serikali haipaswi kuficha chochote ni vema ikatambua kuwa taarifa za vifo na idadi ya watu walioambukizwa zinapatikana kupitia familia na ndugu wa wahusika, hata hivyo kupitia mitandao ya kijamii tunaona na kusoma ujumbe mfupi wa maandishi za familia mbalimbali zikieleza kuhusu wapendwa wao kupata maambukizi na au kupoteza maisha, ukiweka mzania wa mlinganisho wa taarifa hizo na taarifa ya Serikali ni dhahiri kuwa kuna tatizo mahali ya kuficha takwimu halisi za watu waliopata maambukizi na waliofariki. Jambo la kusikitiza zaidi waliofariki wanazikwa usiku kwa usiku huku kukiwa na timu maalum zilizoandaliwa na magari ya kutosha, tunajiuliza nguvu hiyo inayotumika kwanini isingetumika kuokoa maisha ya wagonjwa hao?. Ni vema viongozi mkakumbuka kuficha au kufanya siri jambo linalogusa uhai wa watu ni jambo la hatari sana na linapaswa kupingwa kwa nguvu zote.
  1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inajiuliza ni kwanini Serikali inaficha ukweli wa tatizo hili! Kwanini mnaficha idadi ya vifo na maambukizi yanayotokana na Corona? Ni kwa faida ya nani! Na kwa bahati mbaya zaidi gonjwa hili halichagui wala kubagua linaweza kumpata yeyote bila kujali cheo chake.
  2. Mheshimiwa Spika, Tunachukua fursa hii tena kuishauri Serikali kutoa taarifa sahihi na kwa uwazi kwani kwa kufanya hivyo kutatoa picha halisi na kuwafanya wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zaidi. Hatuna budi kuwaambia watanzania ukweli juu ya janga hili ili kuokoa maisha yao.
  3. Mheshimiwa Spika, kumekuwa na malalamiko ya wananchi wanapokuwa na wagonjwa kukataliwa kupokelewa katika hospitali mbalimbali katika jiji la Dar es Salaam hivyo kupelekea wagonjwa kufariki wakiwa katika mahangaiko ya kutafuta hospitali ambazo watapokelewa  ili kupata huduma licha ya Serikali kuainisha hospitali ambazo watu wenye dalili za Corona wanapaswa kufika kwa ajili ya huduma za matibabu. Sambamba na hilo tumeona kupitia mitandao ya kijamii watu wakianguka na kufariki na kubaki hapo mda mrefu bila kuchukuliwa na mamlaka husika. Ni dhahiri katika mazingira kama hayo Serikali haikujiandaa kukabiliana na janga hili licha ya kufahamu uwepo wa mlipuko wa ugonjwa na bila hata kufuata ushauri na miongozo mbalimbali  iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani kwa nchi za Afrika kuwa zijiandae na janga hili ili kupunguza maafa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, Kuna mkanganyiko wa taarifa zinazotolewa na viongozi mbalimbali za namna bora ya kujilinda na kuchukua hatua  awali za  kujitibu kwa wenye kuonyesha dalili za awali, taarifa hizo zimekuwa zinakinzana na tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya. Kupitia vyombo vya habari tulimsikia Mhe Rais akiwataka watanzania kujifukiza kwa njia ya mvuke kwani kwa kufanya hivyo virusi vya Corona vitakufa, sambamba na hilo wataalamu wa afya wanaeleza madhara ya kujifukiza kunakoweza kusababisha wananchi kupata matatizo mengine ya kiafya ikiwemo kuunguza mfumo wa hewa, kupata upofu kunakotokana na kuchanganya aina mbalimbali ya majani ya miti, na kupelekea uwezekano wa mapafu kujaa maji. Ni dhahiri kuwa jambo hili linaleta mkanganyiko mkubwa miongoni mwa wananchi kwa kutokujua kujifukiza ni njia sahihi au si sahihi. Tunashauri wataalamu watoe ufafanuzi katika sintofahamu hii na/au kuelekeza namna bora ya kufanya jambo hili endapo linakubalika.
 2. Mheshimiwa Spika, Ni wakati muafaka sasa katika nyakati hizi ngumu wataalamu wa afya kupewa nafasi ya kutoa ufafanuzi, miongozo na maelekezo mbalimbali ya kitaaluma ili kutoleta mkanganyiko kwa jamii na sisi wanasiasa tusitoe kauli za kuchanganya wananchi na kuleta taharuki ambayo inaweza kugharimu uhai wa watu.
 3. Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri sasa yale tuliyokuwa tunashuhudia katika nchi mbalimbali duniani ya idadi kubwa ya vifo vya watu kutokana na janga si geni tena hapa nchini. Watu wanakufa, Familia zinaangamia, Ndugu hawazikani tena, Marafiki wanapotea, Taifa linaangamia. Hali ni mbaya. Hali ni mbaya. Mbaya sana. Ni wakati sasa wa Serikali kutambua umuhimu wa kulinda uhai wa wananchi wake.

 

          WATAALAMU WA AFYA NA MAPAMBANO YA CORONA

 1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni inawapongeza wataalamu wote wa Sekta ya Afya hapa nchini walio mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Corona, kwa hakika wamebeba jukumu kubwa la kupambania uhai wa watanzania. Tunawapa pole wote waliopata maambukizi, tunafahamu wapo wengi wamepata maambukizi na kwasasa wanapigania afya zao. Mungu awajalie afya njema na hatimaye mrejee katika majukumu yenu.
 2. Mheshimiwa Spika, Wataalamu hawa wanatekeleza jukumu hili la kuokoa uhai katika mazingira hatarishi kwani hawana vifaa muhimu vya kujikinga ili wasipate maambukizi yaani PPE. Aidha, wataalamu hawa hawajapewa miongozi ya namna bora ya kujilinda ili kukabiliana na janga hili si tu katika vituo vya afya vya Serikali lakini hata katika vituo binafsi. Sambamba na hilo, Serikali inawajibika kuwaandalia mazingira rafiki wataalamu wote kwa kuwapatia posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (risk allowance), pia kuwapatia makazi maalum ya kukaa watakapomaliza majukumu yao ya kila siku ili kulinda familia zao na jamii inayowazunguka kutopata maambukizi endapo wao wakibainika kuwaambukiza.
 3. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa za baadhi ya madaktari na manesi waliopatwa na maambukizi wakiwa wanatekeleza majukumu yao, aidha watalaamu hawa wametengwa katika maeneo maalumu (isolation areas). Serikali inapaswa kuwahudumia wataalamu hawa kwa kuwapatia huduma zote muhimu na za msingi katika kipindi chote wanachopatiwa matibabu na kuhakikisha familia zao zinatunzwa.

 

       UPIMAJI WA VIRUSI VYA CORONA KWA WATANZANIA WOTE.

