MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU HALI YA UCHUMI WA TAIFA, MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020
Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016
A. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, hii ni bajeti ya nne ya Serikali hii ya awamu ya tano ambapo imebaki bajeti moja tu ya mwaka wa fedha 2020/2021 kabla Serikali hii haijamaliza muda wake wa kuwa madarakani. Hata hivyo, pamoja na kwamba imebaki takriban miaka miwili Serikali hii imalize mhula wake wa miaka mitano madarakani, utekelezaji wa bajeti zilizotangulia umekuwa ni wa kusuasua jambo ambalo limeathiri sana sekta nyingi za uzalishaji na hivyo kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.
2. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mara zote Kambi Rasmi ya Upinzani imekuwa ikiishauri Serikali hii juu ya masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa ajili ya ustawi wa wananchi na mustakabali mwema wa taifa letu; na kwa kuwa mara nyingi Serikali imekuwa ikiubeza ushauri huo na kufanya mambo kwa sifa au kwa kiburi cha madaraka bila kuzingatia ushauri wa Bunge; safari hii Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itajikita zaidi katika kutoa misimamo ya kisera katika sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa ili watanzania wajue, Serikali itakayoundwa na CHADEMA itafanya nini katika sekta hizo ikiwa CHADEMA itapewa ridhaa ya kuongoza dola.

B. MAPENDEKEZO YA MFUMO MPYA WA UCHUMI KWA TANZANIA
 UCHUMI WA SOKO JAMII (SOCIAL MARKET ECONOMY)
3. Mheshimiwa Spika, baada kipindi kirefu cha takriban miongo mitano cha mapambano ya Tanzania kujinasua katika lindi la umasikini na kushindwa kufikia lengo hilo; Kambi Rasmi ya Upinzani imegundua kwamba lipo tatizo la msingi katika mfumo wetu wa uchumi. Kwanza mfumo wetu wa uchumi umepitwa na wakati na hauendani na mahitaji ya dunia ya sasa; lakini pili ni uchumi uliohodhiwa na Serikali jambo ambalo limeua nguvu ya soko katika kuamua mustakabali wa uchumi. Mfumo wa Uchumi wetu usipofanyiwa marekebisho makubwa; Tanzania itaendelea kuwa maskini milele yote.
4. Mheshimiwa Spika, uchumi weti umeendelea kwa duni na madeni makubwa, lakini jambo la msingi zaidi ni kwamba; hali hii inazidi kuwaathiri Watanzania. Ukweli huu haupingiki: Mwaka 2017 zaidi ya watanzania milioni 12 waliishi katika umaskini uliokithiri (Benki ya Dunia 2017). Takriban asilimia 28 ya Watanzania walikuwa chini ya Mstari wa Umaskini wa Mahitaji ya Msingi (NBS 2017, uk.52). Mamilioni ya watu hawakuwa na maji wala umeme (Kessy/Mahali 2017). Ukosefu wa ajira umekuwa mkubwa sana kwa kipindi chote cha miaka iliyopita (ILO 2018). Takwimu zinaonyesha kwamba kiwango cha chini cha mahitaji ya kumwezesha mtu kuishi bado hakijafikiwa; na pia maendeleo ya kiuchumi bado hayajapatikana.
5. Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere tayari alishatoa moni yake juu ya viashiria vya umasikini katika miaka ya 1960, akisisitiza kwamba; “Watanzania sasa wanajua kwamba umasikini wetu, ujinga wetu, na maradhi yetu hayawezi kukwepeka kama sehemu ya maisha ya binadamu” (Nyerere 1973, uk.110). Kwa kukubaliana na hoja ya Mwalimu Nyerere, Kambi Rasmi ya Upinzani kupitia CHADEMA inaamini kwamba, kwa namna ile ile, umaskini wa leo umesababishwa na watu. Unaweza ukahusishwa na mfumo mbovu wa uendeshaji wa uchumi na uwepo wa sera mbovu za uchumi. Kwa miongo kadhaa sasa, watawala wamekuwa wakitumia mfumo huo mbovu wa uchumi kuwakandamiza Watanzania. Mfumo wa uchumi umelenga “kulipa madeni”, lakini hautengenezi fursa za maendeleo ya kiuchumi kwa watu. Jambo hili halikubaliki!!!
