TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kutoa taarifa ya kulaani na kupinga ukiukwaji wa Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali uliofanywa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Bwana Gerson Msigwa tarehe 21 na 25 Mei, 2018 ambapo kwa kujua au kutojua au kwa kiburi cha mamlaka aliamua kufanya kazi za Chama cha Mapinduzi (CCM) huku akijua sio kazi zake kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma.

Tarehe 21 Mei, 2018 ilitolewa taarifa ya Ofisi ya Rais Ikulu ikiwa imesainiwa na Gerson Msigwa kuhusu tukio la Mwenyekiti wa CCM Taifa John Pombe Magufuli kupokea taarifa ya ukaguzi wa mali za CCM katika Makao Makuu ya Chama hicho Lumumba Jijini Dar es Salaam.

Kwa mara nyingine tena tarehe 25 Mei, 2018 Msigwa kwa kujua au kutojua au kwa kiburi cha malamka alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa nafasi yake kama Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu kuhusu uteuzi wa Wajumbe wawili wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanywa na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa John Pombe Magufuli.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 3(1) inatamka wazi kuwa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na ni nchi ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. Aidha Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2007, Kanuni ya 5(1) inakataza Chama cha Siasa kutumia mamlaka, rasilimali za serikali, vyombo vya dola au wadhfa wa kiserikali kujinufaisha kisiasa.

Gerson Msigwa kama Mtumishi wa Umma mwenye wadhfa wa Mkurugenzi kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 anatakiwa na anapaswa kuzingatia masharti ya Viongozi wa umma. Kifungu cha 21 cha sheria hiyo kinakataza kiongozi wa umma kutumia mali za serikali isivyoruhusiwa.

Aidha, kama Mtumishi wa umma aliyeajiriwa na analipwa fedha na Watanzania bila kujali itikadi za kisiasa alipaswa kutambua kuwa Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009, Kanuni ya 21 (a)(b)na (f) inatoa katazo kwa Mtumishi wa umma kuwa na wadhfa katika chama siasa, kutofanya siasa katika masaa ya kazi na kufanya shughuli za kisiasa wakati huo.

Kwa kuwa Msigwa ameendelea kunukuliwa akisisitiza kuwa yeye ni Msemaji wa Rais na ambaye ni Mwenyekiti wa CCM huku akijua kufanya hivyo ni kukiuka masharti kama tulivyoeleza, sisi kama Chama cha siasa tunatamka yafuatayo;

1. Tutawasilisha kwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu ukiukwaji wa Misingi na taratibu wa viongozi wa umma uliofanywa na Gerson Msigwa kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995.

2. Tunamtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kutumia mamlaka yake kupitia Kanuni ya 6(1)(d) ya Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa kutoa tamko dhidi ya ukiukwaji wa Kanuni hizo uliofanywa na CCM kwa kutumia mali za umma kwa maslahi yao ya kisiasa. Msajili akishindwa kufanya hivyo tutawasilisha malalamiko rasmi kwake kwa mujibu wa Kanuni ya 6(1)(a)kuhusu ukiukwaji huo.

3. Tunamtaka Katibu Mkuu Kiongozi au Tume ya Utumishi wa Umma kama mamlaka za nidhamu kumchukulia hatua Gerson Msigwa kwa kukiuka masharti ya Utumishi wa Umma kwa kufanya siasa wakati wa masaa ya kazi na pia kujipa nafasi ya kuwa Msemaji wa CCM huku akijua Chama hicho kina Msemaji wake.

4.Tunaahidi kuchukua hatua zaidi endapo mamlaka ambazo tumezitaja zitashindwa kuchukua hatua dhidi ya tabia hii ambayo inakiuka Katiba, Sheria na Kanuni kama tulivyoeleza. Tunaendelea kusisitiza kuwa watumishi wa umma Wana wajibu wa kufuata Katiba, sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali Katika utendaji wao wa kazi za umma.
Imetolewa na;

John Mrema,
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje- CHADEMA
04 Juni, 2018

Share Button
Layout Settings