 1. Mheshimiwa Spika, Zoezi la Upimaji wa wagonjwa wanaodhaniwa kuwa na maambukizi si wa kuridhisha. Kupitia taarifa zetu kwa vyombo vya habari nchini tuliitaka Serikali iweke wazi idadi ya watu waliopimwa toka kuanza kwa janga hili lakini mpaka leo hakuna uwazi wa kuonyesha idadi halisi ya waliopimwa. Sambamba na hili Serikali inatumia maabara moja tu iliyopo Dar es salaam jambo ambalo linaweza lisiwe na ufanisi na kutoleta majibu ya haraka ukilinganisha ukubwa wa nchi yetu.
 2. Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri sasa maambukizi ya ugonjwa wa Corona umesambaa nchi nzima na kwa mujibu wa wataalamu wa afya na tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa wapo watu ambao wanaweza kuwa na virusi lakini wasionyeshe dalili yeyote. Ni wakati sasa serikali ifanye upimaji wa watanzania wote kwa lazima ili kudhibiti maambukizi zaidi. Jambo hili linahitaji maamuzi ya haraka. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kufanya yafuatayo; kuhakikisha tunakuwa na maabara za kutosha zenye uwezo ikiwemo mobile clinic kulingana na jiografia ya nchi yetu, kuhakikisha tuna vitendanishi vya kutosha, kuwa na wataalamu wa afya wa kutosha na kutenga fedha maalum kwa zoezi hili. Aidha, fedha zilizotolewa na wahisani mbalimbali zielekezwe kununua mahitaji yote muhimu ya kusaidia mapambano dhidi ya Corona ikiwemo mashine za kusaidia kupumua. Ni imani yetu Serikali italichukua jambo hili kwa uzito unaostahili.
 3. Mheshimiwa Spika, hakuna shaka yeyote kuwa kupitia janga hili Serikali itakuwa imejifunza na kuona umuhimu wa Sekta ya Afya kwakuwa maisha ya watu ni muhimu kuliko jambo lolote lile. Serikali inapaswa kuwekeza vya kutosha katika Sekta hii kwa kuwa na miundombinu ya kutosha na yenye kukidhi vigezo na mahitaji yote muhimu katika hospitali zetu zote kuanzia vituo vya afya mpaka hospitali za rufaa.
 4. Mheshimiwa Spika, Tunatambua kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wa kada ya afya, vyuo vyetu (binafsi na vya serikali) zinatoa wahitimu wengi na wenye sifa lakini wengi hukimbilia katika sekta binafsi na/au kujiajiri kwakuwa mishahara na marupurupu yanayotolewa Serikalini haitoshelezi ukilinganisha gharama za maisha kupanda mara kwa mara.
 5. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutazama upya mfumo wa ajira na maslahi yote muhimu ya watumishi wa kada ya afya na kwa hakika tunaweza kuwapa stahiki kama ambavyo tunapata sisi wanasisasa, swala ni kufanya maamuzi tu.Aidha,upatikanaji wa vifaa vyote muhimu vya kujikinga kwa watumishi hawa ni jambo muhimu sana katika nyakati zote bila kujali kama ni nyakati za milipuko ya magonjwa au laah. Hata hivyo, ni wakati ambao kama nchi tunapaswa kutotegemea fedha za wafadhili kusaidia sekta ya afya.

 

 1. TATHIMINI YA UTENDAJI WA WIZARA NA UCHAMBUZI WA BAJETI 2016-2020
 2. Mheshimiwa Spika, tangu kuanza kwa Bunge la 11 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tumeendelea kuishauri Serikali namna bora ya kuboresha huduma za afya na ustawi wa Jamii.Pamoja na wingi wa hoja yapo mambo mahususi ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani iliizungumzia kwa mapana kama ifuatavyo;
 • Bajeti ya kila mwaka ya Wizara
 • Bima za Afya kwa Watanzania
 • Hali zahospitali za Rufaa na Mikoa
 • Uhaba wa wataalamu wa afya
 • Maslahi ya wataalamu wa afya
 • Upatikanaji wa vifaa tiba na vitendanishi
 • Masuala yanayohusu magonjwa ya akili
 • Lishe
 • Ndoa na mimba za utotoni
 • Haki za watoto
 • Mafao ya uzee
 • Matatizo yanayotokana na magonjwa ya tabia
 • Tatizo la VVU na Ukimwi
 • Taasisi na vyuo chini ya Wizara ya Afya
 • Hali za afya magerezani
 • Milipuko ya magonjwa
 • Changamoto zinazowakabili kina mama wajawazito na watoto
 • Uwekezaji katika sekta ya Afya na changamoto nyingine nyingi zinazoikabili Wizara.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikisisitiza na kushauri hata hivyo hadi sasa bado changamoto za sekta ya Afya ni nyingi, milipuko ya magonjwa ni mikubwa, hali za afya magerezani haziridhishi, wakina mama wajawazito na watoto wadogo bado wanakabiliwa na changamoto kubwa, huku hali za hospitali za rufaa na maslahi ya watumishi wa kada ya Afya zikiwa mbaya kuliko kipindi kingine chochote kwa kushindwa kupandishwa vyeo na kuboreshewa maslahi yao kwa takribani miaka mitano sasa.

     (i). Bajeti Idara ya afya fungu 52

 1. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa mdau namba moja wa kusimamia masuala ya afya za Watanzania kwani tunaamini hakuna maendeleo katika Taifa kama wananchi wetu hawana huduma bora za afya. Hivyo, Chadema kikiwa Chama kikuu cha Upinzani Bungeni kimeamua kuja na sera mahususi ya afya inayogusa na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya nchini ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo mzuri wa kibajeti wa afya, baada ya sera iliyopo sasa kushindwa kuwahudumia watanzania.
 1. Mheshimiwa Spika,ukiangalia mtiririko wa utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Afya kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia mwaka wa fedha 2019/2020; takwimu zinaonesha kwamba ufanisi kwa Wizara hii muhimu ni mdogo kutokana na ukosefu wa fedha zinazotengwa kutopatikana kama inavyotarajiwa. Kwa Mfano; Bajeti ya Mwaka wa fedha 2016/2017, wizara ilikuwa imepokea jumla ya shilingi 314,673,230,000.95 (bil 314.673) sawa na asilimia 40 ya bajeti ya Wizara zikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida pamoja na miradi ya maendeleo[ii].
 2. Mheshimiwa Spika,kwa upande wa fedha za ndani zilizotolewa kwa mwaka 2016/17 hali ilikuwa mbaya zaidi kwani katika kipindi kama hicho, Wizara ilikuwa imepokea asilimia 37 tu ya fedha zote zilizotarajiwa wakati fedha za nje zilizopokelewa zilikuwa asilimia 6 tu. Hii ikiwa na maana kwamba Idara hii ilipata fedha pungufu kwa asilimia 60. Fedha za ndani hazikutolewa kwa asilimia 63 na fedha za nje hazikutolewa kwa asilimia 94.
 3. Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2017/2018, Wizara hii iliomba shilingi trilioni 1.07[iii]. Pamoja na kwamba fedha hii hazikuweza kutolewa zote, lakini hata kiasi kidogo kilichotolewa kilitegemea wahisani kwa asilimia 71 huku fedha za ndani zilizotolewa kwa asilimia 19 pekee. Takwimu hizi ni ushahidi kwamba serikali imeshindwa kufikia malengo ya kibajeti angalau kwa asilimia 60 pekee kwa Wizara hii.
 4. Mheshimiwa Spika, Mwaka wa fedha 2018/2019, wizara iliomba kiasi cha shilingi bilioni 866.233. kiwango hicho kilikuwa ni pungufu ya shilingi bilioni 211.468 ya bajeti ya mwaka 2017/2018 au anguko la bajeti ya afya kwa asilimia 20. Hata hivyo, pamoja na bajeti hiyo kuwa pungufu kwa 20% zaidi ya asilimia 60 ya bajeti ilitegemea wahisani katika shughuli za ujenzi wa vituo vya afya, ukarabati wa majengo, ununuzi wa vifaa tiba na dawa. Utaratibu huu ni hatarishi kwa Afya za watanzania kutegemea hisani ya fedha za wafadhili ambazo haziji kwa wakati na hata pale zinapokuja haziji kwa utoshelevu matokeo yake panapotokea dharura ya magonjwa ya mlipuko kama ilivyo Corona au Ebola Watanzania tunapata mtihani mkubwa sana wa kukabiliana na dharura kama hizi kutokana na changamoto za kifedha zinazosababishwa na uchaguzi mbaya wa vipaumbele vya Taifa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, hali si tofauti na miaka iliyopita tangu awamu ya tano kuingia madarakani kwani, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Wizara iliomba kuidhinishiwa jumla shilingi bilioni 990.68 lakini hadi kufikia Mwezi Machi, 2020 Wizara ilikuwa imepokea jumla shilingi bilioni 343.5 pekee hii ikiwa ni pungufu ya zaidi ya shilingi bilioni 647. Upande wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wizara iliomba kiasi cha shilingi bil 544 lakini hadi kufikia Machi 2020 wizara ilipokea shilingi mil 83.1 tu sawa na asilimia 15.3 pekee ya fedha zote za miradi ya maendeleo; Kwa utaratibu huu, ni lini Tanzania tutamua kuwekeza nguvu zetu kwenye Afya ya wananchi wetu kama kipaumbele

Jedwali kuonyesha fedha zilizoidhinishwa na Bunge na fedha zilizotolewa 2016-2020.