6. Mheshimiwa Spika, Ili kukabiliana na hali tete ya uchumi wa nchi yetu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia CHADEMA inahimiza uwepo wa mfumo imara wa uchumi unaofanya kazi vizuri. Ili kuwasaidia Watanzania kuondokana na vikwazo vya kijamii vya maisha duni, kuboresha maisha ya mamilioni ya watu na kuiendeleza nchi kwa ujumla wake. Kambi ya Upinzani kupitia CHADEMA inakusudia kutatua changamoto hizo kwa kuanzisha mfumo wa maendeleo ya kiuchumi kwa Watanzania wote. Kwahiyo, CHADEMA inapendekeza kuanzishwa kwa ‘Mfumo wa Uchumi wa Soko Jamii’ nchiniaTanzania – mfumo ambao umefanikiwa kuziimarisha na kuziendeleza nchi mbalimbali duniani, na wakati huohuo, kuwaondoa wananchi wa nchi hizo kwenye umaskini na kuwapatia fursa za ajira zenye uhakika.
7. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia CHADEMA inaungana na mawazo ya Mwalimu Nyerere katika kuamini kwamba; maendeleo halisi yanaweza tu kutokea kwa kuondoa umaskini nchi nzima. Katika mfumo wa uchumi unaopendekezwa, jitihada zote za kiuchumi zitaelekezwa kwenye kuanzisha utajiri na hivyo kuushinda umasikini ambao ni adui wa maendeleo.
8. Mheshimiwa Spika, Uchumi wa Soko Jamii, ni Mfumo wa Uchumi unaolenga kuleta maendeleo shirikishi na endelevu kwa kila mtu. Unatokana na mfumo wa Ubepari, unaojulikana pia kama uchumi wa soko, ambao unalenga kuanzisha soko huru la kiushindani. Changamoto za mfumo wa uchumi wa soko zinaweza kuchukuliwa na mfumo wa uchumi wa kijamaa. Uchumi wa Soko jamii unalenga kukidhi kiwango cha chini cha ustawi wa kiuchumi kwa kila mwananchi.
9. Mheshimiwa Spika, Kimsingi mfumo huu unaleta pamoja faida za ubepari na ujamaa na unaondoa kabisa hasara zake. Hii inaanzisha mfumo mpya wa uchumi ambao unatekelezeka, unakubalika na unaolenga ustawi wa watu. Ili kuimarisha uchumi wa nchi, kila kikwazo kwa maendeleo ya uchumi kinaondolewa. Hata hivyo, kila hatua lazima ichukuliwe kwa kuzingatia ushirikishwaji, uendelevu na kujali utu. Jambo hili hatimaye, litampatia kila Mtanzania fursa za uhakika za kustawi kiuchumi na kuboresha maisha yake.
10. Mheshimiwa Spika, Dhana ya Uchumi wa Soko Jamii imejengwa katika misingi ya mshikamano na imani kwamba, ngazi ya chini kabisa katika jamii mahalia inao uwezo wa kushughulikia masuala yanayoihusu. Kwa upande mwingine, mshikamano unakuza shauku ya umoja katika Taifa. Kutokana na hali hii, viongozi wa kisiasa, waajiri na waajiriwa husimama pamoja kumtetea kila mmoja na kwa sababu hiyo, husababisha maendeleo ya kiuchumi kuwa kwa ajili ya kila mmoja. Halikadhalika, hali ya ngazi ya chini kabisa katika jamii kuwa na uwezo wa kushughulikia masuala yake yenyewe, ni chachu ya kumjengea uwezo kila mtu kushiriki katika maendeleo ya uchumi. Humpa kila mtu, vikundi vidogovidogo na taasisi zilizogatuliwa wajibu wa kushughulikia mambo yanayowahusu, na kupatiwa msaada tu pale inapobidi.
11. Mheshimiwa Spika, Misingi mingine ya Mfumo wa Soko Jamii ni soko huru lenye mfumo huru wa upangaji wa bei, na pia mfumo wa udhibiti ili kuzuia baadhi ya watu au taasisi kuhodhi mwenendo wa soko. Zaidi ya hayo, Uchumi wa Soko Jamii unatoa uhuru kwa kila mtu kumiliki mali binafsi. Serikali huusaidia mfumo huu kwa kutoa huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na mazingira ya uhakika na shirikishi ya hifadhi ya jamii. Misingi na tabia nyingine za Uchumi wa Soko Jamii zipo katika mfumo imara wa kisheria ili kuhakikisha kwamba uchumi unakuwa imara na thabiti kisheria.

