HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHESHIMIWA PASCAL YOHANA HAONGA (MB) WIZARA YA KILIMO, KUHUSU UTEKELEZAJI MPANGO WA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA 2018/2019 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2019/20
(Inatolewa chini ya Kanuni 99(9) ya Kanuni za Bunge Toleo la mwaka 2016)
A. UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu na afya kuweza kusimama mbele ya adhira hii ili kutoa Maoni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Kilimo, kwa mwaka 2018/19 na Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2019/20.

2. Mheshimiwa Spika, nawashukuru wananchi wa Jimbo la Mbozi kwa kuendelea kuniamini na kuniunga mkono mimi na chama change wakati wote ninapoendelea kuwatumikia licha ya changamoto mbalimbali za kisiasa ninazopitia. Kikubwa waelewe kwamba ili dhahabu ing’ae lazima ipitie kwenye moto. Pia waamini kwamba siyo kila changamoto ninayoipitia lengo lake ni kunidhoofisha bali nyingine zinanijenga /kuniimarisha zaidi.

3. Mheshimiwa Spika, nitoepole na pongezi kwa Mheshimiwa Freeman Mbowe, Esther Matiko na wapiganaji wengine kwa magumu wanayopitia, kitu kikubwa ni kuwa waelewe kwamba gereza au mahabusu siyo kaburi.

B. HALI YA CHAKULA KWA MSIMU UJAO WA KILIMO
4. Mheshimimwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa hali ya upatikanaji wa chakula kwa misimu miwili ya 2017/18 ilikuwa ni yenye kutia matumiani sana kwani uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2017/18 ulifikia tani 16,981,974 na mahitaji ya chakula kwa msimu 2018/19 yalikuwa ni tani 13,569,285 na hivyo kuwa na ziada ya tani 3,322,689. Kwa msimu huu wa 2018/19 ni dhahiri dalili zimeanza kuonekana mapema kuwa kutakuwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na kwamba; mbali na mabadiliko ya Tabianchi ambayo yameiikumba mikoa ya Kanda ya Kati yenye mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, Kanda ya Magharibi(Tabora, Katavi na Kigoma) Kanda ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Manyara na Arusha). Lakini kanda ambayo ni mzalishaji mkubwa wa nafaka hasa mahindi (Songea, Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa na Katavi) mvua haikuwa tatizo ila tatizo ni upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na kukosekana kwa soko la kutoa bei nzuri ya mahindi na hivyo kusababisha hasara kubwa kwa wakulima katika msimu uliopita, jambo hilo litasababisha kupungua kwa uzalishaji wa Mahindi kwa msimu huu wa kilimo. Kimsngi bei nzuri ya soko la bidhaa za mkulima na wepesi wa kuuza bidhaa zao nikichocheo kikubwa kwa wakulima kuendelea kuwekeza kuzalisha bidhaa kwaajili ya jamii ya watanzania na kuuza nje ya nchi ili Tanzania iweze kupata fedha za kigeni.
5. Mheshimiwa Spika, aidha, kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameikumba mikoa mingi hapa nchi na hivyo majira ya mvua kubadilika sana na hivyo kusababisha mimea mingi kuharibika kabla ya kufika wakati wa kuvunwa, ni wazi kuwa mkakati tofauti unahitajika ili kuendelea kukidhi mahitaji ya chakula, na Zaidi kufikia soko la bidhaa za kilimo kwenye ukanda wa Afrika Mashariki (Eastern Africa) na Ukanda wa Kusini mwa Afrika (Southern Africa).

6. Mheshimiwa Spika, hivyo basi kwa mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi ambayo inategemea sana kilimo cha mahindi,Karanga, mpunga,mhogo,maharage,kunde,choroko na ufuta. Mkoa huu huzalisha Mihogo, maharage,mahindi na mpunga kama mazao ya chakula pia Michikichi na pamba kama mazao ya biashara.

7. Mheshimiwa Spika, Kwa kawaida katika ukanda wa kati mvua huanza mwezi Novemba hadi mwezi Machi/Aprili. Hali ni tofauti sana kwa mwaka huu kwa kuwa mvua zilianza kunyesha mwezi Desemba haikuchukua muda kukoma hivyo kuwaacha wakulima wakiwa wamepanda kidogo mno. Hali ya ukame iliindelea katika mwezi Januari, Februari hadi mwezi Machi na hivyo kusababisha kukauka kwa mazao yaliyokuwa yamekwisha kupandwa mashambani pia ikumbukwe pia kuwa mikoa hiyo uzalisha malisho kwa ajili ya mifugo.

8. Mheshimiwa Spika,Kutokana na ukame wa mvua hadi mwezi machi, 2019 umepelekea maeneo ya wilaya za Mkoa wa Tabora kwa upande wa mpunga, majaruba ya mpunga kubaki yakiwa hayajapandwa kutokana na kukosekana kwa Maji. Vivyo hivyo kwa mikoa mingine ya nchi, hivyo uzalishaji hafifu kutokana na hali ya hewa ya kutoridhisha, kunaleta tishio kubwa la upungufu wa chakula katika maeneo mengi ya nchi hii.

9. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitahadharisha Serikali kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na akiba ya chakula ya kutosha na inachukua hatua stahiki kupunguza madhara yanayoweza kutokana na hali hii ya ukame ambayo imekikumba kilimo kwa msimu 2018/19.

C. UMUHIMU WA SEKTA YA KILIMO-(MAZAO)
10. Mheshimiwa Spika, Uwezo wa kilimo na biashara ya kilimo ni mkubwa sana kwa Tanzania, lakini matarajio lazima yawekwe inavyostahili. Sehemu kubwa ya sekta hii kwa sasa haina uwezo wa kushindana kwa sababu ya gharama kubwa za uzalishaji, hamasa ndogo miongoni mwa wazalishaji kutokana na muingiliano wa serikali hasa kwenye soko, ubora hafifu wa pembejeo, pamoja na ukosefu wa wagani wa kutosha wenye hamasa,ari ya kazi, weledi na kiunganifu hafifu kati ya watafiti na wakulima.
11. Mheshimiwa Spika, Uzalishaji wa mboga na matunda yenye thamani kubwa, hata hivyo, inaonekana kama ni fursa halisi, kwani iko juu katika orodha iliyoandaliwa na zana zote za uchambuzi zilizotumika katika utafiti wakutambua fura zilizopo na ambazo hazijatumika. Sekta ndogo hii ya uzalishaji wa mboga na matunda imefanya vizuri katika miaka ya karibuni kwa kuzingatia mahitaji yanayokua katika masoko ya ndani, nchi jirani na kimataifa .
12. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa kilimo ndiyo sekta kiongozi au ndio muhimili mkuu katika uchumi wa nchi yetu. Sekta hii inachangia takriban asilimia 25.3 ya Pato la Taifa (GDP), asilimia 30 ya mauzo ya nje; na asilimia 65 malighafi ya viwanda vyetu vya ndani. Aidha, takwimu zinaonesha kuwa sekta ya kilimo kilitoa ajira kwa takriban wastani wa 85%, 75% na 65.5% kwa mwaka 2001, 2006 na 2016 mtawalaia , wakati huo viwanda na sekta za utoaji wa huduma kwa kipindi hicho hicho ajira zilikuwa ni 3%, 5%, 6%; na 15%, 20%, 27% kwa mtawalia. Pia kwa asilimia hizo za waajiriwa katika sekta ya kilimo, kati yao asilimia 53 ya nguvu kazi yote ni wanawake. Aidha takwimu zinaonesha zaidi kuwa asilimia 80 ya watu masikini wanategemea kuedesha maisha yao kupitia kilimo.