 

Mwaka Fedha zilizoidhinishwa Fedha zilizotolewa
2016/2017 Bilioni 796.115 Bilioni 341.673
2017/2018 Trilioni 1.07 Bilioni 617.5
2018/2019 Bilioni 866.233 Bilioni 304.707
2019/2020 Bilioni 990.68 Bilioni 343.5

 

 (ii) Idara ya ustawi wa jamii fungu 53

 1. Mheshimiwa Spika,Idara ya Ustawi wa Jamii pamoja na mambo mengine inalenga kuzuia, kupunguza, na kutatua changamoto za tiba zinazoikabili jamii. Pamoja na jukumu hili kubwa, idara hii inatengewa fedha kidogo sana bila ya kujali umuhimu wake. Idara inahusika moja kwa moja na masuala muhimu ya ustawi wa jamii ya Watanzania katika nyanja za uchumi, kijamii na kiutamaduni. Hata hivyo, fedha inayotolewa ni fedheha kubwa kwa watumishi ambao ni watekelezaji wa miradi ya Idara.
 2. Mheshimiwa Spika, mishahara ya watumishi ndani ya idara hii ni midogo, hawapewi heshima na hadhi wanayostahili kama ilivyo watumishi wengine ndani ya sekta ya afya. Pamoja na ukubwa wa majukumu yao katika jamii bado idadi yao ni ndogo sana ukilinganisha na uhitaji wa wataalamu hawa katika jamii yetu yenye watu takribani milioni 56 na hii inatokana na Serikali ya awamu ya Tano kushindwa kuajiri watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo watumishi wa Idara ya ustawi wa jamii kwa takribani miaka minne sasa. Hata vyuo vinavyozalisha wataalamu hawa vinakabiliwa na changamoto nyingi za kifedha na uchakavu wa miundombinu.
 3. Mheshimiwa Spika, chini ya fungu 53, kwa mwaka wa fedha 2016/17 Idara hii iliidhinishiwa kiasi cha shilingi billion 49.9 kati ya fedha hizo billion 41 zikiwa ni matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 8.8 zikiwa ni fedha za maendeleo. Mpaka Mwezi Machi 2017, Idara ilipokea kiasi cha shilingi million 497.718 kwenye miradi ya maendeleo sawa na asilimia 5.62ya fedha za maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge. Hii maana yake ni kwamba, Serikali ilishindwa kutekeleza Bajeti ya maendeleo katika fungu hili mwaka wa fedha 2016/17 kwa asilimia 95.
 1. Mheshimiwa Spika, Mwaka wa fedha 2019/2020 Bunge lako tukufu liliidhinisha shilingi bil 31.537.kwa ajili ya Idara ya maendeleo ya jamii. Kati ya fedha hizo fedha za matumizi ya kawaida inayohusisha mishahara ya watumishi na matumizi mengineyo zilikuwa shilingi bilioni 28.777 na fedha za miradi ya maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge  zilikuwa shilingi bilioni 2.760 pekee.
 2. Mheshimiwa Spika, hata hivyo mpaka kufikia mwezi Februari 2020 fedha zilizotolewa kwenye matumizi ya kawaida ni shilingi bilioni 19.981 na fedha za maendeleo ni shilingi bilioni 1.644. Fedha hizi zote zilikuwa ni fedha za nje na hakukuwa na fedha zozote za ndani zilizotolewa.
 3. Mheshimiwa Spika, Idara hii inasimamia vyuo takribani 08, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) vituo vya watoto wenye mahitaji maalum, vituo vya wazee n.k na shughuli nyingi chini ya idara hii kutengewa fedha ndogo kiasi hiki ni kuisababishia Idara ishindwe kutekeleza majukumu yake na madhara yake yanaonekana katika jamii ya watanzania kwa kushindwa kustawi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuongeza Bajeti ya Idara hii ili kuwekeza katika ustawi wa watanzania ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa hili, kuliko hali iliyopo sasa.

 

 1. Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba serikali imekuwa na bajeti kubwa ambazo haitekelezeki ikiwa ni pamoja na kushuka kwa makusanyo kwenye sekta mbalimbali, Kambi Rasmi ya Upinzani imebaini yafuatayo katika muelekeo wa kibajeti kwa kipindi cha miaka minne iliyopita na kutoa mapendekezo ili kuboresha bajeti zijazo kama ifuatavyo.
 • Kuanzia Mwaka 2016/17-2019/20 Bajeti ya Wizara ya Afya imekuwa ilitegemea zaidi wahisani kwa zaidi ya 50%. Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya Tano inayojinasibu kutengeneza uchumi wa kati kwa kujenga viwanda  Wizara inapaswa kushirikiana na sekta ya viwanda kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya afya ili kuongeza mapato ya ndani.
 • Serikali haijawahi kutekeleza bajeti inayoombwa na wizara kwa utoshelevu wake kwa kuzingatia unyeti wa Wizara hii. Kutopatikana kwa bajeti iliyopitishwa ni ushahidi dhahiri wa madai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba, Bajeti ya Serikali inayowasilishwa ndani ya Bunge hili tukufu haina uhalisia wowote ilihali tarakimu za kibajeti kuonesha viwango vikubwa vya fedha wakati uwezo wa serikali kukusanya fedha na kuitekeleza Bajeti husika ukiwa ni mdogo. Madhara ya makisio makubwa yasiyo na uhalisia ni kuwa yanaleta matumaini ya uongo. Ni vyema sasa Wizara na serikali kwa ujumla ikaja na makisio yanayoakisi hali halisi ya kifedha ya serikali.
 • Kwa hali ya mwelekeo wa kibajeti ni wazi kuwa hali katika sekta ya afya ni mbaya hasa ukilinganisha ukuaji wa idadi ya watu na bajeti inayotolewa kila Mwaka. Hii ikiwa na maana kwamba nguvu kazi kubwa ya taifa hili iko hatarini mno kutokana na serikali kutokufanya afya za wananchi kuwa kipaumbele.
 • Serikali imeshidwa kufungamanisha sekta ya viwanda na sekta afya na hii ndio sababu bado bajeti inategemea wahisani kwa kiasi kikubwa. Kukosekana kwa mikakati madhubuti ya uwekezaji ndani ya sekta ya afya, sera zisizotabirika za uwekezaji, kodi kubwa na mazingira magumu ya uwekezaji yanawafanya wafanyabiasha wengi kushindwa kuwekeza kwenye sekta ya afya. Mpaka sasa Kenya ni moja ya nchi inayofanya vizuri sana katika uzalishaji wa dawa baridi (Pharmacetical manufacturers). Katika makampuni makubwa ya madawa ndani ya nchi za COMESA, makampuni 32 yanatoka Kenya. Mpaka mwaka 2014 yaani miaka 6 iliyopita soko la madawa pekee lilichangia takriban dola za Marekani 558.5 milioni katika uchumi wa Kenya. Katika bidhaa za kuongeza thamani iliingiza takribani dola za Marekani milioni 60.
 1. Mheshimiwa Spika,bado Tanzania inatumia fedha nyingi kununua madawa nakusafirisha kutoka nchi mbalimbali hasa nchi za Asia. Serikali ilitangaza kufungua milango kwa wawekezaji kwenye sekta ya afya hususani katika viwanda vya kutengeneza madawa lakini mpaka sasa hakuna taarifa ya wazi ya idadi kamili ya viwanda, vinazalisha dawa kiwango gani na vinachangia kiasi gani katika uchumi wa nchi.
 2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kujifunza vyema kupitia nchi majirani au hata nchi za COMESA zinazofanya vizurikwa lengo la kuboresha sekta ya Afya hapa nchini.
 3. Mheshimiwa Spika,ni imani yetu kuwa, kwa kuwa Mwaka wa fedha ujao Serikali itakayokuwa Madarakani itakuwa Chini ya Chadema, tutahakikisha tunaangalia upya muelekeo wa bajeti ya sekta ya afya na iweze kutoa kipaumbele kwa sekta hii kwa kuwa afya ndio msingi wa maendeleo ya taifa lolote duniani. Afya ndio msingi wa maendeleo yetu. Mahatma Gandhi Baba wa Taifa la India aliwahi kusema”It is health that is real wealth and not pieces of gold and silver”.

