MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHESHIMIWA PETER SIMON MSIGWA (MB) KUHUSU UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2018/19 NA MPANGO WA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KWA MWAKA WA FEDHA WA 2019/2020
(Yanatolewa chini ya Kanuni za Bunge, Kanuni ya 99(9), toleo la mwaka 2016)

I. UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika,napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na nguvu katika kipindi hiki kigumu sana katika ufanyaji wa siasa hasa kwa upande shindani na Chama Tawala na kuweka kusimama mbele ya hadhira hii ili kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu sekta nzima ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

2. Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kuwapa pole viongozi wote wa vyama vya Upinzani kwa madhira makubwa wanayokumbana nayo kutoka kwenye vyombo vya dola pamoja na matishio yaliyopo kutokana na sheria mpya na mbaya sana ya kudhibiti vyama vya siasa hasa vile shindani na chama tawala, pia kuwashukuru na kuwapongeza kwa mshikamano ambao unajengwa na hivyo kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao tunaitoa Serikali hii ya awamu tano madarakani.

3. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wapiga kura wangu wa Iringa mjini kwa kuendelea kuniamini, na imani kubwa walio nayo kwangu. Naendelea kuwaahidi kuwa sita waangusha.

II. MWENENDO NA HALI YA MALIASILI NCHINI

a) Sekta ya Uwindaji

4. Mheshimiwa Spika, sekta ya Uwindaji ni sekta muhimu katika Utalii. Kuanzia Mwaka 2009-2016 sekta hii ilichangia takribani dola za kimarekani milioni 163,465,077.01 sawa na takribani shilingi bilioni 3.5 za Kitanzania ndani ya sekta. Mwenendo wa biashara ya Uwindaji, inaonekana kuporomoka kuanzia mwaka 2014/15 mpaka mwaka 2017 ambapo makadirio yanaonyesha kuendelea kuporomoka zaidi. Mwaka 2010/11 mapato yalifikia dola 26,399,634 ikilinganishwa na mwaka 2015/16 ambapo mapato yalifikia kiasi 17,406,860 na mwaka 2016/2017 kiasi cha shilingi 18,787,976 tu .Hii ikiwa na maana kwamba miaka ya nyuma sekta hii ilifanya vizuri tofauti na ilivyo sasa.

5. Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu zimejitokeza changamoto nyingi katika sekta hii ya uwindaji ikiwemo muda uliotolewa kwa uwindaji kupunguzwa kutoka miaka mitano mpaka miaka miwili na kuleta sintofahamu kwa wadau, pamoja na jitihada nyingi zilizofanyika bado kuna changamoto nyingi ikiwemo vitalu vingi kukosa wamiliki na hivyo kupelekea vitalu hivyo kuvamiwa na wafugaji, wawindaji na majangili.

6. Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo Kambi Rasmi ya Upinzani inakemea tabia ya serikali kuendelea kukandamiza sekta binafsi kwa kufanya maamuzi ya kukurupuka bila kuwasikiliza au kushauriana na wadau wa sekta binafsi ili kuleta ufanisi na ushirikiano wa kibiashara. Kambi Rasmi ya Upinzania inaitaka serikali itambue mchango mkubwa wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na makusanyo ya kodi yanayotokana na sekta binafsi.

7. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kukaa upya nawamiliki wa vitalu pamoja na wadau wengine wanaojihusisha na biashara ya utalii na uwindaji ili kufikia maamuzi ya pamoja kwa kuangalia namna bora ya kufanya kazi na kutatua changamoto kubwa na masononeko miongoni mwa wawekezaji katia Sekta hii , ili kulinda sifa ya Tanzania iliyojijengea miaka ya nyuma katika soko la Kimataifa la Utalii.

8. Mheshimiwa Spika, biashara ya uwindaji imekuwa na changamoto nyingi sana zinazowakatisha tamaa wawekezaji. Ni biashara inayoelemewa na wingi wa kodi. Mfano, katika sekta hii ndogo ya Uwindaji kuna takribani tozo 21 za kodi kubwa kuachilia mbali zile za biashara ya utalii. Kodi zenyewe ni kama zifuatazo:

Jedwali 1: Mgao wa leseni, ada, kodi na tozo sekta ya uwindaji nchini
Aina ya Kodi Kiwango (USD) Kiwango (TZS) Muda
Tala A 5,000 11,000,000 Kwa mwaka
Tala B 1,000 2,200,000 Mwindaji Mtaalamu (Professional Hunter-PH)kwa Mwaka
Leseni ya Biashara 3,000 6,600,000 Kwa mwaka
Leseni ya PH 3,000 6,600,000 Kwa Mwaka
Kibali cha kazi 1,000 2,200,000 Kwa Mwaka
Kibali cha Ukazi A 2,050 4,510,000 Kwa kichwa kwa mwaka
Kibali cha Ukazi B 3,050 6,710,000 Kwa kichwa kwa Mwaka
Leseni ya Kuwinda 4,600 10,120,000 Kwa leseni ya mteja kwa kichwa
Category 1 60,000 132,000,000 Kwa mwaka
Category 11 30,000 66,000,000 Kwa Mwaka
Category 111 18,000 39,000,000 Kwa Mwaka
Category 1V 10,000 22,000,000 Kwa Mwaka
Category V 5,000 11,000,000 Kwa Mwaka
Observer Tax 100 220,000 Kwa siku
Hunter Conservation Tax 150 330,000 Kwa siku
Riffle Import permits 120 264,000 Per firearm on application
Trophy handling fee 500 1,100,000 On application
Mchango wa kijamii 5,000 11,000,000 Kwa kitalu kwa mwaka (Ni lazima)
Maombi ya kitalu ya mara nyingine (renewal) 5,000 11,000,000 Kwa kitalu (Non-refundable)
Ada ya kuhamisha kitalu 50,000 110,000,000 Kwa kitalu
Maombi ya kuhamisha kitalu 5,000 11,000,000 Kwa kitalu

9. Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuendelea kukaa na wadau hawa ili kujaribu kutatua changamoto hizo ambazo bado zinaikabili sekta hii ndogo ya uwindaji.

b) Biashara ya Usafirishaji Viumbe Hai Nje ya Nchi

10. Mheshimiwa Spika, tunakumbuka kwamba March, 2016 Serikali ilipiga marufuku usafirishaji wa viumbe hai nje ya nchi, ikitoa sababu kuwa inatengeneza mfumo ambao utaisaidia kudhibiti na kufuatilia kwa karibu biashara hiyo ya viumbe hai. Lakini katika upigaji marufuku huo Serikali haikutoa suluhu kwa wafanyabiashara ambao tayari walikuwa wameishakuwa na bidhaa hiyo tayari kwa usafirishaji na gharama za kuwatunza zitalipwa na nani.

11. Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa ahadi kwa wadu hao kwamba itarejesha tozo na gharama za wafanyabiashara wa viumbe hai ambao tayari walikwisha lipa ambazo hakutaja kiasi chake lakini ni mamilioni ya fedha, baada ya kumaliza zoezi la uhakiki. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata majibu ni kwanini hasa maamuzi ambayo mara nyingi yanapochukuliwa Serikali ndiyo inapata hasara zaidi na pale wahusika wanashindwa kurejeshewa fedha zao kwa wakati ili waweze kuwekeza katika mambo mengine ya kuwaingizia kipato?

12. Mheshimiwa Spika, kwa taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Naibu waziri wakati akiongea na wadau wa biashara hiyo kwamba, Serikali imepoteza kiasi cha shilingi trilioni 2.5 kama mapato yatokanayo na biashara ya usafirishaji wa viumbe hai kwa kipindi cha miaka miwili.

13. Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kufuta agizo lake la kuzuia biashara ya viumbe hai nje ya nchi na iwalipe fidia wafanyabiashara kwa hasara na usumbufu waliowasababishia wafanyabiashara hao.

Uhifadhima
III. MAMLAKA ZA HIFADHI
a) Shirika la Hifadhi za Taifa-TANAPA

14. Mheshimiwa Spika, taasisi za uhifadhi duniani hupatiwa ruzuku kutoka Serikali Kuu ili kujenga miundombinu na maendeleo mengine ya maeneo ya hifadhi, lakini kwetu sisi, TANAPA inajiendesha bila ya kutegemea ruzuku na pia inalazimika kulipa kodi serikalini. Kutokana na mfumo wetu wa kodi ambao badala ya kuipa unafuu TANAPA kutekeleza majukumu yake ya kimsingi unaifanya idhindwe kutimiza majukumu yake. Changamoto hizo za kikodi ni kama ifuatavyo:

Na. % Aina ya kodi inayolipwa
1. 30 Kodi ya makampuni-Corporate tax
2. 18 Kodi ya Ongezeko la thamani-Vat
3. 15 Gawio la Serikali- Hitaji la kisheria
4. 3 Kodi ya maendeleo ya ufundi-SDL
5. Kodi ya Stamp,kodi ya forodha(Import and excise duties
6. Kodi kwa maendeleo ya jamii-CSR
7. Kodi inayotozwa kwenye michango mbalimbali-Taxation on contribution

15. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa ni muda mwafaka sasa kuondoa au kupunguza viwango vya kodi za kisheria zinazopelekwa Serikalini,bodi ya utalii na taasisi za hifadhi na kodi inayokatwa kwenye michango inayogharamia miradi ya kijamii.

16. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi, TANAPA ilitoa kandarasi za miradi miwili mnamo tarehe 06 Mei, 2017 kwa mkandarasi JECCS Construction & Supplies Ltd na tarehe 09 Februari, 2017 na Mkandarasi Secao Builder Co Ltd. Gharama ya mikataba yote miwili ilikuwa ni Sh. milioni 961. Kipindi cha mkataba kwa miradi hii miwili kilimalizika tarehe 17 Februari, 2018 na 10 Oktoba 2017, mtawalia. Hata hivyo, hadi Februari 2019 yapata mwaka mmoja (1) kutoka tarehe iliyopangwa kukamilika, miradi hiyo haikuwa imekamilika. Ujenzi miradi yote miwili bado hadi sasa haijakamilika. Kadhalika, muda wa nyongeza pia ulikuwa umekwisha tangu tarehe 05 Novemba, 2018. Hakukuwa na juhudi zozote zilizofanywa na TANAPA ili kuhakikisha miradi hii inakamilika.

17. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali kutupa utekelezaji wa miradi hiyo na hatua ambazo zimeshachukuliwa kwa Mkandarasi huyo.

b) Mradi wa KFW – Serengeti

18. Mheshimiwa Spika, Tarehe 16 Desemba, 2013, Tanzania kupitia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), iliingia makubaliano ya kifedha na KFW na Frankfurt Zoology Society kwa ajili ya kuendeleza mazingira katika mbuga ya Serengeti na Ngorongoro. Gharama za mradi zilikadiriwa kuwa EUR za Ulaya milioni 24.12. KFW ilikubali kufadhili EUR za Ulaya milioni 20.5, wakati Frankfurt Zoological Society (FZS) ilikubali kufadhili EUR za Ulaya milioni 1, na zilizobaki EUR za Ulaya milioni 2.62 zifadhiliwe na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania. Muda wa mradi ulikadiriwa kuwa miaka mitano kutoka tarehe 11 Julai 2014.

19. Mheshimiwa Spika, Fedha hizi zilitarajia kujenga nyumba za watumishi, vituo vya watalii, mifereji ya maji, kuanzisha mpango wa matumizi ya ardhi vijijini, kurasimisha matumizi ya ardhi, kuanzisha mpango wa matumizi bora ya mali kwenye kanda, na kuanzisha jamii ya Wanyama pori na usimamizi bora wa misitu.

20. Mheshimiwa Spika, Pia, fedha hizo zilitarajia kujenga barabara za kimkakati za vijiji vya wilaya ya Serengeti na Ngorongoro, kusaidia mbuga ya Serengeti, programu ya kugawana faida na kusaidiwa jamii za vijijini, na kujenga miundombinu ya kiuchumi na kijamii. Walikubaliana kuwa kodi zote za serikali na tozo zingine zitagharamiwa na Serikali au Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania, na KFW ina haki ya kukataa kutoa fedha baada ya 30 Juni 2018 kama ilivyoonyeshwa kwenye mkataba wa makubaliano.

21. Mheshimiwa Spika, Mpaka kufikia Januari, 2019, miaka minne baadaye toka kuanza kwa mkataba tarehe 11 Julai, 2014 hamna kilichofanyika. Sababu za kuchelewa ni kwamba vitu vya ujenzi vilitakiwa visamehewe kodi wakati wa kuviingiza nchini kutoka nje. Hata hivyo, mpaka wakati wa ukaguzi Januari 2019, msamaha wa kodi ulikuwa haujakamilika.

22. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa Tanzania tunapoteza fursa nyingi kutokana na kuwapa uongozi/madaraka watendaji wasiokuwa na uwezo wa kibiashara na matokeo yake wao wanaangalia kidogo kilichopo lakini hawaoni kikubwa zaidi kinachokuja kesho au keshokutwa. Hili ni tatizo kubwa la watendaji wetu wa taasisi zinazohusika na utoaji wa vibali na ukusanyaji wa mapato. Kambi rasmi ya Upizani inaishauri Serikali kuzingatia uweledi na uwezo wa watendaji/wataal wanaopewa majukumu ya kaliba hii ili kutuvusha dimbwi la umaskini linalotukabili.

c) Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro

23. Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya hifadhi ya Bonde la Ngorongoro ni moja ya kivutio cha kimataifa katika utalii kutokana na binadamu kuishi pamoja na wanyama, hata hivyo kivutio hiki kiko kwenye hatari ya uharibifu wa mazingira kama hatua stahiki hazitachukuliwa kunusuru bonde mfano :-
 Kuongezeka kwa makazi ya binadamu ndani ya bonde hilo
 Kuongezeka kwa idadi ya mifugo
 Uvamizi na ukataji wa miti
 Kuzuiwa kwa njia za asili za wanyama
 Kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu
 Mahusiano mabaya kati ya jamii na watumishi wa hifadhi ya Ngorongoro.

24. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka serikali kuchukua hatua stahiki katika kunusuru hifadhi hii ya Bonde la Ngorongoro. Matumizi Mabaya ya pesa katika Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro. Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro ilifanya jumla ya vikao 20 na semina 6 kwa mwaka wa fedha 2017/18, ambapo jumla ya Sh. bilioni 1.10 (1,102, 907,602) zilitumika kama ilivyoainishwa hapa chini:

Mchanganuo wa gharama za vikao ulikuwa ni kama ifuatavyo:
 Posho ya kujikimu shilingi 799,906,220.00
 Hela kwa ajili ya mafuta shilingi 81,225,678.00
 Gharama za ukumbi shilingi 29,320,800.00
 Chakula na viburudisho shilingi 34,449,834.00
 Malazi shilingi 57,459,684 .00
 Gharama nyingine za usafiri shilingi 100,545,386.00

25. Mheshimiwa Spika, matumizi ya namna hii ya kuwakirimu wajumbe wa bodi, inaweza ikaleta tafsiri kuwa lengo la menejimenti ni kuwagiribu wajumbe wa bodi ili ishindwe kufanya/kutekeleza jukumu lake la msingi la kuisimamia menejimenti hiyo. Kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona litakuwa ni jambo la busara Waziri kuilekeza bodi ya bonde la Ngorongoro kuijitathmini na kuona kama bado inao uhalali wa kuendelea kuisimamia menejimenti.

