TARIME NI WATU MAJASIRI, TUMIENI UJASIRI HUO KUDAI HAKI ZENU NA DEMOKRASIA YA TAIFA LETU-MBOWE .

 

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana tarehe 22 Octoba 2018 aliongoza kikao cha ndani cha Mkutano mkuu wa chama katika wilaya ya Tarime , ambacho kilikuwa mahususi kwa ajili ya zoezi la Chadema ni msingi zoezi ambalo linaambatana na uchaguzi wa ndani ya chama hicho ambalo limeambatana na usambazaji wa sera mpya za Chama hicho.

 

Katika kikao hicho ambacho aliambatana na viongozi Mbalimbali akiwemo John Cheche ambaye ni Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Mjumbe wa kamati kuu ambaye pia ni mnadhimu wa Mameya wa chama hicho na ambaye ni mwenyekiti wa Halimashauri ya wilaya ya Tarime vijijini Moses Misiwa, Ester Matiko Mbunge wa Tarime Mjini,Lazaro Nyalandu ambaye ni kada wa chama hicho pamoja na viongozi wengine mbalimbali.

 

Katika mkutano huo alionyesha kusikitishwa kwake na jinsi ambavyo serikali ya awamu ya tano chini ya rais Magufuli na uongozi wa CCM unavyopoteza fedha nyingi za walipa kodi kwa ajili ya kufanya chaguzi za marudio ambazo zinasababishwa na watu ambao wanashawishiwa na kurubuniwa kwa rushwa mbalimbali ili wajiengue kwenye nyadhifa ambazo walichaguliwa na wananchi na kwenda kuunga mkono kinachoitwa ‘juhudi’ huku kila anayeondoka akisaini barua inayofanana na yenye makosa yanayofanana na wakitoa sababu zinazofanana.

 

‘Fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinakosekana kumbe zinatumika kununua viongozi wa wananchi na kurudia chaguzi kila siku …hii sio jambo la kujenga taifa bali ni kuangamiza taifa…lazima wote tusimame kukabiliana na hali hii ambayo imelikumba taifa letu…..ndio maana wote mmesikia taarifa ya Mwenyekiti wa Halimashauri akieleza kuwa tangu 2016 hawajawahi kuletewa fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika halimashauri yake’

 

Aidha amewataka wananchi wa Tarime kuwa majasiri na huku wakiendelea kupigania haki zao bila woga wala hofu pamoja na ukweli kuwa taifa linapitia katika kipindi kigumu cha watu kutekwa,kupotezwa , kuuwawa na wengine kuumizwa kwa risasi.

 

‘Nchi imekuwa sio salama tena kwani kumeibuka wimbi la watu kutekwa , kupotezwa ,kuuwawa na wengine kupigwa risasi kama ilivyofanyika kwa Tundu Lissu na hakuna taarifa zozote na hatuoni jitihada za kutosha zikifanyika ili kukomesha hali hii’

 

Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Vijijini ndugu John Heche alieleza kuhusu jitihada mbalimbali ambazo yeye kwa kushirikiana na viongozi wenzake ambavyo wamekuwa wakijenga chama pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo wameweza kuitekeleza tangu walipoingia madarakani katika Wilaya ya Tarime .

 

‘Sisi Tarime tukuhakikishie kuwa tuko imara na hatutarudi nyuma kamwe katika mapambano ya kudai Demokrasia katika Taifa letu na tuko imara sana ….tutaendelea kuwatumikia wananchi wetu ambao walituamini na kamwe tunawaahidi kuwa sisi sio sawa na wale wavulana ambao wameamua kuunga mkono juhudi’

 

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime mjini Mheshimiwa Ester Matiko aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa yeye hayuko tayari kuondoka Chadema na wala hana mpango wowote wa sasa au baadaye wa kuunga mkono “juhudi” na kuwa atafia ndani ya Chama chake.

 

‘Mimi ni Chadema na nitaendelea kuwa Chadema siku zote za maisha yangu, ninaahidi kufia Chadema’

 

Akielezea mafanikio ya Halimashauri ya Wilaya ya Tarime , Mwenyekiti wa Halimashauri hiyo Moses Misiwa alielezea miradi ambayo wameweza kuitekeleza bila kupata fedha yoyote kwa ajili ya miradi ya maendeleo kutoka ngazi ya Serikali kuu tangu mwaka 2016 ambayo wamefanya katika sekta ya elimu, afya na miundombinu.

 

‘Tumeweza kugawa madawati katika shule zote za serikali 105 bila kuwachangisha wananchi na tulitumia jumla ya shilingi milioni 700 ambazo zimetokana na vyanzo vya ndani, tumejenga vituo vya afya 6 katika kata za Nyanungu (50 milioni),Muriba (120 milioni),jengo la upasuaji (200 milioni),miundombinu ya umeme kwa ajili ya upasuaji (120milioni),kata ya Magoto (200 milioni),kata ya sirari (200 milioni), kata ya Nyarwana (230 milioni), kata ya Nyangoto (220 milioni),kata ya kirende (800 milioni) na tumejenga hospitali ya Halimashauri na kuwa Halimashauri ya kwanza nchini kuwa na hospitali yake ambayo ilitugharimu fedha zetu za ndani shilingi bilioni 1.3 ambazo zimetumika kununua vifaa tiba na ujenzi’

Share Button