 

 1. RASILIMALI WATU – SEKTA YA AFYA
 2. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya ni moja ya Wizara yenye upungufu mkubwa wa watumishi. Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda zinahudumia wagonjwa maelfu na hazina idadi ya watumishi inayoendana na ongezeko la watu. Mfano, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kwenye hotuba ya Waziri, serikali imejisifu kuwa katika hospitali za Rufaa za Mikoa zilihudumia wagonjwa 3,292,103 (mil 3.2) wakati ikijua Idadi ya watoa huduma ni ndogo sana. Tatizo kubwa ni kuwa Serikali ya imekuwa ikijivunia idadi ya wagonjwa waliotibiwa quantity (wingi) badala ya ubora(quality) wa huduma inayotolewa.
 3. Mheshimiwa Spika, Mwaka wa fedha 2016/17 katika utekelezaji wa bajeti, Wizara ilikuwa na upungufu wa watumishi kwa asilimia 49. Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 pamoja na kuwa serikali haikutoa tathimini ya uhitaji wa jumla wa watumishi katika sekta hii katika kitabu cha randama fungu 52 kinaonyesha kuwa ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala bora ilitoa nafasi za ajira 3,152 tu. Ikiwa ni ajira za madaktari bingwa 24, madaktari wasaidizi 45, wauguzi daraja wa pili 137 (nurses) na nafasi 2 za madaktari washauri 2 (Medical Consultant na wengine ni kada mbalimbali ndani ya sekta ya afya.
 1. Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba serikali ya awamu ya tano haijatoa ajira kwa muda mrefu. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Wizara iliwasilisha ombi la Ajira mpya 12,775 lakini mpaka sasa serikali haijatangaza imetoa ajira ngapi.Hali hii inaleta wasiwasi mkubwa kwa kuwa bado tatizo la rasilimali watu katika sekta ya afya ni kubwahasa maeneo ya vijijini.
 2. Mheshimiwa Spika, Kuongezeka kwa kasi ya magonjwa na kuibuka kwa magonjwa mapya na ya hatari kama Corona, Dengua na magonjwa ya Homa ya Ini n.k yanaleta sintofahamu kubwa kwa wananchi ambao tegemeo lao kubwa ni upatikanaji wa watalamu wa afya watakaoweza kuwasaidia.
 3. Mheshimiwa Spika, wataalamu wetu wa afya wanafanya kazi kubwa usiku na mchana hasa wakati huu wa ongezeko kubwa la magonjwa na wagonjwa. Pamoja na kuwa serikali imesema imetoa ajira tukumbuke kuwa ni serikali hiyo hiyo ndio inayofanya tafiti za upungufu wa watumishi na ndio hiyo hiyo inayoamua iseme nini kwa umma kuhusiana na ajira au mapungufu ya watumishi jambo ambalo linaathiri uhalisia wa matatizo katika sekta mbalimbali. Jambo hili linatia mashaka katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili serikali.
 4. Mheshimiwa Spika, Tukumbuke kuwa pale ambapo taasisi au watu mbalimbali wanakuwa huru kufanya tafiti ndipo serikali inaweza kujikosoa na kufanya maboresho . Upungufu wa watumishi katika sekta ya afya ni tatizo linalohitaji umakini na weledi mkubwa la kulishugulikia kwani kuna hatari ya kuwepo kwa ongezeko kubwa la vifo vinavyotokana na ukosefu wa tiba kwa wakati.
 1. Mheshimiwa Spika,mwaka 2017 serikali ilikiri uhaba mkubwa wa madaktari. Miaka miwili baadae jambo hilo halizungumzwi tena na Wizara haibebi jambo hilo kama ajenda kuu. Kwa mujibu wa habari za uchambuzi uliofanywa na ‘The citizen Tanzania mwaka 2016’ unaonyesha uwiano wa daktari 1:25,000.kinyume na muongozi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambao ni daktari 1:10,000.
 2. Mheshimiwa Spika, Mpaka Mwaka 2017 Tanzania ilikaririwa kuwa na watu milioni 56. Ikiwa ni moja ya nchi 5 Afrika ambazo idadi ya watu inakuwa kwa kasi. Pamoja na ongezeko hilo kubwa la idadi ya watu, serikali imeshindwa kuzalisha ajira za wataalamu wa afya. Katika vyuo vyetu vya tiba nchini wanaohitimu ni wengi lakini ni wachache sana wanaopata ajira serikalini. Mathalani, katika hospitali kubwa za Rufaa za Kanda mfano, Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) inahudumia wagonjwa kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha,Manyara,Tanga.
 3. Mheshimiwa Spika, Katika hospitali hii wengi wanaohudumu ni wanafunzi. Inapaswa kwa taratibu na sheria za afya wanafunzi hawa kuwa na mwalimu wao wakati wote wanapotoa huduma lakini kutokana na uhitaji kuna wakati inalazimu kufanya kazi wenyewe kutokana na uhaba wa madaktari wazoefu. Hospitali ya Rufaa kanda ya Ziwa inahudumia mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Sinyanga,Kagera, Mara na Kigoma ) Mikoa hii ni mingi, kijiografia ni mikubwa na rufaa zinazofanywa nazo ni nyingi.
 4. Mheshimiwa Spika, pia kwa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya inayobeba mikoa ya Katavi,Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa. Kwa population ya watu maeneo haya ni wengi na rufaa zinazofanywa ni nyingi ukilinganisha na idadi ya watoa huduma za afya.
 1. Mheshimiwa Spika,upatikanaji wa madaktari bingwa hasa wa magonjwa ya wanawake (Obstetric and gynaecology), madaktari wa masikio, pua na koo (ENT), madaktari wa mionzi (radiology) na huduma ya usingizi (anaestthesiology) bado ni wachache sana ukilinganisha na uhitaji.
 2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kupitia wataalamu wake mbalimbali na mabaraza ya madaktari kama Baraza la Madaktari Tanganyika, Baraza la Afya na Mazingira, Baraza la Wauguzi na Kinga na mengine kuja pamoja na kuwa na mjadala wa kitaifa wa namna bora ya kuimarisha sekta ya afya nchini. Mabaraza haya yamekuwa kimya katika kuisemea sekta ya afya ukilinganisha na awamu nyingine za uongozi zilizopita ambapo mabaraza haya yalikuwa active katika kufanya kazi na kuisemea sekta ya afya wakati wote.

 

 1. BOHARI KUU YA DAWA (MSD)
 2. Mheshimiwa Spika, Bohari kuu ya Dawa inajukumu ya kununua, kuhifadhi na kusambaza aina mbalimbali za dawa hapa nchini, vifaa tiba na vitendanishi. Ununuaji wa dawa hufanyika kwa mikataba mbalimbali kati ya MSD na wazalishaji wa dawa na hatimaye kuhifadhiwa katika maghala mbalimbali kote nchini. Aidha, Bohari inajiendesha kupitia mfumo wa fedha wa mzunguko yaani revolving fund kwa ajili ya kufanya manunuzi.
 3. Mheshimiwa Spika, Bohari ya Dawa imekuwa haipati fedha kwa wakati licha ya Bunge lako tukufu kuidhinisha fedha hizo jambo ambalo linaathiri mikataba na wazalishaji wa dawa. Serikali imekuwa na utamaduni wa kuleta maombi ya idhini ya fedha lakini kwenye utekelezaji inakuwa kiini macho jambo ambalo linapunguza ufanisi wa bohari hii na kupelekea uhaba na upungufu wa dawa katika vituo vyetu vya afya hapa nchini.
 4. Mheshimiwa Spika, haya yanadhihirishwa na Ripoti ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali katika ripoti yake ya kufikia June 2019 ikionyesha kuwa Bunge liliidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 260 hadi wakati huo(June 2019) Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 80 tu sawa na asilimia 33 ya bajeti iliyoidhinishwa.
 5. Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali kuacha mzaha na kuwahadaa watanzania katika maswala muhimu kama haya ya dawa kwa watanzania wote kwa kuwa umuhimu wa uwepo wa dawa katika hospitali zetu nchini si jambo la mzaha. Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikijinasibu kwa kujenga vituo vingi va afya hapa nchini, jambo la kujiuliza vituo hivyo vitakuwa na maana gani kama  upatikanaji wa dawa ni wa kusuasua kwa kiwango hiki?
 6. Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, Serikali inadaiwa deni kubwa na Bohari ya Dawa jambo ambalo linapunguza ufanisi wa utendaji wake,kupitia Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali deni limeongezeka kwa asilimia 14 kutoka shilingi bilioni 228.6 mwaka 2017/18 hadi shilingi bilioni 260.45 mwaka 2018/19.
 7. Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri sote tunatambua umuhimu wa bohari hii, ni lazima Serikali kuiwezeshwa pasipo shaka yeyote kwa madeni kulipwa kwa wakati na kupatiwa fedha zote kulingana na mahitaji yao, ni nyakati kama hizi za mlipuko wa magonjwa kama Corona bohari ilipaswa kuwa imara na kusambaza mahitaji yote muhimu kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ikiwemo barakoa na vitakasa mikono.
 8. Mheshimiwa Spika, Serikali lazima itambue umuhimu wa sekta ya afya na kuipa kipaumbele kinachostahili, hatuwezi kujisifia kujenga miradi mikubwa kama reli ya kisasa, stieglers gorge, kujenga barabara za lami na kuelekeza nguvu zote huko na kusahau swala la upatikanaji wa dawa kwa watanzania wote kwa kuiwezesha bohari ya dawa. Miradi mikubwa itakuwa haina maana kama taifa linaugua na hakuna madawa.
 9. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaiitaka Serikali, kulipa madeni yote ya bohari ya dawa na kuipatia fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge hili ili kuwezesha utendaji bora wa chombo hiki muhimu kwa maslahi ya watanzania wote.