d) Utalii katika Fukwe za Bahari

26. Mheshimiwa Spika, utalii wa fukwe ni mojawapo ya kivutio kikubwa sana kwa watalii ambao wengi wao wanatoka katika mataifa ambayo hayakupata bahati kuwa na fukwe, au kutokana na kubadilika sana kwa misimu ya majira ya mwaka.
27. Mheshimiwa Spika, katika hilo kuna visiwa ambavyo vinakodishwa na kumilikiwa na watu binafsi, moja ya visiwa hivyo ni kisiwa cha Shungumbili ambacho kwa sasa kinaitwa Thanda Island ambacho ni sehemu ya kisiwa kilicho ndani ya kisiwa kinachoitwa Nyororo, vyote vikiwa katika Wilaya ya Mafia/kisiwa cha Mafia. Kwa bahati mbaya sana kisiwa hiki cha Shungumbili au Thanda Island ambacho ni Private Island kina hotel ambayo ni ghali kuliko hotel yoyote ile Duniani, kwani kulala kwa siku ni dola za kimarekani 25,000. Mtu kukaa hapo ni lazima ukae kuanzia siku saba, jaribu kufikiria kwa mwaka kisiwa hicho au vingine kama vile visiwa vya;
i. Lupita (klilichopo Ziwa Tanganyika)
ii. Shungumbili/Thanda (Mafia)
iii. Mnemba (Zanzibar)
iv. Funjove
v. Bawe (Zanzibar)
vi. Changuu (Zanzibar)
vii. Chumbe Island (Zanzibar)

28. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitika kusema kuwa katika records za Wizara imeshindwa kupata taarifa za kisiwa hiki cha Shungumbili, na badala yake taarifa zake zinapatikana kutoka “the US military intelligence”, maana yake ni kwamba chochote kinachoendelea kwenye visiwa hivyo vya binafsi Serikali haina taarifa. Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuleta taarifa rasmi za visiwa hivyo vinavyo milikiwa na watu binafsi ili kuwa na taarifa kuhusu watalii wanaoingia katika nchi hii.

e) Mradi wa Theme Park Jijini Dar es Salaam

29. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 serikali ilitenga kiasi cha shilingi 250,000,000 (mil 250) kwa ajili ya upembuzi yakinifu ili kufanya Mji wa Dar es salaam kuwa Mji wa kitalii. katika hotuba ya Kambi ya Upinzani kwa Mwaka wa fedha 2016/2017 iliishauri serikali kutenga eneo la Msitu wa Pande kuwa sehemu ya Bustani ya Wanyamapori ili kupunguza gharama za kujenga eneo jingine litakaloweza kushabihiana na mazingira ya kuishi wanyama ikiwa ni pamoja na eneo la mazalia ya wanyamapori ndani ya Jiji la Dar es Slaam. Kwa mwaka wa fedha 2018/19 mradi huu ulitengewa jumla ya shilingi milioni 500. Lakini hadi mwezi februari 2019 haukuna hata senti iliyotolewa, na kwa mwaka wa fedha 2019/20 hakuna hata shilingi iliyotengwa kwa ajili ya mradi huu.

30. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuhakikisha inatoa fedha zilizotengwa, badala ya mfumo wa sasa unaotumiwa na baadhi ya wanasiasa wa kufanya matumizi ambayo hayajatengwa wala kuidhinishwa na Bunge jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Bajeti. Pamoja na hilo Kambi Rasmi inataka kujua uwepo wa taarifa ya mabasi yaliyonunuliwa kwa ajili ya kutoa huduma za kutembeza watalii katika vivutio mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam? Je, mabasi hayo yaliyonunuliwa ni sehemu ya mradi huu? Je, gharama yake ni shilingi ngapi? Na Je, mabasi hayo ni mangapi?

IV. MWENENDO WA SEKTA YA UTALII NCHINI

31. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa utalii ni hatua ya kujenga uchumi wa Tanzania kutokana na nchi kuwa na vivutio vya asili, utamaduni na kuwa kwenye jiografia ya kimkakati na hivyo kuwa na manufaa makubwa hata katika sekta nyingine za uchumi. Utalii unapanua fursa za ajira zenye kipato cha moja kwa moja au kwa shughuli nyingine zinazofungamana na utalii. Ili kufikia sekta ya utalii kuwa ya manufaa kwa nchi, ushirikishwaji wa sekta binafsi kutasaidia sana katika ujenzi wa miundombinu ya utalii wa kimataifa kwenye maeneo ya bahari, maziwa na misitu. Hivyo utalii utaboresha soko la bidhaa zinazozalishwa nchini, rejea kitabu cha sera cha Chadema uk 24 na 25.
a) Idadi ya Watalii Tanzania Bara na Zanzibar
32. Mheshimiwa Spika, kumekuwa na sintofahamu juu ya takwimu zinazotolewa juu ya idadi ya watalii wanaoingia nchini. Sintofahamu hii inatokana na idadi ya watalii ambayo imekuwa ikiripotiwa kwenye hotuba mbalimbali ikiwemo randama ya Wizara fungu 69. Katika Randama inazoonyesha kuwa kwa mwaka 2016 watalii walioingia nchini walikuwa 1,284,279 na kwa mwaka 2017 walikuwa ni takribani watalii 1,327,143 na kwa mwaka 2018 kufikia 1,494,596. Ripoti hizi zimebainisha kuwa watalii hao waliokuja kutembelea hifadhi za taifa, mamlaka za hifadhi za Ngorongoro na Zanzibar. Hii ina maana kwamba watalii walioingia kutoa Zanzibar nao wamejumuishwa katika idadi ya Watalii wote walioingia nchini kwa mujibu wa maelezo ya Randama.