13. Mheshimiwa Spika, Japokuwa Kilimo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu kwa ushahidi huo, lakini serikali bado haijaweka juhudi kuhakikisha kuwa kilimo kinachangia zaidi na zaidi katika uchumi. Hoja hii inajionesha wazi kutokana na takwimu za ukuaji wa sekta ya kilimo zinavyozidi kushuka kila mwaka ambapo wastani wa ukuaji kwa mwaka 2014 ilikuwa ni asilimia 3.4; 2.3 kwa mwaka 2015 na kwa mwaka 2017 wastani wa ukuaji ukawa 3.1, wastani wa ukuaji huu ni wa chini zaidi kulinganisha na wastani wa kiwango cha azimio la Malabo/CAADP wa 6%. Sambamba na hilo uwekezaji katika sekta ya kilimo umekuwa ukishuka vile vile, Bajeti iliyotengwa kwa kilimo kwa kulinganisha na Bajeti nzima ya Serikali kwa mwaka 2012 ilikuwa ni asilimia 7.2 ikashuka hadi asilimia 4.7 kwa mwaka 2017, kiwango ambacho ni chini ya asilimia 10 ya makubaliano ya Malabo/CAADP.
14. Mheshimiwa Spika, takwimu hizi zinaonesha kuwa kama Serikali itaamua kwa dhati kuwekeza katika sekta ya kilimo ni dhahiri mabadiliko makubwa ya uchumi wa Tanzania sambamba na watanzania tutaondokana na umasikini wa kipato uliokithiri kwa miaka nenda rudi.
15. Mheshimiwa Spika,Ukuaji wa uchumi wetu umejikita katika wastani wa asilimia 6 kwa mwaka, ambapo ukuaji wa pato la nchi ni asilimia 7 toka mwaka 2013. Wachumi wabobezi wanasema kuwa ukuaji wa uchumi ungekuwa ni zaidi ya hapo kama Sekta ya kilimo ingekuwa kwa wastani wa asilimia 6 kama kiwango cha uwekezaji wa asilimia 10 cha azimio la Malabo/CAADP kingezingatiwa, na hivyo uchumi ungekuwa kwa asilimia 8 – 10 kwa mwaka na nchi ingefikia lengo lake la kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa mwaka 2025.
16. Mheshimiwa Spika, uwekezaji kwenye kilimo unajikita kwenye asilimia 4.7 ya jumla ya bajeti kuu ya taifa kwa mwaka 2017/18 kwa kulinganisha na asilimia 7.8 kwa mwaka 2010/11 kiwango cha chini pia kwa kulinganisha na makubaliano ya asilimia 10 ya wakuu wa nchi za SADC kule Malabo. Pia Tanzania ilitoa asilimia 0.29% mwaka 2014 na 0.19% mwaka 2016 kama sehemu ya Mchango wa Kilimo kwenye GDP katika kuwekeza kwenye (R&D) utafiti na maendeleo ya kilimo kulinganisha na makubaliano ya asilimia 1 kwa kila nchi za NEPAD na UN kwa nchi zinazoendelea.
17. Mheshimiwa Spika, pamoja na azimio hilo, Tanzania bado imeshindwa kutekeleza. Takwimu zinaonyesha kwamba; kwa miaka miwili 2015 na 2016 ukuaji wa kilimo nchini Tanzania ulikuwa ni 2.3% na 1.7% mtawalia
18. Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2007/2008 – 2016/2017 Kilimo na Ushirika (Fungu 43) imepata wastani wa shilingi bilioni 250 ambayo ni sawa na 1.8% tu ya bajeti ya taifa. Kati ya wastani huo, bajeti ya maendeleo ilipata wastani wa shilingi bilioni 80.3 ambayo ni sawa na 32% tu ya bajeti ya kilimo na ushirika na 1.6% ya bajeti ya maendeleo taifa.
19. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha kuwa Wizara ya Kilimo kupitia fungu 43 kwa mwaka wa fedha 2015/16 ilitengewa jumla ya Shilingi 206,816,421,000/-. Kati ya fedha hizo, Shilingi 174,103,348,000/- zilikuwa ni fedha za matumizi ya kawaida na Shilingi 32,713,073,000/- ni fedha za maendeleo. Hadi mwaka huo wa fedha unamalizika Wizara ilipokea shilingi 2,663,428,542/- kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikiwa ni fedha za ndani na shilingi 5,035,062,321/- zikiwa ni fedha za nje, na hivyo kufanya jumla ya fedha za maendeleo kwa fungu 43 zilizopokelewa kwa mwaka 2015/16 kuwa shilingi 7,698,490,863/- sawa na asilimia 23.53 ya fedha za maendeleo zilizopitishwa na Bunge.

20. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/17 Fungu 43 lilitengewa jumla ya Shilingi 210,359,133,000 ziliombwa. Kati ya fedha hizo, Shilingi 100,527,497,000 zilikuwa ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Fedha za ndani zilikuwa shilingi 23,000,000,000/- na fedha za nje shilingi 78,527,497,000/- Hadi kufikia mwezi Machi, 2017 fedha zilizokuwa zimetolewa ni shilingi 2,251,881,250/- sawa na asilimia 2.22 tu na kati ya fedha hizo fedha za ndani zilikuwa shilingi 1,382,191,924/- na fedha za nje shilingi 349,081,000/-

21. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/18 wizara fungu 43 iliombakuidhinishiwa jumla ya shilingi 214,815,759,000/- kati ya fedha hizo shilingi 150,253,000,000/- ni fedha za maendeleo, lakini hadi mwezi Machi 1, 2018; shilingi 16,520,540,444/- zimetolewa ambazo ni sawa na asilimia 11 ya fedha zilizoidhinishwa.

22. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 wizara fungu 43 iliombewa jumla ya shilingi 162,224,814,000/- kati ya fedha hizo shilingi 64,105,298,000/- ni fedha za miradi ya maendeleo.

23. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2016/17, sehemu ya Kilimo kifungu cha 3.2.3.3 kinaonesha kuwa; “Lengo ni kuhakikisha uwepo wa chakula cha kutosha na upatikanaji wa uhakika wa malighafi za uzalishaji katika viwanda vya mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi.

24. Mheshimiwa Spika, ufinyu wa bajeti ya maendeleo inayoenda kwenye kilimo fungu 43 ni dhahiri kwamba dhamira ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano kama ilivyonukuliwa hapa juu haiwezi kufikiwa hata kwa robo yake. Hii ni kutokana na mwenendo wa utoaji wa fedha za maendeleo kwa ajili ya miradi ya kilimo kulingana na bajeti zinazokuwa zimeidhinishwa na Bunge.

25. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa wito kwa Serikali kuheshimu ahadi yake ya kutenga walau asilimia 10 ya bajeti yake kwa sekta ya kilimo kama inavyoonekana katika Azimio la Maputo. Kwa mgawo huu wa sasa ambapo chini ya asilimia 10 ya fedha za serikali zinatengwa kwa ajili ya sekta ya kilimo tuna wasiwasi kwamba malengo yaliyopangwa hayatafikiwa.
26. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya benki ya Dunia ni kwamba mikopo kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta umezidi kushuka, kwa mfano mwaka 2013 ilikuwa ni 8.7%, 7.7% mwaka 2015, na 6.9% mwaka 2017 hii ni kutokana na ukweli kwamba benki za biashara zinaamini kuwa uwekezaji kwenye sekta hii ni “high risk investments”. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema jambo hili litamalizika na kuleta imani kwa taasisi za fedha kuhusu kuwekeza/kukopesha wawekezaji kwenye sekta ya kilimo kama kutakuwepo na Uchumi wa soko jamii, ambapo mzalishaji atazalisha ikiwa anafahamu atapata nini kwenye mazao yake.

27. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa hatujachelewa katika kufikia lengo hilo la mwaka 2025, kama tu tutawekeza kwenye sekta ya kilimo ambayo inatoa ajira kwa watu wengi zaidi kuliko sekta nyingine za uchumi.
D. UPOTEVU WA MAZAO BAADA YA MAVUNO (POST HARVEST LOSSES)
28. Mheshimiwa Spika, ukiangalia Randama ya mwaka 2018/19 fungu 43 uk. 28 aya 6.1.3 na pia mwaka 2019/20 katika Randama uk.17 aya 6.3 kuhusu kuimarisha usimamizi wa mazao kabla na baada ya mavuno na kuongeza thamani ya mazao na upatikanaji wa masoko kwa mazao yote ya wakulima. Mradi wa kudhibiti Sumukuvu katika mazao, uliozinduliwa rasmi tarehe 12 Machi, 2019 ili kudhibiti tatizo la uchafuzi wa sumukuvu katika mfumo wa uzalishaji wa mazao ya chakula hususan mahindi na Karanga. Mradi huo wenye thamani ya jumla ya dola za Kimarekani milioni 35.32 sawa na shilingi bilioni 80. Lakini kwa mwaka 2019/20 zimetengwa fedha za ndani shilingi 1,080,000,000.00

29. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inauliza huu mradi ni wa miaka mingapi? Kwani kwa fedha zilizotengwa kwa mwaka huu kulinganisha na thamani ya mradi ni kwamba itahitajika miaka takriban 80 ili mradi huo ukamilike. Je, kwa hili kweli tuko makini na maendeleo ya kilimo chetu?

30. Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba wakulima wengi wanapata hasara sana kutokana na kutokuwa na njia bora za uhifadhi wa mazao yao baada ya mavuno, inakadiriwa kwamba kati ya asilimia 30-40 ya jumla ya mazao hupotea kila mwaka. Upotevu mkubwa kutoka kwenye matunda, mihogo na mboga, kama karoti na vitunguu nk. Tanzania hutumia Zaidi ya dola milioni 200 sawa na bilioni 400 (Mutungi and Affognon 2013) kuagiza chakula kutoka nje ya nchi.

31. Mheshimiwa Spika, Wakulima wadogo wadogo wanalazimika kuuza mazao yao kwa bei ya chini kwa sababu ya uwezo mdogo kwenye usimamizi wa mazao baada ya mavuno. Katika Afrika Mashariki, ni asilimia 5 huwekezwa kwenye usimamizi wa mazao baada ya mavuno ambayo asilimia 95 hutumika katika uzalishaji. Inakadiriwa kwamba kila mwaka hasara inayotokana na kuharibika kwa mazao ya nafaka barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara, inafikia dola za Kimarekani bilioni 4 na hii ni sawa na asilimia 15 ya thamani ya mavuno hayo.

32. Mheshimiwa Spika, hakuna kumbukumbu zinazotaja sera inayohusu suala la kudhibiti upotevu wa mazao baada ya kuvunwa, takwimu zilizopo zinaonesha kwamba kwa miaka 12 Tanzania ina maghala 1,260. Idadi hii ni ndogo mno ukiilinganisha na mahitaji halisi ya takribani vijiji 11,000 vilivyokuwepo, sasa hivi Tanzania ina vijiji vipatavyo 15,082. Hii ni kwa mujibu wa Tanzania Market Plan chini ya utafiti uliofanywa na taasisi zifuatazo
33. Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonesha licha ya ongezeko la uzalishaji wa nafaka kitaifa (uzalishaji ukifikia takriban tani 9,388,772 kwa mwaka) teknolojia zinazotumiwa wakati wa kuvuna na kusindika ni duni sana. Hali hii husababisha upotevu wa mavuno unaokisiwa kuwa tani 1,877,754.4 kila mwaka. Tafsiri ya takwimu hizi ni uwepo wa upotevu wa takribani asilimia 20 baada ya mavuno. Na tukichukulia uzalishaji wa jumla wa mazao yote ya chakula, matunda na mboga wa tani 22,476,504 upotevu wa asilimia 20 ni sawa na tani 4,495,300.8

34. Mheshimiwa Spika, upotevu huu unachangiwa na matatizo mbalimbali kama vile; maghala mengi hayawafai wakulima kwa sababu ya kuwa mbali, baadhi ya maghala ni mabovu kwa kuachwa kwa muda mrefu bila kukarabatiwa, maghala mengine hayakidhi viwango kwa kukosa vifaa muhimu, maghala mengine ama yamekodishwa kwa wafanya-biashara binafsi, au yanatumiwa kwa shughuli nyingine tofauti na kuhifadhi mazao.

Maghala mengi kutokutumika

35. Mheshimiwa Spika, Maghala mengi katika mkoa wa Songwe haya fanyikazi kutokana na kujengwa kwa maelekezo au uamuzi wa watendaji wizarani,au wakala za Serikali na wanasiasa bila ushirikishwaji wa wadau katika wilaya wakiwemo wananchi na mwisho wa siku yamekuwa ni “white elephants”. Kwa wilaya ya Mbozi kuna maghala mengi katika vijiji lakini hayatumiki kuhifadhi nafaka ambazo upotevu ni mkubwa sana.
36. Mheshimiwa Spika, Jambo hili la kutoshirikisha wadau linaleta ugumu kwa watendaji wa Serikali za mitaa katika kutekeleza sera za nchi kwani wanakutana na ugumu toka kwa wadau mbalimbali kutokuona umuhimu wa kile kinachotakiwa kutekelezwa na Serikali kwa wakati huo.

37. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge, idadi halisi ya Maghala iliyopo kwa sasa kulingana na hongezeko la vijiji pamoja na ongezeko la uzalishaji hasa kwa mazao ya nafaka.

38. Mheshimiwa Spika, Serikali haisemi jinsi ya kukabiliana na tatizo ambalo linawakabili wakulima wengi hasa wadogo na badala yake inatoa suluhu ya uongezaji thamani kwa mazao jambo ambalo ni hatua inayofuata baada ya uhifadhi katika ngazi za familia. Tukumbuke wakulima inawalazimu kuuza mazao yao kwa bei ya chini kutokana na kutokuwa na sehemu muafaka za kuhifadhia mazao yao.

E. BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO
39. Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilianzishwa mnamo Septemba 2011 chini ya Sheria ya Makampuni, ya mwaka 2002. Kazi kuu ya Benki ni uhamasishaji utoaji wa huduma za fedha na huduma zisizo za kifedha kwa sekta ya kilimo Tanzania ikiwa ni pamoja na:
i. Kutoa vifaa vya muda mfupi, vya kati na vya muda mrefu kwenye sekta ya kilimo.
ii. Kuchochea utoaji wa mikopo kwa sekta ya kilimo, hivyo kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo.
iii. Kuwa benki kuu inayofadhili sekta ya kilimo,yenye mikakati ya kujenga uwezo, na mipango ya kuimarisha mnyororo wa thamani kwenye sekta hiyo.
iv. Kufadhili shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji nyuki na shughuli za mifugo.
v. Kuimarisha mnyororo wa thamani kwa njia ya mafunzo, utafiti na ushauri.

40. Mheshimiwa Spika, Mnamo Septemba 2014, Serikali ilitoa mtaji wa Shilingi bilioni 60 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, lakini taarifa za ukaguzi zinaonesha kuwa; benki hiyo badala ya kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo ambayo ndiyo shughuli kuu, Benki imekuwa ikiwekeza sehemu kubwa ya fedha zake katika amana za kudumu. Kufikia tarehe 31 Desemba 2016, jumla ya Shilingi bilioni 54.70 zilikuwa zimewekezwa kwenye amana za kudumu, ambayo ni karibu asilimia 91 ya mtaji. Aidha ilibainika kuwa, kati ya jumla ya Shilingi bilioni 3.95 ya mikopo iliyotolewa, Shilingi bilioni 1.71 ni mikopo kwa watumishi na Shilingi bilioni 2.23 tu ndio zimetolewa mikopo kwenye sekta ya kilimo.

41. Mheshimiwa Spika, mpango wa maendeleo wa taifa wa miaka mitano uk. 100 aya ya 5.5.2 unasema kwamba; Serikali imeji-commit kuiongezea mtaji benki hiyo hadi kufikia shilingi trilioni 3 kwa kipindi cha miaka mitano cha uhai wa mpango wa pili wa maendeleo, Kambi Rasmi ya upinzani inapenda kufahamu hadi sasa Benki hiyo imeongezewa fedha kiasi gani kati ya hizo shilingi trilioni 3 zilizoahidiwa na Serikali?

42. Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba uwepo wa benki hii ilitarajiwa kuwa ni mkombozi katika uwekezaji kwenye kilimo pamoja na viwanda vya kuongeza thamani bidhaa za kilimo. Lakini jambo hilo limekuwa ni kinyume sana kutokana na Benki kutokuwa na mtaji wa kutosha kuweza kufanyakazi zake kama yalivyo malengo ya uanzishwaji wake.
43. Mheshimiwa Spika,ukiangalia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2019/20 uk. 57 inaonesha kuwa benki ilitoa mikopo kwa wakulima 1,049,370 wa mahindi,mpunga,shayiri,kahawa, korosho, karafuu, miwa, mbogamboga, ufugaji wa samaki n.k yenye thamani ya shilingi bilioni 95.1 tu, hapa tunataka kujenga Tanzania ya viwanda lakini hatuoni ni kwa jinsi gani benki hii inaenda kujenga Tanzania ya viwanda.

44. Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni kwamba; kutoa mikopo kwa wakulima bila ya kuwa na utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa bei za mazao zitaweza kurudisha mkopo na kumfanya mkopaji kuendelea kwenye kilimo ni njia moja wapo ya kumfukarisha mkulima.

45. Mheshimiwa Spika, ni hatari sana kwa mkulima kukopa fedha kwa ajili ya uzalishaji na baadae akawekewa vikwazo katika uuzaji wa mazao yake, hii ni kinyume na misingi ya biashara. Jambo hili ndilo lilillotokea kwa wakulima wa Mahindi, Kahawa, Korosho na Pamba kwa kuwalazimisha kuuza kwenye ushirika badala ya kuuza kwa makampuni binafsi kulingana na ushindani wa bei inayotolewa baina ya makampuni hayo.

46. Mheshimiwa Spika, ukiangalia Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/20 uk 56 kuhusu Benki ya Uwekezaji (TIB) kuwa imetoa mikopo kwa sekta ya kilimo yenye thamani ya shilingi bilioni 698.6, lakini kwa taarifa ya Benki hiyo iliyotolewa kwenye Kamati ya PAC inaonesha kuwa; Benki inadai (mikopo chechefu) kiasi cha shilingi 230,669,526,932.24 yenye dhamana zenye thamani ya shilingi 550,832,170,833 na hivyo kuifanya benki hiyo kuwa na mikopo chechefu ya 35% kwa Decemba 2016 (2015: 14%) ikiwa ni ongezeko la kama 150%. Kiwango hiki ni kikubwa sana kulinganisha na kiwango kilichotolewa na BOT kuwa mikopo chechefu cha 24% kwa Benki hiyo.
47. Mheshimiwa Spika, taarifa hii ya Benki kutoa fedha hizo zote kwenye sekta ya kilimo ni vyema ikaonekana kama imetolewa kwa miradi inayotekelezwa na Serikali na pia ni miradi gani na iko wapi, au ni kwa sekta binafsi na ni miradi ya aina gani? Jambo hili linasaidia hata waheshimiwa wabunge kufanyakazi yetu ya Tathimni na Ufuatiliaji kwa karibu jambo ambalo litaleta tija zaidi.
48. Mheshimiwa Spika, ni Rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba kilimo kama nguzo kuu katika uchumi wa Tanzania ni lazima kiendeshwe kwa kuzingatia misingi ya uendeshwaji wa uchumi wa soko jamii; ambapo msingi wa mfumo huu ni kujenga na kuruhusu ushindani, soko huria, kuruhusu watu na sekta binafsi kumiliki mali na kuendesha uchumi wa nchi. Kwa msingi huo wa ushiriki wa sekta binafsi Uwekezaji wa ndani na nje utazinufaisha pande zote katika makubaliano ya kibiashara. Rejea Sera ya CHADEMA uk.15, 79 & 80

F. UHUSIANO KATI YA VIWANDA NA KILIMO
49. Mheshimiwa Spika, sekta ya kilimo ina uhusiano wa moja kwa moja na Viwanda na kila kimoja kinategemea kingine ili kukua, kwani malighafi za sekta zote zinategemeana. Kilimo cha miwa ni malighafi ya viwanda vya sukari; viwanda vya ngozi vinategemea mifugo; viwanda vya maziwa vinategemea mifugo (ng’ombe, mbuzi na kondoo), viwanda vya mafuta ya kula vinategemea kilimo cha alizeti, ufuta, soybeans n.k; viwanda vya nguo vinategemea kilimo cha pamba; uzalishaji wa sigara unategemea kilimo cha tumbaku. Ni ukweli kwamba viwanda haviwezi kushamiri bila ya kilimo kushamiri, kwani hizi sekta zina mahusiano ya moja kwa moja.
50. Mheshimiwa Spika, ukweli uliopo kwa upande wa Tanzania ni kuwa mahusiano hayo ya moja kwa moja hayapo, kutokana na kwamba mazao karibu yote yanauzwa nje yakiwa ghafi kutokana na kutokuwepo kwa viwanda vya kuchakata mazao hayo. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema huu ni udhaifu kwa Serikali kwa kutokuwa na vipaumbele na kusimamia vipaumbele hivyo, kwa kuona ni sekta gani inatoa ajira nyingi na ni watu wangapi wanaitegemea ili kuendesha maisha yao.
51. Mheshimiwa Spika, mahusiano hayo ya kilimo na viwanda hayawezi kufanikiwa na kuwa na tija kama sekta binafsi haikupewa nafasi yake katika kuhakikisha biashara baina ya pande zote mbili zinanufaika, kwanza kwa Mkulima kupewa uhakika wa soko na bei ya kumwezesha kuzalisha kwa faida na hivyo ubora wa mazao yake utakuwa wenye uhakika.
52. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, CHADEMA katika sera yetu ukurasa wa 55 & 56 pamoja na 59& 60 tumeeleza ni kwa jinsi gani tutakifanya kilimo kuwa cha kisasa zaidi ili pande zote washirika kunufaika, kwa maendeleo ya Tanzania tunayoitaka.

G. PEMBEJEO- (Agricultural inputs)
53. Mheshimiwa Spika, Ili Tanzania tufanikiwe, tunahitaji kuboresha tija katika mashamba yetu, mashamba yetu mengi yana tija ndogo (kwa mfano, mavuno ya mahindi kwa wastani ni mara tano chini ya yale ya nchi zilizoendelea) ilihali kuna nafasi kubwa ya kufanya maboresho. Iwapo katika kipindi cha muda mrefu ujao sekta ya kilimo yenye tija itatumia wafanyakazi wachache zaidi, basi uwiano kati ya nguvu kazi na teknolojia mpya unaweza kukuzwa wakati wa kipindi cha mpito. Uzalishaji bora wa chakula pia utasaidia kukuza maendeleo ya viwanda vya usindikaji na biashara za bidhaa za kilimo – sekta inayoweza kutoa ajira nyingi nchini Tanzania. Ili kilimo kiwe na tija tunahitaji kuwa na matumizi sahihi ya teknolojia kwa kiwango kikubwa na matumizi ya Pembejeo za kilimo
54. Mheshimiwa Spika, tunapoongelea pembejeo (Agricultural Inputs) katika mustakabali wa kilimo bora na cha kisasa hapa nchini tunajikita katika mambo makuu matatu ambayo ni; upatikanaji wa pembejeo, usambazaji wa Pembejeo na matumizi yake. Pembejeo zinazohitajika kwa wakulima ni Mbegu bora, mbolea na madawa.
55. Mheshimiwa Spika, pembejeo hizo kwa Tanzania kimekuwa ni kilio kikubwa kwa wakulima kiasi kwamba watu wametumia mwanya huo kujinufaisha binafsi kwa kupeleka kwa wakulima pembejeo feki na mwisho wa siku ni wakulima kupata hasara na umasikini kwa wakulima kuzidi kuimarika.
56. Mheshimiwa Spika, Historia inatuonesha kuwa sekta ndogo hii ya pembejeo imekuwa ikifanyiwa majaribio mengi na Serikali kuona ni mfumo upi utafaa, kwa kuanzia uwepo wa viwanda vya mbolea vya Serikali, Serikali kuhodhi ununuzi wa mbolea nje, lakini yote imeshindikana na matatizo yanabakia pale pale.
57. Aidha, Mheshimiwa Spika, uwekezaji wa Serikali kwenye pembejeo umekuwa ukishuka kwani kwa msimu wa 2008/9 ulikuwa ni asilimia 33.9 ya bajeti ya kilimo (mazao) na mwaka 2013/14 ukawa ni asilimia 8.4; matatizo mengine ya sekta hii ndogo ya pembejeo ni; kukosekana na uhakika wa upatikanaji wa pembejeo; kucheleweshwa kwa pembejeo za ruzuku ambazo wengi wanazitegemea (Japokuwa siku hizi hakuna pembejeo za ruzuku); ulanguzi na mbolea zisizo na ubora kupelekwa kwa wakulima.
58. Mheshimiwa Spika, imebainika kuwa matatizo hayo pia yanachangiwa na kutokuwepo kwa watendaji wa kutosha na mazingira magumu ya watendaji yanayochangiwa na ufinyu wa bajeti inayotolewa. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema matatizo hayo hayawezi kumalizika bila ya uhusishwaji kikamilifu kwa sekta binafsi, hivyo basi ni muhimu sana sekta binafsi ikawa ni kiungo kikuu katika kukibadilisha kilimo chetu kuwa cha kisasa na cha kibiashara na endelevu.
H. HUDUMA ZA UGHANI-(Extension Services)
59. Mheshimiwa Spika, sera ya kilimo ya mwaka 2013 na mwongozo vinaeleza bayana kwamba kila kijiji kinahitajika kuwa na afisa ugani mmoja. Aidha, uwiano unaohitajika kati ya afisa ugani na idadi ya wakulima ni 1:600; Utafiti uliyofanyika katika maeneo ya Singida na Chamwino unaonyesha kwamba afisa ugani mmoja huhudumia kijiji zaidi ya kimoja au kata.

60. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Raslimali watu inayotakiwa kwa sekta ya kilimo, watumishi wenye sifa mbalimbali katika kilimo wanaohitajika ni 19,228 lakini waliopo ni 8,756 sawa na 45.4%. Hii ni kwa mujibu wa Utafiti uliofanywa na Jukwaa la Wadau wa Kilimo wasio wa Kiserikali (Agricultural Non – State Actors Forum – ANSAF)mwaka 2017. Utafiti huo unaonyesha kwamba; watumishi wenye taaluma kuanzia ngazi ya shahada na kuendelea mahitaji halisi ni 2,746 lakini waliopo ni 1,530 ambao ni sawa na 55.7%. Wakati wenye taaluma ngazi ya Cheti na Diploma mahitaji ni 16,542 lakini waliopo ni 7,226 sawa na 43.7%

61. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maafisa ugani kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2013 waliokuwepo ni 7,974 wakati Tanzania ina vijiji vilivyo sajiliwa 15,082. Wakati kuna upungufu huo; Muongozo wa Serikali kwa maafisa ugani ni kila kijiji kimoja kuwa na afisa ugani mmoja.
62. Mheshimiwa Spika, Changamoto zilizopo mbali ya uchache/upungufu huo zinazokabili huduma ya ugani ni pamoja na kufanya kazi katika mazingira magumu, mfano: ukosefu wa vitendea kazi (mfano; pikipiki, vifaa vya kupimia udongo na mafunzo ili kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na mabadiliko ya tabianchi.

63. Mheshimiwa Spika, maafisa ugani kupangiwa majukumu ambayo ni nje na ueledi wao, mfano kuwa watendaji wa vijiji/kata.Hata hivyo, utafiti unaonyesha kwamba maafisa ugani hawatimizi wajibu na majukumu yao vizuri, Muda mwingi wanafanya kazi ofisini au shughuli binafsi. Hali hii husababisha njia zisizo bora kwenye kilimo na kuchangia kushuka kwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini

I. MAZAO MAKUU HAPA NCHINI
64. Mheshimiwa Spika, kwa sasa mazao yote yanayolimwa hapa nchini tunaweza kuyaita kuwa ni mazao ya biashara, japokuwa kuna mazao makuu ya biashara(traditional cash crops) ambayo ni Pamba; Korosho; Kahawa; Mkonge; Chai; na Tumbaku.
65. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha wa hotuba hii tutajikita katika baadhi ya mazao ambayo ni kichocheo kikubwa cha kukua au kudumaa kwa uchumi wa nchi yetu.
i. Pamba;
66. Mheshimiwa Spika, zao la Pamba ni zao ambalo linalimwa na wakulima wadogo kati ya 350 na 500,000 katika wilaya 49 za mikoa 17 ya Tanzania bara, japokuwa asilimia 80 ya Pamba yote inalimwa katika mikoa mine ya Simiyu, Shinyanga, Singida na Mwanza. Hii ni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Ndg Marco Mtunga, wakati akitoa taarifa kwa wadau wa Pamba.
67. Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa Pamba unaathiriwa kwa kiwango kikubwa na changamoto zifuatazo:- kucheleweshwa kwa pembejeo; ubora hafifu wa pembejeo (mbegu na madawa); kutokutabirika kwa bei kwenye soko la dunia na bei elekezi kupangwa bila wakulima kushirikishwa; huduma za ugani kuwa duni na hivyo wakulima kutokufuata mahitaji sahihi ya kilimo cha Pamba; matumizi hafifu ya teknolojia katika kilimo cha Pamba (Use of Agricultural mechanization); Kutokuwepo kwa vyama vya ushirika vilivyo imara; Mauzo ya Pamba ghafi kwenda nje inanyima fursa ya ajira kwa watanzania wengi na hivyo kuongeza kipato chao.
68. Mheshimiwa Spika, changamoto hizo kwenye zao la Pamba zimekuwepo kwa kipindi kirefu na Serikali imeshindwa kuzitafutia ufumbuzi. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa mustakabali wa kilimo biashara upo katika soko la mazao na bidhaa za kilimo, ambapo wakulima na wananunuzi wataendesha shughuli zao za kibiashara katika mazingira yanayotabirika, na kwamba wakulima wanaweza kupata bei nzuri kwa mazao yao.
69. Mheshimiwa Spika,Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa katika soko kama hilo litasaidia matumizi ya teknolojia katika kuboresha shughuli za kilimo ili kukidhi viwango vya ubora vya kimataifa na hivyo kuhakikisha kwamba walaji wanapata bidhaa bora.
ii. Kahawa
70. Mheshimiwa Spika, Kahawa ni zao la biashara linalolimwa hapa nchini katika mikoa ya Songwe, Njombe-(Ludewa), Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Ruvuma- (Mbinga), Kagera, Tanga, Iringa, Morogoro, Kigoma, Manyara, Mwanza, Rukwa na Mara. Inakadiriwa kuwa Jumla ya eneo la hekta 265,000 ndilo linatumika kwa ajili ya kilimo cha Kahawa aina ya ARABICA NA ROBUSTA ambazo ndizo zinalimwa sana hapa Tanzania.