 

 1. VIFURUSHI VYA BIMA YA AFYA

 

 1. Mheshimiwa Spika, gharama za matibabu kupitia Bima ya afya nchini zimegeuka mwiba mchungu kwa Watanzania. Mwishoni mwa Mwaka jana (2019) serikali ilitangaza bei mpya ya vifurushi vya bima za afya kupitia mfuko wa Bima ya afya (NHIF). Bei ya vifurushi hivi ni kama mzigo wa gunia la misumari anapobebeshwa mtu kichwani. Ni wazi kuwa bei mpya ya vifurushi vya bima inakwenda kuwagawa Watanzania zaidi katika kundi kubwa la walionacho na wasio nacho.
 2. Mheshimiwa Spika, gharama za vifurushi hivi ziko juu sana na hivyo wananchi wa kawaida hawawezi kuzimudu ukizingatia kuwa zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini wanaishi katika hali ya umaskini wa kutupwa na hawawezi kabisa kumudu gharama za matibabu.
 3. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa bei mpya ya vifurushi vya bima kijana wa kuanzia umri wa miaka 18-35 atalazimika kulipia kiasi cha sh.192,000/= kama kiwango cha chini zaidi kikifuatiwa na kifurushi cha sh. 384,000/= kama kiwango cha kati na sh.516,000/= kama kiwango cha juu. Kuanzia umri wa miaka 36-59 kiwango cha chini kabisa kitaanzia sh. 240,000/= kikifuatiwa na sh.440,000/= ,na kiwango cha juu kikiwa ni sh.612,000/=. Kuanzia umri wa miaka 60 ambao ndio umri wa uzee pale nguvu za mwili zinapokuwa zimekwisha na pia ndio umri ambao binadamu wanashambuliwa na magonjwa mengi zaidi kiasi cha chini kabisa cha bima ya afya kitawagharimu kiasi cha ni sh.360,000/= kikifuatiatiwa na kifurushi cha sh.660,000/= na kiwango cha juu kikiwa sh.984,000/=Bei hizi zote ni kwa ajili ya huduma ya mtu mmoja pekee.
 4. Mheshimiwa Spika, bei hizi ni mara dufu pale ambapo una mwenza au watoto wanaokutegemea. Endapo una watoto wanne wenye umri wa kuanzia miaka 18 mpaka 35 utalazimika kulipia kiasi cha sh. 636,000 mpaka 1,548,000/=.Na endapo ni wenza kuanzia miaka 36-59 watalazimika kulipia kuanzia kiasi cha sh.672,000/- mpaka 1,644,000/ kwa mwaka.
 5. Mheshimiwa Spika, mwezi June 2019, Waziri wa fedha aliwasilisha Bungeni taarifa ya hali ya uchumi wa taifa 2018 na Mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/2020, na alibainisha kuwa pato la kila Mtanzania limefikia shilingi 2.4 milioni mwishoni mwa mwaka 2018. Endapo zaidi ya sh. 600,000 kwa wastani itatumika katika kugharamia huduma za afya pekee je, Mtanzania huyu atawezaje kumudu gharama nyingine za maisha kama kodi mbalimbali, huduma ya chakula, malazi, mavazi, ada mbalimbali n.k?
 6. Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kuwa mpaka sasa yapo magonjwa mengi yanalipiwa nje ya mfumo wa Bima, mfano vipimo kwa ajili ya magonjwa ya saratani,baadhi ya vipimo katika mfumo wa upumuaji, huduma za dawa n.k. Hivyo, ni wazi kuwa Mtanzania ambae hana kipato kikubwa hawezi kabisa kumudu gharama za afya na hii inaongeza idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na kukosa matibabu.
 7. Mheshimiwa Spika,Serikali imefikia hatua mpaka maiti zilizokuwa na deni la matibabu zinalipiwa ndio huduma nyingine zifuate ikiwa ni pamoja na kuhifadhi mwili, au kuruhusu ndugu kuchukua mwili kwa ajili ya maziko. Japokuwa Waziri alishatoa kauli ya kukataza jambo hili bado malalamiko ni mengi kutoka kwa wananchi. Jambo hili linaitia aibu kubwa nchi yetu.
 8. Mheshimiwa Spika, Hii yote ni kutokana na serikali kushindwa kutoa huduma za afya kwa wote bila upendeleo wa kuwagawa wananchi katika makundi hasa wale wenye vipato duni zaidi ambao wanakufa na madeni. Hali ngumu ya kiuchumi iliyopo sasa inahatarisha mamilioni ya Watanzania ambao hawataweza kugharamia gharama za matibabu. Pale mwananchi anapougua anaanza kuwaza madeni kabla hata ya kuwaza ugonjwa au maumivu aliyonayo.
 9. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuanzisha mfumo wa sera ya afya kwa wote kama ilivyokuwa katika sera ya afya ya Chadema ambayo imedhamiria kutoa huduma za bima ya afya kwa wote (universal health insuarance) ili kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata haki ya kupata matibabu kwa unafuu ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya mijini na vijijini.

 