33. Mheshimiwa Spika sote tunatambua kuwa masuala ya sekta ya utalii sio masuala ya Muungano. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ituambie ni lini hasa imeamua mambo ya utalii kuwa sehemu ya Muungano pia tunaitaka serikali itupe takwimu sahihi za watalii wanaoingia nchini kwa maana ya Tanzania Bara.

34. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano, katika kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa endelevu na yenye tija kwa taifa, ikiwa ni pamoja na kuongeza namba ya watalii wanaoingia Tanzania kutoka 1,200,000 mwaka 2016/17 hadi 2,000,000
ifikapo mwaka 2020. Kwa mujibu wa Taarifa ya Wizara ya Utalii na Wanyama Pori ya Kenya, juu ya utendaji wa sekta ya Utalii iliyotolewa mwaka 2018 ni kuwa nchi hiyo kwa mwaka 2017 iliingiza watalii 1,474,671 na mwaka 2018 iliingiza watalii 2,025,206. Wakati huo huo vitanda kwa ajili ya watalii vikiongezeka kutikia milioni 4.05 mwaka 2018 kulinganisha na milioni 3.5 mwaka 2016.

35. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali badala ya kutafuta mchawi itafakari takwimu hizi za washindani wetu na tuje na mkakati wa kuboresha sekta ya utalii katika karne ya 21 ili tuweze kushindana na jirani zetu kwa kuongeza idadi ya watalii na fedha za kigeni.

b) Demokrasia na Ukuaji wa Sekta ya Utalii

36. Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya mwaka 2016/2017 ilitolea mfano wa nchi ya Sri Lanka. Katika gazeti la New York Times, nchi kama Srilanka iliwahi kupata hadhi ya kujulikana kama nchi ya kwanza duniani kwa kivutio cha watalii. Lakini kukandamizwa kwa demokrasia na misukosuko ya kisiasa nchini Sri Lanka kama inavyotokea Tanzania leo ilipelekea utalii wa nchi hiyo kushuka kwa kasi ya asilimia 43 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuanguka kabisa kwa uchumi wa nchi hiyo.Hivyo, kuanza kusuasa kwa sekta hii ya utalii ni dalili mbaya na isipoangaliwa inaweza kutupeleka katika kile kilichotokea Srilanka.

37. Mheshimiwa Spika, katika taarifa za kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Utalii ambayo imetolea mfano wa nchi kama Botswana ambayo imekuwa na tozo la VAT katika huduma za kitalii kwa sasa wameongeza VAT kutoka 14 % kwenda 15 % kama mfano wa nchi Barani Afrika zenye mfumo wa VAT , ni vyema serikali hii ikatambua kuwa pamoja na tozo ya VAT kwenye utalii nchini Botswana bado kiwango hicho haijafikia ukubwa wa tozo kama tozo ya 18 % kama ilivyo kwa Tanzania kwa sasa. Vilevile, ikumbukwe kuwa nchi ya Botswana imepunguza mrundikano wa kodi tofauti na Tanzania yenye takribani kodi 36 kwenye sekta ya utalii pekee. Ukiwa ndio nchi inayoongoza kwa wingi wa kodi katika biashara ya utalii Afrika ya Mashariki. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kurejea tozo hii ya VAT kwenye huduma za utalii

c) Sheria Zinazoendesha Sekta ya Maliasili na Utalii

38. Mheshimiwa Spika, Sera haiwezi kusimama peke yake wakati inatungwa, ni lazima iangalie sera zingine zinasemaje ili kuondoa mwingiliano wa kiutendaji katika kufikia malengo ya sera. Vivo hivyo pia katika utunzi wa sheria, na sheria nzuri inayotoa matunda bora ni lazima vitu vyote vimalizikie kwenye ofisi moja, “one stop center”.

39. Mheshimiwa Spika, katika sekta ya maliasili na utalii inaongozwa na sheria na kanuni zipatazo 13, na vyote hivi vinafanyakazi kwa wakati mmoja na mdau wa utalii ni lazima aendane na matakwa ya sheria hizo na kanuni zake. Uwepo wa sheria na kanuni zipatazo 13 umepelekea ukiritimba uliopitiliza. Mbali ya ukiritimba pia vifungu vya sheria hizo vinakinzana na hivyo kusababisha wadau wa utalii kushindwa kufikia malengo yao.

40. Mheshimiwa Spika, miongoni mwa sheria hizo ambazo vifungu vyake vinakinzana sana na kuleta sintofahamu ni sheria ya ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 na sheria ya wanayapori namba 5 ya mwaka 2009; kanuni na sheria ya wanyapori (wildlife corridors,Dispersal Area, buffer zones and Migratory routes regulations 2018) na sheria ya ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999); Kanuni na sheria ya wanyamapori za mwaka 2018 na sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009; Sheria ya Nyanda za Malisho ya mwaka 2010 na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kwamba, sheria na kanuni zote zinazokinzana ili kuleta utengamano mzuri wa kisheria kwa manufaa na maendeleo ya sekta nzima ya maliasili na utalii.

V. MIGOGORO SUGU BAINA YA SERIKALI NA WANANCHI WANAOISHI KANDO YA HIFADHI

41. Mheshimiwa Spika, tumekuwa na tatizo sugu la migogoro baina ya serikali na wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi kwa muda mrefu sasa. Pamoja na jitihada mbalimbali za kuizungumzia na kushauri hatua stahiki za kuitatua bado hali inaonyesha migogoro hii imekuwa na nguvu kubwa kuliko uwezo wa serikali kuitatua.