71. Mheshimiwa Spika, Kahawa aina ya Arabica inachukua asilimia 70 ya uzalishaji wote wa Kahawa hapa nchini. Aina hii ya Kahawa inalimwa kwa wingi katika Mikoa ya Songwe, Mbeya, Ruvuma na Kilimanjaro. Robusta inazalishwa kwa asilimia 30 na inalimwa zaidi katika Mkoa wa Kagera.
72. Mheshimiwa Spika, Kahawa inalimwa na takriban familia 450,000 kwa Mikoa ambayo imeainishwa hapo awali na familia hizo zinachangia takriban asilimia 90 ya uzalishaji wote wa Kahawa hapa nchini. Asilimia 10 iliyobaki katika uzalishaji inachangiwa na mashamba makubwa yanayomilikiwa na watu au Kampuni binafsi. Kwa ujumla asilimia 6 ya idadi ya watu wote Tanzania (ambayo kwa sasa ni takriban watu milioni 55) wanategemea uchumi wa Kilimo cha Kahawa kuendesha maisha yao.
73. Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ya nne kwa uzalishaji wa Kahawa Afrika baada ya Ethiopia, Ivory Coast na Uganda ambapo kila mwaka huzalisha wastani wa tani 46,000 hadi 60,000 huku mkoa wa Kagera ukizalisha takribani tani 12,131.
74. Mheshimiwa Spika, uzalishaji Kahawa Duniani kwa msimu wa 2016/17 ulifikia magunia milioni 158.93. sawa na tani milioni 9.535 hili ni ongezeko la asilimia 0.8 ikilinganishwa na msimu uliopita wa mwaka 2015/16. Arabika ilizalishwa magunia milioni 98.84 (62%) na Robusta magunia milioni 60.10 (38%).
75. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tanzania uzalishaji kwa mwaka 2014/15 jumla zilizalishwa tani 42,768; mwaka 2015/16 tani 60,188; mwaka 2016/17 tani 47,591.5; mwaka 2017/18 tani 41,679.4
76. Mheshimiwa Spika, Kwa takwimu hizo za uzalishaji wa Kahawa hapa nchini ni dhahiri kuwa kuna tatizo sehemu katika sekta ndogo ya Kahawa, na hivyo ni jukumu letu kama wawakilishi wa wananchi kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
77. Mheshimiwa Spika, Ukirejea nyaraka za watatifi wanasema kuwa sekta ndogo ya Kahawa imekuwa na matatizo mengi miongoni mwake ni hali ya hewa kubadilika sana, kukosekana kwa miundombinu imara ya umwagiliaji wa mashamba (Hili ni kwa mashamba makubwa) na mibuni kuzeeka na hivyo uzalishaji kuwa chini. Aidha kukosekana kwa uwekezaji wakutosha katika ufafiti wa magonjwa ya kahawa na huduma duni za ugani kumeathiri uzalishaji wa zao hili.
78. Mheshimiwa Spika, mbali ya changamoto ya utafiti kwenye zao la kahawa lakini tatizo kubwa zaidi linalowakumba wakulima ni kutokuwepo kwa soko la uhakika la kuweza kununua kahawa kwa bei ambayo italifanya zao hilo kuendelea kulimwa kitaalam zaidi.
79. Mheshimiwa Spika, ukweli ni kuwa changamoto za soko zilikuwepo hata miaka iliyopita, lakini kwa sasa tatizo limekuwa kubwa zaidi kwa sababu limeibuka suala la AMCOS kuhodhi tena soko la Kahawa kwa Wakulima na hivyo kuminya fursa ya wao kuchagua bei kulingana na gharama za uzalishaji. Kambi Rasmi bado inasisitiza katika uwepo wa mfumo huru wa soko ambapo Mkulima na Mnunuzi watakutana na kupanga bei ili kukidha gharama za uzalishaji na kila upande unufaike na biashara hiyo.
iii. Korosho
80. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa takwimu za Randama ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2018/19 zinaonesha kwamba, mwenendo wa uzalishaji wa zao la korosho kwa miaka mitatu kuanzia msimu wa mwaka 2015/16 hadi msimu wa 2018/19 umekuwa unapanda ambapo mwaka 2015/16 uzalishaji ulikuwa tani 155,416; 2016/17 tani 265,238 na 2017/18 uzalishaji ulifikia tani 311,899. Aidha, matarajiokwa mwaka 2018/19 yalikuwa ni kuzalisha tani 350,000.
81. Mheshimiwa Spika, takwimu hizo zinaonesha kwamba, wakulima wadogo wadogo takribani 280,000 wanaendesha maisha yao na familia zao kutegemea moja kwa moja zao la Korosho kwa kulima kati ya eka moja hadi mbili na kufanya eneo linalolimwa zao hilo kufikia ekari 400,000. Na kwa sasa eneo hilo litakuwa limeongezeka kutokana na mwamko wa wananchi kulima zao hilo.

82. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria ya korosho (Cashewnut Industry Act (Cap, 203), inasema kuwa asilimia 65 ya kodi ya mauzo nje yarudishwe kwa wakulima kupitia bodi ya korosho (CBT) na Serikali ibakie na asilimia 35. Mgawo wa hizo asilimia 65 wa export levy, matumizi yake makubwa ni ununuzi wa Pembejeo za kilimo cha Korosho na kuendeleza utafiti kwenye zao la Korosho.
83. Mheshimiwa Spika, katika hali ambayo mpaka sasa haieleweki; Serikali ilivunja bodi ya Korosho; na kutaifisha ile asilimia 65 ya kodi ya mauzo ya korosho nje; na pia kuingilia biashara ya korosho kwa kuwazuia wanunuzi binafsi kununua korosho. Matokeo yake ni kwamba hakuna mauzo ya korosho nje ya nchi yaliyofanyika mpaka sasa; Serikali ilichofanya ni kununua korosho kwa wananchi– tena kwa mkopo kwa ahadi ya shilingi 3,300 kwa kilo lakini wakati wa kulipa bei hiyo ikapungua kwa madai kwamba korosho hazina ubora.
84. Mheshimiwa Spika,uamuzi wa Serikali kununua Korosho toka kwa wakulima badala ya kuhusisha makampuni binafsi umeligharimu taifa letu kwa kukosa fedha za kigeni, mfano kwa mwaka wa fedha 2017/18 fedha za kigeni zilizotokana na korosho zilikuwa ni dola za kimarekani milioni 965, kwa mwaka huu 2018/19 unaoishia hadi sasa ni Zero. Kodi ya mauzo nje (export levy) kwa mwaka 2017/18 ilikuwa ni dola za kimarekani milioni 200; kwa mwaka 2018/19 hakuna chochote.
85. Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya utatanishi Serikali ilisaini mkataba wa kuuza korosho tani laki moja na kampuni ya Indo Power ya Kenya, mkataba ambao haukutekelezeka licha ya kupigiwa debe na Waziri wa Katiba na Sheria wa wakati huo Mheshimiwa Prof. Paramagamba Kabudi(Mb) na Gavana wa Benki Kuu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuwawajibisha wahusika wote kwa kulipotosha Taifa na kuliingizia hasara kubwa kutokana na mkataba ambao haukufanyiwa upembuzi yakinifu.
86. Mheshimiwa Spika,kitendo cha kuvunja Bodi ya Korosho – chombo ambacho kiliundwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge bila kuleta Bungeni muswada wa sheria wa kuifuta sheria hiyo mosi ni ukiukwaji wa katiba, pili ni dharau kwa Bunge; lakini mbaya zaidi ni hujuma kwa wakulima wa zao la korosho ambao mpaka sasa haijulikani zao lao linaratibiwa na chombo gani. Kwa maneno mengine zao la korosho ni kama vile halina mwenyewe na wakulima wa korosho wamekuwa kama kondoo wasio na mchungaji.
87. Mheshimiwa Spika, kutokana na mchanganyiko huo wa mambo kumekuwa pia na sintofahamu ya biashara ya korosho katika msimu huu ambapo wakulima wengi wameshindwa kupata fedha kulingana na mauzo ya korosho zao. Jambo la ajabu ni kwamba korosho ambazo zilikuwa zimechukuliwa na Serikali na kwa maana kwamba kilichokuwa kikisubiriwa ni wananchi kulipwa fedha zao zimeanza kurejeshwa kwa wenyewe kwa madai kuwa hazina ubora unaostahili. Na pia wakulima wenye korosho nyingi kukataliwa kulipwa kwa kigezo cha uhakiki wa mashamba.

88. Mheshimiwa Spika, ni ajabu kwamba; kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania tunakwenda kuhakiki shamba la mkulima kisa tu ana mazao mengi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kuwa uzalishaji mkubwa ni neema kwa nchi kwa kuwa wingi wa korosho ndani ya nchi maana yake ni kupata fedha za kigeni kwa wingi tutakapouza nje na hivyo kukuza uchumi wetu. Inashangaza sana kwa Serikali imeendelea kuweka vikwazo vingi sana katika biashara nzima ya zao la korosho.

89. Mheshimiwa Spika, katika muendelezo wa mauzo na malipo ya korosho, wakulima katika wilaya za Ruangwa, Kitangali-Newala Vijijini na Mjini wakulima walikwisha uza korosho zao lakini kutokana na wasombaji kutokujua jinsi korosho zinavyotakiwa kutunzwa kwenye maghala, zilinyeshewa na mvua na kuharibika. Hivyo iliwalazimu wapokee korosho toka kwa mnunuzi (Serikali) ili wakulima wachambue upya na kuuza upya. Katika kadhia hiyo wakulima wamepata hasara kubwa sana, kwani mkulima aliyekuwa ameuza kilo 500 baada ya kurudishiwa mzigo wa kilo hizo ili kuchambua upya anajikuta anauza upya kilo 300 na hivyo kufanya kilo 200 kuwa ni hasara.

