TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA

KUHUSU UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA (DKWK)

Baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pia kwa kushirikiana na vyama vingine washirika, kuibana mara kadhaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia njia mbalimbali kuitaka isiendelee kukiuka Katiba ya Nchi na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inayoweka utaratibu wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK), hatimae tume hiyo imetoa ratiba ya zoezi la uboreshaji wa daftari hilo kwa nchi nzima, ikionesha kuwa itaanza kuandikisha mwaka huu kuanzia katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na kumaliza mwaka kesho, Mkoa wa Dar es Salaam.

Tofauti na wito wa Chadema ulioitaka NEC kujitokeza hadharani na kutangaza ratiba hiyo kwa umma, tume imetoa ratiba hiyo ‘kimyakimya’ kwa kuiweka mojawapo ya viambatanisho kwenye barua iliyoandika kwa vyama vya siasa na wadau mbalimbali kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Nakala ya ratiba hiyo kutoka NEC iliyoandikwa “Ratiba ya Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2019/2020”, inaonesha kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaanza shughuli hiyo tarehe 23 Juni, mwaka huu, katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Itazunguka katika maeneo mengine ya Tanzania (bara na visiwani) kabla ya kumaliza kazi hiyo Mkoa wa Dar es Salaam, kuanzia tarehe 8-27 Februari, mwaka 2020. Baada ya uboreshaji kufanyika nchi nzima, NEC itaweka wazi daftari hilo mnamo Machi 27 hadi Aprili 15, mwaka 2020.

Pamoja na NEC kutoa ratiba hiyo ndani ya muda mfupi kabla ya kuanza utekelezaji wake, jambo ambalo litawapatia usumbufu mkubwa wadau wengine wa mchakato huu nyeti kuelekea uchaguzi mkuu (vyama vya siasa, asasi za kiraia, waangalizi na watazamaji), ambao wanahitaji kufanya maandalizi muhimu na makubwa ya kushiriki kwa njia mbalimbali nchi nzima, ikiwemo kuhamasisha wananchi, kutoa elimu ya uraia, kutambua, kuandaa na kuweka mawakala wa kufuatilia zoezi hilo, katika hatua hii ya sasa, Chadema inasisitiza yafuatayo;

1.NEC itangaze ratiba yote ya shughuli hiyo ya uboreshaji wa DKWK kwa ukamilifu wake hadharani ili wananchi na wapiga kura ambao ndiyo wadau wakubwa katika mchakato huu, waielewe kisha wajiandae kushiriki kikamilifu kwenye hatua hii muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

2. Itoe maelezo ya kina ya ratiba kwa kwa maeneo yote ili wananchi waweze kutambua na kujipanga mahali watakapoenda kujiandikisha.

3. Itaje orodha ya vituo vitakavyotumika kuandikisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kwa sababu ratiba iliyotolewa haina kipengele hicho muhimu ambacho kitawasaidia wananchi wenye sifa za kuwa wapiga kura kujiandaa na kujua mahali wanapotakiwa kujiandikisha.

4. NEC itangaze hadharani ni lini mchakato wa ajira za muda kwa ajili ya kuajiri wasimamizi wa uboreshaji wa DKWK utafanyika tena baada ya kusimamishwa na tume hiyo hivi karibuni, ikiwa ni siku chache baada ya Chadema kutoa kauli ya kuitaka NEC iongeze muda wa shughuli hiyo kwa sababu muda uliotolewa na tume kwenye tangazo lake la Mei 30, mwaka huu (kuwasilisha maombi ya kazi hiyo mwisho uliwekwa kuwa ni kabla ya Juni 2, 2019), ulikuwa hautoshi. Suala hili la kuwapata Watanzania wenye sifa zinazotakiwa kufanya kazi hiyo ni muhimu, linalohitaji umakini na maandalizi ya kutosha kwa maana ya mafunzo.

5. Watanzania wote, walioko ndani na nje ya nchi, waliofikisha miaka 18 au wanaotarajia kufikisha umri huo mwaka kesho wakati wa kupiga kura, waanze kuhamasishana na kujiandaa kujitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Halikadhalika tunatoa wito pia kwa wapiga kura wote walioandikishwa kupiga kura uchaguzi mkuu wa 2015, wajiandae kufika katika vituo hivyo kuhakiki taarifa zao. Aidha wote waliopoteza vitambulisho vyao na wale ambao vitambulisho vyao vimeharibika au wamehamia makazi katika maeneo hayo kufika katika vituo hivyo kwa ajili ya utaratibu wa kuandikishwa.

6. Kwa kutambua umuhimu na unyeti wa uandikishaji wapiga kura kuwa ni mojawapo ya hatua muhimu katika mchakato wa uchaguzi, hasa Taifa linapojiandaa na uchaguzi mkuu wa 2020, Chadema kimejipanga kushiriki na kufuatilia shughuli hiyo kwa ukaribu na umakini unaohitajika, ikiwemo utaratibu wa kuwa na mawakala katika vituo vyote vya kuandikisha wapiga kura kama taratibu zinavyoelekeza.

Hitimisho

Ni muhimu NEC itimize wajibu wake kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi ambazo zinaipatia mamlaka ya kusimamia jambo nyeti linaloamua hatma ya maisha ya mwananchi mmoja mmoja, makundi, jamii na hatimae taifa kwa ujumla. Tume itambue kuwa wadau mbalimbali wa uchaguzi, hususan wapiga kura, wanafuatilia kwa ukaribu umakini, uwezo na utayari wa NEC kusimamia uchaguzi nchini na kipekee Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Imetolewa leo, Jumatatu Juni 10, 2019 na;

Tumaini Makene

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA

Share Button