 Kwa Nini Tunapendekeza Mfumo waUchumi Wa Soko Jamii?
12. Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Uchumi wa Tanzania umepitia mabadiliko kadhaa kwa kipindi chote cha miaka iliyopita. Ulitoka katika uchumi wa soko wa kikoloni, ukaenda kwenye uchumi wa kijamaa na baadaye ukarudi tena kwenye uchumi wa soko. Licha ya juhudi za kufanya maboresho, hakuna mfumo hata mmoja ambao umefanikiwa kuondoa umaskini na kutengeneza fursa sawa za kiuchumi.
13. Mheshimiwa Spika, Mfumo wa kiuchumi wa kibepari umethibitika kuwa sio mzuri kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa umeshindwa kuziba pengo katika ya matajiri na masikini. Hivyo haukuweza kuliunganisha Taifa katika ukuaji wa uchumi.Uchumi wa Soko Jamii unaziba pengo hilo kwa kutoa fursa za kiuchumi kwa kila mmoja, na wakati huohuo unatoa hifadhi ya jamii katika nyanja za ajira, huduma za afya, elimu na huduma nyingine za jamii.
14. Mheshimiwa Spika, Mfumo wa pili ambao ni wa kijamaa, uliondoa kabisa ushindani katika soko la Tanzania. Kupitia mfumo huu, viwanda vya Tanzania vilikufa kutokana na kukosa mazingira mazuri ya kukua. Uchumi wa Soko Jamii unalinda ushindani wa nchi kwa kujiepusha na vikwazo wa kiuchumi visivyo vya lazima vinavyoweza kuathiri ushindani.
15. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia CHADEMA inaunga mkono uanzishwaji wa Uchumi wa Soko Jamii kutokana na kwamba mfumo huo unatekelezeka. Mfumo huu umechukua baadhi ya mambo mazuri kutoka katika mifumo yote miwili ya ya kiuchumi kutoka katika ujamaa na ubepari na miwili ya kibepari na kijamaa na kuyaunganisha pamoja katika mfumo wa mmoja wa uchumi uliosukwa vizuri. Matokeo ya jambo hili ni kwamba; Tanzania inakwenda kushuhudia maendeleo ya kiuchumi yaliyo imara na shirikishi.
16. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia
CHADEMA inaamini kwamba mfumo huu ndio suluhisho pekee kwa Taifa kusonga mbele kiuchumi. Uchumi wa Soko Jamii unatoa uhakika kwamba, Tanzania inaweza kuwa na ushindani kimataifa na wakati huohuo kuwa na uwezo wa kulinda maslahi ya wananchi wake. Fursa kama hizo, huwawezesha watu kutumia uwezo wao wa kufanya kazi au biashara na hivyo kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini. Ni katika kujitegemea kwa namna hiyo kwa mtu mmoja mmoja, ambapo Tanzania inaweza kujinasua na utegemezi wa kisiasa na kifedha kutoka kwa wafadhili wake. Kutokana na hali hiyo, Watanzania wataweza kutengeneza Sera na kuzitekeleza kwa ajili ya kukidhi malengo ya kuiendeleza nchi yao.
17. Mheshimiwa Spika, Historia ya mafanikio ya uanzishwaji wa Uchumi wa Soko Jamii, imeelezwa katika mawanda mapana ya uchumi wa kimataifa. Kwa jinsi hiyo, mfumo huu umeonyesha mafanikio makubwa katika maendeleo ya kiuchumi katika nchi mbalimbali zikiwemo Sweden, Finland na Ujerumani.
18. Mheshimiwa Spika, CHADEMA inaunga mkono mfumo wa uchumi wa soko Jamii kama hatua ya kurekebisha uchumi wa nchi, kutokana na Serikali kuendelea kushindwa kuleta maendeleo ya kiuchumi.
19. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu historia ya mfumo wetu wa Uchumi na sababu zilizopelekea CHADEMA kubuni sera ya uchumi inayopendekeza kuwa na Mfumo huu mpya wa Uchumi yapo katika kitabu cha Sera ya Uchumi ya CHADEMA kitakachozinduliwa mapema baada ya Mkutano huu wa Bunge, ili kuwa kuwapa watanzania uelewa juu ya mageuzi makubwa ya uchumi tunayokwenda kufanya katika Taifa hili ikiwa tutapewa ridhaa na watanzania ya kuendesha Serikali.

Share Button