 1. CHAKULA NA LISHE
 1. Mheshimiwa Spika, nchi yetu bado inasumbuliwa na tatizo kubwa la usalama wa lishe (nutrition security). Hata baada ya uhuru tuna maelfu ya watoto wa Kitanzania wanaougua unyafudhi na udumavu (malnutrition and stunt) kutokana na lishe duni. Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Afya 2019/2020 takwimu zinaonyesha mpaka mwaka 2018 asilimia 31.8 ya Watanzania wanaugua udumavu na wanaokonda kutokana na kukosa chakula ni asilimia 3.5.
 2. Mheshimiwa Spika, aidha kumekuwa na ongezeko kubwa la wanawake wenye viribatumbo (manyamauzembe). Asilima 31.7 ya wanawake nchini wamekuwa wakiongezeka uzito mkubwa hususani maeneo ya tumbo kutokana na ulaji usiokuwa na mpangilio. Vilevile, tatizo la upungufu wadamu (haemoglobin) hasa kwa wanawake wenye umri wa kuzaa bado ni kubwa. Asilimia 28.8 ya wanawake wanapatwa tatizo la upungufu wa damu kutokana na hedhi, matatizo ya uzazi, na wakati wa ujauzito.
 1. Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa serikali haijatilia mkazo tatizo la chakula na lishe hapa nchini. Hapa nchini kuna taasisi ya chakula na Lishe (TFNC). Taasisi hii ni kama haipo. Haitengewi fedha, haifanyi kazi kwa kujitangaza kwa umma na kutoa elimu ipasavyo. Mfano, kwa mwaka wa fedha 2017/18 katika randama ya Wizara fungu 52 taasisihii ya chakula na lishe Mradi Na. 5496, haikutengewa fedha yoyote. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2018/19, Mwaka 2019/2020 katika hotuba ya Waziri ameeleza kazi ya mafunzo pekee ambayo imefanywa na wizara hii.
 1. Mheshimiwa Spika, katika magonjwa yanayoua sana Watanzania kwa sasa ni pamoja na magonjwa yanasababishwa na ulaji mbaya wa vyakula na mfumo wa maisha (life style). Watu wengi wanakula vyakula vya makopo (processed food), vyakula visivyo na virutubisho,na vyakula vilivyo na kemikali nyingi. Familia nyingi hazili mlo kamilijambo linalowaathiri zaidi,watoto, wazee na kina mama wajawazito kutonana na ukosefu wa virutubisho vinavyohitajika zaidi kwenye miili yao. Ulaji mwingi wa nyama nyekundu na pombe umewafanya watu wengi kupata viriba tumbo. Matokeo ya ulaji mbaya yanasabisha ongezeko kubwa la magonjwa ya sukari, kiharusi,kansa, gout na kadhalika.
 2. Mheshimiwa Spika, mwaka jana 2017 na 2018, Kambi Rasmi ya Upinzani ilizungumzia kwa kina tatizo kubwa la magonjwa yasiyoambukizwa yanayosabishwa na mfumo wa maisha pamoja na tatizo la udumavu hapa nchini. Tatizo hili lina athari kubwa sana kwa taifa kwani kwa kadiri ongezeko la watoto wenye udumavu nchini linavyofumbiwa macho ndivyo hivyo taifa hili linavyozidi kuzalisha watoto wasio na uwezo wa kujifunza darasani na wasio na uwezo wa ung’amuzi wa mambo (reasoning ability) yaani ‘vilaza au mbumbumbu’.
 1. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa utafiti wa REPOA mwaka 2014 takribani watoto milioni 2.4 nchini walikuwa na tatizo la udumavu. Hali hii inatishasana na inazidi kukua kutokana na ukweli kwamba siku hizi watoto wengi mashuleni hawapati lishe kutokana na serikali kupiga marufuku michango mashuleni na huku ikijua wazi haina uwezo wakugawa vyakula mashuleni. Jambo hili linazidi kuhatarisha zaidi afya za watoto hususani wale wanaotoka katika kaya maskini ambapo watoto walitegemea kula mlo mmoja tu shuleni kwa kuwa familia zao wanashindwa kupata angalau milo miwili kwa siku.
 1. Mheshimiwa Spika, tatizo hili la udumavu lina athari za muda mfupi na zile za muda mrefu. Hata kama mtoto aliathirika na udumavu utotoni athari zake zinaweza kuonekana pale anapokuwa mtu mzima. Tatizo hili huonekana pia sio katika elimu pekee bali pia katika uwezo wa kawaida wa ubunifu na ufikiri wa hali ya juu.
 1. Mheshimiwa Spika, kwa sasa taifa letu lina tatizo kubwa la kuwa na watu wasio na uwezo wa kung’amua mambo (udumavu wa akili). Tunashuhudia kundi kubwa la watu wanaokariri kufauli mitihani ila hawawezi kuja na mambo mapya na kuona mbali zaidi ya yale waliojifunza. Ni hatari kuwa na taifa la watu waliokwenda shule kufaulu mitihani.Wapo waliokwenda shule na hawawezi hata kwenda kwenye usahili wa kazi maana hawawezi kujieleza. Haya yote yanachangiwa sana na ukosefu wa lishe bora tangu hatua za awali za ukuaji. Ili uchumi wa taifa uweze kusonga mbele lazima taifaliwe na watu wenye maono na uwezo wa kung’amua mambo magumu.Uwezo huo unaongezeka mara dufu pale ambapo watu watapata lishe bora, chakula cha kutosha na virutubisho
 2. Mheshimiwa Spika, serikali ianze kuona umuhimu wa kitengo cha chakula na lishe na kukitengea bajeti toshelevu katika kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya ulaji na lishe. Matatizo yanayosabishwa na lishe ni mengi. Kuendelea kukua kwa teknolojia hasa ya utengenezaji mbegu za mazao, teknolojia za uhifadhi wa vyakula kwenye makopo vilivyopikwa na vibichi,kuibuka kwa huduma za fast food ambapo familia nyingi zimeacha kupika majumbani pamoja na ulaji usiofaa makazini, mashuleni n.k yote haya yanamweka mwanadamu katika hatari kubwa ya kupata magonjwa.
 1. Mheshimiwa Spika, moja ya kauli iliyowahi kutolewa na shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) inasema“food is a common thread that connects us no matter what culture we come from “ kwa tafsiri isiyo rasmi ni kuwa chakula ndio uzi unaotuunganisha bila kujali tamaduni zetu. Ni muhimu kula kwa kiasi, kula vyakula vyenye virutubisho, kula kwa wakati, na kula makundi mbalimbali ya vyakula. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuona umuhimu wa kuipa nguvu Taasisi ya Chakula na Lishe. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ione umuhimu wa watoto kupata chakula cha kutosha mashuleni.
 2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia nukuu iliyoitoa katika hotuba yake ya Afya kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 iliyosema “Hatuwezi kupata viongozi wa serikali wenye uwezo mkubwa wa kutafuta suluhu ya matatizo yanayolikabili Taifa kama utotoni waliwahi kuugua tatizo la udumavu au hawakupata lishe bora, kamwe hatuwezi kutengeneza think tank ya taifa kama taifa limejaa watoto wenye udumavu au walioathirika na udumavu utotoni.”Udumavu hudumaza akili, husababisha ubongo wa mtoto au mtu mzima kushindwa kufanya kazi kwa haraka na kwa ufasaha.

 