90. Mheshimiwa Spika, mbali ya hasara iliyotokana na uzembe wa utunzaji, lakini wakulima wengi wakienda kudai fedha zao wanawekwa ndani, na hilo limekuwa ni kero kubwa sana kwa wakulima kwa maeneo mengi ya mikoa inayolima korosho.
91. Mheshimiwa Spika,kwa kuwa lengo la nchi ni kuwa na Tanzania ya viwanda, ni muda mwafaka sasa kuhakikisha viwanda vinakuwa na uhakika wa malighafi, na malighafi itapatikana ndani au nje ya mipaka ya nchi yetu.
92. Mheshimiwa Spika, Uchumi wa Viwanda kwa nchi hii utafikiwa tu, pale bei za mazao ya kilimo zitakapokuwa nzuri na hivyo kumfanya mkulima kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia bora na kisasa.Kambi Rasmi Tunaamini kwamba mustakabali wa kilimo cha kisasa, endelevu na cha kibiashara upo katika soko la mazao ya bidhaa za kilimo, ambapo wakulima na wanunuzi wataendesha shughuli zao za kibiashara katika mazingira yanayotabirika,na kwamba wakulima wanaweza kupata bei nzuri kwa mazao yao. Rejea Sera ya Chadema uk.55 sura ya 9.3 Biashara ya Mazao na Bidhaa za Kilimo.

iv. MIWA
93. Mheshimiwa Spika, Kilimo cha miwa ni kilimo chenye tija kwa mkulima, kilimo hiki kinaweza kufanywa na mtu yeyote yule aidha awe ameajiriwa au laaa! Jambo la msingi ni kuhakikisha anajitoa kikamilifu katika kuhakikisha anawekeza akili yake katika kulima kilimo hiki.
94. Mheshimiwa Spika, Wazalishaji wakubwa wa sukari nchini ni: Kilombero Sugar Co. Ltd.; TPC Ltd.; Kagera Sugar Ltd. na Mtibwa Sugar Estates Ltd. Na katika maeneo hayo yote kuna wazalishaji wa nje. Kwa Kampuni ya Sukari ya Kilombero -wakulima wa nje 8,500 wanazalisha 43% ya miwa inayokamuliwa na viwanda vya K1 na K2.
95. Mheshimiwa Spika, Uzalishaji wa sukari ya matumizi ya nyumbani (consumption sugar) umeongezeka mara nne kutoka tani 80,000 (1997/98) kabla ya ubinafsishaji na kufikia tani 330,000 kwa msimu wa 2016/17. Uzalishaji wa sukari nchini huchangia 72% ya mahitaji ya sukari ya matumizi ya nyumbani. Kuna wakulima wa miwa wa nje (Outgrowers) 15,000 waliosajiliwa wanaochangia asilimia thelathini (30%) ya miwa inayosagwa kwa uzalishaji sukari. Hutoa ajira 18,000 kwa wafanyakazi walioajiriwa viwandani na katika mashamba ya miwa. Mapato ya shilingi bilioni 45 kwa wakulima wa nje kila mwaka. Malipo ya zaidi ya shilingi bilioni 100 ya kodi za Serikali kila mwaka.
96. Mheshimiwa Spika, Katika programu iliyokuwa inajulikana kama Matokeo Makubwa Sasa (“Big Results Now”), serikali ilitaka kuongeza uzalishaji wa sukari. Serikali iliahidi kushirikiana na wawekezaji binafsi kuongeza mashamba makubwa ya miwa. Katika program maalum nyingine iitwayo “Southern Agricultural Growth Corridor”, au SAGCOT, serikali ilikuwa na mpango kwa ajili ya wawekezaji binafsi kuanzisha na kupanua mashamba ya miwa na mpango wa wakulima wa nje katika Kijiji cha Ruipa, karibu na Ifakara. Sheria ya Sukari, hairuhusu kwa makampuni mengine kujenga kiwanda cha miwa ndani ya eneo la km 40 za eneo la Kampuni ya Sukari Kilombero iliyopo Kidatu.
97. Mheshimiwa Spika, Makadirio ya mahitaji ya Sukari: Mahitaji ya Sukari kwa matumizi ya nyumbani na viwandani yataongezeka kutoka tani 580,000 mwaka 2016/17 hadi tani 695,000 – 755,000 mwaka 2020/21. Sukari kwa matumizi ya nyumbani: Mahitaji yataongezeka kutoka tani 445,000 mwaka 2016/17 na kufikia tani 535,000 – 580,000 ifikapo mwaka 2020/21. Sukari kwa matumizi ya viwandani: Mahitaji yataongezeka kutoka tani 135,000 hadi tani 160,000 – 175,000 ifikapo mwaka 2020/21 .
98. Mheshimiwa Spika, Sukari ni bidhaa nyeti na yenye changamoto nyingi sehemu nyingi duniani. Ni muhimu mno kuanisha uzalishaji sukari hapa nchini kwa siku za usoni kwa kutathmini mustakabali wa masoko ya sukari ya EAC, SADC, na EU. Ieleweke kwamba karibu nchi zote zinazozalisha sukari duniani, serikali zake hulinda wazalishaji wa ndani kwa njia mbalibali, hasa, kiwango cha sukari inayoingizwa nchini na kwa ushuru wa forodha (import duty).
99. Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumesikia kuwa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, amesema kwamba; “baada ya kufanya mazungumzo na viwanda vinavyozalisha sukari nchini, serikali inatoa ruhusa kwa viwanda vya sukari nchini kuagiza nje sukari pungufu ambayo ni tani 30,000 pekee na viwanda hivyo kufanya biashara na wafanyabiashara wengine nje ya nchi kutokana na viwanda hivyo kuonyesha juhudi katika uzalishaji” .
100. Mheshimiwa Spika, Mahitaji ya sukari mwaka mzima ni tani 670,000 ambapo viwanda hutumia tani 155,000 na matumizi ya kawaida huwa ni tani 515,000. Kwa mujibu wa Waziri huyo, Bodi ya sukari imetoa ripoti Februari mwaka huu na kubaini kuwa jumla ya sukari iliyopo kwa wafanyabiashara na kwenye hifadhi ni tani 129,228. Mheshimiwa Hasunga amevitaja viwanda vitano vinavyozalisha sukari nchini kuwa ni TPC Moshi, Kagera Sugar, Mtibwa, Kilombero na kiwanda kidogo cha Manyara. Viwanda hivyo havizalishi sukari ya viwandani.
101. Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kuna changamoto nyingi kwenye kilimo cha miwa na sukari yenyewe, lakini kitendo cha Serikali kutoa vibali kwa viwanda kuagiza sukari toka nje bila kuweka utaratibu madhubuti na wawazi wa kudhibiti kiasi kinachoagizwa, maana yake ni kuua kilimo cha miwa hapa nchini hasa wakulima wa nje. Tukumbuke kwamba sukari toka nje inazalishwa kwa gharama za chini kulinganishwa na uzalishaji wa sukari yetu, hivyo kutoa upenyo wa viwanda kuagiza ni dhahiri kuwa mahitaji ya miwa toka kwa wakulima yatapungua sana na mipango na uhamasishaji kwa wananchi kulima miwa itakuwa ni kuwaingiza kwenye shimo la hasara kubwa na hivyo kuwaletea umasikini.
J. FURSA ZILIZOPOTEA
102. MheshimiwaSpika,takwimu za kutisha zinaonesha nchi yetu inaendelea kuagiza bidhaa za maziwa, nyama, samaki, mafuta ya kura, ngano, mchele na matufa ya kula, hasa mawese pamoja na sukari. Inakadiriwa kwa mwaka, nchi yetu huagiza bidhaa za chakula zenye gharama ya takribani Tzs 1,345bilioni. Kiwango hiki ni karibia mara tano ya bajeti ya mwaka ya wizara yaKilimo. Bidhaa za mafuta ya kula inagharimu zaidi ya dola za Kimarekani 250 milioni, wakati bidhaa za sukari, ngano, maziwa na nyinginezo hugharimu kiwango kikubwa pia cha fedha za kigeni. Wakati ambapo serikali ya awamu ya Tano inajipambanua na suala la viwanda, ni lazima wizara ya viwanda na Kilimo zilete mkakati wenye kuonesha uratibu halisi wa sekta/minyororo ya thamani ya kimkakati yenye uwezo wakuleta mabadiliko kwa wazalishaji, wafanyabiashara, wachakataji na uchumi wa nchi kwa ujumla.

K. MABADILIKO YA TABIANCHI NA KILIMO
103. Mheshimiwa Spika,Takwimu zilizotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Jumatano tarehe 11 Julai 2018 zinaonesha kwamba kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hadi kufikia mwaka 2050, shughuli za uvuvi baharini hasa katika nchi maskini zaidi duniani, zitaathirika sana, sanjari na kupungua kwa kiwango cha maji baridi duniani. Hali hii itakuwa na madhara makubwa sana kwa mamilioni ya watu wanaotegemea kwa kiasi kikubwa kupata mahitaji yao msingi kutoka katika sekta ya uvuvi baharini. FAO inasema, waathirika wakuu wa athari za mabadiliko ya tabianchi daima wataendelea kuwa ni maskini.