42. Mheshimiwa Spika, migogoro hii imedumu muda mrefu ambapo imegharimu maisha ya wananchi wengi, tumepoteza wanyama ambao ndio fahari yetu na chanzo cha mapato, migogoro hii imesababisha kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na wanyamapori, mifugo na hivyo kuathiri afya za binadamu na wanyama wa kufugwa na wale wa porini. Mheshimiwa Spika, Mifano iliyotolewa ni pamoja na maeneo ya Wilaya ya Bunda yanayopanaka na Pori la Akiba la Grumeti, vijiji vya Kegonga na Masanga, pia maeneo ya Ulanga vijiji vya Iputi na Lupiro yakiwa ni baadhi tu ya maeneo ambayo migogoro imesababishwa na Mamlaka za Wanyamapori.

43. Mheshimiwa Spika, serikali imekuwa ikiwakumbatia baadhi ya wawekezaji ambao wamekuwa chanzo au sehemu ya migogoro sugu ya wanavijiji wanaoishi maeneo ya hifadhi. Mfano, katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 ilizungumzia kwa kina sana Historia ya mgogoro wa Loliondo uliodumu kwa takribani miaka 26. Mgogoro huu uliwahi kuundiwa kamati mbalimbali ili kutafuta suluhu lakini mpaka leo serikali imegoma kurudisha mrejesho kwa wananchi kujua kinagaubaga na hatua mahususi zilizopendekezwa. Ni wazi kuwa migogoro mingi imeendelea kuwepo kutokana na ripoti nyingi kuwa za siri na wananchi kutoshirikishwa ipasavyo katika maamuzi. Jamii pia inapaswa kujua mambo yaliyo katika ripoti hizo na hatua stahiki zitakazochukuliwa. Mara nyingi tumeshuhudia ripoti nyingi zikiwa zimeghubikwa na usiri mkubwa na hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kujua yale yaliyo ndani ya ripoti hizo za kamati huku fedha nyingi zikitumika katika uchunguzi.

44. Mheshimiwa Spika ripoti hufanywa kuwa mali ya watu wachache badala ya mali ya umma. Mfano, katika ripoti mbalimbali za serikali, mashirika na taasisi binafsi pamoja na hotuba mbalimbali za Kambi Rasmi ya Upinzani zimezungumzia kwa kina watuhumiwa wakubwa wa mgogoro wa Loliondo ambapo kampuni ya Otterlo Business Corporation (OBC) ambayo imetuhumiwa kwa muda mrefu kuwa sehemu kubwa ya chanzo cha mgogoro katika Bonde Tengefu la Loliondo mpaka sasa haijatatuliwa kutokana na wananchi wa maeneo hayo kutoridhishwa. Kampuni ya Greenmile Co.Ltd imekuwa na kashfa nyingi na kuwa sehemu ya migogoro,kampuni ya Thomson Safaris imekuwa ikituhumiwa kama sehemu kuu ya mgogoro katika vijiji vilivyo ndani ya hifadhi ya Serengeti n.k

45. Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza bado serikali haijaweza kuziwajibisha kampuni hizi. Hii ni mifano midogo tu kati ya migogoro mingi inayoendelea nchini ambapo serikali imeshindwa kuja na majibu na mikakati ya kudumu jambo ambalo linazua shaka kubwa na ari ya kutaka kujua ni nani hasa mnufaika wa migogoro ya namna hii? Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuhakikisha inaweka wazi ripoti zote za kamati maalum za zilizowahi kushughulikia migogoro hii, ili kutoa fursa kwa wawakilishi wa wananchi kujadili kwa uwazi ripoti hizo na hata kutoa mapendekezo.

VI. UHARIBIFU WA MAZINGIRA KATIKA HIFADHI

46. Mheshimiwa Spika, suala la utunzaji wa mazingira ni muhimu sana kwa ikolojia ya misitu,bahari, mbuga zetu kwani uwepo wa maji, hali nzuri ya hewa na udongo vinapekea mimea na wanyama kuzaliana na kuwa katika hali bora zaidi.

47. Mheshimiwa Spika, Kilombero and Lower Rufiji Wetlands Ecosystem Management mradi namba 4809 ambao ni mradi wa kuendeleza ekolojia ya ardhi oevu ya bonde la kilombero na mto Rufiji, ambao unaendelezwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Ubelgiji. Kwa mwaka wa fedha 2018/19 ulitengewa jumla ya shilingi 1,494,193,471. Lakini hadi mwezi februari 2019 hakuna hata shilingi moja ambayo ilikuwa imekwenda katika mradi huo.

48. Mheshimiwa Spika, umuhimu wa ekolojia ya bonde la Kilombero na mto Rufiji ni muhimu sana kwa sasa kutokana na ukweli kwamba utekelezwaji wa mradi wa ufuaji wa umeme ni kuwa utaleta hasara kwa mazingira kwa kusababisha uharibifu mkubwa wa misituna hivyo kuondoa mazalia ya wanyama na ndege wengi ambao walikuwa wanaleta utofauti mkubwa na wa kipekee wa mbuga ya Selou

49. Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha na fedheha kubwa kwa serikali hii ya awamu ya tano kuwa mstari wa mbele katika kuyafuta yale mazuri tuliyoyaridhia kama taifa ili kulinda mazingira ya sasa na ya vizazi vijavyo. Nayasema haya kwa kuwa serikali hii ya awamu ya tano mapema mwaka jana ilifanya upembuzi katika kile walichokisema ni mpango wa serikali wa kuanzisha mradi mkubwa wa kuzalisha nishati ya umeme yaani Stiegler’s Gorge katika pori la akiba la Selous kwa bei nafuu.

