CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesikitishwa na kushangazwa na kitendo cha Naibu Spika wa Bunge, Ndugu Tulia Ackson, kushindwa kuchukua hatua dhidi ya kitendo cha udhalilishaji wa mhimili wa Bunge kilichofanywa na Mbunge wa CCM kuchana hotuba ndani ya ukumbi wa Bunge, hivyo kinatafakari kuchukua hatua za kisheria dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa Katiba, Sheria na Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa Bunge, vinavyofanywa na Kiti cha Spika kwa kudhalilisha, kukumbatia, kutetea au kulinda vitendo vinavyodhalilisha nafasi ya Kambi ya Upinzani Bungeni, hususan mamlaka iliyonayo ya kutoa maoni mbadala kwa Serikali.

Itakumbukwa kuwa katika siku za hivi karibuni Kiti cha Spika, kimekuwa kikijipatia mamlaka ya kuhariri maoni ya Wasemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni yanayotolewa kupitia wasemaji wakuu wa kambi. Hatua hiyo inayofanywa na Kiti cha Spika inalenga ama kuifurahisha au kuipatia unafuu Serikali iliyoko madarakani kwa kuhariri hotuba za wasemaji wakuu vivuli katika wizara mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuagiza kufutwa kwa baadhi ya maneno, kadri ambavyo kiti hicho kinaona inafaa, badala ya kuzingatia taratibu za uendeshaji wa bunge ambazo zinatambua kuwa kambi hiyo inayo haki na wajibu wa kutoa maoni mbadala (Serikali mbadala) dhidi ya upande wa pili, yaani Serikali iliyopo madarakani.

Wakati Chama kikitafakari hatua hizo ambazo zinalenga kurejesha uimara wa Bunge kuwa chombo cha uwakilishi wa wananchi, kurejesha misingi ya chombo hicho kuendeshwa kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni za Bunge kwa ajili ya kuidhibiti, kuisimamia na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi, katika hatua ya sasa, tunalaani na kukemea kwa nguvu zote vitendo vinavyofanywa na kiti au vinafanywa na wabunge wa CCM kisha kukumbatiwa na kiti hicho dhidi ya maoni rasmi yanayotolewa na Wasemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika wizara mbalimbali, kama ilivyofanyika jana ambapo Kiti cha Spika kikikaliwa na Naibu Spika kilishindwa kuchukua hatua dhidi ya kitendo cha Mbunge wa CCM aliyechana Hotuba ya Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2019/2020. Badala yake akaamua kufanya maamuzi ya uonevu na ukandamizaji kwa wabunge wa Chadema; John Heche (Tarime Vijijini), Ester Matiko (Tarime Mjini) na Dkt. Immaculate Sware Semesi (Viti Maalum Mkoa wa Dodoma) kwa kuagiza watolewe nje ya ukumbi wa Bunge kwa nguvu, kinyume cha taratibu za uendeshaji wa vikao vya Bunge.

Tunakikumbusha kiti hicho kwa maana ya Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kuwa, Kambi ya Upinzani Bungeni ipo na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge ambazo zimetungwa kwa msingi wa ibara ya 89(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni kwa msingi huo, maoni ya bajeti mbadala (ikiwemo hicho kitabu kilichochanwa mbele ya macho ya kiti na kiti hakikuchukua hatua yoyote) yanayotolewa bungeni na Wasemaji Wakuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (Mawaziri Vivuli) kwa mujibu wa Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ni sehemu ya mali za Bunge, hivyo kuchana nyaraka hiyo na kutetea, kulinda au kushindwa kuchukua hatua dhidi ya kitendo hicho, si tu ni kudhalilisha na kubeza muundo wa Bunge ambao uko kwa mujibu wa kanuni lakini pia ni udhalilishaji mkubwa wa Bunge lenyewe kwamba haliwezi kulinda mali na nyaraka zake muhimu.

Kitendo hicho pia kimeonesha hulka na taswira ya Wabunge wa CCM, uchanga na uanangezi wao kwenye ushindani wa hoja katika siasa za kibunge huku kikidhalilisha nafasi ya wananchi ambao Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inawasilisha maoni kwa niaba yao. Nafasi hiyo inapaswa kuheshimiwa na Bunge na kuiacha Serikali ijibu hoja za kambi hiyo badala ya kiti kutumika au kutumia mamlaka yake vibaya kuilinda au kuipatia nafuu Serikali.

Aidha, mbali ya kuwapongeza Wabunge wetu wote ambao walisimama kidete kwa vitendo na kauli, kupinga udhalilishaji wa bunge na waliofanyiwa wabunge wenzao watatu, uliofanyika jana, Chama kiliwaagiza wabunge wake, kwa kushirikiana na Wabunge wengine wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuchukua hatua kadhaa, ikiwemo kuomba mwongozo wa kiti kuhusu tukio hilo na pia kukutana, kujadili na kufanya maamuzi ya hatua zaidi dhidi ya kitendo hicho na utetezi uliofanywa na kiti.

Tunamkumbusha Naibu Spika kuwa kwa taaluma yake ya sheria, nafasi yake ya ubunge, cheo alichonacho cha Naibu Spika na uelewa wa masuala anuai alionao, anajua msemo usemao ‘two wrongs don’t make a right’, hivyo asitumie suala (kosa analolijua yeye Naibu Spika) la Easter Bulaya kujenga hoja za kuendelea kulinda na kutetea badala ya kuchukua hatua dhidi ya kitendo hicho cha mbunge wa CCM ambaye ni vyema akajua kuwa amejifunua uwezo wake wa kutumia akili, amedhalilisha nafasi ya ubunge, Kiti cha Spika na Mhimili wa Bunge, mbele ya wapiga kura wake na Watanzania wote kwa ujumla.

Imetolewa leo Jumatano, Juni 19, 2019 na;

Tumaini Makene

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Share Button