H.KASI YA UKUAJI WA MATATIZO YA UZAZI

 1. Mheshimiwa Spika, nchi yetu kama ilivyo nchi nyingi duniani kwa sasa zinakabiliwa na matatizo makubwa ya uzazi. Matatizo hayo ni kwa wanaume na wanawake pia. Wanaume wengi wamekuwa na matatizo ya nguvu za kiume, kukosa hamu au hisia za tendo la ndoa, kulegea kwa mishipa ya uume n.k. Vilevile kwa wanawake wengi wenye umri wa kuzaa wamekuwa na matatizo ya kutoshika ujauzito kutokana na kuwa na upungufu wa homoni au homoni kutokuwa sawa (hormonal imbalance), uvimbe mbalimbali katika kizazi na vifuko vya mayai, kushindwa kuzalisha vichocheo vya mayai, kupungua kwa vichocheo vya uchavushaji wa mayai, kukosa raha au hisia ya tendo la ndoa, ukavu wa uke n.k
 2. Mheshimiwa Spika, matatizo haya yamewafanya watu wengi kupata magonjwa ya msongo wa mawazo, kukimbia familia, kutopenda kuoa au kuolewa, kupiga punyeto, ndoa au mahusiano kuvunjika n.k
 3. Mheshimiwa Spika, Pamoja na jitihada nyingi zinazofanywa na wataalamu wa tiba asili katika kuhakikisha wanatoa tumaini hususani kwa wana ndoa bado tatizo hili ni kubwa na limeghubikwa na usiri kwa wengi hasa kwa upande wa wanaume. Vijana wengi wamekuwa wakikimbilia dawa zilizopewa majina kama vumbi la kongo, alkasusi, baadhi ya vyakula kama supu ya pweza, vipande vya mihogo na karanga n.k vimekuwa vikitumika zaidi mitaani ili kuweza kuokoa ndoa au kurudisha ujasiri wa wanaume walio wengi.
 4. Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa kuna jitihada katika utoaji wa huduma za upandikizaji wa mimba kama IVF, IUI , uhifadhi wa manii n.k bado kuna uhitaji mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii ili kukabiliana na hali hizi, kutoa elimu ya mahusiano na uzazi kwa vijana,kutoa elimu zaidi juu ya masuala ya mfumo wa maisha kama vile ulaji wa vyakula vyenye virutubisho, kufanya mazoezi, kupunguza matumizi ya vileo,kupata muda wa kupumzika, kuanza mapenzi katika umri unaostahili, kuepuka magonjwa ya zinaa na tabia zisizofaa katika jamii.
 5. Mheshimiwa Spika, serikali inapaswa kutambua ni wajibu wake wa msingi kuhakikisha ustawi wa jamii yake. Kuongezeka kwa matatizo ya uzazi sio mambo ya kufumbia macho. Ni vyema serikali ianze kwa haraka kutafuta ufumbuzi kwa kuanzisha vituo maalum vya huduma ya uzazi na mahusiano kwenye hospitali za rufaa na mikoa. Hii ni pamoja na utoaji wa huduma ya ushauri kwenye masuala ya mapenzi , tendo la ndoa na tiba .
 6. Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa serikali kupitia mamlaka zinazohusika, pamoja na Baraza la Dawa Asili na Tiba Mbadala kuhakikisha dawa zinazotumika kwa ajili ya utatuzi wa masuala ya nguvu za kiume zinachunguzwa ili kuona ubora wake.Zile zenye ubora na zenye kutibu tatizo zithibitishwe na pia kuhakikisha zile zisizo na ubora zinatolewa katika soko ili kupunguza madhara yanayotokea au yanayoweza kutokea kutokana na ongezeko la matumizi ya madawa yanayotolewa kiholela.
 7. ONGEZEKO LA MIMBA ZA UTOTONI
 8. Mheshimiwa Spika, ongezeko la ndoa na mimba za utoto hapa nchini limekuwa ni tatizo sugu ambalo linafanyiwa siasa badala ya utatuzi. Kwa mujibu wa ripoti wa Shirika la UNICEF iliyoripotiwa na BBC Swahili 06 Machi, 2018[1] ilieleza kuwa Tanzania ni nchi ya tatu ukanda wa Afrika Mashariki kwa ndoa za utotoni ikiongozwa na Sudan Kusini na Uganda.
 9. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Takwimu watoto wanaolewa chini ya miaka 18 kwa Tanzania ni asilimia 31, Uganda ni asilimia 40 na Sudan Kusini ni asilimia 51. Takwimu hizi ni kubwa sana hasa tukizingatia watoto ndio nguvu kazi ijayo ya taifa na lazima waweze kuandaliwa kupeleka taifa mbele.
 10. Mheshimiwa Spika, mathalani kwa Mkoa wa Rukwa pekee kuanzia mwaka 2017 mpaka Agosti 2019 wanafunzi 722 walikatiza masomo kutokana na kupata ujauzito. Kati yao wanafunzi wa shule wa msingi 171, na sekondari ni 551. Mpaka sasa mikoa inayoongoza ni Rukwa, Tabora, Mara na Shinyanga.
 11. Mheshimiwa Spika, serikali imekuwa ikilichukualia suala hili la mimba kwa watoto walio chini ya mika 18 hasa wengi wakiwa mashuleni kama ni jambo kawaida na haioni hatari kubwa iliyo mbeleni hasa kwa watoto wanaozaliwa na wale waliowazaa. Ni jambo la kusikitisha sana kwa kuwa hata takwimu za watoto wanaopata mimba wakiwa mashuleni zimekuwa zikifichwa sana nahata baadhi ya mashirika wamekuwa waoga kutoa taarifa za tafiti hizi.
 12. Mheshimiwa Spika, watoto wa hawa wamekuwa wahanga wa mfumo ambao tayari umerithiwa na ujinga,umaskini na maradhi, na sasa wanakabiliwa na tatizo kubwa zaidi la kuwa chini ya serikali isiyojali na isiyowapa mbinu za kukabiliana na hali zao Wengi wamejikuta wakifukuzwa shule, wakifukuzwa majumbani, wakitengwa kwenye nyumba za ibada, wakipata msongo wa mawazo na hivyo wengine wamejitoa uhai, kutumia njia zisizo salama kutoa mimba au kukimbilia mitaani.
 13. Mheshimiwa Spika, sio mara ya kwanza Kambi ya Upinzani kuzungumzia tatizo hili ambalo ni hatari sana kwa maisha ya baadae ya nchi yetu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa serikali inajua ukubwa wa tatizo hili. Mapuuzo ya mambo kama haya yanaathiri zaidi kundi kubwa la wasichana. Pamoja na kuwa afya za mabinti hawa zinaathirika kimwili na kisaikolojia lakini pia wanaathirika zaidi kielimu.
 14. Mheshimiwa Spika, nchi za Umoja wa Afrika (AU) zilipitisha Ajenda ya 2063,mkakati wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa bara zima.Dhamira kuu iliyowekwa ilikuwa nikuhakikisha serikali zinajenga “mtaji wa rasilimali watu” kama rasilimali yenye thamani zaidi. Iwapo ajenda ni kuwa na rasilimali yenye thamani ni lazima serikali ione umuhimu wa kuwekeza kwenye afya na elimu ya mtoto bila ubaguzi wowote.Mwanamke ambae hajapata fursa ya kupata elimu yuko kwenye hatari nyingi za kiafya kuliko mwanamke aliyepata elimu.
 15. Mheshimiwa Spika, pamoja na mijadala inayoendelea nchini ambapo serikali ya CCM haionyeshi dhamira ya dhati ya kumsaidia mtoto aliyepata mimba katika umri mdogo au aliyeolewa. Ni muhimu sanaserikali ikatambua kuwa inatengeneza taifa la watoto ambao asilimia kubwa wataishia kuishi maisha ya umaskini na yasiyo na furaha na kama watakuwa maeneo ya mijini basi wengi huishia kuwa watoto wa mitaani ambao watageuka kuwa vibaka na kuhatarisha masiha ya wengine. Anayeadhibiwa zaidi si mama bali mtoto aliyembeba tumboni kwani mtoto huyu atakuwa na mama ambae hana elimu na hawezi kumsaidia kwa kuwa hana elimu ya malezi na makuzi ya mtoto.
 16. Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara hii iangalie umuhimu wa kuungana na Wizara ya Elimu katika kumpigania mtoto wa kike aweze kupata elimu hata kama atakuwa amepata mtoto kwa kuwa sio kila binti ameyepata ujauzito amepata kwa kupenda. Zipo changamoto za kimazingira ambazo zinachangiwa na kutembea umbali mrefu kwenda mashuleni ambapo wengi hubakwa, zipo sababu za kulazimishwa kuolewa na wazazi kutokana na mila na desturi zisizofaa, umaskini, kukumbana na wanaume mafataki (wasio na adabu wanaowarubuni watoto wa kike kutokana na hali zao za kimaisha), zipo sababu za kibailojia hasa waliofikia umri wa balehe wasipopata elimu ya mahusiano basi wengi huishia kujaribu mambo mbalimbali na wasijue madhara yake.
 17. J. UKATILI WA KIJINSIA KWA WANAWAKE NA WATOTO
 18. Mheshimiwa Spika, bado nchi yetu inakumbwa na tatizo kubwa la unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Serikali ilikuja na mpango wa utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000), Sera ya Maendeleo ya Mtoto, Sheria ya Mtoto 2009, Sheria ya makosa ya kujamiiana yaani SOSPA ya Mwaka 1998, na Mkakati wa taifa wa Maendeleo ya Jinsia 2005  ili kuhakikisha mpaka ifikapo mwaka 2020 matukio ya ukatili wa kijinsia yawe yamepungua kwa asilimia 50.
 19. Mheshimiwa Spika, visa vya mauaji ya watoto wadogo vimekuwa vikiongezeka kila mwaka. Tutakumbuka Mwezi Februari 2019, watoto kumi chini ya umri wa miaka 10 waliokutwa wamefariki katika mazingira ya kutatanisha Wialayani Njombe huku baadhi ya viuongo vyao vya mwili vikiwa vimenyofolewa .Kisa hicho kilifuatiwa na vifo kadhaa vya watoto kikiwemo kifo cha mtoto aliyekutwa amenyogwa katika kijiji cha Matembwe. Mnamo tarehe 03, Machi 2019, polisi walithibitisha kisa cha mtoto aliyeuwa na kukatwa sehemu za mwili wake Mkoani Mbeya.
 20. Mheshimiwa Spika, pamoja na visa vya mauaji kuongezeka visa vingine vya ubakaji, vipigo, ukeketaji, udhalilishaji kwa kutumia lugha au matendo na vile vya ubakaji vimekithiri.Katika ripoti iliyotolewa Shirika la LHRC 2018 kuhusu ukatili wa kingono dhidi ya watoto, ripoti hiyo inaonyesha  matukio 6,376 ya ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa mwaka 2018, ikilinganishwa na visa 4748 mwaka 2017 ikiwa ni ongezeko la visa 1648.
 21. Mheshimiwa Spika, Ubakaji na ulawiti uliongezeka kutoka 759 Mwaka 2017 mpaka 2365 Mwaka 2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 91.Mwaka 2019, ripoti ya Shirika hilo ilionyesha kuanzia mwezi January mpaka June 2019 visa vya udhalilishaji wa kingono kwa watoto vilikuwa takribani asilimia 66. Mikoa ya iliyoongoza ni Dar es Salaam, Mbeya, Iringa na Simiyu huku visa vya ukatili kwa ujumla vikiongoza mikoa ya Kanda ya Ziwa.
 22. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha miaka 5 matukio ya ukatili wa wanawake yameongezeka hasa yale ya ukatili ya kimwili. Kambi Rasmi imezungumzia ukatili huu mara nyingi lakini bado serikali haijachukua jitihada za kutosha kukomesha vitendo hivi. Wanawake wengi wanauawa kutokana na wivu wa kimapenzi na sababu za kishirikina. Vitendo vya biashara ya kuuza sehemu za siri na matiti ya wanawake vinavyohusishwa na imani za kishirikina vimekithiri. Vitendo vya ubakaji kutoka kwenye makundi mbalimbali ya vijana kama Teleza mkoani Kigoma vinaonyesha dhahiri mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii zetu na ukatili mkubwa kwa wanawake.
 23. Mheshimiwa Spika, bado mauaji ya vikongwe yameendelea kutekelezwa. Udhalilishaji wa wanawake kwa kutumia lugha za matusi na dharau katika familia, sehemu za kazi na hata katika mitandao ya kijamii na kufanyiwa mapenzi kinyume na maumbile vimekithiri huku jamii ikiona ni mambo ya kawaida bila kujali wanawake wanaumizwa kwa kiasi gani. Wanawake wamekuwa wakidhalilishwa kutokana na maumbile yao kitendo kinachofanya kuongezeka kwa vitendo vya kubadilisha rangi za ngozi,shepu na hata kuwafanya mabinti wadogo kuishi maisha ya kuiga (fake life) ili waweze kuendana na matakwa ya baadhi ya makundi kwenye jamii.
 24. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa mara nyingine tena inaitaka serikali kuchukua masuala haya kwa uzito.
 25. Serikali haina budi kuhakikisha heshima na utu wa mwanamke au mtoto unalindwa katika hatua zote za kutafuta haki.
 26. Serikali ikishirikiana na taasisi na mashirika binafsi haina budi kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na masuala ya sheria zinazolinda haki za makundi yote kwenye jamii hii ikiwa ni pamoja na mapitio ya sheria na milazote kandamizi zifanyiwe marekebisho au kufutwa. Mfano, sheria za Uraia No.6 ya mwaka 1995 ambayo ina ubaguzi mkubwa kwa kumkosesha nwanamke haki sawa na mwanaume katika masuala ya kuchagua uraia anaoutaka bila kunyang’anywa uraia wake wa asili. Kambi Rasmi pia inashauri mapitio katika Sheria ya ndoa katika dhana nzima ya ndoa kwa kuwa endapo mmoja wa wapenzi akifariki kabla ya kutimiza muda wa kuishi pamojaunaohitajika kisheria basi kuna uwezekano wa mmoja wapo kukosa haki katika mahusiano hayo.Haki ya kukopa katika sheria ya ndoa; pamoja na kuwasaidia wanawake kujikomboa kiuchumi imetokea kuwaumiza wanaume wengi na kujikuta wakipoteza mali
 • Kambi rasmi imekuwa ikisikia malalamiko ya baadhi ya wananchi wanaokumbwa na madhila na hivyo kuhitaji huduma ya PF3 katika vituo vya polisi. Jambo la kushangaza ni kuwa baadhi ya askari wasio waaminifu wamekuwa wakiwatoza fedha wananchi ili kujipatia huduma hii. Mfano katika sakata la ubakaji wa wanawake lililokuwa linafanya na vijana wa Teleza , kina mama wengi walilalamika kutozwa sh. 5,000/ ili waweze kupata PF3 na pia walikutana na lugha za kejeli na udhalilishali. Serikali ihakikishe jambo hili linakomeshwa na pia kuhakikisha inaweka mikakati ya kutosha kutokomeza makundi haya ya kihalifu kama Teleza kwa kuwa tangu mwaka 2014 yamekuwa yakiwasumbua wananchi hususani mkoani Kigoma.
 1. Serikali iweke mikakati ya kuajiri zaidi maafisa maendeleo na maafisa ustawi ya jamii ili kushughulikia zaidi matatizo ya kijamii yanayowakumba wananchi ambayo yanaathiri afya ya akili ya jamii, utu na heshima.