104. Mheshimiwa Spika,Nchi tatu za Afrika ya Mshariki za Tanzania, Kenya na Uganda pamoja na mataifa ya Pwani ya Pembe yataendelea kuwa na upungufu wa mvua kwa kipindi chote cha mwezi wa nne na hali inatarajia kuwa mbaya kutokana na kipindi cha ukame kuendelea na hali isiyo yakawaida ya joto kuwa juu sana

105. Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ilitolewa baada ya kufanyika kwa kikao cha mamlaka ya maendeleo ya mataifa ya IGAD on Climate Prediction and Application Centre (ICPAC) kuwa uwezekano mkubwa wa ukame ambao hautakuwa wa kawaida kwa mikoa yote ya mwambao wa Tanzania, Magharibi ya Kenya, kusini na kusini mashariki mwa Ethiopia, ukanda wa kati na kaskazini mashariki mwa Somalia, Uganda na Sudani ya Kusini. Maeneo hayo yaliyotajwa kwenye mataifa hayo yatakuwa na kipindi cha ukame na joto kuwa la juu kuliko kawaida na hivyo kuwa na athari kwenye malisho, upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu, mifugo na wanyamapori.

106. Mheshimiwa Spika, hili limejitokeza pia kutokana na kukosekana kwa mvua za vuli za Oktoba hadi Desemba, na kufuatiwa na kipindi kisicho cha kawaida cha joto kuwa kali kuanzia mwezi Januari 2019, jambo ambalo limeathiri sana rasilimali za malisho na hivyo kuanza kuathiri maisha ya wananchi ambao kwa kiwango kikubwa mifugo ndio maisha yao.

107. Mheshimiwa Spika, Hii sio kuwa inaathiri jamii za wafugaji tu bali inaathiri pia wakulima waishio kwenye maeneo ya mwambao wa bahari ya Hindi na pia waishio kwenye ukanda wa kati wa nchi yetu ya Tanzania. Jambo hili linaleta madhara makubwa hasa kwa wakulima wa maeneo ya Wilaya za mkoa wa Morogoro, Singida, Dodoma; Pia kwa ukanda wa Magahribi kwa mikoa ya Tabora na Kigoma hali ya upatikanaji wa mvua imekuwa mbaya sana kiasi kwamba hasara kubwa imewakumba wakulima ambao tayari walishafanya maadalizi ya msimu huu wa kilimo.

108. Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, ni kuwa usalama wa chakula ambao pia ni usalama wa nchi kwa mwaka ujao uko mashakani, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuanza kuiona hali hiyo na kuiwekea mkakati wa utekelezaji mapema na sio kusubiri hadi janga litokee.

L. TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI (Fungu 05)
109. Mheshimiwa Spika, Tume ya taifa ya umwagiliaji ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 25.82 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 6 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 19.82 ni fedha za nje.
110. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Februari 2019 shilingi bilioni 5.27 zilikuwa zimetolewa sawa na asilimia 20.4 ya fedha zote za maendeleo zilizokuwa zimeidhinishwa. Licha ya utekelezaji mdogo wa bajeti katika eneo hili la umwagiliaji, bado Serikali imeendelea kuwa tegemezi kwa wahisani wa maendeleo kutoka nje.
111. Mheshimiwa Spika, kutokana na fedha kidogo zilizotolewa kwa Tume, miradi mingi ya umwagiliaji imeshindwa kutekelezwa na mingine kuchukua muda mrefu kukamilika hivyo kuondoa maana halisi ya kupunguza utegemezi wa mvua katika kilimo. Hivyo basi; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuboresha zaidi mazingira ya utendaji kwa Tume ili eneo hili la umwagiliaji liweze kuokoa zaidi ya dola za kimarekani milioni 800 (Shilingi trilioni 1.84) zinazotumika kuagiza chakula kutoka nje ya nchi kila mwaka.
M. UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2018/19 NA MPANGO WA MWAKA 2019/20
112. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2018/19 wizara illidhinishiwa jumla ya shilingi 98,119,516,000.00 kama fedha za miradi ya maendeleo kwa fungu 43, kati ya fedha hizo shilingi 82,000,000,000.00 zilikuwa ni fedha za ndani na shilingi 16,119,516,000.00 zilikuwa ni fedha za nje. Hadi kufikia mwezi Machi, 2019, shilingi 41,222,448,778.00, sawa na asilimia 42 ya fedha zote za bajeti ya maendeleo kwa fungu 43 zilizokuwa zimeidhinishwa ndizo zilikuwa zimetolewa. Kati ya fedha hizo fedha za ndani zilikuwa shilingi 39,964,621,000.00 na fedha za nje ni shilingi 1,257,827,778.00. Fedha za ndani zilizotolewa zikiwa sawa na asilimia 48.74 ya bajeti ya fedha za ndani na asilimia 7.8 ya fedha za nje.
113. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/20 Wizara fungu 43 inaomba jumla ya shilingi 208,115,500,575.00 Kati ya fedha hizo shilingi 143,577,033,140 ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na shilingi 64,538,467,435.00 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 17,992,293,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya wizara.
114. Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo zinaoombwa mwaka 2019/20 ni ongezeko la shilingi 45,457,517,140.00 sawa na asilimia 31.66 kwa kulinganisha na zile zilizoombwa mwaka wa fedha 2018/19
115. Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2015/2016 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Fungu 05 iliidhinishiwa jumla ya shilingi 53,626,690,195. Kati ya fedha hizo shilingi 232,116,195 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 53,394,574,000 ni fedha kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Hadi kufikia tarehe 31, Machi, 2016 fedha za matumizi ya kawaida kiasi cha shilingi 96,884,227 zilitolewa ambayo ni sawa na asilimia 42 ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge. Fedha za maendeleo kiasi cha shilingi 5,131,032,985 zilitolewa ambazo ni sawa na asilimia 10 ya fedha zilizoidhinishwa. (Fedha hizo ni za nje tu na hakuna fedha za ndani zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo).

116. Aidha, Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2015/2016, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji iliidhinishiwa kiasi cha shilingi 53, 394, 574,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo wakati mahitaji halisi yanakadiriwa kufikia shilingi 400,000,000,000. Uwiano huu hauonyeshi dhamira ya dhati ya Serikali ya kutambua na kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na kilimo cha umwagiliaji. Aidha,Fungu 05 lilitengewa jumla ya shilingi 63,412,358,800. Kati ya fedha hizo, shilingi 58,905,747,200 zilikuwa ni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Rejea taarifa ya Kamati ya Bunge ya Kilimo, Maji na Mifugo ya mwaka 2016/17

N. HITIMISHO
117. Mheshimiwa Spika,
Kwa kuwa; Kambi Rasmi ya Upinzani inakichukulia kilimo cha kisasa kama matumizi ya mbinu za kisasa za kilimo ambazo zinahusisha matumizi ya madawa ya kilimo, na teknolojia ya kisasa katika mchakato mzima wa uzalishaji shambani;
Na kwa kuwa; Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba kilimo cha kisasa kinatumia zaidi pembejeo kutoka kwa wasambazaji binafsi ili kukuza uzalishaji uendelevu;
Na kwa kuwa; Kambi Rasmi ya Upinzani inatazama Tanzania kama Taifa ambalo sekta binafsi inatakiwa kuendesha viwanda vya mazao (Agro processing Industries) ili kuongeza ubora wa mazao ya yanayozalishwa na wakulima mashambani;
118. Mheshimiwa Spika, Hivyo basi; Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa mustakabali wa kilimo cha Tanzania upo katika soko la mazao ya bidhaa na bidhaa za kilimo ambapo wakulima na wanununuzi wataendesha shughuli za kibiashara katika mazingira yanayotabirika, na kwamba wakulima wanaweza kupata bei nzuri kwa mazao yao. Soko kama hilo pia litasaidia matumizi ya teknolojia kama kuboresha shughuli za kilimo ili kukidhi viwango vya ubora vya kimataifa na hivyo kuhakikisha kwamba walaji wanapata bidhaa bora. Kwa ufafanuzi zaidi rejea Sera ya Chadema Kuhusu Kilimo.
119. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

………………………………
Pascal Yohana Haonga (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya kilimo
17.05.2019

Share Button