50. Mheshimiwa Spika, hakuna mtu yoyote mwenye akili timamu asiyejua umuhimu wa Pori la Akiba la Selous na umuhimu wa kuilinda kwa wivu mkubwa ikolojia ya eneo hilo ambalo kwa kupitia mto Rufiji imekuwa ni chanzo kikubwa cha maji yanayotegemwa na binadamu, mimea, wanyamapori, samaki na mifugo. Pamoja na serikali kusema imefanya upembuzi yakinifu, ni vyema ikaamua kufanya mkakati wa tathimini ya mazingira kwa miaka mingi ijayo.

51. Mheshimiwa Spika, endapo chanzo hiki cha maji kitaharibiwa basi tujue hata umeme unaotaka kuzalishwa hautakuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo. Tunatambua umuhimu mkubwa wa upatikaji wa nishati ya umeme nchini , lakini serikali hii ya awamu ya tano itambue umuhimu mkubwa wa kuhifadhi vyanzo vya maji hususani chanzo hiki muhimu kwani bila maji hakuna uhai, bila maji hakuna umeme, bila maji hakuna chakula.

52. Mheshimiwa Spika, bado nchi yetu ina namna nyingi ya kuzalisha umeme katika maeneo mengi ambayo athari zake za kimazingira sio makubwa kama itakavyotokea kwenye chanzo hiki cha mto Rufiji. Pori la Akiba la Selous limekuwa chanzo kikubwa cha mapato ya wananchi na ajira kutokana na utalii wa Southern Circuit. Mpaka sasa Pori hili limeorodheshwa katika maliasili zilizo hatarini kupotea kwa mujibu wamkataba wa Urithi wa Dunia kutokana na kuongezeka kwa mauaji ya tembo na kuharibika kwa mapitio ya wanyama. Na endapo mradi huu utalazimishwa kufanyika basi tutambue athari kubwa ya kimazingira huko mbeleni napengine kuweka kabisa kwa pori hili kwani uendeshaji wa mitambi hiyo ya umeme unaotumia maji husababisha joto la maji jambo ambalo ni hatari kwa baionuai .

53. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuangalia upya mikakati ya kimazingira ya muda mrefu kabla ya kuanza kwa mradi huu. Serikali ikumbuke makosa makubwa iliyofanya katika kujenga mradi wa stesheni ya mabasi yaendayo kwa kasi (DART) ambao kwa sasa inaigharimu serikali kutokana tu na kufanya miradi ya namna hii bila kuangalia athari za muda mrefu za kimazingira.

54. Mheshimiwa Spika, kauli ya Mheshimiwa Rais kuhusu kuwaacha wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi kama walikuwa wanafanya shughuli zao za kutafuta riziki kuendelea kufanya hivyo na wasisumbuliwe, je kauli hiyo ya Mheshimiwa Rais hadi sasa Wizara imeishaiwekea utaratibu gani wa kuitekeleza ili iwe ya kisheria badala ya kuwa kauli ya kisiasa kama kauli zingine zinazoongewa katika harakati za kutafuta kuungwa mkono na kundi Fulani katika jamii?

VII. MISITU NA NYUKI
55. Mheshimiwa Spika, sekta ya ufugaji wa nyuki imekuwa haifanyi vizuri kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokupewa kipaumbele ipasavyo. Miradi mingi inayoanzishwa na serikali imekuwa haifanyi vizuri na mingi imeshindwa kuendelea kutokana na utunzaji mbovu na kutofuatilia mara kwa mara.

56. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya CAG 2016/2017 serikali ilitoa kiasi cha shilingi 104,072,000 (mil. 104) kwa wafugaji 7 kwa kipindi cha miaka miwili lakini cha kushangaza mizinga mingi haina nyuki na miradi hiyo imesimama. Mfano, katika mizinga 150 iliyowekwa Manispaa ya Dodoma ni mizinga 7 tu yenye nyuki, katika halmashauri ya Kishapu mizinga 150 imewekwa mahali ambapo sio mazingira sahihi kwa mazalia ya nyuki na hivyo hakuna nyuki. Mradi huu wa Kishapu umegharimu takribani milioni 40. Katika halmashauri ya Misungwi kati ya mizinga 150 ni mizinga 14 tu ndio ilikuwa na nyuki kwa kipindi cha miaka miwili hivyo mizinga 136 haikuwa na nyuki huku mradi ukigharimu takribani shilingi milioni 20. Hii ni baadhi tu ya mifano mingine mingi ambapo fedha nyingi hutumika huku matokeo yakikosa tija kabisa.

57. Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni hatua gani stahiki zimechukuliwa kwa uzembe huu mkubwa wa upotevu wa fedha za umma katika miradi inayogharimu mamilioni bila kuwa na faida yoyote.

58. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2018/19 idara iliomba fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi minne na mwaka wa fedha 2019/20 miradi hiyo hiyo inaombewa fedha, ambayo ni; i. mradi wa misitu asili ulioomba kutekelezwa kwa shilingi 1,364,097,000.00 lakini hadi mwezi februari,2019 shilingi 100,100,000.00 ndizo zilizokuwa zimetolewa. Kwa mwaka wa fedha 2019/20 mradi unaombewa jumla ya shilingi 3,136,480,000.00 fedha za nje. ii. Mradi kuendeleza misitu na ufugaji wa nyuki unaoombewa shilingi 200,000,000.00 fedha za ndani. iii. mradi wa kuongeza thamani kwa mazao ya misitu 2019/20 unaombewa shilingi 4,742,850,000.00. kwa mwaka 2018/19 ziliidhinishwa shilingi 5,950,860,993.00 lakini hadi mwezi februari, 2019 zilipokelewa shilingi 868,341,377.00 tu sawa na asilimia 14.59 na hizi zote ni fedha za nje.

VIII. UTEKELEZAJI WA BAJET 2018/19 NA MPANGO WA MAENDELEO 2019/2020
59. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya Wizara kwa Mwaka wa fedha 2016/2017 sekta ya utalii ilichangia 17.5 % ya pato la taifa (GDP) na takribani 25 % ya fedha za kigeni (foreign currency). Hii ikiwa ni kati ya sekta tano muhimu zinazichangia zaidi katika pato la taifa.

60. Mheshimiwa Spika, takwimu za serikali zinaonyesha sekta hii ya utalii hutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 500,000 na zisizo za moja kwa moja 1,000,000 . Pamoja na hilo, sekta hii ya utalii imekuwa ikichangia katika kukuza kipato cha wananchi mmoja mmoja kutokana na manunuzi ya bidhaa katika hoteli zikiwemo vyakula, huduma za samani, vifaa vya ujenzi na malazi.

61. Mheshimiwa Spika, pamoja na kuona umuhimu huu wa sekta ya utalii na mifano ya nchi mbalimbali wanavyonufaika katika utalii wa aina tofauti tofauti bado hapa nchini kwenye sekta hii imekuwa ikisuasua na kutegemea wahisani katika miradi mbalimbali ya maendeleo hususani World Bank, WWF, Belgium, German, Norway na Finland.

62. Mheshimiwa Spika, katika kuonesha kuwa Serikali haipo makini katika kuinua uchumi wa nchi, kwa kutumia sekta hii ya utalii ili kuiingizia fedha nyingi za kigeni na kuzalisha ajira nyingi. Mwaka wa fedha 2018/19 zilitengwa jumla ya shilingi 7,330,006,404 kwa ajili ya matumizi ya idara, bodi ya utalii na wakala wa chuo cha Taifa cha utalii lakini hadi mwezi februari 2019 zilitolewa jumla ya shilingi 3,615,157,217.01 ambazo ni sawa na asilimia 50.68

63. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Randama ya Wizara Fungu 69 ya Mwaka 2016/2017 fedha za miradi ya Maendeleo zilijumuisha 15,746,682,000 fedha za ndani na 2,000,000,000 fedha za nje. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 fedha za ndani zilizotolewa zilikuwa shilingi 11,353,250,489 na fedha za nje ni shilingi 16,593,530,813 hii ikiwa na maana fedha za ndani zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapungua.

64. Mheshimiwa Spika, makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 zilitengwa shilingi 29,978,082,000 kati ya fedha hizo za ndani ni shilingi 3,000,000,000 na fedha za nje ni shilingi 26,978,082,000 ambazo ni sawa na asilimia 89.99 ya fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya maendeleo. Hadi kufika mwezi februari 2019 fedha zilizopokelewa ni shilingi 10,551,289,825 fedha za nje na sawa na asilimia 35 ya fedha zote za wizara, kwa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Hakuna hata shilingi moja ya fedha za ndani zilizotolewa kwa ajili ya kuendeleza sekta ya utalii hadi mwezi februari.

65. Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2019/20 wizara imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 48.9 ili kutekeleza miradi minane ya maendeleo, kati ya fedha hizo fedha za ndani ni shilingi bilioni moja tu na fedha za nje ni shilingi bilioni 47.9

66. Mheshimiwa Spika, hili ni tishio kubwa kwa Wizara kwani kuzidi kutegemea misaada kutoka kwa wahisani hakuwezi kamwe kunyanyua sekta hii. Hii inaonesha kuwa bado serikali haijakubali kuwekeza ipasavyo kaika sekta hii. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali ione umuhimu wa kuwekeza katika sekta hii nyeti ambayo inauwezo wa kutoa ajira zaidi, kuongeza pato la Taifa na fedha kuongeza fedha za kigeni.

IX. HITIMISHO
67. Mheshimiwa Spika, nashauri sote tutafute makala iliyoandikwa na Yende Nsizwazonke kutoka Africa Kusini inayosema “Natural resources: Are we blessed with a curse or cursed with a blessings? Maneno haya mazito yanaonyesha dhahiri tunahitaji taasisi imara (Strong institutions) ambapo mifumo ya utendaji kazi ndani ya Wizara inakuwa imara katika utendaji na sio kila wakati anapopewa nafasi kiongozi fulani hubadili sera na taratibu kwa kufuata matakwa yake binafsi. Kujenga taasisi zenye mifumo imara itasaidia kuvutia wawekezaji wengi zaidi, itapanua soko la utalii ndani na nje ya nchi, mapato ya ndani yataongezeka na hivyo tutakuwa tumepanua wigo wa fedha nyingi zaidi katika miradi ya maendeleo nchini.

68. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.

…………………………
Mch. Peter Simon Msigwa (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI-
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
23/05/2019

Share Button