 

 1. KUKITHIRI KWA BIASHARA YA UKAHABA KWA NJIA YA MITANDAO

 

 1. Mheshimiwa Spika, kumetokea wimbi kubwa la vijana wadogo wa kike na wa kiume kujiingiza katika vitendo vya ngono kwa njia ya teknolojia ya mitandao. Vijana wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kujitangaza kwa kurusha picha na mawasiliano yao kama njia ya kutafuta wateja wakufanya nao ngono.
 2. Mheshimiwa Spika, kukua kwa utandazi na kumomonyoka kwa maadili kumechochea vijana wengi kujiingiza katika biashara hii haramu bila ya wazazi kufahamu. Hii imekuja kama hatua mpya ya kukabiliana na askari ambao huwafurusha au kuwakamatawakirandaranda usiku kwenye mitaa, mabaa au nyumba za wageni. Wengine hutumia njia hii kuficha aibu ya kujulikana kwa jamii kama makahaba. Kutokana na hali ngumu za maisha wapo vijana wenye elimu za sekondari na vyuo ambao pia wamejikuta wakiingia katika biashara hii haramu.
 3. Mheshimiwa Spika,Vijana hao wamekuwa wakipanga kukutana na wateja wao maeneo mbalimbali ya nchi baada ya kukubaliana bei.Wapo wanaotumiwa nauli na kusafiri kwenda mbali kukutana na wateja wao bila kujali usalama wao.Wapo wateja wengine nao wamejikuta kwenye matatizo. Wengi wa makahaba hawa wameishia kudhulumiwa, kubakwa na kuambukizwa maradhi, kupigwa na hata kuuawa.
 1. Mheshimiwa Spika, serikali haina budi kuanza kuzungumza jambo hili kwa uwazi na kukemea vitendo hivi vinavyodhalilisha utu na kuhatarisha maisha. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuanzisha mitaala inayogusia maisha ya kila siku ya vijana na changamoto wanazokumbana na namna ya kuzitatua. Serikali iweze mazingira rafiki kati ya walimu na wanafunzi ili waweze kuzungumza kwa uwazi changamoto za kimahusiano wanazokumbana nazo. Vilevile, wazazi wachukue jukumu la msingi la kuzungumza na watoto/vijana wao na kujua mienendo yao. Matumizi ya mitandao yawe na mipaka kwa watoto ili kuwaepusha kujiingiza katika hatari hii kubwa itakayowaharibia maisha yao.

 

 1. HITIMISHO
 2. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikishauri mambo mengi ya kuweza kuisaidia serikali kama jicho la pili la serikali. Lakini ni kwa bahati mbaya kutokana na siasa au uelewa tofauti wa watendaji katika nafasi mbalimbali za serikali kudhani kuwa jambo linaloshauriwa na serikali likifutwa serikali itabezwa. Tofauti na nchi nyingi duniani zilizoendelea mambo yanayoshauriwa na upinzani huchukuliwa kwa uzito wake ili kuisaidia serikali husika kufanya mengi mazuri zaidi. Katika hili upinzani tunatimiza wajibu wetu wa kikanuni na matakwa ya wananchi kuhakikisha jicho letu limeona kila mahali penye mapungufu ili yafanyiwe marekebisho. Katika hali iliyopo sasa ya gonjwa la korona ni muhimu bila kujali vyama tufanye kazi kwa pamoja kutoa elimu na ushauri ambao utatusaidia sisi sote kama taifa.
 3. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kupunguza nguvu kubwa inayoitumia kupambana na vyama vya upinzani na wanasiasa na badala yake itumie nguvu kubwa kuboresha afya za watanzania kwa kuwekeza katika sekta ya afya. Maisha yetu sote ni muhimu. Tujilinde na tuwalinde wengine. “Afya bora huzaa Taifa bora”.

………………………

Cecilia Daniel Pareso (Mb)

MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA AFYA,

MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

 

28 APRIL, 2020

[1]https://www.bbc.com/swahili/habari-43299473

[i]https://www.who.int/emergencies/diseases/novel-coronavirus-2019/events-as-they-happen

[ii]

[iii]https://afyablog.moh.go.tz/2018/04/hotuba-ya-waziri-wa-afya-maendeleo-ya.html

Share Button